Karibu AckySHINE

Karibu AckySHINE

Chagua Unachotaka Kusoma Hapa

BURUDANI MAKALA DINI VITABU

Unahakikishiwa kusoma kitu kipya kizuri kila saa unapotembelea ukurasa huu.

Jinsi ya kupika Slesi Za Chokoleti Na Karameli

Viamba upishi

Unga 1 Magi (vikombe vya chai)

Sukari ya browni ½ Magi

Siagi iliyoyayushwa 125 g

Nazi iliyokunwa ½ Magi

Mjazo wa karameli (Caramel filling)

Syrup 1/3 kikombe cha chai

Siagi iliyoyayushwa 125 g

Maziwa matamu ya mgando 2 vikopo (condensed milk)

Mjazo wa chokoleti (Chocolate filling)

Chokoleti 185 g (dark chocolate)

Mafuta 3 Vijiko vya chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya unga, sukari, siagi na nazi iliyokunwa kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.

2. Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30 cm au (8 in kwa 12 in) unaweza kuweka karatasi ya kuchomea chini ukipenda.

3. Choma kwenye moto 325˚C kwa muda wa dakika 15 mpaka 18 au mpaka ibadilike kuwa rangi ya browni.

4. Kwenye sufuria ndogo tia syrup siagi na maziwa matamu ya mgando na changanya kwa moto mdogo mpaka uwe mzito kasha mimina juu ya keki uliyochoma na choma tena kwa muda wa dakika 20 mpaka karameli iwe rangi ya dhahabu.

5. Kwenye sufuria ndogo nyingine tia vipande vya chokoleti na mafuta na ukoroge kwa moto mdogo mpaka iyayuke kisha wacha ipoe kidogo mimina juu ya mjazo wa karameli kisha weka kwenye friji mpaka ishikamane.

6. Kata vipande weka kwenye sahani tiyari kwa kuliwa

Mapishi ya Mandazi ya nazi

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) vikombe 2 na1/2
Sukari (sugar) 1/2 kikombe
Hamira (yeast) 1/2 kijiko cha chai
Hiliki (cardamon powder) 1/4 kijiko cha chai
Tui la nazi (coconut milk) kiasi
Baking powder 1/4 kijiko cha chai
Siagi (butter)1 kijiko cha chakula
Mafuta ya kukaagia

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote kasoro tui la nazi na mafuta ya kukaangia. Ukisha changanyika vizuri tia tui la nazi na uanze kuukanda mpaka uwe mlaini. Baada ya hapo usukume na ukate mandazi katika shape uipendayo, Kisha uyawe katika sehemu yenye joto (warm place) ili yapate kuumuka.
Yakisha uumuka yakaange katika mafuta mpaka yaive kisha ipua na uyaache yapoe tayari kwa kuliwa. (Mafuta ya kukaangia yasiwe yamoto sana kwani yatayababua mandazi na hivyo ndani hayataiva vizuri.

Jinsi ya kung’arisha sura yako kwa kutumia Asali, Sukari, Maziwa, na Limao

Usafi wa uso ni moja ya mambo muhimu sana kwa mwanamke au mwanaume yeyote yule ambaye anapenda kuwa nadhifu na mwenye mvuto. Kumbuka “reception ndio kila kitu “. Unapokutana na mtu sura yako na mwonekano wa sura yako ndio kitu cha kwanza kinachomtambulisha kwamba wewe ni nani na upo kwenye hali gani.

Kuna njia nyingi za kuufanya uso wako uvutie na kupendeza. Leo tutaongelea zaidi jinsi ya kusafisha uso kwa njia ya asili. Mie hupenda kutumia njia ya asili sababu ni rahisi kupata vifaa na ni nafuu . Pia mtu anaweza kufanya kwa mazingira yoyote yale. Na matumizi ya vitu vya asili kwenye mwili husaidia kupunguza sumu mwilini kwani kutumia vipodozi vyenye kemikali husababisha miili yetu kujaaa sumu.

Njia ya asili ya kusafisha na kupendezesha mwili ninayokueleza leo inahitaji vitu vikuu vinne : asali, sukari, maziwa, na limao.

Haijalishi aina gani ya ngozi unayo , njia hii ya asili inaweza kutumika kwa aina yoyote ile ya ngozi iwe ngozi yenye mafuta au ngozi kavu.

Kiasi cha mahitaji yanayohitajika:

  • Kijiko kimoja cha asali
  • Kijiko kimoja cha sukari
  • Kijiko kimoja cha maziwa
  • Kijiko kimoja cha limao

Utaratibu wa kusafisha uso

Weka mahitaji hapo juu kwenye chombo kilicho kisafi, changanya vitu vyako mpaka vilainike, viache kwa muda wa dakika 10 ili viweze kuchanganyikana vizuri na na sukari iweze kuyayuka vizuri.

Baada ya mchanganyiko wako kuwa tayari chukua kipande cha pamba kilicho kisafi tumia kupakia mchanganyiko wako usoni . Na kumbuka ni vizuri uso ukiwa mchafu na upaswi kuosha uso alafu ufanye zoezi hili. Baada ya kupaka mchanganyiko wako usoni kaa kwa dk 15 .

Baada ya hapo chukua maji ya uvuguvugu, kitaulo kisafi na sabuni ya kipande “vizuri kutumia sabuni ya kipande maana haina kemikali nyingi” tumia kitambaa kuoshea uso wako pamoja na sabuni.

Basi baada ya hapo umekuwa umemaliza zoezi lako la usafi wa ngozi yako
Kumbuka njia hii aina madhara yoyote na haibadilishi rangi au muonekano wa ngozi yako na unashauliwa kufanya mara kwa mara ili kukupa mvuto zaidi.

Mambo ya Msingi kujua kuhusu Sakramenti ya Kitubio

Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu gani?
Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu alijua udhaifu wa binadamu hauishi mara anapopokea uzima wa Mungu kwa sakramenti tatu za kuingizwa katika Ukristo. Hivyo alipanga kusaidia mpaka mwisho wa dunia waamini wake watakaopatwa na dhambi na ugonjwa, kama alivyowasaidia wengi aliokutana nao katika maisha yake.
“Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, ‘Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako’… ‘Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi’ – amwambia yule mwenye kupooza – ‘Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako’. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii” (Math 9:2,6-8).

Mungu aliwapa watu (mapadri) amri/uwezo ya kusamehe dhambi kwa njia ya nani? Ni halali kuungama kwa padre?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa njia ya Mwanae. Yesu mfufuka aliwaonyesha Mitume alama ya mateso mwilini mwake, “akawavuvia, akawaambia, ‘Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23).
Katika Kanisa tunafurahi kupewa msamaha wa dhambi kila tunapohitaji, mradi tutubu. Kwa njia ya mwandamizi wa Mitume, Yesu anatuambia,
“Umesamehewa dhambi zako… Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani” (Lk 7:48,50).
Si dhana wala hisia tu, bali ni neno la hakika tunalolipokea kwa masikio yetu.

Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zipi?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zote, kwa sababu upendo mtiifu wa Mwanae aliyejitoa kuwa sadaka ya wokovu wetu unampendeza kuliko dhambi zote zinavyomchukiza. Ila hatuwezi kusamehewa dhambi ya kukataa neema ambayo Roho Mtakatifu anatusukuma tuamini na kutubu, kwa sababu pasipo imani na toba hapana msamaha.
“Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa” (Math 12:31).
“Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure” (2Kor 6:1).

Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu gani?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu amependa washiriki katika kazi zake. Ametuumba kwa njia ya wazazi na kutulea na kutusaidia kwa njia ya wengine pia. Hasa ametuokoa kwa njia ya Yesu, ambaye yupo nasi sikuzote katika Mwili wake, yaani Kanisa, na katika wale walioshirikishwa mamlaka ya Mitume.
“Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:18-20).

Je, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi?
Ndiyo, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi tulizotenda baada ya ubatizo, kwa kuwa hatuwezi kupokea msamaha tukikataa masharti yake, na Mungu ametupangia watu ambao watuondolee kwa niaba yake.
“Watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohane. Lakini, Mafarisayo na wanasheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye” (Lk 7:29-30).
Yesu mwenyewe alikubali kubatizwa na Yohane ili atimize mpango wa Baba.
“Yohane alitaka kumzuia, akisema, ‘Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?’ Yesu akajibu akamwambia, ‘Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Math 3:14-15).
Je, sisi tukatae kumkimbilia padri wa Mungu ili kupokea huruma yake tunayoihitaji kuliko hewa?

Tumuungamie padri dhambi zetu kwa lengo gani? Kwa nini Wakatoliki wanaungama kwa padri?
Tumuungamie padri dhambi zetu ili aweze kutushauri na kuamua kama tuko tayari kuondolewa. Tumweleze kwa unyofu makosa yote tuliyoyafanya na nia tuliyonayo ya kuyafidia na kutoyarudia.
“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu” (1Yoh 1:8-10).
Tukumbuke tulivyo viungo vya Mwili mmoja, hivi kwamba dhambi zetu zimewadhuru wenzetu. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana, mpate kuponywa” (Yak 5:16).
Kutokuwa tayari kufanya hivyo walau sirini kwa padri ni dalili ya kiburi na ya kutotubu.

Je, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi?
Ndiyo, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi kwa niaba ya Mungu aliyempa mamlaka hiyo. Hatusamehewi na utakatifu wa padri, bali na huruma ya Baba kwa njia yake.
Yeye anamtumia padri yeyote ili kuturahisishia kazi, tusihitaji kuchunguza kwanza ubora wa maisha yake, wala kwenda mbali tukampate mmoja asiye na dhambi. Tungefanyeje kuhakikisha ni mtakatifu, wakati hatuwezi kusoma moyo wake? Ingekuwa hivi, tusingepata kamwe hakika ya kusamehewa. Kumbe inatutosha kujua ni padri, kwamba Mungu amempa mamlaka ya kusamehe dhambi, kama Yesu alivyowapa Mitume siku tatu baada ya kumkimbia na hata kumkana. Kila padri anaweza kukiri,
“Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa: ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi” (1Tim 1:15).
Amri ya kusamehe dhambi wamepewa watu, si malaika.
“Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu” (2Kor 4:7).

Je, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo?
Ndiyo, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo, lakini ni vigumu zaidi, kwa sababu hatupati msaada wa sakramenti hiyo maalumu.
Pamoja na nia ya kumuungamia padri mapema tunahitaji neema ya kutubu kikamilifu, si kwa kuhofia adhabu, bali kwa kumpenda Mungu tuliyemchukiza.
“Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana” (Lk 7:47).

Sakramenti ya Kitubio ni nini?
Sakramenti ya Kitubio ndiyo Sakramenti ya kuwaondolea watu dhambi walizotenda baada ya Ubatizo (Yoh 20:22-23)

Lini na kwa maneno gani Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio?
Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio jioni ya ufufuko wake alipowapulizia mitume na kuwaambia maneno haya “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi watakua wameondolewa, wowote mtakaowafungia dhambi watakua wamefungiwa” (Yoh 20:22-23)

Mwenye kuwaondolea watu dhambi ni nani?
Mwenyezi Mungu pekee yake aweza kuwaondolea watu dhambi. Ndiye aliyewapa Mitume, Maaskofu na Mapadri uwezo wa kuwaondolea watu dhambi (Yoh 20:21-23)

Nani yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio?
Kila mkristo aliyetenda dhambi yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio

Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa haya
1. Kutafuta dhambi moyoni (Yoh 3:20-21)
2. Kujuta dhambi
3. Kukusudia kuacha dhambi
4. Kuungama kwa padre
5. Kutimiza malipizi
6. Kumshukuru Mungu aliyemwondolea dhambi

Wakati wa Sakramenti ya Kitubio Utamwomba Roho Mtakatifu kwa sala gani?
Utamuomba Roho Mtakatifu kwa sala hii:
Uje Roho Mtakatifu unisaidie nitambue dhambi zangu, nijute sana, niungame vema, nipate kutubu kweli. Amina

Kutafuta dhambi maana yake ni nini?
Kutafuta dhambi maana yake ni kujiuliza moyoni dhambi nilizotenda Tangu ungamo la mwisho (Ef 4:17-32)

Utafuteje dhambi wakati wa kujiandaa kuungama?
Tafuta dhambi kwa njia hizi
1. Kwa kukumbuka uliyokosa kwa mawazo, kwa maneno na kwa vitendo
2. Katika Amri za Mungu na za Kanisa
3. Katika vichwa vya dhambi
4. Katika kutimiza wajibu

Kutubu dhambi maana yake ni nini?
Kutubu dhambi maana yake ni kuona uchungu na chuki moyoni juu ya dhambi tulizotenda na kukusudia kutotenda dhambi tena (Yoh 8:11)

Kwa nini tujute dhambi zetu?
Tunajuta dhambi zetu kwa sababu tumeukosea Utatu Mtakatifu na tunastahili adhabu yake, na pia bila majuto hatuwezi kupata maondoleo ya dhambi.

Kuna majuto ya namna ngapi?
una majuto ya namna mbili,
1. Majuto kamili/Majuto ya mapendo
2. Majuto yasiyokamili/majuto pungufu/majuto ya hofu

Majuto kamili ni nini?
Majuto kamili ni kujuta kwa sababu tumemchukiza Mungu mwenyewe aliye mwema na mpendelevu kabisa

Majuto yasiyo kamili au majuto pungufu ni nini?
Majuto yasiyokamili ni kujuta kwa sababu tumepoteza furaha za Mbinguni na tunahofia adhabu ya Mungu

Asiyejuta aweza kuondolewa dhambi?
Asiyejuta hawezi kuondolewa dhambi kabisa, na anayeungama bila kujuta anatenda dhambi kubwa ya kufuru.

