Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya tambi za kukaanga

Kupika tambi ni kama ifuatavyo

VIAMBA UPISHI

Tambi pakti moja

Sukari ¾ kikombe cha chai

Mafuta ½ kikombe cha chai

Iliki kiasi

Maji 3 Vikombe vya chai

Vanilla / Arki rose 1-2 Tone

Zabibu Kiasi (Ukipenda)

JINSI YA KUPIKA TAMBI ZAKO

1. Zichambue tambi ziwe moja moja.

2. Mimina mafuta kwenye sufuria yakisha pata moto mimina
tambi,zigeuzegeuze mpaka zibadilike rangi na kuwa brown.

3. Punguza mafuta kwa kuyachuja na zirudishe jikoni.

4. Nyunyizia iliki zilizosagwa koroga kidogo na mimina maji na tia arki
na acha zichemke mpaka maji yakikaribia kukauka mimina sukari
koroga kidogo na punguza moto.
5. Kisha tia zabibu ukipenda, zifunike ili zikaukie vizuri.

6. Zikishakauka pakua kwenye sahani tayari kwa kuliwa

Kidokezi: Itategemea na aina za Tambi unazopika kwa kukisia maji, kama utaona hazijaiva unaweza kuongeza maji kidogo.

Mapishi ya Pilau Ya Mchicha

VIPIMO

Mchele – 3 Vikombe

Mchicha

Mafuta – 1/2 kikombe

Vitunguu maji – 2 vikubwa

Nyanya – 1

Viazi – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 3 vijiko vya supu

Vidonge vya supu (Stock cubes) – 3

Jiyrah (cummin powder) – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ya unga – 1 kijiko cha chai

Hiliki ya unga – 1/2 kijiko cha chai

Mdalasini – 1 kijiti

Maji (inategemea mchele) – 5 vikombe

Chumvi

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

1. Osha na roweka mchele.

2. Osha mchicha, chuja maji na katakata.

3. Katakata vitunguu maji, nyanya.

4. Menya na kata viazi vipande ukaange pekee vitoe weka kando.

5. Katika sufuria tia mafuta na kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi.

6. Tia thomu, bizari zote, kaanga kidogo kisha nyanya.

7. Tia mchicha kaanga kidogo kisha tia mchele, maji na vidonge vya supu, chumvi.

8. Koroga kidogo kisha tia viazi ulivyovikaanga, funika na acha uchemke kidogo katika moto mdogo mdogo.

9. Kabla ya kukauka maji, mimina katika chombo cha kupikia ndani ya oven (oven proof) au katika treya za foil, funika vizuri na upike ndani ya oven moto wa 400º kwa dakika 15-20 upikike hadi uive.

10. Ukishaiva epua na tayari kuliwa na kitoweo chochote upendacho.

Jinsi ya kupika Wali Wa Karoti Na Nyama

Viambaupishi: Wali

Mchele 3 Magi

Mafuta 1/4 kikombe

Karoti unakata refu refu 3

Vitunguu maji kata vikubwa vikubwa 1 kikubwa

Pilipli manga 1/2 kijicho chai

Hiliki 1/2 kijiko chai

Karafuu ya unga 1/4 kijiko cha chai

Mdalasini wa unga 1/2 kijiko cha chai

Zaafarani (ukipenda) roweka katika maji 1 kijiko cha chai

Zabibu kavu (ukipenda) 1/4 kikombe

Chumvi kiasi

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Kwenye sufuria tia mafuta na kaanga karoti kidogo.

2. Tia vitunguu kisha tia bizari zote.

3. Tia maji kiasi (kutegemea aina ya mchele) na chumvi

4. Tia mchele upike uwive.

5. Karibu na kuwvia tia zabibu ukipenda.

6. Funika endelea kuupika hadi uwive.

Viambaupishi kwa Nyama

Nyama 2 Ratili (LB)

Chumvi Kiasi

Mafuta 1/4 kikombe

Kitunguu (kata virefu virefu) 1 Kikubwa

Pilipili mboga kubwa 2

(ukipenda moja nyekundu moja kijani)

unazikata vipande virefu virefu.

