Mafundisho ya Katekisimu

Amri ya Nane ya Mungu: Makatazo na Amri

Amri ya Nane ya Mungu inatukataza nini?

Inakataza haya:

1. Ushahidi wa uongo, kiapo cha uongo na uongo wowote.
2. Hukumu isiyo ya haki, usengenyaji, uchafuzi wa jina na usingiziaji.
3. Kusifu watu uongo, kujisifu mwenyewe au ulaghai.


Katika Amri ya Nane Mungu anaamuru nini?

Katika Amri ya Nane Mungu anaamuru tuseme ukweli na tulinde heshima ya wengine. (Mt 5:37, Yak 5:12).


Twaharibu heshima ya wengine kwa namna gani?

Twaharibu Kwa

1. Kuwadhania vibaya
2. Kuwasengenya (Mith 12:22)
3. Kuwasingizia na kuleta uzushi. (Mdo 5:1-11; Law 19:11)


Aliyeharibu heshima ya mwingine yampasa afanye nini?

Aliyeharibu heshima ya mwingine yampasa kuirudisha kadiri awezavyo.


Tunalinda heshima ya wengine kwa namna gani?

Tunalinda heshima ya wengine kwa kuwaza na kusema mema juu yao. (1Kor 13:6)

Mambo ya Msingi kujua kuhusu Sakramenti ya Kitubio

Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu gani?
Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu alijua udhaifu wa binadamu hauishi mara anapopokea uzima wa Mungu kwa sakramenti tatu za kuingizwa katika Ukristo. Hivyo alipanga kusaidia mpaka mwisho wa dunia waamini wake watakaopatwa na dhambi na ugonjwa, kama alivyowasaidia wengi aliokutana nao katika maisha yake.
“Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, ‘Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako’… ‘Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi’ – amwambia yule mwenye kupooza – ‘Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako’. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii” (Math 9:2,6-8).

Mungu aliwapa watu (mapadri) amri/uwezo ya kusamehe dhambi kwa njia ya nani? Ni halali kuungama kwa padre?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa njia ya Mwanae. Yesu mfufuka aliwaonyesha Mitume alama ya mateso mwilini mwake, “akawavuvia, akawaambia, ‘Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23).
Katika Kanisa tunafurahi kupewa msamaha wa dhambi kila tunapohitaji, mradi tutubu. Kwa njia ya mwandamizi wa Mitume, Yesu anatuambia,
“Umesamehewa dhambi zako… Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani” (Lk 7:48,50).
Si dhana wala hisia tu, bali ni neno la hakika tunalolipokea kwa masikio yetu.

Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zipi?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zote, kwa sababu upendo mtiifu wa Mwanae aliyejitoa kuwa sadaka ya wokovu wetu unampendeza kuliko dhambi zote zinavyomchukiza. Ila hatuwezi kusamehewa dhambi ya kukataa neema ambayo Roho Mtakatifu anatusukuma tuamini na kutubu, kwa sababu pasipo imani na toba hapana msamaha.
“Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa” (Math 12:31).
“Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure” (2Kor 6:1).

Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu gani?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu amependa washiriki katika kazi zake. Ametuumba kwa njia ya wazazi na kutulea na kutusaidia kwa njia ya wengine pia. Hasa ametuokoa kwa njia ya Yesu, ambaye yupo nasi sikuzote katika Mwili wake, yaani Kanisa, na katika wale walioshirikishwa mamlaka ya Mitume.
“Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:18-20).

Je, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi?
Ndiyo, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi tulizotenda baada ya ubatizo, kwa kuwa hatuwezi kupokea msamaha tukikataa masharti yake, na Mungu ametupangia watu ambao watuondolee kwa niaba yake.
“Watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohane. Lakini, Mafarisayo na wanasheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye” (Lk 7:29-30).
Yesu mwenyewe alikubali kubatizwa na Yohane ili atimize mpango wa Baba.
“Yohane alitaka kumzuia, akisema, ‘Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?’ Yesu akajibu akamwambia, ‘Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Math 3:14-15).
Je, sisi tukatae kumkimbilia padri wa Mungu ili kupokea huruma yake tunayoihitaji kuliko hewa?

Tumuungamie padri dhambi zetu kwa lengo gani? Kwa nini Wakatoliki wanaungama kwa padri?
Tumuungamie padri dhambi zetu ili aweze kutushauri na kuamua kama tuko tayari kuondolewa. Tumweleze kwa unyofu makosa yote tuliyoyafanya na nia tuliyonayo ya kuyafidia na kutoyarudia.
“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu” (1Yoh 1:8-10).
Tukumbuke tulivyo viungo vya Mwili mmoja, hivi kwamba dhambi zetu zimewadhuru wenzetu. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana, mpate kuponywa” (Yak 5:16).
Kutokuwa tayari kufanya hivyo walau sirini kwa padri ni dalili ya kiburi na ya kutotubu.

Je, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi?
Ndiyo, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi kwa niaba ya Mungu aliyempa mamlaka hiyo. Hatusamehewi na utakatifu wa padri, bali na huruma ya Baba kwa njia yake.
Yeye anamtumia padri yeyote ili kuturahisishia kazi, tusihitaji kuchunguza kwanza ubora wa maisha yake, wala kwenda mbali tukampate mmoja asiye na dhambi. Tungefanyeje kuhakikisha ni mtakatifu, wakati hatuwezi kusoma moyo wake? Ingekuwa hivi, tusingepata kamwe hakika ya kusamehewa. Kumbe inatutosha kujua ni padri, kwamba Mungu amempa mamlaka ya kusamehe dhambi, kama Yesu alivyowapa Mitume siku tatu baada ya kumkimbia na hata kumkana. Kila padri anaweza kukiri,
“Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa: ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi” (1Tim 1:15).
Amri ya kusamehe dhambi wamepewa watu, si malaika.
“Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu” (2Kor 4:7).

Je, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo?
Ndiyo, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo, lakini ni vigumu zaidi, kwa sababu hatupati msaada wa sakramenti hiyo maalumu.
Pamoja na nia ya kumuungamia padri mapema tunahitaji neema ya kutubu kikamilifu, si kwa kuhofia adhabu, bali kwa kumpenda Mungu tuliyemchukiza.
“Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana” (Lk 7:47).

Sakramenti ya Kitubio ni nini?
Sakramenti ya Kitubio ndiyo Sakramenti ya kuwaondolea watu dhambi walizotenda baada ya Ubatizo (Yoh 20:22-23)

Lini na kwa maneno gani Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio?
Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio jioni ya ufufuko wake alipowapulizia mitume na kuwaambia maneno haya “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi watakua wameondolewa, wowote mtakaowafungia dhambi watakua wamefungiwa” (Yoh 20:22-23)

Mwenye kuwaondolea watu dhambi ni nani?
Mwenyezi Mungu pekee yake aweza kuwaondolea watu dhambi. Ndiye aliyewapa Mitume, Maaskofu na Mapadri uwezo wa kuwaondolea watu dhambi (Yoh 20:21-23)

Nani yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio?
Kila mkristo aliyetenda dhambi yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio

Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa haya
1. Kutafuta dhambi moyoni (Yoh 3:20-21)
2. Kujuta dhambi
3. Kukusudia kuacha dhambi
4. Kuungama kwa padre
5. Kutimiza malipizi
6. Kumshukuru Mungu aliyemwondolea dhambi

Wakati wa Sakramenti ya Kitubio Utamwomba Roho Mtakatifu kwa sala gani?
Utamuomba Roho Mtakatifu kwa sala hii:
Uje Roho Mtakatifu unisaidie nitambue dhambi zangu, nijute sana, niungame vema, nipate kutubu kweli. Amina

Kutafuta dhambi maana yake ni nini?
Kutafuta dhambi maana yake ni kujiuliza moyoni dhambi nilizotenda Tangu ungamo la mwisho (Ef 4:17-32)

Utafuteje dhambi wakati wa kujiandaa kuungama?
Tafuta dhambi kwa njia hizi
1. Kwa kukumbuka uliyokosa kwa mawazo, kwa maneno na kwa vitendo
2. Katika Amri za Mungu na za Kanisa
3. Katika vichwa vya dhambi
4. Katika kutimiza wajibu

Kutubu dhambi maana yake ni nini?
Kutubu dhambi maana yake ni kuona uchungu na chuki moyoni juu ya dhambi tulizotenda na kukusudia kutotenda dhambi tena (Yoh 8:11)

Kwa nini tujute dhambi zetu?
Tunajuta dhambi zetu kwa sababu tumeukosea Utatu Mtakatifu na tunastahili adhabu yake, na pia bila majuto hatuwezi kupata maondoleo ya dhambi.

