Vituko Vya Kukuburudisha

Kilichotokea baada ya kichaa kumfumania mke wake na mwanamme mwingine

Jay akaruhusiwa kwenda nyumbani kutoka hospital ya Vichaa, akapakiwa ktk ambulance hadi karibu na nyumbani kwake, akaulizwa unapakumbuka? akajibu ndio nyumba yangu ileee, mara wakatoka watoto wawili wamevaa uniform akasema watoto wangu walee wanakwenda shule.. akatoka mwanamke akasema na mke wangu yulee, ghafla akatoka mwanaume Jay akasema na mimi yule naenda kazini. hivi Jay kweli kapona?

Utani wa wahindi, cheka kidogo

Mhindi afaulu mtihani wa Kiswahili

(1) Mfa maji ?……………….. Tampa life jacket.
(2) Mwenda pole?………… Tachelewa fika.
(3) Usipoziba ufa ?……….. Mizi taona mpaka dani.
(4) Usilolijua ?……………… Uliza google.
(5) Mbio za utelezini ?……. Chafua guo yako.
(6) Ukipenda boga ?……… Ngoja mezi ya ramzani tapata.
(7) Ukiona vinaelea ?…….. iko nyepesi hiyo.
(8) Maji yakimwagika ?…… Mambie dada tapiga deki.
(9) Chelewa chelewa ?……… Takosa guo ya sikukuu…
(10) Kila ndege ?………….. …Hutua Airport
(11) Bandu bandu ?….. …….Rafiki yake Jecha
(12) Mtaka cha Mvunguni ?… Ondoa tanda
(13) Simba mwenda kimya?….Kama sio gonjwa basi haina njaa.
(14) Aisifuye mvua ?………. Najua iko Mkulima hiyo
(15) Barabara ndefu ?…….. Ongeza mwendo au tachelewa fika.
(16) Mlanawe hafi nawe ila?…. Takimbia
(17) Asie sikia la mkuu ? …….. Tapeleka jela
(18) Hasira za mkizi ? …………..Tatafuna veve
(19) Mchamba wima ?…….. Karibu ya Hurumzi
(20) Akumurikae mchana ?….Kipofu hiyo
(21) Mficha maradhi ?…….. Taenda Loliondo
(22) Mkataa wingi ? ……….Taenda Chadema
(23) Bendera ?……………. Kama sio ya CCM, ya CUF
(24) Baniani mbaya ?……. Peleka Bombay Lakini sio HB kweli, naonea tu
(25) Akili nyingi ?………. Tapasi mtihani yote
(26) Penye kuku wengi ? …….. Chija bili tatu ivi, hapana mtu najua.

Hii ndiyo Ladha ya bia zote usiyoijua

Ladha ya bia ya 1 hadi ya 6..

Kwa wanywaji wazuri wa bia,

chupa ya kwanza 🍺 huwa haileti hisia yoyote. Mnywaji humaliza chupa hiyo bila kuona matokeo yoyote zaidi ya kupoza koo… Na mara nyingi huwa mkimya, pengine huwa anasoma gazeti lake au kwa siku hizi anawasiliana na ndugu na jamaa kupitia simu yake.

chupa ya pili 🍺🍺 kimsingi ndipo mazungumzo ya awali na wanywaji jirani huanza na haya huwa mazungumzo ya busara, yakihusu muelekeo wa ligi mbalimbali, siasa, idadi za ajali na kadhalika na wakati huu hata takwimu hutolewa zilizo sahihi….

Mtu anaweza kukutajia wachezaji wote wa ligi daraja la tatu la huko Ujerumani bila kukosea, hata idadi ya wachezaji wa Yanga bila kukosea.. Ila wakati huu kama unaanzisha mashindano ya kucheua ni wakati mzuri kwani bia ya pili huongeza hisia za kucheua.

Bia ya tatu 🍺🍺🍺 huanza kumfanya mnywaji aanze kusikia furaha na pia huu huwa wakati ambapo karanga na korosho huliwa sana…. Pamoja na mazungumzo kuhusu mpira na siasa, ghafla mazungumzo kuhusu michepuko huanza kujitokeza…..

Bia ya nne 🍺🍺🍺🍺 huanza kusababisha masikio yaanze kupoteza nguvu za kusikia kwani utaona mnywaji ghafla amepandisha sauti, na ukijumlisha na kuwa baa zetu huwa na muziki una kelele utadhani waliopo wote wana matatizo ya kusikia….. bia hii humsaidia kuongea kwa nguvu kushindana na kelele za muziki.

