Mafundisho ya Katekisimu

Mambo ya Muhimu kufahamu kuhusu Mungu

Je, Yatupasa kumtolea Mungu shukrani?

Ndiyo, Yatupasa kumtolea Mungu shukrani kila wakati hasa kwa kuadhimisha Ekaristi Takatifu

Nani ameumba vitu vyote?

Mungu ameumba vitu vyote

Mungu ni nani?

Mungu ndiye muumba wa kila kitu katika uwingu na nchi, Mkubwa wa ulimwengu mwenye kuwatuza watu wema na kuwaadhibu watu wabaya.
“8Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.’’ 9‘‘Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba : “Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe.(Mt. 6:8-9).
17Yesu akamwambia, ‘‘Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ’’ (Yoh 20:17)

Mungu ni Muumba vyote maana yake ni nini?

Mungu ni Muumba vyote Maana yake amefanya vitu vyote kwa kutaka tu pasipo kutumia chochote. (2Wamakabayo 7:28, Yoh 1:3)

Mungu ni nini?

Mungu ni Roho kamili na ukamilifu wake hauna mipaka. (Yoh. 4:24, Kut.3:13-15, Zb. 144:3)

Mungu ni Roho maana yake ni nini?

Mungu ni Roho maana yake haonekani wala hashikiki. (Lk: 24:39)

Mungu ni mweza wa yote maana yake ni nini?

Mungu ni mweza wa yote maana yake kila atakalo hufanya. (Zab 135:6)

Mungu ni wa Milele maana yake ni nini?

Mungu ni wa Milele maana yake hana mwanzo wala mwisho, amekuwapo kabla ya nyakati, yupo na atakuwapo baada ya nyakati, yupo daima. (1Tim, 1:17)

Mungu ni mwema maana yake ni nini?

Mungu ni mwema maana yake apenda na kuvitunza viumbe vyake vyote hasa wanadamu na anawatakia mema tu. (Zab, 25:8-10)

Mungu ni Mwenye haki maana yake ni nini?

Mungu ni Mwenye haki maana yake kila mtu hupata kwa Mungu haki yake kadiri anavyostahili

Mungu aenea pote maaana yake ni nini?

Mungu aenea pote maaana yake yupo kila mahali mbinguni na duniani wala hakuna mahali asipokuwepo?. (Zab, 139:7-12)

Mungu ajua yote maana yake nini?

Mungu ajua yote maana yake ajua ya sasa, ya zamani na ya wakati ujao hata mawazo yetu

Mungu ni mwenye huruma maana yake nini?

Mungu ni mwenye huruma maana yake anawasamehe watu dhambi zao wakitubu.

Mungu ni mwenye subira maana yake ni nini?

Mungu ni mwenye subira maana yake mara nyingi akawia kuwaadhibu wakosefu maana ataka kuwapa nafasi ya kuongoka. (Eze, 33:11, Zb, 102;1-5)

Mungu wako wangapi?

Mungu yupo mmoja tuu Mkubwa wa wote na Baba wa wote. (Is: 44:6)

Katika Mungu mmoja kuna nafsi ngapi?

Katika Mungu mmoja kuna nafsi tatu nazo ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu; nafsi zote ni sawa.

Neno hili kuwa nafsi tatu kwa Mungu mmoja laitwaje?

Laitwa fumbo la Utatu Mtakatifu. (Lk, 3:21-22)

Kwa ajili gani Mwana wa Mungu (Yesu) alijifanya mtu?

Mwana wa Mungu (Yesu) alijifanya mtu kwa ajili yetu wanadamu na wokovu wetu ili atupatanishe na Mungu na kutushirikisha tabia ya umungu. (2Pet, 1:4)

Nafasi ya Heshima kwa Bikira Maria ni ipi?

Nafasi ya Heshima kwa Bikira Maria inafuata baada ya Heshima kwa Utatu Mtakatifu

Tunaanzaje kumjua Mungu?

Tunaanza kumjua Mungu kwa kuzingatia viumbe vyake, hasa dhamiri yetu.
“Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake” (Rom 1:20).

Je, tunaweza kusema juu ya Mungu?

Ndiyo, tunaweza kusema juu ya Mungu kuanzia wema, ukweli na uzuri wa viumbe vyake na kumsifu kiasi chetu kwamba ndiye wema, ukweli na uzuri wenyewe.
Lakini tukiri pia kuwa maneno yetu duni hayawezi kutosha kamwe kufafanua fumbo lake.
“Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua” (Ayu 42:3).
Tungemuelewa, asingekuwa Mungu.

Mwenyezi Mungu yukoje basi?

Mwenyezi Mungu ni ukamilifu mtupu usio na mipaka kwa milele yote.
“Tazama, Mungu ni mkuu, nasi hatumjui; hesabu ya miaka yake haitafutiki” (Ayu 36:26).
“Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” (Yoh 4:24).

Mungu akiwa Roho, viungo ambavyo pengine anapewa vina maana gani?

Mungu akiwa Roho, viungo ambavyo pengine anapewa vinamaanisha tu sifa fulani: k.mf. macho ujuzi wake, mikono uwezo wake, mabawa ulinzi wake, n.k. “Roho haina mwili na mifupa” (Lk 24:39).

Je, Mungu amewasiliana nasi?

Ndiyo, Mungu amewasiliana nasi, akijitambulisha na kujitoa kwetu, tuweze kuishi katika urafiki naye na hatimaye tushiriki heri yake.
“Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota ulizoziratibisha; mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; umemvika taji ya utukufu na heshima” (Zab 8:3-5).
“Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu” (Yoh 15:15).

Hasa Mungu amejifunua kuwa nani?

Hasa Mungu amejifunua kuwa upendo wenyewe.
“Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli” (Kut 34:6).
“Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake” (1Yoh 4:16).
“Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo” (1Yoh 4:8).

Je, Mungu amejitambulisha pia kwa jina?

Ndiyo, Mungu amejitambulisha pia kwa majina mbalimbali. Katika Agano la Kale jina muhimu kuliko yote liliandikwa “YHWH” yaani, “Mimi Ndimi”. Tangu zamani Wayahudi hawalitamki, hivyo wakilifikia wanasoma kwa kutafsiri, “Bwana”.
Ndiyo sababu katika Agano Jipya halitumiki kamwe, isipokuwa Yesu alifunua Umungu wake kwa kujisemea, “Mimi Ndimi” na kwa kukubali kuitwa, “Bwana”. Pamoja na hayo, alisali na kufundisha kusali kwa kumuelekea “ABA” yaani, “Baba”. Ndilo jina ambalo linampendeza zaidi na kutuingiza katika fumbo lake kama wana ndani ya Mwana pekee ambaye “Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba” (Fil 2:9-11).
“Msalipo, semeni, ‘Baba, jina lako litakaswe’” (Lk 11:2).
“Mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’” (Rom 8:15).

Mungu ametufunulia nini?

Mungu ametufunulia pia ukweli juu yetu wenyewe akijibu kabisa maswali yanayotusumbua kuhusu maana na lengo la maisha yetu.
Amefanya hivyo kwa maneno na matendo yanayoshikamana sana kwa kuwa maneno yanafafanua matendo, nayo matendo yanathibitisha maneno.
“Mungu hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli” (1Tim 2:4).
“Mungu si mtu, aseme uongo” (Hes 23:19).
Yeye hadanganyiki wala hadanganyi.

Mungu akiwa wema mkuu na mwenye uwezo wote, mbona katika viumbe vyake kuna ubaya? Kwa nini Mungu anaruhusu mabaya na maovu?

Kwa nini dhambi zipo?

Mungu akiwa wema mkuu na mwenye uwezo wote, hakuumba ubaya wowote. Tena kila anapovumilia ule uliosababishwa na viumbe vyenye hiari anaufanya uzae mema makubwa zaidi kwa njia tusizoweza kuzifahamu vizuri hapa duniani.
“Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu… Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo” (Mwa 45:4-5; 50:20).

Mungu aliwahi kujifunua kwa watu gani?

Mungu aliwahi kujifunua kwa wazazi wetu wa kwanza, akaendelea hasa kwa taifa la Israeli, hadi alipomtuma Mwanae ajifanye mtu wa taifa hilo teule.
“Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana” (Eb 1:1-2).

Je, ufunuo wa Mungu unaendelea hata leo?

Hapana, ufunuo wa Mungu hauendelei, kwa sababu alikwisha kuukamilisha kwa kumtuma duniani Neno wake wa milele.
“Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua” (Yoh 1:17-18).
Baada yake hauwezekani ufunuo mpya. Hatutakiwi kumuamini yeyote akidai eti, ametumwa kukamilisha kazi ya Yesu; kwa kuwa mwenyewe alisema,
“Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe” (Math 24:35).
“Ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe! Kama tulivyotangulia kusema, na sasa nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe!” (Gal 1:8-9).

Ufunuo wa Mungu unatufikiaje miaka elfu mbili baada ya Kristo?

Ufunuo wa Mungu unatufikia kupitia Kanisa lake, lililokabidhiwa Mapokeo ya Mitume na linaloongozwa na Roho Mtakatifu hadi ukweli wote.
Yesu aliahidi kwamba,
“Yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake” (Yoh 16:13).
“Maana Roho huchunguza yote hata mafumbo ya Mungu” (1Kor 2:10).