Kuna majuto ya namna ngapi?
una majuto ya namna mbili,
1. Majuto kamili/Majuto ya mapendo
2. Majuto yasiyokamili/majuto pungufu/majuto ya hofu

Majuto kamili ni nini?
Majuto kamili ni kujuta kwa sababu tumemchukiza Mungu mwenyewe aliye mwema na mpendelevu kabisa

Majuto yasiyo kamili au majuto pungufu ni nini?
Majuto yasiyokamili ni kujuta kwa sababu tumepoteza furaha za Mbinguni na tunahofia adhabu ya Mungu

Asiyejuta aweza kuondolewa dhambi?
Asiyejuta hawezi kuondolewa dhambi kabisa, na anayeungama bila kujuta anatenda dhambi kubwa ya kufuru.

Kabla ya kuungama ni lazima kufanya nini?
Kabla ya kuungama ni lazima kukusudia kuacha dhambi na kuepuka nafasi kubwa ya dhambi bila kusahau kufuata hatua sita za kabla na baada ya kupokea kupokea Sakramenti ya Kutubio ambazo ni,
(1) kuwaza/kutafuta dhambi moyoni,
(2)kutubu/ kujuta,
(3)kukusudia kuacha dhambi,
(4)kuungama kwa padri,
(5)kutimiza kitubio,
(6)kumshukuru Mungu

Anayetaka kweli kuacha dhambi afanye nini?
Anayetaka kuacha dhambi afanye nguvu kuvishinda vishawishi, asali/aombe na apokee Sakramenti Mara nyingi hasa Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi Takatifu.

Kuungama ni kufanya nini?
Kuungama ni kumwambia Padri wazi wazi dhambi zako ulizotenda, zipi na ngapi ili upate maondoleo.

Anayeficha kusudi dhambi ya mauti katika ungamo anaondolewa?
Haondolewi, Bali anatenda dhambi kubwa ya kukufuru Sakramenti ya Kitubio. (Mt 7:21-23, Yoh 20:23, Gal 6:7)

Anayekufuru Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Yampasa kuziungama tena dhambi zake zote alizotenda tangu ondoleo la mwisho

Padri anaondolea dhambi mahali pa nani?
Padri anaondolea dhambi mahali pa Mungu

Padri anaondolea dhambi kwa maneno gani?
Padre anaondolea dhambi kwa maneno haya: Nami “Nakuondolea dhambi zako zote kwa Jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu”.

Kitubio tuwezacho kupewa na padre ni nini?
Kitubio tuwezacho kupewa na Padre ni kama sala, kufunga, kutoa sadaka kwa maskini, kusoma maandiko matakatifu, kuwatazama wagonjwa, n.k.

Kitubio tupewacho na padre chatosha?
Ni shida kutosha. Mara nyingi chataka malipizi ya hapa duniani kama kufunga, magonjwa, masumbuko, sala n.k mateso yasipotosha hapa duniani yatakamilishwa toharani

Kutimiza malipizi maana yake ni ni nini?
Kutimiza malipizi maana yake ni kutekeleza kiaminifu sala au matendo aliyotuagiza padre muungamishi ili kulipa adhabu za muda. (Rom 8:17)

Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema zipi?
Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema hizi;
1. Maondoleo ya dhambi zote kubwa na adhabu ya milele
2. Maondoleo ya dhambi ndogo na adhabu nyingine za muda (Isa 6:5-7, Yoh 8:11)
3. Twarudishiwa na kuongezewa neema ya utakaso
4. Twasaidiwa kuepa dhambi na twapata nguvu ya kutenda mema
5. Twarudishiwa tena mastahili tuliyopoteza kwa dhambi zetu

Amri ya Tano ya Mungu: Kutunza uhai wetu na wa watu wengine

Katika Amri ya Tano ya Mungu tumeamriwa nini?

Tumeamriwa tutunze uhai wetu na wa watu wengine tangu mwanzo hadi mwisho. (Mwa 4:10-11)


Kwa nini ni lazima kutunza uhai wetu na wa wenzetu?

Kwa sababu uhai wa watu wote umetoka kwa Mungu


Haki gani ya Binadamu ni ya msingi kupita zote?

Haki ya binadamu iliyo ya msingi kupita zote ni uhai wake ambao ni lazima uheshimiwe na kulindwa tangu siku ya kutungwa mimba


Nani anatenda dhambi dhidi ya amri ya tano ya Mungu? Mambo yanayovunja Amri ya Tano ya Mungu

Anayetemda dhambi dhidi ya amri ya tano ya Mungu ni yule;-

1. Anayemuua mtu au anayejiua mwenyewe
2. Anayemdhuru mwingine kwa namna yoyote ile
3. Anayeua Mimba na kuharibu nguvu za uzazi
4. Anayesaidia kuua, kumdhuru mtu au anayesaidia kutoa/kuharibu mimba
5. Anayeharibu mazingira yaliyomuhimu kwa uhai
6. Anayetetea au kuendeleza mifumo ya ya dhuluma, uhasama na vita.

Ni nini imani ya Kanisa Katoliki kuhusu msamaha na rehema?

Leo tutajadili kuhusu imani ya Kanisa Katoliki kuhusu msamaha na rehema. Kwa Wakatoliki, msamaha na rehema ni mada muhimu sana katika imani yetu. Tunakubali kwamba sisi sote ni wenye dhambi na tunahitaji kusamehewa dhambi zetu kwa ajili ya kufikia wokovu.

Tunamwamini Mungu kama mwenye rehema, ambaye anatupenda sana hata kama tumeanguka katika dhambi zetu. Kwa sababu ya upendo wake, Mungu ametoa njia ya msamaha na rehema kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu.

Kanisa Katoliki linahimiza Wakatoliki kutubu dhambi zao na kupata Sakramenti ya Upatanisho kama njia ya kupata msamaha wa dhambi. Sakramenti hii inaruhusu Wakatoliki kusema dhambi zao kwa padri na kufanya toba kwa ajili ya dhambi hizo. Padri kisha anawapa Wakatoliki msamaha wa dhambi zao kwa jina la Yesu Kristo.

Kanisa Katoliki linapenda kutumia Biblia kama mbinu ya kuwasilisha ujumbe wake. Katika wosia wa Yohana, tunasoma kwamba "ukiungama dhambi zako, yeye ni mwaminifu na wa haki hata akusamehe dhambi zako, na kukusafisha na uovu wote" (1 Yohana 1:9). Yesu mwenyewe pia alitoa uwezo wa kupata msamaha wa dhambi kwa wanafunzi wake katika Yohana 20:23.

Kanisa Katoliki pia linazingatia Catechism ya Kanisa Katoliki, ambayo inasema kwamba "Sakramenti ya Upatanisho inatupatia msamaha wa dhambi na kutufungulia njia ya kuwa na uhusiano mzuri na Mungu na Kanisa" (CCC 1422).

Kwa hiyo, msamaha na rehema ni muhimu sana katika imani ya Kanisa Katoliki. Tunamwamini Mungu kuwa mwenye rehema na tunajua kuwa kupata msamaha wa dhambi zetu ni njia ya kufikia wokovu. Kwa hiyo, tunahimiza Wakatoliki kuja kwa Sakramenti ya Upatanisho mara kwa mara ili kufurahia msamaha wa dhambi zao na kuwa na uhusiano mzuri na Mungu na Kanisa.

Ni nini imani ya Kanisa Katoliki kuhusu umoja wa Kanisa?

Kanisa Katoliki ni moja ya madhehebu makubwa ya Kikristo duniani. Imani yake kuhusu umoja wa Kanisa ni dhahiri kabisa. Kanisa Katoliki linasimamia umoja wa Kanisa kwa kufuata kanuni za Kikristo na sheria zake. Katika makala hii, tutajadili kwa kina imani ya Kanisa Katoliki kuhusu umoja wa Kanisa.

Kanisa Katoliki linatazama umoja wa Kanisa kama sehemu muhimu ya imani yake. Katika Injili ya Yohana 17:20-21, Yesu alisema, "Nakuomba pia kwa ajili ya wale watakaoniamini kwa sababu ya ujumbe wao, ili wote wawe na umoja. Kama wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi ndani yako, hata hao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ndiwe uliyenituma." Hii ina maana kwamba Yesu alitaka wafuasi wake kuwa na umoja, ili ulimwengu upate kuona kwamba wao ni kweli wanafunzi wake.

Kanisa Katoliki linasisitiza umoja wa Kanisa kwa njia nyingi. Mojawapo ya njia hizo ni kwa kuhakikisha kwamba liturujia zake ni moja, kwa kutumia lugha ya Kilatini. Hii ni kwa sababu lugha ya Kilatini ni lugha ambayo ilikuwa inatumiwa katika Kanisa la mapema, na ina maana ya kuunganisha na kudumisha utamaduni wa Kanisa la mapema.

