Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Wali Wa Kukaanga Kwa Kidari Cha Kuku (Chicken Breast) Wa Kukausha

Viambaupishi

Vipimo vya Wali:

Mchele 3 vikombe

*Maji ya kupikia 5 vikombe

*Kidonge cha supu 1

Samli 2 vijiko vya supu

Chumvi kiasi

Hiliki 3 chembe

Bay leaf 1

Viambaupishi: Kuku

Kidari (chicken breast) 1Kilo

Kitunguu 1

Tangawizi mbichi ½ kipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) 7 chembe

Pilipili mbichi 3

Ndimu 2

Pilipilimanga 1 kijiko cha chai

Mdalasini ½ kijiko cha chai

Jira/Cummin ya unga 1 kijiko cha chai

Maji ¼ kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

Wali:

Osha na roweka mchele kisha weka sufuria katika moto tia samli ipashe moto.

Tia hiliki, bay leaf, kaanga, kisha tia mchele ukaange kidogo.

Tia maji, chumvi na kidonge cha supu, upike wali kama unavyopika pilau.

*Maji kisia kwa kutegemea mchele ulivyo.

  • Unaweza kutumia supu yoyote badala ya kidonge.

Kuku:

Katakata kidari cha kuku vipande vya kiasi, weka katika sufuria, tia ndimu, bizari zote, chumvi.

Katakata kitunguu vipande vidogodogo, pilipili, na kitunguu thomu (chopped), tia katika kuku.

Chuna tangawizi mbichi tia katika kuku. Changanya vitu vyote vizuri.

Tia maji kiasi ¼ kikombe tu kiasi cha kumkaushia kuku. Weka katika moto mpike huku unageuzageuza. Anapokaribia kukauka epua akiwa tayari kuliwa na wali (na saladi upendayo)

Mapishi ya Ndizi mzuzu

Mahitaji

Ndizi tamu (plantain) 3-4
Tui la nazi (coconut milk) kikombe 1 cha chai
Sukari (sugar) 1/4 ya kikombe cha chai
Hiliki (Ground cardamon) 1/4 ya kijiko cha chai
Chumvi (salt) 1/4 ya kijiko cha chai

Matayarisho

Menya ndizi kisha zikwangue utomvu wote. Baada ya hapo zikate kati (kiurefu) na kisha kata tena kati katika kila ndizi vitoke vipande 4. baada ya hapo toa moyo wa katikai wa ndizi. Zioshe na kisha zikaushe maji na uziweke kwenye sufuria ya kupikia. Baada ya hapo tia tui la nazi, sukari, chumvi na hiliki. Ziinjike jikono na uziache zichemke uku ukiwa unalikoroga tui ili lisikatike. Baada ya dakika 10 tui la nazi litakuwa limepungua na kubaki kidogo na hapo ndizi zitakuwa zimeshaiva. Ziache zipoe na zitakuwa tayari kwa kuliwa. Zinaweza kuliwa kama mlo (main meal) au kitinda mlo (dissert) au mlo wa pembeni (side dish) haswa kwa futari.

Mapishi ya Samaki wa kuokwa

Mahitaji

Mackerel 2
Kitunguu swaum na tangawizi (ginger and garlic paste) 1 kijiko cha cha kula
Pilipili iliyo katwakatwa (chopped scotch bonnet ) 1/2
Limao (lemon) 1/2
Chumvi (salt) kiasi
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Coriander powder 1/2 kijiko cha chai
Mafuta 1 kijiko cha chai

Matayarisho

Safisha samaki kisha wakaushe maji ( ukipenda unaweza kuwakata kati au ukawapika wazima) Baada ya hapo wakate mistari kila upande ( ili spaces ziweze kuingia ndani) kisha waweke kwenye bakuli na utie spice zote. Wachanganye vizuri kisha waweke frijini na uwaache wamarinate kwa muda wa masaa 3. Baada ya hapo washa oven kisha wapakaze mafuta na uwafunge kwenye foil na uwatie kwenye oven kwa muda wa dakika 20. Baada ya hapo fungua foil na uwaache kwenye oven kwa muda wa dakika 10 ili wapate kukauka kidogo. Na hapo watakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuwala kwa kitu chochote upendacho.

Madhara ya kula yai bichi

Yai bichi linaweza kuwa na vijidudu viitwavyo kwa kitaalamu “SALMONELLA” vinavyoweza kusababisha tumbo kuuma, kichefuchefu na pia kuharisha.
Vijidudu ya “Salmonella” vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa watoto, wazee na wale wenye hali dhaifu ya kimwili kama wagonjwa wa UKIMWI.

