Mkono wa Mungu
Kila jambo lina Mkono wa Mungu juu yake hata kama limefanyika bila kupangwa au kukusudiwa. Mbele ya Mungu hakuna kitu kinachofanyika kwa Ajali au bahati mbaya.
Kila jambo lina Mkono wa Mungu juu yake hata kama limefanyika bila kupangwa au kukusudiwa. Mbele ya Mungu hakuna kitu kinachofanyika kwa Ajali au bahati mbaya.
Sala ndiyo chimbuko la fadhila. Kwa njia ya sala tunapata fadhila za Kimungu na Neema za Mungu. Asaliye daima hujazwa neema na fadhila.
Ukitaka kupata amani, tumaini katika Ahadi za Mungu. Ahadi ya Mungu ni hii “Hatoacha kutusaidia wala kututupa”.
Kwa njia ya sala Binadamu anampa Mungu Utukufu, Mungu anampa Binadamu Wokovu na Neema.
Hakuna kitu cha Muhimu zaidi Duniani kama kumjua Mungu na kumuishi Mungu. Kila binadamu ameumbwa kwa ajili hii. Na Mungu anachotaka ndicho hichi, kumjua na kumuishi. Mengine yote ni maziada. Ukimuishi Mungu atakufanikisha katika yote.
Sala ni kama chakula cha Roho, Bila sala roho inakufa. Tusali daima ili roho zetu ziwe hai siku zote.
Mungu haangalii matemdo ya mtu ya nje tuu, bali anaangalia ndani kabisa mawazo ya mtu na nia yake. Nia ya mtu ndiyo inayoonyesha mtu alivyo.
Uzuri wa Mungu ni kwamba anasamehe na kisha anasahau. Unapotubu dhambi zako na kutaka huruma zake yeye anakufutia uovu wote na kukufanya mpya.
Uwe na subira Baada ya kuomba kwa Mungu. Sio kila unachoomba kwa Mungu utakipata kwa wakati huo huo au kwa wakati unaofikiri. Mungu ni Mwaminifu Sana Kwenye kujibu maombi lakini vile vile ni mwenye Hekima Kwenye kukujibu, anajua wakati gani ni sahihi kukujibu maombi yako. Anaweza kukujibu saa hiyo hiyo, kesho, keshokutwa au hata mwakani kwa kuangalia wakati ufaao na kwa manufaa yako. Kwa hiyo unapoona hujajibiwa usife moyo, bali uwe na matumaini. Mungu anajua akujibu lini kwa kuwa anajua ni lini wakati ufaao na ni lini kitu kipi kina kufaa.
Mungu daima ni Mwaminifu na mwenye Huruma. Kinachotakiwa ni kuamini kwamba kipo na kitakuwepo. Kusadiki kwamba kitafanyika na kitafanyika. Hii ndiyo Siri ya Imani.
Unapo mwomba Mungu Usisahau Kushukuru. Kushukuru ni kuomba mara ya pili. Utazidishiwa kile ulichokiomba na kupewa hata usichokiomba kwa shukrani yako.
Inashangaza kwa sasa watu wengi hawapendi kuambiwa kuhusu kutubu dhambi zao bali wanataka waambiwe watabarikiwa. Kama vile wewe huwezi kumvika mwanao nguo nzuri kabla ya kumuogesha vivyo hivyo na Mungu hawezi kukubariki kabla ya kukutakasa. Unapotubu unasamehewa na kutakaswa dhambi zako kisha unakua umefungua milango ya baraka. Huwezi kubarikiwa bila kutubu kweli.
Kama vile Baba anavyotamani mwanae akue katika maadili na aelekee katika njia nyoofu. Ndivyo na Mungu anavyotamani uachane na dhambi na kumfuata yeye.
Upendo wa Mungu hauna kikomo. Mama anaweza kumchoka na kumtelekeza mwanae lakini Mungu kamwe hamchoki mtu.
Kama mtu anasali kila siku katika maisha yake hakuna kitu kitakachokuwa kigumu. Sala ni njia ya kujipatia neema za kuendesha maisha yetu. Usiache kusali kila siku hata kama upo katika hali gani.
Uhuru Na Amani Ya Moyoni hupatikana kwa kusali wala sio kwa kusoma vitabu na kujua sana Mambo mengi.
Mungu ni rahisi sana kupatikana. Ugumu ni njia ya Kumtafuta Mungu na namna ya kumuishi Mungu. Hapa ndipo watu wengi wanashindwa.
Sala siyo maneno mazuri, bali sala ni NIA ya Upendo iliyobebwa na maneno mazuri. Tusali kwa kunuia kutoka moyoni na sio kwa kunena maneno tuu mdomoni.
Usifadhaike moyoni pale unapokuwa katika matatizo au unapopitia changamoto katika maisha. Kumbuka kuwa Mungu yupo, anayaona hayo na anataka kukusaidia, ni wewe tuu kumpa nafasi ya kukusaidia. Hatumpi Mungu nafasi pale tunapozani tunaweza wenyewe.
Njia pekee ya Kumrudia Mungu tunapoanguka dhambini ni Njia ya Toba ya kweli ikiambatana na kukiri makosa na kusamehewa. Mara nyingi tunapotubu tunasahau dhambi za mawazo na kukumbuka za matendo tuu. Dhambi ya Mawazo pia ni dhambi yapaswa toba na maondoleo.
Recent Comments