Kabla ya kuungama ni lazima kufanya nini?
Kabla ya kuungama ni lazima kukusudia kuacha dhambi na kuepuka nafasi kubwa ya dhambi bila kusahau kufuata hatua sita za kabla na baada ya kupokea kupokea Sakramenti ya Kutubio ambazo ni,
(1) kuwaza/kutafuta dhambi moyoni,
(2)kutubu/ kujuta,
(3)kukusudia kuacha dhambi,
(4)kuungama kwa padri,
(5)kutimiza kitubio,
(6)kumshukuru Mungu

Anayetaka kweli kuacha dhambi afanye nini?
Anayetaka kuacha dhambi afanye nguvu kuvishinda vishawishi, asali/aombe na apokee Sakramenti Mara nyingi hasa Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi Takatifu.

Kuungama ni kufanya nini?
Kuungama ni kumwambia Padri wazi wazi dhambi zako ulizotenda, zipi na ngapi ili upate maondoleo.

Anayeficha kusudi dhambi ya mauti katika ungamo anaondolewa?
Haondolewi, Bali anatenda dhambi kubwa ya kukufuru Sakramenti ya Kitubio. (Mt 7:21-23, Yoh 20:23, Gal 6:7)

Anayekufuru Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Yampasa kuziungama tena dhambi zake zote alizotenda tangu ondoleo la mwisho

Padri anaondolea dhambi mahali pa nani?
Padri anaondolea dhambi mahali pa Mungu

Padri anaondolea dhambi kwa maneno gani?
Padre anaondolea dhambi kwa maneno haya: Nami “Nakuondolea dhambi zako zote kwa Jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu”.

Kitubio tuwezacho kupewa na padre ni nini?
Kitubio tuwezacho kupewa na Padre ni kama sala, kufunga, kutoa sadaka kwa maskini, kusoma maandiko matakatifu, kuwatazama wagonjwa, n.k.

Kitubio tupewacho na padre chatosha?
Ni shida kutosha. Mara nyingi chataka malipizi ya hapa duniani kama kufunga, magonjwa, masumbuko, sala n.k mateso yasipotosha hapa duniani yatakamilishwa toharani

Kutimiza malipizi maana yake ni ni nini?
Kutimiza malipizi maana yake ni kutekeleza kiaminifu sala au matendo aliyotuagiza padre muungamishi ili kulipa adhabu za muda. (Rom 8:17)

Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema zipi?
Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema hizi;
1. Maondoleo ya dhambi zote kubwa na adhabu ya milele
2. Maondoleo ya dhambi ndogo na adhabu nyingine za muda (Isa 6:5-7, Yoh 8:11)
3. Twarudishiwa na kuongezewa neema ya utakaso
4. Twasaidiwa kuepa dhambi na twapata nguvu ya kutenda mema
5. Twarudishiwa tena mastahili tuliyopoteza kwa dhambi zetu

Dondoo Muhimu kuhusu ugonjwa wa kisukari

Wapendwa, napenda kushirikiana na nyinyi kujuzana hili nililolisikia kupitia channel ten leo asubuhi kuhusu ugonjwa wa kisukari.
Wataalam waliokua wakitoa mada walikua Prof Endrew Swai na Dr Mohamed Juma.
Kwa ufupi wamesisitiza sana kufanya mazoezi kwa takriban nusu saa kwa siku na ambayo mtu anatoa jasho na moyo kumwenda mbio. Hiyo ni kwa ajili ya kusaidia misuli ya miguu,tumbo kifua, mgongo na mikono kutumia kiasi cha sukari kinachozalishwa mwilini.

Kadhalika wamesisitiza sana kula vyakula visivyokobolewa,ikiwamo kula dona badala ya sembe,ulezi,mtama na matunda.
Watu wapunguze na ikiwezekana kuacha kunywa vimiminika vyenye sukari,ikiwamo juice,soda pombe na vinginevyo. Na hiyo nikwasababu vinywaji hivyo havikai tumboni na badala yake huenda moja kwa moja kwenye utumbo mwembamba na kulazimisha kongosho linalozalisha kemikali ya insulin kufanya kazi kwa kiwango cha juu kuliko ilivyo kawaida.
Vyakula visivyokobolewa vinafaida sana kwani vinachukua muda wa kutosha kutoka kwenye tumbo na kwenda kwenye utumbo mwembamba na hatimaye kuvunjwavunjwa kwa ajili ya kutumika mwilini. Kadhalika makapi yatokanayo na hivyo vyakula hutuzuia kupata kansa ya utumbo. La ajabu wametoa takwimu za kutisha kwani ulaya kwasababu wanakula vyakula vilivyokobolewa wanapata kansa ya utumbo kuliko nchi au bara la afrika,
na kansa hiyo ni ya nne kwa kusababisha vifo barani ulaya na amerika.
Tafadhalini tujihadharini kwani mada ilikua ndefu na nzuri sana kwa mustakabali wetu na afya zetu.
1.Mazoezi ni muhimu
2.Vyakula viwe na uasilia wake
3.Mtu aliye na mwenza wake afanye tendo la ndoa kwa kadiri inavyowezekana kwani ni sehemu ya mazoezi
4. Tubadili mifumo ya maisha yetu,kukaa tu bila kuishughulisha miili yetu.
Atakayeona anataka kupata elimu zaidi hao madaktari niliowataja wapo hospitali ya muhimbili kitengo cha tiba ya kisukari.
Ufahamu juu ya afya yako binafsi …nimeikuta sehemu 👆👆👆👆👆👆

Ufugaji wa nguruwe kazi, Cheki jamaa hawa wake walivyompa mtihani

MWANAHARAKATI: Hawa nguruwe unawalishanini?
.

MFUGAJI: Nawalisha mabaki ya chakula toka migahawa mbalimbali
.
MWANAHARAKATI: Hayo ni makosa unawatesawanyama kwa kuwalisha chakula kichafu. Akapigwa faini… Baada ya siku chache wakaja wanaharakati toka Umoja wa Mataifa
.
MWANAHARAKATI: Hawa nguruwe unawalisha nini?
.

MFUGAJI: Huwa nawaanzia siku na uji wa ulezi, halafu mikate, mchana ugali kwa kabeji na usiku viazi
.
MWANAHARAKATI: Loh watu wanakufa kwa njaa wewe unalisha nguruwe, akapigwa faini….siku chache baadae wakaja wanaharakati wa Mazingira
.
MWANAHARAKATI: Hawa nguruwe unawalisha nini?
.
MFUGAJI: (Kwanza akasita kidogo) Hawa huwa nawapa shilingi alfu tano kila mmoja kila siku halafu wao wenyewe wanaenda kununua chakula wanachokitaka.. .