Katika Catechism ya Kanisa Katoliki, kifungu 820 kinasema, "Kanisa, katika Kristo, ni jumuiya ya waamini ambao wanaunganishwa pamoja na wale walioko mbinguni na wale ambao wako njiani kuelekea mbinguni. Ni jumuiya ya watakatifu. Umoja wa Kanisa ni hali ya uaminifu na upendo, ambao unatokana na Roho Mtakatifu." Hii inaonesha jinsi Kanisa Katoliki linavyoona umoja kama sehemu ya imani yake.

Kanisa Katoliki pia linahimiza umoja wa dini katika dunia. Kanisa linakubali kwamba kuna tofauti za kidini, lakini linasisitiza kwamba umoja wa dini ni muhimu kwa ajili ya amani na utulivu wa dunia. Kifungu cha 821 cha Catechism kinasema, "Katika kipindi cha historia, Kanisa limeishi kwa furaha na kwa heshima na dini zote, kwa sababu lilikuwa linatambua kwamba mambo mengi ya kweli na uzuri yanapatikana kwenye dini nyingine."

Kanisa Katoliki pia linahimiza umoja wa familia katika Kanisa. Hii inamaanisha kwamba Kanisa linataka familia zote zifanye kazi pamoja ili kujenga umoja katika Kanisa. Kanisa linahimiza familia kutumia muda pamoja, kusali pamoja na kushiriki Sakramenti pamoja.

Kwa ufupi, Kanisa Katoliki linasisitiza umoja kama sehemu muhimu ya imani yake. Kanisa linataka waamini wake wawe na umoja kama Yesu alivyotaka, ili ulimwengu uweze kuona kwamba wao ni kweli wanafunzi wake. Kanisa pia linahimiza umoja wa dini katika dunia, umoja wa familia katika Kanisa na umoja wa liturujia za Kanisa. Hii ni kwa sababu Kanisa linatambua kwamba umoja ni muhimu kwa ajili ya amani na utulivu wa dunia. Tufuate imani ya Kanisa Katoliki kuhusu umoja wa Kanisa.

Mambo ya Msingi kufahamu kuhusu Ndoa ya Kikatoliki

Daraja na ndoa ni tofauti na sakramenti nyingine kwa sababu gani?
Daraja na ndoa ni tofauti na sakramenti nyingine kwa sababu hazilengi hasa faida ya mtu anayezipokea, bali huduma zake kwa ajili ya Kanisa na jamii. Daraja inatia uwezo wa Kristo kwa ustawi wa Kanisa, Bibi arusi wake. Ndoa inatia upendo wake mwaminifu kwa ustawi wa familia, kanisa dogo la nyumbani.
“Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe” (Mdo 20:28).
“Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa” (Ef 5:29-32).

Kadiri ya mpango wa Muumba, ndoa halisi ina sifa ngapi?
Kadiri ya mpango wa Muumba, ndoa halisi ina sifa tatu: umoja, uimara na utayari wa kuzaa.
“Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, ‘Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja?’ Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe” (Math 19:4-6).
“Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, ‘Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha’” (Mwa 1:28).
Mitara, uzinifu, talaka, ushoga na kukataa uzazi ni kinyume cha mpango huo.

Yesu aliweka sakramenti ya ndoa kwa sababu gani?
Yesu aliweka sakramenti ya ndoa kwa sababu ya umuhimu wa familia kwa ustawi wa mume na mke, watoto, jamii na ufalme wa Mungu, na kwa sababu ya uzito wa majukumu yanayohusika.
“Siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwepo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake” (Yoh 2:1-2), akaleta divai bora ya ndoa sakramenti badala ya ndoa ya kimaumbile.
Hivyo ametuandalia neema tuweze kushinda “ugumu wa mioyo” (Math 19:8) unaohatarisha daima uzuri wa mpango wa Mungu kuhusu upendo mwaminifu katika ndoa. “Mungu aliona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana” (Mwa 1:31).

Ndoa ya Wakristo ni sakramenti ya nani?
Ndoa ya Wakristo ni sakramenti ya Yesu na Kanisa lake.
“Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi arusi, mke wa Mwanakondoo” (Ufu 21:9).
Wakiwa na ndoa halisi, mume na mke waliobatizwa ni ishara wazi ya hao wanaarusi wawili wasioonekana.
“Kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake” (Ef 5:24-25).
Ndiyo sababu Mkatoliki hawezi kufunga ndoa bila ya kuhusisha Kanisa na kufuata taratibu zake.

Ni zipi Sakramenti za Huduma ya ushirika na utume?
Ni Sakramenti mbili ambazo ni Sakramenti ya Daraja na Sakramenti ya Ndoa

Sakramenti ya ndoa ni nini?
Sakramenti ya ndoa ndio yenye kuwaunganisha wakristo wawili mume namke waliopendana kwa hiari bila shuruti au vitisho au kizuizi kwa kuwapa neema ya kuishi pamoja kitakatifu wakiwalea watoto wao katika utakatifu

Je, ndoa halali yaweza kuvunjwa?
Sakramenti ya ndoa iliyofungwa kihalali hudumu milele kwani Yesu anafundisha kuwa “Alichokiunganisha Mungu mwanadamu asikitenganishe” (Mt 19:6)

Ndoa imewekwa na nani?
Ndoa imewekwa na Mungu mwenyewe na Yesu Kristo ameeinua na kuifanya Sakramenti. (Mwz 2:18; Mt 19:1-12)

Kabla ya kupokea Sakramenti ya Ndoa hutakiwa nini?
Kabla ya kupokea Sakramenti ya Ndoa hutakiwa;
1. Uhuru wa kila mmoja
2. Matangazo ya ndoa
3. Wachumba wawe na nia ya kweli ya kuoana
4. Mafundisho na semina ya ndoa
5. Wasiwe na kizuizi chochote cha ndoa
6. Wasikae suria na wapokee Sakramenti ya Kitubio

Mtu aweza kupokea Sakramenti ya ndoa zaidi ya mara moja?
Ndiyo, mwenzi akifa yule aliyebaki yupo huru kufunga ndoa tena (1Kor 7:39)

Vizuizi vya ndoa ni kitu gani?
Vizuizi vya ndoa ni vile vinavyofanya ndoa isiwe halali tangu mwanzo

Vizuizi vya ndoa ni vipi?
Vizuizi vya ndoa ni;
1. Upungufu wa umri
2. Uhanithi
3. Ndoa awali halali
4. Tofauti za dini au upagani
5. Daraja Takatifu
6. Nadhiri
7. Utekaji au kutumia nguvu
8. Taksiri au Jinai au Mauaji ya mwenzi wa ndoa
9. Uhusiano wa damu
10. Uhusiano wa ndoa
11. Ugoni au uhawara
12. Kuasili mtoto au Uhusiano wa kisheria

Ndoa mchanganyiko maana yake ni nini?
Ndoa mchanganyiko ni ndoa kati ya Mkristo Mkatoliki na Mkristo asiye Mkatoliki

Ndoa ya utofauti wa Imani maana yake ni nini?
Ndoa ya utofauti wa Imani ni ndoa kati ya Mkristo Mkatoliki na mtu ambaye hajabatizwa kwa mfano Mpagani, Mwislamu, Yehova, Mlokole tangu kuzaliwa n.k

Mkristo Mkatoliki awezaje kufunga ndoa mchanganyiko au utofauti wa dini kwa uhalali?
Aweza kufunga ndoa hiyo kwa uhalali baada ya kupata ruhusa maalumu ya Askofu kwa Barua.

Ili Askofu atoe ruhusa ya kufungisha ndoa ya mchanganyiko au dini tofauti kuna Masharti gani?
Ndiyo, Askofu atatoa ruhusa baada ya Mkristo Mkatoliki kuahidi kwamba;
1. Atabaki Imani Katoliki mpaka kufa na isiwe amedanganya
2. Watoto wote watabatizwa na kulelewa katika Kanisa Katoliki
3. Huyo anayefunga naye ndoa akubali bila masharti yoyote

Je, Mchumba Mkatoliki aweza kuiacha Imani yake kwa sababu ya Ndoa?
Hapana, Kwa kuwa Kanisa Katoliki limeasisiwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo kama la lazima kwa kupata wokovu, wanaokataa kuingia au kuhudumu ndani yake hawawezi kuokolewa.

