Mafundisho ya Katekisimu

Maswali na Majibu kuhusu Malaika

Kwanza Mungu aliumba nini?

Kwanza Mungu aliumba Malaika (Kol 1:16)


Malaika ni viumbe gani?

Malaika ni viumbe vya Mungu vilivyo roho tu wenye akili na utashi. (Zab 91:11, Ebr 1:7, Ufu 12:7-9)


Mungu aliumba Malaika katika hali gani?

Mungu aliumba Malaika katika hali njema na heri kubwa.


Malaika wote walidumu katika hali njema na ya heri?

Siyo, Malaika wengine walikosa kwa kumkaidi Mungu, Wakatupwa Motoni.
Ndio Mashetani ambao Mkubwa wao ni Lusiferi. (Yoh 8:44, Uf 12:7-9)


Kwa nini Mungu ameumba Malaika?

Mungu ameumba Malaika ili wamtukuze, wafurahi naye Mbinguni, na wawe matarishi wake kwa wanadamu. (Tob 12:12, Lk 16:22)


Malaika wema kazi yao ni nini?

Malaika wema kazi yao ni kutuombea, kutumwa na Mungu kwetu, na wanatulinda kama Malaika wetu Walinzi. (Ebr 13:2)


Kila Mwanadamu anaye Malaika wake wa kumlinda?

Ndiyo, Kila Mwanadamu anaye Malaika wake wa kumlinda ndiye Malaika Mlinzi. (Mt. 18:10)


Malaika Walinzi wanatutendea nini?

Malaika walinzi hutupenda, hutuongoza, na kutulinda roho na mwilini (Zab 90:11)


Je Malaika wote ni sawa?

Hapana. Malaika wote sio sawa, maana kuna;
1. Malaika wakuu
2. Malaika wanaomtumikia Mungu Mbinguni yaani Makerubi na Maserafi
3. Malaika Walinzi


Malaika wakuu wako watatu ambao ni?

Malaika wakuu wako watatu: Mikaeli, Raphaeli na Gabrieli (Dn 10:13, Tobiti 12:15, Lk 1:26)


Makao ya shetani ni wapi na anatamani nini?

1. Mashetani kazi yao ni kuteswa Motoni
2. Hutaka kutudhuru roho na mwili na kutupoteza milele (1 Petro 5:8, Yoh 8:44)


Kisha kuumba Malaika Mungu aliumba nini?

Kisha kuumba Malaika Mungu aliumba Mbingu na dunia, na viumbe vingine vingi vyenye kuonekana mimea na watu. (Mwanzo 1;31)


Viumbe vyenye hiari ni vipi?

Malaika na watu ndio viumbe pekee vyenye hiari ya kuchagua wenyewe wachangie mpango wa Mungu au la.
“Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi, chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako” (Kumb 30:19-20).


Malaika na watu wanaweza kuchagua hata nini?

Malaika na watu wanaweza kuchagua hata wawe wema au wabaya milele.
“Kulikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni” (Ufu 12:7-8).
Chaguo letu binadamu linafanyika siku kwa siku kwa kuchukua misimamo mizuri au mipotovu kuhusu dini na maadili.
“Mwayachunguza Maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima” (Yoh 5:39-40).


Malaika wakoje?

Malaika ni roho tupu walioumbwa na Mungu ili wamtukuze milele, wamlinde kila mtu na kumtumikia Bwana Yesu katika kutuokoa.
“Angalieni, msidharau mmojawapo wadogo hawa, kwa maana nawaambia ya kwamba malaika zao mbinguni sikuzote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni” (Math 18:10).


Je, toka mwanzo sisi watu tunaasi mpango wa Mungu peke yetu?

Hapana, toka mwanzo sisi watu tunaasi mpango wa Mungu kwa kuvutwa na mashetani, yaani malaika waliokataa moja kwa moja kumtumikia; baada ya dhambi ya asili hao wanatutumia sisi pia tuangushane na wenzetu.
Lakini Mungu aliwahi kumuambia Shetani:
“Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako, na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino” (Mwa 3:15).
“Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke” (Gal 4:4).

Mambo ya Msingi kujua kuhusu Sakramenti ya Kitubio

Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu gani?
Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu alijua udhaifu wa binadamu hauishi mara anapopokea uzima wa Mungu kwa sakramenti tatu za kuingizwa katika Ukristo. Hivyo alipanga kusaidia mpaka mwisho wa dunia waamini wake watakaopatwa na dhambi na ugonjwa, kama alivyowasaidia wengi aliokutana nao katika maisha yake.
“Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, ‘Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako’… ‘Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi’ – amwambia yule mwenye kupooza – ‘Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako’. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii” (Math 9:2,6-8).

Mungu aliwapa watu (mapadri) amri/uwezo ya kusamehe dhambi kwa njia ya nani? Ni halali kuungama kwa padre?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa njia ya Mwanae. Yesu mfufuka aliwaonyesha Mitume alama ya mateso mwilini mwake, “akawavuvia, akawaambia, ‘Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23).
Katika Kanisa tunafurahi kupewa msamaha wa dhambi kila tunapohitaji, mradi tutubu. Kwa njia ya mwandamizi wa Mitume, Yesu anatuambia,
“Umesamehewa dhambi zako… Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani” (Lk 7:48,50).
Si dhana wala hisia tu, bali ni neno la hakika tunalolipokea kwa masikio yetu.

Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zipi?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zote, kwa sababu upendo mtiifu wa Mwanae aliyejitoa kuwa sadaka ya wokovu wetu unampendeza kuliko dhambi zote zinavyomchukiza. Ila hatuwezi kusamehewa dhambi ya kukataa neema ambayo Roho Mtakatifu anatusukuma tuamini na kutubu, kwa sababu pasipo imani na toba hapana msamaha.
“Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa” (Math 12:31).
“Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure” (2Kor 6:1).

Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu gani?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu amependa washiriki katika kazi zake. Ametuumba kwa njia ya wazazi na kutulea na kutusaidia kwa njia ya wengine pia. Hasa ametuokoa kwa njia ya Yesu, ambaye yupo nasi sikuzote katika Mwili wake, yaani Kanisa, na katika wale walioshirikishwa mamlaka ya Mitume.
“Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:18-20).

Je, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi?
Ndiyo, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi tulizotenda baada ya ubatizo, kwa kuwa hatuwezi kupokea msamaha tukikataa masharti yake, na Mungu ametupangia watu ambao watuondolee kwa niaba yake.
“Watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohane. Lakini, Mafarisayo na wanasheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye” (Lk 7:29-30).
Yesu mwenyewe alikubali kubatizwa na Yohane ili atimize mpango wa Baba.
“Yohane alitaka kumzuia, akisema, ‘Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?’ Yesu akajibu akamwambia, ‘Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Math 3:14-15).
Je, sisi tukatae kumkimbilia padri wa Mungu ili kupokea huruma yake tunayoihitaji kuliko hewa?

