Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya Sambusa za nyama

Mahitaji

Nyama ya kusaga (minced beef 1/4 kilo)
Vitunguu maji vilivyokatwakatwa(diced onion 2 vikubwa )
Kitunguu swaum/ tangawizi (garlic and ginger paste 1 kijiko cha chakula)
Chumvi (salt)
Pilipili iliyokatwakatwa (scotch bonnet 1)
Limao (lemon 1/2)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Cinnamon powder 1/4 kijiko cha chai
Coriander powder 1/4 kijiko cha chai
Cumin powder 1/4 kijiko cha chai
Unga wa ngano (all purpose flour kidogo)
Manda za kufungia (spring roll pastry)
Giligilani (fresh coriander kiasi)
Mafuta ya kukaangia

Matayarisho

Changanya nyama na limao, chumvi, pilipili,kitunguu swaum, tangawizi na spice zote, kisha pika katika moto wa kawaida mpaka nyama iive na maji yote yakauke. Baada ya hapo kabla hujaipua nyama tia vitunguu na giligilani na uvipike pamoja kwa muda wa dakika 2 na uipue weka pembeni na uache viipoe. Baada ya hapo tia unga kidogo katika bakuli nauchanganye na maji kidogo kupata uji mzito kwa ajili ya kugundishia manda. Baada ya hapo tia nyama katika manda na kisha zifunge kwa kugundishia na unga wa ngano.Ukisha maliza kuzifunga zote zikaange mpaka ziwe za brown na uzitoe. Na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya wali Wa Nazi Kwa Mchuzi Wa Nyama Ng’ombe Na Mchicha

Wali Wa Mpunga

Mchele wa mpunga – 4 Vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha

Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.

Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Mchuzi wa nyama Ng’ombe

Nyama – 1 kilo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa -2 viijiko vya supu

Viazi/mbatata – 2

Kitunguu maji kilokatwakawa (slice ndogo) – 2

Nyanya/tungule – 4

Nyanya kopo – 3 vijiko vya supu

Majani ya mchuzi/mvu – 3 msongo (bunches)

Bizari ya mchuzi (simba 2) – I kijiko cha chai

Ndimu – 1 kamua

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama katika sufuri, tia kijiko kimoja cha kitunguu thomu na tangawizi, chumvi, ndimu na chemsha nyama hadi iwive na ibakie supu yake kidogo.
Weka mafuta katika sufuri nyingine, kaanga kitunguu. Vinapogeuka rangi tia majani ya mchuzi endelea kukaanga hadi vigeuke rangi ya hudhurungi (golden brown)
Tia nyanya/tungule, viazi/mbatata, endelea kukaanga mpaka nyanya ziive.
Tia nyama na supu yake kisha tia nyanya ya kopo, kotmiri, bizari ya mchuzi, chumvi uache mchuzi kidogo katika moto hadi viazi viive vikiwa tayari.

Mboga Mchicha

Mchicha – 4 michano/vifungu

Kitunguu – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 3

Nyanya/tungule – 2

Tui la nazi zito – 1 kikombe cha chai

Chumvi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mboga iache ichuje maji.
Ikatekate kisha weka katika sufuria.
Katika kitunguu maji, kitunguu thomu kisage au kikatekate kidogodogo (chopped), nyanya.
Weka jikoni ipikike kwa maji yake na mvuke.
Tia tui endelea kuweka katika moto mdogomdogo hadi ikaribie kukauka ikiwa tayari.

Jinsi ya kupika Cookies Za Jam Ya Peach Na Raspberry

MAHITAJI

Unga kikombe 1 ½

Siagi ½ kikombe

Sukari ½ kikombe

Yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jam ya peach na raspberry

MAANDALIZI

Wash oven moto wa takriban 180 – 190 Deg F
Piga siagi na sukari katika mashine mpaka iwe laini na nyororo (creamy) kisha weka yai na vanilla.
Tia unga kidogo kidogo uchanganye kwa mwiko wa mbao (wooden spoon).
Pakaza mkononi unga uchukue vidonge ubonyeze kufanya vishimo vya kuwekea jam.
Panga katika treya uliyopakaza siagi.
Tia nusu yake jam ya peach na nusu jam ya raspberry
Bake katika oven kiasi robo saa mpaka ziwive na kugeuka rangi ya brown light.
Epua vikiwa tayari

Jinsi ya kuandaa Pilau ya sosi ya soya, nyama na mboga

Mahitaji

Nyama isiyokuwa na mifupa – 1 ½ Lb(ratili)
Mchele wa Basmati (rowanisha) – 3 Magi
Vitunguu maji – 2
Mchanganyiko wa mboga za barafu – 1 Magi
(karoti, mahindi, njegere)
Pilipili Mbichi – 3
Pilipili mboga kijani na nyekundu – 1
Pilipili manga – ½ kijiko cha chai
Chumvi – Kiasi
Sosi ya soya (soy sauce) – 5 Vijiko vya supu
Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 Kijiko cha supu
Mchanganyiko wa bizari (garam masala) – 1 Kijiko cha supu
Kotmiri iliyokatwa – ½ Kikombe
Mafuta ya kukaangia – Kiasi

Namna Ya Kutaarisha

Ndani ya sufuria, tia mafuta yakipata moto kaanga vitunguu mpaka ziwe rangi ya hudhurungi.
Kisha tia nyama iliyokatwa vipande vidogo vidogo pamoja na maji ya kiasi na viungo vyote isipokuwa mchele, mboga zote na kotmiri. chemsha mpaka nyama iwive na maji yakauke.
Halafu changanya na mboga na iwache kwa muda wa dakika kumi kisha tia kotmiri na umimine kwenye bakuli au treya ya oveni na uweke kando.
Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja, kisha umwagie juu ya ile treya ya nyama.
Nyunyizia mafuta na sosi ya soya na ipike katika oveni moto wa 350° kwa muda wa dakika 20 hivi.
Ukishawiva, uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Wali Wa Tambi Na Kuku Wa Sosi Ya Mtindi