Kuna kosa gani kama mmoja wapo atakuwa amedanganya ili aruhusiwe kufunga ndoa mseto au mchanganyiko
Kama mmoja amedanganya basi ndoa hiyo ingawa imefungwa haitakuwa halali kabisa mpaka mwisho. Watadumu katika dhambi mpaka kufa au watubu.

Kanisa linatoa ushahuri gani kuhusu ndoa halali au ya mseto?
Kanisa linatambua hatari kubwa kwa Imani linashauri watoto wake wawe na busara kubwa wanapoamua kupendana kwa lengo la kufunga ndoa.

Je, ndoa halali inaweza kuvunjwa?
Hapana, Hakuna yeyote anayeweza kuvunja ndoa halali isipokuwa kifo. (Mt 19:4-6)

Anayevunja ndoa na kuoa au kuolewa anaweza kupokea Sakramenti?
Hapana, Anayevunja maagano ya ndoa na kuoa au kuolewa hawezi kupokea Sakramenti ya Ekaristi wala Kitubio hadi afanye toba na kurekebisha hali hiyo. (Mk 10:11-12)

Ni nani wahudumu wa Sakramenti ya ndoa?
Wahiudumu rasmi wa Sakramenti ya ndoa ni wachumba wenyewe, Padri kama shahidi rasmi wa kanisa. Tena ni lazima ifungwe mbele ya mashahidi wengine wawili.

Watu wa jinsia moja waweza kuoana?
Hapana, watu wa Jinsia moja hawawezi kuoana na wakifanya hinyo wanatenda dhambi kubwa inayomlilia Mungu. (Wal 18:22)

Maswali na Majibu kuhusu Sala

Sala ni nini?

Sala ni kuinua mioyo yetu kwa Mungu na kuongea nae. Kuongea maana yake ni kusema na Kusikiliza. Sala sio kuongea tuu, sala ni kuongea na kusikiliza. Mungu anatualika tuongee nae kwa kusema na kusikiliza. Kwenye Biblia tunasoma Hivi;
“Niite, nami nitakujibu na kukuambia mambo makubwa yaliyofichika ambayo hujapata kuyajua”.(Yeremia 33:3)
Vile tunavyokuwa na juhudi ya kusali kwa kusema mbele ya Mungu ndivyo hivyo hivyo tunatakiwa tuwe na juhudi ya kumsikiliza Mungu kile anachotuambia.
Tunaweza kumsikiliza Mungu ndani kabisa ya Mioyo yetu, mara nyingine kwa kupitia dhamira zetu, kupitia watu wengine na kupitia neno lake (Biblia). Tuombe neema ya kutambua sauti yake anaposema nasi ili tuweze kumsikiliza na kutengeneza mahusiano mazuri kati yetu na yeye.
Mungu ni Baba yetu, anatupenda sana na yupo tayari kutusikiliza wakati wote ndio maana Mungu anatualika kwa kutuambia;
“Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”. (Isaya 1:18)
Tudumu katika sala daima kwa sababu njia ya sala ndipo tunaweza kusema yale tunayotaka mbele ya Mungu na kusikia yale anayotaka Mungu.


Kwa nini tunasali?

Tunasali ili kudumisha mahusiano yetu na Mungu na ili kutimiza wajibu wetu Mbele ya Mungu. Sababu kuu za kusali ni;
  1. Kumwabudu Mungu,
  2. Kumshukuru Mungu,
  3. Kuomba neema na baraka kwa ajili yetu na wenzetu,
  4. Kuomba msamaha,
  5. Kumsifu na kumtukuza Mungu

1. Kumwabudu Mungu

Tunasali ili kumwabudu Mungu, yaani kumpa heshima ya mwisho juu ya kila kitu. Kuonyesha kuwa ni mkuu na wa kipekee kuliko mtu au kitu chochote.

2. Kumshukuru Mungu

Tunasali ili kumshukuru Mungu kwa yale yote aliyokwisha kuyatenda, anayoyatenda na yale atakayoyatenda. Tunamshukuru Mungu kwa yote kwa kuwa yote anayoyafanya anayafanya kwa Mapenzi/ Matakwa yake Matakatifu. Nia ya Mungu ni njema daima ndio maana tunapoona ameruhusu mambo ambayo kwa akili zetu tunayaona ni magumu na sio mema tunapaswa kushukuru kwa sababu ameyafanya kwa makusudi mema.
Biblia inatuambia hivi;
16 Furahini siku zote; 17ombeni bila kukoma; 18shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. (1 Wathesalonike 5:16-18)
Tunatakiwa kumshukuru Mungu kwa Kila jambo na kumshukuru huku ni kwa njia ya sala.

3. Kuomba neema na baraka kwa ajili yetu na wenzetu

Tunasali kwa kuomaba neema na baraka kwa ajili yetu sisi wenyewe na kwa ajili ya wenzetu. Tunamuomba Mungu baraka na Mkono wake katika yale tunayoyafanya na kwa yale wanayoyafanya wengine.
Maombi yetu ili ykubalike mbele ya Mungu ni lazima yawe katika mapenzi yake na yawe na nia njema. Tunafundishwa hivi katika biblia;
3Tena, mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu. (Yakobo 4:3)
Tunatakiwa tusali kwa kuomba mema na kwa nia njema ili tuweze kupata yale tunayoyaomba kwa Mungu.

4. Kuomba Msamaha

Tunasali ili kuomba msamaha mbele ya Mungu kwa yote mabaya tuliyoyafanya. Mungu ni mwaminifu hasa kwenye kutusamehe na kutuondolea dhambi zetu.
9Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. (1 Yohana 1:9)
Vilevile Tunatakiwa kusali katika mapungufu yetu na kuwa na matumaini.
9Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. (2 Wakorinto 12:9)

6. Kumsifu na kumtukuza Mungu

Tunasali ili kusifu na kumtukuza Mungu. Mungu anapenda kusifiwa na kutukuzwa. Kwa njia ya sifa tunapokea neema na baraka hata ambazo hatujaziomba.
1Mfanyieni BWANA shangwe, dunia yote;
2Mtumikieni BWANA kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba;
3 Jueni kwamba BWANA ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
4Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake;
5 Kwa kuwa BWANA ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (Zaburi 100:1-4)


Nani anapaswa kusali?

Watu wote wanapaswa kusali, wema na wabaya. Sala ndiyo njia pekee ya kumuunganisha Mwanadamu na Mungu. Tunapaswa kusali Katika hali yoyote. Tunapokuwa katika hali ya neema tunapaswa kusali vivyo hivyo tunapokuwa katika hali ya dhambi tunapaswa kusali.
Tunapokuwa katika hali ya neema tunapaswa kusali. Tunasali ili tuweze kudumu katika hali ya neema. Hatupaswi kuacha kusali kama tunajiona hali yetu ya kiroho ipo vizuri. Hatupaswi kuacha kusali kama tumepata neema ya kusimama vyema mbele ya Mungu.
Tunapokuwa katika hali ya dhambi tunapaswa kusali. Tunasali ili tuweze kurudi katika hali ya neema. Hatupaswi kuacha kusali kama tunajiona tupo katika hali ya dhambi. Kwa njia ya sala ndipo tutakapoweza kutoka katika hali ya dhambi.
Mungu yupo tayari kusikiliza ukiwa katika hali ya neema au kama ukiwa katika hali ya dhambi. Ndio maana tunapaswa kumwelekea Mungu katika hali yoyote tulio nayo.
14Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. 15Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. (1 Yohane 5:15)
Tena Mungu anasubiri tumuombe ili furaha yetu itimilike.
24Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu. (Yohane 16:24)
Hata kama tuna dhambi Mungu yupo tayari kutupokea na kutusikiliza.
“Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”. (Isaya 1:18)
Mungu yupo tayari kutusikiliza hata tunapokuwa wadhambi kwa kuwa haziweki dhambi zetu na makosa yetu mbele yetu. Huruma yake ni kubwa kushinda dhambi zetu.
12 Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
13 Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake,
Ndivyo BWANA anavyowahurumia wamchao. (Zaburi 103:12-13)
Mungu anatuwazia mema daima ndio maana tunapaswa kusali kwake
11Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. 12Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. (Yeremia 29:11-13)


Yatupasa kusali lini?

Yatupasa kusali kila siku bila kukata tamaa (Lk 18:1) Sala ndiyo njia pekee ya kutuunganisha na Mungu.
Tunatakiwa tusali daima Kama Yesu alivyotuhimiza kwa mfano huu;
1 Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.
2 Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.
3 Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.
4 Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,
5 lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.
6 Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.
7 Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?
8 Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? 
(Lk 18:1-8)
Kwa hiyo basi, Tusali daima kila siku, kila saa na katika hali yoyote. Tusichoke kusali hata kama maombi Yetu hayajajibiwa. Mungu ni mwenye Hekima na anajua lini hasa akujibu kile unachokiomba kwa manufaa yako wewe. Usipopewa Leo kile ukiombacho unaweza kukipata kwa wakati ufaao tena bila ya Kukiomba.

