Mafundisho ya Katekisimu

Maswali na Majibu kuhusu Marehemu

Ufufuko wa wafu maana yake nini?

Ufufuko wa wafu maana yake mwisho wa dunia watu wote watafufuka na miili yao na kwenda nayo katika furaha ya milele au moto wa milele. (Ayu 19:25-26, Mt 22:30-32, Yh 28-29)


Baada ya kifo cha mtu nini hutokea?

Baada ya kifo roho yake inafika mbele ya Mungu kwa hukumu ya mtu binafsi.


Matokeo ya hukumu hiyo ni nini?

Matokeo ya Hukumu hiyo ni roho kwenda Mbinguni, Toharani au Motoni. (Mt 25:34-46)


Mbinguni ni mahali pa namna gani?

Mbinguni ni makao mema ya heri na furaha (2Kor 5:1, Ufu, 2:17).
Waendao mbinguni ni wale wanaokufa katika hali ya neema ya utakaso na urafiki na Mungu na waliotakaswa kikamilifu


Motoni ni nini?

Motoni ni makao mabaya kwa Shetani walaaniwa wakaapo mbali na Mungu wakiteswa milele. (Mt 25:41, Mik 9:42-43, 1Yoh 14:15)


Uzima wa milele ni nini?

Uzima wa milele ni maisha ya kukaa mbinguni na Mungu yasiyokua na mwisho.


Toharani ni mahali gani?

Toharani ni mahali pa mateso zinakosafishwa roho ambazo hazikutimiza kitubio vizuri baada ya kuungama dhambi. (1Kor 3:15, 1Pet 1:7).


Je, hatuwezi kupunguza mateso ya roho za marehemu waliokwenda toharani?

Ndiyo: twaweza kupunguza hata kuyamaliza kwa kuwasalia na kuwapatia rehema na hasa kwa kuadhimisha Misa kwa ajili yao. (2Mik 12:38-46)


Mambo makuu manne ya mwisho ni yapi?

Mambo hayo ni;
1. Kifo
2. Hukumu
3. Jehanamu (Motoni)
4. Paradiso. (Toharani/Mbinguni)


Je, ufufuko wa Yesu ni muhimu kwetu pia?

Ndiyo, ufufuko wa Yesu ni muhimu kwetu pia, kwa sababu kwa njia yake tu tunatiwa uzima: sasa rohoni kwa kuondolewa dhambi, na siku ya mwisho mwilini pia kwa kufufuliwa.
Mwenyewe alisema, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele” (Yoh 11:25- 26).
“Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu” (1Kor 15:20-21).
“Alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuka ili tupate kuhesabiwa haki” (Rom 4:25).


Je, ni muhimu tujiandae kufa?

Ndiyo, ni muhimu tujiandae kufa wakati wowote na namna yoyote kwa kuishi kitakatifu sasa na kwa kujiombea neema tutakazohitaji saa ya kufa kwetu, tukijua tumewekewa “kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu” (Eb 9:27).
“Katika mambo yako yote uukumbuke mwisho wako, hivyo hutakosa kamwe hata hatima” (YbS 7:36).
“Hamjui yatakayokuwako kesho! Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka” (Yak 4:14).
“Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni” (Math 26:41).


Je, ina thamani machoni pa Bwana mauti ya mtu aliyemcha?

Ndiyo, “ina thamani machoni pa Bwana mauti ya wacha Mungu wake” (Zab 116:15).
Hasa utiifu wa Yesu msalabani umegeuza laana ya kifo iwe baraka kwa waamini wake.
“Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao” (Ufu 14:13).


Tutakapofariki dunia itatutokea nini?

Tutakapofariki dunia roho yetu isiyokufa, mbali na mwili unaooza, itapewa tuzo au adhabu tuliyostahili kwa maisha yetu. “Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake” (Lk 16:22-23). “Kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida… ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo, maana ni vizuri zaidi sana” (Fil 1:21,23). “Nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana” (2Kor 5:8). Kwa kuwa kifo ni “mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa” (Mhu 12:7). Siku ya ufufuo roho na mwili vitaungana tena kwa ajili ya uzima au moto wa milele. “Pumzi iliwaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno” (Ez 37:10).

Je baada ya kufa ni hapo hapo roho inaenda motoni au mbinguni, Au ni mpaka Siku ya hukumu Yesu Atakaporudi?