Mapishi ya Chai ya maziwa, mandazi, uyoga na mayai

Mahitaji

Mandazi (angalia jinsi ya kupika katika recipe ya mandazi ya nyuma)
Uyoga (mashroom kikombe 1 cha chai)
Mayai (eggs 4)
Hoho (greenpepper 1/4 ya hoho)
Nyanya (fresh tomato 1)
Kitunguu (onion 1/4 ya kitunguu)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Hiliki nzima (cardamon 4)
Masala ya chai (tea masala 1 kijiko cha chai)
Pilipili mtama iliyosagwa (ground black pepper 1/4 ya kijiko cha chai)
Maziwa (fresh milk 1 kikombe cha chai)
Majani ya chai (tea leaves)
Maji kiasi.
Sukari (sugar)

Matayarisho

Jinsi ya kupika chai, weka maziwa, maji kiasi,hiliki, masala ya chai, pilipili mtama na majani katika sufuria. Chemsha kwa muda wa dakika 10 na chai itakuwa tayari.
Jinsi ya kupika mayai, weka mafuta kiasi katika fry pan na utie vitunguu, vikaange kidogo kisha tia nyanya, chumvi na hoho. Pika kwa muda wa dakika 4 kisha tia mayai na uyaache yaive mpaka yakauke kisha geuza upande wa pili na uyapike mpaka ya ive kisha ipua.
Jinsi ya kupika uyoga, weka mafuta kidogo katika fry pan kisha tia uyoga na chumvi na ukaange mpaka uive katika moto wa wastani. Ukisha iva breakfast yako itakuwa teyari kwa kuseviwa.

JE,SHERIA YA MAPADRE KUTOOA NA KUISHI USEJA IMEANDIKWA WAPI KATIKA BIBLIA AU IMETUNGWA TU NA PAPA?

Pengine umewahi kuulizwa swali hili wakati fulani.Na jibu lake ni kama ifuayavyo:
Mtu anapouliza kila kitu kimeandikwa wapi katika Biblia ni kudhihirisha kutokuijua au kuielewa vizuri Biblia Takatifu na historia yake.Mtu anapong’ang’ania “nionyeshe kitu fulani kimeandikwa wapi kwenye Biblia”ni kutaka kujiona ya kwamba yeye anaielewa sana Biblia na ameisoma yote kwa hiyo kila kitu kilichopo kwenye Biblia anakifahamu kumbe haijui Biblia bali anakariri Biblia!
Na hili suala la kushupalia swala la kuoa linadhihirisha jinsi gani tulivyo kizazi cha zinaa,ni kama tunadhani kuwa UZIMA upo katika kujamiiana!La hasha.
Paulo anasema “Kwasababu ya zinaa ni bora kuoa na kuolewa”(1Wakorintho 7:2.9) haya sio maneno ya kufurahia na kuchekelea tu maana “YANAWALENGA WALE WALIOSHINDIKANA KATIKA YALE YAPENDEZAYO”(1Wakorintho 7:1.8)sasa ni lazima tujiulize je tumeshindikana kiasi hicho?,hiyo sio sifa!
1Wakorintho 7:1.8
“Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika,ni heri mwanaume asimguse mwanamke,8.Lakini nawaambia wale wasiooa bado na wajane heri wakae kama mimi nilivyo”
Na Paulo Mtume anasema “Ni bora kuoa au kuolewa” lakini hakusema “Ni LAZIMA kuoa au kuolewa”
Suala la kutooa kwa mapadre kadiri ya historia lilianza tangu zamani kabisa mwanzoni mwa milenia ya pili katika mtagusi wa pili wa Laterani mwaka wa 1139 ili waweze kumtumikia Mungu kwa uhuru na bila mawaa wala pasipo vikwazo(1wakorintho 7:32-35)
1wakorintho 7:32-35
“32Lakini nataka msiwe na masumbufu.Yeye asiyeoa hujishughulisha zaidi na mambo ya Bwana ampendezeje Bwana;33.bali yeye aliyeoa hujishughulisha zaidi na mambo ya dunia hii,jinsi atakavyompendeza mkewe.34-Tena iko tofauti kati ya mke na mwanamwali.Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana ili apate kuwa mtakatifu mwili na Roho.Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii,jinsi atakavyompendezesha mumewe.,35.Nasema hayo niwafaidie ninyi,si kwamba niwategee tanzi,bali kwaajili ya vile vipendezavyo,tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine”
Maandiko hayo hapo juu yanajieleza wala sidhani kama yanahitaji kufafanuliwa zaidi ya yanavyojifafanua yenyewe.
Watu wengine wanafikiri kwamba kutooa ni dhambi,kama ni hivyo basi hata Yesu mwenyewe alikosa maana hata yeye mwenyewe hakuoa.
Yesu mwenyewe anafundisha kuhusu ubikira(Mathayo 19:10-12)
Mathayo 19:10-12,
“Wanafunzi wake wakamwambia,kama mambo ya mme na mke yakiwa hivyo ni afadhali kutuooa kabisa.Lakini Yeye akawaambia ‘SI WOTE WAWEZAO KULIPOKEA NENO HILO,ILA TU WALE WALIOJALIWA,maana wako MATOWASHI waliozaliwa katika hali hiyo toka matumboni mwa mama zao;tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi,tena wako Matowashi WALIOJIFANYA WENYEWE KUWA MATOWASHI KWAAJILI YA UFALME WA MBINGUNI’,awezaye kulipokea neno hili na alipokee”
Yesu mwenyewe analifafanua jambo hili kwa mapana,katika orodha ya matowashi Yesu aliowataja,Mapadre ni Matowashi waliojifanya hivyo kwaajili ya huduma ya kanisa na ufalme wa Mungu.
Tena Yesu anatuambia waziwazi kwamba”sio wote wawezao kulipokea neno hilo”yaani sasa sio wote wawezao kuwa Matowashi(Mapadre)bali ni wale tu waliojaliwa na Mungu neema hiyo.wale wasioweza kuishi upadre huoa na kuwa na familia.Tena Yesu anamalizia kwa kusema “Awezaye kulipokea fundisho hili na alipokee”,kwa maana nyingine ni kusema “Fundisho au Utowashi huu sio wa lazima”anayeweza kuishi maisha hayo basi na ayapokee na yule asiyeweza basi aache!
Vilevile Mitume ili kumfuata Yesu kikamilifu waliyaacha yote waliokuwa nayo ikiwepo familia zao ili wamtumikie Bwana(Mathayo 19:27.29)
Mathayo 19:27.29:
“Ndipo Petro akajibu akamwambia ‘Tazama sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe,tutapata nini basi?29.Amini nawaambia,kila mtu aliyeacha nyumba au ndugu wa kiume au wakike,au baba au mama au watoto au mashamba KWAAJILI YA JINA LANGU,atapokea mara mia zaidi na kuurithi uzima wa milele”
katika injili hiyo,Yesu anadhihirisha kwamba aliyeacha hayo yaliotajwa si kwasababu hawezi kuyapata la hasha,bali ameyaacha hayo yote KWAAJILI YA JINA LA YESU atapokea mengi hapa duniani halafu tena ataurithi ufalme wa mbinguni.
Mapadre wameyaacha hayo yote,wameacha nyumba,familia zao na kila kitu SIO KWASABABU HAWANA UWEZO AU HAWAWEZI KUPATA MAMBO HAYO bali WAMEACHA KWASABABU YA KUMTUMIKIA MUNGU KWA KADIRI YA MAANDIKO MATAKATIFU na kwakutaka kwao kuyaishi kimamilifu MASHAURI YA INJILI ikiwepo USEJA.
Maneno ya Paulo na yale ya Yesu mwenyewe kuhusu kumtumikia Mungu bila kuoa sio ya bahati mbaya bali ndiyo njia bora na inayofaa sana na kukubalika mbele ya Mungu.
Kwahiyo unapowaona mapadre hawaoi ujue sababu yake ni hiyo kwamba “Wamejitoa kwaajili ya kulihudumia kanisa”
(Na pia huwa nawashangaa mno watu wanaowapiga vita Mapadre kwamba kwanini hawaoi,najiuliza je,hao Mapadre wamewakataza wao kwamba wasioe?.)..na kama jibu ni hapana,sasa Je,”Pilipili ya shamba usiyoila inakuwashia nini?”
TUMSIFU YESU KRISTO!