Sala ni Hazina

Sala ni hazina. Kusali ni kujiwekea hazina. Sala unayosali leo inaweza kukunufaisha wakati usioutarajia.

Maana ya Sala kwa Mkristo Mkatoliki

Maana ya sala kwa Mristu Mkatoliki sio kuomba tuu. Sala kwa Mkatoliki ni zaidi ya kuomba. Kwa Mkatoliki sala inamaanisha kufanya haya;
  1. Tunasali kushukuru,
  2. Tunasali kuomba,
  3. Tunasali kusifu na Kutukuza,
  4. Tunasali kumshirikisha Mungu Furaha zetu na huzuni zetu,
  5. Tunasali kuomba Toba na Msamaha,
  6. Tunasali kumshirikisha Mungu Juhudi zetu na Mipango yetu,
  7. Tunasali kumshirikisha Mungu changamoto zetu.
Tuna kila sababu ya Kusali kila Siku na Kila saa. Maisha yetu yote yanatakiwa yawe Maisha ya Sala. Usifikiri kwamba Wakati wote unaposali lazima utamke maneno Mengi sana ili uwe umesali, Sala haipimwi kwa Maneno. Sala inapimwa kwa nia yake na Kujiweka wazi mbele ya Mungu.
Kila Usalipo Jijengee Tabia ya kunuia, kuwa wazi na kusali kwa ukweli wa Moyo wako. Hata kama ni sentesi Moja fupi Kabisa itamke kwa Upendo na Imani. Kwa Mfano, kuna wakati inatosha kabisa kusema Ee Mungu wangu ninakushukuru kwa hili, hii inaweza kuwa sala Yenye nguvu Kama imetamkwa kwa Imani, Shukrani na Mapendo ya Kweli. Maneno machache yanayotamkwa kwa Imani na Mapendo yanaweza kuzidi Mkesha wa Kusali Usiku Mzima huku unasinzia.
Pamoja na kwamba sala fupi ni nzuri na inafaa sana, kuna haja pia ya kujitengea Muda wa Kutosha Kusali na Kutafakari Huku tukiungana na Mungu. Kila siku tunanye mambo yote mengine lakini tusisahau kuwa Tunahitaji kuwa na Muda wa Kusali.
Tusali daima, Kila wakati na Maisha yetu yawe ni Maisha ya Sala.
Mungu Akubariki sana, Azijibu sala zako na Akujalie Neema ya Kuwa Mtu wa Sala.


Yatupasa kusali namna gani?

Yatupasa kusali kwa Unyenyekevu, Ibada, Matumaini na kwa Saburi. Yesu alitufundisha kuhusu kusali kwa kutumia mfano huu;
9 Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.
10 Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.
11 Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.
12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.
13 Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.
14 Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. 
Luka 18:9-14
Tunatakiwa tusali kwa nia njema na kwa kufuata Mapenzi ya Mungu ili sala zetu zipate kibali mbele za Mungu. Tunapoomba kwa nia mbaya ya tamaa na majivuno hatuwezi kupata kile tukiombacho.
3Tena, mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu. Yakobo 4:3
Mungu anajibu sala zetu kulingana na nia ya kile tunachokiomba. Watu wote waliofanikiwa Katika sala zao walifanikiwa kwa sababu ya nia ya kile walichokiomba.
Sala sio kutamka manano tuu, sala ni kutamka maneno kwa kunuia. Tena tusalipo yatupasa kujua kuwa tunaongea na Mungu na sio tuu kwamba tunatamka maneno. Tusisahau nia kuu ya kusali ambayo ni mawasiliano Yetu na Mungu.
Tunaposali Tunapaswa Kukumbuka na kuzingatia haya;
  1. Nia na Imani (Kuamini na Kuwa na Uhakika na Unachokifanya)
  2. Unyenyekevu wa Kweli
  3. Ibada na Uchaji
  4. Upendo na Uwazi (Honest)
  5. Matumaini na Saburi (Subira)
Kila unaposali jiulize unasali kwa kwa sababu gani? Kila ubapoomba, jiulize unamuomba Mungu ili nini? Sababu yako ndio kibali cha sala yako.
Mungu Akubariki kwa Kukujalia Imani, Unyenyekevu, Ibada, Uwazi na Matumaini Usalipo. Uwe na Amani.


Sala zipo za namna ngapi?

Sala zipo za namna tatu,
1. Sala ya sauti
2. Sala ya fikara
3. Sala ya taamuli


Sala ya Taamuli ni nini?

Sala ya taamuli ni sala ya kumtazama tuu Mungu kwa upendo mkubwa moyoni


Sala ya sauti ni nini?

Sala ya sauti ni sala asaliyo mtu au kundi kwa kutamka maneno


Sala ya fikara ni nini?

Sala ya fikra ni sala asaliyo mtu peke yake au akiwa na wengine kimya kimya akimuwaza Mungu


Sala ya kanisa ni nini?

Sala ya kanisa ni sala maalumu wasaliyo Maklero, Watawa, na Walei kwa ajili ya Kanisa zima


Ni nyakati gani zafaa kwa sala?

Nyakati zote zafaa kwa sala hasa:
1. Asubuhi na jioni
2. Kabla na baada ya kula
3. Kila Dominika
4. Sikukuu za amri
5. Kabla na baada ya kazi
6. Katika kishawishi


Yesu alitufundisha sala gani?

Yesu alitufundisha sala ya Baba Yetu (Mt. 6:9-13)


Je, yatupasa kuombea wengine?

Ndiyo. Yatupasa kuwaombea watu wote hasa wenye shida, wakosefu na hata maadui zetu.


Vyanzo vya sala za Kikristo

Vyanzo vya sala za kikristo ni;
1. Neno la Mungu
2. Litrujia ya kanisa
3. Fadhila za Kimungu
4. Matukio ya kila siku


Je, ni sahihi kusali sala kwa kurudia rudia mfano Novena?

Ndiyo, Hii ni kwa sababu sala nyingi za kurudia ni za Ahadi na zinasaliwa ili kutimiza ahadi ile. Mfano Novena husaliwa kwa siku 7 au 9 kwa nia ya kupata kile kilichoahidiwa au kinachodhamiriwa. Mungu alishawahi kuwaagiza Waisraeli wafanye Ibada maalumu kwa kurudiarudia mfano wakati walipoangusha kuta za Yeriko walifanya Ibada maalumu kwa siku 7 (Saba).
“Waisraeli walipopita waliagizwa na Mungu kuzunguka Mji wa Yeriko 2Kisha BWANA akamwambia Yoshua,“Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na watu wake wa vita. 3Zunguka mji mara moja pamoja na watu wako wote wa vita. Fanya hivi kwa siku sita. 4Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo waume mbele ya sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo. 5Utakaposikia makuhani wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na watu watakwea, kila mtu aingie ndani moja kwa moja kutokea pale alipo.’’ (Yoshua 6:2-5).
Naamani aliambiwa na Nabii Elisha aoge mara saba kwenye mto Yordani ili apone.
14Hivyo akashuka na kujizamisha ndani ya mto Yordani mara saba, kama vile huyo mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia, nayo nyama ya mwili wake ikapona na kutakasika kama ya mwili wa mvulana mdogo. (2 Wafalme 5:14)
Yesu alisali sala ya kurdia rudia kama tunavyosoma,
39Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi akaomba, akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniepuke, lakini si kama nitakavyo mimi bali kama utakavyo Wewe.’’ 40Kisha akarudi kwa wanafunzi wake na kuwakuta wamelala. Akamwuliza Petro, “Je, hamkuweza kukesha pamoja nami kwa saa moja? 41‘‘Kesheni na mwombe, msije mkaanguka majaribuni. Hakika roho iko radhi lakini mwili ni dhaifu.’’ 42Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama ikiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, mapenzi yako yafanyike.’’ 43Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. 44Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale. (Mathayo 26:39-44)

Je ni makosa kurudia sala maneno yale yale kwa Mfano Rozari?

