Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

LISHE BORA KWA WATU WENYE AFYA NZURI

• Kula chakula bora kunamaanisha kula vyakula aina tofauti ya vyakula kila siku kama vile matunda, mboga, maziwa na aina ya vyakula vyenye asili ya nyama wa kufuga kama kuku, mbuzi, ngombe, samaki na na vyakula vya nafaka.

• Lishe bora linamaanisha pia kula chakula ambacho hakina mafuta mengi, sukari au chumvi nyingi

• Zingatia angalau vyakula vya nafaka kama vile mtama, mahindi, mchele, ngano, wimbi, ndegu, njegere. n.k

• Ni bora kula matunda mengi kama ‘maembe, ndizimbivu, papai, pera, chungwa, ubuyu, nanasi, pesheni, zambarau” na mbogamboga kama vile “mchicha, majani ya mboga, karoti, nyanya chungu, nyanya, mkunde, biringanya” mara tano kwa siku.

• Kama mboga na matunda hazipatikani ni bora kununua zile ambazo zimehifadhiwa tayari kwenye mikebe au zile ziko kwenye jokofu (friji).

• Punguza kula vyakula ambavyo vinapikwa kwa mafuta mengi na chumvi nyingi

• Lishe bora hukusaidia wewe na jamii yako kuishi vyema, kuwa na afya bora, kufanya kazi vizuri na kwa bidii, shuleni na hata kucheza.

Mapishi ya Ndizi na samaki

Mahitaji

Ndizi laini (Matoke 6)
Viazi mbatata (potato 3)
Samaki wabichi wa wastani ( Fresh tilapia 2)
Kitunguu swaum (garlic 6 cloves)
Tangawizi (fresh ground ginger vijiko 2 vya chai)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2 kopo)
Vitunguu (onion 1)
Pilipili (chilli 1 nzima)
Chumvi (salt to your taste)
Mafuta (vegetable oil)
Limao (lemon 1/2)
Curry powder (1/2 kijiko cha chai)

Matayarisho

Safisha samaki kisha wakate vipande vitatu. Wakaushe maji kisha wamarinate na kitunguu swaum,tangawizi, chumvi, na limao kwa muda wa masaa 2. baada ya hapo waoke kwenye oven kwa muda wa dakika 30. baada ya hapo andaa ndizi na viazi kwa kuzimenya na kuziosha kisha ziweke pembeni. Kisha katakata vitunguu maji, Tangawizi, vitunguu swaum na nyanya kisha vitie kwenye blenda na usage mpaka mchanganyiko usagike vizuri. Baada ya hapo tia mchanganyiko katika sufuria na ubandike jikoni, acha uchemke mpaka maji yote yakauke. Maji yakisha kauka punguza moto na utie mafuta, curry powder, pilipili na chumvi. Kaangiza mpaka mchanganyiko uive na baada ya hapo tia viazi na maji kiasi na uache viazi vichemke mpaka vikaribie kuiva kisha tia ndizi na samaki na ufunike. Pika mpaka ndizi na viazi viive. Baada ya hapo chakula kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Mapishi ya Viazi vitamu na kachumbari

Mahitaji

Viazi utamu 3
Nyanya 2 kubwa
Kitunguu
Tango
Limao
Chumvi
Pilipili
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Menya viazi na kisha vikate katika vipande. Tia mafuta kwenye chuma cha kukaangia, yakisha pata moto tia viazi nauviache vikaangike mpaka upande mmoja uwe wa brown na kisha geuza upande wa pili na upike mpaka uwe wa brown. Vikisha iva ipua na uweke kwenye kitchen towel ili vikauke mafuta.
Kachumbali: Katakata vitunguu katika bakuli na kisha tia chumvi kwa ajili ya kuondoa ukali wa vitunguu. Baada ya hapo vioshe mpaka chumvi yote iishe. osha nyanya, Pilipili tango na kisha katakata slice nyembamba na uchanganye na vitunguu. Baada ya hapo tia chumvi, kamulia limao na uchanganye zote pamoja .Baada ya hapo viazi na kachumbali vitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali, samaki wa nazi na kisamvu

Mahitaji

Mchele
Kisamvu kilichotwangwa
Samaki
Mbaazi
Nyanya chungu
Vitunguu
Nyanya ya kopo
Tangawizi
Kitunguu swaum
Vegetable oil
Curry powder
Tui la nazi (kopo 2)
Chumvi
Pilipili
Limao

