Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya Chicken Curry

Leo wapendwa nitaenda kuzungumzia mapishi ya mchuzi wa kuku (chicken curry).

Mahitaji

Kuku mzima
Nyanya kubwa 3
Karoti mbili
Pilipili hoho
Kotmiri
Tangawizi
Kitunguu maji
Kitunguu saumu kidogo
Ndimu
Mafuta ya kupikia
Chumvi (pilipili ukipenda)

Matayarisho

1. Menya vitunguu saumu na tangawizi na uvitwange pamoja.
2. Katakata kuku vipande vidogo kisha ukamulie ndimu na kupaka mchanganyiko wa tangawizi na vitunguu saumu (kiasi tu).
3. Katakata vitunguu maji na pilipili hoho uweke pembeni.
4. Grind (Kwangua) kwenye grater nyanya na karoti pia uweke pembeni.
5.Katakata kotmiri vipande vidogo uweke pembeni.
6. Andaa kikaango na jiko.

Mapishi

1. Bandika kikaango jikoni na mafuta kiasi, yakishachemka weka vitunguu maji na kaanga hadi vimelainika na kuiva (hakikisha haviungui).
2. Weka pilipili hoho na karoti na endelea kukoroga hadi vyote viive na kulainika, Kisha weka chumvi.
3. Sasa weka vipande vya nyama koroga na funikia kwa dakika 3, kisha weka nyanya zako ulizo grind na koroga ili zichanganyike vizuri, vikishachanganyika weka kotmiri na pilipili kama utapenda. Acha vichemke kwa dakika 5. Hakikisha moto sio mkali sana.
4. Angalia kama nyama zimeiva vizuri kisha epua mchuzi wako.
5. Pakua kwenye bakuli na katakata kotmiri uweke kwa juu.
Unaweza kula kwa ugali, wali, ndizi rost au chipsi.

Mapishi ya Firigisi za kuku

Mahitaji

Filigisi (chicken gizzard) 1/2 kilo
Carrot iliyokwanguliwa 1
Nyanya 1/2 kopo
Vitunguu maji 1 kikubwa
Tangawizi/swaum 1 kijiko cha chai
Hoho 1 iliyokatwakatwa
Limao 1/2
Chumvi
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Chilli powder 1/4 kijiko cha chai
Mafuta
Chopped coriander

Matayarisho

Safisha filigisi kisha zikate vipande vidogo vidogo.Zichemshe pamoja na chumvi, limao na nusu ya tangawizi na swaum mpaka ziive (hakikisha unabakiza supu kidogo). Baada ya hapo kaanga vitunguu mpaka viwe vya brown kisha tia tangawizi na swaum iliyobakia na kaanga kidogo kisha tia nyanya. Zipike mpaka ziive kisha tia spice zote pamoja na chilli. Zipike kidogo kisha tia filigisi (bila supu kwanza) Zichanganye vizuri na uzipike kidogo. Baada ya hapo tia carrot na hoho na supu iliyobakia. Vipike pamoja mpaka viive na supu ibakie kidogo sana. Malizia kwa kutia coriander na uipue na hapo firigisi zako zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Madhara ya kula yai bichi

Yai bichi linaweza kuwa na vijidudu viitwavyo kwa kitaalamu “SALMONELLA” vinavyoweza kusababisha tumbo kuuma, kichefuchefu na pia kuharisha.
Vijidudu ya “Salmonella” vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa watoto, wazee na wale wenye hali dhaifu ya kimwili kama wagonjwa wa UKIMWI.

Pia yai bichi lililowazi linaweza kuwa zalio zuri la vimelea vya maradhi mbalimbali. Inashauriwa kupika yai mpaka liive kabisa, na kuhakikisha kwamba hakuna ute unaoteleza.

Kama ni yai la kuchemsha, lichemshwe kwa dakika kumi zaidi baada ya maji kuchemka. Pia ni muhimu kuhakikisha kwamba vyombo vilivyotumika k u k o rogea yai bichi vinaoshwa kwa maji na sabuni kabla ya kuvitumia tena kwa matumizi mengine ili kuepuka maradhi.

