Mafundisho ya Katekisimu

Je, Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha umuhimu wa sala katika maisha ya Kikristo?

Sala ni sehemu muhimu katika maisha ya Kikristo. Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha umuhimu wake katika maisha ya waumini. Kupitia sala, tunaweza kuwasiliana na Mungu na kumwomba msaada katika maisha yetu. Sala inatusaidia kupata amani ya nafsi na kuimarisha imani yetu. Ni kwa sababu hii Kanisa Katoliki linahimiza waumini wake kusali mara kwa mara.

Katika Biblia, tunasoma maneno ya Yesu yaliyosema, “Omba na utapewa; tafuta na utapata, piga hodi na mlango utafunguliwa” (Mathayo 7:7). Hii inaonyesha kuwa sala ni njia ya kuomba msaada kutoka kwa Mungu. Pia, Biblia inatueleza kuwa Yesu mwenyewe alikuwa akipenda kwenda peke yake kusali. Kwa hivyo, kama wafuasi wa Yesu tunapaswa kufanya hivyo pia.

Kanisa Katoliki linatumia sala kama sehemu ya ibada. Sala ni sehemu ya liturujia, ambayo ni ibada ya Kanisa Katoliki. Liturujia inajumuisha sala, nyimbo, na maandiko kutoka kwa Biblia. Kupitia sala, waumini wanashiriki katika ibada ya Kanisa na wanapata baraka kutoka kwa Mungu.

Kanisa Katoliki pia linatumia sala kama njia ya kutubu dhambi zetu. Katika sala ya kitubio, waumini wanakiri dhambi zao kwa padri na kupata msamaha wa Mungu. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kusafisha roho zetu na kuanza upya.

Kanisa Katoliki linatufundisha kuwa sala ni zaidi ya kuomba msaada kutoka kwa Mungu. Sala ni njia ya kuimarisha uhusiano wetu na Mungu. Kupitia sala, tunaweza kumjua Mungu vizuri zaidi na kupata ufahamu wa mapenzi yake. Sala inatuwezesha kusikiliza sauti ya Mungu na kufuata njia yake.

Kanisa Katoliki linatufundisha sala za kawaida kama vile Sala ya Bwana, Salamu Maria, na Tafakari ya Rozari. Sala hizi zinahimizwa kwa waumini ili kusali mara kwa mara na kuimarisha uhusiano wao na Mungu. Sala za kawaida pia zinafaa kama njia ya kufundisha watoto wetu umuhimu wa sala na kujifunza Biblia.

Kwa ujumla, sala ni sehemu muhimu ya maisha ya Kikristo. Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha umuhimu wake kwa waumini wake. Kupitia sala, tunaweza kuwasiliana na Mungu, kusafisha roho zetu, na kuimarisha uhusiano wetu na Mungu. Kwa hivyo, tunahimizwa kusali mara kwa mara na kufuata mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu sala. Kama Catechism ya Kanisa Katoliki inasema, “Sala ni moyo wa maisha ya kiroho; ni sehemu muhimu ya uhusiano wetu na Mungu” (CCC 2558).

Amri ya Nane ya Mungu: Makatazo na Amri

Amri ya Nane ya Mungu inatukataza nini?

Inakataza haya:

1. Ushahidi wa uongo, kiapo cha uongo na uongo wowote.
2. Hukumu isiyo ya haki, usengenyaji, uchafuzi wa jina na usingiziaji.
3. Kusifu watu uongo, kujisifu mwenyewe au ulaghai.


Katika Amri ya Nane Mungu anaamuru nini?

Katika Amri ya Nane Mungu anaamuru tuseme ukweli na tulinde heshima ya wengine. (Mt 5:37, Yak 5:12).


Twaharibu heshima ya wengine kwa namna gani?

Twaharibu Kwa

1. Kuwadhania vibaya
2. Kuwasengenya (Mith 12:22)
3. Kuwasingizia na kuleta uzushi. (Mdo 5:1-11; Law 19:11)


Aliyeharibu heshima ya mwingine yampasa afanye nini?

Aliyeharibu heshima ya mwingine yampasa kuirudisha kadiri awezavyo.


Tunalinda heshima ya wengine kwa namna gani?

Tunalinda heshima ya wengine kwa kuwaza na kusema mema juu yao. (1Kor 13:6)

Maswali na Majibu kuhusu Rehema

Rehema ni nini?
Rehema ni msamaha au ondoleo la adhabu ya dhambi tulizostahili sababu ya dhambi zilizokwisha ondolewa

Rehema hutolewa na nani?
Rehema hutolewa na Kanisa Katoliki kwa kutugawia mastahili ya Yesu Kristo, Bikira Maria na Ya Watakatifu

Kuna Rehema za namna ngapi?
Rehema za namna mbili
1. Rehema kamili
2. Rehema pungufu (Rehema isiyo kamili)

Rehema kamili ni nini?
Rehema kamili ni msamaha wa kufutiwa adhabu zote za muda za dhambi

Rehema isiyo kamili (pungufu) ni nini?
Rehema isiyo kamili (pungufu) ni msamaha wa kupunguziwa adhabu ya dhambi

Adhabu za dhambi huondolewa kwa namna gani? Jinsi ya kupata rehema
Adhabu za dhambi huondolewa kwa;
1. Kufanya malipizi au majuto kamili
2. Kuvumilia taabu na mateso katika maisha
3. Kuvishinda vishawishi na majaribu
4. Kusali sala mbalimbali
5. Kuomba Misa kwa ajili hiyo.
6. Kusoma neno la Mungu na kulitafakari na kulinganisha na maisha yetu ya kila siku
7. Utakaso wa Toharani kama adhabu hizi hazikuondolewa duniani

Kipimo cha Rehema ni nini?
Kipimo cha Rehema hutegemea uzito wa majuto na mapendo mtu aliyonayo kwa Mungu Muumba wake. (1Kor 9:11)

Mtu akitaka kupata Rehema za Kanisa Katoliki yampasa nini?
Mtu akitaka kupata Rehema za Kanisa Katoliki yampasa;
1. Kujua na kufuata utaratibu unaotolewa na Kanisa Katoliki wa kupata Rehema
2. Awe katika hali ya neema ya Utakaso
3. Kufanya matendo yote yanayotakiwa kwa kupata rehema hiyo, kwa mfano;
a). Hija au Kuhiji katika mwaka wa Jubilei katika Kanisa lililo teuliwa na Askofu
b). Kufanya mafungo – Kama vyama vya kitume
c). Kuzuru makaburi (Kutembelea) yaliyobarikiwa
d). Katika hatari ya kufa padri hutoa rehema pamoja na Sakramenti ya wagonjwa
e). Kusali kwa nia za Baba Mtakatifu

Maswali na majibu kuhusu Mpako wa wagonjwa au Mpako wa Mwisho

Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu gani?
Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu alijua udhaifu wa binadamu hauishi mara anapopokea uzima wa Mungu kwa sakramenti tatu za kuingizwa katika Ukristo. Hivyo alipanga kusaidia mpaka mwisho wa dunia waamini wake watakaopatwa na dhambi na ugonjwa, kama alivyowasaidia wengi aliokutana nao katika maisha yake.
“Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, ‘Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako’… ‘Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi’ – amwambia yule mwenye kupooza – ‘Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako’. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii” (Math 9:2,6-8).