Matayarisho

Safisha samaki kisha wamarineti na kitunguu swaum, tangawizi, pilipili, chumvi na limao kwa muda wa masaa 3.Baada ya hapo wakaange na usiwakaushe sana na uwaweke pembeni kwa ajili ya kuungwa.Katakata vitunguu maji, saga tangawizi na kitunguu swaum. Baada ya hapo injika sufuria ya mchuzi jikoni na mafuta kiasi ya kupikia, mafuta yakisha pata moto, tia vitunguu maji na vikaange mpaka viwe vya rangi ya brown. kisha tia kitunguu swaum na tangawizi.kaanga kidogo kisha tia nyanya ya kopo moja na ufunike. acha mpaka nyanya ziive. Kisha tia chumvi na curry powder na uache ikaangike kwa muda wa dakika 2 kisha tia samaki na nyanya chungu nakisha kamulia nusu ya limao. Geuza mpaka mchanganyiko uchanganyike vizuri kisha tia tui la nazi kopo moja na uache ichemke mpaka mchuzi uive.

Baada ya hapo chemsha kisamvu pamoja na mbaazi Kikisha iva, kaanga kitu na nyanya pembeni mpaka ziive kisha tia kisamvu. geuza mchanganyiko mpaka uchanganyike vizuri kisha tia tui la nazi na chumvi na aacha ichemke mpaka tui liive kisha ipua.malizia kwa kupika wali ambapo utachemsha maji kisha tia mafuta,chumvi na mchele na uupike mpaka uive kisha sevu na mboga ulizopika na mlo wako utakuwa tayari kwa kuliwa.

Upishi kwa Ajili ya Kusaidia Kinga: Kujenga Uimara

Upishi kwa Ajili ya Kusaidia Kinga: Kujenga Uimara 🍎🥦🏋️‍♀️

Habari za leo wapenzi wasomaji! Hali yenu iko vipi leo? Ni furaha kubwa kuweza kuandika makala hii ambayo itakusaidia kuelewa umuhimu wa upishi na jinsi unavyoweza kusaidia kuimarisha kinga yako. Naitwa AckySHINE na kama mtaalamu katika uwanja huu, nitakuwa nikikupa ushauri wa kitaalamu kuhusu jinsi ya kujenga uimara wako kupitia upishi sahihi.

Upishi ni njia muhimu sana ya kuleta mabadiliko chanya katika afya yako. Chakula chetu kinaweza kuwa silaha yetu ya kwanza katika kupambana na magonjwa. Hivyo basi, ni muhimu kuzingatia lishe bora ili kusaidia kuimarisha mfumo wako wa kinga. Hapa chini ni orodha ya mambo 15 muhimu ya kuzingatia katika upishi wako kwa ajili ya kusaidia kinga yako:

  1. Kula matunda na mboga za majani kwa wingi 🍎🥦: Matunda na mboga za majani zina virutubisho vingi vinavyosaidia kuimarisha kinga yako. Vitamini C inayopatikana katika matunda kama machungwa na pilipili ni muhimu katika kukuza seli za kinga. Pia, mboga za majani kama spinach zina madini muhimu yanayosaidia mwili kupambana na magonjwa.

  2. Ongeza protini katika lishe yako 🥩🍗: Protini ni muhimu sana katika kujenga tishu za mwili na kuimarisha kinga. Chagua chanzo cha protini bora kama vile samaki, kuku, maharage, na karanga.

  3. Punguza matumizi ya sukari na vyakula vyenye mafuta mengi 🍬🍔: Vyakula vyenye sukari nyingi na mafuta mengi vinaweza kudhoofisha kinga yako. Badala yake, chagua vyakula vyenye afya kama vile matunda, nafaka nzima, na njugu.

  4. Kunywa maji ya kutosha 💦: Maji ni muhimu kwa afya yako yote, ikiwa ni pamoja na kinga. Kunywa angalau lita mbili za maji kila siku ili kuweka mwili wako unyevu na kuondoa sumu.

  5. Pata muda wa kutosha wa kupumzika 😴: usingizi wa kutosha unachangia sana katika kuimarisha kinga yako. Hakikisha unapata angalau masaa 7-8 ya usingizi kila usiku ili kuweka mwili wako na akili yako katika hali nzuri.

  6. Fanya mazoezi mara kwa mara 🏋️‍♀️: Mazoezi ya kimwili yanaweza kuimarisha kinga yako kwa kukuza mzunguko mzuri wa damu na kusaidia mwili wako kuondoa sumu. Fanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki kwa muda mfupi kama dakika 30.

  7. Punguza msongo wa mawazo 🧘‍♀️: Msongo wa mawazo unaweza kudhoofisha kinga yako. Jaribu njia za kupumzika kama yoga, meditation, au kutembea katika maeneo yenye utulivu.

  8. Epuka uvutaji wa sigara 🚭: Sigara inaweza kuathiri vibaya mfumo wako wa kinga na kukufanya uwe katika hatari kubwa ya kupata magonjwa. Ni bora kuacha kabisa uvutaji wa sigara ili kuimarisha kinga yako.