Ni siku ile ile Roho ya mtu aliyekufa inaenda Mbinguni, toharani au Motoni. Yesu alimwahidi yule mtu waliyesulubiwa pamoja kuwa watakuwa peponi pamoja siku hiyo hiyo na sio siku ya hukumu.
“Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.” 43 Yesu akamwambia, “Nakwambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.” (Luka 23:42-43)
Sauli aliweza kuongea na Samweli hata baada ya kufa na Samweli alimbashiria mambo yatakayotokea kwa Sauli maanake ni kwamba Japokuwa alikuwa amekufa bado anayomuungano na Mungu ndio maana aliweza kumwambia Sauli mambo yatakayompata,
“7Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi ili nimwendee nipate kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, “Yuko mwanamke mmoja huko Endori.” 8Hivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie na unipandishie huyo nitakayekutajia,” 9Huyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya mfalme Sauli. Amewakatilia mbali wapunga pepo, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?” 10Sauli akamwapia huyo mwananmke kwa Jina la BWANA, akasema, “Kwa hakika kama BWANA aishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.” 11Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani? Sauli akasema, “Nipandishie Samweli.” 12Yule mwanamke alipomwona Samweli alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamwuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.” 13Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini? Yule mwanamke akasema, “Naona Mungu anapanda kutoka ardhini.” 14Sauli akamwuliza, “Ni mfano wa nini?” Yule mwanamke akasema, “Ni mwanaume mzee amevaa joho anayepanda.” Ndipo Sauli akatambua kwamba ni Samweli. Sauli akasujudu kifudifudi uso wake hadi ardhini. 15Samweli akamwuliza Sauli, Kwa nini unanitaabisha, kunipandisha juu?” Sauli akasema, “Mimi ninasumbuka sana, kwa maana Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, naye Mungu ameniacha. Hanijibu tena wala kwa njia ya manabii wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita wewe ili unijulishe lakufanya.” 16Samweli akamwuliza, “Kwa nini uniulize mimi, maadam BWANA amekuacha na kuwa adui yako? 17BWANA ametenda lile alilotangulia kusema kwa kupitia kwangu. BWANA ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, naye amempa mmoja wa jirani zako, yaani, Daudi. 18Kwa sababu wewe hukumtii BWANA, wala hukumtimizia ghadhabu yake kali juu ya Waamaleki, BWANA amekutendea mambo haya leo. 19Zaidi ya hayo, BWANA atawatia Israeli pamoja na wewe mkononi mwa Wafilisti na kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. BWANA pia atalitia jeshi la Israeli mkononi mwa Wafilisti.
Mfano Wa Tajiri Na Maskini Lazaro Yesu alisimulia hivi
19 Akasema, “Palikuwa na tajiri mmoja aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, nguo za gharama kubwa, kila siku. 20 Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima, alikuwa akiletwa mlangoni kwa huyo tajiri kila siku. 21 Lazaro alikuwa akitamani kula makombo yaliyodondoka mezani kwa tajiri. Hata mbwa walikuwa wakiramba vidonda vyake. 22 “Hatimaye, yule maskini alikufa. Malaika wakamchukua akakae pamoja na Ibrahimu mbinguni. Yule tajiri naye pia akafa, akazikwa. 23 Alipokuwa kuzimuni ambapo alikuwa akiteseka, alita zama juu, akamwona Ibrahimu kwa mbali na Lazaro karibu yake. 24 Akaita, ‘Baba Ibrahimu, nionee huruma umtume Lazaro achovye japo ncha ya kidole chake katika maji aupoze ulimi wangu maana ninateseka kwenye moto huu.’ 25 Lakini Ibrahimu akamjibu, ‘Mwa nangu, kumbuka kwamba ulipokuwa hai ulipata kila kitu kizuri uli chotaka, ambapo Lazaro alipokea mabaya. Lakini sasa anafarijika hapa na wewe unateseka. 26 Isitoshe, kati yetu na ninyi huko, kumewekwa bonde kubwa lisilopitika ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko au kutoka huko kuja huku wasiweze.’ 27 Akasema, ‘Basi, baba, tafadhali umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu, 28 awaonye ndugu zangu, wasije wao pia wakaletwa mahali hapa pa mateso watakapokufa.’ 29 Ibrahimu akamjibu, ‘Ndugu zako wanazo sheria za Musa na maandiko ya Manabii. Itawapasa watii hayo.’ Lakini yule tajiri akazidi kumsihi, 30 ‘Hapana baba Ibrahimu, ndugu zangu hawatashawishiwa na hayo. Lakini mtu kutoka kuzimu akitumwa kwao watatubu na kuziacha dhambi zao.’ 31 “Ibrahimu akamwambia, ‘Wasiposikiliza na kutii sheria za Musa na Maandiko ya manabii, hawatashawishika kutubu hata kama mtu akifufuka kutoka kuzimu.”’ (Luka 16:19-31)
Wakati Yesu anabadilika Sura walitokea Musa na Eliya.
“Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane nduguye, akaenda nao peke yao juu ya mlima mrefu. 2 Huko, wakiwa wanamtazama, akageuka sura, uso wake ukang’aa kama jua na mavazi yake yakawa meupe kama nuru. 3 Mose na Eliya wakawatokea, wakawa wanazungumza naye. 4 Hapo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri sana kwamba tupo hapa! Ukipenda nitajenga vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya.” (Mathayo 17:1-5)
Yesu alituambia kuwa Mungu sio wa wafu bali wa walio hai ndio maana akaitwa Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo kwa kuwa Wote wako hai kwake.
37Hata Mose alidhihirisha kuwa wafu wanafufuka, kwa habari ya kile kichaka kilichokuwa kikiwaka moto bila keteketea, alipomwita Bwana ‘Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki na Mungu wa Yakobo.’ 38Yeye Mungu si Mungu wa wafu bali wa walio hai, kwa kuwa Kwake wote ni hai.” (Luka 20:37-38)
Yesu alimwahidi yule mtu waliyesulubiwa pamoja kuwa watakuwa peponi pamoja siku hiyo hiyo na sio siku ya hukumu.
“Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.” 43 Yesu akamwambia, “Nakwambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.” (Luka 23:42-43)
Angalia pia wakati Stefano akipigwa Mawe aliikabidhi roho yake kwa Mungu baada ya kuona mbingu zimefunguka hii ni kama Yesu alivyokuwa pale msalabani aliikabidhi Roho yake kwa Baba yake.
55Lakini yeye Stefano akiwa amejazwa Roho Mtakatifu, alikaza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu, naye Yesu akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu. 56Akasema, “Tazameni! Naona mbingu zimefunguka na Mwana wa Adamu amesimama upande wa kuume wa Mungu.’’ 57Lakini wao wakapiga kelele kwa sauti kubwa, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja. 58Wakamtupa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni mwa kijana mmoja aitwae Sauli. 59Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu” 60Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.’’ Baada ya kusema haya, akalala. (Mdo 7:55-60)
Kwenye Ufunuo tunasoma (Ufunuo 6:9-10) “Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi? Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vile vile kama wao.”
Kwa hiyo mtu akifa anaenda mbinguni au motoni kulingana na alivyoishi.
“Nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana” (2Kor 5:8). Kwa kuwa kifo ni “mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa” (Mhu 12:7).
Siku ya ufufuo roho na mwili vitaungana tena kwa ajili ya uzima au moto wa milele.
“Kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida… ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo, maana ni vizuri zaidi sana” (Fil 1:21,23).
Mtume Petro ameandika hivi…
“18 Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa,19 ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri; 20 watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji.” (1Petro 3:18-20)


Je, sisi wanyonge tunaweza kushiriki uzima wa milele wa Mungu?

