Mambo ya Muhimu kujua kuhusu dhambi

Dhambi ya asili ndio nini?
Dhambi ya asili ambayo binadamu wote wanazaliwa nayo, ni hali ya kukosa utakatifu na hali ya asili ya urafiki na Mungu


Adhabu gani walipewa Adamu na Eva?
Adamu na Eva kwa ukubwa wa dhambi yao ya kiburi na ya uasi:
1. Walipoteza neema ya utakaso
2. Walifukuzwa paradisini
3. Walipungukiwa akili na kushikwa na tamaa ya kutenda dhambi
4. Walipitia mahangaiko na taabu nyingi
5. Kupaswa kufa. (Mwa 3:16-20: 5:5)


Kisha kosa la Adamu na Eva Mungu aliahidi nini?
Kisha kosa la Adamu na Eva Mungu aliahidi kuwaletea Mkombozi. (Mwa 3:15)


Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili maana yake ni nini?
Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili maana yake hakuzaliwa na dhambi ya asili kama binadamu wengine


Mungu akiwa wema mkuu na mwenye uwezo wote, mbona katika viumbe vyake kuna ubaya? Kwa nini Mungu anaruhusu mabaya na maovu?
Kwa nini dhambi zipo?
Mungu akiwa wema mkuu na mwenye uwezo wote, hakuumba ubaya wowote. Tena kila anapovumilia ule uliosababishwa na viumbe vyenye hiari anaufanya uzae mema makubwa zaidi kwa njia tusizoweza kuzifahamu vizuri hapa duniani.
β€œMimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu… Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo” (Mwa 45:4-5; 50:20).


Mungu angeweza kuzuia watu wasitende dhambi?
Ndiyo, Mungu angeweza kuzuia watu wasitende dhambi, lakini aliwaacha watende kwa hiari yao awaonyeshe ukuu wa huruma yake.
β€œMaana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote” (Rom 11:32).


Je, toka mwanzo sisi watu tunaasi mpango wa Mungu peke yetu?
Hapana, toka mwanzo sisi watu tunaasi mpango wa Mungu kwa kuvutwa na mashetani, yaani malaika waliokataa moja kwa moja kumtumikia; baada ya dhambi ya asili hao wanatutumia sisi pia tuangushane na wenzetu.
Lakini Mungu aliwahi kumuambia Shetani:
β€œNitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako, na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino” (Mwa 3:15).
β€œHata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke” (Gal 4:4).


Je, dhambi zote zinahusiana?
Ndiyo, dhambi zote zinahusiana kwa sababu dhambi zinazaa dhambi nyingine ndani mwetu na katika mazingira yetu.
β€œHamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya” (1Kor 5:6-7).


Dhambi zimetuathiri vipi tena?
Dhambi zimetuathiri kwa ndani zaidi, zikitutia udhaifu katika mwili, ujinga katika akili na uovu katika utashi; madonda hayo yanatufanya tuzidi kushindwa.
β€œKwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii” (Rom 8:7).


Katika unyonge wetu tutumainie nini?
Katika unyonge wetu tutumainie huruma ya Mungu aliyetutumia Mkombozi hata β€œdhambi ilipozidi, neema ikawa kubwa zaidi” (Rom 5:20).
Ushindi wake juu ya dhambi umetupatia mema makubwa kuliko tuliyoyapoteza kwa dhambi.
β€œMungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu; alituuhisha pamoja na Kristo; yaani, mmeokolewa kwa neema” (Ef 2:4-5).