Vipimo Vya Wali

Mchele – 3 vikombe

Tambi – 2 vikombe

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi

Vipimo Vya Kuku

Kuku kidari (boneless) aliyekatwa katwa vipande – 1 Kilo

Kitunguu maji kilichokatwa katwa – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Paprika – 1 kijiko cha supu

Masala ya kuku (tanduri au yoyote) – 1 kijiko cha supu

Ndimu – 2 vijiko vya supu

Mtindi (yoghurt) au malai (cream) – 1 kikombe

Mafuta – ¼ kikombe

Majani ya kotmiri (coriander) – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Wali:

Osha Mchele, uroweke.
Tia mafuta katika sufuria, kaanga tambi zilizokatwakatwa hadi zigeuke rangi kuwa nyekundu.
Tia mchele endelea kukaanga kidogo.
Tia maji kiasi cha wali kupikika kama unavyopika pilau. Kiasi cha maji kinategemea aina ya mchele
Funika katika moto mdogo mdogo hadi uive ukiwa tayari.

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Kuku

Katika bakuli, changanya vitu vyote isipokuwa mtindi na kitunguu.
Tia mafuta katika karai, kisha tia kitunguu ukaange muda mdogo tu, usikiache kugeuka rangi.
Tia kuku na masala yake, endelea kukaanga, kisha tia mtindi au malai ufunike apikike na kuiva vizuri.
Nyunyuzia kotmiri iliyokatwakatwa ikiwa tayari kuliwa na wali wa tambi.

Jinsi ya kupika Biryani ya mbogamboga

Biriani ni miongoni mwa vyakula ambavyo ni nadra sana kupikwa katika familia nyingi tofauti na vyakula vingine. Inawezekana ni kutokana na watu wengi kutoelewa namna ya kuoika chakula hiki kutokana na kuhitaji viungo vingi ambavyo huwapa usumbufu wapishi.
Kuna aina mbalimbali za upishi wa biriani ambapo mara nyingi hutofautiana kutokana na viungo vinavyotumika katika upishi.
Biriani la mbogamboga ni miongoni mwa aina hizo za upishi. Chakula hiki kinaweza kuliwa na kila mtu hususan wale wasiotumia nyama wala samaki.

Mahitaji:

½ kg mchele wa basmati
Kitunguu maji kikubwa 1
Nyanya 1 kubwa
Karoti 1 kubwa
Njegere robo kikombe
Kiazi ulaya 1 kikubwa
Tangawizi za kusaga kijiko 1
Kitunguu swaumu cha kusaga kijiko 1
Karafuu kijiko 1
Majani ya kotimili fungu 1
Maziwa ya mtingi ¼ kikombe
Chumvi na pilipili kiasi
Unga wa dhani kijiko 1 cha mezani
Juisi ya limao kijiko 1 cha mezani
Mafua ¼ lita

Maandalizi:

Chemsha mchele na kisha weka pembeni
Osha mbogamboga zote isipokuwa vitunguu na nyanya
Changanya mtindi na tangawizi pamoja na kitunguu swaumu viache vikae kwa muda wa saa moja
Chukua sufuria weka mafuta na kisha kaanga vitunguu maji, weka nyanya, chumvi, kotimili na limao halafu weka karafuu na kanga hadi vichanganyike vizuri
Miminia mchanganyiko wa mtindi na baadaye weka pilipili na baadaye weka unga wa dhania
Chukua mchele uliochemshwa changanya na mchanganyiko huo
Palia moto juu ya chakula chako na acha kwa muda wa dakika 30
Baada ya hapo chakula chako cha biriani kitakuwa tayari kwa kuliwa

Jinsi ya kupika Baklawa Za Pistachio Na Lozi

VIAMBAUPISHI

Philo (thin pastry) manda nyembamba – 1 paketi

Siagi – ¼ Kikombe cha chai

Baking powder – 2 Vijiko vya chai

Pistachio/ lozi – 2 vikombe vya chai

Mafuta – ½ Kikombe

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 Vikombe vya chai

Maji – 2 ½ Vikombe vya chai

ndimu – ½ kijiko cha chai

JINSI YA KUANDAA

Tafuta treya iliyokuwa sawa na ukubwa wa hizo manda nyembamba (philo) au zikate hizo manda kwa ukubwa wa treya (mraba au mstatili)
Kisha yeyusha siagi changanya na mafuta.
Kisha panga manda moja pakaza mafuta juu yake kisha weka manda nyingine juu yake kisha pakaza mafuta tena weka manda nyingine juu yake, endelea kufanya hivyo mpaka ziwe kama sita au saba kisha nyunyizia pistachio na lozi halafu panga tena manda na mafuta manda na mafuta tena sita au saba kisha nyunyizia tena pistachio na lozi.
Panga namna hivyo mpaka treya ijae inapofika manda ya mwisho kata vipande vya mraba vidogodogo humo humo kwenye treya kisha nyunyizia mafuta yaliyobaki.
Washa moto wa oven 350°F kwa muda wa dakika 20 au hadi rangi ibadilike kidogo (isikauke sana)
Chemsha syrup yako kama shira ya majimaji lakini isiwe nzito sana ikishakuwa tayari mwisho tia ndimu acha ipoe kidogo kisha miminia juu ya treya yote halafu malizia kunyunyizia pistachio na lozi zilizobaki.
Zikishakuwa tayari zipange kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

ANGALIZO

Ukishatoa treya kwenye oven wacha ipoe kidogo na syrup yako pia wacha ipoe kidogo kabla hujamimina, ukitia ya motomoto zitalainika.
Manda nyembamba za baklawa zinauzwa tiyari madukani kwenye pakiti.