Pia yai bichi lililowazi linaweza kuwa zalio zuri la vimelea vya maradhi mbalimbali. Inashauriwa kupika yai mpaka liive kabisa, na kuhakikisha kwamba hakuna ute unaoteleza.

Kama ni yai la kuchemsha, lichemshwe kwa dakika kumi zaidi baada ya maji kuchemka. Pia ni muhimu kuhakikisha kwamba vyombo vilivyotumika k u k o rogea yai bichi vinaoshwa kwa maji na sabuni kabla ya kuvitumia tena kwa matumizi mengine ili kuepuka maradhi.

Jinsi ya kupika Pilau Ya Nyama Ya Ng’ombe Na Nyanya

Viambaupishi

Mchele (Basmati) 3 vikombe

Nyama ya ngo’mbe 1 kg

Pilipili boga 1 kubwa

Nyanya 2 kubwa

Vitunguu maji 2 vikubwa

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa 1 kijiko cha supu

Tangawizi 1 kijiko cha chai

Ndimu 1

Mafuta ya kupikia ½ kikombe

Mdalasini ½ kijiko cha chai

Binzari nyembamba 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ½ Kijiko cha chai

Hiliki ½ Kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

Loweka mchele wako katika chombo

Chukuwa nyama na ioshe vizuri na itie thomu, tangawizi, ndimu, pilipili manga na chumvi kiasi

Iweke jikoni hadi ikauke maji na kuwa imewiva huku ukiikaanga kaanga kwa hayo hayo mafuta yake hadi kuwa rangi ya hudhurungi

katakata Vitunguu na nyanya weka pembeni

Chukua pilipili boga, thomu, tangawizi na visage katika mashine ya kusagia

Weka sufuria pembeni na utie mafuta, subiri yapate moto

Kisha tia vitunguu na vikaange hadi kuwa hudhurungi na tia nyanya

Kisha mimina mchanganyiko wako ulio usaga wa pilipili boga, thomu na tangawizi

Koroga kwa dakika kadhaa Kisha mininia nyama uliyokuwa tayari, maji kiasi na chumvi wastani na subiri maji hayo yachemke

Weka mchele humo na koroga kiasi na onja chumvi kama ipo sawa au kama ndogo unaweza kuongeza

Funika na punguza moto na uache uive taratibu

Baada ya kukauka maji kabisa basi ugeuze na subiri tena kwa dakika kama mbili na tayari kuliwa.

Mapishi – Mayai Mchanganyiko, Tosti na Soseji

Karibu tena jikoni, leo tunaandaa vitafunwa kwa ajili ya kifungua kinywa asubuhi.

Mahitaji

Mayai 3
Soseji 2
Mkate slesi 2
Mafuta ya kupikia vijiko 2
Chumvi

Matayarisho

Piga piga mayai vizuri kwenye bakuli na weka chumvi kidogo kisha weka kikaango kwenye moto na mafuta kidogo.

Kikisha pata moto miminia mchanganyiko wa mayai na uanze kukorogo pale tu unapomiminia, endelea kukoroga hadi uone yanakuwa magumu na kuanza kuiva. Pika kwa kiwango unachopendelea na kusha epua na weka kwenye sahani.

Weka mafuta kijiko kimoja kwenye kikaango na kisha weka soseji zako na uzipike kiasi pande zote kisha epua na weka pembeni.

Weka slesi za mikate kwenye toster na zikiwa tayari unaweza weka siagi ili kuongeza ladha na mvuto.
Andaa mlo wako pamoja na juice, maziwa au chai.

Mapishi ya Mchuzi wa kambale

Mahitaji

Kambale 2
Nazi kopo 1
Nyanya kopo 1
Vitunguu 2
Curry powder 1 kijiko cha chai
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Binzari nyembamba ya unga 1/2 kijiko cha chai
Swaum/ tangawizi 1 kijiko cha chakula
Giligilani kiasi
Limao 1/2
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Loweka samaki katika maji ya moto kwa muda wa muda wa nusu saa.Baada ya hapo Saga pamoja nyanya, vitunguu, swaum na tangawizi kisha vibandike jikoni na uvipike mpaka maji yote yakauke kisha tia mafuta. Pika mpaka nyanya zitengane na mafuta kisha tia spice zote.Zipike kwa muda mdogo kisha tia tui la nazi, maji kiasi, samaki, pilipili nzima, chumvi na kamulia limao. Pika mpaka tui la nazi litakapoiva na samaki pia wawe wameiva na mchuzi ubakie kiasi. Baada ya hapo ipua kisha tia giligilani iliyokatwa na mchuzi utakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuulia kwa chochote kile upendacho. Mi hupendaga kuulia na ugali mlaiiini au na wali pia.

