Upendo wa siku zote
Upendo wa siku zote huo ndio upendo atakao Mungu. Chuki na unafiki ni tabia ya Shetani, umoja ni tabia ya Mungu.
Upendo wa siku zote huo ndio upendo atakao Mungu. Chuki na unafiki ni tabia ya Shetani, umoja ni tabia ya Mungu.
Hakuna sala yeyote itolewayo kwa unyenyekevu wa kweli katika imani, matumaini na mapendo inayopita bure mbele ya Mungu. Mungu hamtupi mwenye unyoofu wa moyo.
Sala ni Hazina. Kusali ni muhimu sana. Sala unayosali leo inaweza kukusaidia hata miaka kumi ijayo au ikasaidia watoto wa watoto wako. Mungu ni mwenye fadhila na anakumbuka yote. Mwombe Mungu akulinde ukiwa mzima ili uwapo hatarini akukumbuke hata kabla hujamwomba.
Upendo hauandamani na ubinafsi. Huwezi kusema una upendo wa kweli kama huwezi kujinyima vile unavyovipenda kwa ajili ya yule au wale unaowapenda. Upendo wa kweli ni kujitoa.
Huwezi kusema unampenda Mungu usiyemuona kama huwapendi watu wale unaowaona. Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe. Vile unavyotaka akutendee mtendee vivyo hivyo.
Mawazo ya Mungu ni makuu. Mungu anatuwazia mema daima. Hata unapopitia shida na matatizo katika maisha nia ya Mungu inabaki kuwa njema ya Kukuonyesha ukuu wake na kukuwezesha kumjua yeye. Pengine usingejua matendo ya Mungu bila kupitia shida na changamoto katika maisha. Mungu hapendi upate shida bali anaruhusu hayo ili upate faida ya kumjua na kujua uwezo wake. Hata Yesu ilibidi apitie mateso na kifo ili uwezo wa Mungu udhihirike baada ya kufufuliwa. Amini kuwa kuna mema mbele yako baada ya mateso haya ya sasa.
Mungu anamjibu mtu sala zake kutokana na anachonuia.
Kukosa hata mara moja inahesabika ni kukosea mbele ya Mungu. Kwa kuwa kwa Mungu hakuna kusema, ‘Kukosea mara moja sio kosa bali kurudia kosa ndio kosa’. Mbele ya Mungu kila kosa lina uzito wake haijalishi ni kosa la mara ya kwanza.
Kutubu ndio njia pekee ya kumrudia Mungu. Toba ya kweli ndiyo iletayo maondoleo ya dhambi. Ukiondolewa dhambi unaimarishwa na kufanywa mya. Tubu usamehewe na kufanywa mpya.
Sala sio maneno mengi au maneno ya kurudiarudia. Sala ni maneno au hata neno moja la kimapendo litamkwalo kwa imani na kwa nia thabiti.
Uhuru Na Amani Ya Moyoni hupatikana kwa kusali wala sio kwa kusoma vitabu na kujua sana Mambo mengi.
Uzuri wa Mungu ni kwamba anasamehe na kisha anasahau. Unapotubu dhambi zako na kutaka huruma zake yeye anakufutia uovu wote na kukufanya mpya.
Uwe na subira Baada ya kuomba kwa Mungu. Sio kila unachoomba kwa Mungu utakipata kwa wakati huo huo au kwa wakati unaofikiri. Mungu ni Mwaminifu Sana Kwenye kujibu maombi lakini vile vile ni mwenye Hekima Kwenye kukujibu, anajua wakati gani ni sahihi kukujibu maombi yako. Anaweza kukujibu saa hiyo hiyo, kesho, keshokutwa au hata mwakani kwa kuangalia wakati ufaao na kwa manufaa yako. Kwa hiyo unapoona hujajibiwa usife moyo, bali uwe na matumaini. Mungu anajua akujibu lini kwa kuwa anajua ni lini wakati ufaao na ni lini kitu kipi kina kufaa.
Kama mtu anasali kila siku katika maisha yake hakuna kitu kitakachokuwa kigumu. Sala ni njia ya kujipatia neema za kuendesha maisha yetu. Usiache kusali kila siku hata kama upo katika hali gani.
Vile unavyomsogelea Mungu ndivyo na yeye anavyokusogelea. Vile unavyomkubali Mungu katika Maisha yako ndivyo na yeye anavyotenda kazi kwako.
Unapo mwomba Mungu Usisahau Kushukuru. Kushukuru ni kuomba mara ya pili. Utazidishiwa kile ulichokiomba na kupewa hata usichokiomba kwa shukrani yako.
Sala pasipo Imani thabiti, ya nia ya kweli, upendo wa kweli, unyenyekevu wa ndani na tumaini la kweli katika Amani ya rohoni; Haijakamilika na haifai kitu.
Mungu haangalii matemdo ya mtu ya nje tuu, bali anaangalia ndani kabisa mawazo ya mtu na nia yake. Nia ya mtu ndiyo inayoonyesha mtu alivyo.
Mungu ni mwenye Huruma na Upendo na Anataka watu wote waokolewe naye. Mungu hayupo kwa ajili ya kukuhukumu bali kwa ajili ya kukuhurumia na kukurehemu.
Mtumainie Mungu kwa maana Mungu hawatupi wale wamtumainiao na kumgoja. Mkono wake upo tayari kwa ajili ya kuwaokoa wale wanaomwelekea.
Recent Comments