Namna ya kupika Biskuti Za Kuchoveya Chokoleti

VIAMBAUPISHI

Unga 300gm

Siagi 225gm

Icing Sugar 60gm

Chokoleti iliyokoza (Dark Chocolate) – 225gm

Vanilla – Vijiko 2 vya chai

Yai -1

Baking Powder ½ kijiko cha chai

Njugu za vipande ½ kikombe cha chai

Njugu zilizosagwa ¼ kikombe cha chai

JINSI YA KUTAYARISHA

Piga sukari na siagi katika mashine ya keki mpaka iwe laini
Kisha mimina yai na vanilla koroga vizuri
Mwisho mimina unga na baking powder polepole mpaka ichanganyike.
Kata kata umbo (shape) lolote unavyopenda (kama nyota, pembetatu,duara, kopa n.k)
Panga kwenye treya na choma kwa moto wa 350°C , vikibadilika rangi kidogo tu vitoe
Yayusha chokoleti tia kwenye bakuli ndogo.
kisha paka kwa kijiko au chovyea upande mmoja mmoja wa biskuti kisha nyunyizia njugu za kipande na njugu ya unga.
Panga kwenye sahani tiyari kunywewa na chai ya maziwa au kahawa.

Jinsi ya kupika Mkate

Mahitaji

Unga wa ngano ( self risen flour) kikombe 1 na 1/2
Hamira (yeast) 1 kijiko cha chai
Sukari (sugar) 1 kijiko cha chakula
Chumvi (salt) 1/2 kijiko cha chai
Siagi iliyoyeyushwa (melted butter) 1 kijiko cha chakula
Maji ya uvuguvugu ( warm water) kiasi

Matayarisho

Changanya vitu vyote katika bakuli kubwa kisha aanza kukanda mpaka upate donge laini.Baada ya hapo liweke hilo donge kwenye bakuli la plastic na weke katika sehemu yenye joto ili unga uumuke. Hakikisha unga unaumuka zaidi (yani unaji double size) unaweza kuchukua kama saa 1 na nusu hivi. Baada ya hapo ukande tena na uache uumuke tena kwa mara ya pili, Ukisha umuka pakaza butter katika baking tin (chombo cha kuokea) na upakaze mkate butter kwa juu,kisha uoke katika oven kwa muda wa dakika 30 (katika moto wa 200C) (hakikisha juu na chini unakuwa wa brown Na hapo mkate wako utakuwa tayari

Mapishi ya Biriani Ya Kuku Wa Kuchoma Wa Tanduri

Mahitaji

Mchele – 4 vikombe

Kuku – 1

Vitunguu – 3

Nyanya/tungule – 4

Zabibu kavu – ½ kikombe

Tangawizi na kitunguu (thomu/galic) – 2 vijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Mtindi (yoghurt) – 2 kijiko cha supu

Masala ya tanduri – 2 vijiko vya supu

Pilipili manga – 1 kijiko cha chai

Hiliki – ½ kijiko cha chai

Mdalasini – kijiti kimoja

Ndimu – 3 vijiko vya supu

Chumvi – kiasi

Zaafarani (saffron) – 1 kijiko cha chai

Mafuta – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Kuku:

Baada ya kumsafisha kuku, mkate vipande vikubwa vikubwa kiasi upendavyo, muoshe mchuje atoke maji.
Katika bakuli, tia tangawizi, kitunguu thomu ilosagawa, pilipili mbichi ilosagwa, chumvi, ndimu, mtindi, masala ya tanduri na uchanganye vizuri, kisha mtie kuku na uchanganye tena na acha arowanike kwa muda wa kiasi saa au zaidi.
Panga kuku katika sinia ya kuchoma ndani ya oveni. Kisha mchome (grill) hadi awive, mtoe acha kando. Mwagia juu yake masala yatakayobakia katika sinia baada ya kumchoma.

Namna Ya Kutayarisha Masala Ya Nyanya:

Weka mafuta katika karai, tia vitunguu ulivyokatakata, kaanga hadi vianze kugeuka rangi.
Tia nyanya ulizokatakata, tia pilipili manga, hiliki, mdalasini, chumvi, na zabibu. Kaanga kidogo tu yakiwa tayari.

Namna Ya Kutayarisha Wali:

Osha na roweka mchele wa basmati.
Roweka zaafarani kwa maji ya moto kiasi robo kikombe weka kando.
Chemsha maji, tia chumvi, kisha tia mchele uive nusu kiini.
Mwaga maji uchuje mchele kisha rudisha katika sufuria au sinia ya foil. Nyunyizia zaafarini, na rudisha katika moto upike hadi uive kamili.
Epua, kisha pakua wali katika sahani au chombo upendacho, mwagia juu yake masala ya nyanya. Kisha weka vipande vya kuku ulivyochoma, biriani ikiwa tayari

Jinsi ya kupika Biskuti Za Ufuta Na Jam

Viamba upishi

Unga 2 Viwili

Sukari ya kusaga 1/4 Kikombe

Siagi 250 gms

Jam kisia

Ufuta Kisia

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai, sukari na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.

2. Tia baking powder, na unga na changanya kwa mkono vizuri.

3. Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.