Mapishi ya wali wa Kiafrika Mangaribi

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 2 na 1/2)
Vitunguu (onion 2)
Nyanya ya kopo (tin tomato kopo 1)
Tangawizi (ginger paste kijiko 1 cha chakula)
Kitunguu swaum (garlic paste kijiko 1 cha chakula)
Paprika (kijiko 1 na 1/2 cha cha chai)
Pilipil (scotch bonnet pepper 1)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Maggi cubes 3(unaweza kutumia yenye ladha ya chicken, beef au vegetable. Inategemea unasevu na mchuzi wa aina gani)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka mchele kwa muda wa dakika 10.Katakata vitunguu kisha weka pembeni, saga pamoja nyanya ya kopo,pilipili, tangawizi na kitunguu swaum kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikiiva tia curry powder, maggi cubes, chumvi na paprika na uchanganye vizuri. Kisha tia mchanganyiko wa nyanya na uupike mpaka uive. Baada ya hapo tia mchele na maji na uupike mpaka ukaribie kuiva kisha ugeuze na umalizie kwa kutia njegere na umalizie kuupika mpaka uive. baada ya hapo utakuwa tayari kuseviwa na mboga yoyote kama kuku, nyama, samaki au assorted meat (Mchanganyiko wa utumbo, makongoro na nyama), Hapo mimi nili-save na mchuzi wa kuku wa kienyeji.

Mapishi ya Pilau Ya Sosi Ya Soya Na Mboga

Viambaupishi

Kuku (mkate mkate vipande) 1

Mchele wa Basmati (rowanisha) 3 magi

Mdalasini 1 mchi mmoja

Vitunguu maji (vilivyokatwa vyembamba) 6

Mchanganyiko wa mboga za barafu 1 magi

(karoti, mahindi, njegere)

Kabichi (iliyokatwa katwa nyembamba) 1 magi

Pilipili mbichi (iliyosagwa) 3

Pilipili boga iliyokatwa vipande vidogo vidogo 1

Pilipili manga 1 kijiko cha chakula

Chumvi 1 kijiko cha chakula

Sosi ya soya (soy sauce) 5 vijiko vya chakula

Kotmiri iliyokatwa katwa 1 magi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa 2 vijiko vya chakula

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Tia mafuta ndani ya karai. Yakipata moto kiasi, mimina vitunguu maji na mdalasini 1 mzima kaanga. Itachukua muda kidogo. Kaanga mpaka viwe rangi ya hudhurungi (brown). Viepue na uweke kando.

2. Ndani ya sufuria kubwa, mimina kuku, chumvi, thomu na tangawizi, sosi ya soya, pilipili manga, pilipili mbichi, chemsha mpaka kuku awive na maji yakauke.

3. Changanya vitunguu ulivyokaanga, kabichi, pilipili, mboga, kotmiri, mchanganyiko wa mboga za barafu na weka kwa muda wa dakika tano au kumi. Tia na mafuta kidogo uliyokaangia vitunguu .

4. Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja. Ukishauchuja umwagie katika masala ya kuku.

5. Nyunyizia mafuta kidogo uliokaangia vitunguu.

6. Weka moto mdogo mpaka wali ukishawiva. Uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa.

KIDOKEZO:

Unaweza kuupika wali huo ndani ya jiko, yaani badala ya kutia masala kwenye sufuria ukayatia katika bakuli au treya ya jiko (oven), kisha ukamwagia wali uliouchuja humo na kuupika kaitka moto wa 400-450 Deg kwa muda wa dakika 15-20.

Mapishi ya Wali, Mchuzi Wa Nazi Wa Samaki Nguru

Mahitaji

Mchele – 3 vikombe

Samaki Nguru (king fish) – 5 vipande

Vitunguu – 2

Nyanya/tungule – 4

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi zito – 2 vikombe

Pilipili mbichi – 5-7

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 7-9 chembe

Kotmiri – 1 msongo (bunch)

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 2-3

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha samaki, kata vipande kiasi weka kando.
Katakata kitunguu na nyanya vipande vidogo vidogo sana (crush) .
Katakata kotmiri weka kando.
Saga pamoja, pilipili mbichi, kitunguu thomu, ndimu na chumvi.
Changanya pamoja na bizari ya samaki kisha paka katika vipande vya samaki acha kidogo vikolee.
Weka mafuta katika sufuria au karai, kaanga vitunguu kidogo tu kisha tia nyanya/tungule endelea kukaanga hadi vilainike na kupondeka.
Tia kikombe kimoja na nusu cha tui la nazi, kisha tia vipande vya samaki na masala yake, acha mchuzi uchemke samaki aive. Ongeza chumvi, ndimu, pilipili ikihitajika.
Ongezea tui lilobakia acha motoni kwa daika chache tu.
Epua mwagia kotmiri mchuzi ukiwa tayari.