Mpako wa Wagonjwa ulianzishwa na nani?
Mpako wa Wagonjwa ulianzishwa na Yesu, kama sakramenti zote. Maandiko yanasimulia huruma yake iliyomfanya awaponye wengi kwa namna mbalimbali na kuwapa Mitume uwezo wa kufanya vilevile kwa “kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina” (Math 10:1). Nao
“wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza” (Mk 6:13).
“Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa, nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa” (Yak 5:14-15).


Mafuta ya mpako wa wagonjwa yanamaanisha nini?
Mafuta ya wagonjwa yanamaanisha lengo la kuwaponya na kuwarudishia nguvu na uzuri.
Kama kawaida, maneno yanaweka wazi zaidi kuwa lengo si kuponya mwili tu, bali hasa roho kwa kuitia msamaha na faraja katika mateso ambayo huenda yakaendelea. Kwa kuwa Mungu haponyi mwili kila mara, isipokuwa kwa faida na wokovu wa mgonjwa na wa wengine. Kama ndiyo mapenzi yake, kila mmoja ajifunze kufaidika vilevile na ugonjwa:
“Makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, ‘Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu’. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu” (2Kor 12:7-9).
“Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu, tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake” (Kol 1:24).


Sakramenti ya Mpako wa wagonjwa ni nini?
Ni Sakramenti ambayo Padri humuombea neema ya Mungu na kumpaka Mafuta Matakatifu mgonjwa aliye katika hatari ya kifo kwa ajili ya neema ya roho na mwili. (Yak 5:14-15, Mk 6:13)
Sakramenti ya Mpako wa wagonjwa ilianza lini? Je, wakati wa Yesu kulikuwa na sakramenti hii?
Sakramenti ya mpako wa wagonjwa ilikuwepo tangu wakati Yesu akiwa hai. Tunaweza kuiona Kwenye Biblia tunaposoma Yesu alivyowatuma wanafunzi wake waliwapaka watu mafuta. “Waliwatoa pepo wengi Wabaya, wakawapaka wagonjwa wengi mafuta wakawaponya. (Marko 6:13)


Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa inaadhimishwaje?
Inaadhimishwa kwa Padre kumuombea mgonjwa, kumuwekea mikono na kumpaka mafuta katika panda la uso na viganja vya mikono; kwa kutumia mafuta aliyobariki Askofu siku ya Alhamisi kuu.


Sakramenti ya Mpako Wa Wagonjwa inamanufaa gani rohoni mwa mtu?
Manufaa ya Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa ni
1. Nguvu ya kuvumilia mateso na kuyaunganisha na mateso ya Yesu Kristo
2. Maondoleo ya dhambi zote asizoweza kuziungama
3. Nafuu ya mwili, hata uzima ikifaa kwa wokovu wa roho yake
4. Neema ya kujiandaa kuaga dunia na kuingia katika uzima wa milele


Ni nani anayetoa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa?
Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa hutolewa na kuhani tuu yaani Askofu au Padri


Padri aitwe kwa mgonjwa lini?
Padri aitwe kwa mgonjwa mara inapoonekana Hatari ya Kifo na kamwe isisubiriwe mpaka mgonjwa apoteze fahamu.


Ni nani aweza kupokea Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa?
Ni kila Mkatoliki aliyefikia umri wa kufikiri na aliye katika hatari ya kufa kwa ugonjwa au uzee aweza kupokea Sakramenti hii.


Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa yaweza kupokelewa mara ngapi?
Sakramenti hii yaweza kupokelewa mara nyingi ugonjwa ukizidi au akipatwa na ugonjwa mwingine mkubwa


Alama wazi ya Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa ni nini?
Alama wazi ya Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa ni tendo la kupaka Mafuta Matakatifu wagonjwa na kutamka maneno
“Kwa mpako huu Mtakatifu na kwa pendo lake kuu, Bwana Akujaze na nguvu ya Roho Mtakatifu. Amina Akuondoe katika enzi ya dhambi, akuweke huru. Kwa wema wake akupe nafuu katika mateso yako na kukujalia neema. Amina”


Kama padri hatapatika na mgonjwa afanye nini?
Kama padri hatapatikana mgonjwa aweke nia ya kuungama na afanye majuto kamili


Komunyo pamba ndio nini?
Komunyo pamba ndio Ekaristi inayopokelewa na wale wanaokaribia kuaga maisha ya duniani na wanaojiandaa kuvukia uzima wa milele

Kuhusu Ubatizo, Haya ndiyo mambo ya Msingi unayotakiwa kufahamu

Kwa nini ubatizo unafanyika kwa maji?

Ubatizo unafanyika kwa maji kwa kuwa ndiyo ishara ya usafi na ya uhai unaotupatia kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
“Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu” (Ez 36:26-27).
“Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwanakondoo” (Ufu 22:1).


Ubatizo unatolewa pia kwa maji machache tangu lini?

Ubatizo unatolewa pia kwa maji machache tangu mwanzo. Kutokana na umuhimu wa sakramenti hiyo Yesu ametuagiza twende kubatiza watu duniani kote.
Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaonyesha waamini walivyotekeleza agizo hilo katika mazingira mbalimbali, sio tu yalipopatikana maji mengi. Hivyo Paulo alipokuwa ndani ya nyumba “akasimama akabatizwa” (Mdo 9:18).
Kumbe Yohane Mbatizaji hakusogea mbali na mto Yordani, akisubiri watu wamuendee kutoka maeneo yote ya nchi ile kame.
“Alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele” (Yoh 3:23).


Je, ubatizo uliotolewa na Yohane Mbatizaji ulikuwa sakramenti?

Hapana, ubatizo uliotolewa na Yohan Mbatizaji haukuwa sakramenti, kwa sababu yeye alikuwa mtangulizi tu wa Yesu, mwanzilishi wa sakramenti zote.
“Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto” (Math 3:11).
Paulo aliuliza watu, “‘Mlibatizwa kwa ubatizo gani?’ Wakasema, ‘Kwa ubatizo wa Yohane’. Paulo akasema, ‘Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu’. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu” (Mdo 19:3-5).


Tofauti kubwa kati ya ubatizo wa Yohane na ule wa Yesu ni zipi?

Tofauti kubwa kati ya ubatizo wa Yohane na ule wa Yesu ni kwamba sakramenti inategemea imani kwa Kristo na kutushirikisha kifo na ufufuko wake.
“Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo” (Gal 3:27).
Ndivyo inavyoondolea dhambi zote na kuingiza katika uzima wa Utatu Mtakatifu. Kwa sababu hiyo Yesu aliagiza tubatize “kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” (Math 28:19).
Maneno hayo ndiyo muhimu zaidi katika sakramenti hiyo. Maji peke yake, hasa yakiwa mengi, yanaweza kuosha mwili, lakini si roho. Kumbe ubatizo unaotuokoa
“siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu” (1Pet 3:21).


Je, watoto wachanga wanaweza kubatizwa?

Ndiyo, watoto wachanga wanaweza kubatizwa kwa sababu hawakatai neema ya Mungu. Wanafunzi wa Yesu walipotaka kuwazuia wasiletwe kwake “alichukizwa sana, akawaambia, ‘Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni: Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa” (Mk 10:14-15).
Yeremia aliambiwa,
“Kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa” (Yer 1:5).
Yohane Mbatizaji alitabiriwa “atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye” (Lk 1:15).
Mitume walipokea katika Kanisa familia nzima, si wazazi tu.
Walibatizwa “yeye na nyumba yake”, “yeye na watu wake wote” (Mdo 16:15,33);
“watu wa nyumbani mwa Stefana” (1Kor 1:16).
Kwa hiyo tunaona kuwa tangu wakati wa Mitume sio watu wazima tuu waliokua wakibatizwa bali na watoto pia.