Jinsi ya kupika wali wa Tuna (samaki/jodari)

VIAMBAUPISHI VYA TUNA

Tuna (samaki/jodari) – 2 Vikopo

Vitunguu (kata kata) – 4

Nyanya zilizosagwa – 5

Nyanya kopo – 3 Vijiko vya supu

Viazi (vilivyokatwa vipande vidogo – cubes) – 4

Dengu (chick peas) – 1 kikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic)&Tangawizi iliyosagwa 1 Kijiko cha supu

Hiliki – 1/4 kijiko cha chai

Mchanganyiko wa bizari – 1 kijiko cha supu

Chumvi – kiasi

Pilipili manga – 1 Kijiko cha chai

Vipande cha Maggi (Cube) – 2

VIAMBAUPISHI VYA WALI

Mchele – 3 Vikombe vikubwa (Mugs)

Mdalasini – 2 Vijiti

Karafuu – chembe 5

Zaafarani – kiasi
Jirsh (Komamanga kavu au zabibu kavu -raisins) – 1/2 Kikombe

JINSI YA KUANDAA

Kosha Mchele na roweka.
Kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi (brown) chuja mafuta uweke kando.
Kaanga viazi, epua
Punguza mafuta, kaanga nyanya.
Tia thomu/tangawizi, bizari zote, vipande vya Maggi, nyanya kopo, chumvi.
Mwaga maji ya tuna iwe kavu, changanyisha kwenye sosi.
Tia zaafarani kidogo katika sosi na bakisha ya wali.
Chemsha mchele pamoja na mdalasini na karafuu.
Karibu na kuwiva, chuja maji utie katika chombo cha kupikia katika jiko (oven)
Nyunyizia zaafarani, mwagia vitunguu, viazi, na dengu juu ya wali.
Mwagia sosi ya tuna na pambia jirshi (au zabibu).
Funika wali na upike katika jiko moto wa 450º kwa muda wa kupikika wali. Epua upakue.

Mapishi ya Pilau Ya Sosi Ya Soya Na Mboga

Viambaupishi

Kuku (mkate mkate vipande) 1

Mchele wa Basmati (rowanisha) 3 magi

Mdalasini 1 mchi mmoja

Vitunguu maji (vilivyokatwa vyembamba) 6

Mchanganyiko wa mboga za barafu 1 magi

(karoti, mahindi, njegere)

Kabichi (iliyokatwa katwa nyembamba) 1 magi

Pilipili mbichi (iliyosagwa) 3

Pilipili boga iliyokatwa vipande vidogo vidogo 1

Pilipili manga 1 kijiko cha chakula

Chumvi 1 kijiko cha chakula

Sosi ya soya (soy sauce) 5 vijiko vya chakula

Kotmiri iliyokatwa katwa 1 magi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa 2 vijiko vya chakula

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Tia mafuta ndani ya karai. Yakipata moto kiasi, mimina vitunguu maji na mdalasini 1 mzima kaanga. Itachukua muda kidogo. Kaanga mpaka viwe rangi ya hudhurungi (brown). Viepue na uweke kando.

2. Ndani ya sufuria kubwa, mimina kuku, chumvi, thomu na tangawizi, sosi ya soya, pilipili manga, pilipili mbichi, chemsha mpaka kuku awive na maji yakauke.

3. Changanya vitunguu ulivyokaanga, kabichi, pilipili, mboga, kotmiri, mchanganyiko wa mboga za barafu na weka kwa muda wa dakika tano au kumi. Tia na mafuta kidogo uliyokaangia vitunguu .

4. Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja. Ukishauchuja umwagie katika masala ya kuku.

5. Nyunyizia mafuta kidogo uliokaangia vitunguu.

6. Weka moto mdogo mpaka wali ukishawiva. Uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa.

KIDOKEZO:

Unaweza kuupika wali huo ndani ya jiko, yaani badala ya kutia masala kwenye sufuria ukayatia katika bakuli au treya ya jiko (oven), kisha ukamwagia wali uliouchuja humo na kuupika kaitka moto wa 400-450 Deg kwa muda wa dakika 15-20.