Ndiyo, sisi wanyonge tunaweza kushiriki uzima wa milele wa Mungu: hapa duniani katika mwanga hafifu wa imani, na kisha kufa katika uangavu wa utukufu usiofifia kamwe. Kwa kuwa lengo la Baba ni kwamba tuungane na Yesu Mwanae kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ili tuwe na utukufu wake.
“Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yoh 17:3).
“Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa” (2Pet 1:3-4).
Sisi tuliobatizwa tunaitwa “wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo!” (1Yoh. 3:1).
Kwa sababu tumesadiki kwamba “Mungu ni upendo” (1Yoh 4:8) na kwamba “hakuna lisilowezekana kwa Bwana” (Lk 1:37).
“Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’ Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu” (Gal 4:6-7).


Aliyezungumzia moto wa milele ni nani?

Aliyezungumzia moto wa milele ni hasa Yesu: akitufunulia ukuu wa upendo wa Mungu, aliye heri yetu pekee, alituangalisha juu ya hatari ya kutengana naye milele kwa dhambi. Mwenyewe atatoa hukumu hiyo:
“Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake” (Math 25:41).
“Humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki” (Mk 9:48).
“Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku” (Ufu 14:11).


Toharani maana yake nini?

Toharani maana yake kuna hali ya muda ambayo huruma ya Mungu inawatakasa marehemu waliofariki dunia katika urafiki naye lakini bila ya usafi kamili unaotakiwa kwa kuingia mbinguni. Sisi tunaweza kuharakisha utakaso wao kwa kumtolea Mungu sala na sadaka, hasa ekaristi. Yuda Mmakabayo “alichanga fedha kwa kila mtu jumla drakma elfu mbili, akazipeleka Yerusalemu kutoa sadaka ya dhambi.
Kwa kufanya hivi alitenda vema na kwa haki, kwa kuwa aliukumbuka ufufuo wa wafu. Maana kama asingalitumaini ya kuwa wale waliokufa watafufuka, ingalikuwa kazi bure isiyo na maana kuwaombea wafu. Lakini kwa kuwa aliufikiri utukufu wa thawabu waliowekewa wale wafao katika utauwa, wazo lake lilikuwa takatifu na la kicho. Ndiyo sababu alifanya upatanisho kwa wafu ili wafunguliwe dhambi zao” (2Mak 12:43-46). Imani hiyohiyo iliongoza Wakristo wa kwanza kuwafanyia marehemu ibada ambayo haieleweki vizuri, lakini hailaumiwi na Mtume Paulo: “Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao?” (1Kor 15:29).


Je, mwili utakaofufuliwa ni huuhuu tulionao sasa?

Ndiyo, mwili utakaofufuliwa ni huuhuu tulionao sasa, lakini katika hali tofauti: > “hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika” (1Kor 15:42).
Siku ya ufufuo “ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi” (Lk 21:27).
“Saa yaja ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuko wa uzima, na waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu” (Yoh 5:28-29).
“Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele” (Math 25:46).


Siku ya ufufuo Kristo mfalme atatuhukumu vipi?

Siku ya ufufuo Kristo mfalme atatuhukumu kwa kudhihirisha misimamo ya watu wote ambao, kwa kupokea au kukataa upendo wa Mungu moyoni mwao, wametenda mema au la.
“Imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyopenda, kwamba ni mema au mabaya” (2Kor 5:10).
“Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu” (1Kor 4:5).
“Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake. Na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, ‘Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia… Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi’” (Math 25:31-36,40).
“Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema” (Math 5:7).


Baada ya hukumu ya mwisho itakuwaje?

Baada ya hukumu ya mwisho, waadilifu watatukuzwa mwili na roho pamoja na Yesu, na ulimwengu pia utageuzwa.
“Kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake” (2Pet 3:13).
“Na Roho na Bibi arusi wasema, ‘Njoo!’ naye asikiaye na aseme, ‘Njoo!’… Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, ‘Naam, naja upesi’. Amina. Na uje, Bwana Yesu! Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina” (Ufu 22:17,20-21).


Kanisa linaheshimu marehemu kwa namna gani?

Kanisa linaheshimu marehemu kwa kuwafanyia mazishi huku likiwaombea kwa Mungu.
“Watu watauwa walimzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu” (Mdo 8:2).
Yeye kama mfiadini, aliyefikia upeo wa upendo kwa kutoa uhai wake, hakuhitaji kuombewa. Lakini wafu wengine walitolewa sala na sadaka tangu Israeli ilipoanza kusadiki ufufuo.
“Kama asingalitumaini kuwa wale waliokufa watafufuka, ingalikuwa kazi bure isiyo na maana kuwaombea wafu. Lakini kwa kuwa aliufikiri utukufu wa thawabu waliowekewa wale wafao katika utauwa, wazo lake lilikuwa takatifu na la kicho. Ndiyo sababu alifanya upatanisho kwa wafu ili wafunguliwe dhambi yao” (2Mak 12:44-46).
“Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao?” (1Kor 15:29).