Tumuungamie padri dhambi zetu kwa lengo gani? Kwa nini Wakatoliki wanaungama kwa padri?
Tumuungamie padri dhambi zetu ili aweze kutushauri na kuamua kama tuko tayari kuondolewa. Tumweleze kwa unyofu makosa yote tuliyoyafanya na nia tuliyonayo ya kuyafidia na kutoyarudia.
“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu” (1Yoh 1:8-10).
Tukumbuke tulivyo viungo vya Mwili mmoja, hivi kwamba dhambi zetu zimewadhuru wenzetu. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana, mpate kuponywa” (Yak 5:16).
Kutokuwa tayari kufanya hivyo walau sirini kwa padri ni dalili ya kiburi na ya kutotubu.

Je, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi?
Ndiyo, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi kwa niaba ya Mungu aliyempa mamlaka hiyo. Hatusamehewi na utakatifu wa padri, bali na huruma ya Baba kwa njia yake.
Yeye anamtumia padri yeyote ili kuturahisishia kazi, tusihitaji kuchunguza kwanza ubora wa maisha yake, wala kwenda mbali tukampate mmoja asiye na dhambi. Tungefanyeje kuhakikisha ni mtakatifu, wakati hatuwezi kusoma moyo wake? Ingekuwa hivi, tusingepata kamwe hakika ya kusamehewa. Kumbe inatutosha kujua ni padri, kwamba Mungu amempa mamlaka ya kusamehe dhambi, kama Yesu alivyowapa Mitume siku tatu baada ya kumkimbia na hata kumkana. Kila padri anaweza kukiri,
“Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa: ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi” (1Tim 1:15).
Amri ya kusamehe dhambi wamepewa watu, si malaika.
“Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu” (2Kor 4:7).

Je, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo?
Ndiyo, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo, lakini ni vigumu zaidi, kwa sababu hatupati msaada wa sakramenti hiyo maalumu.
Pamoja na nia ya kumuungamia padri mapema tunahitaji neema ya kutubu kikamilifu, si kwa kuhofia adhabu, bali kwa kumpenda Mungu tuliyemchukiza.
“Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana” (Lk 7:47).

Sakramenti ya Kitubio ni nini?
Sakramenti ya Kitubio ndiyo Sakramenti ya kuwaondolea watu dhambi walizotenda baada ya Ubatizo (Yoh 20:22-23)

Lini na kwa maneno gani Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio?
Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio jioni ya ufufuko wake alipowapulizia mitume na kuwaambia maneno haya “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi watakua wameondolewa, wowote mtakaowafungia dhambi watakua wamefungiwa” (Yoh 20:22-23)

Mwenye kuwaondolea watu dhambi ni nani?
Mwenyezi Mungu pekee yake aweza kuwaondolea watu dhambi. Ndiye aliyewapa Mitume, Maaskofu na Mapadri uwezo wa kuwaondolea watu dhambi (Yoh 20:21-23)

Nani yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio?
Kila mkristo aliyetenda dhambi yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio

Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa haya
1. Kutafuta dhambi moyoni (Yoh 3:20-21)
2. Kujuta dhambi
3. Kukusudia kuacha dhambi
4. Kuungama kwa padre
5. Kutimiza malipizi
6. Kumshukuru Mungu aliyemwondolea dhambi

Wakati wa Sakramenti ya Kitubio Utamwomba Roho Mtakatifu kwa sala gani?
Utamuomba Roho Mtakatifu kwa sala hii:
Uje Roho Mtakatifu unisaidie nitambue dhambi zangu, nijute sana, niungame vema, nipate kutubu kweli. Amina

Kutafuta dhambi maana yake ni nini?
Kutafuta dhambi maana yake ni kujiuliza moyoni dhambi nilizotenda Tangu ungamo la mwisho (Ef 4:17-32)

Utafuteje dhambi wakati wa kujiandaa kuungama?
Tafuta dhambi kwa njia hizi
1. Kwa kukumbuka uliyokosa kwa mawazo, kwa maneno na kwa vitendo
2. Katika Amri za Mungu na za Kanisa
3. Katika vichwa vya dhambi
4. Katika kutimiza wajibu

Kutubu dhambi maana yake ni nini?
Kutubu dhambi maana yake ni kuona uchungu na chuki moyoni juu ya dhambi tulizotenda na kukusudia kutotenda dhambi tena (Yoh 8:11)

Kwa nini tujute dhambi zetu?
Tunajuta dhambi zetu kwa sababu tumeukosea Utatu Mtakatifu na tunastahili adhabu yake, na pia bila majuto hatuwezi kupata maondoleo ya dhambi.

Kuna majuto ya namna ngapi?
una majuto ya namna mbili,
1. Majuto kamili/Majuto ya mapendo
2. Majuto yasiyokamili/majuto pungufu/majuto ya hofu

Majuto kamili ni nini?
Majuto kamili ni kujuta kwa sababu tumemchukiza Mungu mwenyewe aliye mwema na mpendelevu kabisa

Majuto yasiyo kamili au majuto pungufu ni nini?
Majuto yasiyokamili ni kujuta kwa sababu tumepoteza furaha za Mbinguni na tunahofia adhabu ya Mungu

Asiyejuta aweza kuondolewa dhambi?
Asiyejuta hawezi kuondolewa dhambi kabisa, na anayeungama bila kujuta anatenda dhambi kubwa ya kufuru.

Kabla ya kuungama ni lazima kufanya nini?
Kabla ya kuungama ni lazima kukusudia kuacha dhambi na kuepuka nafasi kubwa ya dhambi bila kusahau kufuata hatua sita za kabla na baada ya kupokea kupokea Sakramenti ya Kutubio ambazo ni,
(1) kuwaza/kutafuta dhambi moyoni,
(2)kutubu/ kujuta,
(3)kukusudia kuacha dhambi,
(4)kuungama kwa padri,
(5)kutimiza kitubio,
(6)kumshukuru Mungu

Anayetaka kweli kuacha dhambi afanye nini?
Anayetaka kuacha dhambi afanye nguvu kuvishinda vishawishi, asali/aombe na apokee Sakramenti Mara nyingi hasa Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi Takatifu.

Kuungama ni kufanya nini?
Kuungama ni kumwambia Padri wazi wazi dhambi zako ulizotenda, zipi na ngapi ili upate maondoleo.

Anayeficha kusudi dhambi ya mauti katika ungamo anaondolewa?
Haondolewi, Bali anatenda dhambi kubwa ya kukufuru Sakramenti ya Kitubio. (Mt 7:21-23, Yoh 20:23, Gal 6:7)

Anayekufuru Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Yampasa kuziungama tena dhambi zake zote alizotenda tangu ondoleo la mwisho

Padri anaondolea dhambi mahali pa nani?
Padri anaondolea dhambi mahali pa Mungu

Padri anaondolea dhambi kwa maneno gani?
Padre anaondolea dhambi kwa maneno haya: Nami “Nakuondolea dhambi zako zote kwa Jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu”.

Kitubio tuwezacho kupewa na padre ni nini?
Kitubio tuwezacho kupewa na Padre ni kama sala, kufunga, kutoa sadaka kwa maskini, kusoma maandiko matakatifu, kuwatazama wagonjwa, n.k.