Je, Mungu amegawanyika sehemu tatu?

Hapana, Mungu hagawanyiki hata kidogo, bali daima ni Umoja kamili.
“Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja” (Mk 12:29).
Tumuabudu yeye peke yake katika nafsi tatu, na Utatu wa nafsi katika Umoja wa hali yake, tusichanganye nafsi wala kugawa Umungu. Baba si Mwana wala Roho Mtakatifu. Mwana si Baba wala Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu si Baba wala Mwana. Lakini milele yote nafsi hizo tatu ni Mungu yuleyule pasipo tofauti ya kuzitenganisha: kila moja imo ndani ya nyingine.
“Mimi na Baba tu umoja” (Yoh 10:30).

Tumejuaje kuwa Mungu ni Umoja wa nafsi tatu?

Tumejua kuwa Mungu ni Umoja wa nafsi tatu kwa sababu Baba aliwatuma kwetu Mwanae na Roho Mtakatifu.
“Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake. Na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, ‘Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye’” (Math 3:16-17).
Naye akaagiza, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu” (Math 28:19).
Ni nafsi tatu zenye jina moja, yaani Umungu mmoja tu.

Umoja wa Mungu unategemea nini?

Umoja wa Mungu unategemea hasa kwamba Mwana na Roho Mtakatifu wanachanga Umungu wa Baba, ambaye wanatokana naye pasipo utengano wowote. Baba anajifahamu na kujipenda: wazo analojifahamu ndiye Mwana, upendo anaojipenda katika wazo hilo ndiye Roho Mtakatifu.
“Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu” (Yoh 17:24).

Je, nafsi tatu za Mungu zina Umoja hata katika utendaji?

Ndiyo, nafsi tatu za Mungu zina Umoja hata katika utendaji, kila nafsi akiuchangia kulingana na sifa yake maalumu ndani ya Utatu. Baba Mwenyezi sifa yake ni Uwezo. Mwana kama Neno la Baba sifa yake ni Hekima. Roho kama Pumzi ya uhai ya Baba sifa yake ni Upendo.
Katika Uwezo wake Baba anafanya yote kwa Hekima na Upendo, hasa katika utume wa Mwana aliyefanyika mtu na katika utume wa Roho kama paji.
“Amin, amin, nawaambia: Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vilevile” (Yoh 5:19).

Mungu angeweza kuzuia watu wasitende dhambi?

Ndiyo, Mungu angeweza kuzuia watu wasitende dhambi, lakini aliwaacha watende kwa hiari yao awaonyeshe ukuu wa huruma yake.
“Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote” (Rom 11:32).

Yesu ni Mungu au mtu?

Yesu ni Mungu na mtu kwa pamoja, ndiyo sababu ni mshenga pekee kati ya Mungu na watu. “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, mwanadamu Kristo Yesu” (1Tim 2:5). “Katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili” (Kol 2:9). Hivyo ni Mungu kweli na mtu kweli.

1 Hapo mwanzo, kabla ya kuwapo kitu kingine cho chote, aliku wapo Neno. Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye alikuwa Mungu. 2 Tangu mwanzo Neno amekuwa na Mungu. 3 Vitu vyote viliumbwa na yeye, wala hakuna cho chote kilichoumbwa ambacho hakukiumba. 4 Uzima ulikuwa ndani yake na uzima huo ndio ulikuwa nuru ya watu. 5 Nuru hiyo huangaza gizani na giza haliwezi kamwe kuizima.
6 Mtu mmoja aitwaye Yohana alitumwa na Mungu 7 awaambie watu kuhusu hiyo nuru, ili kwa ushuhuda wake wapate kuamini. 8 Yohana mwenyewe hakuwa ile nuru. Yeye alitumwa kuishuhudia hiyo nuru. 9 Nuru halisi ambayo inawaangazia watu wote ilikuwa inakuja ulim wenguni. 10 Neno alikuwepo ulimwenguni, lakini japokuwa aliumba ulimwengu, watu wa ulimwengu hawakumtambua! 11 Alikuja nyumbani kwake, lakini watu wake hawakumpokea! 12 Bali wote waliompokea na kumwamini aliwapa haki ya kufanywa watoto wa Mungu. 13 Hawa hawakuwa watoto wa Mungu kwa kuzaliwa kwa njia ya asili, wala kwa mapenzi au mipango ya watu bali wamezaliwa na Mungu mwenyewe.
14 Neno akawa mwanadamu akaishi kati yetu akiwa amejaa utu kufu na kweli. Tuliona utukufu wake, utukufu wa Mwana pekee wa Baba. 15 Yohana alishuhudia habari zake, akatangaza: “Huyu ndiye yule niliyewaambia kuwa, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi kwa kuwa alikuwapo kabla sijazaliwa.”’ 16 Na kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema tele. 17 Musa alitule tea sheria kutoka kwa Mungu, lakini Yesu Kristo ametuletea neema na kweli. 18 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Lakini Mwanae pekee, ambaye ana uhusiano wa karibu sana na Baba yake, amemdhihirisha Mungu kwetu. Yohana 1:1-6:37

5 Tomaso akamwuliza, “Bwana, hatujui unakokwenda; tutaijuaje njia?” 6 Yesu akawaam bia, “Mimi ndiye Njia na Kweli na Uzima; mtu hawezi kufika kwa Baba bila kupitia kwangu. 7 Kama mngekuwa mnajua mimi ni nani, mngemfahamu na Baba yangu. Tangu sasa mnamfahamu Baba yangu na mmemwona.”
8 Filipo akamwambia Yesu, “Bwana, tuonyeshe Baba yako nasi tutaridhika.” 9 Yesu akamjibu, “Filipo, imekuwaje hunifahamu baada ya mimi kuwa pamoja nanyi muda wote huu? Mtu ye yote ambaye ameniona mimi, amemwona Baba. Sasa inakuwaje unasema, ‘Tuonyeshe Baba’? 10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba yangu, na Baba yangu yuko ndani yangu? Mambo ninayowaambia siyasemi kwa mamlaka yangu mwenyewe, bali yanatoka kwa Baba yangu ambaye anaishi ndani yangu, na ndiye anayetenda haya yote. Yohane 14:5-10

29 Baba yangu ambaye amenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwatoa hawa kutoka katika mikono yake. 30 Mimi na Baba yangu tu mmoja.”
31 Kwa mara nyingine wale Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo. 32 Yesu akawauliza, “Nimewaonyesha mambo mengi mazuri kutoka kwa Baba yangu. Kati ya hayo ni lipi linalosababisha mtake kunipiga mawe?” 33 Wao wakamjibu, “Tunataka kukupiga mawe si kwa sababu ya mambo mema uliyotenda bali ni kwa kuwa umekufuru. Wewe ni mtu tu lakini unajiita Mungu.” Yohane 10: 29-33

Yesu anapatikana wapi? Yesu anakaa wapi? Yesu Yupo wapi kwa sasa?

Yesu kama Mungu yupo kila mahali, hakuna mahali asipokuwepo. Yesu kama mwanadamu yupo Mbinguni kwa Baba na anakaa nasi duniani katika Maumbo ya Mkate na Divai Katika Ekaristi.


Je, Umungu na utu wa Yesu vinachanganyikana?

Hapana, Umungu na utu wa Yesu vimeunganika katika nafsi moja visichanganyikane, kwa kuwa ndani yake hali hizo mbili zinatenda kila moja ya kwake.
“Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, ‘Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu’” (Mk 15:39).

Je, Mwana wa Mungu tangu atwae mwili ni mtu kamili mwenye akili na utashi wa kibinadamu?

Ndiyo, Mwana wa Mungu tangu atwae mwili ni mtu kamili mwenye akili na utashi wa kibinadamu. Katika umoja wa nafsi yake vipawa hivyo vinatenda kulingana na Umungu anaouchanga na Baba na Roho Mtakatifu milele.
“Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake” (Yoh 14:10).

Kwa nini Maria anastahili kuitwa “Mama wa Mungu”?

Maria anastahili kuitwa “Mama wa Mungu” kwa sababu Mwana wa milele wa Mungu, ambaye ni Mungu sawa na Baba, alifanyika mtu toka kwake. Akiwa mja mzito alishangiliwa: “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?
” (Lk 1:42-43).

Je, Bikira Maria ni kama Bahasha au chombo cha kumleta Yesu tuu Duniani au anayo thamani zaidi?

Bikira Maria sio kama bahasha au chombo cha kumleta Yesu tuu duniani. Yesu ametokana na Bikira Maria katika ubinadamu wake. Mwili wa Yesu wa kiubinadamu ni sehemu au uzao wa Bikira Maria. Bikira Maria anayo uhusiano wa damu na Yesu Kristu. Ndiyo maana Mungu alimtakasa Bikira Maria Ili atakayezaliwa kutoka kwake awe na yeye mtakatifu.
Mungu alimtakasa Bikira Maria kabla ya Kuamua kuzaliwa kupitia yeye kwa kuwa Mungu ni Mtakatifu. Ubinadamu wa Yesu (MWILI – Nyama na Damu) asili yake ni Bikira Maria.