Yesu ni Mungu au mtu?
Yesu ni Mungu na mtu kwa pamoja, ndiyo sababu ni mshenga pekee kati ya Mungu na watu. β€œKwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, mwanadamu Kristo Yesu” (1Tim 2:5). β€œKatika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili” (Kol 2:9). Hivyo ni Mungu kweli na mtu kweli.
1 Hapo mwanzo, kabla ya kuwapo kitu kingine cho chote, aliku wapo Neno. Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye alikuwa Mungu. 2 Tangu mwanzo Neno amekuwa na Mungu. 3 Vitu vyote viliumbwa na yeye, wala hakuna cho chote kilichoumbwa ambacho hakukiumba. 4 Uzima ulikuwa ndani yake na uzima huo ndio ulikuwa nuru ya watu. 5 Nuru hiyo huangaza gizani na giza haliwezi kamwe kuizima.
6 Mtu mmoja aitwaye Yohana alitumwa na Mungu 7 awaambie watu kuhusu hiyo nuru, ili kwa ushuhuda wake wapate kuamini. 8 Yohana mwenyewe hakuwa ile nuru. Yeye alitumwa kuishuhudia hiyo nuru. 9 Nuru halisi ambayo inawaangazia watu wote ilikuwa inakuja ulim wenguni. 10 Neno alikuwepo ulimwenguni, lakini japokuwa aliumba ulimwengu, watu wa ulimwengu hawakumtambua! 11 Alikuja nyumbani kwake, lakini watu wake hawakumpokea! 12 Bali wote waliompokea na kumwamini aliwapa haki ya kufanywa watoto wa Mungu. 13 Hawa hawakuwa watoto wa Mungu kwa kuzaliwa kwa njia ya asili, wala kwa mapenzi au mipango ya watu bali wamezaliwa na Mungu mwenyewe.
14 Neno akawa mwanadamu akaishi kati yetu akiwa amejaa utu kufu na kweli. Tuliona utukufu wake, utukufu wa Mwana pekee wa Baba. 15 Yohana alishuhudia habari zake, akatangaza: β€œHuyu ndiye yule niliyewaambia kuwa, β€˜Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi kwa kuwa alikuwapo kabla sijazaliwa.”’ 16 Na kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema tele. 17 Musa alitule tea sheria kutoka kwa Mungu, lakini Yesu Kristo ametuletea neema na kweli. 18 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Lakini Mwanae pekee, ambaye ana uhusiano wa karibu sana na Baba yake, amemdhihirisha Mungu kwetu. Yohana 1:1-6:37


5 Tomaso akamwuliza, β€œBwana, hatujui unakokwenda; tutaijuaje njia?” 6 Yesu akawaam bia, β€œMimi ndiye Njia na Kweli na Uzima; mtu hawezi kufika kwa Baba bila kupitia kwangu. 7 Kama mngekuwa mnajua mimi ni nani, mngemfahamu na Baba yangu. Tangu sasa mnamfahamu Baba yangu na mmemwona.”
8 Filipo akamwambia Yesu, β€œBwana, tuonyeshe Baba yako nasi tutaridhika.” 9 Yesu akamjibu, β€œFilipo, imekuwaje hunifahamu baada ya mimi kuwa pamoja nanyi muda wote huu? Mtu ye yote ambaye ameniona mimi, amemwona Baba. Sasa inakuwaje unasema, β€˜Tuonyeshe Baba’? 10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba yangu, na Baba yangu yuko ndani yangu? Mambo ninayowaambia siyasemi kwa mamlaka yangu mwenyewe, bali yanatoka kwa Baba yangu ambaye anaishi ndani yangu, na ndiye anayetenda haya yote. Yohane 14:5-10


29 Baba yangu ambaye amenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwatoa hawa kutoka katika mikono yake. 30 Mimi na Baba yangu tu mmoja.”
31 Kwa mara nyingine wale Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo. 32 Yesu akawauliza, β€œNimewaonyesha mambo mengi mazuri kutoka kwa Baba yangu. Kati ya hayo ni lipi linalosababisha mtake kunipiga mawe?” 33 Wao wakamjibu, β€œTunataka kukupiga mawe si kwa sababu ya mambo mema uliyotenda bali ni kwa kuwa umekufuru. Wewe ni mtu tu lakini unajiita Mungu.” Yohane 10: 29-33


Yesu anapatikana wapi? Yesu anakaa wapi? Yesu Yupo wapi kwa sasa?
Yesu kama Mungu yupo kila mahali, hakuna mahali asipokuwepo. Yesu kama mwanadamu yupo Mbinguni kwa Baba na anakaa nasi duniani katika Maumbo ya Mkate na Divai Katika Ekaristi.