Mambo 13 katika pesa ambayo unapaswa kuzingatia

1. Usikope pesa ya riba ili uanzishe biashara.
Usitegemee pesa ya mkopo kuianzishia biashara, upate faida kisha uirudishe pesa ya mkopo na riba yake.

2. Usitumie pesa ambayo bado haipo mikononi mwako.
Wala usije ukamuahidi mtu kumpa pesa ambayo umeahidiwa mahali fulani.

Kama kuna mtu kakwambia, Flan njoo kesho nikulipe deni lako- Basi ww usiende kukopa vitu dukani au kumuahidi mtu mwingine kumpa pesa ambayo na ww umeahidiwa

3. Kama unataka kuhifadhi/kutunza pesa, kila unapopata pesa usianze kuitumia kwanza kisha ukategemea kutunza kiasi kitakachosalia.

Hivyo basi, ukipata tu pesa, weka pembeni kiasi unachodhani kinafaa kutunzwa/kuhifadhiwa kisha tumia kiasi kilichobaki.

4. Ukipata nafasi ya kuonana na mtu tajiri, kamwe usiombe pesa.
Omba maarifa ya kutengeneza pesa kama yeye, tena kwa mtaji mdogo.

Maarifa ndio mtaji wa kwanza.
Unaweza kupewa/kusaidiwa pesa iwapo una mawazo mazuri ya kuzalisha pesa. Baadhi husema, “Omba ndoano, usiombe samaki”

5. Usitunze mbegu badala ya kuipanda.
Watu wengi hufurahia pesa wanayolipwa/kuipata kisha wanaiweka bank au nyumbani bila kuiwekeza.
Wekeza pesa ili uzalishe zaidi. Usiogope kuingia hasara, kila aliefanikiwa alipoteza kwanza kabla hajafanikiwa.Wengi walipoteza muda, pesa, afya na hata matumaini ya kufanikiwa, ila kwa uthubutu wao, mwisho wa siku walifanikiwa”

6. Kamwe usimkopeshe mtu pesa ambayo unahisi hatorudisha.

Unapomkopesha mtu huyo pesa, jiridhishe mwenyewe moyoni kuwa kama hatoweza kulipa basi deni lake-halitoathiri urafiki wenu. Ukihisi kwamba kushindwa kwake kulipa kunaweza kuathiri urafiki wenu, basi mshauri aende bank akakope”

7. Usikubali kumdamini mtu ambae huna uhakika kuwa atalipa kile unachomdhamini.
Kumbuka- dhamana maana yake utawajibika iwapo atashindwa kulipa

8. Epuka kutembea na pesa nyingi ambazo hata huna matumizi nazo wakati huo.
Unaweza kujikuta unafanya matumizi ambayo hayakuwa kwenye ratiba sababu ya ushawishi wa pesa ya mfukoni.
Ili kuepuka haya, tembea na pesa uliyopanga kuitumia katika safari yako.
Pesa nyingine itunze mahali pengine palipo salama”

9. Epuka kutunza pesa mahali pasipo sahihi.
Maeneo kama kwenye soksi, sidiria, chini ya mto wa kulalia, chini ya begi, kwenye kopo au hata kwenye begi la safari, si maeneo salama.
~Ni rahisi kusahau, kuibiwa au kupoteza pesa zako.

Ni bora ukatunza pesa kieletroniki; yaani bank au kwenye simu au kwenye pochi yenye kamba ngumu ya kuivaa mabegani au wallet ambayo inatosha kwenye mifuko imara na yenye vifungo kwenye nguo zako hasa uwapo safarini.

10. Usitumie pesa kwa kitu ambacho hakikuwa kwenye ratiba yako.

Jiulize kwanza kabla hujanunua,
“Bila kitu hiki, maisha yataenda au lah?”
Ukiona maisha yataenda bila kitu hicho, acha kukinunua. Tabasamu kisha ondoka.

12. Matumizi yako ya pesa yasizidi pato lako.

Unaweza kuwa una ndoto kubwa/matumizi makubwa ya pesa kuzidi pato lako.

Unapaswa kuwa bahili katika matumizi yako. Cheza na pato lako.
Fanya matumizi makubwa pale tu pato lako litakapoongezeka. Hii itakuepushia kushindwa kufanya baadhi ya mambo ya msingi na kisha ukajikuta unaishia kwenye madeni makubwa.
13. Una ndoto kubwa hapo baadae; labda kujenga nyumba, kununua gari, kununua kiwanja, simu nzuri hata pikipiki.

Usikurupuke, ukanunua kitu cha ndoto yako sasa eti tu sababu umekipata kwa bei ya punguzo.

Usichanganye kati ya mahitaji ya baadae na ya sasa.

Pesa unayotumia kutimizia ndoto sasa itumie kwa mahitaji ya sasa. Ndoto ibaki kuwa ndoto.

Hii itakuepushia kuingia katika madeni au kuishi kwa shida sababu ya tamaa.
Jipange taratibu kutimiza ndoto yako.

*Mwendo*

Jinsi ya kuepuka kunuka mdomo

Kuwa na harufu mbaya mdomoni ni kitendo kinachoweza kuathiri maisha ya mtu kimahusiano si kwa mpenzi tu bali marafiki na jamii kwa ujumla. Pia kuwa na harufu mbaya mdomoni uondoa haiba ya kupendwa kwani hata unapoongea wengi watakwepa kuongea moja kwa moja na wewe kwa sababu ya harufu mbaya inayotoka mdomoni mwako.

Chakula unachokula kina athiri hewa inayotoka mdomoni au sehemu nyingine za mwili wako. Baadhi ya vyakula vina matokeo mabaya sana kwa hurufu unayotoa mdomoni. Harufu mbaya mdomoni si ugonjwa wa kuambukiza haina haja kuogopa ukikutana na mtu mwenye harufu mbaya mdomoni kwamba atakuambukiza.

Pia tatizo kubwa ni kwamba watu wenye harufu mbaya mdomoni hawajijui kwamba wana harufu mbaya. Asilimia 85 – 90% ya tatizo la harufu mbaya mdomoni asili yake ni kinywa chenyewe. Pia kiwango cha harufu hutofautiana kutokana na muda (mchana, usiku na asubuhi).