Jinsi ya kuandaa Vileja Vya Karanga

MAHITAJI

Mayai 5

Sukari 450gm (1 lb)

Unga wa Ngano 1 kg

Siagi 450gm (1 lb)

Baking powder ½ Kijiko cha chai

Unga wa Custard Vijiko 2 vya chakula

Karanga za kusaga 250gm

Jam ½ kikombe

MAANDALIZI

Chukua bakuli la kiasi, weka sukari na siagi.
Changanya sukari na siagi kwa kutumia mashine ya kukorogea keki (cakemixer), mpaka sukari ichanganyike na siagi.
Vunja yai moja moja na weka kiini chake kwenye mchanganyiko wa sukari na siagi, endelea kuchanganya mpaka ichanganyike vizuri. Hifadhi ute wa mayai ndani ya kibakuli.
Mimina unga wa ngano ndani ya mchanganyiko wako huku ukichanganya Changanya unga wa custard na baking powder.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Vichovye viduara ndani ya ute wa yai kisha zimwagie unga wa karanga na kuzipanga kwenye tray ya kuchomea.
Weka dole gumba kati kati ya kila kiduara na uweke jam.
Washa jiko (oven) 350F na uchome vileja vyako kwa dakika 20.
Toa vileja vyako vipoe na uviweke ndani ya sahani tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Supu ya makongoro

Mahitaji

Makongoro (miguu ya ng’ombe) kiasi
Limao 1 kubwa
Kitunguu swaum
Tangawizi
Chumvi
Pilipili

Matayarisho

Safisha makongoro kisha yatie kwenye pressure cooker. Kisha tia kitunguu swaum, tangawizi, chumvi,limao na maji kiasi. Baada ya hapo yachemshe mpake yaive na yawe malaini na pia ubakize supu kiasi inaweza kuchukua kama dk 45 au saa 1 hivi. Baada ya hapo yaipue na upakue supu yako kwenye bakuli katia pilipili kiasi kisha itakuwa tayari kwa kuliwa.

Note:
Ukiwa unanunua makongoro hakikisha unachukuwa yale yasiyokuwa na manyoya na pia
hakikisha usiyachemshe kupitiliza kwani yakiwa malaini sana utashindwa kuyaenjoy.

Jinsi ya kupika Visheti Vya Kastadi Vya Shepu Ya Kombe

Viamba upishi

Unga wa ngano 1 Kilo

Siagi ¼ kilo

Mayai 2

Kastadi (custard) 3 vijiko vya supu

Baking powder 1 kijiko cha chai

Maziwa 1 ½ gilasi

Mafuta Ya kukaangia kiasi katika karai

Maandalizi na upikaji

Weka unga katika bakuli kubwa kisha changanya na unga wa kastadi na baking powder.
Tia siagi uchanganye vizuri.
Tia mayai, kisha maziwa ya baridi uchanganye vizuri usiukande sana.
Fanya madonge kisha kata vipande vidogovidogo kisha ubonyeze kwa kidole uvikwaruze kwenye chujio lenye tundu itokee shepu (design) yake.

5- Tia mafuta katika karai yakipata moto, kaanga visheti hadi viive. Usiache hadi vikageuka rangi sana.

6- Eupua, weka katika sufuria au chombo kikubwa kusubiri shira.

Vipimo Vya Shira

Sukari ½ kilo

Hiliki ilosagwa 1 kijiko cha chai

‘arki (rose flavor) 5 matone

Maji 1 gilasi

Namna Ya Kutyarisha

Changanya sukari na maji uipike hadi iwe nzito.
Ukiona mapovu yanatoka tia hilik na ‘arki .
Mwagia katika visheti uchanganye vizuri hadi vishike na sukari.

Mapishi ya wali Wa Nazi Kwa Mchuzi Wa Nyama Ng’ombe Na Mchicha

Wali Wa Mpunga

Mchele wa mpunga – 4 Vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha

Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.

Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Mchuzi wa nyama Ng’ombe

Nyama – 1 kilo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa -2 viijiko vya supu

Viazi/mbatata – 2

Kitunguu maji kilokatwakawa (slice ndogo) – 2

Nyanya/tungule – 4

Nyanya kopo – 3 vijiko vya supu

Majani ya mchuzi/mvu – 3 msongo (bunches)

Bizari ya mchuzi (simba 2) – I kijiko cha chai

Ndimu – 1 kamua

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama katika sufuri, tia kijiko kimoja cha kitunguu thomu na tangawizi, chumvi, ndimu na chemsha nyama hadi iwive na ibakie supu yake kidogo.
Weka mafuta katika sufuri nyingine, kaanga kitunguu. Vinapogeuka rangi tia majani ya mchuzi endelea kukaanga hadi vigeuke rangi ya hudhurungi (golden brown)
Tia nyanya/tungule, viazi/mbatata, endelea kukaanga mpaka nyanya ziive.
Tia nyama na supu yake kisha tia nyanya ya kopo, kotmiri, bizari ya mchuzi, chumvi uache mchuzi kidogo katika moto hadi viazi viive vikiwa tayari.