Kitubio tupewacho na padre chatosha?
Ni shida kutosha. Mara nyingi chataka malipizi ya hapa duniani kama kufunga, magonjwa, masumbuko, sala n.k mateso yasipotosha hapa duniani yatakamilishwa toharani

Kutimiza malipizi maana yake ni ni nini?
Kutimiza malipizi maana yake ni kutekeleza kiaminifu sala au matendo aliyotuagiza padre muungamishi ili kulipa adhabu za muda. (Rom 8:17)

Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema zipi?
Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema hizi;
1. Maondoleo ya dhambi zote kubwa na adhabu ya milele
2. Maondoleo ya dhambi ndogo na adhabu nyingine za muda (Isa 6:5-7, Yoh 8:11)
3. Twarudishiwa na kuongezewa neema ya utakaso
4. Twasaidiwa kuepa dhambi na twapata nguvu ya kutenda mema
5. Twarudishiwa tena mastahili tuliyopoteza kwa dhambi zetu

Je, Kanisa Katoliki linatambua na kufundisha Maandiko Matakatifu kuwa Neno la Mungu?

Je, Kanisa Katoliki linatambua na kufundisha Maandiko Matakatifu kuwa Neno la Mungu? Ndio! Kanisa Katoliki linatambua na kufundisha kwamba Maandiko Matakatifu ni Neno la Mungu lililoongozwa na Roho Mtakatifu. Kwa kweli, Kanisa Katoliki linapenda na kuthamini Maandiko Matakatifu sana kwamba inaweka Maandiko kama msingi wa imani yake yote.

Katika Catechism of the Catholic Church, Kanisa Katoliki linasema kuwa, "Kanisa limetambua maandiko matakatifu kama Neno la Mungu liliyo geuzwa kuwa lugha ya mwanadamu. Kwa sababu hiyo, Kanisa Katoliki linaheshimu sana Maandiko Matakatifu na kuzitumia kama msingi wa kufundisha imani yake."

Kwa maneno mengine, Maandiko Matakatifu ni muhimu sana kwa Kanisa Katoliki. Ni kwa njia ya Maandiko Matakatifu tu ndipo Kanisa linaweza kufundisha juu ya imani na maadili, na ni kwa njia ya Maandiko Matakatifu tu ndipo Kanisa linaweza kujibu maswali ya wakristo kuhusu maisha yao ya kiroho.

Kwa hivyo, kwa nini Kanisa linathamini sana Maandiko Matakatifu? Kwanza, Maandiko Matakatifu ni Neno la Mungu, na Kanisa Katoliki linapenda na kuheshimu Neno la Mungu. Kwa njia ya Maandiko Matakatifu, tunapata kujua zaidi juu ya Mungu, kujifunza juu ya upendo wake na mpango wake wa wokovu wa mwanadamu.

Pili, Maandiko Matakatifu ni msingi wa imani yetu. Kila kitu tunachofundisha kuhusu imani yetu, kila kitu tunachojua kuhusu Mungu na mpango wake wa wokovu, kinatokana na Maandiko Matakatifu. Kwa hiyo, Kanisa Katoliki linapaswa kuheshimu na kutambua Maandiko Matakatifu kama Neno la Mungu lisilo na makosa.

Tatu, Kanisa Katoliki linaamini katika ufunuo kamili wa Mungu. Maandiko Matakatifu yana ufunuo kamili wa Mungu, na kwa sababu hiyo, Maandiko Matakatifu ni msingi wa ufunuo wetu wa Mungu. Kwa njia ya Maandiko Matakatifu, tunaweza kujua zaidi juu ya Mungu wetu na mapenzi yake kwa maisha yetu.

Katika Maandiko Matakatifu, tunapata maelezo ya wazi ya jinsi ya kuishi maisha ya Kikristo, kujifunza juu ya upendo wa Mungu kwa wanadamu, na kuelewa mpango wake wa wokovu. Kwa hiyo, Kanisa Katoliki linaamini kuwa Maandiko Matakatifu ni msingi wa imani yetu na utambuzi wa Mungu.

Kanisa Katoliki linatumia Maandiko Matakatifu kufundisha imani yake na kuelezea mafundisho yake kwa wakristo wote. Maandiko Matakatifu yanatuita kufanya kazi pamoja na Mungu ili kuleta ufalme wa Mungu duniani. Kwa hiyo, Kanisa Katoliki linatambua na kufundisha kwamba Maandiko Matakatifu ni Neno la Mungu na msingi wa imani yetu na maisha ya kikristo.

Kwa kuhitimisha, Kanisa Katoliki linatambua na kufundisha kwamba Maandiko Matakatifu ni Neno la Mungu lililofunuliwa kwa wanadamu kupitia Roho Mtakatifu. Maandiko Matakatifu ni msingi wa imani yetu na maisha ya kikristo, na Kanisa Katoliki linatumia Maandiko Matakatifu kufundisha na kuelezea mafundisho yake. Kwa hivyo, ni muhimu sana kwetu kusoma, kutafakari, na kuelewa Maandiko Matakatifu ili tuweze kujua zaidi juu ya Mungu wetu na mpango wake wa wokovu.

Mambo ya Muhimu kufahamu kuhusu Ishara ya Msalaba

Ishara ya msalaba ni nini?
Ishara ya Msalaba ni tendo la mtu kugusa panda la uso, kifua na mabega kwa kutumia mkono wa kulia na kutamka “Kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina”


Kwa kugusa paji la uso tuna maana gani?
Kwa kugusa paji la uso tuna maana ya kukubali kwa akili


Kwa kugusa kifua tuna maana gani?
Kwa kugusa kifua maana yake ni kuupokea na kuukubali msalaba moyoni.


Kwa kugusa mabega tuna maana gani?
Kwa kugusa mabega maana yake ni kuwa tayari kuubeba msalaba kwa nguvu zetu zote


Kwa nini tunafanya Ishara ya Msalaba?
Tunafanya Ishara ya Msalaba kwa nia ya kumkiri Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Pia msalaba ni Ishara ya Ukombozi wetu


Ishara ndogo ya Msalaba juu ya panda la uso, mdomo, na kifua kabla ya Injili ina maana gani?
Maana yake ni kama Ahadi kuwa, Niko tayari kulifahamu Neno la Mungu kwa akili yangu, Nitalitangaza kishujaa kwa Midomo yangu, Nitalipenda na kulishika kwa Moyo wangu wote.

Amri ya Tano ya Mungu: Kutunza uhai wetu na wa watu wengine

Katika Amri ya Tano ya Mungu tumeamriwa nini?

Tumeamriwa tutunze uhai wetu na wa watu wengine tangu mwanzo hadi mwisho. (Mwa 4:10-11)


Kwa nini ni lazima kutunza uhai wetu na wa wenzetu?

Kwa sababu uhai wa watu wote umetoka kwa Mungu


Haki gani ya Binadamu ni ya msingi kupita zote?