Harufu nyingi mbaya mdomoni hutokana na vyakula vyenye asilia ya protein. Kuna zaidi ya aina 600 ya bacteria wanaoishi kwenye kinywa cha Binadamu (sehemu ya juu ya ulimi, fizi na kuzunguka meno).

 

KINACHO SABABISHA HARUFU MBAYA MDOMONI

 

Kutokuwa makini na usafi wa kinywa kama vile kupiga mswaki vizuri kunakoacha mabaki ya chakula ambayo huoza na kusababisha harufu mbaya mdomoni. (Wengi hupiga mswaki haraka haraka na kuacha mabaki ya chakula). Maambukizi ya magonjwa kama vile fizi kutoka damu, mfumo wa upumuaji na kisukari. Kinywa kuwa kikavu kutokana na madawa (medications) Kuvuta sigara, kunywa kahawa, ulaji wa vyakula vyenye viungo vikali kama vile vitunguu maji au thaumu.

 

NAMNA YA KUJUA KAMA UNA HARUFU MBAYA MDOMONI

 

Wanasayansi wamekiri kwamba ni ngumu sana mtu kujijua mwenyewe kama ana harufu mbaya kwa sababu ya mazoea (habituation).
Ni rahisi sana kutambua harufu kutoka kwenye kinywa cha mtu mwingine. Unaweza kutambua kama una harufu mbaya mdomoni kwa kumuuliza mtu unayemuamini.
Pia unaweza kujua harufu mbaya kwa kulamba nyuma ya kiganja na kunusa, wengine hupumua mbele ya kioo na kunusa. Pia unaweza kutumia kijiti cha kuchokonolea meno na kukinusa. Kisayansi unaweza kutumia vifaa kama Halimeter, Gas Chromatography na BANA Test.

NAMNA YA KUJILINDA NA HARUFU MBAYA MDOMONI (TIBA) 

 

Kula vyakula vyenye afya na vyakula ambavyo wakati unakula vinaweza kusafisha kinywa vizuri. Kusafisha meno mara kwa mara au kwa uchache mara mbili kwa siku asubuhi na baada ya mlo wa usiku, hii usaidia kuondoa au kujikinga na harufu mbaya mdomoni. Vilevile unashauriwa kutumia KISAFISHA ULIMI (tongue cleaner) kusafishia ulimi wako. Tumia bazooka (chewing gum) ambazo husaidia kuongeza kiasi cha mate kwenye kimywa kilichokauka. Baadhi ya gums zina viungo vinavyoondoa harufu mbaya mdomoni na zingine husafisha kinywa na bacteria wanaosababisha harufu mbaya. Tumia dawa ya kusukutua mdomoni (mouthwash) kabla ya kulala usiku. Kuwa makini na afya ya kichwa chako kama vile kupiga mswaki vizuri, kuondoa mabaki ya vyakula kwenye meno na kumuona daktari kila unapoona una Matatizo ya meno au kinywa au kila baada ya miezi sita kwa uchache.
Kuhakikisha unakunywa maji ya kutosha kila siku angalau glass mbili za maji.
Mwone daktari wako ukiona una tatizo la harufu mbaya mdomoni.

NAMNA YA KUJIKINGA NA KUONDOA HARUFU MBAYA MDOMONI!

Watu wengi husumbuliwa na tatizo la kunuka mdomo bila hata kujijua hivyo kuwa kero kwa wenzao na wakati mwingine hujishushia hadhi mbele ya jamii. Mara nyingi ugonjwa wa kunuka mdomo (Halitosis) husababishwa na uchafu wa kinywa na ulaji wa vyakula usiosahihi lakini ni tatizo linalotibika.

Ni rahisi kulizuia na kuliondoa tatizo la kunuka mdomo iwapo utaamua kufuata kanuni za usafi wa kinywa na unywaji wa maji kwa kufuata kwa makini muongozo ufuatao:

KUPIGA MSWAKI

Kitu cha kwanza kufanya ni kupiga mswaki kwa ukamilifu kila uamkapo asubuhi. Wakati wa kupiga mswaki, utatakiwa siyo tu kusugua meno, bali pia ulimi, sehemu ya katikati hadi karibu na koromeo kwa kusugua vizuri.
Vile vile kila uamkapo baada ya kulala mchana au jioni, hakikisha unapiga mswaki, kwani bakteria wa kinywani, hutawala kinywa kila ulalapo. Mara baada ya kupiga mswaki na kusugua ulimi sawaswa, hakikisha unasukutua vizuri kwa maji, kwani hapa ndipo baadhi ya watu hukosea kwa kupiga mswaki bila kusukutua kwa maji.

KUNYWA MAJI MENGI

Maji ni muhimu sana karibu kila eneo la mwili wa binadamu. Unywaji wa maji ya kutosha kila siku utakusaidia kudhibiti na hatimaye kuondoa tatizo la kunuka mdomo. Unywaji wa maji mengi ni muhimu, hasa kwa wale watu wenye ugonjwa wa kukauka midomo (xerostomia).

Mara nyingi harufu itokayo mdomoni, hutokea tumboni na siyo kinywaji peke yake kama unavyoweza kudhani. Hivyo, kama tumbo litakuwa chafu, hata kama utasafisha kinywa vizuri bado harufu mbaya inaweza kuendelea kutoka. Harufu mbaya ya tumboni hutokea pale tumbo linapokuwa chafu kutokana na kutopata choo kwa muda mrefu. Miongoni mwa mambo yanayochangia kukosekana kwa choo kwa muda mrefu ni pamoja na tabia ya kutokunywa maji ya kutosha kwa siku, hivyo hakikisha unakunywa maji, kiasi kisichopungua lita moja na nusu hadi mbili au zaidi, kutegemeana na kazi unazozifanya.

Ukiwa na tatizo la kukaukiwa maji mwilini kila mara, mwili hujaribu kutumia njia zake za kiasili kupunguza uzalishaji wa mate ili kuhifadhi maji kwa ajiili ya matumizi mengine, kitendo hicho huchangia kunukisha mdomo kwa sababu ndani ya mate huwa kuna kinga muhimu dhidi ya baktetria wanaonukisha kinywa.

Kwa upande mwingine, ili kuzuia kinywa kunuka pale mdomo unapokuwa umekaukiwa na mate, ni vizuri kutafuna vitu kama bazooka (chewing gum) yoyote ili kuzalisha mate ambayo huhitajika katika kudhibiti bakteria.

MWISHO:

Hakikisha unasukutua sawaswa baada ya kula chakula chochote, hata kama ni juisi isipokuwa unapokunywa maji tu ya kawaida. Bila shaka, ukizingatia haya, tatizo ulilonalo la kunuka mdomo litataoweka na kubaki historia.

Padri Akimbia wakati wa kuungamisha, chanzo ni hiki

Padri alikuwa amekaa katika confession booth kanisani
peke yake.
Mara kukaingia jamaa mmoja akapiga magoti upande wa
pili, akafanya ishara ya msalaba kisha akaanza kuungama
{confess}
“Padri nimekuja kuungama dhambi zangu, leo nimefanya
dhambi kubwa sana.”
Padri, “Endelea…”

“Bosi wangu aliniita nyumbani kwake, akaniambia
amegundua nimeiba shilingi millioni 100 kazini. Akasema
nisipozitoa atanipeleka polisi, sa kwa ukweli mi naogopa
kufungwa.
Nikatazama huku na huku nikagundua tuko wawili peke
yetu,nikatoa bastola nikamuua….. Yesu atanisamehe?”