Mboga Mchicha

Mchicha – 4 michano/vifungu

Kitunguu – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 3

Nyanya/tungule – 2

Tui la nazi zito – 1 kikombe cha chai

Chumvi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mboga iache ichuje maji.
Ikatekate kisha weka katika sufuria.
Katika kitunguu maji, kitunguu thomu kisage au kikatekate kidogodogo (chopped), nyanya.
Weka jikoni ipikike kwa maji yake na mvuke.
Tia tui endelea kuweka katika moto mdogomdogo hadi ikaribie kukauka ikiwa tayari.

Jinsi ya kupika Biriani Ya Nyama Mbuzi Ya Mtindi Na Zaafaraan

Vipimo – Nyama

Nyama mbuzi – 1 kilo

Kitunguu menya katakata – 1

Nyanya/tungule – 2

Thomu (kitunguu saumu/garlic) saga – 5 chembe

Tangawizi mbichi – kuna/grate au saga – 1 kipande

Pilipili mbichi saga – 2

Bizari ya pilau nzima (cumin seeds) – ½ kikombe cha kahawa

Mdalasini – 1 kijiti

Karafuu nzima – 5 chembe

Gilgilani/dania (coriander seeds) – ½ kikombe cha kahawa

Bizari ya mchuzi – 1 Kijiko cha supi

Chumvi – Kiasi

Mtindi – 1 glass

Hiliki ilopondwa – 2 vijiko vya chai

Vitunguu – menya katakata slices kwa ajili ya kukaanga- 7- 9

Mafuta – Kiasi ya kukaangai vitunguu

Vipimo – Wali

Mchele wa pishori/basmati – 4 glass

Zaafarani roweka katika kikombe cha kahawa – Kiasi

Mafuta – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katika sufuria, changanya nyama pamoja, kitunguu kimoja, tangawizi, thomu, nyanya, na viungo vyake isipokuwa mtindi, hiliki na vitunguu vilobakia.

Tia maji kisha funika ichemke mpaka iwive nyama na ikauke supu.

Tia mtindi na hiliki changanya pamoja.

Weka mafuta katika karai, kaanga vitunguu mpaka viwe rangi ya hudhurungi. Toa uchuje mafuta. Kisha viponde ponde kwa mkono uchanganye na nyama.

Chemsha mchele uive nusu kiini, mwaga maji.

Mimina katika nyama utie zaafarani, funika upike wali hadi uwive.

Epua ukiwa tayari.

Jinsi ya kupika Pilau Ya Nafaka Na Nyama Ya Kusaga

Viambaupishi

Mchele 3 vikombe

Nyama ya kusaga 1 LB

Mchanganyiko wa Nafaka (upendavyo) 1 kikopo

(maharagwe, njegere, mbaazi, na kadhalika)

Vitunguu maji kata vipande vipande 3 vya kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi 2 vijiko vya supu

Mafuta ½ Kikombe

Mchanganyiko wa bizari (Garam Masala) 2 vijiko vya chai

Vipande vya supu (Maggi cubes) 3

Maji (inategemea mchele) 5

Chumvi Kiasi

Jinsi ya kuandaa na kupika

1) Osha mchele na roweka.

2) Weka mafuta katika sufuria na kaanga vitunguu mpaka viwe brown.

3) Tia Thomu na tangawizi, kaanga kidogo.

4) Weka nyama ya kusaga, chumvi na garam masala, endelea kukaanga mpaka nyama iwive.

5) Mwaga maji yaliomo katika kopo la nafaka na utie nafaka pekee humo.

6) Tia maji na vipande vya supu (Maggi cubes) huku unavivuruga, koroga kidogo.

