Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya Chapati za maji za vitunguu

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour) 1/4
Kitunguu kikubwa (chopped/slice onion) 1
Yai (egg) 1
Chumvi (salt)
Mafuta (cooking oil)

Matayarisho

Tia unga, chumvi na maji kiasi katika bakuli kisha koroga mpaka madonge yote yaondoke. Baada ya hapo tia yai na vitunguu kisha koroga tena mpaka mchanganyiko wote uchanganyike vizuri. baada ya hapo choma chapati zako kama kawaida (jinsi ya kuchoma unaweza kuangalia kwenye recipe yangu ya chapati za maji katika older posts) na baada ya hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Mchuzi wa kambale

Mahitaji

Kambale 2
Nazi kopo 1
Nyanya kopo 1
Vitunguu 2
Curry powder 1 kijiko cha chai
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Binzari nyembamba ya unga 1/2 kijiko cha chai
Swaum/ tangawizi 1 kijiko cha chakula
Giligilani kiasi
Limao 1/2
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Loweka samaki katika maji ya moto kwa muda wa muda wa nusu saa.Baada ya hapo Saga pamoja nyanya, vitunguu, swaum na tangawizi kisha vibandike jikoni na uvipike mpaka maji yote yakauke kisha tia mafuta. Pika mpaka nyanya zitengane na mafuta kisha tia spice zote.Zipike kwa muda mdogo kisha tia tui la nazi, maji kiasi, samaki, pilipili nzima, chumvi na kamulia limao. Pika mpaka tui la nazi litakapoiva na samaki pia wawe wameiva na mchuzi ubakie kiasi. Baada ya hapo ipua kisha tia giligilani iliyokatwa na mchuzi utakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuulia kwa chochote kile upendacho. Mi hupendaga kuulia na ugali mlaiiini au na wali pia.

Namna ya kupika Biskuti Za Kuchoveya Chokoleti

VIAMBAUPISHI

Unga 300gm

Siagi 225gm

Icing Sugar 60gm

Chokoleti iliyokoza (Dark Chocolate) – 225gm

Vanilla – Vijiko 2 vya chai

Yai -1

Baking Powder ½ kijiko cha chai

Njugu za vipande ½ kikombe cha chai

Njugu zilizosagwa ¼ kikombe cha chai

JINSI YA KUTAYARISHA

Piga sukari na siagi katika mashine ya keki mpaka iwe laini
Kisha mimina yai na vanilla koroga vizuri
Mwisho mimina unga na baking powder polepole mpaka ichanganyike.
Kata kata umbo (shape) lolote unavyopenda (kama nyota, pembetatu,duara, kopa n.k)
Panga kwenye treya na choma kwa moto wa 350°C , vikibadilika rangi kidogo tu vitoe
Yayusha chokoleti tia kwenye bakuli ndogo.
kisha paka kwa kijiko au chovyea upande mmoja mmoja wa biskuti kisha nyunyizia njugu za kipande na njugu ya unga.
Panga kwenye sahani tiyari kunywewa na chai ya maziwa au kahawa.

Mapishi ya Wali Wa Mboga Na Samaki Wa Pink Salmon

Vipimo

Mchele 3 vikombe

Mboga mchanganyiko 1 kikombe

Samaki wa Pink Salmon 5 -6 vipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa 1 kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Pilipili manga ya unga ½ kijiko cha chai

Pilipili nyekundu ya unga ½ kijiko cha chai

Ndimu zilokamuliwa 2

Parsley kavu (aina ya kotmiri) 2 vijiko vya supu

Bizari ya mchuzi 1 kijiko cha supu

Kidonge cha supu (stock) 2

Mafuta ¼ kikombe

Maji ½ kikombe

Namna ya Kutayarisha Na Kupika

Samaki:

Katika kibakuli kidogo, changanya; kitunguu thomu, tangawizi, chumvi, pilipili zote za unga, ndimu, parsely, bizari ya mchuzi na mafuta vijiko viwili vya supu.

Pakaza kwenye samaki.

Weka vipande vya samaki katika treya ya oveni kisha uchome (grill) huku ukigeuza hadi samaki awive. Epua weka kando.

Wali:

Osha mchele roweka kisha uchemshe uive nusu kiini

Mwaga maji uchuje mchele

Weka mafuta katika sufura, tia mboga mchanganyiko kakaanga kidogo

Weka vidonge vya supu, tia maji ½ kikombe, tia chumvi kiasi

Mimina mchele uchanganye vizuri, kisha funika hadi uive wali ukiwa tayari

Pakua katika sahani pamoja na samaki

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Nazi Wa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia, Mboga Ya Matembele Na Samaki Wa Kukaanga

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4

Maji – 6 kiasi kutegemea na aina ya unga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka maji katika moto.