Haki ya binadamu iliyo ya msingi kupita zote ni uhai wake ambao ni lazima uheshimiwe na kulindwa tangu siku ya kutungwa mimba


Nani anatenda dhambi dhidi ya amri ya tano ya Mungu? Mambo yanayovunja Amri ya Tano ya Mungu

Anayetemda dhambi dhidi ya amri ya tano ya Mungu ni yule;-

1. Anayemuua mtu au anayejiua mwenyewe
2. Anayemdhuru mwingine kwa namna yoyote ile
3. Anayeua Mimba na kuharibu nguvu za uzazi
4. Anayesaidia kuua, kumdhuru mtu au anayesaidia kutoa/kuharibu mimba
5. Anayeharibu mazingira yaliyomuhimu kwa uhai
6. Anayetetea au kuendeleza mifumo ya ya dhuluma, uhasama na vita.

Je, Kanisa Katoliki linatetea na kufundisha maadili ya kijinsia na thamani ya ndoa kati ya mwanaume na mwanamke?

Katoliki ni dini inayoheshimu na kufundisha thamani ya maisha ya binadamu. Kanisa Katoliki linafundisha maadili ya kijinsia na thamani ya ndoa kati ya mwanaume na mwanamke. Katika maudhui haya, tunaweza kuelewa jinsi Kanisa Katoliki linavyolinda na kufundisha thamani ya kijinsia na ndoa.

Kanisa Katoliki linatetea maadili ya kijinsia kwa sababu binadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu na anastahili kuheshimiwa. Maadili ya kijinsia yanahusu uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke. Kwa maana hiyo, Kanisa linafundisha kwamba ngono ni kitendo kitakatifu na kinapaswa kufanywa ndani ya ndoa tu.

Ndoa ni sakramenti na ina thamani kubwa katika Kanisa Katoliki. Inapasa ichukuliwe kama ndoa ya kiroho, kati ya mwanaume na mwanamke, na haihusishi mtu mwingine yoyote katika uhusiano huo. Kama ilivyoelezwa katika Kitabu cha Mwanzo, mwanaume na mwanamke waliunganishwa na Mungu wakati walipoumbwa. Ndoa inaunganisha mwanamume na mwanamke katika upendo wa Mungu.

Neno la Mungu linaelezea wazi na kwa undani jinsi Kanisa Katoliki linavyofundisha maadili ya kijinsia na thamani ya ndoa. Kwa mfano, katika Mathayo 19:5 inasema, "Kwa sababu hiyo, mwanamume ataacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja." Hii inaonyesha kwamba ndoa ni kati ya mwanaume na mwanamke na hawapaswi kutengana.

Kwa mujibu wa Catechism ya Kanisa Katoliki, ndoa inapaswa kuwa na upendo wa dhati kati ya wawili na inapaswa kuheshimiwa. Kwa mfano, ndoa inapaswa kutimiza mahitaji ya kiroho, kihisia na kijamii ya wanandoa. Ndoa inapaswa kuwa ya kitakatifu na inapaswa kutimiza matakwa ya Mungu.

Kwa ufupi, Kanisa Katoliki linatetea na kufundisha maadili ya kijinsia na thamani ya ndoa kati ya mwanaume na mwanamke. Ndoa inapaswa kuwa ya kitakatifu na kutimiza mahitaji ya kiroho, kihisia, na kijamii ya wanandoa. Ndoa ni sakramenti katika Kanisa Katoliki na linapaswa kuheshimiwa na kufanywa ndani ya ndoa, kulingana na neno la Mungu.

Ni nini imani ya Kanisa Katoliki kuhusu dini na dini nyingine?

Kanisa Katoliki ni mojawapo ya madhehebu makubwa zaidi ya Ukristo ulimwenguni. Imani yake ina msingi katika mafundisho ya Yesu Kristo na inaamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa ulimwengu wote. Hii ni imani ambayo ina nguvu na inaleta amani kwa wafuasi wake. Lakini, je, Kanisa Katoliki lina imani gani kuhusu dini na dini nyingine?

Kanisa Katoliki linadai kuwa kuna Mungu mmoja tu, ambaye ndiye muumba wa ulimwengu wote. Wale wote wanaomwamini Mungu huyo na kufuata maadili yake, wameunganishwa kupitia Roho Mtakatifu. Hata hivyo, Kanisa linajua kuwa kuna dini nyingine na hata wale ambao hawana dini. Kanisa linawapa heshima na kuwathamini wote ambao wanatafuta ukweli na njia ya kumfikia Mungu kwa kutumia njia yao wenyewe.

Kanisa linabainisha kuwa, hata kama dini zote zina mambo mengi yanayofanana, ni lazima kutambua kuwa Kanisa Katoliki lina ufunuo mkuu zaidi kuliko dini nyingine yoyote ile. Kama Wakatoliki, tunajua kuwa, Yesu Kristo ndiye njia, ukweli na uzima. Hii inamaanisha kuwa tunapaswa kufanya kazi yetu yote kwa kumfuata Yesu Kristo na kusaidia wengine kufanya hivyo pia.

Kanisa Katoliki linatambua kuwa kila mtu ana uhuru wa kidini na uhuru wa kufuata imani yake. Kwa kweli, uhuru huu ndio msingi wa Kanisa kuhusu uhuru wa dini. Kanisa linaheshimu imani za watu wengine na linawatafuta kwa upendo wa Mungu. Hata hivyo, Kanisa linatambua kuwa kuna dini zingine ambazo zinapinga au kukinzana na imani ya Kikristo. Kwa hiyo, ni muhimu kwa Wakatoliki kutambua na kuelewa mafundisho na imani ya Kanisa, kama inavyoelezwa katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki.

Kanisa Katoliki linaamini kuwa Mungu ni wa upendo na kwamba anatualika sote kuwa wamoja katika upendo wake. Kwa hiyo, tunapaswa kuheshimiana na kuheshimu uhuru wa dini kwa watu wote. Kwa kuwa sisi ni Wakatoliki, tunapaswa kujifunza na kuelewa imani yetu na kuwa wazuri katika mazungumzo yetu kuhusu dini na imani ya wengine.

Kanisa Katoliki hufundisha kuwa, lengo la dini ni kumkaribia Mungu na kuishi maisha ya haki na ya upendo. Hii inafanyika kwa kumfuata Yesu Kristo na kufuata maelekezo yake kama yalivyoelezwa katika Biblia. Tunashauriwa kufuata mafundisho ya Kanisa na kuepuka mafundisho yanayopingana na mafundisho ya Kanisa.

Kwa hiyo, Kanisa Katoliki linaheshimu imani ya wengine na linatumia njia ya upendo na heshima katika kuelezea imani yake. Hata hivyo, Kanisa Katoliki linajua kuwa kumfuata Yesu Kristo ndiyo njia pekee ya kufikia ukamilifu wa kiroho na kuwa mtu wa Mungu.