7) Tia mchele, koroga kidogo.

8) Funika na pika kwa moto mdogo mpaka karibu na kukauka ukikorogoka kidogo. (kama unavyopika pilau ya kawaida)

9) *Epua uipike katika moto wa oven 350-400 Deg kwa muda wa dakika 15.

*Kama sufuria uliyotumia sio ya kupikia katika oven, mimina katika chombo chochote kinachotumika kwa oven kama bakuli la pyrex au treya za foil.

10) Pakua katika sahani na iko tayari kuliwa.

Mapishi ya Samaki wa kupaka

Mahitaji

Samaki (Tilapia 2)
Nyanya ya kopo (Tomato tin 1)
Kitunguu (Onion 1)
Tangawizi (ginger kiasi)
Kitunguu swaum (garlic clove )
Mafuta (Vegetable oil)
Pilipili (scotch bonnet pepper 1)
Tui la nazi zito (coconut milk 2 vikombe vya chai)
Curry powder 1/2 cha kijiko cha chai
Binzari nyembamba ya unga (ground cumin 1/2 kijiko cha chai
Binzari manjano (turmaric 1/2 kijiko cha chai
Chumvi (salt)
Limao (lemon 1)
Giligilani (fresh coriander)

Matayarisho

Marinate samaki na chumvi, limao, kitunguu swaum, tangawizi kwa muda wa masaa 6 au zaidi. Baada ya hapo wakaange au waoke katika oven mpaka waive ila usiwakaushe sana. Baada ya hapo saga pamoja nyanya ya kopo, kitunguu maji, kitunguu swaum na tangawizi. Kisha bandika huo mchanganyiko jikoni na upike mpaka ukauke maji kisha tia mafuta, binzari zote, curry powder, chumvi na pilipili na upike kwa muda wa dakika 5. Baada ya hapo tia maji kidogo (kama 1/2 kikombe) pamoja na tui la nazi. Acha uchemke mpaka tui liive na mchuzi ubakie kiasi. Baada ya hapo waweke samaki kwenye sufuria ya kuokea na kisha umwagie huo mchuzi juu ya hao samaki na owaoke (bake) kwa muda wa dakika 20. Ukisha toa kwenye oven katakata giligilani na utie kwenye hao samaki na hapo watakuwa tayari kwa kuliwa. unaweza kuwala na wali, ugali au chapati

Mapishi ya Boga La Nazi

Vipimo

Boga la kiasi – nusu yake

Tui zito la nazi 1 ½ gilasi

Sukari ½ kikombe

Hiliki ½ kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Menya boga kisha katakata vipande vya kiasi.
Weka katika sufuri tia maji kiasi ya kuchemshia na kuwiva bila ya kubakia maji mengi.
Changanya tui na sukari na hiliki kisha mimina juu ya boga wacha katika moto dakika chache tu bila ya kufunika.
Epua mimina katika chombo likiwa tayari.

Mapishi ya Wali Wa Mboga Na Samaki Wa Pink Salmon

Vipimo

Mchele 3 vikombe

Mboga mchanganyiko 1 kikombe

Samaki wa Pink Salmon 5 -6 vipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa 1 kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Pilipili manga ya unga ½ kijiko cha chai

Pilipili nyekundu ya unga ½ kijiko cha chai

Ndimu zilokamuliwa 2

Parsley kavu (aina ya kotmiri) 2 vijiko vya supu

Bizari ya mchuzi 1 kijiko cha supu

Kidonge cha supu (stock) 2

Mafuta ¼ kikombe

Maji ½ kikombe

Namna ya Kutayarisha Na Kupika

Samaki:

Katika kibakuli kidogo, changanya; kitunguu thomu, tangawizi, chumvi, pilipili zote za unga, ndimu, parsely, bizari ya mchuzi na mafuta vijiko viwili vya supu.

Pakaza kwenye samaki.

Weka vipande vya samaki katika treya ya oveni kisha uchome (grill) huku ukigeuza hadi samaki awive. Epua weka kando.