  9. Jifunze kupika vyakula vyenye virutubisho vingi 🍳: Kupika chakula chako mwenyewe kutakupa udhibiti kamili juu ya viungo unavyotumia na kiasi gani cha mafuta au sukari kinachoingia katika chakula chako. Jifunze mapishi mapya na jaribu chakula kipya kila mara ili kufurahia upishi wako.

  10. Tumia viungo vya asili vinavyosaidia kinga yako 🌿: Viungo kama tangawizi, mdalasini, na vitunguu swaumu vina mali ya antibakteria na antioxidant ambayo inaweza kuimarisha kinga yako. Ongeza viungo hivi katika vyakula vyako kwa ladha nzuri na faida za afya.

  11. Pata chanjo zinazopendekezwa na wataalamu wa afya 💉: Chanjo ni njia bora ya kuzuia magonjwa hatari. Hakikisha unapata chanjo zote zinazopendekezwa na wataalamu wa afya ili kuimarisha kinga yako na kulinda mwili wako.

  12. Epuka vyakula vilivyosindikwa kwa wingi 🍔🍟: Vyakula vilivyosindikwa mara nyingi vina viungo vya kemikali na sukari nyingi ambazo zinaweza kudhoofisha kinga yako. Badala yake, chagua vyakula vyenye asili na ubora wa juu.

  13. Kula kwa kiasi 🍽️: Kula kwa kiasi ni muhimu ili kuzuia matatizo ya kiafya kama vile unene kupita kiasi na ugonjwa wa kisukari. Chukua muda wako kula polepole na kusikiliza mwili wako unaposema "nimeshiba".

  14. Zingatia usafi wa vyakula 🧼: Usafi wa vyakula ni muhimu ili kuzuia magonjwa yanayosababishwa na vimelea. Safisha vyakula vyako vizuri kabla ya kula na hakikisha unatumia vyakula safi na salama.

  15. Shauriana na mtaalamu wa lishe 📞: Mtaalamu wa lishe ataweza kutoa ushauri wa kitaalamu kulingana na mahitaji yako ya kipekee. Ni muhimu kushauriana na mtaalamu wa lishe ili kuunda mpango wa lishe unaofaa kwako na kusaidia kuimarisha kinga yako.

Kwa ufupi, upishi ni zana ya muhimu katika kusaidia kuimarisha kinga yako. Kula vyakula vyenye virutubisho, kufanya mazoezi mara kwa mara, kupata usingizi wa kutosha, na kuzingatia usafi wa vyakula ni njia bora za kujenga uimara wa mwili wako. Kumbuka, kinga yako ni muhimu katika kupambana na magonjwa na kuwa na afya njema. Je, wewe unafikiri ni nini kingine kinaweza kusaidia kuimarisha kinga yako? Asante kwa kusoma na natarajia maoni yako! 🌟😊

Mapishi ya visheti vitamu

VIAMBAUPISHI

Unga – Vikombe 2

Samli au shortening ya mboga – 2 Vijiko vya supu

Maziwa ¾ Kikombe

Iliki – Kiasi

Mafuta ya kukarangia Kiasi

VIAMBAUPISHI :SHIRA

Sukari – 1 Kikombe

Maji ¾ Kikombe

Vanila ½ Kijiko cha chai

Zafarani (ukipenda) – Kiasi

JINSI YA KUPIKA

Katika kisufuria pasha moto maziwa na wakati huo huo chemsha Samli katika kisufuria kengine.
Tia unga katika bakuli na iliki, kisha mimina samli iliyochemka na huku unachanganya.
Tia maziwa na uwendele kuchanganya vizuri isiwe na madonge, ikiwa maziwa haitoshi ongeza maji kidogo.
Kisha uwache unga ukae mahali pa joto kwa muda wa dakika 10 hivi.
Halafu fanya viduara vidogo vidogo, kisha finyiza kwenye greta yenye vishimo vidogo ili upate umbo lake.
Kisha karanga kwenye mafuta yaliyopata moto hadi vibadilike rangi ya dhahabu, kisha viepue vichuje mafuta.
Chemsha shira, ikiwa tayari mimina visheti na upepete na kuzichanganya zipate shira kote.
Weka kwenye sahani na zitakuwa tayari kwa kuliwa na kahawa.