4. Tengeneza viduara vidogo vidogo.

5. Bonyeza kila kiduara katikati kwa kidole, kisha weka jam, halafu juu yake paka mayai na unynyuzie ufuta.

6. Pika katika moto wa chini 350ºF kwa muda wa dakika 20-25.

7. Tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Wali Wa Dengu Kwa Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 Vikombe

Dengu – 2 vikombe

Viazi – 3 vikubwa

Kitunguu – 2 kubwa

Nyanya – 2

Pilipili mbichi kubwa – 3

Pilipilimanga – ½ kijiko cha chai

Garama Masala (bizari mchanganyiko) -1 kijiko cha chai

Supu ya vidonge (stock cubes) – 2 vidonge

Chumvi – kiasi

Mafuta – ¼ kikombe

Zaafarani – 1 kijiko cha chai

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Dengu kama sio za tayari kwenye kopo, roweka na zichemshe hadi ziwive

Maandalizi ya Masala Ya Dengu:

Zaafarani – iroweke katika maji ya dafu dafu (warm) ya chini ya robo kikombe weka kando.
Osha mchele, roweka.
Menya viazi na vitunguu, katakata vitunguu, na nyanya , weka kando.
Katakata viazi vipande vidogo vidogo kwa umbo la mchemraba (cubes).
Katika sufuria tia mafuta yakipata moto, tia viazi ukaange kidogo kwa moto mdogo mdogo hadi kukaribia kuwiva, toa weka kando.
Kaanga vitunguu hadi vigeuka rangi ya hudhurungi isiyokoza (light brown) kisha tia nyanya ukaange kidogo.
Tia vidonge vya supu (stock cubes) uvivuruge katika mchanganyiko, katakata pilipili mbichi kwa urefu tia, uendelee kukakaanga. Tia bizari, chumvi.
Zima moto, changanya dengu na viazi katika mchanganyiko huo.

Mapishi ya Wali:

Chemsha mchele kama kawaida ya kupika wali mweupe, kiini kiwe kimewiva nusu yake.
Chuja maji kisha changanya katika mchanganyiko wa dengu.
Nyunyizia zaafarani, uchanganye wali na mchanganyiko kidogo tu.
Funika acha uive katika mtoto mdogo mdogo au tia katika oveni hadi uive kama kawaida ya kupika wali.
Pakua katiha sahani na tolea na samaki yoyote wa kukaanga.

Mapishi ya Mitai

VIAMBAUPISHI

Unga wa ngano – magi 2 (vikombe vikubwa)

Hamira kijiko 1 cha chai

Sukari Vijiko 2 vya supu

Maziwa ¾ Magi

Siagi Vijiko 2 vya supu

Mafuta ya kukaangia kiasi

VIAMBAUPISHI:SHIRA

Sukari ¾ Kikombe

Maji ¾ Kikombe

Illiki ya unga kiasi

Zafarani kiasi

JINSI YA KUPIKA

Katika bakuli, changanya vipimo vyote pamoja na ukande unga usiwe mgumu wala laini sana uwe kiasi.
Kisha fanya donge moja na iache pahali penye joto mpaka iimuke.
Halafu weka mafuta ya kukaangia kwenye moto.
Sukuma donge hadi liwe duara sio nyembamba sana, kisha katakata kama maandazi.
Mafuta ya kisha pata moto choma mittai hukuunazigeuza hadi ziwive na kugeuka rangi.
Katika sufuria tia vipimo vya shira na iache ichemke isiwe nzito sana.
Mimina mitai kwenye shira na uzipepete, kisha weka kwenye sahani na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Ndizi Za Supu Ya Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi – 15 takriiban

Nayma ya ng’ombe – 1 kilo

Kitunguu maji – 1

Nyanya – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) kilosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi ilopondwa – 2

Jira/cummin/bizari ya pilau ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 1

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chemsha nyama kwa ndimu, chumvi na tangawizi mbichi na kitunguu thomu.
Menya ndizi na zikatekate vipande kiasi, weka katika sufuria.
Katakata kitunguu na nyanya utie katika ndizi.
Tia jira na chumvi.
Nyama ikiwiva mimina pamoja na supu yake ufunike ndizi ziwive na kuwa tayari kuliwa.
Ukipenda tia pilipili mbuzi zichemke pamoja na ndizi.

Jinsi ya kuandaa biskuti za Siagi Na Jam

MAHITAJI

Unga – 2 Vikombe
Sukari ya icing – 1 Kikombe
Siagi – 250 gm
Yai – 1
Vanilla – 2 Vijiko vya chai
Baking powder -1 Kijiko cha chai
Jam – ¼ kikombe
Lozi – ¼ kikombe

JINSI YA KUPIKA

Koroga siagi na sukari katika mashine ya keki (cake mixer) mpaka iwe laini (creamy).
Tia yai na vanilla koroga mpaka mchanganyiko uwe laini kama sufi.
Tia unga na baking powder changanya na mwiko.
Chota mchanganyiko kwa mkono (kiasi cha kijiko kimoja cha supufanya duara kisha weka kwenye treya ya kupikia.
Bonyeza kila kiduara katikati kwa kidole, kisha weka jam na tupia lozi zilizomenywa na kukatwa katwa.
Pika (bake) katika oven moto wa 375° F kama muda wa dakika 15 hivi huku unazitazama tazama

Virutubishi, kazi zake katika mwili na vyanzo vyake

Virutubishi

ni viini vilivyoko kwenye chakula ambavyo vinauwezesha mwili kufanya kazi zake, karibu vyakula vyote huwa na kirutubishi zaidi ya kimoja ila hutofautiana kwa kasi na ubora. Kila kirutubishi kina kazi yake mwilini na mara nyingi hutegemeana ili viweze kufanya kazi yake kwa ufanisi. Hakuna chakula kimoja chenye virutubishi vya aina zote isipokuwa maziwa ya mama kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto, ni mhimu kula vyakula vya aina mbalimbali ili kuwezesha mwili kupata virutubishi mchanganyiko vinavyohitajika.