Kwa nini Yesu alishawishiwa/alijaribiwa na Shetani?

Yesu alishawishiwa na Shetani kwa kuwa ni mtu kweli, akamshinda kwa niaba ya watu wote, akituonyesha namna ya kumtii Mungu moja kwa moja, “hata mauti, naam, mauti ya msalaba” (Fil 2:8).
“Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki” (Rom 5:19).

Je, Mungu Baba alihusika na sadaka ya Mwanae?

Ndiyo, Mungu Baba alihusika sana na sadaka ya Mwanae, kwa sababu;
“Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake… Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika yeye” (2Kor 5:19,21).

Roho Mtakatifu ni nani?

Roho Mtakatifu ni upendo wa Mungu, nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu, mwenye Umungu mmoja na Baba na Mwana.
“Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:5).
Ametumwa kwetu atufanyie kazi pasipo kuonekana.
“Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho” (Yoh 3:8).
“Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” (Rom 8:14).

Je, tumuadhimishe Mungu katika Nafsi zake tatu pia?

Ndiyo, tumuadhimishe Mungu katika Nafsi zake tatu pia: Baba kama asili ya umungu na ya uhai wote, Mwana kama Neno wake aliyejifanya mtu atukomboe, tena Roho Mtakatifu kama Upendo wao ambao unawaunganisha na kututakasa.
Pamoja na viumbe vyote tuwaimbie usiku na mchana, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja!” (Ufu 4:8).
“Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” (Yoh 4:24).

Hamu kuu ya binadamu ni ipi?

Hamu kuu ya binadamu ni kumwona Mungu

Je, Yatupasa kumwomba Roho Mtakatifu?

Ndiyo, kwani twataka kwake maonyo na msaada. Tusipokuwa na neema yake hatuwezi kutenda jambo jema la kufaa kutuokoa. (Yoh 16:13)

Je, Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha umuhimu wa kusamehe na kupokea msamaha katika maisha ya Kikristo?

Neno la Mungu linatufundisha kuhusu msamaha na upendo, ndiyo maana Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha umuhimu wa kusamehe na kupokea msamaha katika maisha yetu ya Kikristo. Kwa sababu kwa kufanya hivyo tunaonyesha upendo wa Mungu kwa wengine na kufungua mlango wa huruma ya Mungu kwetu.

Katika kitabu cha Mathayo, Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kwamba wanapaswa kusamehe kila mara wanapowasamehe wengine. “Kwa maana kama mnavyowasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi” (Mathayo 6:14). Kusamehe sio tu ni amri ya Mungu, lakini pia ni muhimu kwa amani ya akili yetu na afya ya mwili.

Kusamehe ni ngumu, lakini hatuwezi kufikia ukamilifu wa Kikristo bila kuwa na uwezo wa kusamehe. Ni muhimu kwa Kanisa Katoliki kutoa mwongozo juu ya jinsi ya kuomba msamaha na kusamehe, kwa sababu tunajua kwamba sisi sote hukosea na tunahitaji msamaha kutoka kwa Mungu na wengine.

Kwa mujibu wa Katekisimu ya Kanisa Katoliki, msamaha ni “kutoka moyoni kutenda upendo wa huruma kwa yule aliyesababisha uchungu” (CCC 2839). Kupokea msamaha pia ni muhimu kwa sababu inatuwezesha kuyaponya majeraha ya roho zetu na kujenga upya uhusiano wetu na wengine.

Kanisa Katoliki linatufundisha kuwa tuna wajibu wa kuomba msamaha kwa wale ambao tumeumiza au kukosea. Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kuwa “kama upepo wa mashariki unavyoondoa mawingu, ndivyo unafanyika ugonjwa unaotokana na uchungu na hasira na kutoa nafasi kwa upendo wa Mungu” (CCC 2839). Kwa hiyo, kama Wakristo, tunapaswa kuwa tayari kuomba msamaha na pia kusamehe wengine.

Kusamehe hakumaanishi kwamba tunapaswa kusahau kile kilichotokea au kufumbia macho uovu uliofanywa dhidi yetu. Hata hivyo, tunapaswa kufikiria kwa makini juu ya kile kilichotokea na kujifunza kutokana na hali hiyo ili tusifanye kosa kama hilo tena. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kuzuia kutokea kwa uchungu na kusaidia kujenga uhusiano bora.

Kwa hiyo, ni muhimu kwa Kanisa Katoliki kuendelea kuhubiri na kufundisha umuhimu wa kusamehe na kupokea msamaha. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kusaidia kujenga uhusiano mzuri na Mungu na wengine, na kufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kama Mtume Paulo alivyosema, “Vumilieni ninyi kwa ninyi, mkisameheana kama Kristo alivyowasamehe ninyi, ili Mungu awasamehe ninyi” (Wakolosai 3:13).

Ni nini imani ya Kanisa Katoliki kuhusu ngono na maadili ya kijinsia?

Kanisa Katoliki ni moja ya madhehebu makubwa duniani, na imani yake juu ya ngono na maadili ya kijinsia ni muhimu sana. Kanisa hili linazingatia mafundisho ya Biblia na Catechism ya Kanisa Katoliki katika kuelezea maadili ya kijinsia na ngono.

Kwa mujibu wa Kanisa Katoliki, ngono ni kitendo kinachofanywa kati ya mwanamume na mwanamke, ambao wamefunga ndoa. Ni kitendo kitakatifu kinachopaswa kufanywa kwa upendo na kwa lengo la kuwaleta watoto duniani. Ni dhambi kufanya ngono kabla ya ndoa au kufanya ngono bila lengo la kuzaa watoto.

Kanisa Katoliki linasisitiza kuwa wanaume na wanawake wote ni sawa mbele ya Mungu na wanapaswa kutendewa kwa heshima na upendo. Uhusiano wa kimapenzi kati ya wanaume ama kati ya wanawake una kinyume na mafundisho ya Kanisa. Hata hivyo, Kanisa Katoliki linapenda na kuheshimu watu wote bila kujali kama wana tabia za kimapenzi ama la.

Kanisa Katoliki linasisitiza kuwa ngono inapaswa kutendeka kwa heshima na utu wa binadamu. Ni muhimu kufuata maadili ya kijinsia kwa kuepuka dhambi ya uzinzi, ngono haramu, na ukahaba. Kila mtu anapaswa kuishi maisha yenye maadili ya kijinsia, na kuhakikisha wanapata elimu ya kutosha juu ya maadili haya.

Katika Catechism ya Kanisa Katoliki, tunasoma "Maadili ya kijinsia ni sehemu ya maadili ya kichungaji yanayohusiana na afya ya mtu na pia kuhusiana na maadili ya ndoa inayohusisha upendo wa kudumu kati ya mume na mke." (CCC 2351)

Kanisa Katoliki linasisitiza umuhimu wa kutumia njia za uzazi wa mpango ambazo hazimzuia Mungu kwa kuua mimba. Kanisa linapendekeza njia za uzazi wa mpango kama vile uzazi wa mpango wa asili, kufahamu kwa kina kuhusu mzunguko wa hedhi, na njia za uzazi wa mpango zinazorejesha udhibiti wa uzazi kwa mwanamke.

Kanisa Katoliki linakemea ngono kwa ajili ya kufurahisha nafsi ama kwa ajili ya ngono yenyewe, bila lengo la kuzaa watoto. Ngono inapaswa kuwa kwa lengo la kuunganisha mume na mke na kuwaleta watoto duniani kama zawadi kutoka kwa Mungu.

Hatimaye, Kanisa Katoliki linasisitiza umuhimu wa kuishi maisha ya utakatifu. Wanawake na wanaume wote wanapaswa kuishi maisha safi ya kijinsia, kufuata maadili ya kijinsia, kuheshimiana, na kuepuka kila aina ya dhambi. Kwa kufuata mafundisho ya Kanisa na kufuata Biblia na Catechism, tunaweza kuishi maisha yenye maadili ya kijinsia na mafanikio katika maisha.

Je, Kanisa Katoliki linaheshimu na kufundisha juu ya maombi kwa watakatifu?

Je, Kanisa Katoliki linaheshimu na kufundisha juu ya maombi kwa watakatifu? Jibu ni ndio! Kanisa Katoliki inathamini na kuheshimu watakatifu kama walio ndani ya utukufu wa mbinguni na walinzi wema kwa ajili yetu. Naam, tunaweza kusali na kuwaomba watakatifu wamsaidie Mungu atusikilize na kutusaidia katika mahitaji yetu.

Kanisa linatambua kuwa watakatifu wanaishi katika utukufu wa mbinguni pamoja na Mungu, na wanaweza kusikia sala zetu na kutuombea mbele za Mungu. Kama vile tunavyoomba msaada kutoka kwa marafiki na familia zetu, tunaweza pia kuomba msaada kutoka kwa watakatifu.

Katika Biblia tunasoma juu ya watakatifu wakati wa Agano la Kale na Jipya. Kwa mfano, 2 Wafalme 2:9 inaelezea jinsi Eliya alivyoondoka duniani na kwenda mbinguni akiongozana na gari la moto na farasi wa moto. Na Luka 16:19-31 inaelezea mfano wa tajiri na Lazaro, ambapo Lazaro alipewa heshima ya kuwa katika utukufu wa mbinguni. Watakatifu pia wanatajwa katika kitabu cha Ufunuo 5:8 ambapo Biblia inaeleza kuwa wao wana uwezo wa kuleta sala zetu mbele ya Mungu.