Mapishi ya Mchemsho wa ndizi na nyama

Mahitaji

Ndizi mbichi 6
Nyama ya ng’ombe (nusu kilo)
Viazi mviringo 2
Kitunguu swaum
Tangawizi
Kitunguu maji
Nyanya 1 kubwa
Mafuta (vegetable oil)
Chumvi
Limao
Pilipili

Matayarisho

Chemsha nyama na limao, kitunguu swaum, tangawizi chumvi na maji kiasi mpaka nyama iive, Hakikisha unaiacha na supu kiasi kwa ajili ya kuwekea kwenye ndizi.Kisha katakata nyanya na vitunguu na uweke pembeni .Menya ndizi na viazi kisha zichemshe pamoja na vitunguu, nyanya, maji kidogo, mafuta na uhakikishe haziivi kabisa. Baada ya hapo tia nyama na supu yake, pilipili mzima na chumvi na uache uchemke mpaka ndizi na viazi viive.Na baada ya hapo mchemsho wako utakuwa tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Biriani Ya Kuku Wa Kuchoma Wa Tanduri

Mahitaji

Mchele – 4 vikombe

Kuku – 1

Vitunguu – 3

Nyanya/tungule – 4

Zabibu kavu – ½ kikombe

Tangawizi na kitunguu (thomu/galic) – 2 vijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Mtindi (yoghurt) – 2 kijiko cha supu

Masala ya tanduri – 2 vijiko vya supu

Pilipili manga – 1 kijiko cha chai

Hiliki – ½ kijiko cha chai

Mdalasini – kijiti kimoja

Ndimu – 3 vijiko vya supu

Chumvi – kiasi

Zaafarani (saffron) – 1 kijiko cha chai

Mafuta – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Kuku:

Baada ya kumsafisha kuku, mkate vipande vikubwa vikubwa kiasi upendavyo, muoshe mchuje atoke maji.
Katika bakuli, tia tangawizi, kitunguu thomu ilosagawa, pilipili mbichi ilosagwa, chumvi, ndimu, mtindi, masala ya tanduri na uchanganye vizuri, kisha mtie kuku na uchanganye tena na acha arowanike kwa muda wa kiasi saa au zaidi.
Panga kuku katika sinia ya kuchoma ndani ya oveni. Kisha mchome (grill) hadi awive, mtoe acha kando. Mwagia juu yake masala yatakayobakia katika sinia baada ya kumchoma.

Namna Ya Kutayarisha Masala Ya Nyanya:

Weka mafuta katika karai, tia vitunguu ulivyokatakata, kaanga hadi vianze kugeuka rangi.
Tia nyanya ulizokatakata, tia pilipili manga, hiliki, mdalasini, chumvi, na zabibu. Kaanga kidogo tu yakiwa tayari.

Namna Ya Kutayarisha Wali:

Osha na roweka mchele wa basmati.
Roweka zaafarani kwa maji ya moto kiasi robo kikombe weka kando.
Chemsha maji, tia chumvi, kisha tia mchele uive nusu kiini.
Mwaga maji uchuje mchele kisha rudisha katika sufuria au sinia ya foil. Nyunyizia zaafarini, na rudisha katika moto upike hadi uive kamili.
Epua, kisha pakua wali katika sahani au chombo upendacho, mwagia juu yake masala ya nyanya. Kisha weka vipande vya kuku ulivyochoma, biriani ikiwa tayari

Mapishi ya Wali Mweupe Kwa Mchuzi Wa Kuku Wa Balti

Vipimo

Kuku 1 mkate vipande vipande

Vitunguu 3 katakata (chopped)

Nyanya 5 zikatekate (chopped)

Tangawizi mbichi ilokunwa au ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Thomu (kitunguu saumu) kilosagwa kijiko 1 cha kulia

Bizari mchanganyiko (garam masala) kijiko 1 cha chai

Jira/bizari ya pilau (cummin powder) kijiko 1 cha chai

Dania/gilgilani ilosagwa (coriander powder) kijiko 1 cha chai

Mtindi/maziwa lala (yoghurt) vijiko vya kulia 4 mjazo au paketi moja ndogo.

Malai ya kupikia (cooking cream) kikombe 1

Kasuri methi (majani makavu ya uwatu/dried fenugreek leaves) 1 kijiko cha kulia

Mafuta ya kupikia ½ kikombe

Chumvi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha kuku vizuri mwache achuje maji.
Weka mafuta katika sufuria kaanga vitunguu mpaka vianze kugeuka rangi ya brown hafifu. Kisha tia tangawizi na thomu ukaange.
Tia kuku ukaange mpaka ageuke mweupe kisha tia nyanya endelea kukaanga ziwive.
Piga mtindi vizuri katika kibakuli uwe nyororo.
Epua sufuria weka kando kisha tia mtindi uchanganye vizuri pamoja na kuku.
Rudisha katika moto acha uchanganyike na kuku kidogo kisha mwagia malai ya kupikia (cooking cream)
Tia kasuri methi/majani makavu ya uwatu yaliyovurugwa. Acha katika moto dakika 1 tu.
Epua umimine katika chombo na nyunyizia ikiwa tayari kuliwa na wali mweupe.