Figili mwitu (celery) kata vipande Miche miwili

virefu virefu

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Chemsha nyama hadi iwive

2. Ikaange kwa mafuta hadi iwe nyekundu

3. Weka vitunguu, pilipili mboga na figili mwitu

4. Kaanga kidogo tu kama dakika moja.

Jinsi ya kuishi maisha marefu (Mambo ya kuzingatia ili uishi maisha marefu)

Kuishi ukiwa na afya na kuishi maisha marefu kunawezekana kwa kubadili hali ya maisha unayoishi inayoharibu afya yako mfano uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi,kutokufanya mazoezi na kutokula matunda na mbogamboga.

Mambo yanayoweza kukusaidia kuishi maisha marefu ni kama yafuatayo

  1. Kuuandaa mwili kwa maisha marefu kwa kufanya mazoezi
  2. Kuwa makini kutambua na kutibu matatizo ya kiafya
  3. Kuepuka mazingira na kufanya kazi kwa namna au kazi zinazoweza kudhuru maisha yako. Mfano kuendesha gari bila kufuata utaratibu, kutokuvaa vifaa vya kujikinga wakati wa kazi
  4. Epuka vitu vyenye sumu vinavyoweza kudhuru afya yako na kukuletea matatizo ya kiafya kama dawa za mimea na mifugo, zitumie kama inavyotakiwa
  5. Usinywe pombe, usivute sigara wala kutumia dawa za kulevya
  6. Kula mlo kamili
  7. Usile vyakula vyenye chumvi na mafuta mengi
  8. Kunywa maji mengi ili kusafisha mwili
  9. Epuka msongo wa mawazo

Mapishi ya Ugali Mchuzi Wa Samaki Nguru Wa Nazi Na Bamia Za Kukaanga

Vipimo Vya Ugali:

Unga wa mahindi/sembe – 4

Maji – 6 takriban

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chota unga kidogo katika kibakuli uchanganye na maji kidogo .
Weka maji mengineyo katika sufuria kwenye moto.
Changanya na mchanganyiko mdogo ufanya kama uji.
Kisha kidogo kidogo unaongeza sembe huku unakoroga na kuusonga ugali hadi uive.

Vipimo Vya Mchuzi Wa Samaki Wa Nazi

Samaki nguru – 5 vipande

Pilipili mbichi ilosagwa

Kitunguu maji kilosagwa – 1 kimoja

Nyanya ilosagwa – 2

Haldi/tumeric/bizari ya manjano – ¼ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 kamua

Tui la nazi zito – 2 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Baada ya kumuosha samaki, weka katika sufuria.
Tia chumvi, ndimu, pilipili mbichi ilosagwa.
Tia vitunguu na nyanya zilosagwa
Mkaushe kwa hivyo viungo, akianza kukauka tia tui la nazi.
Acha kidogo tu katika moto tui liwive mchuzi ukiwa tayari.

Vipimo Vya Bamia

Bamia – ½ kilo takriban

Nyanya kopo – 1 kijiko cha chai

Methi/uwatu/fenugreek seeds ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Dania/corriander ilosagwa – ½ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta – 1 kikombe cha kahawa

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata bamia kwa urefu.
Weka mafuta katika karai, kisha tia bizari zote na nyanya kopo, kaanga kidogo.
Tia bamia endelea kukaanga, kisha acha katika moto mdogomdogo ufunike.
Kila baada ya muda funua karai ukaange bamia hadi ziwive zikiwa tayari.

Jinsi ya kuandaa Pilau ya sosi ya soya, nyama na mboga

Mahitaji

Nyama isiyokuwa na mifupa – 1 ½ Lb(ratili)
Mchele wa Basmati (rowanisha) – 3 Magi
Vitunguu maji – 2
Mchanganyiko wa mboga za barafu – 1 Magi
(karoti, mahindi, njegere)
Pilipili Mbichi – 3
Pilipili mboga kijani na nyekundu – 1
Pilipili manga – ½ kijiko cha chai
Chumvi – Kiasi
Sosi ya soya (soy sauce) – 5 Vijiko vya supu
Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 Kijiko cha supu
Mchanganyiko wa bizari (garam masala) – 1 Kijiko cha supu
Kotmiri iliyokatwa – ½ Kikombe
Mafuta ya kukaangia – Kiasi