Kwa hitimisho, Kanisa Katoliki linatambua kuwa kuna dini nyingine na linawaheshimu wale wote ambao wanafuata imani yao. Hata hivyo, Kanisa linasisitiza kuwa Yesu Kristo ndiye njia ya pekee ya kufikia Mungu. Kama Wakatoliki, tunapaswa kujifunza na kuelewa imani yetu na kuwa wazuri katika mazungumzo yetu kuhusu dini na imani ya wengine, tukiwa na upendo na heshima.

Kuhusu Ubatizo, Haya ndiyo mambo ya Msingi unayotakiwa kufahamu

Kwa nini ubatizo unafanyika kwa maji?

Ubatizo unafanyika kwa maji kwa kuwa ndiyo ishara ya usafi na ya uhai unaotupatia kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
“Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu” (Ez 36:26-27).
“Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwanakondoo” (Ufu 22:1).


Ubatizo unatolewa pia kwa maji machache tangu lini?

Ubatizo unatolewa pia kwa maji machache tangu mwanzo. Kutokana na umuhimu wa sakramenti hiyo Yesu ametuagiza twende kubatiza watu duniani kote.
Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaonyesha waamini walivyotekeleza agizo hilo katika mazingira mbalimbali, sio tu yalipopatikana maji mengi. Hivyo Paulo alipokuwa ndani ya nyumba “akasimama akabatizwa” (Mdo 9:18).
Kumbe Yohane Mbatizaji hakusogea mbali na mto Yordani, akisubiri watu wamuendee kutoka maeneo yote ya nchi ile kame.
“Alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele” (Yoh 3:23).


Je, ubatizo uliotolewa na Yohane Mbatizaji ulikuwa sakramenti?

Hapana, ubatizo uliotolewa na Yohan Mbatizaji haukuwa sakramenti, kwa sababu yeye alikuwa mtangulizi tu wa Yesu, mwanzilishi wa sakramenti zote.
“Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto” (Math 3:11).
Paulo aliuliza watu, “‘Mlibatizwa kwa ubatizo gani?’ Wakasema, ‘Kwa ubatizo wa Yohane’. Paulo akasema, ‘Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu’. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu” (Mdo 19:3-5).


Tofauti kubwa kati ya ubatizo wa Yohane na ule wa Yesu ni zipi?

Tofauti kubwa kati ya ubatizo wa Yohane na ule wa Yesu ni kwamba sakramenti inategemea imani kwa Kristo na kutushirikisha kifo na ufufuko wake.
“Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo” (Gal 3:27).
Ndivyo inavyoondolea dhambi zote na kuingiza katika uzima wa Utatu Mtakatifu. Kwa sababu hiyo Yesu aliagiza tubatize “kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” (Math 28:19).
Maneno hayo ndiyo muhimu zaidi katika sakramenti hiyo. Maji peke yake, hasa yakiwa mengi, yanaweza kuosha mwili, lakini si roho. Kumbe ubatizo unaotuokoa
“siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu” (1Pet 3:21).


Je, watoto wachanga wanaweza kubatizwa?

Ndiyo, watoto wachanga wanaweza kubatizwa kwa sababu hawakatai neema ya Mungu. Wanafunzi wa Yesu walipotaka kuwazuia wasiletwe kwake “alichukizwa sana, akawaambia, ‘Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni: Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa” (Mk 10:14-15).
Yeremia aliambiwa,
“Kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa” (Yer 1:5).
Yohane Mbatizaji alitabiriwa “atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye” (Lk 1:15).
Mitume walipokea katika Kanisa familia nzima, si wazazi tu.
Walibatizwa “yeye na nyumba yake”, “yeye na watu wake wote” (Mdo 16:15,33);
“watu wa nyumbani mwa Stefana” (1Kor 1:16).
Kwa hiyo tunaona kuwa tangu wakati wa Mitume sio watu wazima tuu waliokua wakibatizwa bali na watoto pia.


Mbona watoto wachanga hawawezi kuelewa kinachofanyika wakati wa ubatizo halafu wanabatizwa?

Ingawa watoto wachanga hawawezi kuelewa kinachofanyika, Mungu anaweza kuwamiminia rohoni mwanga wa imani.
“Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao umeiweka misingi ya nguvu” (Zab 8:2).
“Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake… kwa shangwe” (Lk 1:41,44).
“Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako” (Math 11:25-26).


Je, watu wazima wanaweza kuelewa sakramenti kwa dhati?

Hapana, watu wazima hawawezi kuelewa sakramenti kwa dhati, kwa kuwa zote ni mafumbo yanayotuzidi. Basi, kama Petro alipooshwa miguu, tumuachie Bwana atufanyie kazi anavyojua yeye.
“Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye” (Yoh 13:7).
Kisha kuoshwa tuzidi kuchimba mafumbo hayo kwa mwanga wa Neno na wa Roho Mtakatifu.
“Je, mmeelewa na hayo niliyowatendea?… Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yoh 13:12,15).


Je, imani ya watu wazima inaweza kufaidisha watoto?

Ndiyo, imani ya watu wazima inaweza kufaidisha watoto kama wengine pia.
Walimletea Yesu “mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne… Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, ‘Mwanangu, umesamehewa dhambi zako” (Mk 2:5).
Yesu aliiona imani yao akamponya. Imani ya watu wengine ndio ilivyopelekea kuponywa kwa huyu mtu. Vivyo hivyo Imani ya Mzazi inaweza kumsaidia mtoto.
Kwa ubatizo watoto wanaunganishwa naye na kuanza kuponywa madonda ya dhambi ya asili.
“Tazama, mimi naliumbwa kati hali ya uovu, mama yangu alinichukua mimba hatiani” (Zab 51:5).
“Ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo” (Rom 5:19).


Ubatizo wa watoto wachanga unafanyika tangu lini?

Ubatizo wa watoto wachanga unafanyika tangu mwanzo, usipingwe na yeyote kwa miaka elfu na zaidi. Ni kwamba Wayahudi walipokea watoto katika dini yao kwa kuwatahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa.
“Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu” (Lk 2:21).
Watu wa mataifa walipoongokea dini hiyo, walioshwa na kutahiriwa pamoja na watoto wao. Mitume pia walipokea katika Kanisa familia nzima, si wazazi tu. Walibatizwa “yeye na nyumba yake”, “yeye na watu wake wote” (Mdo 16:15,33); “watu wa nyumbani mwa Stefana” (1Kor 1:16).
Kwa hiyo tunaona kuwa tangu wakati wa Mitume sio watu wazima tuu waliokua wakibatizwa bali na watoto pia.
Kwa Kanisa Katoliki, ubatizo sio ukamilifu wa kuwa Mkristo. Ubatizo ni Sakramenti ya kwanza ambayo inakamilishwa na Sakramenti ya Kipaimara ambayo humfanya Mkristo kuwa mkamilifu kwa kukiri na kuahidi mwenyewe kuwa Mfuasi wa Yesu Kristu kwa kumkataa Shetani na Mambo yake yote. Kwa maana hiyo, watoto wanapobatizwa wazazi wanamtoa au wanamwalika mtoto katika Imani ya Kikristu wakiahidi kumtumza na kumwelekeza katika njia ya Imani kwa Yesu Kristu mpaka atakapokua mkubwa na kuwa na ufahamu na Elimu ya kutosha kuhusu Imani yake ndipo na yeye atakiri na kuahidi mwenyewe wakati wa Sakramenti ya Kipaimara.