Jinsi ya kupika wali wa Tuna (samaki/jodari)

VIAMBAUPISHI VYA TUNA

Tuna (samaki/jodari) – 2 Vikopo

Vitunguu (kata kata) – 4

Nyanya zilizosagwa – 5

Nyanya kopo – 3 Vijiko vya supu

Viazi (vilivyokatwa vipande vidogo – cubes) – 4

Dengu (chick peas) – 1 kikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic)&Tangawizi iliyosagwa 1 Kijiko cha supu

Hiliki – 1/4 kijiko cha chai

Mchanganyiko wa bizari – 1 kijiko cha supu

Chumvi – kiasi

Pilipili manga – 1 Kijiko cha chai

Vipande cha Maggi (Cube) – 2

VIAMBAUPISHI VYA WALI

Mchele – 3 Vikombe vikubwa (Mugs)

Mdalasini – 2 Vijiti

Karafuu – chembe 5

Zaafarani – kiasi
Jirsh (Komamanga kavu au zabibu kavu -raisins) – 1/2 Kikombe

JINSI YA KUANDAA

Kosha Mchele na roweka.
Kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi (brown) chuja mafuta uweke kando.
Kaanga viazi, epua
Punguza mafuta, kaanga nyanya.
Tia thomu/tangawizi, bizari zote, vipande vya Maggi, nyanya kopo, chumvi.
Mwaga maji ya tuna iwe kavu, changanyisha kwenye sosi.
Tia zaafarani kidogo katika sosi na bakisha ya wali.
Chemsha mchele pamoja na mdalasini na karafuu.
Karibu na kuwiva, chuja maji utie katika chombo cha kupikia katika jiko (oven)
Nyunyizia zaafarani, mwagia vitunguu, viazi, na dengu juu ya wali.
Mwagia sosi ya tuna na pambia jirshi (au zabibu).
Funika wali na upike katika jiko moto wa 450º kwa muda wa kupikika wali. Epua upakue.

Madhara ya nyama nyekundu kwa mtu mwenye VVU

Kuna nyama za aina mbili, nazo ni nyama nyeupe na nyama nyekundu.

Nyama nyeupe

Hizi ni nyama zitokanazo na samaki, kuku, ndege wa aina zote, bata, wadudu

Nyama nyekundu

Hutokana na ng’ombe, mbuzi, kondoo,nguruwe na wanyama wa porini.

Nyama ina virutubishi vingi muhimu kwa afya ya binadamu kama protini, vitamini na madini. Madini ya chuma yanayopatikana kwenye nyama ni rahisi sana kusharabiwa (kufyonzwa) mwilini na ni muhimu kwa kuongeza wekundu wa damu.
Uwezo wa miili ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kuyeyusha chakula na kusharabu (kufyonza) virutubishi hupungua. Utumiaji wa nyama nyekundu kwa wingi unaweza kuwaletea matatizo hasa katika uyeyushwaji tumboni kwani nyama nyekundu si rahisi kuyeyushwa ukilinganisha na nyama nyeupe.

Hata hivyo katika nchi yetu watu walio wengi wanatumia nyama kwa kiasi kidogo sana na mara chache. Si vyema watu hawa waache kabisa nyama nyekundu. Jambo la muhimu ni kutumia njia mbalimbali ili kuifanya nyama hii iyeyushwe kwa urahisi tumboni.

Namna ya kusaidia uyeyushwaji ni pamoja n a : –

• Kutafuna vizuri au kutumia nyama ya kusaga (kwa wanaoipata).
• Kupika nyama na viungo vinavyosaidia kulainisha kama vile papai bichi, limao, vitunguu saumu n.k.
• Kula nyama pamoja na papai

Kwa hiyo, kwa anayepata nyama nyekundu kwa wingi, kupunguza kiasi cha nyama hiyo na kuongeza kiasi cha nyama nyeupe. Na kwa yule asiyepata nyama nyeupe, apatapo nyama nyekundu asiache kutumia kwani ina umuhimu mwilini mwake.

Mapishi mazuri ya Uji wa ulezi

Mahitaji

Unga wa ulezi (millet flour vijiko 3 vya chakula)
Maziwa fresh (milk 1/2 kikombe)
Sukari (sugar 1/4 ya kikombe cha chai)
Siagi (butter kijiko 1 cha chakula)
Maji (vikombe 4 vya chai) (serving ya watu wawili)

Matayarisho

Chemsha maji ya uji, Kisha koroga unga na maji ya baridi kiasi na uchanganye kwenye maji ya moto yanayochemka. Endelea kukoroga mpaka uchemke ili kuhakikisha uji haupatwi na madonge. Ukishachemka tia, maziwa, sukari na butter. Kisha acha uchemke kwa muda wa dakika 10 na hapo uji utakuwa tayari.