Mbona watoto wachanga hawawezi kuelewa kinachofanyika wakati wa ubatizo halafu wanabatizwa?

Ingawa watoto wachanga hawawezi kuelewa kinachofanyika, Mungu anaweza kuwamiminia rohoni mwanga wa imani.
“Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao umeiweka misingi ya nguvu” (Zab 8:2).
“Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake… kwa shangwe” (Lk 1:41,44).
“Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako” (Math 11:25-26).


Je, watu wazima wanaweza kuelewa sakramenti kwa dhati?

Hapana, watu wazima hawawezi kuelewa sakramenti kwa dhati, kwa kuwa zote ni mafumbo yanayotuzidi. Basi, kama Petro alipooshwa miguu, tumuachie Bwana atufanyie kazi anavyojua yeye.
“Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye” (Yoh 13:7).
Kisha kuoshwa tuzidi kuchimba mafumbo hayo kwa mwanga wa Neno na wa Roho Mtakatifu.
“Je, mmeelewa na hayo niliyowatendea?… Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yoh 13:12,15).


Je, imani ya watu wazima inaweza kufaidisha watoto?

Ndiyo, imani ya watu wazima inaweza kufaidisha watoto kama wengine pia.
Walimletea Yesu “mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne… Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, ‘Mwanangu, umesamehewa dhambi zako” (Mk 2:5).
Yesu aliiona imani yao akamponya. Imani ya watu wengine ndio ilivyopelekea kuponywa kwa huyu mtu. Vivyo hivyo Imani ya Mzazi inaweza kumsaidia mtoto.
Kwa ubatizo watoto wanaunganishwa naye na kuanza kuponywa madonda ya dhambi ya asili.
“Tazama, mimi naliumbwa kati hali ya uovu, mama yangu alinichukua mimba hatiani” (Zab 51:5).
“Ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo” (Rom 5:19).


Ubatizo wa watoto wachanga unafanyika tangu lini?

Ubatizo wa watoto wachanga unafanyika tangu mwanzo, usipingwe na yeyote kwa miaka elfu na zaidi. Ni kwamba Wayahudi walipokea watoto katika dini yao kwa kuwatahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa.
“Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu” (Lk 2:21).
Watu wa mataifa walipoongokea dini hiyo, walioshwa na kutahiriwa pamoja na watoto wao. Mitume pia walipokea katika Kanisa familia nzima, si wazazi tu. Walibatizwa “yeye na nyumba yake”, “yeye na watu wake wote” (Mdo 16:15,33); “watu wa nyumbani mwa Stefana” (1Kor 1:16).
Kwa hiyo tunaona kuwa tangu wakati wa Mitume sio watu wazima tuu waliokua wakibatizwa bali na watoto pia.
Kwa Kanisa Katoliki, ubatizo sio ukamilifu wa kuwa Mkristo. Ubatizo ni Sakramenti ya kwanza ambayo inakamilishwa na Sakramenti ya Kipaimara ambayo humfanya Mkristo kuwa mkamilifu kwa kukiri na kuahidi mwenyewe kuwa Mfuasi wa Yesu Kristu kwa kumkataa Shetani na Mambo yake yote. Kwa maana hiyo, watoto wanapobatizwa wazazi wanamtoa au wanamwalika mtoto katika Imani ya Kikristu wakiahidi kumtumza na kumwelekeza katika njia ya Imani kwa Yesu Kristu mpaka atakapokua mkubwa na kuwa na ufahamu na Elimu ya kutosha kuhusu Imani yake ndipo na yeye atakiri na kuahidi mwenyewe wakati wa Sakramenti ya Kipaimara.


Je, ubatizo tuu unatosha?

Hapana, ubatizo hautoshi, bali unahitaji kukamilishwa na kipaimara na ekaristi, kama vile baada ya kuzaliwa tunahitaji kukomaa na kudumisha uhai wetu kwa chakula.
Sakramenti hizo tatu kwa pamoja ni msingi wa maisha ya Wakristo wote, kumbe nyingine zinahitajika tu katika hali na nafasi maalumu. Mitume waliwaendea Wasamaria
“wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu” (Mdo 8:15-16).
“Amin, amin, nawaambieni: Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndaniyenu” (Yoh 6:53).


Sakramenti inayohusiana zaidi na ubatizo ni ipi?

Sakramenti inayohusiana zaidi na ubatizo ni kipaimara, kinachoendeleza kazi yake.
“Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao” (Mdo 19:5-6).
Sakramenti hizo ni kama pande mbili za pesa moja. Zinahusiana kama Pasaka na Pentekoste, ambayo ni utimilifu wake, kwa kuwa siku alipofufuka Yesu aliwapulizia Mitume Roho Mtakatifu, ambaye siku hamsini baadaye akawajia kama
“upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote” (Mdo 2:2).


Sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ipi?

Sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ekaristi, iliyo kuu kuliko sakramenti zote kwa sababu ndiyo Yesu mzima, Mungu-mtu, katika maumbo ya mkate na divai.
Sisi ambao tulishiriki kifumbo kifo na ufufuko wake tukapokea kwake paji la Roho Mtakatifu, tunaalikwa kukaribia mara kwa mara meza anapotulisha na kutunywesha Mwili na Damu yake ili tushiriki uhai wake kwa dhati zaidi na zaidi.
“Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yoh 6:56-57).
Ubatizo na kipaimara havirudiwi, vinadumu ndani mwetu kama mifupa ambayo ekaristi ya mara kwa mara inazidi kuitia mwili na damu.


Sakramenti ya ubatizo ni nini?

Sakramenti ya Ubatizo ni Sakramenti yenye kuondoa dhambi ya asili pamoja na dhambi nyingine zote tulizotenda, kufufua roho zetu kwa kututia uzima wa Mungu, Kutuandika Wakristu Watoto wateule wa Mungu na wa Kanisa.


Ubatizo ni nini?

Ubatizo ni Sakramenti inayotuwezesha kuzaliwa mara ya pili kwa Maji na Roho Mtakatifu, ni mlango (Kiingilio) kwa Sakramenti nyingine zote na ni ufunguo wa uzima wa milele. (Yoh 3:3, Mt28:19)


Sakramenti ya Ubatizo yatuletea nini?

Sakramenti ya Ubatizo yatuletea;
1. Maondoleo ya dhambi ya asili
2. Maondoleo ya dhambi zote za binafsi na adhabu zake
3. Neema ya Utakaso kwa mara ya kwanza
4. Yatutia alama isiyofutika (1Kor 6:11, 12:13)


Kuna Ubatizo wa namna ngapi?

Kuna Ubatizo wa namna tatu;
1. Ubatizo wa maji – Ubatizo wa kawaida
2. Ubatizo wa tamaa – Mfano mtu akifa akiwa na nia ya kubatizwa au akitamani kubatizwa
3. Ubatizo wa Damu – Mtu akiifia Imani japo hajabatizwa


Nani aweza kubatiza?