Lakini ni muhimu kukumbuka kuwa sala kwa watakatifu sio sawa na ibada ya dini. Katika Kanisa Katoliki, tunaamini kuwa Mungu pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa na kutukuzwa. Kwa hivyo, kutafuta msaada kutoka kwa watakatifu sio sawa na kuwaabudu.

Kanisa Katoliki linathamini sana maombi kwa watakatifu, na inawafundisha waumini wake kuomba msaada kutoka kwa watakatifu. Kulingana na Katekisimu ya Kanisa Katoliki, "Kanisa linawadhamini waumini wake kuomba msaada kutoka kwa watakatifu walioko mbinguni na kuwaombea ili waweze kutusaidia kwa upendo wao na ujuzi wao" (956).

Sala kwa watakatifu inaonekana kama kitu kimoja na sala kwa Mungu. Kwa kuwa watakatifu wanaiheshimu na kuitumikia dini yetu katika maisha yao ya kidunia, watakatifu wanaweza kutusaidia katika sala zetu kwa kuwa wao ni marafiki wazuri wa Mungu. Kwa hivyo, Kanisa linatuhimiza sisi kusali kwa watakatifu kwa sababu kuwa karibu na watakatifu kunaweza kutusaidia kuwa karibu zaidi na Mungu.

Kwa hiyo, kushiriki katika maombi kwa watakatifu sio tu inathibitisha imani yetu katika utukufu wa mbinguni bali pia inaturuhusu kuwa karibu zaidi na watakatifu na Mungu. Kwa kuwa tunawaombea watakatifu kwa msaada wao, tunalinda imani yetu na tunatafuta msaada wake kwa upendo.

Kwa hivyo, kuna thamani kubwa katika maombi kwa watakatifu na Kanisa Katoliki linawaheshimu na kuwajumuisha katika sala zetu za kawaida. Sala kwa watakatifu inatuwezesha kuwa karibu na watakatifu na Mungu, na haitupunguzi kwa kumwabudu Mungu pekee. Kwa hiyo, hebu tuendelee kusali na kuomba msaada kutoka kwa watakatifu na wawe walinzi wetu wema katika safari yetu ya kiroho.

Maswali na Majibu kuhusu dhamira

Dhamiri adilifu ni nini?
Dhamiri adilifu, iliyo ndani kabisa mwa mtu, ni uamuzi wa akili ambao kwa wakati wake unamuagiza mtu atende mema na kukwepa maovu


Katika hukumu zake dhamira ifuate nini?
Katika hukumu zake dhamira ifuate daima Injili, Amri za Mungu na za Kanisa na wajibu zetu.


Twajenga na kutunza dhamira zetu namna gani?
Twajenga na kutunza dhamira zetu kwa;-
1. Kufuata sauti ya Roho Mtakatifu
2. Kuzingatia mafundisho ya dini
3. Kuzingatia mila na desturi njema tulizopata katika malezi.
4 Kufuata mifano na tabia njema ya wenzetu na ya Watakatifu


Hadhi ya nafsi ya mtu inadai nini kuhusu dhamiri adilifu?
Hadhi ya nafsi ya mtu inadai unyofu wa dhamiri adilifu, yaani upande wa akili na sheria ya Mungu


Dhamiri adilifu inaundwa namna gani iwe nyofu na ya kweli?
Dhamiri nyofu inayosema kweli inaundwa kwa;
1. Malezi
2. Upokeaji wa neno la Mungu
3. Upokeaji wa Mafundisho ya Kanisa
4. Sala
5. Utafiti wa dhamiri


Dhamiri adilifu inatengenezwa na kusaidiwa na nini?
Dhamiri adilifu inatengenezwa na vipaji vya Roho Mtakatifu na kusaidiwa na mashauri ya watu wenye busara.


Dhamiri inatakiwa kufuata daima masharti gani?
Dhamira inatakiwa kufuata daima masharti yafuatayo
1. Hairuhusiwi kutenda maovu kusudi yapatikane mema
2. Yoyote muyatakayo mtendewe na watu, ninyi watendeeni vivyo hivyo. (Mt 7:12)
3. Upendo hufuata daima nia na heshima kwa jirani na kwa dhamira yake

Maswali na Majibu kuhusu Rehema

Rehema ni nini?
Rehema ni msamaha au ondoleo la adhabu ya dhambi tulizostahili sababu ya dhambi zilizokwisha ondolewa

Rehema hutolewa na nani?
Rehema hutolewa na Kanisa Katoliki kwa kutugawia mastahili ya Yesu Kristo, Bikira Maria na Ya Watakatifu

Kuna Rehema za namna ngapi?
Rehema za namna mbili
1. Rehema kamili
2. Rehema pungufu (Rehema isiyo kamili)

Rehema kamili ni nini?
Rehema kamili ni msamaha wa kufutiwa adhabu zote za muda za dhambi

Rehema isiyo kamili (pungufu) ni nini?
Rehema isiyo kamili (pungufu) ni msamaha wa kupunguziwa adhabu ya dhambi

Adhabu za dhambi huondolewa kwa namna gani? Jinsi ya kupata rehema
Adhabu za dhambi huondolewa kwa;
1. Kufanya malipizi au majuto kamili
2. Kuvumilia taabu na mateso katika maisha
3. Kuvishinda vishawishi na majaribu
4. Kusali sala mbalimbali
5. Kuomba Misa kwa ajili hiyo.
6. Kusoma neno la Mungu na kulitafakari na kulinganisha na maisha yetu ya kila siku
7. Utakaso wa Toharani kama adhabu hizi hazikuondolewa duniani

Kipimo cha Rehema ni nini?
Kipimo cha Rehema hutegemea uzito wa majuto na mapendo mtu aliyonayo kwa Mungu Muumba wake. (1Kor 9:11)

Mtu akitaka kupata Rehema za Kanisa Katoliki yampasa nini?
Mtu akitaka kupata Rehema za Kanisa Katoliki yampasa;
1. Kujua na kufuata utaratibu unaotolewa na Kanisa Katoliki wa kupata Rehema
2. Awe katika hali ya neema ya Utakaso
3. Kufanya matendo yote yanayotakiwa kwa kupata rehema hiyo, kwa mfano;
a). Hija au Kuhiji katika mwaka wa Jubilei katika Kanisa lililo teuliwa na Askofu
b). Kufanya mafungo – Kama vyama vya kitume
c). Kuzuru makaburi (Kutembelea) yaliyobarikiwa
d). Katika hatari ya kufa padri hutoa rehema pamoja na Sakramenti ya wagonjwa
e). Kusali kwa nia za Baba Mtakatifu

Maswali yanayoulizwa sana kuhusu Ibada ya Kanisa Katoliki

Masifu ni nini?

Masifu ni sala au wimbo unaomsifu na kumtambua Mungu kuwa Mungu


Ishara ndogo ya Msalaba juu ya panda la uso, mdomo, na kifua kabla ya Injili ina maana gani?

Maana yake ni kama Ahadi kuwa, Niko tayari kulifahamu Neno la Mungu kwa akili yangu, Nitalitangaza kishujaa kwa Midomo yangu, Nitalipenda na kulishika kwa Moyo wangu wote.


Kwa nini wakatoliki wanaweka sanamu Kanisani?

Tunaweka sanamu Kanisani kwa sababu tunaheshimu anayewakilishwa na sanamu hiyo kwa mfano Yesu Kristo, Mama Bikira Maria, Malaika na Watakatifu; na kamwe hatuziabudu. (Kutoka 25:18-22)
Hata Waisraeli kwenye hekalu lao walikua na sanamu kama tunavyosoma hapa;
“18 Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. 19 Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku.20 Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. 21 Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. 22 Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli. (Kutoka 25 :18-22.)
Kwa hiyo kama Mungu mwenyewe aliagiza Sanamu za Malaika zichongwe na kusema atakua hapo na kuongea na watu wake. Je sio vyema zaidi kuwa na sanamu na Picha ya Mwanae wa Pekee Yesu Kristo na kuongea na Mungu mbele yake kama alitaka ya malaika ambao sio Mungu?
Mfano mwingine ni pale Mungu alivyomwabia Musa achonge Sanamu ya Nyoka wa shaba.
“BWANA akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba na umweke juu ya mti, ye yote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama na akaishi tena.’’ 9Kwa hiyo Mose akatengeneza nyoka wa shaba na kumweka juu ya mti. Kisha wakati mtu ye yote alipoumwa na nyoka, naye akamtazama yule nyoka wa shaba, aliishi.” (Hesabu 21:8-9).
Kwa Mfano huu Je tunaweza kusema kuwa sanamu ya nyoka ina nguvu ya uponyaji kuliko ya Yesu aliye Mungu? Kumbuka hapa watu walioona sanamu hii ya nyoka hawakukoponywa na nguvu ya sanamu ya shaba bali kwa nguvu ya neema ya Mungu kupitia Imani kwa Mungu. Kwa hiyo unaposali mbele ya picha au sanamu hautegemei nguvu ya sanamu bali unategemea neema ya Mungu kwa njia ya Imani yako kwa Mungu.
Kama vile Sanamu hii ya nyoka aliyoagiza Mungu iwekwe ilivyowekwa kwa nia ya uponyaji kwa yule aitazamaye vivyo hivyo Sanamu na Picha za Kanisani zinawekwa kwa nia maalumu na kwa neema maalumu. Ndiyo maana hazifanani. Na zinabarikiwa kwa kuombewa Baraka Ili zizae neema kwa wanaozitumia.

