SALA WAKATI WA KUJIBARIKI NA MAJI YA BARAKA
Kwa njia ya Maji haya ya Baraka,
na kwa njia ya Damu yako azizi,
na kwa maombezi ya Moyo Safi wa Maria,
unioshe na uovu wangu wote na uwasaidie roho zinazoteseka toharani. Amina.
Kwa njia ya Maji haya ya Baraka,
na kwa njia ya Damu yako azizi,
na kwa maombezi ya Moyo Safi wa Maria,
unioshe na uovu wangu wote na uwasaidie roho zinazoteseka toharani. Amina.
Ee Bikira Maria uliyekingiwa dhambi ya asili, utuombee sisi wenye kukimbilia kwako, uwaombee na wale wasioukimbilia kwako, hasa maadui wa Kanisa Takatifu, na wale waliokabidhiwa kwako. Amina.
(Sala hii inafaa sana kwa ajili ya kutetea uhai wa watoto wachanga wakiwa tumboni mwa mama zao, dhidi ya utoaji mimba au hatari nyingine dhidi ya uhai wa binadamu)
Ee Mt. Yosefu, wewe ni Mchumba safi na Mpenzi wa Bikira Maria, u Baba Mlishi wa Yesu, mlinzi na mtunzaji wa Familia Takatifu, na wa familia zote. Tuna imani kabisa katika uangalizi wako uliojaa upendo, juu ya uhai mpya, na uaminifu wako kwa familia.
Tunaweka jitihada zetu chini ya ulinzi wa sala zako. Utusaidie daima katika kutetea zawadi ya uhai wa binadamu, ili ukue hadi uzima wa milele ulioahidiwa na kujaliwa kwetu na Mwanao, Ndugu yetu, Yesu Kristu.
Amina.
Ee Mtukufu Mt. Yosefu, ulichaguliwa na Mungu kuwa Baba Mlishi wa Yesu, mchumba safi kabisa wa Maria Bikira Milele, na mkubwa wa Familia Takatifu. Umechaguliwa na Mwakilishi wa Kristu kama Msimamizi wa kimbingu na mlinzi wa Kanisa alilolianzisha Kristu. Ndiyo maana ninakuomba kwa matumaini makuu usaidizi wako wenye nguvu kwa ajili ya Kanisa zima duniani.
Mlinde kwa namna ya pekee, kwa upendo wa kikweli wa ki-baba, Baba Mtakatifu na Maaskofu wote na Mapadre wenye ushirika na Kiti cha Petro. Uwe mlinzi wao wote wanaotumikia wokovu wa wanadamu kati ya majaribu na mahangaiko ya maisha haya, na utujalie kwamba watu wote wa dunia hii wamfuate Kristu na Kanisa alilolianzisha.
Mpendwa Mtakatifu Yosefu, ukubali majitoleo ya nafsi yangu ambayo sasa ninafanya. Ninajiweka wakfu kwako kwa ajili ya utumishi wako, ili daima wewe uwe baba yangu, mlinzi wangu, na kiongozi wangu katika njia ya wokovu. Unijalie usafi mkuu wa moyo na matamanio makuu ya maisha ya kiroho. Unijalie ili matendo yangu yote, kwa mfano wako, yawe kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, pamoja na Moyo wa kimungu wa Yesu, moyo safi wa Maria, na moyo wako wa ki-baba. Uniombee, nami nishiriki kifo chako cha furaha na kitakatifu.
Amina.
Malaika wa Mungu Mlinzi wangu mpenzi,
Ambaye upendo wake unanifanya niwepo hapa,
Uwe nami leo hii,
Kuniangaza na kunilinda,
Kunitawala na kuniongoza.
Amina.
Ee Mt. Yosefu mwenye heri, tunakimbilia kwako katika masumbuko yetu, na kisha omba shime ya Mchumba wako Mtakatifu, tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako. Kwa ajili ya mapendo uliyompenda Bikira Mtakatifu Mzazi wa Mungu, na kwa ajili ya kumtunza Mtoto Yesu, twakuomba sana, utuangalie kwa wema sie tuliokuwa fungu lake Yesu Kristu, tukakombolewa kwa damu yake. Tusimamie katika masumbuko yetu kwa enzi na shime yako.
Ee Mlinzi amini wa jamaa takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristu.
Ee Baba uliyetupenda mno tuepushe na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji, utusimamie huko juu mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwopoa Mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa, na leo hivi likinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida yote; mtunze daima kila mmoja wetu, tufwate mfano wako, ili tupate na msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupata mbinguni makao ya raha milele.
Amina.