Wali:

Osha mchele roweka kisha uchemshe uive nusu kiini

Mwaga maji uchuje mchele

Weka mafuta katika sufura, tia mboga mchanganyiko kakaanga kidogo

Weka vidonge vya supu, tia maji ½ kikombe, tia chumvi kiasi

Mimina mchele uchanganye vizuri, kisha funika hadi uive wali ukiwa tayari

Pakua katika sahani pamoja na samaki

Mapishi ya Ugali, dagaa (wabichi) na matembele

Mahitaji

Dagaa wabichi (Fresh anchovies packet 1)
Unga wa ugali (corn meal flour 1/4 kilo) (unaweza kutumia unga wa choice uipendayo)
Matembele ya kukaushwa (dried sweet potato leaves, handful)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1)
Kitunguu maji (onion 2)
Limao (lemon 1/4)
Pilipili mbuzi nzima bila kukata (scotch bonnet pepper1, do not chop)
Chumvi (salt 1/2 ya kijiko cha chai)
Mafuta (vegetable oil)
Hoho (green pepper 1)
Kitunguu swaum (garlic 5 cloves)
Tangawizi (ginger 1 kijiko cha chai)
Binzari ya curry (Curry powder 1/2 kijiko cha chai)

Matayarisho

Safisha dagaa kwa kutoa vichwa na utumbo kisha waoshe na uwakaushe na kitchen towel na uwaweke pembeni. Baada ya hapo katakata, vitunguu na hoho kisha weka pembeni. Baada ya hapo weka sufuria jikoni na utie mafuta yakisha pata moto tia dagaa na uwakaange mpaka wawe wa brown, kisha tia kitunguu swaum,curry powder na tangawizi, kaanga kidogo kisha malizia kwa kutia vitunguu maji, hoho,pilipili,chumvi na ukamulie limao. Kaanga kwa muda wa dakika 3-4 na hakikisha vitunguu na hoho haviivi sana na hapo dagaa watakuwa tayari.

Baada ya hapo yaoshe na uyaloweka matembele (kama ni makavu) kwa muda wa dakika 15, Kisha yatoe na uyaweke kwenye sufuria pamoja na kitunguu, nyanya, chumvi ,kamulia limao kidogo, pilipili na maji kiasi. acha matembele yachemke kwa muda wa dakika 20 na uhakikishe yameiva kwa kuwa laini. Baada ya hapo yapike mpaka maji yote yakauke na mafuta yatok na hapo matembele yatakuwa tayari.

Ukisha maliza kupika dagaa na matembele andaa chungu cha ugali. Kwanza unatakiwa kuchemsha maji ya moto, kisha koroga pembeni unga kiasi katika maji ya baridi na utie kwenye maji yanayochemka, Fanya kama unatengeneza uji, uji wa ugali ukishachemka tia unga na uanze kuusonga mpaka ugali uive. Ukisha iva pakua na usevu na mboga tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4 vikombe

Maji – 6 kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria wacha yachemke hasa

Tia unga kidogo kidogo huku ukikoroga mpaka ukamatane

Punguza moto huku ukiendelea kuusonga

Endelea kusonga kwa dakika kadhaa mpaka uanze kuchambuka

Kisha mimina kwenye bakuli au sahani na itakuwa tayari

Vipimo Ya Upishi Wa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma Wa Nazi

Samaki:

Samaki wa Nguru – kiasi vipande 5 – 6

Pilipili mbichi – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 5 chembe

Tangawizi mbichi – 1 kipande

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha supu

Pilipili nyekundu ya unga – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 3 kamua

Chumvi – kiasi

Ukipenda mkate samaki vipande kiasi.
Saga vipimo vyote vinginevyo katika mashine. Mchanganyiko ukiwa mzito ongezea ndimu
Changanya pamoja na samaki upake vizuri vipande vya samaki
Acha kwa muda wa nusu saa vikolee mchanganyiko
Panga samaki katika treya ya kupikia ndani ya oveni, kisha mchome (grill) samaki huku ukigeuza hadi viwive.
Epua weka kando.

Kuandaa Mchuzi:

Nyanya/tungule – 3

Kitunguu – 2

Bizari ya manjano/haldi – ¼ kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi zito – 3 vikombe

Chumvi – kiasi

Katakata vitunguu na nyanya vidogodogo (chopped) weka kando

Weka mafuta katika karai au sufuria, kaanga vitunguu hadi vianze kugeuka rangi

Tia nyanya kaanga pamoja na tia bizari ya njano/haldi .