Kwa nini Yesu alishawishiwa/alijaribiwa na Shetani?
Yesu alishawishiwa na Shetani kwa kuwa ni mtu kweli, akamshinda kwa niaba ya watu wote, akituonyesha namna ya kumtii Mungu moja kwa moja, β€œhata mauti, naam, mauti ya msalaba” (Fil 2:8).
β€œKwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki” (Rom 5:19).


Kwa nini Yesu aliteswa hadi kuuawa msalabani?
Yesu aliteswa hadi kuuawa msalabani ili abebe kwa upendo na kufidia dhambi za watu wote, alivyotabiriwa:
β€œTulimdhania ya kuwa amepigwa, amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu; adhabu ya amani ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona” (Isa 53:4-5).
Tangu mwanzo Wakristo wanakiri kwa ufupi kwamba,
β€œKristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo Maandiko” (1Kor 15:3).
β€œAlijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema” (Tit 2:14).
β€œAlijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote” (1Tim 2:6).
β€œIli kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa” (Eb 2:14-15).


Je, Kanisa linaweza kutuondolea dhambi yoyote?
Ndiyo, Kanisa linaweza kutuondolea dhambi yoyote katika ubatizo na kitubio kwa kutumia mamlaka ambayo Yesu mfufuka aliwashirikisha Mitume wake alipowavuvia akisema:
β€œPokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23).
β€œMlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu” (1Kor 6:11).


Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu gani?
Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu alijua udhaifu wa binadamu hauishi mara anapopokea uzima wa Mungu kwa sakramenti tatu za kuingizwa katika Ukristo. Hivyo alipanga kusaidia mpaka mwisho wa dunia waamini wake watakaopatwa na dhambi na ugonjwa, kama alivyowasaidia wengi aliokutana nao katika maisha yake.
β€œYesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, β€˜Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako’… β€˜Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi’ – amwambia yule mwenye kupooza – β€˜Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako’. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii” (Math 9:2,6-8).


Mungu aliwapa watu (mapadri) amri/uwezo ya kusamehe dhambi kwa njia ya nani? Ni halali kuungama kwa padre?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa njia ya Mwanae. Yesu mfufuka aliwaonyesha Mitume alama ya mateso mwilini mwake, β€œakawavuvia, akawaambia, β€˜Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23).
Katika Kanisa tunafurahi kupewa msamaha wa dhambi kila tunapohitaji, mradi tutubu. Kwa njia ya mwandamizi wa Mitume, Yesu anatuambia,
β€œUmesamehewa dhambi zako… Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani” (Lk 7:48,50).
Si dhana wala hisia tu, bali ni neno la hakika tunalolipokea kwa masikio yetu.


Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zipi?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zote, kwa sababu upendo mtiifu wa Mwanae aliyejitoa kuwa sadaka ya wokovu wetu unampendeza kuliko dhambi zote zinavyomchukiza. Ila hatuwezi kusamehewa dhambi ya kukataa neema ambayo Roho Mtakatifu anatusukuma tuamini na kutubu, kwa sababu pasipo imani na toba hapana msamaha.
β€œKila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa” (Math 12:31).
β€œNasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure” (2Kor 6:1).


Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu gani?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu amependa washiriki katika kazi zake. Ametuumba kwa njia ya wazazi na kutulea na kutusaidia kwa njia ya wengine pia. Hasa ametuokoa kwa njia ya Yesu, ambaye yupo nasi sikuzote katika Mwili wake, yaani Kanisa, na katika wale walioshirikishwa mamlaka ya Mitume.
β€œLakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:18-20).


Je, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi?
Ndiyo, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi tulizotenda baada ya ubatizo, kwa kuwa hatuwezi kupokea msamaha tukikataa masharti yake, na Mungu ametupangia watu ambao watuondolee kwa niaba yake.
β€œWatu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohane. Lakini, Mafarisayo na wanasheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye” (Lk 7:29-30).
Yesu mwenyewe alikubali kubatizwa na Yohane ili atimize mpango wa Baba.
β€œYohane alitaka kumzuia, akisema, β€˜Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?’ Yesu akajibu akamwambia, β€˜Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Math 3:14-15).
Je, sisi tukatae kumkimbilia padri wa Mungu ili kupokea huruma yake tunayoihitaji kuliko hewa?