Mwenye mamlaka ya kubatiza kwa kawaida ni yule mwenye dataja takatifu katika Kanisa, lakini katika hatari ya kufa kila mtu anaweza kubatiza.


Kwa nini Kanisa linabatiza watoto wadogo?

Kwa sababu wanazaliwa na dhambi ya asili hivyo wanahitaji kuwekwa huru kutoka mamlaka ya yule mwovu na kuingizwa katika ufalme wa uhuru wa wana wa Mungu


Je, Ubatizo ni lazima kwa wokovu?

Ndiyo, nilazima kwa wokovu kwa wale ambao wametangaziwa injili na wanasifa ya kuomba Sakramenti hiyo


Anayebatizwa yampasa nini?

Yampasa kuungama imani yake ama mwenyewe akiwa mtu mzima ama kupitia wazazi kama akiwa mtoto mdogo


Alama wazi ya Sakramenti ya Ubatizo ni nini?

Alama wazi ya Sakramenti ya Ubatizo ni kumwagia maji katika panda la uso na kutamka maneno “Fulani (jina lake linatajwa) nakubatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” (Mt 28:19)


Msimamizi wa ubatizo ana wajibu gani?

Msimamizi wa ubatizo ana wajibu hizi;
1. Kutoa mfano mzuri wa maisha ya Kikristo
2. Kumuongoza mbatizwa katika maisha ya Ukristo
3. Kumuombea mbatizwa
4. Kushirikiana na wazazi katika malezi

Maswali na Majibu kuhusu dhamira

Dhamiri adilifu ni nini?
Dhamiri adilifu, iliyo ndani kabisa mwa mtu, ni uamuzi wa akili ambao kwa wakati wake unamuagiza mtu atende mema na kukwepa maovu


Katika hukumu zake dhamira ifuate nini?
Katika hukumu zake dhamira ifuate daima Injili, Amri za Mungu na za Kanisa na wajibu zetu.


Twajenga na kutunza dhamira zetu namna gani?
Twajenga na kutunza dhamira zetu kwa;-
1. Kufuata sauti ya Roho Mtakatifu
2. Kuzingatia mafundisho ya dini
3. Kuzingatia mila na desturi njema tulizopata katika malezi.
4 Kufuata mifano na tabia njema ya wenzetu na ya Watakatifu


Hadhi ya nafsi ya mtu inadai nini kuhusu dhamiri adilifu?
Hadhi ya nafsi ya mtu inadai unyofu wa dhamiri adilifu, yaani upande wa akili na sheria ya Mungu


Dhamiri adilifu inaundwa namna gani iwe nyofu na ya kweli?
Dhamiri nyofu inayosema kweli inaundwa kwa;
1. Malezi
2. Upokeaji wa neno la Mungu
3. Upokeaji wa Mafundisho ya Kanisa
4. Sala
5. Utafiti wa dhamiri


Dhamiri adilifu inatengenezwa na kusaidiwa na nini?
Dhamiri adilifu inatengenezwa na vipaji vya Roho Mtakatifu na kusaidiwa na mashauri ya watu wenye busara.


Dhamiri inatakiwa kufuata daima masharti gani?
Dhamira inatakiwa kufuata daima masharti yafuatayo
1. Hairuhusiwi kutenda maovu kusudi yapatikane mema
2. Yoyote muyatakayo mtendewe na watu, ninyi watendeeni vivyo hivyo. (Mt 7:12)
3. Upendo hufuata daima nia na heshima kwa jirani na kwa dhamira yake

Mambo ya Muhimu kufahamu kuhusu Mungu

Je, Yatupasa kumtolea Mungu shukrani?

Ndiyo, Yatupasa kumtolea Mungu shukrani kila wakati hasa kwa kuadhimisha Ekaristi Takatifu

Nani ameumba vitu vyote?

Mungu ameumba vitu vyote

Mungu ni nani?

Mungu ndiye muumba wa kila kitu katika uwingu na nchi, Mkubwa wa ulimwengu mwenye kuwatuza watu wema na kuwaadhibu watu wabaya.
“8Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.’’ 9‘‘Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba : “Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe.(Mt. 6:8-9).
17Yesu akamwambia, ‘‘Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ’’ (Yoh 20:17)

Mungu ni Muumba vyote maana yake ni nini?

Mungu ni Muumba vyote Maana yake amefanya vitu vyote kwa kutaka tu pasipo kutumia chochote. (2Wamakabayo 7:28, Yoh 1:3)

Mungu ni nini?

Mungu ni Roho kamili na ukamilifu wake hauna mipaka. (Yoh. 4:24, Kut.3:13-15, Zb. 144:3)

Mungu ni Roho maana yake ni nini?

Mungu ni Roho maana yake haonekani wala hashikiki. (Lk: 24:39)

Mungu ni mweza wa yote maana yake ni nini?

Mungu ni mweza wa yote maana yake kila atakalo hufanya. (Zab 135:6)

Mungu ni wa Milele maana yake ni nini?

Mungu ni wa Milele maana yake hana mwanzo wala mwisho, amekuwapo kabla ya nyakati, yupo na atakuwapo baada ya nyakati, yupo daima. (1Tim, 1:17)

Mungu ni mwema maana yake ni nini?

Mungu ni mwema maana yake apenda na kuvitunza viumbe vyake vyote hasa wanadamu na anawatakia mema tu. (Zab, 25:8-10)

Mungu ni Mwenye haki maana yake ni nini?

Mungu ni Mwenye haki maana yake kila mtu hupata kwa Mungu haki yake kadiri anavyostahili

Mungu aenea pote maaana yake ni nini?

Mungu aenea pote maaana yake yupo kila mahali mbinguni na duniani wala hakuna mahali asipokuwepo?. (Zab, 139:7-12)

Mungu ajua yote maana yake nini?

Mungu ajua yote maana yake ajua ya sasa, ya zamani na ya wakati ujao hata mawazo yetu

Mungu ni mwenye huruma maana yake nini?

Mungu ni mwenye huruma maana yake anawasamehe watu dhambi zao wakitubu.

Mungu ni mwenye subira maana yake ni nini?

Mungu ni mwenye subira maana yake mara nyingi akawia kuwaadhibu wakosefu maana ataka kuwapa nafasi ya kuongoka. (Eze, 33:11, Zb, 102;1-5)

Mungu wako wangapi?

Mungu yupo mmoja tuu Mkubwa wa wote na Baba wa wote. (Is: 44:6)

Katika Mungu mmoja kuna nafsi ngapi?

Katika Mungu mmoja kuna nafsi tatu nazo ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu; nafsi zote ni sawa.

Neno hili kuwa nafsi tatu kwa Mungu mmoja laitwaje?

Laitwa fumbo la Utatu Mtakatifu. (Lk, 3:21-22)

Kwa ajili gani Mwana wa Mungu (Yesu) alijifanya mtu?

Mwana wa Mungu (Yesu) alijifanya mtu kwa ajili yetu wanadamu na wokovu wetu ili atupatanishe na Mungu na kutushirikisha tabia ya umungu. (2Pet, 1:4)

Nafasi ya Heshima kwa Bikira Maria ni ipi?

Nafasi ya Heshima kwa Bikira Maria inafuata baada ya Heshima kwa Utatu Mtakatifu

Tunaanzaje kumjua Mungu?