Tia unga kidogo katika kibakuli, koroga ufanye uji.

Maji yakichemka tia kwenye maji uwe uji.

Ujii ikiiva punguza kidogo tia unga kidogokidogo na usonge ugali. Ikiwa unga ni mgumu utaongeza maji ya ule uji ulopunguza usonge hadi uive ukiwa tayari.

Vipimo Vya Mchuzi Wa Nazi Kwa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia

Nyanya chungu/mshumaa/Ngogwe – 7

Bamia – 10

Kitunguu maji – 2

Nyanya/tungule – 2

Tui la nazi jepesi – 2 viwili

Tui la nazi zito – 2

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 mbili kamua

Bizari manjano/haldi/turmeric – ½ kijiko cha chai

Pilipili mbuzi – 3

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata kitunguu maji na nyanya vipande vidogodogo sana kisha weka katika sufuria.

Iache ichemke kwa maji yake ya nyanya, ikishachemka tia maji kidogo kama robo kikombe.

Tia nyanya chungu, bamia na koleza ndimu, chumvi.

Iache ichemke. Inapokuwa tayari imeiva tia tui jepesi endelea kuacha katika moto huku unakoroga kidogo kidogo.

Tui jepesi likipungua kiasi chake, tia tui zito, kisha usiachie mkono koroga ikichemka kidog kiasi cha kuiva tui mchuzi tayari.

Vipimo Vya Mboga Ya Matembele

Matembele – 5 mafungu

Mafuta – ¼ kikombe

Kitunguu maji kilokatwakatwa – 1

Nyanya/tungule – 4

Chumvi – 1

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Punguza miche ya matembele kwa kuikata ncha kisha osha majani yake. Acha yachuje maji .
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji na nyanya hadi viivie.
Tia mboga, Iache ichemke kwa maji yake hadi iive. Ukiona bado haikuiva tia maji kidogo tu.
Ukipenda unatia ndimu kiasi cha kipande kimoja ukamue .

Samaki Wa Nguru Wa Kukaanga

Samaki Wa Nguru – 4 vipande

Kitunguu saumu(thom/galic) na tangawizi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi – 4

Ndimu – 2 kamua

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Mwoshe samaki kisha mtie kitunguu thomu, tangawizi ilosagwa, chumvi, pilipilimbichi ilosagwa, ndimu na bizari ya samaki.
Mwache akolee viungo kwa muda kidogo.
Makaange katika mafuta hadi aive akiwa tayari.

Mapishi ya Wali Wa Kukaanga Kwa Kidari Cha Kuku (Chicken Breast) Wa Kukausha

Viambaupishi

Vipimo vya Wali:

Mchele 3 vikombe

*Maji ya kupikia 5 vikombe

*Kidonge cha supu 1

Samli 2 vijiko vya supu

Chumvi kiasi

Hiliki 3 chembe

Bay leaf 1

Viambaupishi: Kuku

Kidari (chicken breast) 1Kilo

Kitunguu 1

Tangawizi mbichi ½ kipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) 7 chembe

Pilipili mbichi 3

Ndimu 2

Pilipilimanga 1 kijiko cha chai

Mdalasini ½ kijiko cha chai

Jira/Cummin ya unga 1 kijiko cha chai

Maji ¼ kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

Wali:

Osha na roweka mchele kisha weka sufuria katika moto tia samli ipashe moto.

Tia hiliki, bay leaf, kaanga, kisha tia mchele ukaange kidogo.

Tia maji, chumvi na kidonge cha supu, upike wali kama unavyopika pilau.

*Maji kisia kwa kutegemea mchele ulivyo.

  • Unaweza kutumia supu yoyote badala ya kidonge.

Kuku:

Katakata kidari cha kuku vipande vya kiasi, weka katika sufuria, tia ndimu, bizari zote, chumvi.

Katakata kitunguu vipande vidogodogo, pilipili, na kitunguu thomu (chopped), tia katika kuku.

Chuna tangawizi mbichi tia katika kuku. Changanya vitu vyote vizuri.

Tia maji kiasi ¼ kikombe tu kiasi cha kumkaushia kuku. Weka katika moto mpike huku unageuzageuza. Anapokaribia kukauka epua akiwa tayari kuliwa na wali (na saladi upendayo)

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About