Sanamu au picha sio haramu bali maana ya hiyo sanamu au picha ndio inaiharamisha.

Kuna tofauti kati ya kuabudu na kuheshimu. Wakatoliki wanaweka sanamu kwa heshima na sio kwa kuabudu, ndio maana unaposali mbele ya picha ya Yesu hausali ee sanamu nisaidie bali unasema ee Yesu nisaidie.
Je tuseme tunamwabudu Raisi kwa kuheshimu picha yake kwa kuiinamia? Je tunaabudu bendera kwa kuheshimu na kupigia saluti? Je taratibu zabunge za kutoa heshima na taratibu za mahakama ni kuabudu?. Je kuapa mbele ya picha ya Raisi ni kumuabudu Raisi? Je kuapa na Biblia ni kuabudu Biblia? Je tunapobusu Biblia na kuitunza kwa heshima tunaiabudu? Tofauti ya Biblia na sanamu ni nini? Je, kwenye Biblia kinachoheshimiwa ni karatasi au maana ya yale maneno kwenye karatasi. Pengine usingeheshimu kama hujajua kuyasoma.
Kuna tofauti gani kati ya biblia yenye Maandishi na msalaba wa kuchonga wenye kuonyesha kile kinachosemwa na biblia? kama unaweza kuheshimu biblia yenye karatasi tena pale unapoweza kuzisoma na pengine ungeizarau kama ni ya lugha tofauti na hujui kilichoandikwa? Je Msalaba uliobeba maana ya kile kilichoandikwa kwenye Biblia unaona si kitu? Kama Kinachoheshimiwa kwenye Biblia sio karatasi bali maana maneno yaliyoandikwa vivyo hivyo kinachoheshimiwa kwenye picha au sanamu sio chuma yake au mti ukiochongwa bali ni maana ya hiyo sanamu.
Hii ndio maana nasema kuna tofauti ya kuabudu na kuheshimu.
Kumbuka kuwa picha au sanamu yoyote ya Kikatoliki lazima ibarikiwe kwanza ndio uweze Kusali mbele yake. Inapobarikiwa inaombewa uwepo wa yule anayewakilishwa na picha/sanamu hiyo uwe pale sanamu ilipo na anayesali pale sala yake Ifike kwa mlengwa anayeonekana kwa ishara ya sanamu/picha. Kwa Mfano askofu au padri anapobariki sanamu ya Yesu anaomba kuwa “Yesu awepo pale kwenye sanamu na Neema zake”, kwa hiyo yeyote anayesali mbele ya sanamu hiyo anaamini kuwa Yesu yuko pale na anasali Mbele yake. Kwa hiyo kinachopewa heshima sio ile sanamu bali ni yule anayeonekana kwa ishara ya ile sanamu au picha.

Tofauti ya Sanamu za Kikatoliki na za kipagani ni Kwamba,

Sanamu za Kipagani: Sanamu hizi huchukuliwa kama Mungu na huabudiwa na kutolewa Sadaka kama Mungu Mwenyewe.

Sanamu za Kikatoliki: Sanamu hizi huchukuliwa kama ishara ya kile inachokiwakilisha, haiabudiwi kamwe bali inaheshimiwa tuu.

Daima Tumia Sanamu na Picha zilizobarikiwa kwani zimenuiwa uwepo wa yule inayemuwakilisha na utaongea naye hapo. Sisi tunaamini kwamba kwenye Sanamu ya Yesu kuna uwepo wa Yesu. Kama vile Mungu anavyowaambia Waisraeli katika (Kutoka 25 :22) baada ya kuwaagiza wachonge sanamu za Makerubi (Malaika) 22 Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli. (Kutoka 25 :22)Sanamu au picha ni ishara wazi ya uwepo wa kile kisichoonekana.

Jifunze kupitia Sanduku la Agano na Msalaba wa Yesu

Kwenye Agano la kale: Ndani ya hekalu la Waisraeli walikua na Sanduku la agano, sanduku hilo lilikua na vibao vya Amri za Mungu ambavyo ni Ishara ya Agano lao na Mungu na ndani ya sanduku kulikuwepo pia Mfano wa Kiti ambacho kimezugukwa na sanamu za viumbe kama malaika nyuso zao zikielekea kiti hicho Kutoka 25:10-22. Waisraeli walikua wanasali kuelekea sanduku la Agano wanapokuwa Hekaluni na hata wakiwa majumbani mwao walisali kuelekea upande lilipo Hekalu. Waisraeli walisali kuelekea Sanduku la Agano wakiamini kwamba Mungu yupo kati ya sanduku lile. Lakini sanduku lile halikuwa Mungu. Waisraeli waliona fahari juu ya Sanduku lile na walilithamini na kuliheshimu kwa kuwa lilionyesha uwepo wa Mungu na popote lilipokuwa waliamini Mungu yupo.
Kwenye Agano jipya: Wakristu wanasali Mbele ya Msalaba wa Yesu ambao unaonyesha kazi ya wokovu alioufanya Yesu kwa wanadamu ya Kuwakomboa watu kwa kifo chake Msalabani. Na Msalaba huo ni Ishara ya Ukombozi wa Agano jipya na la Milele. Kama ilivyokuwa kwa Sanduku la Agano, Wakristu wanaheshimu msalaba ambao ni ishara ya wokovu wao na wanaamini kuwa Mungu yupo kati ya Msalaba huo lakini Msalaba huo sio Mungu. Wakristu wanaona fahari juu ya msalaba wa Yesu kwa kuwa ndio ishara ya wokovu wao.
FUNZO:Kupitia Mfano wa Sanduku la Agano na Msalaba tunajifunza kuwa Vyote havikuwa Mungu ila vinaheshimiwa kwa Imani kuwa Mungu yupo pale. Vilevile, vyote ni ishara ya wazi ya Agano la Mungu na Wanadamu.

Kwa nini tunasali mbele ya Picha/Sanamu na Hasa kufanya Ishara ya msalaba?

Tunasali mbela ya sanamu kwa sababu tunaamini sanamu inaakisi uwepo wa mhusika aliyechorwa au kuchongwa kwenye hiyo sanamu/picha. Ndio maana wakatoliki wanasali kwenye picha au sanamu iliyobarikiwa tuu kwa sababu Sanamu inapobarikiwa inaombewa uwepo wayule anayewakilishwa pale.
Tunafanya ishara ya msalaba kwenye sanamu kama sala ya utangulizi ambayo inathibitisha kuwa hatuabudu kile kilichoko pale bali kile tunachokifanya tunakifanya huku tukikiri Umungu na Heshima ya Utatu Mtakatifu (Mungu; Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.). Vile vile tunamtukuza Mungu katika Utatu Mtakatifu kwa sababu ya yule anayewakilishwa na picha au sanamu.

Kwa nini watu wanabusu picha na sanamu?

Hii ni ishara ya Upendo kwa yule anayewakilishwa kwenye picha au sanamu husika. Hata katika maisha ya kawaida watu hubusu picha za wazazi na wapendwa wao. Maana ni ile ile.


Tumuadhimishe nani?

Tumuadhimishe Mungu pekee siku zote za maisha yetu kwa tumaini la kumuadhimisha milele.
“Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, nitalihimidi jina lako milele na milele. Kila siku nitakuhimidi, nitalisifu jina lako milele na milele” (Zab 145:1-2).
“Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina” (Rom 11:36).


Je, tumuadhimishe Mungu katika Nafsi zake tatu pia?

Ndiyo, tumuadhimishe Mungu katika Nafsi zake tatu pia: Baba kama asili ya umungu na ya uhai wote, Mwana kama Neno wake aliyejifanya mtu atukomboe, tena Roho Mtakatifu kama Upendo wao ambao unawaunganisha na kututakasa.
Pamoja na viumbe vyote tuwaimbie usiku na mchana, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja!” (Ufu 4:8).
“Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” (Yoh 4:24).


Tumuadhimishe Mungu kwa jinsi alivyo au kwa maajabu anayotutendea?

Tumuadhimishe Mungu kwa jinsi alivyo, halafu kwa maajabu anayotutendea tangu awali, ambayo anatujulisha kidogo jinsi alivyo.
“Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele” (Zab 136:1).


Tumuadhimishe Mungu hasa kwa maajabu gani?

Tumuadhimishe Mungu hasa kwa maajabu aliyoyatenda katika Yesu, lakini pia katika Maria na wengine ambao wamefanana naye na kutuonyesha uwezo wa neema yake kwetu.
“Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa” (Ef 1:5-6).
Yeye atakuja “ili kutukuzwa katika watakatifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki” (2Th 1:10).


Tumuadhimishe Mungu kwanza kwa njia gani?