Namna Ya Kutaarisha

Ndani ya sufuria, tia mafuta yakipata moto kaanga vitunguu mpaka ziwe rangi ya hudhurungi.
Kisha tia nyama iliyokatwa vipande vidogo vidogo pamoja na maji ya kiasi na viungo vyote isipokuwa mchele, mboga zote na kotmiri. chemsha mpaka nyama iwive na maji yakauke.
Halafu changanya na mboga na iwache kwa muda wa dakika kumi kisha tia kotmiri na umimine kwenye bakuli au treya ya oveni na uweke kando.
Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja, kisha umwagie juu ya ile treya ya nyama.
Nyunyizia mafuta na sosi ya soya na ipike katika oveni moto wa 350° kwa muda wa dakika 20 hivi.
Ukishawiva, uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Ufuta Na Jam

VIAMBAUPISHI

Unga vikombe 2

Sukari ya kusaga 1/4 Kikombe

Siagi 250 gms

Jam kisia

Ufuta kisia

Vanilla 1 kijiko cha chai

MAPISHI

Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai, sukari na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.
Tia baking powder, na unga na changanya kwa mkono vizuri.
Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Bonyeza kila kiduara katikati kwa kidole, kisha weka jam, halafu juu yake paka mayai na unynyuzie ufuta.
Pika katika moto wa chini 350ºF kwa muda wa dakika 20-25.
Tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali Mweupe Kwa Mchuzi Wa Kuku Wa Balti

Vipimo

Kuku 1 mkate vipande vipande

Vitunguu 3 katakata (chopped)

Nyanya 5 zikatekate (chopped)

Tangawizi mbichi ilokunwa au ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Thomu (kitunguu saumu) kilosagwa kijiko 1 cha kulia

Bizari mchanganyiko (garam masala) kijiko 1 cha chai

Jira/bizari ya pilau (cummin powder) kijiko 1 cha chai

Dania/gilgilani ilosagwa (coriander powder) kijiko 1 cha chai

Mtindi/maziwa lala (yoghurt) vijiko vya kulia 4 mjazo au paketi moja ndogo.

Malai ya kupikia (cooking cream) kikombe 1

Kasuri methi (majani makavu ya uwatu/dried fenugreek leaves) 1 kijiko cha kulia

Mafuta ya kupikia ½ kikombe

Chumvi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha kuku vizuri mwache achuje maji.
Weka mafuta katika sufuria kaanga vitunguu mpaka vianze kugeuka rangi ya brown hafifu. Kisha tia tangawizi na thomu ukaange.
Tia kuku ukaange mpaka ageuke mweupe kisha tia nyanya endelea kukaanga ziwive.
Piga mtindi vizuri katika kibakuli uwe nyororo.
Epua sufuria weka kando kisha tia mtindi uchanganye vizuri pamoja na kuku.
Rudisha katika moto acha uchanganyike na kuku kidogo kisha mwagia malai ya kupikia (cooking cream)
Tia kasuri methi/majani makavu ya uwatu yaliyovurugwa. Acha katika moto dakika 1 tu.
Epua umimine katika chombo na nyunyizia ikiwa tayari kuliwa na wali mweupe.

Mapishi ya wali wa Kiafrika Mangaribi

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 2 na 1/2)
Vitunguu (onion 2)
Nyanya ya kopo (tin tomato kopo 1)
Tangawizi (ginger paste kijiko 1 cha chakula)
Kitunguu swaum (garlic paste kijiko 1 cha chakula)
Paprika (kijiko 1 na 1/2 cha cha chai)
Pilipil (scotch bonnet pepper 1)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Maggi cubes 3(unaweza kutumia yenye ladha ya chicken, beef au vegetable. Inategemea unasevu na mchuzi wa aina gani)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka mchele kwa muda wa dakika 10.Katakata vitunguu kisha weka pembeni, saga pamoja nyanya ya kopo,pilipili, tangawizi na kitunguu swaum kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikiiva tia curry powder, maggi cubes, chumvi na paprika na uchanganye vizuri. Kisha tia mchanganyiko wa nyanya na uupike mpaka uive. Baada ya hapo tia mchele na maji na uupike mpaka ukaribie kuiva kisha ugeuze na umalizie kwa kutia njegere na umalizie kuupika mpaka uive. baada ya hapo utakuwa tayari kuseviwa na mboga yoyote kama kuku, nyama, samaki au assorted meat (Mchanganyiko wa utumbo, makongoro na nyama), Hapo mimi nili-save na mchuzi wa kuku wa kienyeji.