Ee Yesu, kupitia mikono safi ya Bikira Maria, na kwa maungano na sadaka yako kuu, ninakutolea sala, matendo, kazi, masumbuko, na furaha zangu zote za siku hii ya leo, kwa ajili ya nia za Moyo wako Mtakatifu, Ee Yesu ufalme wako utufikie!
Baba Yetuโฆ.
Salamu Maria, โฆ..
Nasadiki โฆโฆ.
Amri za Mungu โฆโฆ
Amri za Kanisa โฆโฆ
Ee Bwana Yesu Kristo. Mkombozi wetu, kwa mapendo na tamaa yako ya kutaka kulinda vema Kanisa lako, ukachagua Mapadri wawe Wachungaji na Viongozi wa roho za watu. Nakuomba sana; ubariki nia na bidii inayowapasa Mapadri wote katika kazi zao. Uwaongezee Utakatifu.
Uwatie moyo mzuri wenye mapendo makubwa kwako na roho za watu. Hivyo wakiisha kupata wenyewe Utakatifu, waweze kuwaongoza vizuri watu walio chini ya ulinzi wao, katika njia ya Utakatifu na furaha ya milele. Uwajalie neema zote za hali ya Upadri. Uwajalie ili waonyeshe kila siku ya maisha yao mfano wa kila fadhila ya mapendo na ya uaminifu katika Kanisa, kwa Baba Mtakatifu na kwa Maaskofu.
Yesu mpendelevu, uangalie kwa mapendo kazi na mateso ya Mapadri wako; ubariki na ustawishe mafundisho yao; wanapowafundisha watoto, wanapowahubiria watu, wanapowatuliza wakosefu watubu na wanapowasaidia wagonjwa na wale wanaokaribia mauti, Ee Yesu uwe pamoja nao. Uwakinge na hatari zote za roho na za mwili.
Mwokozi Yesu, ulijalie Kanisa liwe na Mapadri wengi walio Watakatifu. Uwajalie watoto na vijana wengi wasikie wito wa Upadri, uwatie furaha na Utakatifu na roho za Mapadri waliokufa uzijalie punziko la amani.
Kwa mimi mwenyewe Ee Yesu mpendelevu, naomba unijalie roho ya imani na utii mnyenyekevu ili niwaheshimu Mapadri kama Mawakili wa Mungu. Niwatii katika njia zote za wokovu wa roho yangu. Amina.
Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakukimbilia, ninakuja kwako katika mikono yako yenye huruma. Ndiwe tegemeo langu na tumaini langu dhabiti. Ndiwe mwenye dawa ya maovu yangu yote, malipizi ya makosa yangu yote. Waweza kunipatia haja zangu na neema ninazoziomba mimi na wengine. Wewe uko ili kutusaidia sote, ndiwe mwanga mkuu usiozimika, ndiwe chanzo cha nguvu, uvumilivu, amani na faraja. Nina hakika kuwa maombi yangu hayatakuchosha, nawe hutaacha kunisaidia, kunilinda, kunipenda, kwani, ee Moyo Mtakatifu , upendo wako hauna mwisho. Ee Moyo Mtakatifu, unihurumie, kwa ajili ya maombi yangu, kadiri ya huruma yako. Nawe katika sisi, na kwa ajili yetu, ufanye lolote unalolihitaji, kwani tunajitoa kwako kwa imani na uhakika thabiti kwamba kamwe hautatuacha, kwa milele. Amina.
Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
Tunakushukuru, ee Mungu, kwa mapaji uliyotujalia leo. Amina.
Baba yetu โฆ
Salamu Maria โฆ
Mungu wangu, nasadiki maneno yote. Linayosadiki na linayofundisha Kanisa Katoliki la Roma. Kwani ndiwe uliyetufumbulia hayo. Wala hudanganyiki, wala hudanganyi. Amina.
Mungu wangu, natumaini kwako, nitapewa kwa njia ya Yesu Kristo. Neema zako hapa duniani, na utukufu mbinguni. Kwani ndiwe uliye agana hayo nasi, nawe mwamini. Amina.
Mungu wangu, nakupenda zaidi ya chochote. Kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu, kama nafsi yangu, kwa ajili yako. Amina.
Tuwaze katika moyo wetu makosa ya leo tuliyomkosea Mungu kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu. (Husubiri kidogo ).
Nakuungamia Mungu Mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno, kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo, na kwa kutotimiza wajibu.
Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndiyo maana nakuomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.
Mungu Mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele. Amina.
Ee Mungu, nawaombea watu wa nchi hii, wapate kusikia maneno yako na kukupenda wewe Bwana Mungu wetu.
Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari zote za roho na za mwili. Amina.