Mapishi ya Ndizi Za Supu Ya Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi – 15 takriiban

Nayma ya ng’ombe – 1 kilo

Kitunguu maji – 1

Nyanya – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) kilosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi ilopondwa – 2

Jira/cummin/bizari ya pilau ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 1

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chemsha nyama kwa ndimu, chumvi na tangawizi mbichi na kitunguu thomu.
Menya ndizi na zikatekate vipande kiasi, weka katika sufuria.
Katakata kitunguu na nyanya utie katika ndizi.
Tia jira na chumvi.
Nyama ikiwiva mimina pamoja na supu yake ufunike ndizi ziwive na kuwa tayari kuliwa.
Ukipenda tia pilipili mbuzi zichemke pamoja na ndizi.

Mapishi ya Biriani Ya Samaki Nguru, Njegere Na Snuwbar (UAE)

Mahitaji

Mchele wa basmati – 4 cups

Samaki nguru (king fish) – 7 vipande au zaidi

Kitunguu – 5

Nyanya/tungule – 3

Njegere – 1 kikombe

Snuwbar (njugu za pine) – 1 kikombe

Viazi – 2 kata kata mapande makubwa

Tangawizi mbichi – 1 kijiko cha supu

Kitunguu saumu – 1 kijiko cha supu

Pilipili nyekundu – 1 kijiko cha chai

Bizari ya biriani/garama masala – 1 kijiko cha supu

Namna Ya Kupika:

Kaanga samaki mbali kwa viungo upendavyo umkoleze vizuri. Au choma (bake/grill) katika oveni ukipenda.
Weka mafuta katika sufuria, tia vitunguu kaanga hadi vigeuka rangi. Gawa sehemu mbili.
Sehemu moja bakisha katika sufuria kisha tia tangawizi mbichi na kitunguu thomu ukaange.
Tia nyanya kaanga kisha tia bizari zote endelea kukaanga, tia njegere, njugu za snuwbar na ndimu kavu.
Tia viazi ulivyokwishakaanga, na vitunguu vilobakia.
Tia mapande ya samaki, changanya na masala bila ya kumvuruga samaki.
Chemsha wali kisha mwagia juu yake, funika upike ndani ya oveni au mkaa hadi wali uive kama unavyopika kawaida ya biriani.
Epua pakua huku ukichanganya na masala ya samaki.

Mapishi ya Chicken Curry

Leo wapendwa nitaenda kuzungumzia mapishi ya mchuzi wa kuku (chicken curry).

Mahitaji

Kuku mzima
Nyanya kubwa 3
Karoti mbili
Pilipili hoho
Kotmiri
Tangawizi
Kitunguu maji
Kitunguu saumu kidogo
Ndimu
Mafuta ya kupikia
Chumvi (pilipili ukipenda)

Matayarisho

1. Menya vitunguu saumu na tangawizi na uvitwange pamoja.
2. Katakata kuku vipande vidogo kisha ukamulie ndimu na kupaka mchanganyiko wa tangawizi na vitunguu saumu (kiasi tu).
3. Katakata vitunguu maji na pilipili hoho uweke pembeni.
4. Grind (Kwangua) kwenye grater nyanya na karoti pia uweke pembeni.
5.Katakata kotmiri vipande vidogo uweke pembeni.
6. Andaa kikaango na jiko.

Mapishi

1. Bandika kikaango jikoni na mafuta kiasi, yakishachemka weka vitunguu maji na kaanga hadi vimelainika na kuiva (hakikisha haviungui).
2. Weka pilipili hoho na karoti na endelea kukoroga hadi vyote viive na kulainika, Kisha weka chumvi.
3. Sasa weka vipande vya nyama koroga na funikia kwa dakika 3, kisha weka nyanya zako ulizo grind na koroga ili zichanganyike vizuri, vikishachanganyika weka kotmiri na pilipili kama utapenda. Acha vichemke kwa dakika 5. Hakikisha moto sio mkali sana.
4. Angalia kama nyama zimeiva vizuri kisha epua mchuzi wako.
5. Pakua kwenye bakuli na katakata kotmiri uweke kwa juu.
Unaweza kula kwa ugali, wali, ndizi rost au chipsi.