Tunaanza kumjua Mungu kwa kuzingatia viumbe vyake, hasa dhamiri yetu.
“Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake” (Rom 1:20).

Je, tunaweza kusema juu ya Mungu?

Ndiyo, tunaweza kusema juu ya Mungu kuanzia wema, ukweli na uzuri wa viumbe vyake na kumsifu kiasi chetu kwamba ndiye wema, ukweli na uzuri wenyewe.
Lakini tukiri pia kuwa maneno yetu duni hayawezi kutosha kamwe kufafanua fumbo lake.
“Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua” (Ayu 42:3).
Tungemuelewa, asingekuwa Mungu.

Mwenyezi Mungu yukoje basi?

Mwenyezi Mungu ni ukamilifu mtupu usio na mipaka kwa milele yote.
“Tazama, Mungu ni mkuu, nasi hatumjui; hesabu ya miaka yake haitafutiki” (Ayu 36:26).
“Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” (Yoh 4:24).

Mungu akiwa Roho, viungo ambavyo pengine anapewa vina maana gani?

Mungu akiwa Roho, viungo ambavyo pengine anapewa vinamaanisha tu sifa fulani: k.mf. macho ujuzi wake, mikono uwezo wake, mabawa ulinzi wake, n.k. “Roho haina mwili na mifupa” (Lk 24:39).

Je, Mungu amewasiliana nasi?

Ndiyo, Mungu amewasiliana nasi, akijitambulisha na kujitoa kwetu, tuweze kuishi katika urafiki naye na hatimaye tushiriki heri yake.
“Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota ulizoziratibisha; mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; umemvika taji ya utukufu na heshima” (Zab 8:3-5).
“Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu” (Yoh 15:15).

Hasa Mungu amejifunua kuwa nani?

Hasa Mungu amejifunua kuwa upendo wenyewe.
“Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli” (Kut 34:6).
“Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake” (1Yoh 4:16).
“Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo” (1Yoh 4:8).

Je, Mungu amejitambulisha pia kwa jina?

Ndiyo, Mungu amejitambulisha pia kwa majina mbalimbali. Katika Agano la Kale jina muhimu kuliko yote liliandikwa “YHWH” yaani, “Mimi Ndimi”. Tangu zamani Wayahudi hawalitamki, hivyo wakilifikia wanasoma kwa kutafsiri, “Bwana”.
Ndiyo sababu katika Agano Jipya halitumiki kamwe, isipokuwa Yesu alifunua Umungu wake kwa kujisemea, “Mimi Ndimi” na kwa kukubali kuitwa, “Bwana”. Pamoja na hayo, alisali na kufundisha kusali kwa kumuelekea “ABA” yaani, “Baba”. Ndilo jina ambalo linampendeza zaidi na kutuingiza katika fumbo lake kama wana ndani ya Mwana pekee ambaye “Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba” (Fil 2:9-11).
“Msalipo, semeni, ‘Baba, jina lako litakaswe’” (Lk 11:2).
“Mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’” (Rom 8:15).

Mungu ametufunulia nini?

Mungu ametufunulia pia ukweli juu yetu wenyewe akijibu kabisa maswali yanayotusumbua kuhusu maana na lengo la maisha yetu.
Amefanya hivyo kwa maneno na matendo yanayoshikamana sana kwa kuwa maneno yanafafanua matendo, nayo matendo yanathibitisha maneno.
“Mungu hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli” (1Tim 2:4).
“Mungu si mtu, aseme uongo” (Hes 23:19).
Yeye hadanganyiki wala hadanganyi.

Mungu akiwa wema mkuu na mwenye uwezo wote, mbona katika viumbe vyake kuna ubaya? Kwa nini Mungu anaruhusu mabaya na maovu?

Kwa nini dhambi zipo?

Mungu akiwa wema mkuu na mwenye uwezo wote, hakuumba ubaya wowote. Tena kila anapovumilia ule uliosababishwa na viumbe vyenye hiari anaufanya uzae mema makubwa zaidi kwa njia tusizoweza kuzifahamu vizuri hapa duniani.
“Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu… Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo” (Mwa 45:4-5; 50:20).

Mungu aliwahi kujifunua kwa watu gani?

Mungu aliwahi kujifunua kwa wazazi wetu wa kwanza, akaendelea hasa kwa taifa la Israeli, hadi alipomtuma Mwanae ajifanye mtu wa taifa hilo teule.
“Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana” (Eb 1:1-2).

Je, ufunuo wa Mungu unaendelea hata leo?

Hapana, ufunuo wa Mungu hauendelei, kwa sababu alikwisha kuukamilisha kwa kumtuma duniani Neno wake wa milele.
“Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua” (Yoh 1:17-18).
Baada yake hauwezekani ufunuo mpya. Hatutakiwi kumuamini yeyote akidai eti, ametumwa kukamilisha kazi ya Yesu; kwa kuwa mwenyewe alisema,
“Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe” (Math 24:35).
“Ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe! Kama tulivyotangulia kusema, na sasa nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe!” (Gal 1:8-9).

Ufunuo wa Mungu unatufikiaje miaka elfu mbili baada ya Kristo?

Ufunuo wa Mungu unatufikia kupitia Kanisa lake, lililokabidhiwa Mapokeo ya Mitume na linaloongozwa na Roho Mtakatifu hadi ukweli wote.
Yesu aliahidi kwamba,
“Yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake” (Yoh 16:13).
“Maana Roho huchunguza yote hata mafumbo ya Mungu” (1Kor 2:10).

Je, Mungu amegawanyika sehemu tatu?

Hapana, Mungu hagawanyiki hata kidogo, bali daima ni Umoja kamili.
“Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja” (Mk 12:29).
Tumuabudu yeye peke yake katika nafsi tatu, na Utatu wa nafsi katika Umoja wa hali yake, tusichanganye nafsi wala kugawa Umungu. Baba si Mwana wala Roho Mtakatifu. Mwana si Baba wala Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu si Baba wala Mwana. Lakini milele yote nafsi hizo tatu ni Mungu yuleyule pasipo tofauti ya kuzitenganisha: kila moja imo ndani ya nyingine.
“Mimi na Baba tu umoja” (Yoh 10:30).

Tumejuaje kuwa Mungu ni Umoja wa nafsi tatu?

Tumejua kuwa Mungu ni Umoja wa nafsi tatu kwa sababu Baba aliwatuma kwetu Mwanae na Roho Mtakatifu.
“Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake. Na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, ‘Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye’” (Math 3:16-17).
Naye akaagiza, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu” (Math 28:19).
Ni nafsi tatu zenye jina moja, yaani Umungu mmoja tu.

Umoja wa Mungu unategemea nini?

Umoja wa Mungu unategemea hasa kwamba Mwana na Roho Mtakatifu wanachanga Umungu wa Baba, ambaye wanatokana naye pasipo utengano wowote. Baba anajifahamu na kujipenda: wazo analojifahamu ndiye Mwana, upendo anaojipenda katika wazo hilo ndiye Roho Mtakatifu.
“Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu” (Yoh 17:24).

Je, nafsi tatu za Mungu zina Umoja hata katika utendaji?