Hapana sio Makosa. Kwa Mfano Biblia inatuambia kuwa Malaika humtukuza Mungu kwa maneno ya kurudia rudia.
“8Kila mmoja wa hawa viumbe wenye uhai wanne, alikuwa na mabawa sita na kujawa na macho pande zote, hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawakuacha kusema: ‘‘Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.’’ (Ufunuo 4:8).
Vile vile tunasoma katika kitabu cha Isaya kuwa malaika walikua wakimsifu na kumtukuza Mungu kwa sala/ maneno ya kurudiarudia. “Katika mwaka ule mfalme Uzia alipokufa, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza hekalu. 2Juu yake walikuwepo maserafi, kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa menngine mawili walifunika miguu yao na kwa mawili walikuwa wakiruka. 3Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ni BWANA Mwenye Nguvu, Dunia yote imejaa utukufu wake.”
Kama Malaika humtukuza Mungu kwa maneno ya kurudia rudia kwa nini sisi tukifanya hivyo tuwe tunakosea? Na sisi tunaweza kumuomba, kumsifu na kumtukuza Mungu kwa sala au maneno ya kurudiarudia kama walivyofanya malaika. Kwa hiyo sala za kurudia rudia sio makosa.
Tukiangalia Zaburi ya 136 inarudia maneno “kwa maana fadhili zake zadumu milele” mara 26 yaani kwenye mistari yake yote. (Zaburi 136:1-26)
Yesu pia allimuomba Mungu Baba kwa kurudia maneno yale yale kama tunavyosoma,
39Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi akaomba, akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniepuke, lakini si kama nitakavyo mimi bali kama utakavyo Wewe.’’ 40Kisha akarudi kwa wanafunzi wake na kuwakuta wamelala. Akamwuliza Petro, “Je, hamkuweza kukesha pamoja nami kwa saa moja? 41‘‘Kesheni na mwombe, msije mkaanguka majaribuni. Hakika roho iko radhi lakini mwili ni dhaifu.’’ 42Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama ikiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, mapenzi yako yafanyike.’’ 43Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. 44Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale. (Mathayo 26:39-44)

Sala kwa Mkatoliki ni nini hasa? Tunaposema sala tunamaanisha nini hasa?

Sala ni kuongea na Mungu. Sala kwa Mkatoliki inajumuisha maombi, tafakari, ibada, taamuli, shukrani na sifa. Maana ya sala kwa Mkristo Mkatoliki sio kuomba tuu kama wanavyotafsiri watu wasio wakatoliki. Wengi wa wasio Wakatoliki wanaposema Sala wanamaanisha Maombi.
Kwa hiyo kwa Mkatoliki, Sala ni zaidi ya Maombi. Ndiyo maana kwa mkatoliki kuna sala za namna mbalimbali kama vile za Tafakari, za Maombi za Sifa na za kushukuru. Mfano sala ya Atukuzwe Baba sio maombi bali ni sala ya kumtukuza Mungu kwa maana hiyo sio Maombi, ndiyo maana husaliwa baada ya sala au matukio fulani kama ishara ya kumtukuza Mungu na kutambua ukuu wa Mungu

Yesu alifundisha tusali vipi?

Kisha Yesu akawapa wanafunzi Wake mfano ili kuwaonyesha kuwa yawapasa kuomba pasipo kukata tamaa.
2Akawaambia, “Katika mji mmoja alikuwapo hakimu ambaye hakumwogopa Mungu wala kumjali mtu. 3Katika mji huo alikuwako mjane mmoja ambaye alikuwa akija kwake mara kwa mara akimwomba, ‘Tafadhali nipatie haki kati yangu na adui yangu.’ Wa Mjane Asiyekata Tamaa 4“Kwa muda mrefu yule hakimu alikataa. Lakini hatimaye akasema moyoni mwake, ‘Japokuwa simwogopi Mungu wala simjali mwanadamu, 5lakini kwa kuwa huyu mjane ananisumbuasumbua, nitahakikisha amepata haki yake ili asiendelee kunichosha kwa kunijia mara kwa mara!’ ” 6Bwana akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu. 7Je, Mungu hatawatendea haki wateule Wake wanaomlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasaidia? 8Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?” (Luka 18:1-8)


Roho Mtakatifu ana nafasi gani katika sala?

Roho Mtakatifu ndiye Mlezi wa ndani wa sala ya Kikristo


Ni ipi sala kubwa ya Kanisa?

Sala kubwa ya Kanisa ni Misa Takatifu


Ni ipi sala bora kwa Bikira Maria? Kwa nini Tunasali kwa Bikira Maria?

Sala bora kwa Bikira Maria ni Rozari Takatifu

Kwa nini watu wengi wanaomba kwa Bikira Maria?

Watu wengi wanaomba kupitia Bikira Maria kwa sababu wanashuhudia sala zao kujibiwa kirahisi zaidi wanaposali kupitia Bikira Maria kwani Bikira Maria anatuombea kile tunacho mwomba. Bikira Maria anasimama Kama mwombezi wetu mbele ya Mungu hasa pale tunaposhindwa kusali Inavyotakiwa.

Bikira Maria anatuombea kwa jina na mamlaka ya nani?

Bikira Maria anatuombea kwa jina la Yesu Kristu na kwa mamlaka ya Yesu Kristu aliye mwanaye. Hakuna Sala yoyote inayotolewa kwa Bikira Maria moja kwa moja kwani Sala zote kwa Bikira Maria zinatolewa kwa kusema utuombee ikimaanisha kuwa utupelekee Maombi yetu kwa Mungu. Bikira Maria hatusaidii sisi moja kwa moja bali anatusaidia kwa kutuombea msaada kutoka kwa Mungu.

Je ni halali au ni sawa kwa Bikira Maria kutuombea kwa Jina la Yesu? Na Je tunajuaje kuwa Bikira Maria anaushirika na Yesu?

Ni halali na nisawa kabisa Bikira Maria kutuombea. Tunajua kuwa Bikira Maria anaushirika na Yesu kwa kuwa Yesu mwenyewe alituambia kuwa “asiyepingana na sisi yupo upande wetu”. Biblia iintuambia…
“Yohane akadakia na kusema “Umemwona Mtu mmoja akifukuza pepo kwa kutumia jina lako, nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa si mmoja wetu.” Lakini Yesu akawaambia, “Msimkataze kwani asiyepingana nanyi yupo upande wenu” (Luka 9:49-50).
Kwa hiyo Bikira Maria anapolitumia jina la Yesu bila kupingana na sisi wala Yesu ni ishara tosha kuwa ni mshirika wa Mungu (Yesu)

Je ni kweli kwamba Bikira Maria ni Malkia wa Kipepo?

Sio kweli kwamba Bikira Maria ni Malkia wa Kipepo/Kishetani
Sababu hizi zifuatazo zinadhihirisha kuwa Bikira Maria sio Malkia wa kipepo;
1) Kuomba kwa jina la Yesu: Angekua ni Malkia wa Kipepo asingeomba kwa Jina la Yesu. Kama ilivyoelezwa hapo juu. Biblia iintuambia linapotamkwa Jina la Yesu mapepo hukimbia. Sasa iweje yeye alitumie Jina hilo kutuombea Kama yeye ni pepo? (Luka 10:17)
2) Hafundishi uovu/dhambi: Mbali na kuomba kwa jina la Yesu, vilevile Yesu alituambia tuzichunguze roho na tutazitambua roho hizo kwa matendo yake. Kwa lengo hili tukichunguza kuhusu Bikira Maria tutaona kuwa Bikira Maria ni Mtakatifu aliye upande wa Mungu kwa sababu Mara zote alipowatokea watu amekuwa akifundisha na kuelekeza watu kuishi maisha ya utakatifu na kumfuata Mungu kweli kwa kutii amri zake na kufuata mafundisho ya mwanae ambayo ni yakuelekea katika utakatifu. Hakuna hata Mara moja mafundisho ya Bikira Maria yalihusishwa na vitendo viovu au vya kuvunja Amri za Mungu.
3) Mafundisho yake yanaendana na Neno la Mungu (Biblia): Bikira Maria hajawaji hata mara moja kufundisha na kuelekeza vitu vilivyo nje ya Mafundisho ya neno la Mungu (Biblia). Hakuna hata Mara moja mafundisho ya Bikira Maria yalikinzana na Mafundisho ya Neno la Mungu.
4) Anahubiri Wema, Unyenyekevu, Upole na Utii: mambo ambayo ni alama ya kudhihirisha Utakatifu.
5) Anasisitiza Upendo kwa Binadamu wenzetu na kwa Mungu: Anahubiri Upendo hasa kwa Maadui zetu na wale wanaoipinga Imani ya Kikristu na wanaomkataa Yesu Kristu. Anasisitiza mara zote Tumpende Mungu na kumtii.
6) Anahubiri Amani: Anahubiri Injili ya Amani na Mara zote anasisitiza tuombe amani ambapo amani ndio Ishara ya Utakatifu.
7) Hajitukuzi mbele ya Mungu bali anajinyenyekesha: Hajawahi kufundisha kwamba tumtukuze yeye au tumuheshimu yeye. Mara zote anahubiri tumheshimu Mungu pekee na kumtukuza Mungu. Amekua akijishusha kwa unyenyekevu huku akituelekeza tuige mfano wake wa unyenyekevu wa kumuelekea Mungu aliye Baba wa huruma na upendo.
8) Anaongeza imani kwa Mungu: Kwa sala na Ibada za Bikira Maria waumini wanapata kuongezewa Imani na Uchaji wao kwa Mungu. Wengi wanabadili maisha yao ya dhambi na kuelekea Maisha mema ya utakatifu ya Kumtumikia Mungu.
9) Sala Ibada yake inachanganyika na Ibada nyingine za Kikristu: Hakuna mgongano/ushindani wa Ibada kwa Bikira Maria na Ibada nyingine za Kikristu. Kama angekua ni pepo kamwe Ibada yake isingechanganyika na Ibada Takatifu.
10) Ibada kwa Bikira Maria Imedumu: Haikufifia wala kupotea bali ilizidi kuendelea vizazi hata vizazi. Hii inadhihirisha kwamba kuna Neema ya Mungu.
Kwa sababu hizi unaweza ukaona kwamba Bikira Maria anaushirika na Mungu na ni Mtakatifu.