Je, ubatizo tuu unatosha?

Hapana, ubatizo hautoshi, bali unahitaji kukamilishwa na kipaimara na ekaristi, kama vile baada ya kuzaliwa tunahitaji kukomaa na kudumisha uhai wetu kwa chakula.
Sakramenti hizo tatu kwa pamoja ni msingi wa maisha ya Wakristo wote, kumbe nyingine zinahitajika tu katika hali na nafasi maalumu. Mitume waliwaendea Wasamaria
“wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu” (Mdo 8:15-16).
“Amin, amin, nawaambieni: Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndaniyenu” (Yoh 6:53).


Sakramenti inayohusiana zaidi na ubatizo ni ipi?

Sakramenti inayohusiana zaidi na ubatizo ni kipaimara, kinachoendeleza kazi yake.
“Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao” (Mdo 19:5-6).
Sakramenti hizo ni kama pande mbili za pesa moja. Zinahusiana kama Pasaka na Pentekoste, ambayo ni utimilifu wake, kwa kuwa siku alipofufuka Yesu aliwapulizia Mitume Roho Mtakatifu, ambaye siku hamsini baadaye akawajia kama
“upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote” (Mdo 2:2).


Sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ipi?

Sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ekaristi, iliyo kuu kuliko sakramenti zote kwa sababu ndiyo Yesu mzima, Mungu-mtu, katika maumbo ya mkate na divai.
Sisi ambao tulishiriki kifumbo kifo na ufufuko wake tukapokea kwake paji la Roho Mtakatifu, tunaalikwa kukaribia mara kwa mara meza anapotulisha na kutunywesha Mwili na Damu yake ili tushiriki uhai wake kwa dhati zaidi na zaidi.
“Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yoh 6:56-57).
Ubatizo na kipaimara havirudiwi, vinadumu ndani mwetu kama mifupa ambayo ekaristi ya mara kwa mara inazidi kuitia mwili na damu.


Sakramenti ya ubatizo ni nini?

Sakramenti ya Ubatizo ni Sakramenti yenye kuondoa dhambi ya asili pamoja na dhambi nyingine zote tulizotenda, kufufua roho zetu kwa kututia uzima wa Mungu, Kutuandika Wakristu Watoto wateule wa Mungu na wa Kanisa.


Ubatizo ni nini?

Ubatizo ni Sakramenti inayotuwezesha kuzaliwa mara ya pili kwa Maji na Roho Mtakatifu, ni mlango (Kiingilio) kwa Sakramenti nyingine zote na ni ufunguo wa uzima wa milele. (Yoh 3:3, Mt28:19)


Sakramenti ya Ubatizo yatuletea nini?

Sakramenti ya Ubatizo yatuletea;
1. Maondoleo ya dhambi ya asili
2. Maondoleo ya dhambi zote za binafsi na adhabu zake
3. Neema ya Utakaso kwa mara ya kwanza
4. Yatutia alama isiyofutika (1Kor 6:11, 12:13)


Kuna Ubatizo wa namna ngapi?

Kuna Ubatizo wa namna tatu;
1. Ubatizo wa maji – Ubatizo wa kawaida
2. Ubatizo wa tamaa – Mfano mtu akifa akiwa na nia ya kubatizwa au akitamani kubatizwa
3. Ubatizo wa Damu – Mtu akiifia Imani japo hajabatizwa


Nani aweza kubatiza?

Mwenye mamlaka ya kubatiza kwa kawaida ni yule mwenye dataja takatifu katika Kanisa, lakini katika hatari ya kufa kila mtu anaweza kubatiza.


Kwa nini Kanisa linabatiza watoto wadogo?

Kwa sababu wanazaliwa na dhambi ya asili hivyo wanahitaji kuwekwa huru kutoka mamlaka ya yule mwovu na kuingizwa katika ufalme wa uhuru wa wana wa Mungu


Je, Ubatizo ni lazima kwa wokovu?

Ndiyo, nilazima kwa wokovu kwa wale ambao wametangaziwa injili na wanasifa ya kuomba Sakramenti hiyo


Anayebatizwa yampasa nini?

Yampasa kuungama imani yake ama mwenyewe akiwa mtu mzima ama kupitia wazazi kama akiwa mtoto mdogo


Alama wazi ya Sakramenti ya Ubatizo ni nini?

Alama wazi ya Sakramenti ya Ubatizo ni kumwagia maji katika panda la uso na kutamka maneno “Fulani (jina lake linatajwa) nakubatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” (Mt 28:19)


Msimamizi wa ubatizo ana wajibu gani?

Msimamizi wa ubatizo ana wajibu hizi;
1. Kutoa mfano mzuri wa maisha ya Kikristo
2. Kumuongoza mbatizwa katika maisha ya Ukristo
3. Kumuombea mbatizwa
4. Kushirikiana na wazazi katika malezi

Maswali na Majibu kuhusu Hukumu ya Mwisho

Ufufuko wa wafu maana yake nini?
Ufufuko wa wafu maana yake mwisho wa dunia watu wote watafufuka na miili yao na kwenda nayo katika furaha ya milele au moto wa milele. (Ayu 19:25-26, Mt 22:30-32, Yh 28-29)


Baada ya kifo cha mtu nini hutokea?
Baada ya kifo roho yake inafika mbele ya Mungu kwa hukumu ya mtu binafsi.


Matokeo ya hukumu hiyo ni nini?
Matokeo ya Hukumu hiyo ni roho kwenda Mbinguni, Toharani au Motoni. (Mt 25:34-46)


Mbinguni ni mahali pa namna gani?
Mbinguni ni makao mema ya heri na furaha (2Kor 5:1, Ufu, 2:17).
Waendao mbinguni ni wale wanaokufa katika hali ya neema ya utakaso na urafiki na Mungu na waliotakaswa kikamilifu


Motoni ni nini?
Motoni ni makao mabaya kwa Shetani walaaniwa wakaapo mbali na Mungu wakiteswa milele. (Mt 25:41, Mik 9:42-43, 1Yoh 14:15)


Uzima wa milele ni nini?
Uzima wa milele ni maisha ya kukaa mbinguni na Mungu yasiyokua na mwisho.


Toharani ni mahali gani?
Toharani ni mahali pa mateso zinakosafishwa roho ambazo hazikutimiza kitubio vizuri baada ya kuungama dhambi. (1Kor 3:15, 1Pet 1:7).