Mapishi ya mboga ya mnavu

Viamba upishi

Mnavu mkono 1
Kitungu 1
Karoti 2
Maziwa kikombe 1
Mafuta vijiko viubwa 4
Karanga zilizosagwa kikombe 1
Chumvi kiasi ½

Hatua

• Chambua mnavu, osha na katakata.
• Menya, osha na katakata kitunguu.
• Osha, menya na kwaruza karoti.
• Kaanga karanga, ondoa maganda na saga zilainike.
• Kaanga vitunguu na karoti mpaka zilainike ukikoroga.
• Weka mnavu na chumvi koroga sawa sawa, funika kwa dakika 5-10 (kama ni kavu weak maji kidogo).
• Changanya maziwa na karanga, ongeza kwenye mnavu ukikoroga kisha punguza moto kwa dakika 5.
• Onja chumvi na pakua kama kitoweo.
Uwezekano
Weka nyanya kidogo.
Tumia tui la nazi au krimu badala ya maziwa.
Weka nyama au dagaa au Mayai badala ya Karanga.

Upishi na Karanga na Mbegu: Vyakula vya Virutubishi

Upishi wa vyakula vya virutubishi kama vile karanga na mbegu ni muhimu sana kwa afya yetu. Kwa bahati nzuri, vyakula hivi vina ladha tamu na virutubishi vingi, ambavyo vinaweza kuboresha afya yetu kwa njia nyingi. Kwa hiyo, leo, katika makala hii, nataka kuzungumzia faida za upishi wa vyakula hivi na jinsi unavyoweza kuyatayarisha ili kuwa na chakula bora zaidi.

  1. Mbegu kama vile alizeti, ufuta, na maboga ni matajiri katika asidi ya mafuta muhimu, ambayo ni muhimu kwa afya ya moyo na mishipa ya damu.🌻🌰
  2. Karanga nazo zina protini nyingi, mafuta yenye afya, na nyuzinyuzi, ambazo zinaweza kusaidia kudhibiti kisukari na kukidhi mahitaji ya protini ya mwili.🥜💪
  3. Vyakula hivi vinaweza kuongezwa kwenye sahani za mboga, kachumbari au hata katika smoothies za asubuhi ili kuongeza ladha na virutubishi.🍛🥗🥤
  4. Kwa upande mwingine, unaweza pia kutumia karanga na mbegu kama vitafunio vya afya kati ya milo yako.🍿🌰
  5. Kwa kuwa karanga na mbegu hazina cholesterol, zinaweza kuwa chaguo bora badala ya vitafunio vingine vyenye mafuta mabaya.🚫🍔
  6. Upishi wa vyakula hivi kunaweza kufanywa kwa njia nyingi tofauti. Kwa mfano, unaweza kuchoma karanga kwenye sufuria kavu au kuzipika kwa maji chumvi.🌰🔥
  7. Kwa mbegu, unaweza kuzikaanga kwenye mafuta kidogo au kuzitumia kama kiungo katika mikate, keki, au saladi.🥖🥗
  8. Kumbuka tu kuwa, ili kuhakikisha unapata virutubishi vyote kutoka kwa vyakula hivi, ni muhimu kula kiasi cha kutosha na kupunguza matumizi ya viungo vingine hatari kama vile mafuta ya ziada na sukari.🚫🍩🍟
  9. Vyakula vya virutubishi kama vile karanga na mbegu vinafaa kwa watu wa kila umri na wanaweza kusaidia kuboresha afya ya watoto, vijana, watu wazima na wazee.👶👵
  10. Kwa mfano, watoto wanaweza kula mlo ulio na karanga na mbegu kwa kutengeneza sandwich ya karanga au kuongeza mbegu kwenye tambi au supu.🥪🍜
  11. Watu wazima wanaweza kujaribu kuchanganya karanga na mbegu katika sahani za mboga au kwenye saladi ili kuongeza ladha na virutubishi.🥙🥗
  12. Na kwa watu wazee, vyakula hivi vinaweza kusaidia kuboresha afya ya akili na kusaidia kuzuia magonjwa ya kuzeeka kama vile ugonjwa wa Alzheimer’s.🧠💡
  13. Karanga na mbegu pia zinaweza kuwa chaguo bora kwa watu ambao wanahitaji kupata nguvu zaidi, kama vile wanariadha au watu wanaofanya kazi ngumu kimwili.💪🏃‍♀️
  14. Kwa kuwa karanga na mbegu zina kiwango cha juu cha kalori, ni muhimu kuzingatia kiasi unachokula ili kuepuka kuongeza uzito kupita kiasi.⚖️📉
  15. Kwa hiyo, kwa kumalizia, nataka kukuhimiza kuongeza vyakula vya virutubishi kama vile karanga na mbegu katika lishe yako ya kila siku. Chakula chako kitakuwa si tu kitamu zaidi, lakini pia kitajaa virutubishi muhimu kwa afya yako. Kumbuka tu kula kwa kiasi na kuzingatia lishe yenye usawa.🌰🍽️