Ni zipi sala Muhimu kwa Mkristo?

Sala muhimu kwa Mkristo ni;
1. Misa Takatifu
2. Baraka ya Sakramenti Kuu
3. Litania Takatifu
4. Njia ya Msalaba
5. Rozari Takatifu
6.Novena


Ipi ni shule ya kwanza ya sala?

Familia ni shule ya kwanza ya sala


Mahali gani panafaa kwa sala?

Mtu anaweza kusali mahali popote lakini Kanisani ndipo mahali Rasmi pa sala


Mwenye kusali anakutana na majaribu gani?

Anakutana na Majaribu haya;
1. Mtawanyiko wa Mawazo
2.Ukavu wa moyo
3. Uvivu na Uregevu
Ndiyo maana kwa Wakatoliki sala nyingi zimeandikwa ili kutuongoza hasa tunapokuwa majaribuni katika sala.


Neno “Amina” katika sala lina maana gani?

Neno “Amina” katika sala lina maanisha “Na iwe Hivyo” (Hesabu 5:22)


“Aleluya” katika sala, hasa zaburi ina maana gani?

“Aleluya” katika sala, hasa zaburi ina maanisha “Msifuni Mungu”


Ishara ya msalaba ni nini?

Ishara ya Msalaba ni tendo la mtu kugusa panda la uso, kifua na mabega kwa kutumia mkono wa kulia na kutamka “Kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina”


Kwa kugusa paji la uso tuna maana gani?

Kwa kugusa paji la uso tuna maana ya kukubali kwa akili


Kwa kugusa kifua tuna maana gani?

Kwa kugusa kifua maana yake ni kuupokea na kuukubali msalaba moyoni.


Kwa kugusa mabega tuna maana gani?

Kwa kugusa mabega maana yake ni kuwa tayari kuubeba msalaba kwa nguvu zetu zote


Kwa nini tunafanya Ishara ya Msalaba?

Tunafanya Ishara ya Msalaba kwa nia ya kumkiri Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Pia msalaba ni Ishara ya Ukombozi wetu


Ishara ndogo ya Msalaba juu ya panda la uso, mdomo, na kifua kabla ya Injili ina maana gani?

Maana yake ni kama Ahadi kuwa, Niko tayari kulifahamu Neno la Mungu kwa akili yangu, Nitalitangaza kishujaa kwa Midomo yangu, Nitalipenda na kulishika kwa Moyo wangu wote.


Sala zina faida gani? Kwa nini watu tunasali?

Sala zina faida hizi;
1. Zinaleta neema nyingi
2. Zinatuimarisha ili kushinda vishawishi na dhambi
3. Zinatuunganisha na Mungu
4. Zinatudumisha katika kutenda mema


Mazinguo ndiyo nini?

Mazinguo ni sala za kupungia mashetani ili kuepusha watu na balaa au madhara, hasa kama wamepagawa nao.
“Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu” (Mk 5:8).
“Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena!” (Mk 9:25).
Yesu ameliachia Kanisa mamlaka yake juu yao.
“Aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu” (Mk 6:7).
“Paulo alisikitika, akageuka akamwambia yule pepo, ‘Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu’. Akamtoka saa ileile” (Mdo 16:18).


Ikiwa sala ni maongezi ya Mungu na mtu, kwanza tufanye nini?

Ikiwa sala ni maongezi ya Mungu na mtu, kwanza tumsikilize kwa makini na kutafakari alichosema ili tukifanyie kazi. Tukisema peke yetu si sala, kwa kuwa ukisema upande mmoja tu si maongezi.
“Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia” (1Sam 3:10).
“Nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku” (Zab 63:6).
“Sheria yako naipenda mno ajabu, ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa” (Zab 119:97).
“Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu” (Yer 15:16).


Kielelezo cha sala yetu ni nani?

Kielelezo cha sala yetu ni Yesu Kristo.
“Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, ‘Bwana, tufundishe sisi kusali” (Lk 11:1).
Yeye kama binadamu alichota humo uaminifu kwa wito wake wa pekee.
“Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe” (Yoh 17:1).
“Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe” (Mk 14:36).


Kama binadamu Yesu alijifunza kusali kwa nani?

Kama binadamu Yesu alijifunza kusali kwa Mama yake na kwa mapokeo yote ya Israeli, yaliyojitokeza hasa katika Zaburi.
“Wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu” (Lk 2:41-42).
“Saa tisa Yesu alipaza sauti yake kwa nguvu, ‘Eloi, Eloi, lama sabakthani?’” (Mk 15:34).
“Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu” (Lk 23:46).


Je, sala ya Yesu inatokana na utu wake tu?

Hapana, sala ya Yesu haitokani na utu wake tu, bali katika huo Mwana wa milele ndiye anayemuelekezea Baba yake sala kamili ya kitoto.
“Saa ileile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, ‘Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili, umewafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza” (Lk 10:21).
“Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote” (Yoh 11:41- 42).
“Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo” (Lk 23:34).


Yesu alisali vipi?

Yesu alisali kila mahali na kila wakati, akidumisha ushirika wa upendo kati yake na Baba katika Roho Mtakatifu.
“Saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu” (Yoh 4:23).
Pamoja na kushiriki kiaminifu ibada za taifa lake, mara nyingi alijitafutia mahali pa faragha.
“Aliongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani” (Lk 4:1).
“Alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba” (Lk 5:16).
“Aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu” (Lk 6:12).
Ndiyo sababu ametuambia,
“Wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini” (Math 6:6).
Tusipojua kuongea na Baba moyo kwa moyo, tutawezaje kuongea naye kati ya umati?


Yesu ametufundisha kusali vipi?

Yesu ametufundisha kusali akitueleza misimamo ambayo tuwe nayo.
“Upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako… Waombeeni wanaowaudhi… Msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu” (Math 5:24,44; 6:5).
“Mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipigapiga kifua akisema, ‘Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi’. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki” (Lk 18:13-14).
Hasa ametutia Roho Mtakatifu atuongoze kama alivyomfanyia yeye.


Je, Yesu ametufundisha maneno ya sala pia?

Ndiyo, Yesu ametufundisha maneno ya sala ya ‘Baba Yetu’, kamili kuliko zote. Maombi yake saba yanategemea utangulizi ambao tunamuendea Mungu kwa ujasiri na furaha kama watoto wake, ndugu kati yetu.
Maombi matatu ya kwanza yanalenga atukuzwe, atawale, apate ushirikiano wetu. Maombi manne ya mwisho yanalenga tupate chakula cha roho na cha mwili, msamaha wa dhambi, ushindi katika vishawishi, usalama dhidi ya yule Mwovu.
“Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi…” (Math 6:8-9).


Je, sala inategemea maneno?

Hapana, sala haitegemei maneno mengi mazuri, bali kujijenga
“juu ya imani… na kuomba katika Roho Mtakatifu” (Yud 20).
“Mkiwa katika kusali, msipayukepayuke, kama watu wa mataifa; maana hao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi” (Math 6:7).
Hii haituzuii tusirudie maneno yetu kwa dhati zaidi na zaidi.
Yesu “alikwenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yaleyale” (Math 26:44).
Tunaweza kusali kimoyomoyo pia.
“Hana alikuwa akinena moyoni mwake, midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe… ‘Nimeimimina roho yangu mbele za Bwana’” (1Sam 1:13,15).
“Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako, Ee Bwana” (Zab 19:14).