Ndiyo, nafsi tatu za Mungu zina Umoja hata katika utendaji, kila nafsi akiuchangia kulingana na sifa yake maalumu ndani ya Utatu. Baba Mwenyezi sifa yake ni Uwezo. Mwana kama Neno la Baba sifa yake ni Hekima. Roho kama Pumzi ya uhai ya Baba sifa yake ni Upendo.
Katika Uwezo wake Baba anafanya yote kwa Hekima na Upendo, hasa katika utume wa Mwana aliyefanyika mtu na katika utume wa Roho kama paji.
“Amin, amin, nawaambia: Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vilevile” (Yoh 5:19).

Mungu angeweza kuzuia watu wasitende dhambi?

Ndiyo, Mungu angeweza kuzuia watu wasitende dhambi, lakini aliwaacha watende kwa hiari yao awaonyeshe ukuu wa huruma yake.
“Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote” (Rom 11:32).

Yesu ni Mungu au mtu?

Yesu ni Mungu na mtu kwa pamoja, ndiyo sababu ni mshenga pekee kati ya Mungu na watu. “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, mwanadamu Kristo Yesu” (1Tim 2:5). “Katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili” (Kol 2:9). Hivyo ni Mungu kweli na mtu kweli.

1 Hapo mwanzo, kabla ya kuwapo kitu kingine cho chote, aliku wapo Neno. Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye alikuwa Mungu. 2 Tangu mwanzo Neno amekuwa na Mungu. 3 Vitu vyote viliumbwa na yeye, wala hakuna cho chote kilichoumbwa ambacho hakukiumba. 4 Uzima ulikuwa ndani yake na uzima huo ndio ulikuwa nuru ya watu. 5 Nuru hiyo huangaza gizani na giza haliwezi kamwe kuizima.
6 Mtu mmoja aitwaye Yohana alitumwa na Mungu 7 awaambie watu kuhusu hiyo nuru, ili kwa ushuhuda wake wapate kuamini. 8 Yohana mwenyewe hakuwa ile nuru. Yeye alitumwa kuishuhudia hiyo nuru. 9 Nuru halisi ambayo inawaangazia watu wote ilikuwa inakuja ulim wenguni. 10 Neno alikuwepo ulimwenguni, lakini japokuwa aliumba ulimwengu, watu wa ulimwengu hawakumtambua! 11 Alikuja nyumbani kwake, lakini watu wake hawakumpokea! 12 Bali wote waliompokea na kumwamini aliwapa haki ya kufanywa watoto wa Mungu. 13 Hawa hawakuwa watoto wa Mungu kwa kuzaliwa kwa njia ya asili, wala kwa mapenzi au mipango ya watu bali wamezaliwa na Mungu mwenyewe.
14 Neno akawa mwanadamu akaishi kati yetu akiwa amejaa utu kufu na kweli. Tuliona utukufu wake, utukufu wa Mwana pekee wa Baba. 15 Yohana alishuhudia habari zake, akatangaza: “Huyu ndiye yule niliyewaambia kuwa, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi kwa kuwa alikuwapo kabla sijazaliwa.”’ 16 Na kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema tele. 17 Musa alitule tea sheria kutoka kwa Mungu, lakini Yesu Kristo ametuletea neema na kweli. 18 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Lakini Mwanae pekee, ambaye ana uhusiano wa karibu sana na Baba yake, amemdhihirisha Mungu kwetu. Yohana 1:1-6:37

5 Tomaso akamwuliza, “Bwana, hatujui unakokwenda; tutaijuaje njia?” 6 Yesu akawaam bia, “Mimi ndiye Njia na Kweli na Uzima; mtu hawezi kufika kwa Baba bila kupitia kwangu. 7 Kama mngekuwa mnajua mimi ni nani, mngemfahamu na Baba yangu. Tangu sasa mnamfahamu Baba yangu na mmemwona.”
8 Filipo akamwambia Yesu, “Bwana, tuonyeshe Baba yako nasi tutaridhika.” 9 Yesu akamjibu, “Filipo, imekuwaje hunifahamu baada ya mimi kuwa pamoja nanyi muda wote huu? Mtu ye yote ambaye ameniona mimi, amemwona Baba. Sasa inakuwaje unasema, ‘Tuonyeshe Baba’? 10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba yangu, na Baba yangu yuko ndani yangu? Mambo ninayowaambia siyasemi kwa mamlaka yangu mwenyewe, bali yanatoka kwa Baba yangu ambaye anaishi ndani yangu, na ndiye anayetenda haya yote. Yohane 14:5-10

29 Baba yangu ambaye amenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwatoa hawa kutoka katika mikono yake. 30 Mimi na Baba yangu tu mmoja.”
31 Kwa mara nyingine wale Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo. 32 Yesu akawauliza, “Nimewaonyesha mambo mengi mazuri kutoka kwa Baba yangu. Kati ya hayo ni lipi linalosababisha mtake kunipiga mawe?” 33 Wao wakamjibu, “Tunataka kukupiga mawe si kwa sababu ya mambo mema uliyotenda bali ni kwa kuwa umekufuru. Wewe ni mtu tu lakini unajiita Mungu.” Yohane 10: 29-33

Yesu anapatikana wapi? Yesu anakaa wapi? Yesu Yupo wapi kwa sasa?

Yesu kama Mungu yupo kila mahali, hakuna mahali asipokuwepo. Yesu kama mwanadamu yupo Mbinguni kwa Baba na anakaa nasi duniani katika Maumbo ya Mkate na Divai Katika Ekaristi.


Je, Umungu na utu wa Yesu vinachanganyikana?

Hapana, Umungu na utu wa Yesu vimeunganika katika nafsi moja visichanganyikane, kwa kuwa ndani yake hali hizo mbili zinatenda kila moja ya kwake.
“Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, ‘Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu’” (Mk 15:39).

Je, Mwana wa Mungu tangu atwae mwili ni mtu kamili mwenye akili na utashi wa kibinadamu?

Ndiyo, Mwana wa Mungu tangu atwae mwili ni mtu kamili mwenye akili na utashi wa kibinadamu. Katika umoja wa nafsi yake vipawa hivyo vinatenda kulingana na Umungu anaouchanga na Baba na Roho Mtakatifu milele.
“Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake” (Yoh 14:10).

Kwa nini Maria anastahili kuitwa “Mama wa Mungu”?

Maria anastahili kuitwa “Mama wa Mungu” kwa sababu Mwana wa milele wa Mungu, ambaye ni Mungu sawa na Baba, alifanyika mtu toka kwake. Akiwa mja mzito alishangiliwa: “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?
” (Lk 1:42-43).

Je, Bikira Maria ni kama Bahasha au chombo cha kumleta Yesu tuu Duniani au anayo thamani zaidi?

Bikira Maria sio kama bahasha au chombo cha kumleta Yesu tuu duniani. Yesu ametokana na Bikira Maria katika ubinadamu wake. Mwili wa Yesu wa kiubinadamu ni sehemu au uzao wa Bikira Maria. Bikira Maria anayo uhusiano wa damu na Yesu Kristu. Ndiyo maana Mungu alimtakasa Bikira Maria Ili atakayezaliwa kutoka kwake awe na yeye mtakatifu.
Mungu alimtakasa Bikira Maria kabla ya Kuamua kuzaliwa kupitia yeye kwa kuwa Mungu ni Mtakatifu. Ubinadamu wa Yesu (MWILI – Nyama na Damu) asili yake ni Bikira Maria.

Kwa nini Yesu alishawishiwa/alijaribiwa na Shetani?