Pika wali wa maji/mweupe kama kawaida utolee na mchuzi.

Mapishi ya Kabichi

Mahitaji

Kabichi 1/2 kilo
Nyanya ya kopo 1/2
Kitunguu 1
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Kwanza kabisa bandua magada ya juu ya kabichi, kisha ioshe na uikaushe maji baaba ya hapo katakata kabichi (inapendeza zaidi kama ikikatwa nyembamba) kisha saga pamoja nyanya na kitunguu. Baada yahapo tia katika sufuria ya kupikia, ipike mpaka maji yote yatakapokauka kisha tia chumvi, curry powder na mafuta pika kwa muda kiasi kisha tia kabichi na upunguze moto. Pika mpaka kabishi itakapoiva kisha ipua na itakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuila kwa wali au ugali.

Jinsi ya kutengeneza Bisikuti Za Kaukau Na Kahawa (Cocoa Coffee Biscuits)

MAHITAJI

Maji baridi – kikombe 1

Biskuti za kawaida – paketi 2

Kaukau (cocoa) – vijiko 3 vya kulia

Kahawa ya unga – kijiko 1 cha kulia

Njugu mchanganyiko zilokatwakatwa – kikombe 1

Sukari – kiasi upendavyo

MAANDALIZI

Changanya maji na kaukau na kofi na sukari
Katakata biskuti kisha tia paketi moja na nusu uchanganye vizuri.
Kisha nusu ya biskuti zilobakia katakata vipande vikubwa na weka juu ya mchanganyiko, kisha changanya kidogo tu.
Weka katika foil paper na zungusha (roll)
Kisha fungua umwagie njugu au mkassaraat zilosagwa
Kisha roll katika foil paper na uweke katika freezer mpaka igande
Kisha kata kata slices na iko tayari

Mapishi mazuri ya Chapati za maji

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour) ( 1/4 kilo)
Yai (egg 1)
Sukari (sugar 1/4 kikombe cha chai)
Chumvi (salt 1/4 kijiko cha chai)
Hiliki (ground cardamon 1/4 kijiko cha chai)
Maji kiasi
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Tia unga kwenye bakuli, kisha weka sukari, chumvi, hiliki na maji kiasi. Kisha koroga mpaka mchanganyiko wako uwe mzito. Baada ya hapo tia yai na ukoroge tena. hakikisha mchanganyiko hauwi mzito sana au mwepesi sana.Baada ya hapo onja kama kila kitu kimekolea. Injika chuma cha kupikia chapati (fry-pan) jikoni katika moto wa wastani. Baada ya hapo tia nusu kijiko cha chakula cha mafuta katika fry-pan na kisha yatandaze. Hakikisha chuma kinapata moto na weka upawa mmoja wa unga wa chapati na uutandaze mpaka uwe flat. Baada ya hapo subiri mpaka chapati ikauke juu na kisha igeuze upande wa pili tia mafuta kijiko 1 kikubwa cha chakula kwa upande wa chini na wa juu kisha uanze kuikandamiza kwa juu na kijiko ili iweze kuiva vizuri kwa chini. Ikisha kuwa ya rangi ya brown igeuze na upike upande wa pili kiasi kisha iipue na uiweke kwenye sahani yenye kitchen towel ili kukausha mafuta. Rudia hii process kwa unga wote uliobakia. Na chapati zitakuwa tayari

Mapishi mazuri ya Uji wa ulezi

Mahitaji

Unga wa ulezi (millet flour vijiko 3 vya chakula)
Maziwa fresh (milk 1/2 kikombe)
Sukari (sugar 1/4 ya kikombe cha chai)
Siagi (butter kijiko 1 cha chakula)
Maji (vikombe 4 vya chai) (serving ya watu wawili)

Matayarisho

Chemsha maji ya uji, Kisha koroga unga na maji ya baridi kiasi na uchanganye kwenye maji ya moto yanayochemka. Endelea kukoroga mpaka uchemke ili kuhakikisha uji haupatwi na madonge. Ukishachemka tia, maziwa, sukari na butter. Kisha acha uchemke kwa muda wa dakika 10 na hapo uji utakuwa tayari.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Ufuta Na Jam