Maswali na Majibu kuhusu Rehema

Rehema ni nini?
Rehema ni msamaha au ondoleo la adhabu ya dhambi tulizostahili sababu ya dhambi zilizokwisha ondolewa

Rehema hutolewa na nani?
Rehema hutolewa na Kanisa Katoliki kwa kutugawia mastahili ya Yesu Kristo, Bikira Maria na Ya Watakatifu

Kuna Rehema za namna ngapi?
Rehema za namna mbili
1. Rehema kamili
2. Rehema pungufu (Rehema isiyo kamili)

Rehema kamili ni nini?
Rehema kamili ni msamaha wa kufutiwa adhabu zote za muda za dhambi

Rehema isiyo kamili (pungufu) ni nini?
Rehema isiyo kamili (pungufu) ni msamaha wa kupunguziwa adhabu ya dhambi

Adhabu za dhambi huondolewa kwa namna gani? Jinsi ya kupata rehema
Adhabu za dhambi huondolewa kwa;
1. Kufanya malipizi au majuto kamili
2. Kuvumilia taabu na mateso katika maisha
3. Kuvishinda vishawishi na majaribu
4. Kusali sala mbalimbali
5. Kuomba Misa kwa ajili hiyo.
6. Kusoma neno la Mungu na kulitafakari na kulinganisha na maisha yetu ya kila siku
7. Utakaso wa Toharani kama adhabu hizi hazikuondolewa duniani

Kipimo cha Rehema ni nini?
Kipimo cha Rehema hutegemea uzito wa majuto na mapendo mtu aliyonayo kwa Mungu Muumba wake. (1Kor 9:11)

Mtu akitaka kupata Rehema za Kanisa Katoliki yampasa nini?
Mtu akitaka kupata Rehema za Kanisa Katoliki yampasa;
1. Kujua na kufuata utaratibu unaotolewa na Kanisa Katoliki wa kupata Rehema
2. Awe katika hali ya neema ya Utakaso
3. Kufanya matendo yote yanayotakiwa kwa kupata rehema hiyo, kwa mfano;
a). Hija au Kuhiji katika mwaka wa Jubilei katika Kanisa lililo teuliwa na Askofu
b). Kufanya mafungo – Kama vyama vya kitume
c). Kuzuru makaburi (Kutembelea) yaliyobarikiwa
d). Katika hatari ya kufa padri hutoa rehema pamoja na Sakramenti ya wagonjwa
e). Kusali kwa nia za Baba Mtakatifu

Je, Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha umuhimu wa kuheshimu uhuru wa dini na kukuza uelewa na amani kati ya dini mbalimbali?

Je, Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha umuhimu wa kuheshimu uhuru wa dini na kukuza uelewa na amani kati ya dini mbalimbali? Ndio! Kanisa Katoliki linapenda kuhimiza kila mtu kuheshimu uhuru wa dini na kuheshimu imani ya wengine, na kukuza uelewa na amani kati ya dini mbalimbali. Kama Wakatoliki, tunapaswa kuwa mfano wa amani na upendo kwa wengine, hata kwa wale ambao hawana imani yetu.

Katika Injili, Yesu Kristo alipenda kutangaza amani na upendo kwa kila mtu. Yeye alisema katika Mathayo 5:9 "Heri wenye amani, kwa kuwa wao watapewa na Mungu jina lao la kuwa wana." Hii inaonyesha jinsi Mungu anavyopenda amani na upendo, na hivyo tunapaswa kuwa wakazi waadilifu wa dunia hii, wakipenda amani na kuheshimu wengine.

Kanisa Katoliki linafundisha kuwa kila mtu ana haki ya uhuru wa dini na kukubaliwa kwa imani yake, bila kujali ni dini gani. Hii inamaanisha kwamba kila mtu anapaswa kuheshimiwa kwa imani yake na kuheshimu imani ya wengine. Wakatoliki tunapaswa kuwa na heshima ya wengine, hata kama kuna tofauti za kidini.

Kanisa Katoliki linapendekeza kwamba sisi sote tunapaswa kuchangia katika kukuza uelewa na amani kati ya dini mbalimbali. Hii inaweza kufanywa kwa njia ya majadiliano, kutembeleana, na kushirikiana kwa malengo mema. Kwa mfano, tunaweza kuwaalika wenzetu wa dini nyingine kwa misa zetu au hata kushiriki katika shughuli za kijamii na za kimaendeleo.

Kanisa Katoliki linasema pia katika Catechism of the Catholic Church kwamba "uhuru wa dini unahusisha haki ya kila mtu ya kufuata dhamiri yake katika mambo yote yanayohusiana na dini" (CCC 2106). Hii ni sehemu ya haki ya binadamu ambayo inapaswa kulindwa kote ulimwenguni. Kwa hiyo, kama Wakatoliki, tunapaswa kuongoza kuwa mfano wa kulinda haki hii ya binadamu.

Katika Wagalatia 5:13, Paulo anasema "Kwa maana ninyi, ndugu, mliitwa kwa ajili ya uhuru; lakini msitumie uhuru wenu kuwa sababu ya kufanya mambo maovu, bali tumikianeni kwa upendo." Hii inaonyesha kwamba uhuru unapaswa kutumika kwa njia ya upendo na kuheshimu wengine. Tunapaswa kutumia uhuru wetu kwa kusaidiana kwa upendo na kuheshimiana wengine.

Mwisho, tunahitaji kuwa na ufahamu wa kutosha juu ya dini mbalimbali. Kwa kweli, tunapaswa kujua imani yetu kwa undani, lakini pia tunapaswa kuelewa imani za wengine. Hii itatusaidia kuheshimu imani ya wengine na kuwa mfano wa amani na upendo.

Kwa hiyo, tunapaswa kuheshimu uhuru wa dini na kuheshimu imani ya wengine, kukuza uelewa na amani kati ya dini mbalimbali, na kuwa mfano wa upendo na amani kwa wengine. Neno la Mungu linasema, "Bwana wa amani mwenyewe awape amani kwa njia zote. Bwana na awe pamoja ninyi nyote" (2 Wathesalonike 3:16).