Mapishi ya Wali Wa Nazi Kwa Mchuzi Wa Samaki Na Rojo La Bilingani Na Viazi/Mbatata

Wali Wa Nazi

Mpunga – 4 vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha
Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.
Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Mchuzi Wa Samaki Nguru

Samaki – 4

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 2 viijiko vya supu

Kitunguu maji kilokatwakawa – 2 slice ndogo

Nyanya/tungule – 4

Nyanya kopo – 3 vijiko vya supu

Pilipili mbichi – 2

Kotmiri ilokatwakatwa – 3 msongo (bunches)

Bizari ya mchuzi (simba 2) – I kijiko cha chai

Ndimu – 1 kamua

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata samaki mkaange kwa kumtia viungo.
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu. Vinapogeuka rangi thomu na tangawizi mbichi, nyanya, nyanya kopo, kitunguu na bizari ya mchuzi endelea kukaanga.
Tia maji kiasi na ndimu, pilipili mbichi ilosagwa kisha tia kotmiri.
Mwisho tia nusu ya samaki alokaangwa ukiwa tayari

Bilingani Za Kukaanga Na Viazi

Bilingani – 4 madogodogo

Viazi/mbatata – 3

Nyanya – 3

Majani ya mchuzi/mvuje/curry leaves – kiasi 6-7

Nnyanya kopo – 2 vijiko vya supu

Methi/uwatu ulosagwa – 1 kijiko cha chia

Rai/mustard seeds – 1 kijiko cha supu

Bizari ya manjano/haldi/turmeric – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

1. Weka mafuta ya kukaangia katika karai

2. Katakakata bilingani vipande vipande vya mraba (cubes) kaanga katika mafuta ya moto hadi yageuke rangi. Eupa weka kando.

3. Katakataka viazi/mbatata vipande vidogodogo vya mraba (cubes) Kaanga hadi viive epua weka kando.

4. Ondosha mafuta yote katika karai bakisha kidogo tu kiasi ya vijiko 2 vya supu.

5. Kaanga rai kisha majani ya mchuzi, na methi/uwatu kisha kaanga nyanya.

6. Tia nyanya ya kopo kisha changanya pamoja bilingani na viazi ikiwa tayari.

Mapishi ya wali wa mboga

Mahitaji

Wali uliopikwa (cooked rice) kiasi
Hoho la kijani (green pepper) 1/2
Hoho jekundu (red pepper) 1/2
Carrot 1
Kitunguu kikubwa (onion) 1
Njegere (pears) 1/2 kikombe cha chai
Mayai (eggs) 2
Uyoga (mushroom) 2 vikombe vya chai
Soy source 2 vijiko vya chakula
Chumvi (salt) kiasi
Mafuta (veg oil) 3 vijiko vya chakula

Matayarisho

Katakata hoho, kitunguu,na uyoga vipande vikubwa kiasi(chunks) kisha katakata carrot zisiwe nene au nyembamba sana. Baada ya hapo weka mafuta katika katika frying pan yako isiyoshika chini acha yapate moto kisha tia uyoga na ukaange mpaka uive.Baada ya hapo tia vegetable zote na uzikaange pamoja na uyoga kwa muda wa dakika 2, kisha katika hiyohiyo frying pan zisogeze vegetable zako pembeni (ili kupata nafasi ya kukaangia mayai).Yakaange mayai katika hiyo sehemu yakiisha iva yavuruge na kisha yachanganye pamoja na vegetable na kisha tia chumvi kidogo sana. Baada ya hapo malizia kwa kutia wali na soy source kisha koroga vizuri mpaka mchanganyiko wako wote uchanganyike vizuri (hakikisha wali unapata moto na vegetable haziivi sana) . Na baada ya hapo chakula chako kitakuwa tayari.