Kwa maoni yako, je, wewe hula karanga na mbegu mara ngapi kwa wiki? Je, unapenda kuzipika vipi? Ningependa kusikia kutoka kwako! 🌰🍽️🤔

Mapishi ya chipsi

Mahitaji

Viazi (potato) 1/2 kilo
Mafuta ya kukaangia (veg oil)
Chumvi

Matayarisho

Menya viazi kisha vioshe na vikaushe maji yote kwa kutumia kitchen towel.Baada ya hapo katakata katika shape ya chips uzipendazo either nyembamba au nene kisha zikaushe tena maji na uzitie chumvi. Baada ya kuzitia chumvi tu zitie kwenye mafuta ya kukaangia straightaway (hakikisha mafuta yasiwe ya moto sana kwani utazibabua) Zipike upande mmoja ukiiva geuza upande wa pili. Baada ya hapo endelea kuzipika uku ukiwa unazigeuzageuza mpaka kwa nje ziwe light brown na crisps.Baada ya hapo zitoe na uziweke kwenye kitchen towel ili zichuje mafuta na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Supu ya makongoro

Mahitaji

Makongoro (miguu ya ng’ombe) kiasi
Limao 1 kubwa
Kitunguu swaum
Tangawizi
Chumvi
Pilipili

Matayarisho

Safisha makongoro kisha yatie kwenye pressure cooker. Kisha tia kitunguu swaum, tangawizi, chumvi,limao na maji kiasi. Baada ya hapo yachemshe mpake yaive na yawe malaini na pia ubakize supu kiasi inaweza kuchukua kama dk 45 au saa 1 hivi. Baada ya hapo yaipue na upakue supu yako kwenye bakuli katia pilipili kiasi kisha itakuwa tayari kwa kuliwa.

Note:
Ukiwa unanunua makongoro hakikisha unachukuwa yale yasiyokuwa na manyoya na pia
hakikisha usiyachemshe kupitiliza kwani yakiwa malaini sana utashindwa kuyaenjoy.

Mchemsho wa samaki na viazi

Mahitaji

Samaki mbichi (1)
Viazi mbatata (3)
Nyanya (1)
Kitunguu maji
Limao
Kitunguu saumu
Tangawizi
Chumvi
Pilipili
Vegetable oil

Matayarisho

Safisha samaki kisha mmarinate na tangawizi, kitunguu swaum, chumvi na limao kwa muda wa masaa mawili. Baada ya hapo menya viazi na uvikate vipande vidogo kisha vioshe na viweke kwenye sufuria yenye maji kiasi kwa ajili ya kuvichemsha. Viinjike jikoni na uviache vichemke kwa dakika 7. Vikisha chemka tia samaki, katia kitunguu,pilipili, chumvi, limao, vegetable oil na nyanya na uache supu ichemke mpaka samaki na viazi vitakapoiva. baada ya hapo supu itakuwa tayari kwa kuliwa.

Madhara ya nyama nyekundu kwa mtu mwenye VVU

Kuna nyama za aina mbili, nazo ni nyama nyeupe na nyama nyekundu.

Nyama nyeupe

Hizi ni nyama zitokanazo na samaki, kuku, ndege wa aina zote, bata, wadudu

Nyama nyekundu

Hutokana na ng’ombe, mbuzi, kondoo,nguruwe na wanyama wa porini.