Bia ya tano 🍺🍺🍺🍺🍺 ni hatari kidogo kwani ukiinuka kwenda chooni mara nyingi unarudi hujafunga zipu……na kipindi hiki ni kibaya kwa wanywaji wa kike maana unaweza kumkuta akienda chooni akijiangalia kwenye kioo anaanza kulia peke yake na kulalamika; ‘Mi sipendwi mpaka leo sijaolewa’ au ‘ Mume wangu sijui yukoje hanijali’

Japokuwa lazima isemwe ukweli ukifikisha bia hii, maisha ni raha sana unaweza ukaanzisha shoo ya kukata mauno katikati ya baa na kudai wewe ni mkali kuliko Shilole.

Kuanzia bia ya sita 🍺🍺🍺🍺🍺🍺 na kuendelea, chochote utakachosema au kufanya ni wazi kesho yake asubuhi utajilaumu sana. ……. …Kuna watu husema ukilewa ndipo unakuwa mkweli, hivyo basi wakati huu hata bosi wako akitokeza unamueleza ukweli jinsi alivyo fala na hajui kuendesha kampuni.

Au unasema ukweli jinsi unavyompenda mke wa jirani yako ambaye mmekaa mnakunywa naye. Kimsingi uwezekano wa kutapika pia upo karibu na kama umekaa na mchumba wako huu ni muda ambao pia uchumba unaweza kuvunjika…….

Cheki huyu mzee alichomfanyia muuzaji wa pharmacy

Mzee kaingia pharmacy,
MZEE: Mambo mwanangu, kuna kitu naomba uonje nitakulipa
MFAMASIA: Kitu gani?….Mzee akatoa kichupa na kijiko akaweka …majimaji yaliyomo kwenye
kichupa kwenye kijiko na kumwambia mfamasia aonje, mfamasia akatia yale maji mdomoni na kuyazungusha zungusha mdomoni akionja;

MZEE: Nipe jibu, ina utamu wa sukari au chumvi au pilipili?
MFAMASIA: Kama chumvichumvi
MZEE: Hakuna sukari
MFAMASIA: Sukari hakuna kabisa
MZEE: Loh asante chukua hii alfu tano nashukuru sana, dokta alinambia nipime mkojo wangu kama nina kisukari, kumbe sina asante bwana mdogo

Utani wa wachaga

Wachaga wamegawanyika kama ifuatavyo, sio wote wajanja. Kuna:-

1. WAROMBO; Hawa wajanja sana kibiashara/wezi pia. wanapenda dili za magendo. Ni walevi sana hupeleka wake zao vijijini wakileta kiburi mjini. Wanaume wa Rombo wanachunwa sana na wanawake wa Marangu na wanawaita “vishohia”. Wanawake wa Rombo ni mama Huruma, wanaachia tu.. Ukioa Mrombo ujue umeolea kijiji.

2. WAMARANGU; Ni wazuri sana wa sura na umbo, wanavutia. Lakini wanawachuna sana Warombo. Wanawake wa Marangu wana dharau sana na wanaume ni waoga kuliko wanawake. Mwanaume wa Marangu kupigwa na mkewe si jambo la ajabu.

3. WAKIBOSHO; wanafanana na Warombo lakini ni wavumilivu zaidi. Biashara kubwa wanayofanya ni ya kuchinja… wengi wanamiliki mabucha. Wana hasira sana na ni wakatili.. Akikuchoma kisu, siku ya mazishi anakuja kudai kisu chake.

4. WAMACHAME; hawa ni wezi sana, ukifanya nae dili umeliwa. Ni wasiri sana lakini wako makini mno hasa kwenye pesa. Wakiwa na hasira hawaoneshi waziwazi, so Mmachame anaweza kukuua huku akitabasamu. Sio waaminifu sana lakini wanaenda kanisani mara nyingi zaidi kuliko Wachaga wote. Wanawake wa machame wanaitwa ‘Wapalestina’.. Mume ukitajirika mkeo anakuua ili arithi mali.