Aina za virutubishi vinavyohitajika mwilini

  1. Kabohaidreti / vyakula vya wanga
  2. Mafuta ya Wanyama na Mimea
  3. Protini
  4. Vitamini na Madini
  5. Maji

Kabohaidreti / vyakula vya wanga

Kabohaidreti / vyakula vya wanga huvipa mwili nguvu inayoihitajika kujiendesha. Vyakula
hivi vyaweza kuwa sahili au changamani. Hii inahusu jinsi ambavyo chakula chaweza
kubadilisha sukari katika mwili. Vyakula vya wanga na sukari huvipa mwili nguvu
inayohitajika kuufanya upumue na kuendelea kuishi, kuwa na mwendo na utoaji joto, na kwa
ukuaji na utengenezaji wa mkusanyiko wa seli (tishu). Baadhi ya wanga na sukari
hubadilishwa kuwa mafuta mwilini.
Ufumwele utokanao na kabohaidreti hufanya kinyesi kiwe laini na kingi na huondoa kemikali
za sumu, na hivyo hufanya matumbo yawe na afya njema. Hupunguza uyeyushaji na
ufyonzaji wa virutubishi katika vyakula, na husaidia kupunguza unene.

Vyanzo vya kabohaidreti

Vyanzo vikuu vya kabohaidreti ni:

• Nafaka

– Mahindi/ugali
– Serena
– Mtama
– Mchele
– Unga wa ngano

• Mizizi ya vyakula vya wanga

– Viazi vitamu
– jimbi
– Viazi mviringo
– Muhogo mbichi
– Unga wa muhogo
– Ndizi

Mahitaji ya kabohaidreti mwilini

– Mahitaji hutofautiana kutegemea na umri, jinsi, jinsia, shughuli, hali ya kiafya
– Kula mara tatu au zaidi kwa siku.

Mafuta ya Wanyama na Mimea

Mafuta ya wanyama na mimea kwenye chakula na tishu ya shahamu kwenye miili yetu huwa
na shughuli nyingi

Kazi za mafuta ya wanyama kwenye mwili

• Virutubishi: mafuta ya wanyama hutoa tindikali za mafuta muhimu, ambazo
huhitajika katika ukuaji wa kawaida kwa watoto wachanga na watoto wengine na
kwa uzalishaj wa michanganyiko ya aina ya kihomoni inayorekebisha upeo mpana
wa shughuli za kimwili na kukufanya uwe mwenye afya njema.
• Usafirishaji: mafuta ya wanyama hubeba mafuta ya miyeyusho ya vitamini (A, D,
E, na K) na kurahisisha ufyonzaji wake.
• Ufahamu: mafuta ya wanyama huchangia kwenye harufu nzuri na ladha ya
chakula.
• Umbile la asili: mafuta ya wanyama hufanya chakula (hususan nyama na vyakula
vya kukaushwa) kuwa nyororo.
• Ukinaishaji: mafuta ya wanyama hukipa chakula ukinaishaji, hivyo hujikuta
umeshiba na kutosheka kwa muda mrefu baada ya chakula.
• Mafuta ya wanyama ni chanzo cha utoaji wa mkusanyiko wa kalori. Hili ni jambo
jema unapokuwa kwenye safari ndefu, itumiayo nguvu nyingi, ukiwa umebeba
chakula chako.

Mafuta ya wanyama mwilini hufanya yafuatayo:

• Mafuta ni muundo mkuu wa mwili wa kuhifadhi nishati (ambazo ni muhimu wakati wa
ugonjwa au kupungua kwa ulaji chakula)
• Mafuta hutoa sehemu kubwa ya nishati inayotumika kwenye kufanyiza kazi misuli.
• Mafuta hukinga viungo vya ndani na kuhami miili yetu dhidi ya hali za joto
zinazopitiliza mipaka.
• Mafuta huunda malighafi kuu ya utando wa seli (hususan seli za ubongo na za
mishipa ya fahamu)
• Mafuta hugeuzwa kuwa aina nyingi za homoni (ikiwemo homoni za mambo yahusuyo
mapenzi)
Mafuta ki kitu kizuri! Isipokuwa tu pale uzuri unapozidi kiwango ndipo kunapokua na tatizo.

Aina za mafuta:

mafuta yaliyokolea dhidi ya yale yasiyokolea
Kama ambavyo kuna aina kuu mbili za kabohaidreti, kuna aina kuu mbili za mafuta
kutegemea na mfumo wake wa kikemia; mafuta yaliyokolea na yale ambayo hayajakolea.
Aina hizi za mafuta zina athali tofauti kabisa kwa afya yako.

1. Mafuta yaliyokolea

• Huwa na kawaida ya kuongeza lehemu “mbaya” kwenye damu na kuongeza
uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo.
• Mafuta yaliyokolea huwa na kawaida ya kuganda kwenye hali ya joto la kawaida.
• Hupatikana kwa wingi kutokana na vyanzo vya mafuta ya wanyama.
Vyanzo vya mafuta yaliyokolea
• Siagi, malai, mafuta ya nyama ya ngómbe, ngozi ya kuku, mafuta ya maziwa yenye
malai, jibini, aisikirimu, siagi, samli, mafuta ya nguruwe/ya kupikia, mafuta
yatokanayo na nyama, mawese mekundu, na nazi.
• Yaliyopo nje ya utaratibu: mafuta ya nchi za joto (ikiwemo ya nazi na mawese) yana
kiwango kikubwa cha mafuta yaliyokolea.