Tumuungamie padri dhambi zetu kwa lengo gani? Kwa nini Wakatoliki wanaungama kwa padri?
Tumuungamie padri dhambi zetu ili aweze kutushauri na kuamua kama tuko tayari kuondolewa. Tumweleze kwa unyofu makosa yote tuliyoyafanya na nia tuliyonayo ya kuyafidia na kutoyarudia.
β€œTukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu” (1Yoh 1:8-10).
Tukumbuke tulivyo viungo vya Mwili mmoja, hivi kwamba dhambi zetu zimewadhuru wenzetu. β€œUngameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana, mpate kuponywa” (Yak 5:16).
Kutokuwa tayari kufanya hivyo walau sirini kwa padri ni dalili ya kiburi na ya kutotubu.


Je, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi?
Ndiyo, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi kwa niaba ya Mungu aliyempa mamlaka hiyo. Hatusamehewi na utakatifu wa padri, bali na huruma ya Baba kwa njia yake.
Yeye anamtumia padri yeyote ili kuturahisishia kazi, tusihitaji kuchunguza kwanza ubora wa maisha yake, wala kwenda mbali tukampate mmoja asiye na dhambi. Tungefanyeje kuhakikisha ni mtakatifu, wakati hatuwezi kusoma moyo wake? Ingekuwa hivi, tusingepata kamwe hakika ya kusamehewa. Kumbe inatutosha kujua ni padri, kwamba Mungu amempa mamlaka ya kusamehe dhambi, kama Yesu alivyowapa Mitume siku tatu baada ya kumkimbia na hata kumkana. Kila padri anaweza kukiri,
β€œNi neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa: ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi” (1Tim 1:15).
Amri ya kusamehe dhambi wamepewa watu, si malaika.
β€œTuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu” (2Kor 4:7).


Je, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo?
Ndiyo, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo, lakini ni vigumu zaidi, kwa sababu hatupati msaada wa sakramenti hiyo maalumu.
Pamoja na nia ya kumuungamia padri mapema tunahitaji neema ya kutubu kikamilifu, si kwa kuhofia adhabu, bali kwa kumpenda Mungu tuliyemchukiza.
β€œAmesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana” (Lk 7:47).


Dhambi za uchafu huleta hasara gani?
Huleta hasara hizi;
1. Kuharibu usafi wa Moyo na Hekalu la Mungu
2. Huleta Magonjwa duniani na hasara ya baadae. mf UKIMWI. (Efe 5:5)
3. Huvunja amani ya familia
4. Kujijengea mazoea ya uchafu


Mambo yanayomzuia mtu kuishi maisha mema ni yapi?
Mambo hayo ni;
1. Dhambi
2. Vilema
3. Vishawishi


Dhambi ni nini?
Dhambi ni kosa la Mtu mwenye kuvunja Amri ya Mungu au ya Kanisa kwa mawazo (tamaa), kwa maneno au kwa matendo


Je kuna aina tofauti ya dhambi?
Ndiyo, kuna dhambi za mawazo, maneno, matendi na kutotimiza wajibu.


Dhambi zinatofautianaje katika uzito?
Kuna:
1. Dhambi ya Mauti (Dhambi kubwa) na
2. Dhambi nyepesi (Dhambi ndogo)


Dhambi ya mauti ni nini?
Dhambi ya Mauti ni kosa la kuvunja Amri ya Mungu au ya Kanisa, katika jambo kubwa, kwa fahamu na kusudi. (1 Yoh 5:16)


Dhambi ya Mauti hutupotezea nini?
Dhambi ya Mauti hutupotezea;
1. Upendo ndani mwetu
2. Neema ya Utakaso


Anayekufa akiwa na dhambi ya mauti huenda wapi?
Anayekufa akiwa na dhambi ya mauti hutupwa motoni milele. (Mt 25:41)


Dhambi nyepesi ni nini?
Dhambi nyepesi ni kosa la kuvunja Amri ya Mungu au ya Kanisa katika jambo dogo, au jambo kubwa kwa makusudi yasiyo kamili. (1 Yoh 5:17)


Dhambi nyepesi hutupotezea nini?
1. Hudhoofisha upendo ndani mwetu
2. Huzuia Maendeleo ya roho zetu kwa kuzuia fadhila na kutenda mema.