Je, Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha Ndoa kama sakramenti ya agano la upendo na uaminifu?

Je, Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha Ndoa kama sakramenti ya agano la upendo na uaminifu?

Ndio, Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha Ndoa kama sakramenti ya agano la upendo na uaminifu. Kwa mujibu wa kanuni za Kanisa Katoliki, ndoa ni sakramenti ambayo inawezeshwa na Mungu kwa ajili ya wawili wanaokubali kwenda pamoja kwa maisha yao yote. Ndoa ina maana kubwa sana kwetu sote, kwani ni wakati ambapo tunaahidi kuwa na mtu mwingine maisha yetu yote.

Kama vile Kristo alivyohusisha sakramenti yake ya mwili na damu yake na Wakristo wake, vivyo hivyo ndoa inahusisha sakramenti ya upendo na uaminifu kati ya wawili wanaotaka kuwa pamoja maisha yao yote. Ndoa ina lengo la kuleta furaha, amani, na upendo kwa wawili hao, na kuunda familia ambayo inaishi kwa upendo na amani.

Ndoa ina thamani kubwa sana kwa Mungu, na ndio maana inahusishwa na agano la upendo na uaminifu. Katika agano hili, wawili wanakubali kuwa pamoja maisha yao yote, na kuahidi kuwa waaminifu kwa kila mmoja, kushirikiana katika matatizo na furaha, na kujenga familia ambayo inaishi kwa upendo na amani.

Katika Biblia, tunaona jinsi ndoa inavyopewa umuhimu mkubwa. Kwa mfano, katika Mwanzo 2:24, tunasoma "Kwa hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja." Hii inaonyesha jinsi Mungu alivyokusudia ndoa iwe kitu cha maana sana katika maisha yetu.

Kwa mujibu wa Catechism ya Kanisa Katoliki, ndoa ina maana kubwa sana kwetu sote. Inasema kuwa ndoa ni "umoja wa maisha ya wanaume na wanawake, ambao unawekwa na Mungu mwenyewe, na ambao unapatikana kwa njia ya kujitolea kwa kila mmoja na kwa ajili ya ajili ya watoto." (Catechism ya Kanisa Katoliki, 1601).

Kanisa Katoliki linahubiri na kufundisha Ndoa kama sakramenti ya agano la upendo na uaminifu kwa sababu inajua jinsi muhimu ndoa ni katika maisha yetu. Ndoa inatuletea furaha, amani, na upendo, na inatufanya tuishi kwa amani na upendo na wale tunaowapenda. Tunapofuata kanuni za Kanisa Katoliki, tunaweza kuishi kwa amani na upendo na wale tunaowapenda, na kusaidia kujenga familia ambayo inaishi kwa upendo na amani.

Ni nini imani ya Kanisa Katoliki kuhusu upendo na huruma?

Karibu kwenye makala yangu kuhusu imani ya Kanisa Katoliki kuhusu upendo na huruma. Katika kanisa Katoliki, upendo ni jambo muhimu sana katika maisha yetu ya Kikristo. Kulingana na Biblia, Mungu ni upendo na ametualika sisi sote tuweze kuishi kwa upendo (1 Yohana 4:8).

Kanisa Katoliki linatueleza kuwa upendo ni kitu ambacho kinatoka kwa Mungu na kinapaswa kuongoza maisha yetu. Tunapaswa kuwapenda wenzetu kama tunavyojipenda wenyewe (Marko 12:31). Kwa hivyo, Kanisa Katoliki linatufundisha kufurahia upendo wa Mungu na kuwa na upendo kwa jirani yetu.

Katika kufuata njia ya upendo, Kanisa Katoliki pia linatufundisha kuhusu huruma. Huruma ni tendo la upendo ambalo linatupatia fursa ya kuonyesha upendo huo kwa wengine. Kama vile Mungu alivyotupatia huruma na msamaha kupitia Yesu Kristo, tunaweza pia kuwa na huruma kwa wengine.

Kwa kufuata kanuni za Kanisa Katoliki, tunapaswa kujitolea kwa wengine na kuwa tayari kuwasaidia wakati wanapohitaji msaada. Kwa kufanya hivyo, tunakuwa chombo cha upendo na huruma ya Mungu katika ulimwengu huu.

Kanisa Katoliki pia linatufundisha kuwa na huruma kwa wale wanaohitaji. Kama vile Yesu Kristo alivyowaonyesha huruma wenye shida, tunapaswa kuwa tayari kuwasaidia wale wanaohitaji msaada wetu. Kwa kufanya hivyo, tunakuwa vyombo vya upendo na huruma ya Mungu katika maisha yetu.

Kanisa Katoliki linatufundisha kuwa na huruma pia kwa wale ambao wametukosea. Kama vile Mungu alivyotupatia msamaha wetu kupitia Yesu Kristo, tunapaswa kuwa tayari kuwasamehe wale ambao wametukosea. Kwa kufanya hivyo, tunakuwa vyombo vya upendo na huruma ya Mungu katika ulimwengu huu.

Kwa kumalizia, Kanisa Katoliki linatueleza kuwa upendo na huruma ni muhimu sana kwa maisha yetu ya Kikristo. Kwa kufuata njia ya upendo na huruma, tunakuwa vyombo vya upendo na huruma ya Mungu katika ulimwengu huu. Kwa hivyo, tunapaswa kuwa tayari kuwa na upendo na huruma kwa wengine katika maisha yetu ya kila siku. Kama vile Catechism ya Kanisa Katoliki inatueleza, "Upendo ni roho ya maisha ya Kikristo".

Amri ya nne ya Mungu: Kuheshimu Wazazi

Katika Amri ya nne ya Mungu tumeamriwa nini?