5. WAURU; hawa hupenda kusoma sana lakini hawapendi maendeleo kabisa. Hadi leo eneo lao la Kishumundu linatumika ku-identify wachagga washamba. Wanawake wakifikisha umri wa miaka 40 hua wehu na wanaume huwa vichaa mapema zaidi. Wanaume ni wavivu, lakini wanawake ni wachapakazi hodari. Wanazurura mjini na mabeseni wakiuza ndizi mbivu.. Ukioa Uru jiandae kulea kichaa.

6. WASIHA; Kwanza hawapendi kuitwa Wachagga. Wanajiita watu wa West-Kilimanjaro. Ni mchanganyiko wa Wachagga na WaMeru. Hawapendi shule ila wanapenda zaidi kazi za ufundi na kilimo. Viazi vingi vya Chips Arusha na Moshi vinatoka kwao. Wanawake zao wana “vigimbi” mguuni sababu ya kulima mno.!

7. WAKIRUA; wanapenda sifa kama Wahaya. Wanawake wa Kirua ni wachawi kupindukia.. Wanaloga hata jiwe ili tu alikomoe.. Wanaume wa Kirua hawapendi kuoa kwao.. Hawapendi kuishi mjini maana wanaogopa gharama.. lakini siku wakija mjini wawili tu utadhani wako mia.

8. WA OLD-MOSHI; Hawa ni mafundi stadi wa ujenzi wa nyumba, japo hawajengi kwao. Mpaka leo hamna daladala ya kwenda Old-Moshi inayoanzia Moshi mjini, maana ni wabishi kulipa nauli na pesa inaishia kwenye mbege njiani. Wanaume wamezoea kutoka nyumbani saa kumi na moja alfajiri na kurudi saa sita ya usiku kwa miguu.!

Wachaga mnisamehe!
🏃🏃🏃🏃✋✋

Vichekesho vya kukuondoa mawazo leo

Soma vichekesho hivi;

Mwizi wa atm

Jamaa aliibiwa kadi yake ya benk akaulizwa kama ameripoti polisi akajibu “sijaripoti bado, mwizi mwenyewe hamfikii matumizi kama mke wangu.

Cheka kidogo

Njia rahisi kusahau matatizo yako (japo kwa muda mfupi) vaa viatu vinavyokubana.

Mlizi mbio mbio

Tulikuwa bar moja jana mlinzi kaingia spidi, akamwambia jamaa mmoja aliyekaa kaunta, Mlinzi: Mzee gari lako limeibiwa Mzee: Umemtambua aliyeiba? Mlinzi: Hapana lakini nimeandika namba za gari hizi hapa.

13, 13…

Jamaa alikuwa anapita nje ya wodi ya vichaa akasikia mtu anasema, 13, 13, 13, 13, 13, 13,….. akaamua kuchungulia kwenye kitundu alichokiona ajue kuna nini, ile kuchungulia tu akamwagiwa mchanga wa machoni, sauti ikabadili ikaanza 14,14,14,14,14……

WATAALAM

Jamaa alikuwa anaumwa sana, mkewe akamwita daktari, alipofika akamkuta jamaa kafumba macho;
Dokta: Huyu mbona amekwisha kufa?
Jamaa: Sijafa bwana
Mke: Hebu nyamaza bwana acha kubishana na wataalamu.

Ya leo mgonjwa

Dokta alipotembelea wodi ya mgonjwa wake aliyepata ajali. Mgonjwa akiwa amening’inizwa mikono juu akauliza “dokta ntaweza kweli kupiga kinanda nkitoka hospitali?”
Dokta: Bila shaka utaweza, wewe ni mpiga kinanda mzuri enh?
Mgonjwa: Hapana sijawahi kabisa bado.

4WD

Mwanaume alimnunulia pete ya almasi mkewe, rafiki akauliza “si ulisema anapenda gari yenye four wheel drive, mbona umenunua pete?” Mume akajibu “unadhani wapi ntapata rav4 feki?”