Je, sala yetu inasikilizwa daima?

Ndiyo, sala yetu inasikilizwa daima kwa kuwa imeunganika kwa imani na ile ya Yesu, njia pekee ya kumuendea Baba.
“Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata, furaha yenu iwe timilifu” (Yoh 16:24).
Lakini Baba, kwa ujuzi na upendo usio na mipaka, anaweza akatupatia mambo tofauti na yale tuliyomuomba.
“Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, ‘Nipe maji ninywe’, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai” (Yoh 4:10).
“Ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je, Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” (Lk 11:13).
Imani yetu ikubali kwamba aliyotupatia ni bora zaidi.


Je, sala inaweza kumuendea Yesu?

Ndiyo, sala inaweza kumuendea Yesu, Bwana wetu na kaka yetu, aliye hai mbinguni, kama ilivyomuendea na kusikilizwa alipokuwa duniani.
Mhalifu alisema,
“‘Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako’. Yesu akamwambia, ‘Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi” (Lk 23:42-43).
Stefano aliomba,
“‘Bwana Yesu, pokea roho yangu’. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, ‘Bwana, usiwahesabie dhambi hii’” (Mdo 7:59-60).
“Roho na Bibi arusi wasema, ‘Njoo!’. Naye asikiaye na aseme, ‘Njoo!’… Na uje, Bwana Yesu!” (Ufu 22:17,20).


Roho Mtakatifu anatusaidiaje kusali?

Roho Mtakatifu anatusaidia tusali kama Yesu, akiwa mlezi wa ndani na kutumia vipaji vyake saba.
“Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’” (Gal 4:6).
“Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa… huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu” (Rom 8:26-27).
Ndiyo sababu Kanisa linatuhimiza tumtamani na kumualika kila mara, ‘Njoo, Roho Mtakatifu!’ yaani kumuomba Baba kwa njia ya Mwana amtume zaidi na zaidi ndani mwetu.


Roho Mtakatifu anaweza kutufikisha hadi wapi?

Roho Mtakatifu anaweza kutufikisha hadi muungano wa dhati na Mungu.
“Yeye awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake, katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” (Ef 3:16-19).
“Huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote” (Yoh 16:13).
Safari hiyo inategemea sana sala isiyoishia katika maneno bali inalenga kupenya mafumbo kwa imani na upendo.


Je, sala inaweza kuwaendea Mama na marafiki wa Yesu (Watakatifu)?

Ndiyo, sala inaweza kuwaendea Mama na marafiki wa Yesu, walioungana naye kuwa mwili mmoja, wasiweze kutenganishwa na chochote.
“Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Rom 8:38-39).
“Kwangu mimi kuishi na Kristo, na kufa ni faida… Ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo” (Fil 1:21,23)
.
Kwa kuwa hao wako na Kristo mbinguni, wanatuombea mfululizo pamoja naye.
“Niliona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, ‘Ee Mwenyezi, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini…’” (Ufu 6:9-10).
Tunawaomba wazidi kutuombea kwa Mungu, kama tunavyowaomba wenzetu waliopo duniani.
“Mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi” (Ef 6:18-19).


Je, Yatupasa kumwomba Roho Mtakatifu?

Ndiyo, kwani twataka kwake maonyo na msaada. Tusipokuwa na neema yake hatuwezi kutenda jambo jema la kufaa kutuokoa. (Yoh 16:13)

Ni nini imani ya Kanisa Katoliki kuhusu maisha ya sala?

Kanisa Katoliki linathamini sana maombi kama sehemu muhimu ya maisha yetu ya kiroho. Imani yetu inatufundisha kuwa kupitia maombi tunawasiliana na Mungu na kuimarisha uhusiano wetu naye. Hii ni kwa sababu tumeumbwa kwa mfano wa Mungu na tunaishi kwa neema yake.

Maombi ni mawasiliano ya moyo na Mungu, ambayo yanatuwezesha kumwomba msamaha kwa dhambi zetu na kupata nguvu za kushinda majaribu. Kwa hivyo, sala ni sehemu muhimu ya maisha ya Kikatoliki na inahitajika kwa maendeleo yetu ya kiroho.

Tunapata mafundisho haya kutoka kwa Yesu mwenyewe, ambaye aliwaambia wanafunzi wake kuwa wasali daima na kutokata tamaa (Luka 18: 1). Katika Yohana 15: 7, Yesu anatuambia kuwa ikiwa tunakaa ndani yake na neno lake linakaa ndani yetu, tunaweza kuomba chochote tunachotaka, na Mungu atatupa.

Kanisa Katoliki pia linatupa mfano wa sala kwa kufundisha kwamba sala ya Bwana ni muhimu sana. Sala hii inatufundisha kumwomba Mungu kwa njia ya kinafiki na kutambua kwamba yeye ndiye muumba wetu. Tunamuomba Mungu kwa mahitaji yetu ya kila siku, pamoja na kupata nguvu za kushinda dhambi.

Katika Catechism ya Kanisa Katoliki, tunaambiwa kuwa sala ya Kanisa ni muhimu sana. Sala hii inaundwa na sala za Wakristo wote na inaunganisha Kanisa kama mwili wa Kristo. Sala hii inatupa nguvu za kuishi maisha ya Kikristo kwa kupata nguvu zetu kutoka kwa Roho Mtakatifu.

Kwa hivyo, kama Wakatoliki, tunahimizwa kuomba kwa nguvu zetu zote na kwa moyo wote. Tunatafuta kumjua Mungu vizuri zaidi na kukuza uhusiano wetu naye kupitia sala. Kwa njia hii, tunaweza kuwa na maisha yenye furaha, amani, na raha ya ndani.

Kwa hiyo, tunakuhimiza, mpendwa msomaji, kuanza maisha ya sala na kujitolea kwa Bwana wetu. Kwa kufanya hivyo, utapata furaha ya kweli na utaishi maisha yenye maana. "Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; pigeni hodi, nanyi mtafunguliwa" (Mathayo 7: 7).

Maswali na Majibu kuhusu Rehema

Rehema ni nini?
Rehema ni msamaha au ondoleo la adhabu ya dhambi tulizostahili sababu ya dhambi zilizokwisha ondolewa

Rehema hutolewa na nani?
Rehema hutolewa na Kanisa Katoliki kwa kutugawia mastahili ya Yesu Kristo, Bikira Maria na Ya Watakatifu

Kuna Rehema za namna ngapi?
Rehema za namna mbili
1. Rehema kamili
2. Rehema pungufu (Rehema isiyo kamili)

Rehema kamili ni nini?
Rehema kamili ni msamaha wa kufutiwa adhabu zote za muda za dhambi

Rehema isiyo kamili (pungufu) ni nini?
Rehema isiyo kamili (pungufu) ni msamaha wa kupunguziwa adhabu ya dhambi

Adhabu za dhambi huondolewa kwa namna gani? Jinsi ya kupata rehema
Adhabu za dhambi huondolewa kwa;
1. Kufanya malipizi au majuto kamili
2. Kuvumilia taabu na mateso katika maisha
3. Kuvishinda vishawishi na majaribu
4. Kusali sala mbalimbali
5. Kuomba Misa kwa ajili hiyo.
6. Kusoma neno la Mungu na kulitafakari na kulinganisha na maisha yetu ya kila siku
7. Utakaso wa Toharani kama adhabu hizi hazikuondolewa duniani

Kipimo cha Rehema ni nini?
Kipimo cha Rehema hutegemea uzito wa majuto na mapendo mtu aliyonayo kwa Mungu Muumba wake. (1Kor 9:11)

Mtu akitaka kupata Rehema za Kanisa Katoliki yampasa nini?
Mtu akitaka kupata Rehema za Kanisa Katoliki yampasa;
1. Kujua na kufuata utaratibu unaotolewa na Kanisa Katoliki wa kupata Rehema
2. Awe katika hali ya neema ya Utakaso
3. Kufanya matendo yote yanayotakiwa kwa kupata rehema hiyo, kwa mfano;
a). Hija au Kuhiji katika mwaka wa Jubilei katika Kanisa lililo teuliwa na Askofu
b). Kufanya mafungo – Kama vyama vya kitume
c). Kuzuru makaburi (Kutembelea) yaliyobarikiwa
d). Katika hatari ya kufa padri hutoa rehema pamoja na Sakramenti ya wagonjwa
e). Kusali kwa nia za Baba Mtakatifu
Shopping Cart
31
    31
    Your Cart
    Kitabu cha SMS Maalumu kwa Umpendaye
    Kitabu cha SMS Maalumu kwa Umpendaye
    1 X Sh2,500 = Sh2,500
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About