Dondoo za Mapishi na Lishe

Jinsi ya kupika Baklawa Za Pistachio Na Lozi

VIAMBAUPISHI

Philo (thin pastry) manda nyembamba – 1 paketi

Siagi – ¼ Kikombe cha chai

Baking powder – 2 Vijiko vya chai

Pistachio/ lozi – 2 vikombe vya chai

Mafuta – ½ Kikombe

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 Vikombe vya chai

Maji – 2 ½ Vikombe vya chai

ndimu – ½ kijiko cha chai

JINSI YA KUANDAA

Tafuta treya iliyokuwa sawa na ukubwa wa hizo manda nyembamba (philo) au zikate hizo manda kwa ukubwa wa treya (mraba au mstatili)
Kisha yeyusha siagi changanya na mafuta.
Kisha panga manda moja pakaza mafuta juu yake kisha weka manda nyingine juu yake kisha pakaza mafuta tena weka manda nyingine juu yake, endelea kufanya hivyo mpaka ziwe kama sita au saba kisha nyunyizia pistachio na lozi halafu panga tena manda na mafuta manda na mafuta tena sita au saba kisha nyunyizia tena pistachio na lozi.
Panga namna hivyo mpaka treya ijae inapofika manda ya mwisho kata vipande vya mraba vidogodogo humo humo kwenye treya kisha nyunyizia mafuta yaliyobaki.
Washa moto wa oven 350°F kwa muda wa dakika 20 au hadi rangi ibadilike kidogo (isikauke sana)
Chemsha syrup yako kama shira ya majimaji lakini isiwe nzito sana ikishakuwa tayari mwisho tia ndimu acha ipoe kidogo kisha miminia juu ya treya yote halafu malizia kunyunyizia pistachio na lozi zilizobaki.
Zikishakuwa tayari zipange kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

ANGALIZO

Ukishatoa treya kwenye oven wacha ipoe kidogo na syrup yako pia wacha ipoe kidogo kabla hujamimina, ukitia ya motomoto zitalainika.
Manda nyembamba za baklawa zinauzwa tiyari madukani kwenye pakiti.

Namna ya kutengeneza Visheti Vya Nazi Na Njugu (Sudani)

VIAMBAUPISHI

Unga – 3 mug za chai

Samli – ½ mug ya chai

Maziwa – 1¼ mug ya chai

Baking powder – 2 vijiko vya chai

VIAMBAUPISHI VYA MJAZO

Njugu zilizomenywa vipande vipande – 2 vikombe cha chai

Sukari – ½ kikombe cha chai

Iliki – 1 kijiko cha chai

Nazi iliyokunwa – 2 vikombe vya chai

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 vikombe vya chai

Maji – 1 kikombe cha chai

Ndimu – 1

JINSI YA KUVIANDAA

1-Changanya unga na samli kisha tia baking powder na maziwa. Ukande ulainike kisha

uwache kama dakika 5 uumuke.

2-Kwenye bakuli nyingine changanya njugu, sukari na iliki.

3-Kata madonge madogo dogo sukuma kila donge duara jembamba, kisha tia kijiko cha mchanganyiko wa njugu juu yake ifunikie juu yake na ibane pembeni.

4-Panga kwenye treya isiyoganda (non stick) kisha choma kwenye oven kwa moto wa chini

(bake) 350° C kwa dakika kama 15-20.

5-Chemsha maji na sukari katika sufuria ndogo kisha tia ndimu acha ichemke mpaka inatenate unapoigusa.

6-Kwenye sahani ya chali mimina nazi iliyokunwa.