Adhabu ya dhambi ndogo ni nini?
Adhabu ya dhambi ndogo ni mateso duniani na Toharani


Je, Tunawajibika kwa dhambi zilizotendwa na wengine?
Ndiyo, Tunawajibika kwa dhambi zilizotendwa na wengine iwapo tunazichangia kwa kutenda kosa husika.
Mfano Utoaji wa Mimba, anayetolewa, anayetoa, anayeshauri na aliyejua lakini hakuzuia wote wanatenda dhambi.


Dhambi zinazomlilia Mungu ni zipi?
Dhambi zinazomlilia Mungu ni;
1. Kuua Binadamu, Mfano Kaini na Abeli
2. Ulawiti na ushoga. (Wag 5:18-21)
3. Kilio cha wanaogandamizwa
4. Kilio cha mgeni, mjane, yatima na walemavu
5. Kukosea haki waajiriwa.


Sakramenti ya Kitubio ni nini?
Sakramenti ya Kitubio ndiyo Sakramenti ya kuwaondolea watu dhambi walizotenda baada ya Ubatizo (Yoh 20:22-23)


Lini na kwa maneno gani Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio?
Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio jioni ya ufufuko wake alipowapulizia mitume na kuwaambia maneno haya “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi watakua wameondolewa, wowote mtakaowafungia dhambi watakua wamefungiwa” (Yoh 20:22-23)


Mwenye kuwaondolea watu dhambi ni nani?
Mwenyezi Mungu pekee yake aweza kuwaondolea watu dhambi. Ndiye aliyewapa Mitume, Maaskofu na Mapadri uwezo wa kuwaondolea watu dhambi (Yoh 20:21-23)


Nani yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio?
Kila mkristo aliyetenda dhambi yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio


Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa haya
1. Kutafuta dhambi moyoni (Yoh 3:20-21)
2. Kujuta dhambi
3. Kukusudia kuacha dhambi
4. Kuungama kwa padre
5. Kutimiza malipizi
6. Kumshukuru Mungu aliyemwondolea dhambi


Wakati wa Sakramenti ya Kitubio Utamwomba Roho Mtakatifu kwa sala gani?
Utamuomba Roho Mtakatifu kwa sala hii:
Uje Roho Mtakatifu unisaidie nitambue dhambi zangu, nijute sana, niungame vema, nipate kutubu kweli. Amina


Kutafuta dhambi maana yake ni nini?
Kutafuta dhambi maana yake ni kujiuliza moyoni dhambi nilizotenda Tangu ungamo la mwisho (Ef 4:17-32)


Utafuteje dhambi wakati wa kujiandaa kuungama?
Tafuta dhambi kwa njia hizi
1. Kwa kukumbuka uliyokosa kwa mawazo, kwa maneno na kwa vitendo
2. Katika Amri za Mungu na za Kanisa
3. Katika vichwa vya dhambi
4. Katika kutimiza wajibu


Kutubu dhambi maana yake ni nini?
Kutubu dhambi maana yake ni kuona uchungu na chuki moyoni juu ya dhambi tulizotenda na kukusudia kutotenda dhambi tena (Yoh 8:11)


Kwa nini tujute dhambi zetu?
Tunajuta dhambi zetu kwa sababu tumeukosea Utatu Mtakatifu na tunastahili adhabu yake, na pia bila majuto hatuwezi kupata maondoleo ya dhambi.


Kuna majuto ya namna ngapi?
una majuto ya namna mbili,
1. Majuto kamili/Majuto ya mapendo
2. Majuto yasiyokamili/majuto pungufu/majuto ya hofu


Majuto kamili ni nini?
Majuto kamili ni kujuta kwa sababu tumemchukiza Mungu mwenyewe aliye mwema na mpendelevu kabisa


Majuto yasiyo kamili au majuto pungufu ni nini?
Majuto yasiyokamili ni kujuta kwa sababu tumepoteza furaha za Mbinguni na tunahofia adhabu ya Mungu


Asiyejuta aweza kuondolewa dhambi?
Asiyejuta hawezi kuondolewa dhambi kabisa, na anayeungama bila kujuta anatenda dhambi kubwa ya kufuru.