Padri: “Utasamehewa.”
“Basi wakati nataka kuondoka nikasikia mlango
unafunguliwa kutazama, Loh! Mke wa bosi, alipoona
kilichotokea akasema anapiga polisi simu.
Kutazama huku na huku nikagundua tuko wawili peke
yetu, nikamuua na yeye pia… Yesu atanisamehe hilo?”
Padri: “Utasamehewa.”

Nikatoka nje, nikawasha gari niondoke, lakini mlinzi
akakataa kunifungulia, ati amesikia mlio wa
bastola. Nikaona ataniletea kizuizi huyu.
Nikatazama huku na huku nikagundua tuko wawili peke
yetu, nikamuua….. Yesu atanisamehe?”
Padri:”Utasamehewa.”

“Nikajifungulia geti mwenyewe nikaenda
nyumbani, wakati napanga kuja kuungama mtoto wa bosi
akabisha hodi, nikawaza mambo gani tena, akasema alirudi
nyumbani na kukuta yaliyotokea akanionesha diary ya
babake, inayoonesha nilikuwa na appointment naye
wakati nilipomuua. Nikamuuliza nani mwingine anayejua?
Akasema ameanzia kwangu kisha anaenda polisi.

Nikatazama huku na huku nikakuta tuko wawili peke
yetu, nikamuua….. Yesu atanisamehe na hilo?”

Kimyaa….
“Padri yesu atanisamehe?”
kimya….

Jamaa akatazama kwenye confession booth padri
hayupo, lakini kwenye kona moja akaona kabati la nguo
za mapadri linatikisika. Kufungua akaona padri kajificha ndani anatetemeka huku akitokwa na jasho.

Jamaa, “Sasa baba mbona umekimbia?”
Padri kwa taabu akajibu, “Nilitazama huku na huku
nikagundua tuko wawili peke yetu…….”

Mapishi ya Wali Wa Nazi Wa Adesi, Bamia Na Mchuzi Wa Kamba

Mahitaji

Mchele – 2 vikombe

Adesi -1 ½ vikombe

Nazi ya unga – 1 Kikombe

Maji (inategemea mchele) – 3

Chumvi – Kiasi

Vipimo Vya Bamia:

Bamia – ½ kilo

Vitunguu maji – 2 vya kiasi

Nyanya iliyosagwa – 1 kubwa

Nyanya ya kopo – 2 vijiko vya chai

Pilipili manga – ½ kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika:

Wali wa adesi

Osha na roweka mchele na adesi .
Chuja nazi kwa vikombe 3 vya maji tia chumvi kisha weka jikoni.
Tui la nazi likishachemka tia mchele na adesi pamoja. Punguza moto, funika wali upikike kwa moto mdogo mpaka ukauke vizuri.

Bamia

Katakata bamia vipande vya kiasi/ Katakakata vitunguu weka kando.
Katika sufuria tia mafuta na kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi.
Tia nyanya ilosagwa na nyanya ya kopo na pilipili manga na chumvi.
Kisha Tia bamia punguza moto mdogo mdogo mpaka ziwive.

Vipimo: Mchuzi Wa Kamba

Kamba – 1Lb

Vitunguu vilokatwa katwa – 2

Nyanya ilokatwa katwa – 2

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 Kijiko cha chai

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 Kijiko cha chai

Bizari ya mchuzi (curry powder) – ½ Kijiko cha chai

Haldi – bizari ya manajano – ½ kijiko cha chai

Nyanya ya kopo – ½ Kijiko cha chai

Ndimu – 1

Chumvi – Kiasi

Mafuta ya kukaangia – 2 Vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Kaanga vitunguu kidogo hadi vilainike,
Tia nyanya, thomu na piilipili mbichi. Endelea kukaanga, tia nyanya ya kopo, chumvi, bizari zote.
Tia tia kamba na huku unakoroga mpaka wabadilike rangi na kuwiva. Kamulia ndimu na mchuzi uko tayari.

Mapishi ya Wali wakukaanga

Mahitaji

Mchele (Basmati rice) 1 kilo
Vitunguu (chopped onion) 2 vikubwa
Garlic powder 1/2 kijiko cha chai
Njegere (peas) 1 kikombe
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Coriander powder 1/2 kijiko cha chai
Cumin seeds 1/2 kijiko cha chai
Mafuta ya kupikia 2 vijiko vya chakula
Chumvi kiasi

Matayarisho

Osha kisha loweka mchele kwa muda wa dakika 5 na kisha uchuje maji na uweke pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu mpaka viwe vya brown na kisha tia spices zote.Zikaange kwa muda wa dakika 3 kisha tia mchele na uchanganye vizuri na spice.Ukaange mchele pamoja na spice uku ukiwa unageuzageuza kwa muda wa dakika 5. Baada ya hapo tia maji ya moto(kiasi ya kuivisha wali) na chumvi kisha ufunike. Upike mpaka uive kisha malizia kwa kutia njegere na uchanganye vizuri baada ya dakika 2 uipue utakuwa tayari kwa kuliwa.Unaweza kuula kwa mboga yoyote uipendayo

Ziara za kushtukiza zinachekesha sana

Mimi Nimecheka sana
👇👇👇👇👇👇👇👇👇👇

ZIARA ZA KUSHTUKIZA😀😀
Mimi ni msomaji mzuri wa magazeti, na msikilizaji mzuri wa redio, huwa naangalia luninga mara chache sana kama nikibahatika kupita mahala kuna luninga. Sasa wiki hii nimesikia mengi kuhusu hizi ziara za kushtukiza za viongozi wetu, nikaona hili ni jambo zuri tena linafaa kuigwa na sisi wananchi wapenda maendeleo. Nikaona nijipange na mimi nifanye ziara kadhaa za kushtukiza katika sehemu mbalimbali zinazonihusu.

Nikaona nianze na ziara ya kushtukiza pale shuleni kwa huyu mwanangu, maana kila siku anakunywa chai na kuondoka na daftari zake na mie sijawahi kwenda shuleni kwao toka nilipomuandikisha shule mwezi Januari. Nilifika shuleni na kumuona mwalimu mkuu, ambae alianza kutetemeka nilipomuambia kuwa nimekuja pale kwa ziara ya kustukiza, sijui alidhani mi ni mmoja wa Mawaziri wapya, maana nilimuona jasho linamtiririka ghafla. Akanikaribisha ofisi yake iliyokuwa na vitabu kila kona, na kuita waalimu wote na kunitambulisha kuwa ni kiongozi nimekuja kwenye ziara ya kustukiza.