2. Mafuta yasiyokolea

• Mafuta yasiyokolea ni aina ya mafuta ambayo kwa ujumla yanahusishwa na afya bora.
• Yana kwaida ya kushusha viwango vya lehemu na kupunguza hatari za magojwa ya
moyo.
• Mafuta yasiyokolea huwa na kawaida ya kuwa ya mmiminiko katika joto la kawaida.
• Hupatikana kwa wingi kutokana na mimea.
Vyanzo vya mafuta yasiyokolea
• Mafuta yatokanayo na mboga za majani, mizeituni, miparachichi, njugu, mafuta ya
karanga, maharagwe meupe, mbegu za alizeti, mbegu za ufuta na aina nyingine za
mbegu, mafuta ya samaki na soya.
• siagi, samli, mafuta ya nguruwe/ya kupikia, maziwa yenye malai, jibini, mafuta
yatokanayo na nyama, mawese mekundu, na nazi.

Kuna mafuta yatokanayo na kuchujwa kwa mafuta ya mbogamboga na kugandishwa. Mafuta
haya huishia kuwa na tabia za mafuta yaliyokolea. Mafuta haya pia hayapashwi kutumiwa
kwa wingi.

Vyanzo ni:

• majarini, mafuta ya nguruwe, vyakula vya kukaangwa, donati, keki, biskuti, aiskrimu.

Mahitaji ya mafuta mwilini

Mahitaji ya mafuta huelezewa kama ‘ni asilimia ya mahitaji yote ya nishati’. Kiwango chote
cha asilimia ya nishati kinachopashwa kitokane na mafuta katika mlo bora uliokamilika ni
kama ifuatvyo:
• Asilimia 30-40 kwa watoto hadi kufikia miaka miwili kwenye milo ya nyongeza
• Asilimia 15-30 kwa watoto wakubwa na wengi wa watu wazima; kwa watu wazimu
wenye afya – hadi asilimia 35 inakubalika.
• Angalau asilimia 20 hadi 30 kwa akina mama wenye umri wa kuweza kuzaa (15-45).

Protini

Protini ni zana za ujenzi wa misuli yetu, viungo na baadhi ya vitu vingi vinavyotengeneza
miili yetu. Hutoa tindikali muhimu za amino zitumiwazo na mwili kutengeneza misuli ya tishu.
Mwili unahitaji protini na kalori kila siku.
Unapokosa kupata kalori na protini za kutosha kila siku, mwili wako hutumia akiba yake
kufidia pengo la ukosefu wa nishati. Hali hii huinyima mwili wako kalori unazohitaji kuufanya
uwe na afya bora na hivyo kusababisha kupungua kwa uzito.

Vyanzo vya protini

Protini yaweza kupatikana kwenye vyakula vya wanyama na mimea.

1. Vyanzo vitokanavyo na wanyama

• Nyama, kuku/mabata n.k., samaki, mayai, jibini, maziwa na mtindi.
• Vyakula hivi vinachukuliwa kuwa kama ‘kamili’ au ‘vyenye kiwango cha juu’cha
protini kwa kuwa vina aina zote za ‘tindikali muhimu za amino’. ‘Muhimu”inamaanisha
lazima vitumiwe kwenye milo yetu; miili yetu haiwezi kuzitengeneza.

2. Vanyzo vitokanavyo na mimea

• Bidhaa zitokanazo na soya, (tofu, tempeh), maziwa ya soya na mazao mengine
yatengenezwayo na soya), maharagwe, mbegu na njugu.
• Viwango vidogo vya protini vinapatikana vilevile kwenye mikate, mahindi /ngano, na
aina nyinge ya nafaka, na mbogamboga pia.
• Vyanzo hivi vya protini vinachukuliwa kama ‘si kamili’kwa kuwa vinakosa moja au
zaidi ya tindikali muhimu za amino.
• Protini ya maharagwe meupe ndiyo ya kipekee. Haya yanachukuliwa kuwa ni kamili.

Mahitaji ya protini mwilini

Mahitaji hutofautiana kulingana na umri, jinsi, jinsia, na shughuli.

Vitamini na Madini

• Vitamini husaidia mwili kugeuza chakula kuwa nishati na tishu.
• Kuna aina 13 za vitamini kwa ujumla: Vitamini A; vitamini B; vitamini B mchanganyiko
unayojumuisha vitamini B1, Vitamini B2, Viamnini B3 vitamin, B6, Vitamini C, Vitamin
B12 tindikali ya pantotheniki (pantothenic acid), na biotini (biotin); na vitamini C, D, E,
na K.
• Madini yanahitajika katika ukuaji na utunzaji wa miundo ya mwili. Yanahitajika pia
katika kutunza juisi za uyeyushaji chakula na mimiminiko iliyopo ndani na
kandokando mwa seli.
• Madini hayatokani na mimea wala wanyama. Mimea hupata madini kutokana na maji
au udongo, na wanyama hupata madini kwa kula mimea au wanyama wanaokula
mimea.
• Vitamini na madini hujulikana pia kama vyakula vya ujenzi na ulinzi wa mwili.
• Vijirutubishi ambavyo havipatikani kwa wingi na ambavyo husababisha matatizo
mengi yatokanayo na utapiamlo wa ukosefu wa vijirutubish duniani ni kama
vifuatavyo; madini ya joto, zinki, vitamini A, chuma na folate.