Kabla ya kuungama ni lazima kufanya nini?
Kabla ya kuungama ni lazima kukusudia kuacha dhambi na kuepuka nafasi kubwa ya dhambi bila kusahau kufuata hatua sita za kabla na baada ya kupokea kupokea Sakramenti ya Kutubio ambazo ni,
(1) kuwaza/kutafuta dhambi moyoni,
(2)kutubu/ kujuta,
(3)kukusudia kuacha dhambi,
(4)kuungama kwa padri,
(5)kutimiza kitubio,
(6)kumshukuru Mungu


Anayetaka kweli kuacha dhambi afanye nini?
Anayetaka kuacha dhambi afanye nguvu kuvishinda vishawishi, asali/aombe na apokee Sakramenti Mara nyingi hasa Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi Takatifu.


Kuungama ni kufanya nini?
Kuungama ni kumwambia Padri wazi wazi dhambi zako ulizotenda, zipi na ngapi ili upate maondoleo.


Anayeficha kusudi dhambi ya mauti katika ungamo anaondolewa?
Haondolewi, Bali anatenda dhambi kubwa ya kukufuru Sakramenti ya Kitubio. (Mt 7:21-23, Yoh 20:23, Gal 6:7)


Anayekufuru Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Yampasa kuziungama tena dhambi zake zote alizotenda tangu ondoleo la mwisho


Padri anaondolea dhambi mahali pa nani?
Padri anaondolea dhambi mahali pa Mungu


Padri anaondolea dhambi kwa maneno gani?
Padre anaondolea dhambi kwa maneno haya: Nami “Nakuondolea dhambi zako zote kwa Jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu”.


Kitubio tuwezacho kupewa na padre ni nini?
Kitubio tuwezacho kupewa na Padre ni kama sala, kufunga, kutoa sadaka kwa maskini, kusoma maandiko matakatifu, kuwatazama wagonjwa, n.k.


Kitubio tupewacho na padre chatosha?
Ni shida kutosha. Mara nyingi chataka malipizi ya hapa duniani kama kufunga, magonjwa, masumbuko, sala n.k mateso yasipotosha hapa duniani yatakamilishwa toharani


Kutimiza malipizi maana yake ni ni nini?
Kutimiza malipizi maana yake ni kutekeleza kiaminifu sala au matendo aliyotuagiza padre muungamishi ili kulipa adhabu za muda. (Rom 8:17)


Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema zipi?
Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema hizi;
1. Maondoleo ya dhambi zote kubwa na adhabu ya milele
2. Maondoleo ya dhambi ndogo na adhabu nyingine za muda (Isa 6:5-7, Yoh 8:11)
3. Twarudishiwa na kuongezewa neema ya utakaso
4. Twasaidiwa kuepa dhambi na twapata nguvu ya kutenda mema
5. Twarudishiwa tena mastahili tuliyopoteza kwa dhambi zetu


Mkristo akipokea Ekaristi Takatifu akiwa na dhambi rohoni anatenda dhambi gani?
Mkristo akipokea Ekaristi Takatifu akiwa na dhambi anatenda dhambi kubwa yaani kufuru Sakramenti.
26 Maana kila mnapokula mkate huu na kukinywa kikombe hiki, mwatangaza kifo cha Bwana, mpaka atakapokuja. 27 Kwa hiyo, kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana. (1 Kor 11;26 – 27)
28Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho; 29 maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe. 30 Ndiyo maana wengi kati yenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine kadhaa wamekufa. 31 Kama tungejichunguza wenyewe vizuri hatungeadhibiwa hivyo. 32Lakini tunapohukumiwa na Bwana, tunafunzwa tuwe na nidhamu, ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu. (1 Kor 11;28 – 32)
Melkisedeck Leon Shine

Editor: Melkisedeck Leon Shine. About Me | Contact Me | LinkedIn | TikTok | WhatsApp

Read and Write Comments
Shopping Cart