(kipindi kisicho cha Pasaka)
Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria.
Naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Salamu, Maria,โฆ..
Ndimi mtumishi wa Bwana.
Nitendewe ulivyonena.
Salamu, Mariaโฆ.
Neno la Mungu akatwaa mwili.
Akakaa kwetu.
Salamu, Mariaโฆ.
Utuombee, Mzazi mtakatifu wa Mungu.
Tujaliwe ahadi za Kristu.
Tuombe:
Tunakuomba, Ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika kwamba Mwanao amejifanya Mtu kwa mateso na msalaba wake tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. AMINA.
Malkia wa mbingu, furahi, aleluya.
Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.
Amefufuka alivyosema, Aleluya.
Utuombee kwa Mungu, Aleluya.
Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Alaluya.
Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.
Tuombe.
Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao, fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.
ATUKUZWE (mara tatu)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina.
Enyi Yesu, Maria na Yosefu nawatolea moyo na roho na uzima wangu!
Enyi Yesu, Maria na Yosefu mnijilie saa ya kufa kwangu!
Enyi Yesu, Maria na Yosefu mnijalie nife mikononi mwenu!
(Rehema ya siku 300).
Kwa heri Yesu mpenzi mwema,
Naenda usiudhike mno.
Nakushukuru, nakupenda,
Kwa hizo nyimbo za mwisho.
Asubuhi nitarudi.
Yesu kwa heri.
Kwa heri Mama mtakatifu,
Sasa napita pumzika.
Asante kwa moyo na nguvu,
Leo umeniombea.
Asubuhi nitarudi.
Mama kwa heri.
Kwa heri Yosefu mnyenyekevu,
Kazi zatimilizika.
Kama mchana, leo usiku,
Nisimamie salama.
Asubuhi nitarudi.
Yosefu kwa heri.
Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
Mungu wangu naenda kulala naomba malaika 14, waende nami, wawili juu, wawili chini, wawili upande wa kuume, wawili upande wa kushoto, wawili wanifunike, wawili waniamshe, wawili wanipeleke juu mbinguni. Mimi mtoto mdogo, roho yangu ni ndogo, haina nafasi kwa mtu yoyote ila kwa Yesu pekee. Amina.
Roho ya Kristo unitakase
Mwili wa Kristo uniokoe
Damu ya Kristo unifurahishe
Maji ya ubavu wake Kristo yanioshe
Mateso ya Kristo nguvu yanizidishie
Ee Yesu mwema unisikilize
Katika madonda yako unifiche
Usikubali nitengwe nawe
Na adui mwovu unikinge
Saa ya kufa kwangu uniite
Uniamuru kwako nije
Na watakatifu wako nikutukuze
Milele na milele.
Amina.
Nasadiki kwa Mungu, Baba Mwenyezi,/ mwumba mbingu na dunia./ Na kwa Yesu Kristu, Mwanaye wa pekee, Bwana wetu;/ aliyetungwa kwa Roho Mtakatifu,/ akazaliwa na Bikira Maria,/ akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato,/ akasulubiwa, akafa, akazikwa,/ akashukia kuzimu;/ siku ya tatu akafufuka katika wafu;/ akapaa mbinguni;/ amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi;/ toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu,/ Kanisa takatifu katoliki,/ ushirika wa Watakatifu,/ maondoleo ya dhambi,/ ufufuko wa miili,/ uzima wa milele. Amina.
Ee Moyo Mtakatifu sana wa Yesu, chemchemi ya kila baraka, ninakuabudu, ninakupenda, na kwa majuto halisi ya dhambi zangu, nakutolea moyo wangu dhaifu. Nifanye mnyenyekevu, mvumilivu na safi, nikikubali na kuyatii kabisa mapenzi yako. Ee Yesu mwema, unijalie niishi nawe na kwa ajili yako. Unilinde niwapo katikati ya hatari, unifariji katika mateso, unipe afya ya mwili na msaada katika mahitaji ya mwili, Baraka yako juu ya kila nilifanyalo, na neema ya kifo chema. Amina.
Ee Yesu uliyesema โKweli nawaambieni, ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, gongeni nanyi mtafunguliwaโ, tazama ninagonga, ninatafuta na kuomba โฆโฆ.. (Taja ombi lako)
Baba Yetuโฆ.., Salamu Maria โฆโฆ.., Atukuzwe Babaโฆโฆ..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!
Ee Yesu uliyesema โKweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu mtapewaโ, tazama kwa jina lako ninaomba โฆโฆ. (Taja ombi lako)
Baba Yetuโฆ.., Salamu Maria โฆโฆ.., Atukuzwe Babaโฆโฆ..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!