Mapishi ya Chapati za Kusukuma kitaalamu

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour 1/2 of kilo)
Siagi (butter vijiko 2 vya chakula)
Yai (egg 1)
Chumvi (1/2 ya kijiko cha chai)
Hiliki (ground cardamon 1/4 ya kijiko cha chai)
Maji ya uvuguvugu (warm water)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Weka unga wa ngano katika bakuli la kukandia, kisha tia chumvi na hiliki na uchanganye kwanza, baada ya hapo tia siagi na uichanganye vizuri na unga mpaka ipotee. Baada ya hapo tia tena yai na uchanganye vizuri. Mchanganyiko ukishachanganyika vizuri sasa unaweza kutia maji ya uvuguvugu kidogo, kidogo huku ukiwa unauchanganya ili kupata donge. Baada ya hapo anza kukanda hilo donge mpaka mabuje yote yapotee na unga uwe mlaini, ambapo itakuchukua kama dakika 15. Baada ya hapo tawanyisha unga katika madonge ya wastani (yasiwe makubwa sana au madogo sana) Ukimaliza hapo, andaa kibao cha kusukumia chapati kwa kukitia unga kidogo ili chapati isinatie kwenye kibao. Sukuma donge moja la chapati mpaka liwe flat na kisha weka kijiko kimoja cha mafuta na usambaze. ukisha maliza ikunje (roll). Fanya hivyo kwa madonge yote yaliyobakia.
Baada ya hapo andaa chuma cha kuchomea (fry-pan) katika moto wa wastani. Kisha anza kusukuma chapati (ni vizuri ukaanza na zile ulizozikunja mwanzo ili kuzipa nafasi zile za mwisho ziweze kulainika) ukiwa unasukuma hakikisha zinakuwa flat (na zisiwe nene sana au nyembamba sana) Ukishamaliza hapo tia kwenye chuma cha kuchomea. Acha iive upande mmoja then igeuze upande wa pili. Tia mafuta ama kijiko kimoja kikubwa upande wa chini wa chapati na uanze kuukandamiza kwa juu uku ukiwa unaizungusha. fanya hivyo uku ukiwa unaigeuza kuiangalia kwa chini ili isiungue. ikishakuwa ya brown, geuza upande wa pili na urudie hivyohiyvo mpaka chapati iive. Rudia hii process kwa chapati zote zilizobakia.

Siri ya chapati kuwa laini ni kutia siagi au mafuta ya kutosha kipindi unazikanda na pia kuzikanda mpaka unga uwe laini.

Mapishi ya Chapati za maji za vitunguu

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour) 1/4
Kitunguu kikubwa (chopped/slice onion) 1
Yai (egg) 1
Chumvi (salt)
Mafuta (cooking oil)

Matayarisho

Tia unga, chumvi na maji kiasi katika bakuli kisha koroga mpaka madonge yote yaondoke. Baada ya hapo tia yai na vitunguu kisha koroga tena mpaka mchanganyiko wote uchanganyike vizuri. baada ya hapo choma chapati zako kama kawaida (jinsi ya kuchoma unaweza kuangalia kwenye recipe yangu ya chapati za maji katika older posts) na baada ya hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

MAPISHI YA LADU

VIAMBAUPISHI

Unga – 6 vikombe

Samli – ½kikombe

Baking Powder – ½kijiko cha chai

Maziwa- 1 kikombe

Maji -Kisia kiasi kama unga bado mzito

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 5 vikombe

Maji – 2 1/2 vikombe

Vanilla – 2 vijiko vya chai

Rangi ya orange – 1 kijiko cha chai

Iliki ya unga – 1 Kijiko cha chai

MAANDALIZI

Changanya unga wa dengu, samli, baking powder pamoja na maziwa katika mashine ya keki (cake mixer).
Ukisha changanya angalia kama mchanganyiko wako umekua mwepesi kidogo kuliko wa keki, kama bado mzito basi ongeza maji kiasi.
Kisha weka mafuta kiasi kwenye karai,weka na samli kikombe kimoja, weka kwenye moto wa kiasi.
Mafuta yakisha pata moto, chukua kijiko kikubwa cha matundu chota mchanganyiko wako na kijiko cha kawaida tia kwenye kijiko cha matundu. Hakikisha kijiko cha matundu kiwe juu ya karai ili mchanganyiko wako uchuruzike ndani ya mafuta yalio pata moto.
Pika ndani ya mafuta mpaka iwive, ila usiache ikawa brown.
Toa mchanganyiko ulowiva tia ndani ya shira uliyo pika. Hakikisha shira iwe imepoa kabla ya kutia mchanganyiko huo.
Endelea kupika mchanganyiko wako mpaka uishe, kila ukitoa katika mafuta hakikisha unatia ndani ya shira.
Ukishamaliza wote kanda huo mchanganyiko ulokua ndani ya shira mpaka uone shira yote imekauka (yaani iwe imeingia ndani ya mchanganyiko).
Tupia zabibu kavu na lozi zilizo katwa, changanya na mkono.
Wacha mchanganyiko katika bakuli, funika na foil mpaka siku ya pili.
Siku ya pili chukua mchanganyiko kiasi katika mkono tengeneza mviringo (round).

MAANDALIZI YA SHIRA

Katika sufuria, tia sukari, maji, iliki, vanilla na rangi.
weka kwenye moto wacha ichemke mpaka itowe povu (bubbles) juu.
Kisha toa povu, wacha shira kwenye moto kama dakika 3.
Hakikisha shira yako iwe inanata kiasi kwenye vidole, lakini iwe nyepesi kidogo kuliko shira ya kaimati.

Shopping Cart
29
    29
    Your Cart
    Kitabu cha SMS Maalumu kwa Umpendaye
    Kitabu cha SMS Maalumu kwa Umpendaye
    1 X Sh2,500 = Sh2,500
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About