Tumuadhimishe Mungu kwanza kwa kumsikiliza kwa makini na kumuitikia kwa imani.
“Masikio ya watu wote yalikisikiliza kitabu cha torati… watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati” (Ne 8:3,9).
Kunyamaza ni sehemu ya ibada yoyote: tunahitaji kimya ili tuelewe tunachoambiwa na tunachosema.
“Nisikieni nyote na kufahamu” (Mk 7:14).
“Hamjui mnaloliomba” (Mk 10:38).


Je, ibada zetu ziishie katika kusadiki?

Hapana, ibada zetu zisiishie katika kusadiki, kwa kuwa tangu Agano la Kale Mungu aliagiza matendo mbalimbali ya ibada yanayolisha imani.
“Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako: Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa… Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu” (Mwa 17:10,12).
“Mwanakondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja… Kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni… Ni Pasaka ya Bwana… Siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana” (Kut 12:5,6,11,14).
Kwetu sisi Wakristo ni yale tuliyoagizwa na Yesu ili yatuletee wokovu.
“Aaminiye na kubatizwa ataokoka” (Mk 16:16).


Kanisa linaitaje ibada hizo tulizoagizwa na Yesu?

Kanisa linaita ibada hizo tulizoagizwa na Yesu sakramenti, yaani mafumbo. Ziko saba: Ubatizo, Kipaimara, Ekaristi, Kitubio, Mpako wa Wagonjwa, Daraja na Ndoa. Ndiyo “mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono” (Eb 6:2) tuliyoyapata kupitia Mitume.
Tujihadhari na madhehebu yaliyopunguza sakramenti hizo saba tulizoachiwa na wema wa Yesu kwa kuwa alijua tunavyozihitaji.


Je, tuishie katika kusadiki na kuadhimisha mafumbo?

Hapana, tusiishie katika kusadiki na kuadhimisha mafumbo, kwa kuwa imani na sakramenti zinadai kutekelezwa maishani.
“Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?… Itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana” (Rom 6:2-3; 12:1).
“Nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Math 5:16).


Matendo yetu yasipomtukuza Mungu, maana yake nini?

Matendo yetu yasipomtukuza Mungu, maana yake mafumbo hayakuadhimishwa vizuri.
“Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa” (Yak 2:26).


Mungu ametuagiza matendo maalumu ya ibada kwa sababu gani?

Mungu ametuagiza matendo maalumu ya ibada kwa kuzingatia umbile letu, kwamba binadamu ni umoja wa roho na mwili, hivyo anahitaji mwili na hisi zake ili kuingiza chochote rohoni na kutokeza yaliyomo katika roho yake isiyoonekana.
Ndiyo sababu Yesu alipoletewa kiziwi mwenye utasi “akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, ‘Efatha’, maana yake, ‘Funguka!’” (Mk 7:33-34).
Hizo zote ni ishara wazi kwa milango yetu ya fahamu.


Je, hisi zetu zote zinaweza kutumika kuadhimishia mafumbo?

Ndiyo, hisi zetu zote zinaweza kutumika kuadhimishia mafumbo, kila moja kadiri ya uwezo wake: macho kwa kuona, pua kwa kunusa, kinywa kwa kuonja na kusema, mwili mzima kwa kugusa na kutenda, lakini hasa masikio kwa kupokea maneno yaletayo uzima wa Kimungu.
“Maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima” (Yoh 6:63).
“Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia… Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo” (Rom 10:13-14,17).


Kwa nini maneno ndiyo muhimu zaidi kuadhimishia mafumbo?

Maneno ndiyo muhimu zaidi kuadhimishia mafumbo kwa sababu yanafafanua ishara nyingine na kuzitia nguvu ya kututakasa.
“Kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno” (Ef 5:25-26).
Pasipo maneno hapana sakramenti yoyote.


Ishara za mafumbo zimetokana na nini?

Ishara za mafumbo zimetokana na viumbe (maji, mafuta, mkate, divai n.k.) na maisha ya jamii (kuosha, kupaka, kula na kunywa pamoja n.k.) na historia ya wokovu (kunyunyiza na kuzamisha, kuwekea mikono, kula Pasaka, n.k.),
lakini ni kwa kuagizwa na Yesu kwamba zinabeba kazi yake ya kuokoa na kutakasa.
“Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (Lk 22:19).


Maneno na ishara kwenye ibada vinaweza kubadilishwa na nani?

Maneno na ishara vinaweza kubadilishwa na waandamizi wa Mitume, waliokabidhiwa na Yesu mamlaka ya kuendeleza kazi yake katika mazingira mbalimbali hata mwisho wa dunia.
“Amin, nawaambieni: Yoyote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni, na yoyote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni” (Math 18:18).
Hao Maaskofu wanakiri hawawezi kamwe kuyabadilisha yale ambayo Yesu aliyaweka kuwa ya lazima kama yalivyo mafumbo yenyewe.
“Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi” (1Kor 11:23).
Mengine yote wanaweza kuyapanga na kuyarekebisha kadiri ya mazingira, kuanzia lugha, wakilenga daima wokovu wa watu.


Faida ya kupanga taratibu za ibada ni ipi?

Faida ya kupanga taratibu za ibada ni hasa kuhakikisha yote yafuate usahihi wa imani na maadili, yakidumisha umoja na upendo, badala ya kumuachia kiongozi au mwingine yeyote aseme na kufanya anavyotaka. Mitume wenyewe walianza kazi hiyo, wakidhibiti hata karama.
“Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga. Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri. Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu. Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue. Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze… Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni maagizo ya Bwana. Lakini mtu akiwa mjinga, na awe mjinga… Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu” (1Kor 14:26-30,37-38,40).
Polepole taratibu ziliongezeka na ibada zikapata mtiririko rasmi wa kueleweka: ndizo liturujia za mashariki na za magharibi ambazo zinaweza kuwa mbalimbali mradi zisipishane upande wa imani.


Mhusika mkuu wa mafumbo hayo ni nani?

Mhusika mkuu wa mafumbo hayo ni Mungu ambaye kwa njia hiyo anazidi kutufanyia maajabu alivyoyafanya Yesu alipokuwa duniani. Kama tunda la kutukomboa kwa kifo na ufufuko wake, Baba anatujaza humo Roho Mtakatifu kama advansi ya uzima wa milele.
“Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi yake aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake” (Ef 1:13-14).


Sisi tunahusika na mafumbo hayo kama nani?

Sisi tunahusika na mafumbo hayo kama walengwa ambao tuyatumie vema ili yazae matunda yote yaliyokusudiwa na Mungu.
Ndiyo kiini cha ukuhani wetu ambao tunashiriki ule wa Kristo tangu tubatizwe.
“Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo” (1Pet 2:4-5).


Tunapoadhimisha mafumbo hayo, Mungu anatukuzwa vipi?

Tunapoadhimisha mafumbo hayo, Mungu anatukuzwa kwa kuwa ndivyo anavyotufanya “tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo… tupate kuwa sifa ya utukufu wake” (Ef 1:4,12).
Tukipokea neema hiyo tunampatia ibada, sifa na shukrani na tunazidi kumuomba atujaze Roho Mtakatifu kwa njia ya Mwanae.
“Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina” (Ef 3:20-21).


Je, mafumbo yote saba yanazaa matunda yaleyale?

Hapana, mafumbo yote saba hayazai matunda yaleyale, bali Yesu aliweka kila moja kwa lengo maalumu, litupatie Roho Mtakatifu kadiri ya nafasi na haja fulani ya maisha yetu.
Ubatizo, kipaimara na ekaristi vinatuingiza katika fumbo la Pasaka tuweze kuishi upya kama wana wa Mungu.
Kitubio na mpako wa wagonjwa vinatuponya roho na hata mwili. Daraja na ndoa zinatufanya wahudumu wa Kanisa na wa familia.
Ni muhimu tujue tunachohitaji na tukipate vipi.
“Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa” (1Kor 11:29-31).


Tushiriki mafumbo hayo mara ngapi?

Tushiriki mafumbo hayo kadiri ya umbile la kila mojawapo. Kuna “ubatizo mmoja” (Ef 4:5) kwa sababu ni kuzaliwa upya “kwa maji na kwa Roho” (Yoh 3:5), jambo lisiloweza kurudiwa.
Vilevile katika kipaimara na daraja, karama inayopatikana kwa kuwekewa mikono na mwandamizi wa Mitume haifutiki, inadai kuchochewa tu.
“Nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu” (1Tim 1:6).
Kumbe tunahitaji ekaristi mara nyingi, kwa sababu ni chakula cha roho.
“Bwana, sikuzote utupe chakula hiki” (Yoh 6:34).
“Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo” (1Kor 11:26).


Je, mafumbo yote yanaweza kuadhimishwa na yeyote?

Hapana, si mafumbo yote yanaweza kuadhimishwa na yeyote, bali mengine yanahitaji mhudumu wake awe amepewa daraja inayoshirikisha uwezo ambao Yesu aliwapa Mitume wake.
“Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume” (Lk 6:12-13).
“Yesu aliwaambia tena, ‘Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi’. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, ‘Pokeeni Roho Mtakatifu’” (Yoh 20:21-22).
Kwa kuwa Waprotestanti hawana sakramenti ya daraja, kati yao zinapatikana sakramenti zile mbili tu zisizohitaji padri, yaani ubatizo na ndoa.