Vyanzo vya Vitamini na Madini

• Mboga jamii ya machungwa, kama vile viazi vitamu vya njano na karoti, matunda jamii
ya machungwa kama vile, embe, papai, na mawese mekundu ni vyanzo vizuri sana
vya vitamini A.
• Matunda mengi yatokanayo na jamii ya michungwa na mboga zisizoivishwa sana
huwa na vitamini C.
• Mboga za kijani kibichi hutupatia folate na kiasi cha vitamini A.
• Mbogamboga nyingi (mf. nyanya, vitunguu) hutoa vijirutubishi muhimu vya nyongeza
viwezavyo kukinga mwili dhidi ya magonjwa sugu kama ya mioyo.
• Njia bora ya kuhakikisha tunapata vijirutubishi na ufumwele wa kutosha ni kula aina
mbalimbali za mbogamboga, matunda na nafaka zisizokobolewa kila siku.
• Nyama, viungo vya ndani vya wanyama na maini ya aina zote ni chanzo kizuri sana
cha vitamini A.

Mahitaji ya vitamin na madini mwilini

• Vitamini na madini vinahitajika kwa viwango vidogo vidogo.
• Mahitaji hutegemea umri, jinsi na kiwango cha shughuli, na ulaji wa aina mbalimbali
za matunda, mbogamboga na nafaka zisizokobolewa.

Maji

Maji ni kirutubishi muhimu sana. Hakika, zaidi ya nusu ya mwili ni maji. Unaweza kuishi bila
ya chakula kwa wiki kadhaa, bali hauwezi kuishi zaidi ya wiki moja bila ya maji.
Mwili unahitaji maji ili kufanya kazi.

Umuhimu wa maji mwilini

• Kuhifadhi joto la mwili;
• Kusafirisha virutubishi mwilini;
• Kuvifanya viungo viwe na unyevunyevu;
• Kuyeyusha chakula;
• Kuondoa uchafu mwilini;
• Kupoza mwili.
(Fikiria matumizi ya maji unapojenga nyumba; bila ya maji: saruji, mchanga na zege
havitakuwa na matumizi yeyote).

Vyanzo vya maji mwilini

• Maji yenyewe
• Juisi za matunda
• Supu
• Maziwa
• Uji
• Vinywaji visivyo na kafeini (vinywaji vyenye kafeini na kileo vina madawa ya
kuongeza mkojo (diuretics) inayosababisha upotevu wa maji mwilini)

Mahitaji ya maji mwilini

Lita 1.5 au glasi 8 kwa siku.

Jinsi ya kutengeneza saladi

Mahitaji

Tango 1/2
Kitunguu 1/2
Cherry tomato 8
Lettice kiasi
Green olives kidogo
Black olives kidogo
Hoho jekundu 1
Carrot
Giligilani kidogo

Salad dressing
Yogurt 1/2 kikombe
Swaum 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/2
Pilipili ya unga 1/4 kijiko cha chai
Chumvi kidogo
Olive oil kiasi

Matayarisho

Osha vitu vyote kisha vikaushe maji. Baada ya hapo ktk bakuli kubwa katakata, lettice, tango,hoho, kitunguu,giligilani na kisha ikwangue carrot na utie bila kusahau nyanya zote pamoja na olives.Baada ya hapo ichanganye vizuri, kisha tengeneza salad dressing kwa kuchanganya vitu vyote vilivyo (kwenye list ya salad dressing) kisha koroga vizuri.Baada ya hapo ichanganye na salad.Na hapo salad yako itakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuila na chochote upendacho kama vile chips, nyama choma au au chakula kikuu.

Mapishi ya Mchuzi wa kambale

Mahitaji

Kambale 2
Nazi kopo 1
Nyanya kopo 1
Vitunguu 2
Curry powder 1 kijiko cha chai
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Binzari nyembamba ya unga 1/2 kijiko cha chai
Swaum/ tangawizi 1 kijiko cha chakula
Giligilani kiasi
Limao 1/2
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Loweka samaki katika maji ya moto kwa muda wa muda wa nusu saa.Baada ya hapo Saga pamoja nyanya, vitunguu, swaum na tangawizi kisha vibandike jikoni na uvipike mpaka maji yote yakauke kisha tia mafuta. Pika mpaka nyanya zitengane na mafuta kisha tia spice zote.Zipike kwa muda mdogo kisha tia tui la nazi, maji kiasi, samaki, pilipili nzima, chumvi na kamulia limao. Pika mpaka tui la nazi litakapoiva na samaki pia wawe wameiva na mchuzi ubakie kiasi. Baada ya hapo ipua kisha tia giligilani iliyokatwa na mchuzi utakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuulia kwa chochote kile upendacho. Mi hupendaga kuulia na ugali mlaiiini au na wali pia.

Sanaa ya Upishi Imara: Kupata Lishe Muhimu

Sanaa ya Upishi Imara: Kupata Lishe Muhimu

Jambo hilo kuu kwa afya njema na maisha bora ni kula chakula chenye lishe bora. Lishe bora inatusaidia kuwa na nguvu, kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa, na kuwa na akili timamu. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuelewa sanaa ya upishi imara ili kupata lishe muhimu ili kukuza afya yetu. Kupitia makala hii, nataka kushiriki vidokezo kadhaa ambavyo vitasaidia kuboresha lishe yako na kufurahia maisha yenye afya.

  1. Punguza matumizi ya chumvi na sukari. Chumvi inaweza kuongeza hatari ya shinikizo la damu na magonjwa ya moyo, wakati sukari inaweza kusababisha unene na ugonjwa wa kisukari. Kwa hiyo, jaribu kutumia viungo mbadala kama vile pilipili, tangawizi, na viungo vingine vyenye ladha nzuri.

  2. Ongeza matunda na mboga katika mlo wako. Matunda na mboga ni vyakula vyenye lishe bora na vitamini muhimu kwa afya ya mwili. Jaribu kula aina tofauti za matunda na mboga kila siku ili kuhakikisha unapata virutubisho vyote muhimu.