Je, hatuwezi kupunguza mateso ya roho za marehemu waliokwenda toharani?
Ndiyo: twaweza kupunguza hata kuyamaliza kwa kuwasalia na kuwapatia rehema na hasa kwa kuadhimisha Misa kwa ajili yao. (2Mik 12:38-46)


Mambo makuu manne ya mwisho ni yapi?
Mambo hayo ni;
1. Kifo
2. Hukumu
3. Jehanamu (Motoni)
4. Paradiso. (Toharani/Mbinguni)


Je, ufufuko wa Yesu ni muhimu kwetu pia?
Ndiyo, ufufuko wa Yesu ni muhimu kwetu pia, kwa sababu kwa njia yake tu tunatiwa uzima: sasa rohoni kwa kuondolewa dhambi, na siku ya mwisho mwilini pia kwa kufufuliwa.
Mwenyewe alisema, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele” (Yoh 11:25- 26).
“Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu” (1Kor 15:20-21).
“Alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuka ili tupate kuhesabiwa haki” (Rom 4:25).


Je, ni muhimu tujiandae kufa?
Ndiyo, ni muhimu tujiandae kufa wakati wowote na namna yoyote kwa kuishi kitakatifu sasa na kwa kujiombea neema tutakazohitaji saa ya kufa kwetu, tukijua tumewekewa “kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu” (Eb 9:27).
“Katika mambo yako yote uukumbuke mwisho wako, hivyo hutakosa kamwe hata hatima” (YbS 7:36).
“Hamjui yatakayokuwako kesho! Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka” (Yak 4:14).
“Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni” (Math 26:41).


Je, ina thamani machoni pa Bwana mauti ya mtu aliyemcha?
Ndiyo, “ina thamani machoni pa Bwana mauti ya wacha Mungu wake” (Zab 116:15).
Hasa utiifu wa Yesu msalabani umegeuza laana ya kifo iwe baraka kwa waamini wake.
“Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao” (Ufu 14:13).


Tutakapofariki dunia itatutokea nini?
Tutakapofariki dunia roho yetu isiyokufa, mbali na mwili unaooza, itapewa tuzo au adhabu tuliyostahili kwa maisha yetu. “Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake” (Lk 16:22-23). “Kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida… ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo, maana ni vizuri zaidi sana” (Fil 1:21,23). “Nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana” (2Kor 5:8). Kwa kuwa kifo ni “mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa” (Mhu 12:7). Siku ya ufufuo roho na mwili vitaungana tena kwa ajili ya uzima au moto wa milele. “Pumzi iliwaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno” (Ez 37:10).
Je baada ya kufa ni hapo hapo roho inaenda motoni au mbinguni, Au ni mpaka Siku ya hukumu Yesu Atakaporudi?
Ni siku ile ile Roho ya mtu aliyekufa inaenda Mbinguni, toharani au Motoni. Yesu alimwahidi yule mtu waliyesulubiwa pamoja kuwa watakuwa peponi pamoja siku hiyo hiyo na sio siku ya hukumu.
“Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.” 43 Yesu akamwambia, “Nakwambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.” (Luka 23:42-43)
Sauli aliweza kuongea na Samweli hata baada ya kufa na Samweli alimbashiria mambo yatakayotokea kwa Sauli maanake ni kwamba Japokuwa alikuwa amekufa bado anayomuungano na Mungu ndio maana aliweza kumwambia Sauli mambo yatakayompata,
“7Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi ili nimwendee nipate kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, “Yuko mwanamke mmoja huko Endori.” 8Hivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie na unipandishie huyo nitakayekutajia,” 9Huyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya mfalme Sauli. Amewakatilia mbali wapunga pepo, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?” 10Sauli akamwapia huyo mwananmke kwa Jina la BWANA, akasema, “Kwa hakika kama BWANA aishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.” 11Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani? Sauli akasema, “Nipandishie Samweli.” 12Yule mwanamke alipomwona Samweli alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamwuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.” 13Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini? Yule mwanamke akasema, “Naona Mungu anapanda kutoka ardhini.” 14Sauli akamwuliza, “Ni mfano wa nini?” Yule mwanamke akasema, “Ni mwanaume mzee amevaa joho anayepanda.” Ndipo Sauli akatambua kwamba ni Samweli. Sauli akasujudu kifudifudi uso wake hadi ardhini. 15Samweli akamwuliza Sauli, Kwa nini unanitaabisha, kunipandisha juu?” Sauli akasema, “Mimi ninasumbuka sana, kwa maana Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, naye Mungu ameniacha. Hanijibu tena wala kwa njia ya manabii wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita wewe ili unijulishe lakufanya.” 16Samweli akamwuliza, “Kwa nini uniulize mimi, maadam BWANA amekuacha na kuwa adui yako? 17BWANA ametenda lile alilotangulia kusema kwa kupitia kwangu. BWANA ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, naye amempa mmoja wa jirani zako, yaani, Daudi. 18Kwa sababu wewe hukumtii BWANA, wala hukumtimizia ghadhabu yake kali juu ya Waamaleki, BWANA amekutendea mambo haya leo. 19Zaidi ya hayo, BWANA atawatia Israeli pamoja na wewe mkononi mwa Wafilisti na kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. BWANA pia atalitia jeshi la Israeli mkononi mwa Wafilisti.
Mfano Wa Tajiri Na Maskini Lazaro Yesu alisimulia hivi
19 Akasema, “Palikuwa na tajiri mmoja aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, nguo za gharama kubwa, kila siku. 20 Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima, alikuwa akiletwa mlangoni kwa huyo tajiri kila siku. 21 Lazaro alikuwa akitamani kula makombo yaliyodondoka mezani kwa tajiri. Hata mbwa walikuwa wakiramba vidonda vyake. 22 “Hatimaye, yule maskini alikufa. Malaika wakamchukua akakae pamoja na Ibrahimu mbinguni. Yule tajiri naye pia akafa, akazikwa. 23 Alipokuwa kuzimuni ambapo alikuwa akiteseka, alita zama juu, akamwona Ibrahimu kwa mbali na Lazaro karibu yake. 24 Akaita, ‘Baba Ibrahimu, nionee huruma umtume Lazaro achovye japo ncha ya kidole chake katika maji aupoze ulimi wangu maana ninateseka kwenye moto huu.’ 25 Lakini Ibrahimu akamjibu, ‘Mwa nangu, kumbuka kwamba ulipokuwa hai ulipata kila kitu kizuri uli chotaka, ambapo Lazaro alipokea mabaya. Lakini sasa anafarijika hapa na wewe unateseka. 26 Isitoshe, kati yetu na ninyi huko, kumewekwa bonde kubwa lisilopitika ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko au kutoka huko kuja huku wasiweze.’ 27 Akasema, ‘Basi, baba, tafadhali umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu, 28 awaonye ndugu zangu, wasije wao pia wakaletwa mahali hapa pa mateso watakapokufa.’ 29 Ibrahimu akamjibu, ‘Ndugu zako wanazo sheria za Musa na maandiko ya Manabii. Itawapasa watii hayo.’ Lakini yule tajiri akazidi kumsihi, 30 ‘Hapana baba Ibrahimu, ndugu zangu hawatashawishiwa na hayo. Lakini mtu kutoka kuzimu akitumwa kwao watatubu na kuziacha dhambi zao.’ 31 “Ibrahimu akamwambia, ‘Wasiposikiliza na kutii sheria za Musa na Maandiko ya manabii, hawatashawishika kutubu hata kama mtu akifufuka kutoka kuzimu.”’ (Luka 16:19-31)
Wakati Yesu anabadilika Sura walitokea Musa na Eliya.
“Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane nduguye, akaenda nao peke yao juu ya mlima mrefu. 2 Huko, wakiwa wanamtazama, akageuka sura, uso wake ukang’aa kama jua na mavazi yake yakawa meupe kama nuru. 3 Mose na Eliya wakawatokea, wakawa wanazungumza naye. 4 Hapo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri sana kwamba tupo hapa! Ukipenda nitajenga vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya.” (Mathayo 17:1-5)
Yesu alituambia kuwa Mungu sio wa wafu bali wa walio hai ndio maana akaitwa Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo kwa kuwa Wote wako hai kwake.
37Hata Mose alidhihirisha kuwa wafu wanafufuka, kwa habari ya kile kichaka kilichokuwa kikiwaka moto bila keteketea, alipomwita Bwana ‘Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki na Mungu wa Yakobo.’ 38Yeye Mungu si Mungu wa wafu bali wa walio hai, kwa kuwa Kwake wote ni hai.” (Luka 20:37-38)
Yesu alimwahidi yule mtu waliyesulubiwa pamoja kuwa watakuwa peponi pamoja siku hiyo hiyo na sio siku ya hukumu.
“Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.” 43 Yesu akamwambia, “Nakwambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.” (Luka 23:42-43)
Angalia pia wakati Stefano akipigwa Mawe aliikabidhi roho yake kwa Mungu baada ya kuona mbingu zimefunguka hii ni kama Yesu alivyokuwa pale msalabani aliikabidhi Roho yake kwa Baba yake.
55Lakini yeye Stefano akiwa amejazwa Roho Mtakatifu, alikaza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu, naye Yesu akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu. 56Akasema, “Tazameni! Naona mbingu zimefunguka na Mwana wa Adamu amesimama upande wa kuume wa Mungu.’’ 57Lakini wao wakapiga kelele kwa sauti kubwa, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja. 58Wakamtupa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni mwa kijana mmoja aitwae Sauli. 59Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu” 60Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.’’ Baada ya kusema haya, akalala. (Mdo 7:55-60)
Kwenye Ufunuo tunasoma (Ufunuo 6:9-10) “Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vile vile kama wao.”
Kwa hiyo mtu akifa anaenda mbinguni au motoni kulingana na alivyoishi.
“Nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana” (2Kor 5:8). Kwa kuwa kifo ni “mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa” (Mhu 12:7).
Siku ya ufufuo roho na mwili vitaungana tena kwa ajili ya uzima au moto wa milele.
“Kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida… ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo, maana ni vizuri zaidi sana” (Fil 1:21,23).
Mtume Petro ameandika hivi…
“18 Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa,19 ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri; 20 watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji.” (1Petro 3:18-20)