Ee Yesu uliyesema โKweli nawaambieni, mbingu na dunia zitapita lakini maneno yangu hayatapita kamweโ, tazama, nikitiwa nguvu na maneno yako ya kweli ninaomba โฆโฆ.. (Taja ombi lako)
Baba Yetuโฆ.., Salamu Maria โฆโฆ.., Atukuzwe Babaโฆโฆ..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!
Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambaye kwako ni kitu kimoja tu kisichowezekana, ambacho ni kutoacha kutowaonea huruma wenye huzuni, utuhurumie sisi wakosefu maskini na utujalie neema tukuombayo kwa njia ya Moyo Imakulata wa Maria, Mama yetu mpole.
Sali โSalamu Malkiaโ na kuongezea, โMtakatifu Yosefu Baba Mlishi wa Yesu, utuombeeโ.
P.S. โ Sala hii ya Novena ilisaliwa kila siku na PADRE PIO kwa ajili ya kuwaombea wale wote waliomwomba msaada wa sala zake. Unaweza kuisali kwa namna tofauti tofauti. Mfano, kama Novena ya siku tisa, ambapo unasali sala hii mara moja au zaidi kila siku kwa siku tisa, au unaweza kuifanya kama Novena ya masaa, ambapo unasali sala hii kila baada ya saa moja kwa masaa tisa kwa siku hiyo hiyo, hasa kama kitu unachokiomba ni cha haraka au umesongwa moyoni. Vilevile unaweza kuifanya sala hii kama sehemu ya sala zako za kila siku katika mwezi Juni ambao ni mwezi uliotengwa na Kanisa kwa ajili ya kuuheshimu Moyo Mtakatifu wa Yesu, na hapo utaitumia kuwaombea watu waliokuomba msaada wa sala zako kama alivyofanya Mtakatifu Padre Pio. Pia unaweza kuitumia kama sala yako ya siku zote au ya mara kwa mara kwa ajili ya mahitaji mbalimbali.
Ewe Mtakatifu Yuda Tadei,/ mtume mtukufu na shahidi wa Kristo,/ umesifika pote kwa wepesi wako wa kutoa misaada/ kwa wanaokukimbilia katika matatizo yao mazito./ Pia ni mwombezi wa waliopondeka moyo./
Mimi ni mmoja wa hao./ Nakujia na moyo uliojaa shida na matatizo./ Nakusihi kwa moyo wote/ unisaidie kwa maombezi yako yenye nguvu/ kufikia utatuzi unaofaa kadiri ya mapenzi ya Mungu./ Maisha yangu yamejaa misalaba,/ siku kwa siku matatizo hayapungui./ Moyo wangu umekuwa bahari ya siki chungu sana./ Mapito yangu nayaona yamejaa miiba mikali./ Roho yangu imezama katika dimbwi la machozi na kite./ Nafsi yangu imezingirwa na giza nene./ Ghasia na kukatishwa tamaa ya kuishi/ hunyemelea roho yangu./ Maongozi ya Mungu na imani naviona vinanitoka kidogo kwa kidogo./
Nikielemewa na mawazo kama hayo/ najikuta sina nguvu za kuishi,/ na maisha kwangu ni msalaba mzito/ ninaouogopa hata kuunyakua./ Wewe unaweza kabisa kunitoa katika balaa hili./ Sitaacha kukusihi/ hadi hapo utakaponisaidia/ au kunijulisha mapenzi ya Mungu kwangu./ Natangulia kutoa shukrani kwa jibu liwalo lote.
Ee Yesu mwenye huruma, mpenda roho za watu, nakuomba kwa ajili ya kuzimia kwa Moyo wako Mtakatifu, na kwa ajili ya Mama Yako asiye na doa, uwatakase kwa damu yako, watu wote wenye dhambi wanaokufa sasa, na watakaokufa leo.
Moyo wa Yesu uliozomia, uwahurumie watu wanaokufa X3.
Ee Mt. Yosefu, Baba Mlishi wa Mwokozi wangu, na mchumba safi wa Mama wa Mungu, leo ninakuchagua wewe, kama mwombezi wangu kwa Mungu Mwenyezi, na pia kama mfano wangu, na mlinzi wangu, na baba yangu, katika bonde hili la ugenini.
Ee Mt. Yosefu, ambaye Bwana alikufanya mlinzi wa Familia yake, ninakuomba uwe mlinzi wangu mwema katika mambo yangu yote. Uniwashie moyoni mwangu moto wa mapendo makuu kwa Yesu, na uniwezeshe kumtumikia kwa bidii na kwa uaminifu kwa mfano wako. Nisaidie katika udhaifu wangu katika kumheshimu Mama Maria kama Mwombezi wangu.