Je, tunapoadhimisha mafumbo hayo tuko peke yetu?

Hapana, tunapoadhimisha mafumbo hayo hatuko peke yetu, bali tunashiriki ibada ambayo Yesu anamtolea Baba milele.
“Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao” (Math 18:20).
Kwa kuungana na Kristo Kichwa, tunaungana na viungo vyote vya Mwili wake, vya duniani, toharani na mbinguni.
“Ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu wa kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili” (Eb 12:22-24).


Je, kuna nyakati za kufaa zaidi kumuadhimishia Mungu?

Ndiyo, kuna nyakati za kufaa zaidi kumuadhimishia Mungu. Yesu aliyesema, “Sikuja kutangua, bali kutimiliza” (Math 5:17), alifuata kalenda ya dini ya Kiyahudi, halafu kwa kufa na kufufuka amekuwa kiini cha ibada zetu zote. Hivyo Mitume waliadhimisha siku aliyofufuka kama “siku ya Bwana” (Ufu 1:10) ambapo wakutane “ili kumega mkate” (Mdo 20:7) wa ekaristi.
Vilevile kwenye Pasaka hawakuadhimisha tu kazi ya Musa, bali ukumbusho wa Yesu.
“Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo” (1Kor 5:7).
Fumbo hilo ndio moyo wa mwaka wa liturujia, yaani wa mpangilio wa maadhimisho katika mzunguko wa mwaka.
“Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo” (Kol 2:16).


Je, kuna mahali pa lazima pa kumuadhimishia Mungu?

La! Hakuna mahali pa lazima pa kumuadhimishia Mungu, kwa kuwa yeye hafungwi na mahali.
“Mungu je, atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga!” (1Fal 8:27).
“Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono” (Mdo 17:24).
Hata hivyo sisi watu tunahitaji mahali maalumu kwa matendo yetu mbalimbali, na kumwekea Mungu mahali patakatifu.
“Mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu asema: Ki wapi chumba changu cha wageni, niile Pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu?’ Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni” (Mk 14:14-15).


Hekalu ndiyo nini?

Hekalu ndipo tunapomuendea Mungu kwa ibada. Vilevile sisi wenyewe ni Mahekalu.
Yesu aliheshimu na kutakasa hekalu pekee la taifa lake kama “nyumba ya Baba” yake (Yoh 2:16), lakini alitabiri kuwa litabomolewa moja kwa moja, na kuwa watu watapaswa kuabudu ndani yake aliye hekalu hai. “Wayahudi walisema, ‘Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu?’ Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake” (Yoh 2:20-21).
“Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho” (Ef 2:22).
“Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi” (1Kor 3:16-17).


Je, sanaa zinafaa kumuadhimishia Mungu?

Ndiyo, sanaa zinafaa kumuadhimishia Mungu kwa sababu tunapaswa kutumia kwa utukufu wake vipawa alivyotujalia, kama vile vya kujenga, kupamba, kuchonga, kuchora na kucheza. Kwa njia hizo tutokeze na kukoleza imani yetu na ya wenzetu.
Mungu “amewajaza watu hao akili za moyoni, ili watumike katika kazi za kila aina, ya mwenye kuchora mawe, na kazi ya werevu, na ya mwenye kutia taraza, katika nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na ya mwenye kufuma nguo; ya hao wafanyao kazi yoyote, na ya wenye kuvumbua kazi za werevu. Basi, Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye Bwana amemtia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa huo utumishi wa mahali patakatifu, kama hayo yote Bwana aliyoyaagiza” (Kut 35:35-36:1).
“Maskani zako zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi!” (Zab 84:1).


Kati ya sanaa kwenye ibada/kumuadhimisha Mungu, muhimu zaidi ni ipi?

Kati ya sanaa, muhimu zaidi ni uimbaji, kwa kuwa unahusiana zaidi na Neno la Mungu, ukilitia maanani kwa uzuri wa muziki. Katika Agano la Kale, kitabu cha Zaburi ni nyimbo tupu za kutumia katika ibada.
“Msifuni kwa mvumo wa baragumu; msifuni kwa kinanda na kinubi! Msifuni kwa matari na kucheza; msifuni kwa zeze na filimbi! Msifuni kwa matoazi yaliayo; msifuni kwa matoazi yavumayo sana!” (Zab 150:3-5).
Agano Jipya pia linatuletea nyimbo nyingi.
“Mjazwe Roho, mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu” (Ef 5:18-19).
Mbinguni washindi wana “vinubi vya Mungu. Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwanakondoo” (Ufu 15:2-3).


Kuimba wakati wa ibada ni kazi ya nani?

Kuimba ni kazi ya kusanyiko lote, yaani ya kila mwamini. Kwaya ziimbishe watu wamwadhimishe Mungu, zisiwaimbie tu na kuwanyima nafasi ya kuimba.
“Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote, mtumikieni Bwana kwa furaha, njoni mbele zake kwa kuimba” (Zab 100:1-2).
“Kila kiumbe kilichopo mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi na juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, ‘Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwanakondoo, hata milele na milele’” (Ufu 5:13).


Katika kutumia sanaa kwa ibada tuzingatie nini?

Katika kutumia sanaa kwa ibada tuzingatie utakatifu na ukweli, si uzuri tu. Zisiigeuze kamwe kuwa igizo wala tamasha, kwa kuwa lengo si kuchangamsha watu bali kumtukuza Mungu.
Ziinue mioyo kwake, zitokeze na kuchangia maisha safi, zilete ujumbe sahihi kadiri ya imani na maadili, kama ilivyo lazima kwa mahubiri na mafundisho.
“Watu hawa huniheshimu kwa midomo, ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu” (Math 15:8-9).


Je, ni halali kuheshimu sanamu?

Ndiyo, ni halali kuheshimu sanamu kama viwakilishi vya Yesu, Mama yake na watakatifu wake, ambao zinaleta sura zao.
Kwa msingi huo walimsihi Yesu “waguse hata pindo la vazi lake tu. Na wote waliogusa wakaponywa kabisa” (Math 14:36).
“Mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote il msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo” (Gal 6:14).


Wakati wa ibada tuvae vipi?

Wakati wa ibada tuvae namna inayodhihirisha malengo ya moyo wetu, hasa usafi na heshima, unyenyekevu na udugu.
“Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki, kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote” (Math 23:27).
“Akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri, kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, ‘Keti wewe hapa mahali pazuri’, na kumwambia yule maskini, ‘Simama wewe pale’, au ‘Keti miguuni pangu’, je, hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu?” (Yak 2:2-4).
“Wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani, bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu” (1Tim 2:9-10).
Kanisa si mahali pa mashindano: hatuendi kupendeza watu, ila Mungu.
“Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu?” (1Kor 11:22).


Mbali ya sakramenti, Kanisa linamuadhimisha Mungu vipi?

Mbali ya sakramenti, Kanisa linamuadhimisha Mungu hasa kwa Liturujia ya Vipindi, yaani kwa sala rasmi zinazotolewa mara kadhaa kwa siku, kufuatana na ratiba ya binadamu ya usiku na mchana. Hivyo linajitahidi kutimiza agizo la kusali daima.
“Imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa” (Lk 18:1).
“Kesheni ninyi kila wakati, mkiomba” (Lk 21:36).
“Ombeni bila kukoma, shukuruni kwa kila jambo” (1Thes 5:17).
“Kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote” (Ef 6:18).
“Huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku” (1Tim 5:5).


Kanisa linamuadhimishaje Mungu tena?

Kanisa linamuadhimisha Mungu tena kwa visakramenti ambavyo kwa mamlaka ya Kristo linawatia watu neema zake katika nafasi yoyote ya maisha. Kati yake muhimu zaidi ni baraka na mazinguo, ambavyo vipo tangu zamani, hata nje ya taifa la Israeli.
Melkisedek alisema, “Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako” (Mwa 14:19-20).
Farao aliomba, “Mkanibariki mimi pia” (Kut 12:32).
Balaam alisifiwa, “Najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa” (Hes 22:6).
“Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha” (1Sam 16:23).
“Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je, wana wenu huwatoa kwa nani?” (Math 12:27).


Maana ya baraka ni ipi?

Maana ya baraka ni kumsifu Mungu kwa yale aliyokwishatujalia na kumuomba azidi kutujalia kadiri ya mahitaji ya wahusika. Mara nyingi inatolewa na mtu mwenye daraja au mamlaka fulani.
Yesu aliletewa “watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea” (Math 19:13).
Siku ya kupaa mbinguni “aliinua mikono yake akawabariki” (Lk 24:50).
“Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao” (Mdo 13:3).
Pengine vinabarikiwa vitu vinavyotumiwa na watu, au mahali wanapoishi.
“Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake ili wawaandikie mkutano” (Lk 9:16).


Mazinguo ndiyo nini?

Mazinguo ni sala za kupungia mashetani ili kuepusha watu na balaa au madhara, hasa kama wamepagawa nao.
“Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu” (Mk 5:8).
“Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena!” (Mk 9:25).
Yesu ameliachia Kanisa mamlaka yake juu yao.
“Aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu” (Mk 6:7).
“Paulo alisikitika, akageuka akamwambia yule pepo, ‘Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu’. Akamtoka saa ileile” (Mdo 16:18).