Nyama ina virutubishi vingi muhimu kwa afya ya binadamu kama protini, vitamini na madini. Madini ya chuma yanayopatikana kwenye nyama ni rahisi sana kusharabiwa (kufyonzwa) mwilini na ni muhimu kwa kuongeza wekundu wa damu.
Uwezo wa miili ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kuyeyusha chakula na kusharabu (kufyonza) virutubishi hupungua. Utumiaji wa nyama nyekundu kwa wingi unaweza kuwaletea matatizo hasa katika uyeyushwaji tumboni kwani nyama nyekundu si rahisi kuyeyushwa ukilinganisha na nyama nyeupe.

Hata hivyo katika nchi yetu watu walio wengi wanatumia nyama kwa kiasi kidogo sana na mara chache. Si vyema watu hawa waache kabisa nyama nyekundu. Jambo la muhimu ni kutumia njia mbalimbali ili kuifanya nyama hii iyeyushwe kwa urahisi tumboni.

Namna ya kusaidia uyeyushwaji ni pamoja n a : –

• Kutafuna vizuri au kutumia nyama ya kusaga (kwa wanaoipata).
• Kupika nyama na viungo vinavyosaidia kulainisha kama vile papai bichi, limao, vitunguu saumu n.k.
• Kula nyama pamoja na papai

Kwa hiyo, kwa anayepata nyama nyekundu kwa wingi, kupunguza kiasi cha nyama hiyo na kuongeza kiasi cha nyama nyeupe. Na kwa yule asiyepata nyama nyeupe, apatapo nyama nyekundu asiache kutumia kwani ina umuhimu mwilini mwake.

Mapishi ya Dagaa wa nazi, nyanya chungu na bamia

Mahitaji

Dagaa waliokaushwa (dried anchovy 2 kikombe cha chai)
Bamia (okra 5)
Nyanya chungu (garden egg 5)
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)
Nyanya (fresh tomato 2)
Kitunguu (onion 1)
Curry powder 1/2 ya kijiko cha chai
Turmeric powder 1/2 kijiko cha chai
Limao (lemon 1/2)
Chumvi (salt kiasi)
Pilipili (scotch bonnet 1)
Mafuta (veg oil)

Matayarisho

Safisha dagaa na uwaweke pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikianza kuwa vya brown tia dagaa wakaange kidogo kisha tia chumvi, pilipili, curry powder, turmeric, bamia na nyanya chungu, koroga vizuri mpaka mchanganyiko wote uchanganyike vizuri kisha tia nyanya na ufunike. Pika mpaka nyanya iive kisha kamulia limao,na pia hakikisha nyanya chungu na bamia zimeiva kidogo(usiache mpaka ziive sana manake zitavurugika pindi utakapotia tui la nazi) kisha malizia kwa kutia tui la nazi na uache lichemke mpaka rojo ibakie kidogo. Hakikisha nyanya chungu na bamia zimeiva ndo uipue. Na hapo dagaa wako watakuwa tayari kwa kuliwa na wali au ugali.

Jinsi ya kupika Pilau Ya Nafaka Na Nyama Ya Kusaga

Viambaupishi

Mchele 3 vikombe

Nyama ya kusaga 1 LB

Mchanganyiko wa Nafaka (upendavyo) 1 kikopo

(maharagwe, njegere, mbaazi, na kadhalika)

Vitunguu maji kata vipande vipande 3 vya kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi 2 vijiko vya supu

Mafuta ½ Kikombe

Mchanganyiko wa bizari (Garam Masala) 2 vijiko vya chai

Vipande vya supu (Maggi cubes) 3

Maji (inategemea mchele) 5

Chumvi Kiasi

Jinsi ya kuandaa na kupika

1) Osha mchele na roweka.

2) Weka mafuta katika sufuria na kaanga vitunguu mpaka viwe brown.

3) Tia Thomu na tangawizi, kaanga kidogo.

4) Weka nyama ya kusaga, chumvi na garam masala, endelea kukaanga mpaka nyama iwive.

5) Mwaga maji yaliomo katika kopo la nafaka na utie nafaka pekee humo.

6) Tia maji na vipande vya supu (Maggi cubes) huku unavivuruga, koroga kidogo.

7) Tia mchele, koroga kidogo.