Tumeamriwa tuwaheshimu wazazi wetu na wakubwa wetu wote, tuwapende, tuwatii na tuwaombee. (Kut 20:12, Kol 3:20)


Amri ya Nne ya Mungu tumeamriwa nini?

Tumeamriwa tuwaheshimu wazazi wetu na wakubwa wote, tuwapende, tuwatii na tuwaombee. (Kut 20:12), Kol 3:20


Kwa sababu gani yatupasa kuwaheshimu Baba na Mama?

Yatupasa kuwaheshimu Baba na Mama kwa sababu;

1. Wameshirikiana na Mungu kutuleta duniani walipotuzaa
2. Wamewekwa na Mungu ili watulee na kutuongoza Mbinguni
3. Mungu ameamuru tuwapende wazazi mara baada ya Yeye. (Ayu 3:1-9)


Wazazi na wakubwa wameamriwa nini?

Wazazi na wakubwa wameamriwa watutunze na kutulea


Tuwaheshimu Baba na Mama kwa matendo gani?

Tuwaheshimu Baba na Mama kwa matendo ya adabu, heshima, utii na mapendo (Ayu 3:12)


Twawakosea Heshima Baba na Mama kwa kufanya nini?

Twawakosea Heshima Baba na Mama kwa;

1. Tukiwakasirisha na kuwatukana
2. Tukiwakaidi na kuwapiga
3. Tukiacha kuwaombea
4. Tukiacha kuwasaidia katika shida na uzee. (Kut 21:15-17)


Wazazi wawaleeje watoto wao katika imani ya Kikristo?

Wawalee hasa kwa mfano wao, kwa sala, kwa katekesi ya kifamilia na kushiriki maisha ya Kanisa


Lini tunakatazwa kuwatii watu?

Tunakatazwa kuwatii watu wanaotuamuru jambo lililokatazwa na Mungu (Mdo 5:29)


Katika Amri ya Nne ya Mungu tumekatazwa nini?

Tumekatazwa haya;

1. Kukaidi wazazi na wakubwa wetu
2. Kuwakasirisha.
3. Kuwadharau.


Wakubwa tunaopaswa kuwaheshimu ni kina nani?

Wakubwa hao ni;

1. Viongozi wa Kanisa
2. Viongozi wa Serikali
3. Walimu na walezi
4. Wakubwa wa kazi (War 13:1)
5. Viongozi wa Jumuiya

Je, Kanisa Katoliki linakiri na kufundisha amri kumi za Mungu kama mwongozo wa maisha ya Kikristo?

Je, Kanisa Katoliki linakiri na kufundisha amri kumi za Mungu kama mwongozo wa maisha ya Kikristo? Ndio, Kanisa Katoliki linakiri na kufundisha amri kumi za Mungu kama mwongozo wa maisha ya Kikristo. Amri hizi ni kanuni za msingi za maisha ya Kikristo na zinapaswa kufuatwa na Wakristo wote. Kwa kufuata amri hizi, Wakristo wanaweza kuishi maisha yao kwa kufuata mapenzi ya Mungu.

Katika Agano la Kale, Mungu alitoa amri kumi za kufuata kwa watu wake. Amri hizi zilikuwa na lengo la kuwafundisha watu wake jinsi ya kuishi maisha yao kwa kumtii Mungu. Amri hizi zilikuwa ni mwongozo wa maisha ya Kikristo na zinabaki kuwa ndivyo hadi leo.

Katoliki inafundisha kuwa amri kumi za Mungu ni za msingi na zinapaswa kufuatwa na Wakristo wote. Kufuata amri hizi kunamaanisha kuwa tunamheshimu Mungu, tunawaheshimu wazazi wetu, tunawapenda jirani zetu kama sisi wenyewe, tunaheshimu maisha ya wengine, tunawaheshimu washirika wetu wa maisha, tunazungumza kwa ukweli, tunawaombea wengine, tunachukia uovu, tunathamini vitu vya wengine, na hatutamani vitu vya wengine.

Kufuata amri hizi kunaleta baraka za Mungu katika maisha yetu na inatuwezesha kuishi maisha yenye furaha na amani. Kupitia Biblia, tunajifunza kuwa kufuata amri hizi ni muhimu sana kwetu kuishi maisha ya Kikristo.

Kanisa Katoliki linafundisha kuwa amri kumi za Mungu ni sehemu muhimu ya Maandiko Matakatifu. Kwa mfano, katika Kitabu cha Kutoka 20: 1-17, Mungu anatoa amri kumi za kufuata. Katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5: 6-21, amri kumi za Mungu zinarejelewa tena. Pia, katika Agano Jipya, Yesu Kristo anasisitiza umuhimu wa kufuata amri hizi.

Kanisa Katoliki linasisitiza umuhimu wa kufuata amri hizi kwa sababu zinaonyesha upendo wetu kwa Mungu na kwa jirani zetu. Wakati tunafuata amri hizi, tunatii mapenzi ya Mungu na tunaheshimu wengine kama sisi wenyewe. Kufuata amri hizi ni muhimu sana katika kujenga jamii ya Wakristo ambayo ina upendo, furaha, na amani.

Kwa ufupi, kufuata amri kumi za Mungu ni muhimu sana katika maisha yetu ya Kikristo. Amri hizi ni mwongozo wa maisha yetu na zinapaswa kufuatwa kwa umakini. Kufuata amri hizi kunatuletea baraka za Mungu na inatuwezesha kuishi maisha yenye furaha na amani. Kama Wakatoliki, tunapaswa kuwa na hamu ya kufuata amri hizi na kuishi maisha ya kujitolea kwa Mungu na kwa wengine. Kama inavyoelezwa katika Catechism of the Catholic Church, amri kumi za Mungu ni "misingi ya maadili ya Kikristo, kwa sababu zinakumbusha wajibu wa upendo wa Mungu na jirani."