Je, sisi wanyonge tunaweza kushiriki uzima wa milele wa Mungu?
Ndiyo, sisi wanyonge tunaweza kushiriki uzima wa milele wa Mungu: hapa duniani katika mwanga hafifu wa imani, na kisha kufa katika uangavu wa utukufu usiofifia kamwe. Kwa kuwa lengo la Baba ni kwamba tuungane na Yesu Mwanae kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ili tuwe na utukufu wake.
“Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yoh 17:3).
“Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa” (2Pet 1:3-4).
Sisi tuliobatizwa tunaitwa “wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo!” (1Yoh. 3:1).
Kwa sababu tumesadiki kwamba “Mungu ni upendo” (1Yoh 4:8) na kwamba “hakuna lisilowezekana kwa Bwana” (Lk 1:37).
“Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’ Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu” (Gal 4:6-7).


Aliyezungumzia moto wa milele ni nani?
Aliyezungumzia moto wa milele ni hasa Yesu: akitufunulia ukuu wa upendo wa Mungu, aliye heri yetu pekee, alituangalisha juu ya hatari ya kutengana naye milele kwa dhambi. Mwenyewe atatoa hukumu hiyo:
“Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake” (Math 25:41).
“Humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki” (Mk 9:48).
“Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku” (Ufu 14:11).


Toharani maana yake nini?
Toharani maana yake kuna hali ya muda ambayo huruma ya Mungu inawatakasa marehemu waliofariki dunia katika urafiki naye lakini bila ya usafi kamili unaotakiwa kwa kuingia mbinguni. Sisi tunaweza kuharakisha utakaso wao kwa kumtolea Mungu sala na sadaka, hasa ekaristi. Yuda Mmakabayo “alichanga fedha kwa kila mtu jumla drakma elfu mbili, akazipeleka Yerusalemu kutoa sadaka ya dhambi.
Kwa kufanya hivi alitenda vema na kwa haki, kwa kuwa aliukumbuka ufufuo wa wafu. Maana kama asingalitumaini ya kuwa wale waliokufa watafufuka, ingalikuwa kazi bure isiyo na maana kuwaombea wafu. Lakini kwa kuwa aliufikiri utukufu wa thawabu waliowekewa wale wafao katika utauwa, wazo lake lilikuwa takatifu na la kicho. Ndiyo sababu alifanya upatanisho kwa wafu ili wafunguliwe dhambi zao” (2Mak 12:43-46). Imani hiyohiyo iliongoza Wakristo wa kwanza kuwafanyia marehemu ibada ambayo haieleweki vizuri, lakini hailaumiwi na Mtume Paulo: “Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao?” (1Kor 15:29).


Je, mwili utakaofufuliwa ni huuhuu tulionao sasa?
Ndiyo, mwili utakaofufuliwa ni huuhuu tulionao sasa, lakini katika hali tofauti: > “hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika” (1Kor 15:42).
Siku ya ufufuo “ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi” (Lk 21:27).
“Saa yaja ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuko wa uzima, na waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu” (Yoh 5:28-29).
“Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele” (Math 25:46).


Siku ya ufufuo Kristo mfalme atatuhukumu vipi?
Siku ya ufufuo Kristo mfalme atatuhukumu kwa kudhihirisha misimamo ya watu wote ambao, kwa kupokea au kukataa upendo wa Mungu moyoni mwao, wametenda mema au la.
“Imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyopenda, kwamba ni mema au mabaya” (2Kor 5:10).
“Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu” (1Kor 4:5).
“Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake. Na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, ‘Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia… Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi’” (Math 25:31-36,40).
“Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema” (Math 5:7).


Baada ya hukumu ya mwisho itakuwaje?
Baada ya hukumu ya mwisho, waadilifu watatukuzwa mwili na roho pamoja na Yesu, na ulimwengu pia utageuzwa.
“Kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake” (2Pet 3:13).
“Na Roho na Bibi arusi wasema, ‘Njoo!’ naye asikiaye na aseme, ‘Njoo!’… Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, ‘Naam, naja upesi’. Amina. Na uje, Bwana Yesu! Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina” (Ufu 22:17,20-21).

Shopping Cart
2
    2
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About