8) Funika na pika kwa moto mdogo mpaka karibu na kukauka ukikorogoka kidogo. (kama unavyopika pilau ya kawaida)

9) *Epua uipike katika moto wa oven 350-400 Deg kwa muda wa dakika 15.

*Kama sufuria uliyotumia sio ya kupikia katika oven, mimina katika chombo chochote kinachotumika kwa oven kama bakuli la pyrex au treya za foil.

10) Pakua katika sahani na iko tayari kuliwa.

Mapishi – Saladi ya Matunda

Matunda ni mojawapo wa kundi la vyakula, ni muhimu sana kwa afya bora. Matunda yakitengenezwa vizuri yanavutia sana na yanakuwa ni chakula kizuri sana.

Mahitaji

Embe iliyoiva kiasi
Nanasi
Tango
Tikiti maji
Zabibu
Papai

Matayarisho

1. Ondoa maganda kwenye embe, nanasi, tango, papai na tikiti maji kisha kata kata vipande vidogo vidogo vya mraba

2. Changanya vipande vya matunda kwenye bakuli safikisha weka na zabibu zilizotolewa kwenye kikonyo chake.

3. Weka kwenye friji yapate ubaridi kidogo

4. Saladi yako tayari kwa kuliwa

Waweza kula saladi hii kama mlo wa kati au kama mlo kamili wa usiku.

Jinsi ya kutengeneza Wali Wa Dengu Kwa Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 Vikombe

Dengu – 2 vikombe

Viazi – 3 vikubwa

Kitunguu – 2 kubwa

Nyanya – 2

Pilipili mbichi kubwa – 3

Pilipilimanga – ½ kijiko cha chai

Garama Masala (bizari mchanganyiko) -1 kijiko cha chai

Supu ya vidonge (stock cubes) – 2 vidonge

Chumvi – kiasi

Mafuta – ¼ kikombe

Zaafarani – 1 kijiko cha chai

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Dengu kama sio za tayari kwenye kopo, roweka na zichemshe hadi ziwive

Maandalizi ya Masala Ya Dengu:

Zaafarani – iroweke katika maji ya dafu dafu (warm) ya chini ya robo kikombe weka kando.
Osha mchele, roweka.
Menya viazi na vitunguu, katakata vitunguu, na nyanya , weka kando.
Katakata viazi vipande vidogo vidogo kwa umbo la mchemraba (cubes).
Katika sufuria tia mafuta yakipata moto, tia viazi ukaange kidogo kwa moto mdogo mdogo hadi kukaribia kuwiva, toa weka kando.
Kaanga vitunguu hadi vigeuka rangi ya hudhurungi isiyokoza (light brown) kisha tia nyanya ukaange kidogo.
Tia vidonge vya supu (stock cubes) uvivuruge katika mchanganyiko, katakata pilipili mbichi kwa urefu tia, uendelee kukakaanga. Tia bizari, chumvi.
Zima moto, changanya dengu na viazi katika mchanganyiko huo.

Mapishi ya Wali:

Chemsha mchele kama kawaida ya kupika wali mweupe, kiini kiwe kimewiva nusu yake.
Chuja maji kisha changanya katika mchanganyiko wa dengu.
Nyunyizia zaafarani, uchanganye wali na mchanganyiko kidogo tu.
Funika acha uive katika mtoto mdogo mdogo au tia katika oveni hadi uive kama kawaida ya kupika wali.
Pakua katiha sahani na tolea na samaki yoyote wa kukaanga.

Jinsi ya kutengeneza Nangatai

MAHITAJI

Unga wa ngano – 2 – 2 ¼ Vikombe

Siagi – 1 ½ Kikombe

Sukari – 1 Kikombe

Yai – 1

Vanilla -Tone moja

Baking Powder -kijiko 1 cha chai

Chumvi – Kiasi kidogo (pinch)

Unga wa Kastadi – 2 Vijiko vya supu

MATAYARISHO

Changanya vitu vyote isipokuwa unga.
Tia unga kidogo kidogo mpaka mchanganyiko uwe sawa.
Kisha fanya duara ndogo ndogo uzipange kwenye treya na utie rangi katikati.
Halafu zichome katika moto wa 300°F kwa muda wa dakika 20 – 25 na zisiwe browni .
Kisha panga kwenye sahani tayari kuliwa na chai.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About