Mambo ya Msingi kujua kuhusu Sakramenti ya Kitubio

Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu gani?
Yesu aliweka Kitubio na Mpako wa Wagonjwa kwa sababu alijua udhaifu wa binadamu hauishi mara anapopokea uzima wa Mungu kwa sakramenti tatu za kuingizwa katika Ukristo. Hivyo alipanga kusaidia mpaka mwisho wa dunia waamini wake watakaopatwa na dhambi na ugonjwa, kama alivyowasaidia wengi aliokutana nao katika maisha yake.
“Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, ‘Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako’… ‘Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi’ – amwambia yule mwenye kupooza – ‘Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako’. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii” (Math 9:2,6-8).

Mungu aliwapa watu (mapadri) amri/uwezo ya kusamehe dhambi kwa njia ya nani? Ni halali kuungama kwa padre?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa njia ya Mwanae. Yesu mfufuka aliwaonyesha Mitume alama ya mateso mwilini mwake, “akawavuvia, akawaambia, ‘Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23).
Katika Kanisa tunafurahi kupewa msamaha wa dhambi kila tunapohitaji, mradi tutubu. Kwa njia ya mwandamizi wa Mitume, Yesu anatuambia,
“Umesamehewa dhambi zako… Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani” (Lk 7:48,50).
Si dhana wala hisia tu, bali ni neno la hakika tunalolipokea kwa masikio yetu.

Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zipi?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zote, kwa sababu upendo mtiifu wa Mwanae aliyejitoa kuwa sadaka ya wokovu wetu unampendeza kuliko dhambi zote zinavyomchukiza. Ila hatuwezi kusamehewa dhambi ya kukataa neema ambayo Roho Mtakatifu anatusukuma tuamini na kutubu, kwa sababu pasipo imani na toba hapana msamaha.
“Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa” (Math 12:31).
“Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure” (2Kor 6:1).

Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu gani?
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu amependa washiriki katika kazi zake. Ametuumba kwa njia ya wazazi na kutulea na kutusaidia kwa njia ya wengine pia. Hasa ametuokoa kwa njia ya Yesu, ambaye yupo nasi sikuzote katika Mwili wake, yaani Kanisa, na katika wale walioshirikishwa mamlaka ya Mitume.
“Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:18-20).

Je, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi?
Ndiyo, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi tulizotenda baada ya ubatizo, kwa kuwa hatuwezi kupokea msamaha tukikataa masharti yake, na Mungu ametupangia watu ambao watuondolee kwa niaba yake.
“Watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohane. Lakini, Mafarisayo na wanasheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye” (Lk 7:29-30).
Yesu mwenyewe alikubali kubatizwa na Yohane ili atimize mpango wa Baba.
“Yohane alitaka kumzuia, akisema, ‘Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?’ Yesu akajibu akamwambia, ‘Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Math 3:14-15).
Je, sisi tukatae kumkimbilia padri wa Mungu ili kupokea huruma yake tunayoihitaji kuliko hewa?

Tumuungamie padri dhambi zetu kwa lengo gani? Kwa nini Wakatoliki wanaungama kwa padri?
Tumuungamie padri dhambi zetu ili aweze kutushauri na kuamua kama tuko tayari kuondolewa. Tumweleze kwa unyofu makosa yote tuliyoyafanya na nia tuliyonayo ya kuyafidia na kutoyarudia.
“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu” (1Yoh 1:8-10).
Tukumbuke tulivyo viungo vya Mwili mmoja, hivi kwamba dhambi zetu zimewadhuru wenzetu. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana, mpate kuponywa” (Yak 5:16).
Kutokuwa tayari kufanya hivyo walau sirini kwa padri ni dalili ya kiburi na ya kutotubu.

Je, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi?
Ndiyo, padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi kwa niaba ya Mungu aliyempa mamlaka hiyo. Hatusamehewi na utakatifu wa padri, bali na huruma ya Baba kwa njia yake.
Yeye anamtumia padri yeyote ili kuturahisishia kazi, tusihitaji kuchunguza kwanza ubora wa maisha yake, wala kwenda mbali tukampate mmoja asiye na dhambi. Tungefanyeje kuhakikisha ni mtakatifu, wakati hatuwezi kusoma moyo wake? Ingekuwa hivi, tusingepata kamwe hakika ya kusamehewa. Kumbe inatutosha kujua ni padri, kwamba Mungu amempa mamlaka ya kusamehe dhambi, kama Yesu alivyowapa Mitume siku tatu baada ya kumkimbia na hata kumkana. Kila padri anaweza kukiri,
“Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa: ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi” (1Tim 1:15).
Amri ya kusamehe dhambi wamepewa watu, si malaika.
“Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu” (2Kor 4:7).

Je, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo?
Ndiyo, nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo, lakini ni vigumu zaidi, kwa sababu hatupati msaada wa sakramenti hiyo maalumu.
Pamoja na nia ya kumuungamia padri mapema tunahitaji neema ya kutubu kikamilifu, si kwa kuhofia adhabu, bali kwa kumpenda Mungu tuliyemchukiza.
“Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana” (Lk 7:47).