Je, ni halali kwa Wakristo kujitungia ibada nyingine?

Ndiyo, ni halali kwa Wakristo kujitungia ibada nyingine, mradi wakubali zipimwe na Maaskofu kama zinalingana na imani, maadili na taratibu za Kanisa.
“Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure… Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu” (Kol 2:18,23).
“Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao” (2Tim 3:14).


Ni halali kujitungia ibada kwa sababu gani?

Ni halali kujitungia ibada kwa sababu sala ni hasa maongezi ya Mungu na mtu.
Adamu na Eva “walisikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga” (Mwa 3:8).
Yeye hachoki kumvuta kila mmojawetu kwake na kumtia hamu ya kumhimidi na kumuabudu, kumuomba kwa ajili yake na ya wengine, kumshukuru na kumsifu.
“Ee Bwana, uisikie sala yangu, uzisikilize dua zangu, kwa uaminifu wako unijibu kwa haki yako” (Zab 143:1).
Hata tukisali pamoja, uhusiano wa kila mmojawetu na Mungu ni wa pekee. Tusiposali kwa moyo, ibada ni ya bure.
“Watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami” (Isa 29:13).


Ikiwa sala ni maongezi ya Mungu na mtu, kwanza tufanye nini?

Ikiwa sala ni maongezi ya Mungu na mtu, kwanza tumsikilize kwa makini na kutafakari alichosema ili tukifanyie kazi. Tukisema peke yetu si sala, kwa kuwa ukisema upande mmoja tu si maongezi.
“Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia” (1Sam 3:10).
“Nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku” (Zab 63:6).
“Sheria yako naipenda mno ajabu, ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa” (Zab 119:97).
“Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu” (Yer 15:16).


Kielelezo cha sala yetu ni nani?

Kielelezo cha sala yetu ni Yesu Kristo.
“Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, ‘Bwana, tufundishe sisi kusali” (Lk 11:1).
Yeye kama binadamu alichota humo uaminifu kwa wito wake wa pekee.
“Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe” (Yoh 17:1).
“Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe” (Mk 14:36).


Kama binadamu Yesu alijifunza kusali kwa nani?

Kama binadamu Yesu alijifunza kusali kwa Mama yake na kwa mapokeo yote ya Israeli, yaliyojitokeza hasa katika Zaburi.
“Wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu” (Lk 2:41-42).
“Saa tisa Yesu alipaza sauti yake kwa nguvu, ‘Eloi, Eloi, lama sabakthani?’” (Mk 15:34).
“Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu” (Lk 23:46).

Amri Kumi za Mungu: Mambo ya Msingi unayopaswa kufahamu

Amri kumi za Mungu ni zipi?

1. Ndimi Bwana, Mungu wako usiabudu miungu wengine.
2. Usiape bure kwa jina la Mungu wako.
3. Fanya siku ya Mungu

4. Waheshimu Baba na Mama, upate miaka mingi na heri duniani.
5. Usiue
6. Usizini
7. Usiibe
8. Usiseme uongo
9. Usitamani mwanamke asiye mke wako.
10. Usitamani mali ya watu.


Je, ni lazima kila mtu ashike Amri kumi za Mungu?

Ndiyo. Ni lazima kila mtu ashike Amri kumi za Mungu hata kama si Mkristo kwa sababu Mungu ni mkubwa wa watu wote. (Kut 20:1-17, Kumb 5:1-21)


Kwa nini Mungu alitupa Amri kumi?

Mungu alitupa amri kumi ili kutufudisha mambo yatupasayo kwa Mungu, kwa watu na kwetu sisi wenyewe


Katika amri ya kwanza ya Mungu tumeamriwa nini?

Tumeamriwa tusadiki kuwa Mungu ni mmoja, ndiye Baba yetu na Mkubwa wetu: tumpende, tumwabudu yeye peke yake. (Mt 10:33, Kumb 6:4-9)


Wakatoliki tunamwabudu Mungu kwa namna gani?

Tunamwabudu Mungu kwa sala , sadaka na matendo mema


Katika amri ya kwanza ya Mungu tumekatazwa nini?

Tumekatazwa kumdharau Mungu na kuweka imani yetu katika viumbe badala ya Mungu.


Je, kuna viumbe ambavyo tunaviheshimu kwa kumtukuza Mungu?

Ndiyo twamuheshimu Bikira Maria, Malaika na Watakatifu.


Kwa nini yatupasa kuwaheshimu Watakatifu?

Kwa sababu hao ni washindi, rafiki wa Mungu na waombezi wetu.


Je, tuna ruhusa ya kuwaabudu Watakatifu?

Hatuna ruhusa ya kuwaabudu Watakatifu tunawaheshimu tu.


Je sanamu zimekatazwa?

Sanamu hazijakatazwa, ila tunaziheshimu kwa sababu zinatukumbusha Mungu na Watakatifu. (Kut 25:18-22).

18 Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. 19 Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. 20 Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. 21 Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. 22 Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli. Kutoka 25 :18-22.

Vile vile Mungu alishawahi kuwaagiza Waisraeli Wachonge sanamu ya nyoka na yeyote atakayeumwa na nyoka akiiangalia atapona.


Mfano wa sanamu takatifu ni zipi?

Sanamu ya Bikira Maria, Mtoto Yesu, Mt. Yosefu, Moyo wa Yesu na za Watakatifu.


Ni nanai ana kosa kumuabudu Mungu?

Anayekosa kumuabudu Mungu ni yule;

1. Anayeacha kusali au anayesali hovyo
2. Anayemkufuru Mungu
3. Anayeamini na kushika mambo ya kipagani


Mambo gani yanavunja amri ya kwanza ya Mungu?

Mambo hayo ni;

1. Kuabudu sanamu
2. Kufanya matambiko
3. Kwenda kwa waganga
4. Kupiga bao au ramli
5. Kuvaa hirizi
6. Kushiriki mambo ya kichawi n.k.


Ni nini maana ya kuabudu sanamu?

Kuabudu sanamu ni kukipa kiumbe chochote heshima au upendo anaostahili Mungu peke yake.

Je, Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha umuhimu wa sala katika maisha ya Kikristo?

Sala ni sehemu muhimu katika maisha ya Kikristo. Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha umuhimu wake katika maisha ya waumini. Kupitia sala, tunaweza kuwasiliana na Mungu na kumwomba msaada katika maisha yetu. Sala inatusaidia kupata amani ya nafsi na kuimarisha imani yetu. Ni kwa sababu hii Kanisa Katoliki linahimiza waumini wake kusali mara kwa mara.

Katika Biblia, tunasoma maneno ya Yesu yaliyosema, “Omba na utapewa; tafuta na utapata, piga hodi na mlango utafunguliwa” (Mathayo 7:7). Hii inaonyesha kuwa sala ni njia ya kuomba msaada kutoka kwa Mungu. Pia, Biblia inatueleza kuwa Yesu mwenyewe alikuwa akipenda kwenda peke yake kusali. Kwa hivyo, kama wafuasi wa Yesu tunapaswa kufanya hivyo pia.

Kanisa Katoliki linatumia sala kama sehemu ya ibada. Sala ni sehemu ya liturujia, ambayo ni ibada ya Kanisa Katoliki. Liturujia inajumuisha sala, nyimbo, na maandiko kutoka kwa Biblia. Kupitia sala, waumini wanashiriki katika ibada ya Kanisa na wanapata baraka kutoka kwa Mungu.

Kanisa Katoliki pia linatumia sala kama njia ya kutubu dhambi zetu. Katika sala ya kitubio, waumini wanakiri dhambi zao kwa padri na kupata msamaha wa Mungu. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kusafisha roho zetu na kuanza upya.

Kanisa Katoliki linatufundisha kuwa sala ni zaidi ya kuomba msaada kutoka kwa Mungu. Sala ni njia ya kuimarisha uhusiano wetu na Mungu. Kupitia sala, tunaweza kumjua Mungu vizuri zaidi na kupata ufahamu wa mapenzi yake. Sala inatuwezesha kusikiliza sauti ya Mungu na kufuata njia yake.

Kanisa Katoliki linatufundisha sala za kawaida kama vile Sala ya Bwana, Salamu Maria, na Tafakari ya Rozari. Sala hizi zinahimizwa kwa waumini ili kusali mara kwa mara na kuimarisha uhusiano wao na Mungu. Sala za kawaida pia zinafaa kama njia ya kufundisha watoto wetu umuhimu wa sala na kujifunza Biblia.

Kwa ujumla, sala ni sehemu muhimu ya maisha ya Kikristo. Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha umuhimu wake kwa waumini wake. Kupitia sala, tunaweza kuwasiliana na Mungu, kusafisha roho zetu, na kuimarisha uhusiano wetu na Mungu. Kwa hivyo, tunahimizwa kusali mara kwa mara na kufuata mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu sala. Kama Catechism ya Kanisa Katoliki inasema, “Sala ni moyo wa maisha ya kiroho; ni sehemu muhimu ya uhusiano wetu na Mungu” (CCC 2558).

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About