Daima uwe kiongozi wangu katika njia ya fadhila na ibada, na unijalie, baada ya kukufuasa kwa uaminifu katika njia ya haki, nipate ulinzi wako wenye nguvu katika saa ya kufa kwangu.
Amina
Enyi Yesu na Maria na Yosefu,
nawatolea Moyo, na roho, na uzima wangu.
Enyi Yesu na Maria na Yosefu,
mnipokee saa ya kufa kwangu.
Enyi Yesu na Maria na Yosefu,
mnijalie nife mikoni mwenu.
Mama Mtakatifu, Mama wa Mungu na Malkia wa Mashahidi, leo nakuchagua Wewe uwe mfano wangu, mkingaji na mteteaji wangu. Naweka roho fukara katika moyo wako uliotobolewa na panga nyingi za mateso. Unipokee mimi niwe mtumishi wako wa pekee na mshiriki wa mateso yako. Nijalie nguvu niwe daima karibu na msalaba ule alikosulibiwa Yesu. Nakutolea nafsi yangu na mali yangu yote. Pokea kila tendo langu jema ukalisindikize kwa Mwanao, Mama, nifanye nistahili kuitwa mtumishi wa Maria, Simama karibu yangu katika matendo yangu yote ili yafanwe kwa sifa ya Mungu. Ulivyosimama karibu kabisa ya Mwanao alipokufa msalabani uwe karibu nami saa ya kufa kwangu. Nijalie niweze kutaja jina lako na la Mwana wako nikisema: โYesu, Maria na Yosef mnisaidie saa ya kufa kwangu. Yesu, maria na Yosef, naomba nife kwa amani kati yenu!โ . Amina.
Mzee Simeoni aliagua kuwa Moyo wa Mama Maria utachomwa kwa upanga.
Tuombe neema ya kuvumilia mateso.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โฆโฆโฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โฆโฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Maria na Yosefu walikimbilia Misri usiku ili kumficha Mtoto Yesu asiuawe na Herodi.
Tuombe neema ili miili yetu iwe kimbilio lake Yesu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โฆโฆโฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โฆโฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Mama Maria aliona uchungu sana Mtoto Yesu alipopotea kwa siku tatu.
Tuombe neema ya kudumu na Yesu mioyoni mwetu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โฆโฆโฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โฆโฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Mama Maria aliona uchungu sana alipokutana na Mwanae Yesu katika njia ya Msalaba.
Tuombe neema ya kudumu na Yesu siku zote.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โฆโฆโฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โฆโฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Mama Maria aliona uchungu sana alipomwona Mwanae Yesu akisulibiwa Msalabani.
Tuombe neema ya kufa mikononi mwa Yesu na Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โฆโฆโฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โฆโฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Mama Maria aliona uchungu sana alipopakata maiti ya Mwanae Yesu baada ya kushushwa Msalabani.
Tuombe neema ya kutotenda dhambi.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โฆโฆโฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โฆโฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Mama Maria aliona uchungu sana aliporudi nyumbani baada ya kumzika Mwanae Yesu
Tuombe neema ya kitulizo kwa Mama Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โฆโฆโฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โฆโฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Novena ya Noeli (maarufu kama novena ya Mt. Andrea)
Husaliwa kuanzia tar 30 Nov hadi usiku wa Noeli, tar 24 Disemba. Inajulikana kama novena ya Mt. Andrea kwa sababu novena hii huanza kusaliwa katika siku ya kumbukumbu ya Mt. Andrea Mtume.
“IHESHIMIWE, NA IBARIKIWE, SAA ILE NA WAKATI ULE, AMBAO MWANA WA MUNGU, ALIZALIWA NA BIKIRA MBARIKIWA SANA, USIKU WA MANANE, KULE BETHLEHEM, WAKATI WA BARIDI KALI.
WAKATI HUO, UPENDE E MUNGU WANGU, KUSIKIA MAOMBI YANGU, NA KUNIJALIA YALE NINAYOYAOMBA KWAKO, KWA NJIA YA MASTAHILI YA MWOKOZI WETU YESU KRISTO, NA YA MAMA YAKE MBARIKIWA. AMINA. (Sali mara 15 kwa siku).
Inasadikika kuwa chochote uombacho kwa imani kwa sala hii utakipata mradi kipatane na mapenzi ya Mungu. Sali na watoto/ familia kuwatafakarisha na kuwaongezea matazamio juu ya sikukuu ya Noeli.
Isambaze sala hii kwa wengine.
Recent Comments