  3. Chagua nafaka nzima badala ya nafaka zilizosafishwa. Nafaka nzima kama vile mahindi, mchele wa kahawia, na ngano nzima zina nyuzi zaidi na virutubisho vingine vya muhimu kuliko nafaka zilizosafishwa. Ni chaguo bora kwa lishe bora.

  4. Tumia mafuta yenye afya kama vile mafuta ya mizeituni na mafuta ya alizeti. Mafuta haya yana asidi ya mafuta yenye afya na husaidia kudumisha moyo na mishipa ya damu kuwa na afya nzuri.

  5. Pika chakula chako mwenyewe badala ya kununua vyakula vilivyopikwa. Kwa njia hii, unaweza kudhibiti viungo na kiasi cha mafuta na chumvi unachotumia katika chakula chako.

  6. Kula protini ya kutosha kama vile nyama, samaki, maharagwe, na karanga. Protini ni muhimu kwa ukuaji na ukarabati wa misuli na tishu za mwili.

  7. Kunywa maji ya kutosha kila siku. Maji ni muhimu kwa afya ya mwili na husaidia kudumisha unyevunyevu wa ngozi, kuondoa sumu mwilini, na kuhakikisha kazi nzuri ya viungo vyote.

  8. Epuka vyakula vyenye mafuta mengi na vyenye sukari nyingi. Vyakula kama vile vyakula vya haraka, vyipsi, na vinywaji baridi ni tishio kwa lishe bora na yanaweza kusababisha unene kupita kiasi.

  9. Usisahau kuhusu mlo wa watoto wako. Watoto wanahitaji lishe bora ili kukua na kuendeleza akili zao. Hakikisha kuwapa matunda, mboga, na vyakula vyenye protini kwa wingi.

  10. Kula kwa utaratibu na kwa utulivu. Kula kwa haraka na bila kufikiria kunaweza kusababisha matatizo ya kumeng’enya chakula na kunenepesha. Kula polepole na kufurahia kila kitu unachokula.

  11. Panga mlo wako vizuri. Hakikisha unapata vyakula vyote muhimu kama vile protini, wanga, mafuta, na nyuzi kwa uwiano mzuri. Chakula cha mchana kinaweza kuwa na nafaka nzima, protini kama kuku au samaki, na mboga za majani.

  12. Tafuta mlo unaofaa kwa hali yako ya kiafya. Kama una magonjwa kama vile kisukari au shinikizo la damu, unapaswa kuzungumza na daktari wako au mtaalamu wa lishe ili kupata mwongozo sahihi wa lishe.

  13. Fanya mazoezi mara kwa mara. Lishe bora pekee haitoshi kuwa na afya njema. Mwili unahitaji mazoezi ili kuwa na nguvu na kuimarisha mfumo wa kinga.

  14. Heshimu na kufuata mila na tamaduni za lishe. Kila tamaduni ina vyakula na njia zake za kupika ambazo zinaweza kutoa lishe bora. Kwa mfano, vyakula vya Mediterania kama vile mizeituni na samaki ni sehemu muhimu ya lishe yenye afya.

  15. Kuwa na usawa katika kila kitu. Kula vyakula vyote kwa usawa na kupata lishe muhimu. Kula kwa furaha na kufurahia chakula chako, lakini pia kumbuka kuzingatia afya yako.

Kwa hiyo, kama AckySHINE, nashauri kufuata vidokezo hivi ili kupata lishe muhimu na kuboresha afya yako. Kumbuka, afya njema ni utajiri mkubwa, na kula lishe bora ni hatua muhimu katika kufikia lengo hilo. Je, wewe una mawazo gani juu ya sanaa ya upishi imara na lishe muhimu?

Mapishi ya Mandazi Matamu

Mahitaji

Unga wa ngano (nusu kilo)
Sukari (Kikombe 1 cha chai)
Chumvi (nusu kijiko cha chai)
Hamira (kijiko kimoja cha chai)
Yai (1)
Maziwa ya unga (vijiko 2 vya chakula)
Butter (kijiko 1 cha chakula)
Hiliki (kijiko1 cha chai)
Maji ya uvuguvugu ya kukandia
Mafuta ya kuchomea

Matayarisho

Tia unga kwenye bakuli kisha tia sukari, chumvi, yai, maziwa ya unga, butter na hiliki kisha uchanganye pamoja mpaka mchanganyiko wote uchanganyike vizuri. Baada ya hapo tia maji ya uvuguvugu kiasi na uanze kuukanda. Ni vizuri ukaukanda kwa muda wa dakika 15 ili kuhakikisha donge lote la unga limelainika vizuri.
Baada ya hapo Tawanyishaa unga uliokwandwa katika madonge 4. Tia unga wa ngano kidogo katika kibao cha kusukumia na uanze kusukuma donge moja katika shape ya chapati na hakikisha haiwi nyembamba sana wala nene sana yani inatakiwa iwe ya wastani.Ukishamaliza kusukuma unatakiwa ukate shape uipendayo na uyatandaze katika kitu kilichopo flat na kiwe kimenyunyuziwa unga wa ngano ili kuyazuia yasigandie. Rudia hiyo process kwa madonge yote yaliyobakia. Baada ya hapo yaweke mandazi katika sehemu iliyokuwa na joto ili yaweze kuumuka (inaweza kuchukua masaa 3 kuumuka). Yakisha umuka unatakiwa uweke mafuta katika karai la kuchomea. Yakisha pata joto la kiasi unatakiwa utumbukize mandazi na unaze kuyachoma mpaka yawe ya brown. Yakisha iva yaipue na uyaweke kwenye kitchen towel iliyakauke mafuta. Yakisha poa yatakuwa tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
2
    2
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About