Ajali ilivyotokea

Trafiki polisi akihoji palipotokea ajali “ahaa! Sasa naanza elewa embu nielezee jinsi ajali ilivyotokea wewe ukiwa kama dereva mhusika.” Dereva akajibu “hata sikumbuki nlifumba macho”

Faini ya kukojoa

Polisi alimdaka jamaa anakojoa pembezoni mwa ukuta.
Polisi: Wewe unajua panakatazwa kukojoa hapa?
Jamaa: Sasa nimebanwa nifanyaje?
Polisi: Faini yake elfu tano.
Jamaa akatoa noti ya elfu 10.
Polisi: Sasa chenji tunaipataje?
Jamaa: Tafuta chenji unipe changu.
Polisi: Basi kojoa tena…

Mume anaenda kazini

Jamaa kaamka asubuhi sana Jumamosi, mvua inanyesha kang’ang’ania kuwa anaenda ofisini. Kawasha gari yake, kufika njiani hali ilikuwa mbaya kaamua kurudi. Kafika home kavua nguo kaingia tena kitandani, kamnong’oneza mkewe aliyekuwa usingizini; “Yaani hali ya hewa huko nje mbaya sana” Mke: Si ndio nimemshangaa huyu mpumbavu eti kaenda kazini…

Hasira za mtoto

Baba na mtoto:
Baba: Mwanangu ukiwa na hasira unafanya nini?
Mtoto: Naenda chooni.
Baba: Chooni? Kufanya nini?
Mtoto: Kusafisha.
Baba: Halafu ndio hasira zinaisha?
Mtoto: Ndio. Nasafisha choo kwa mswaki wako.

Mgonjwa na Dokta

Mgonjwa: Dokta nimekuja nahisi ninaumwa Malaria na kifua.
Dokta: Sasa ushajua unaumwa nini hapa umefuata nini kwangu?
Mgonjwa: Sasa si nimekuja kwa dokta.
Dokta: Wanaojua kuwa wanaumwa kama wewe wanapitiliza maabara.

Pilau la bachela

Bachela mmoja aliyekua akiishi kwa muda mrefu peke yake kwenye nyumba aliyopanga siku moja alitaka kupika pilau kwa mara ya kwanza. Sasa asijue nini kinachobadilisha rangi ya wali kuwa rangi ya brown, yeye akapika kama kawaida (wali) kisha wakati wa kula akavaa miwani yenye rangi ambayo ukiuangalia wali unauona kama pilau wakati anakula.

Mwizi na chizi

Mwizi kaiba TV na kuanza kukimbia nayo, kumbe ile nyumba mlikuwa na chizi, akaanza kumkimbiza yule mwizi. Kila mwizi akiongeza mbio chizi nae huyo, mwishowe mwizi akasalimu amri na kusimama, yule chizi akamsogelea na kumwambia.. Daah umesahau remote hii hapa mwizi kafleti.

Chemsha bongo

Baba akimuuliza chemsha bongo mwanae anayesoma shule ya chekechea “haya niambie kitu gani hakiwezi kuliwa wakati wa breakfast?” Mtoto akajibu “hiyo mbona rahisi baba, si lunch na dinner”

Status za Whatsapp za Wazungu na Wabongo

STATUS ZA WAZUNGU kwenye Whatsapp vere vere kliaaa…
👉sick
👉at movie
 👉 in a meeting2
👉 kind of happy,, 👉busy,,
👉available
👉Driving
👉sleeping

STATUS ZA WABONGO SASA MBUTA NANGA MBONGO NGAFU

“Akutake nani una shepu la Kitorondo utaishia kumegwa na kuachwa

“Watu tuna nyota za Chips Mayai sio wewe mwenye Nyota ya Punda,halulaaa”

👌Kantangazeee ndo Kwanza naanza na ntakukomesha Mwanaharamu we!

😍 I love yu so much ur my only one,No one lyk yu and I mean it 🎶 Yu ma numba1 ma sweet sweet namba1 roho yangu mama,,

👍 Asante 😍 vimenitoshaaa tena kama ulijua 😘😘😘😘😘,

💪 unajifanya simba kumbe nyau mimi ndo maji kama hujanioga utaninywaa,

🙈 nauza Ubuyu kwa bei nafuuu kama unataka inbox me plz

😔 poleee jaman utapona wangu,,,

💪 utalijua jiji na chuki zako walingia na tako wakati hadi nyani analo kitu sura dada…

😡 usinisemeshe usiniongeleshe tena utaniambia vizur ulikuwa wapi..

😷 mdomo kaumbiwa mwanadamu ongeeni nyie me sijali ya wanafiki nafanya yangu huna hadhi ya kujibiwa na mimi
pamoja na ya kwako uloweka🙈😆😆😆

Angalia nilivyoingizwa mjini na ujanja wangu wote

Ndio nilikuwa nimeshuka kwenye basi la SAI BABA pale Ubungo, nina Begi kubwa Mgongoni na begi Dogo la Lap Top mkononi, sura inatazama Mbele Very Serious kama nipo kwenye Gwaride la Uhuru!..Mabega juu yanafanya Cheers na Mawingu!, natembea kwa madoido…..leo nimetoka Likizo Moshi,

“Brother Simu ya ukweli hii..kitu cha Tecno C9 bei poa” hii ilikuwa sauti ya Teja mmoja hivi!