VIAMBAUPISHI

Unga vikombe 2

Sukari ya kusaga 1/4 Kikombe

Siagi 250 gms

Jam kisia

Ufuta kisia

Vanilla 1 kijiko cha chai

MAPISHI

Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai, sukari na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.
Tia baking powder, na unga na changanya kwa mkono vizuri.
Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Bonyeza kila kiduara katikati kwa kidole, kisha weka jam, halafu juu yake paka mayai na unynyuzie ufuta.
Pika katika moto wa chini 350ºF kwa muda wa dakika 20-25.
Tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Kidheri – Makande

Mahitaji

Nyama (kata vipande vidogodogo) – ½ kilo

Maharage – 3 vikombe

Mahindi – 2 vikombe

Kitunguu – 1

Nyanya – 2

Kabichi lililokatwa – 2 vikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha chai

Vidonge vya supu – 2

Chumvi – kiasi

Mafuta -1au 2 vijiko vya chakula

Namna Yakutayarisha

Chemsha mahindi mpaka yawive na maji yakauke kiasi.
Chemsha maharage pembeni nayo mpaka yawive na maji yakaukie kiasi.
Tia mafuta kwenye sufuria anza kukaanga vitunguu , thomu na vidonge vya supu koroga kiasi.
Kisha mimina nyama iliyokatwa vipande acha ikaangike kidogo na chumvi.
Nyama ikishakaangika tia nyanya funika kwa moto mdogo mpaka nyama iwive.
Kisha mimina mahindi na maharage yaliyochemshwa na maji yake kiasi koroga mpaka ichanganyike na mwisho mimina kabichi funikia mpaka kabichi iwive onja chumvi kama imekolea
Halafu malizia kukoroga mpaka ichanganyike na ikaukie kisha pakua kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Cornflakes

MAHITAJI

Unga – 1 Kikombe

Sukari ya kusaga – 3/4 Kikombe

Siagi – 125 gms

Yai – 1

Baking powder – 1/2 kijiko cha chai

Zabibu kavu – 1/2 kikombe

Cornflakes iliyovunjwa (crushed) – 2 Vikombe

Vanilla – 1 kijiko cha chai

MAANDALIZI

Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.
Tia baking powder, zabibu na unga na changanya vizuri.
Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Weka cornflakes katika sahani ya chali (flat) na zungusha viduara humo kisha upange katika sinia ya oveni.
Pika katika moto wa 350ºF kwa muda wa dakika 20-25 hadi vigeuke rangi na viwive.

Mapishi ya Boga La Nazi

Vipimo

Boga la kiasi – nusu yake

Tui zito la nazi 1 ½ gilasi

Sukari ½ kikombe

Hiliki ½ kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Menya boga kisha katakata vipande vya kiasi.
Weka katika sufuri tia maji kiasi ya kuchemshia na kuwiva bila ya kubakia maji mengi.
Changanya tui na sukari na hiliki kisha mimina juu ya boga wacha katika moto dakika chache tu bila ya kufunika.
Epua mimina katika chombo likiwa tayari.

Mapishi ya Pilau Ya Mchicha

VIPIMO

Mchele – 3 Vikombe

Mchicha

Mafuta – 1/2 kikombe

Vitunguu maji – 2 vikubwa

Nyanya – 1

Viazi – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 3 vijiko vya supu

Vidonge vya supu (Stock cubes) – 3

Jiyrah (cummin powder) – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ya unga – 1 kijiko cha chai

Hiliki ya unga – 1/2 kijiko cha chai

Mdalasini – 1 kijiti

Maji (inategemea mchele) – 5 vikombe

Chumvi

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

1. Osha na roweka mchele.

2. Osha mchicha, chuja maji na katakata.

3. Katakata vitunguu maji, nyanya.

4. Menya na kata viazi vipande ukaange pekee vitoe weka kando.

5. Katika sufuria tia mafuta na kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi.

6. Tia thomu, bizari zote, kaanga kidogo kisha nyanya.

7. Tia mchicha kaanga kidogo kisha tia mchele, maji na vidonge vya supu, chumvi.

8. Koroga kidogo kisha tia viazi ulivyovikaanga, funika na acha uchemke kidogo katika moto mdogo mdogo.

9. Kabla ya kukauka maji, mimina katika chombo cha kupikia ndani ya oven (oven proof) au katika treya za foil, funika vizuri na upike ndani ya oven moto wa 400º kwa dakika 15-20 upikike hadi uive.

10. Ukishaiva epua na tayari kuliwa na kitoweo chochote upendacho.

Shopping Cart
3
    3
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About