SALA YA KUOMBEA FAMILIA

Ewe Mungu Mwenyezi, sisi kama familia tunakushukuru kwa zawadi ya Mama Kanisa Katoliki ambaye siku zote hutupatia malezi bora kwa ajili ya wokovu wetu. Kanisa halichoki kutuhimiza tutafakari na kuishi utakatifu wa familia ya Nazareti ya Yesu, Maria na Yosefu. Familia hii iliishi upendo uliojengwa kwa fadhila za imani, uaminifu, utii, uvumilivu na upole hata wakawa watakatifu. Tunapoadhimisha mwaka wa Familia, tunaiweka mbele yetu familia ya Nazareti iwe dira, baraka na mfano kwa familia zetu.

Tunakushukuru Baba kwa ajili ya familia zote zinazojitahidi kuishi fadhila hizo za Familia takatifu na tunakuomba uzidi kuwaimarisha wanandoa ili tupate kwao mifano mingi na bora ya kuigwa. Ee Bwana, tunaomba Roho Mtakatifu atuangazie tuweze: kutambua familia kuwa Kanisa la nyumbani na shule ya imani na upendo; kuimarisha familia kwa sala, sakramenti na tunu za kiinjili na kushirikiana kwa heshima katika familia kwa usitawi wa roho na wa mwili kwa wanafamilia wote.

Tunaziombea familia zetu na Jumuiya Ndogondogo za Kikristo ziwe bustani bora na salama za kuchipusha na kulea miito mitakatifu ya Ndoa, Utawa na Upadre. Tunawaombea vijana na watoto wetu Uchaji wa Mungu ili wawe na bidii ya kujitunza kwa kushika amri za Mungu na kuishi fadhila za kiinjili, wawe na roho ya kimisionari yaani walipende Kanisa na kuwa na moyo wa kueneza ufalme wako kwa matendo ya imani. Baba wa huruma, tunakukabidhi familia zenye misukosuko ya mafarakano, ulevi, ubinafsi, uregevu-dini, uvivu, ushirikina, hofu, magonjwa sugu na mengineyo yenye kuleta huzuni; kwa hisani yako uwape neema, mwanga na nguvu za kuanza maisha mapya yenye amani, waweze kufurahia upatanisho na uponyi wa pendo lako la kibaba kati yao.

Tunaomba toba na msamaha kwa ukatili, manyanyaso na hata mauaji katika familia zetu na uwaponye wote waliojeruhiwa kwa maneno, matendo na makwazo ya aina yeyote. Aidha tunakuomba uwe kitulizo na faraja kwa wagonjwa na wazee, pia tegemeo la yatima na wajane. Wenye matatizo ya kiafya au ya kijamii wasikate tamaa bali waunganishe hali zao na msalaba wa Mwanao na kukutumaini wewe Mweza yote. Jamii iwajibike nao kwa kuzijali haki zao na kuwapa misaada wanayohitaji.

Tunakuomba ubariki miradi na kazi zetu ili familia zipate usitawi na maendeleo; na utujalie hekima ya kukushukuru kwa maisha ya haki, amani na ukarimu na mwisho tukaimbe sifa zako pamoja na familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefuna jeshi lote la mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

Baba yetu… …..Salamu Maria….…Atukuzwe Baba………

Melkisedeck Leon Shine

Editor: Melkisedeck Leon Shine. About Me | Contact Me | LinkedIn | TikTok | WhatsApp

Read and Write Comments

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Shopping Cart