7-Vibiskuti vikiwa tayari vya motomoto chovea kwenye shira kisha zungushia katika nazi iliyokunwa,

panga kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

JINSI YA KUANDAA VILEJA

MAHITAJI

Unga wa mchele – 500g

Samli – 250g

Sukari – 250g

Hiliki iliyosagwa – 1/2 kijiko cha chai

Arki (rose flavour) – 1/2 kijiko cha chai

Baking powder – 1 kijiko cha chai

Mayai – 4

Maji ya baridi – 1/2 kikombe cha chai

MAANDALIZI

Saga sukari iwe laini kiasi, changanya unga wa mchele, baking powder, hiliki na sukari.
Pasha moto samli mpaka iwe nyepesi kama maji mimina kwenye ule mchanganyiko wa unga wa mchele, kisha uchanganye pamoja na arki.
Ongeza mayai yaliopigwa endelea kuchanganya mpaka unga umeanza kuchanganyika vizuri.
Ongeza maji ya baridi sana kama nusu kikombe tu ili uchanganyike vizuri.
Kata kwa design unayotaka viwe vinene visiwe kama cookies za kawaida kama ilivyo kwenye picha na ukipenda utaweka kidoto kwa kutumia zaafarani katikati ya kileja kama inavyoonesha hapo juu.
Choma kwa moto wa baina ya 300F na 350F kwa dakika 15 mpaka 20 visiwe vyekundu toa na tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Cornflakes

MAHITAJI

Unga – 1 Kikombe

Sukari ya kusaga – 3/4 Kikombe

Siagi – 125 gms

Yai – 1

Baking powder – 1/2 kijiko cha chai

Zabibu kavu – 1/2 kikombe

Cornflakes iliyovunjwa (crushed) – 2 Vikombe

Vanilla – 1 kijiko cha chai

MAANDALIZI

Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.
Tia baking powder, zabibu na unga na changanya vizuri.
Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Weka cornflakes katika sahani ya chali (flat) na zungusha viduara humo kisha upange katika sinia ya oveni.
Pika katika moto wa 350ºF kwa muda wa dakika 20-25 hadi vigeuke rangi na viwive.

MAPISHI YA LADU

VIAMBAUPISHI

Unga – 6 vikombe

Samli – ½kikombe

Baking Powder – ½kijiko cha chai

Maziwa- 1 kikombe

Maji -Kisia kiasi kama unga bado mzito

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 5 vikombe

Maji – 2 1/2 vikombe

Vanilla – 2 vijiko vya chai

Rangi ya orange – 1 kijiko cha chai

Iliki ya unga – 1 Kijiko cha chai

MAANDALIZI

Changanya unga wa dengu, samli, baking powder pamoja na maziwa katika mashine ya keki (cake mixer).
Ukisha changanya angalia kama mchanganyiko wako umekua mwepesi kidogo kuliko wa keki, kama bado mzito basi ongeza maji kiasi.
Kisha weka mafuta kiasi kwenye karai,weka na samli kikombe kimoja, weka kwenye moto wa kiasi.
Mafuta yakisha pata moto, chukua kijiko kikubwa cha matundu chota mchanganyiko wako na kijiko cha kawaida tia kwenye kijiko cha matundu. Hakikisha kijiko cha matundu kiwe juu ya karai ili mchanganyiko wako uchuruzike ndani ya mafuta yalio pata moto.
Pika ndani ya mafuta mpaka iwive, ila usiache ikawa brown.
Toa mchanganyiko ulowiva tia ndani ya shira uliyo pika. Hakikisha shira iwe imepoa kabla ya kutia mchanganyiko huo.
Endelea kupika mchanganyiko wako mpaka uishe, kila ukitoa katika mafuta hakikisha unatia ndani ya shira.
Ukishamaliza wote kanda huo mchanganyiko ulokua ndani ya shira mpaka uone shira yote imekauka (yaani iwe imeingia ndani ya mchanganyiko).
Tupia zabibu kavu na lozi zilizo katwa, changanya na mkono.
Wacha mchanganyiko katika bakuli, funika na foil mpaka siku ya pili.
Siku ya pili chukua mchanganyiko kiasi katika mkono tengeneza mviringo (round).

MAANDALIZI YA SHIRA

Katika sufuria, tia sukari, maji, iliki, vanilla na rangi.
weka kwenye moto wacha ichemke mpaka itowe povu (bubbles) juu.
Kisha toa povu, wacha shira kwenye moto kama dakika 3.
Hakikisha shira yako iwe inanata kiasi kwenye vidole, lakini iwe nyepesi kidogo kuliko shira ya kaimati.

Shopping Cart