Tia tui la nazi, chumvi koroga .

Mwishowe tia vipande vya samaki na rojo lake litakalobakia katika treya, mchuzi uko tayari

Upishi na Matunda ya Mzabibu: Vitamu vyenye Antioxidants

Upishi na Matunda ya Mzabibu: Vitamu vyenye Antioxidants 🍇

Habari za leo wapenzi wa chakula na afya! Leo nataka kuzungumzia faida ya upishi na matunda ya mzabibu. Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, matunda haya matamu yanajulikana kuwa na virutubisho na antioxidants nyingi ambazo zinaweza kuleta manufaa makubwa kwa afya yetu. Kama AckySHINE, nina ushauri muhimu na maelezo kuhusu jinsi ya kufurahia vitu hivi vyenye faida ya ajabu. Soma makala hii ili kujua zaidi!

  1. 🍇 Faida ya kwanza ya matunda ya mzabibu ni kwamba yana antioxidants nyingi ambazo husaidia kupambana na athari za radicals huru katika mwili wetu. Hii husaidia kulinda seli zetu dhidi ya uharibifu na kuimarisha mfumo wetu wa kinga.

  2. 🍇 Kula matunda ya mzabibu kunaweza kusaidia kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo. Antioxidants zilizopo katika matunda haya husaidia kupunguza viwango vya cholesterol mbaya na kuboresha afya ya moyo.

  3. 🍇 Matunda ya mzabibu yana kiwango kizuri cha vitamini C, ambayo ni muhimu kwa afya ya ngozi yetu. Vitamini C husaidia kujenga collagen, ambayo ina jukumu kubwa katika kuifanya ngozi yetu ionekane nzuri na yenye afya.

  4. 🍇 Kwa kuwa na kiwango cha juu cha maji, matunda ya mzabibu yanaweza kusaidia katika kudumisha afya ya figo. Maji ya kutosha mwilini ni muhimu kwa kazi nzuri ya figo.

  5. 🍇 Pia, matunda haya yana kiwango kikubwa cha resveratrol, ambayo inajulikana kwa uwezo wake wa kupambana na uchochezi. Hii inaweza kuwa na manufaa sana kwa watu wenye matatizo ya uchochezi kama vile ugonjwa wa arthritis.

  6. 🍇 Kwa kuwa ni chanzo kizuri cha nyuzi za chakula, kula matunda ya mzabibu kunaweza kusaidia katika kudumisha afya njema ya utumbo wetu. Nyuzi hizi husaidia katika kuzuia matatizo ya kuvuja kwa utumbo na kuboresha mwendo wa utumbo.

  7. 🍇 Je, umewahi kusikia kuhusu mafuta ya mbegu za mzabibu? Mafuta haya yana virutubisho muhimu kama vile asidi ya linoleiki na vitamini E ambavyo husaidia kulinda ngozi yetu dhidi ya madhara ya mazingira na kuifanya iwe laini na yenye afya.

  8. 🍇 Kulingana na utafiti, matunda ya mzabibu yameonyeshwa kuwa na uwezo wa kuboresha kumbukumbu na afya ya ubongo. Polyphenols katika matunda haya yana jukumu katika kuboresha afya ya ubongo na kuzuia uharibifu wa seli za ubongo.

  9. 🍇 Matunda ya mzabibu ni chanzo kizuri cha nishati. Kwa sababu ya sukari asili iliyomo, matunda haya yanaweza kutoa nguvu na kuongeza kiwango chako cha nishati katika siku yako.

  10. 🍇 Kwa wale wanaopenda kupunguza uzito, matunda ya mzabibu yanaweza kuwa msaada mzuri. Kwa kuwa yana kiwango cha chini cha kalori na mafuta, yanaweza kusaidia katika kudhibiti hamu ya kula na kusaidia katika kupunguza uzito.

  11. 🍇 Kumbuka, ingawa matunda ya mzabibu ni yenye manufaa kwa afya, ni muhimu kula kwa kiasi. Kula matunda mengi sana ya mzabibu kunaweza kuwa na athari hasi kama vile kuongeza uzito na kuathiri viwango vya sukari mwilini.