Yesu alishawishiwa na Shetani kwa kuwa ni mtu kweli, akamshinda kwa niaba ya watu wote, akituonyesha namna ya kumtii Mungu moja kwa moja, “hata mauti, naam, mauti ya msalaba” (Fil 2:8).
“Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki” (Rom 5:19).

Je, Mungu Baba alihusika na sadaka ya Mwanae?

Ndiyo, Mungu Baba alihusika sana na sadaka ya Mwanae, kwa sababu;
“Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake… Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika yeye” (2Kor 5:19,21).

Roho Mtakatifu ni nani?

Roho Mtakatifu ni upendo wa Mungu, nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu, mwenye Umungu mmoja na Baba na Mwana.
“Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:5).
Ametumwa kwetu atufanyie kazi pasipo kuonekana.
“Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho” (Yoh 3:8).
“Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” (Rom 8:14).

Je, tumuadhimishe Mungu katika Nafsi zake tatu pia?

Ndiyo, tumuadhimishe Mungu katika Nafsi zake tatu pia: Baba kama asili ya umungu na ya uhai wote, Mwana kama Neno wake aliyejifanya mtu atukomboe, tena Roho Mtakatifu kama Upendo wao ambao unawaunganisha na kututakasa.
Pamoja na viumbe vyote tuwaimbie usiku na mchana, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja!” (Ufu 4:8).
“Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” (Yoh 4:24).

Hamu kuu ya binadamu ni ipi?

Hamu kuu ya binadamu ni kumwona Mungu

Je, Yatupasa kumwomba Roho Mtakatifu?

Ndiyo, kwani twataka kwake maonyo na msaada. Tusipokuwa na neema yake hatuwezi kutenda jambo jema la kufaa kutuokoa. (Yoh 16:13)

Amri ya Saba ya Mungu: Usiibe – Tambua mali ya mtu na kuheshimu

Je, Amri ya Saba ya Mungu inafundisha nini?

Amri ya saba ya Mungu inafundisha kuitambua mali ya mtu na kuiheshimu.


Mali ya mtu ni ipi?

Mali ya mtu ni ile aliyoipata kwa njia halali yaani kwa haki.


Lengo la mali ya binafsi ni lipi?

Kutosheleza mahitaji yake mtu binafsi, ya familia, ya wenye shida na ya kanisa.


Mtu awatendeje wanyama?

Mtu anatakiwa kuwatendea wanyama kwa wema kama viumbe wa Mungu


Amri ya saba ya Mungu inakataza nini?

Inakataza haya;

1. Wizi
2. Kulangua
3. Kutapeli
4. Kughushi
5. Kufuja mali
6. Kutoa au kupokea rushwa
7. Ufisadi
8. Kuharibu mali ya mtu au jamii


Anayejipatia mali kwa njia isiyo ya halali yampasa kufanya nini?

Anayejipatia mali kwa njia isiyo ya halali yampasa kurudisha gharama yake kwa mwenye mali


Anayeharibu mali ya mwingine lazima afanye nini?

Anayeharibu mali ya mwingine lazima alipe hasara aliyosababisha. (Lk 19:8)


Je yatupasa kufanya kazi?

Ndiyo, kwa sababu:

1. Kazi inampa mwanadamu heshima
2. Kufanya kazi ni wajibu wa haki. (Mwa 1:28)


Je ni lazima kuwasaidia masikini na fukara?

Ndiyo, Kuwatendea Masikini mema ni kumtendea Yesu mwenyewe. (Mt 25:40)

Mambo ya Msingi kujua kuhusu Sakramenti ya Kitubio

Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu gani?
Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu alijua udhaifu wa binadamu hauishi mara anapopokea uzima wa Mungu kwa sakramenti tatu za kuingizwa katika Ukristo. Hivyo alipanga kusaidia mpaka mwisho wa dunia waamini wake watakaopatwa na dhambi na ugonjwa, kama alivyowasaidia wengi aliokutana nao katika maisha yake.
“Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, ‘Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako’… ‘Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi’ – amwambia yule mwenye kupooza – ‘Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako’. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii” (Math 9:2,6-8).

Mungu aliwapa watu (mapadri) amri/uwezo ya kusamehe dhambi kwa njia ya nani? Ni halali kuungama kwa padre?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa njia ya Mwanae. Yesu mfufuka aliwaonyesha Mitume alama ya mateso mwilini mwake, “akawavuvia, akawaambia, ‘Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23).
Katika Kanisa tunafurahi kupewa msamaha wa dhambi kila tunapohitaji, mradi tutubu. Kwa njia ya mwandamizi wa Mitume, Yesu anatuambia,
“Umesamehewa dhambi zako… Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani” (Lk 7:48,50).
Si dhana wala hisia tu, bali ni neno la hakika tunalolipokea kwa masikio yetu.

Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zipi?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zote, kwa sababu upendo mtiifu wa Mwanae aliyejitoa kuwa sadaka ya wokovu wetu unampendeza kuliko dhambi zote zinavyomchukiza. Ila hatuwezi kusamehewa dhambi ya kukataa neema ambayo Roho Mtakatifu anatusukuma tuamini na kutubu, kwa sababu pasipo imani na toba hapana msamaha.
“Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa” (Math 12:31).
“Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure” (2Kor 6:1).

Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu gani?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu amependa washiriki katika kazi zake. Ametuumba kwa njia ya wazazi na kutulea na kutusaidia kwa njia ya wengine pia. Hasa ametuokoa kwa njia ya Yesu, ambaye yupo nasi sikuzote katika Mwili wake, yaani Kanisa, na katika wale walioshirikishwa mamlaka ya Mitume.
“Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:18-20).

Je, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi?
Ndiyo, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi tulizotenda baada ya ubatizo, kwa kuwa hatuwezi kupokea msamaha tukikataa masharti yake, na Mungu ametupangia watu ambao watuondolee kwa niaba yake.
“Watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohane. Lakini, Mafarisayo na wanasheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye” (Lk 7:29-30).
Yesu mwenyewe alikubali kubatizwa na Yohane ili atimize mpango wa Baba.
“Yohane alitaka kumzuia, akisema, ‘Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?’ Yesu akajibu akamwambia, ‘Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Math 3:14-15).
Je, sisi tukatae kumkimbilia padri wa Mungu ili kupokea huruma yake tunayoihitaji kuliko hewa?

Tumuungamie padri dhambi zetu kwa lengo gani? Kwa nini Wakatoliki wanaungama kwa padri?
Tumuungamie padri dhambi zetu ili aweze kutushauri na kuamua kama tuko tayari kuondolewa. Tumweleze kwa unyofu makosa yote tuliyoyafanya na nia tuliyonayo ya kuyafidia na kutoyarudia.
“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu” (1Yoh 1:8-10).
Tukumbuke tulivyo viungo vya Mwili mmoja, hivi kwamba dhambi zetu zimewadhuru wenzetu. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana, mpate kuponywa” (Yak 5:16).
Kutokuwa tayari kufanya hivyo walau sirini kwa padri ni dalili ya kiburi na ya kutotubu.