Sakramenti ya Kitubio ni nini?
Sakramenti ya Kitubio ndiyo Sakramenti ya kuwaondolea watu dhambi walizotenda baada ya Ubatizo (Yoh 20:22-23)

Lini na kwa maneno gani Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio?
Yesu aliweka Sakramenti ya Kitubio jioni ya ufufuko wake alipowapulizia mitume na kuwaambia maneno haya “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi watakua wameondolewa, wowote mtakaowafungia dhambi watakua wamefungiwa” (Yoh 20:22-23)

Mwenye kuwaondolea watu dhambi ni nani?
Mwenyezi Mungu pekee yake aweza kuwaondolea watu dhambi. Ndiye aliyewapa Mitume, Maaskofu na Mapadri uwezo wa kuwaondolea watu dhambi (Yoh 20:21-23)

Nani yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio?
Kila mkristo aliyetenda dhambi yampasa kupokea Sakramenti ya Kitubio

Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Mkristo akitaka kupokea Sakramenti ya Kitubio yampasa haya
1. Kutafuta dhambi moyoni (Yoh 3:20-21)
2. Kujuta dhambi
3. Kukusudia kuacha dhambi
4. Kuungama kwa padre
5. Kutimiza malipizi
6. Kumshukuru Mungu aliyemwondolea dhambi

Wakati wa Sakramenti ya Kitubio Utamwomba Roho Mtakatifu kwa sala gani?
Utamuomba Roho Mtakatifu kwa sala hii:
Uje Roho Mtakatifu unisaidie nitambue dhambi zangu, nijute sana, niungame vema, nipate kutubu kweli. Amina

Kutafuta dhambi maana yake ni nini?
Kutafuta dhambi maana yake ni kujiuliza moyoni dhambi nilizotenda Tangu ungamo la mwisho (Ef 4:17-32)

Utafuteje dhambi wakati wa kujiandaa kuungama?
Tafuta dhambi kwa njia hizi
1. Kwa kukumbuka uliyokosa kwa mawazo, kwa maneno na kwa vitendo
2. Katika Amri za Mungu na za Kanisa
3. Katika vichwa vya dhambi
4. Katika kutimiza wajibu

Kutubu dhambi maana yake ni nini?
Kutubu dhambi maana yake ni kuona uchungu na chuki moyoni juu ya dhambi tulizotenda na kukusudia kutotenda dhambi tena (Yoh 8:11)

Kwa nini tujute dhambi zetu?
Tunajuta dhambi zetu kwa sababu tumeukosea Utatu Mtakatifu na tunastahili adhabu yake, na pia bila majuto hatuwezi kupata maondoleo ya dhambi.

Kuna majuto ya namna ngapi?
una majuto ya namna mbili,
1. Majuto kamili/Majuto ya mapendo
2. Majuto yasiyokamili/majuto pungufu/majuto ya hofu

Majuto kamili ni nini?
Majuto kamili ni kujuta kwa sababu tumemchukiza Mungu mwenyewe aliye mwema na mpendelevu kabisa

Majuto yasiyo kamili au majuto pungufu ni nini?
Majuto yasiyokamili ni kujuta kwa sababu tumepoteza furaha za Mbinguni na tunahofia adhabu ya Mungu

Asiyejuta aweza kuondolewa dhambi?
Asiyejuta hawezi kuondolewa dhambi kabisa, na anayeungama bila kujuta anatenda dhambi kubwa ya kufuru.

Kabla ya kuungama ni lazima kufanya nini?
Kabla ya kuungama ni lazima kukusudia kuacha dhambi na kuepuka nafasi kubwa ya dhambi bila kusahau kufuata hatua sita za kabla na baada ya kupokea kupokea Sakramenti ya Kutubio ambazo ni,
(1) kuwaza/kutafuta dhambi moyoni,
(2)kutubu/ kujuta,
(3)kukusudia kuacha dhambi,
(4)kuungama kwa padri,
(5)kutimiza kitubio,
(6)kumshukuru Mungu

Anayetaka kweli kuacha dhambi afanye nini?
Anayetaka kuacha dhambi afanye nguvu kuvishinda vishawishi, asali/aombe na apokee Sakramenti Mara nyingi hasa Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi Takatifu.

Kuungama ni kufanya nini?
Kuungama ni kumwambia Padri wazi wazi dhambi zako ulizotenda, zipi na ngapi ili upate maondoleo.

Anayeficha kusudi dhambi ya mauti katika ungamo anaondolewa?
Haondolewi, Bali anatenda dhambi kubwa ya kukufuru Sakramenti ya Kitubio. (Mt 7:21-23, Yoh 20:23, Gal 6:7)

Anayekufuru Sakramenti ya Kitubio yampasa nini?
Yampasa kuziungama tena dhambi zake zote alizotenda tangu ondoleo la mwisho

Padri anaondolea dhambi mahali pa nani?
Padri anaondolea dhambi mahali pa Mungu

Padri anaondolea dhambi kwa maneno gani?
Padre anaondolea dhambi kwa maneno haya: Nami “Nakuondolea dhambi zako zote kwa Jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu”.

Kitubio tuwezacho kupewa na padre ni nini?
Kitubio tuwezacho kupewa na Padre ni kama sala, kufunga, kutoa sadaka kwa maskini, kusoma maandiko matakatifu, kuwatazama wagonjwa, n.k.

Kitubio tupewacho na padre chatosha?
Ni shida kutosha. Mara nyingi chataka malipizi ya hapa duniani kama kufunga, magonjwa, masumbuko, sala n.k mateso yasipotosha hapa duniani yatakamilishwa toharani

Kutimiza malipizi maana yake ni ni nini?
Kutimiza malipizi maana yake ni kutekeleza kiaminifu sala au matendo aliyotuagiza padre muungamishi ili kulipa adhabu za muda. (Rom 8:17)

Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema zipi?
Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema hizi;
1. Maondoleo ya dhambi zote kubwa na adhabu ya milele
2. Maondoleo ya dhambi ndogo na adhabu nyingine za muda (Isa 6:5-7, Yoh 8:11)
3. Twarudishiwa na kuongezewa neema ya utakaso
4. Twasaidiwa kuepa dhambi na twapata nguvu ya kutenda mema
5. Twarudishiwa tena mastahili tuliyopoteza kwa dhambi zetu
Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About