Yaani huyu Teja Bwege kweli,anataka kumuuzia nani sabuni? mimi sio wa kuja!…kamwe Siwezi kuibiwa hapa Town,hakuna wizi au utapeli nisioujua!, Mimi nimezaliwa Mwananyamala kwa Manjunju, nikalelewa Tandale kwa Mtogole, Shule ya msingi nimesoma Turiani Magomeni, Hivi Mbwa gani aniibie?…kwa Style ipi?

Sipendi kabisa Upuuzi!, Wajinga ndio wataibiwa, sio Mimi!…sasa Kwa mwendo wa haraka nikatoka nje kabisa ya Stendi ya Ubungo straight mpaka Stendi ya dala dala za Kariakoo, hapo ndipo nikakutana na Vijana wawili wadogo wakiwa na mzani wa kupimia uzito,…hakika napenda sana vijana wanaojituma kama hawa na sio ile Mijizi ya kule ndani Stendi!!,….hapa sasa nikapata wazo!

“Dogo mnapima uzito kwa shilingi ngapi?”

“Mia mbili tu Kaka!”

”Ok”

Kwa mwendo wa kikakamavu nikapanda juu ya mzani,lengo hapa ni kujua uzito wangu, Mtori niliokula mwezi mzima kule kwa Mshekuu sio mchezo, hapa nahisi nacheza kwenye kg za John Cena,

“Mama wee! Dogo mzani mzima huu kweli? Mbona nina kilo 134?” (Nilihamaki)

“Aaah! Brother huoni umepanda na Mabegi juu ya mzani?”’

Hahaha! kweli nimechanganyikiwa!…Sasa nikatoa mabegi yote mawili na kurudi juu ya Mzani, hapa ndipo Uzito ukashuka kutoka kg 134 mpaka kg 56!…My God kweli Body la “One Pack ” haliongopi! thats means mabegi yaliniongezea kg 78! duh hii ni hatari!

“Yaani we Dogo kitambi chote hiki kg 56? huu Mzani Mzima kweli?”

Kimya…

“Dogo huu Mzani vipi?”

Kimya…

Dogo ana dharau huyu!…Sasa ndio nikabandua macho yangu toka kwenye kioo cha mzani ili nimtazame huyu dogo asiyejibu!….ndipo macho yangu yakakutana na Kigoda tupu kilichochongwa Mvomero!…Dogo hakuwepo!….na Mabegi pia hayapo!…lap top haipo!….NIMEPIGWA!

Ni dhahiri watoto wa Mjini walikuwa wameniacha juu ya Mzani, wamechukua Lap top ya Milioni na wameniachia Mzani chakavu wa elfu 40, what a stress!….sasa nilirudisha macho kwenye kioo cha uzito na sasa kilisoma KG 38!…yaani dakika hii hii nimepungua kilo zingine 18, Hakiyamama nahisi hata utumbo wangu wamebeba!…niitieni Ambulance!

🙆🏼🙆🏼🙆🏼🙆🏼🙆🏼🙆🏼🙆🏼🙆🏼🙆🏼🙆🏼🙆🏼

Kilichompata sista duu bishoo wakati akijidai kununua pete

Mwanamke mmoja aliingia duka la vito vya thamani, akaona pete moja ya dhahabu nzuri sana amabayo ilikuwa kwenye shelf ya chini, wakati anainama apate kuitazama vizuri kwa bahati mbaya (au nzuri!), shuzi likamtoka- druuuuuu, soni ikamuingia huku akigeuka haraka kuangalia kama kuna yeyote dukani pale ameliskia shuzi lake, macho yakagongana na mwenye duka ambaye alikuwa karibu huku uso ukiwa umejaa tabasamu zito, mwana mama hakuwa na uhakika kama amesikika au hakusikika, akaona atumie nafasi ile kuyeyusha…Akauliza “Hii pete bei gani?” . Jamaa mwenye duka, huku akiangua kicheko, akajibu “Umeiona tu umejamba, je nikikuambia bei yake si utakunya kabisa?”

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About