  12. 🍇 Kwa upande mwingine, unaweza pia kufurahia faida za matunda ya mzabibu kupitia juisi yake. Juisi ya mzabibu inaweza kuwa chaguo nzuri kwa wale ambao hawapendi kula matunda yenyewe.

  13. 🍇 Je, umewahi kufikiria kutumia matunda ya mzabibu kwenye sahani yako ya salad? Matunda haya yanaweza kuongeza ladha na ladha ya kipekee kwenye saladi yako na pia kuongeza faida ya kiafya.

  14. 🍇 Unaweza pia kuongeza matunda ya mzabibu kwenye smoothie yako ya asubuhi. Itakupa ladha tamu na virutubisho muhimu kwa mwili wako.

  15. 🍇 Kwa kuhitimisha, matunda ya mzabibu ni chakula kizuri sana kwa afya yetu na inaweza kuongeza ladha katika milo yetu ya kila siku. Kama AckySHINE, napendekeza kujumuisha matunda haya matamu katika lishe yako na kufurahia faida zake nyingi!

Je, umewahi kula matunda ya mzabibu? Una maoni gani kuhusu faida zake? Tuambie katika sehemu ya maoni hapa chini! 🍇😊

Mapishi ya Bilinganya

Mahitaji

Bilinganya 2 za wastani
Nyanya kubwa 1
Kitunguu maji 1 kikubwa
Swaum 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/4
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Parpika 1/4 kijiko cha chai
Pilipili mtama 1/4 kijiko cha chai
Curry powder1/4 kijiko cha chai
Chumvi kiasi
Coriander
Olive oil

Matayarisho

Katakata bilinganya slice nyembamba kisha ziweke pembeni. Baada ya hapo kaanga kitunguu maji mpaka kiwe cha brown kisha tia swaum na spice zote, zikaange kidogo kisha tia nyanya na chumvi kiasi. Pika nyanya mpaka iive na itengane na mafuta. Baada ya hapo tia mabilinganya na ukamulie limao kisha punguza moto na uyafunike na mfuniko usioruhusu kutoa mvuke ili yaivie na huo mvuke. Baada ya hapo yaonje kama yameiva na malizia kwa kutia fresh coriander na baada ya hapo yatakuwa tayari kwa kuliwa. kwa kawaida mi hupendaga kuyalia na wali na maharage badala ya kachumari kwahiyo nakuwa naitumia hiyo kama kachumbari

Jinsi ya kuandaa Vileja Vya Tambi

MAHITAJI

Tambi (vermiceli Roasted) Mifuko 2

Siagi – 4 Vijiko vya supu

Maziwa (condensed) 300Ml

Lozi zilizokatwakatwa – 1 kikombe

Zabibu kavu – 1 Kikombe

Arki (essence) – 1 Kijiko cha supu

MAPISHI

Weka karai kwenye moto kiasi
Tia siagi
Tia tambi uzikaange usiachie mkoni mpaka ziwe rangu ya dhahabu.
Weka lozi na zabibu huku unakoroga
Tia maziwa na huku unakoroga usiachie mkono.
Tia arki
Epua karai, tumia kijiko cha chai kwa kuchotea na utie kwenye kikombe cha kahawa nusu usikijaze.
Kipindue kwenye sahani utoe kileja.
Fanya hivyo mpaka umalize vyote.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Tende Na Ufuta

MAHITAJI

Unga – 3 Vikombe vya chai

Baking powder – 1 ½ Vijiko vya chai

Sukari – 1 Kikombe cha chai

Siagi – 1 Kikombe cha chai

Mayai – 2

Maji – kiasi ya kuchanganyia

Tende – 1 Kikombe

ufuta – ¼kikombe

MAPISHI

  1. Changanya unga, siagi, baking powder, na sukari katika bakuli
  2. Tia mayai, na maji kidogo uchanganye vizuri.
  3. Sukuma kiasi kama unavyosukuma chapati duara kubwa.
  4. Tandaza tende juu yake halafu kunja hadi mwisho.
  5. Paka mayai juu yake halafu mwagia ufuta kisha kata kata vipande.
  6. Vipange kwenye treya ya oveni kisha choma(bake)moto wa 350°F kwa muda wa nusu saa takriban.
  7. Ziepue katika moto naziache zipowe. Panga katika sahani.
Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About