Je, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi?
Ndiyo, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi kwa niaba ya Mungu aliyempa mamlaka hiyo. Hatusamehewi na utakatifu wa padri, bali na huruma ya Baba kwa njia yake.
Yeye anamtumia padri yeyote ili kuturahisishia kazi, tusihitaji kuchunguza kwanza ubora wa maisha yake, wala kwenda mbali tukampate mmoja asiye na dhambi. Tungefanyeje kuhakikisha ni mtakatifu, wakati hatuwezi kusoma moyo wake? Ingekuwa hivi, tusingepata kamwe hakika ya kusamehewa. Kumbe inatutosha kujua ni padri, kwamba Mungu amempa mamlaka ya kusamehe dhambi, kama Yesu alivyowapa Mitume siku tatu baada ya kumkimbia na hata kumkana. Kila padri anaweza kukiri,
“Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa: ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi” (1Tim 1:15).
Amri ya kusamehe dhambi wamepewa watu, si malaika.
“Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu” (2Kor 4:7).

Je, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo?
Ndiyo, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo, lakini ni vigumu zaidi, kwa sababu hatupati msaada wa sakramenti hiyo maalumu.
Pamoja na nia ya kumuungamia padri mapema tunahitaji neema ya kutubu kikamilifu, si kwa kuhofia adhabu, bali kwa kumpenda Mungu tuliyemchukiza.
“Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana” (Lk 7:47).

Sakramenti ya Kitubio ni nini?
Sakramenti ya Kitubio ndiyo Sakramenti ya kuwaondolea watu dhambi walizotenda baada ya Ubatizo (Yoh 20:22-23)

Lini na kwa maneno gani Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio?
Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio jioni ya ufufuko wake alipowapulizia mitume na kuwaambia maneno haya “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi watakua wameondolewa, wowote mtakaowafungia dhambi watakua wamefungiwa” (Yoh 20:22-23)

Mwenye kuwaondolea watu dhambi ni nani?
Mwenyezi Mungu pekee yake aweza kuwaondolea watu dhambi. Ndiye aliyewapa Mitume, Maaskofu na Mapadri uwezo wa kuwaondolea watu dhambi (Yoh 20:21-23)

Nani yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio?
Kila mkristo aliyetenda dhambi yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio

Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa haya
1. Kutafuta dhambi moyoni (Yoh 3:20-21)
2. Kujuta dhambi
3. Kukusudia kuacha dhambi
4. Kuungama kwa padre
5. Kutimiza malipizi
6. Kumshukuru Mungu aliyemwondolea dhambi

Wakati wa Sakramenti ya Kitubio Utamwomba Roho Mtakatifu kwa sala gani?
Utamuomba Roho Mtakatifu kwa sala hii:
Uje Roho Mtakatifu unisaidie nitambue dhambi zangu, nijute sana, niungame vema, nipate kutubu kweli. Amina

Kutafuta dhambi maana yake ni nini?
Kutafuta dhambi maana yake ni kujiuliza moyoni dhambi nilizotenda Tangu ungamo la mwisho (Ef 4:17-32)

Utafuteje dhambi wakati wa kujiandaa kuungama?
Tafuta dhambi kwa njia hizi
1. Kwa kukumbuka uliyokosa kwa mawazo, kwa maneno na kwa vitendo
2. Katika Amri za Mungu na za Kanisa
3. Katika vichwa vya dhambi
4. Katika kutimiza wajibu

Kutubu dhambi maana yake ni nini?
Kutubu dhambi maana yake ni kuona uchungu na chuki moyoni juu ya dhambi tulizotenda na kukusudia kutotenda dhambi tena (Yoh 8:11)

Kwa nini tujute dhambi zetu?
Tunajuta dhambi zetu kwa sababu tumeukosea Utatu Mtakatifu na tunastahili adhabu yake, na pia bila majuto hatuwezi kupata maondoleo ya dhambi.

Kuna majuto ya namna ngapi?
una majuto ya namna mbili,
1. Majuto kamili/Majuto ya mapendo
2. Majuto yasiyokamili/majuto pungufu/majuto ya hofu

Majuto kamili ni nini?
Majuto kamili ni kujuta kwa sababu tumemchukiza Mungu mwenyewe aliye mwema na mpendelevu kabisa

Majuto yasiyo kamili au majuto pungufu ni nini?
Majuto yasiyokamili ni kujuta kwa sababu tumepoteza furaha za Mbinguni na tunahofia adhabu ya Mungu

Asiyejuta aweza kuondolewa dhambi?
Asiyejuta hawezi kuondolewa dhambi kabisa, na anayeungama bila kujuta anatenda dhambi kubwa ya kufuru.

Kabla ya kuungama ni lazima kufanya nini?
Kabla ya kuungama ni lazima kukusudia kuacha dhambi na kuepuka nafasi kubwa ya dhambi bila kusahau kufuata hatua sita za kabla na baada ya kupokea kupokea Sakramenti ya Kutubio ambazo ni,
(1) kuwaza/kutafuta dhambi moyoni,
(2)kutubu/ kujuta,
(3)kukusudia kuacha dhambi,
(4)kuungama kwa padri,
(5)kutimiza kitubio,
(6)kumshukuru Mungu

Anayetaka kweli kuacha dhambi afanye nini?
Anayetaka kuacha dhambi afanye nguvu kuvishinda vishawishi, asali/aombe na apokee Sakramenti Mara nyingi hasa Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi Takatifu.

Kuungama ni kufanya nini?
Kuungama ni kumwambia Padri wazi wazi dhambi zako ulizotenda, zipi na ngapi ili upate maondoleo.

Anayeficha kusudi dhambi ya mauti katika ungamo anaondolewa?
Haondolewi, Bali anatenda dhambi kubwa ya kukufuru Sakramenti ya Kitubio. (Mt 7:21-23, Yoh 20:23, Gal 6:7)

Anayekufuru Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Yampasa kuziungama tena dhambi zake zote alizotenda tangu ondoleo la mwisho

Padri anaondolea dhambi mahali pa nani?
Padri anaondolea dhambi mahali pa Mungu

Padri anaondolea dhambi kwa maneno gani?
Padre anaondolea dhambi kwa maneno haya: Nami “Nakuondolea dhambi zako zote kwa Jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu”.

Kitubio tuwezacho kupewa na padre ni nini?
Kitubio tuwezacho kupewa na Padre ni kama sala, kufunga, kutoa sadaka kwa maskini, kusoma maandiko matakatifu, kuwatazama wagonjwa, n.k.

Kitubio tupewacho na padre chatosha?
Ni shida kutosha. Mara nyingi chataka malipizi ya hapa duniani kama kufunga, magonjwa, masumbuko, sala n.k mateso yasipotosha hapa duniani yatakamilishwa toharani

Kutimiza malipizi maana yake ni ni nini?
Kutimiza malipizi maana yake ni kutekeleza kiaminifu sala au matendo aliyotuagiza padre muungamishi ili kulipa adhabu za muda. (Rom 8:17)

Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema zipi?
Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema hizi;
1. Maondoleo ya dhambi zote kubwa na adhabu ya milele
2. Maondoleo ya dhambi ndogo na adhabu nyingine za muda (Isa 6:5-7, Yoh 8:11)
3. Twarudishiwa na kuongezewa neema ya utakaso
4. Twasaidiwa kuepa dhambi na twapata nguvu ya kutenda mema
5. Twarudishiwa tena mastahili tuliyopoteza kwa dhambi zetu
Shopping Cart
32
    32
    Your Cart
    Kitabu cha SMS Maalumu kwa Umpendaye
    Kitabu cha SMS Maalumu kwa Umpendaye
    1 X Sh2,500 = Sh2,500
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About