Nilipojitambulisha kuwa ni mzazi, waalimu wote nikawaona waanza kupumua kwa raha. Nikawaambia kuwa mimi nina mwanafunzi pale na nilikuja ziara ya kustukiza kujua maendeleo yake. Baada ya mwalimu mkuu kusaka jina la mwanangu nae akanambia, “Mzee huyu mtoto hajaja shule mwezi wa tatu sasa, tulijaribu kukutafuta ikashindikana, hatujui yu wapi” Jasho likaanza kunitoka mimi, yule mtoto kila asubuhi nampa nauli anaenda shule, na mara nyingi ananiomba michango kumbe hata shule haji. Niliondoka bila kuaga presha ikiwa juu.

Nikaona niende kwenye genge la mke wangu nae nikamfanyie ziara ya ghafla nimhadithie mambo ya mwanae, nilipofika pale nikakuta kuna mdada mwingine anauza genge. Nikamsalimu, na kumuuliza mwenye genge ntampataje, jibu lake lingeniua kama ningekuwa si mkakamavu, “Mume wake kaja kumchukua na gari wameenda kununua shamba Bagamoyo”. Nikaondoka nimechanganyikiwa, nikajuwa hapa dawa yangu moja tu, nayo ni Sabrina, mtoto wa Kinyaturu pale ambapo nikipata maudhi huwa naenda kubembelezwa.

Nikatwanga mguu kwa Sabrina nae nikamfanyie ziara ya ghafla ili anipoze moyo. Nilipogonga mlango wa chumba chake akatoka mbaba wa miraba minne, akanisalimia kwa upole, “Salama kaka unasemaje?” Jibu likanitoka “Samahani mie nilimkopesha huyu dada wa chumba hiki vitenge, nilikuja kuuliza kama ameshapata hela yangu” Ziara za kushtukiza zinataka moyo wa chuma jamani

Kilimo kizuri cha pilipili hoho

Pilipili hoho ni zao la jamii ya pilipili isiyo kali, tunda lake ni nene kiasi la duara pia linaweza kuwa lililochongoka. Pilipili hoho hutumika katika kutengeneza rangi za asili za vyakula ambazo kwa sasa hupendwa zaidi kuliko zile zinazotokana na kemikali na pia huongeza ladha na harufu katika vyakula. Hivyo hutumika katika viwanda vya kusindika vyakula, kwa mapishi ya nyumbani na hata katika viwanda vya vipodozi kama rangi ya mdomo, uso n.k. Ina virutubisho muhimu vinavyohitajika mwilini kama madini ya chuma, vitamin A na C.

Hali ya hewa

Hoho hustawi vema katika maeneo ya usawa wa bahari hadi mwinuko wa mita 2,000 yenye mvua ya wastani wa mm.600-1,250 na wastani wa joto la nyuzi za sentigredi 21 hadi 24.

Udongo

Udongo wa tifitifu wenye rutuba, usiotuamisha maji na wenye hali ya uchachu (pH) kati ya 5.0-6.5 hufaa zaidi. Umwagiliaji ni muhimu pale mvua inapokuwa chache.

Jinsi ya kulima hoho

Kitalu

Tayarisha kitalu kabla ya msimu wa mvua. Andaa vizuri matuta manne yenye urefu wa wastani wa mita 10 kila moja na upana wa mita moja (1) ili kustawisha miche inayotosha ekari moja. Chagua eneo katika ardhi isiyo na mtelemko mkali na yenye rutuba ya kutosha. Ardhi iwe imepumzishwa bila kuoteshwa mazao ya jamii ya pilipili, biringanya, nyanya, n.k. ili kuepukana na mashambulizi ya wadudu na magonjwa.

Upandaji wa mbegu

Mwagilia maji ya kutosha siku moja kabla ya kusia mbegu na endelea kunyweshea kulingana na hali ya hewa na hali ya udongo. Sia mbegu kwenye, mstari, nafasi kati ya mstari na mstari ni sm 10 na kina cha sm1. Kiasi cha mbegu cha nusu kilo kinatosha eneo la hekta moja. Weka matandazo kwenye kitalu au tumia nailoni nyeusi ili kuhifadhi unyevunyevu na kuzuia uotaji wa magugu.
Mbegu ambazo hutumika ni chotara ambazo huuzwa kwenye maduka ya pembejeo za kilimo nchi nzima. Haishauriwi kutumia mbegu kutoka zao la msimu uliopita kwani ubora wa paprika utaharibika na hivyo kuharibu soko unashauriwa kununua mbegu bora.

Utayarishaji wa shamba

Shamba lilimwe vizuri na kuweka matuta ili kuhifadhi unyevunyevu na kurahisisha umwagiliaji. Matuta yanaweza kuwa makubwa au madogo kulingana na matakwa ya mkulima. Matuta makubwa hupandwa mistari miwili na matuta madogo hupandwa mstari mmoja.

Upandaji wa miche

Mbegu huoteshwa na kukuzwa kitaluni kwa muda wa wiki 6-8 na miche hupandikizwa shambani ikiwa na urefu wa sm.6-10. Mwagilia maji kitaluni kabla ya kuhamisha miche. Panda shambani kwa nafasi ya sm.75-90 kati ya miche kwa sm.90-105 kati ya mistari, wastani wa miche 12,500 itapatikana kwa hekta. Weka samadi shambani tani 25-37 kwa hekta wiki 1-2 kabla ya kupandikiza miche, au kilo 560-670 za NPK (mbolea ya viwandani) kwa hekta kwa uwiano wa 4:7:7 katika udongo usio na rutuba ya kutosha.

Utunzaji wa shamba

Tumia mbolea kiasi cha kilo 140 za SA au CAN kwa hekta hasa wakati mmea inapotoa matunda ili kupata matunda makubwa na kuvuna kwa muda mrefu (hadi miezi 10). Palizi ifanyike mara magugu yanapotokea shambani. Umwagiliaji maji ufanyike kama ilivyo kwa mazao mengine kama nyanya.

Wadudu Waharibifu

  • Funza wa vitumba
  • Vidukari
  • Kidomozi (Leaf miner)

Kudhibiti: Tumia dawa aina ya permethrin

Magonjwa

  • Kuoza mizizi
  • Mnyauko wa majani
  • Batobato

Kudhibiti: Choma nyasi kwenye kitalu kabla ya kusia mbegu.
Badilisha mazao yasiyo ya jamii ya pilipili.

Uvunaji

Matunda ya kwanza huwa tayari kuvunwa kuanzia miezi 2-3 baada ya kupandikizwa; matunda yaliyokomaa vizuri na kuwa na rangi nyekundu ndiyo huvunwa. Matunda 30-80 hupatikana kwa mmea mmoja.
Ubora wa hoho huongezeka kutegemeana na kiwango cha rangi yake ikiwa ni nyekundu njano au kijani. Mazao kiasi cha tani 3.5 kwa hekta hupatikana. Baada ya kuvuna mwagilia maji, piga dawa (kama ni muhimu) na weka mbolea kuongeza uzalishaji unaofuata.

Usindikaji

Hoho huuzwa ikiwa bado fresh tofauti na jamii nyingine za pilipili ambazo zinaweza kukaushwa na kusindikwa kasha kuuzwa baadae.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About