Uhuru na Amani ya Moyoni
Uhuru Na Amani Ya Moyoni hupatikana kwa kusali wala sio kwa kusoma vitabu na kujua sana Mambo mengi.
Uhuru Na Amani Ya Moyoni hupatikana kwa kusali wala sio kwa kusoma vitabu na kujua sana Mambo mengi.
Vile unavyomsogelea Mungu ndivyo na yeye anavyokusogelea. Vile unavyomkubali Mungu katika Maisha yako ndivyo na yeye anavyotenda kazi kwako.
Inashangaza kwa sasa watu wengi hawapendi kuambiwa kuhusu kutubu dhambi zao bali wanataka waambiwe watabarikiwa. Kama vile wewe huwezi kumvika mwanao nguo nzuri kabla ya kumuogesha vivyo hivyo na Mungu hawezi kukubariki kabla ya kukutakasa. Unapotubu unasamehewa na kutakaswa dhambi zako kisha unakua umefungua milango ya baraka. Huwezi kubarikiwa bila kutubu kweli.
Upendo wa siku zote huo ndio upendo atakao Mungu. Chuki na unafiki ni tabia ya Shetani, umoja ni tabia ya Mungu.
Fikiria umenunua zawadi nzuri ya gharama sana na unataka kumpa mtu umpendaye sana. Akipokea zawadi yako unafurahi sana, akikataa kuipokea zawadi inaumiza sana, lakini inaumiza zaidi akiipokea kisha akaitupa mbele yako na kuona haina maana. Hiki ndicho kinachotokea kwa Yesu. Yesu yupo kwa ajili ya kutupa zawadi ya Wokovu alyogharamia kwa uhai wake. Tunapoipokea tunamfurahisha sana, tukiikataa tunamhuzunisha na tunapoipokea na kuiacha baadae tunamhuzunisha kwelikweli.
Upendo wa Mungu hauna kikomo. Mama anaweza kumchoka na kumtelekeza mwanae lakini Mungu kamwe hamchoki mtu.
Upendo hauandamani na ubinafsi. Huwezi kusema una upendo wa kweli kama huwezi kujinyima vile unavyovipenda kwa ajili ya yule au wale unaowapenda. Upendo wa kweli ni kujitoa.
Uwe na maono au ndoto ya mambo unayotaka kufanya maishani naye Mungu atakubariki na kujidhihirisha katika ndoto zako.
Mungu anasubiri sala zako kila siku. Anasubiri sala zako akujibu ili uone utukufu wake. Anasubiri sala zako ili akuze mahusiano yake na wewe. Sali daima kwani Mungu yupo milele kukusikiliza na kukuhudumia.
Mungu ni rahisi sana kupatikana. Ugumu ni njia ya Kumtafuta Mungu na namna ya kumuishi Mungu. Hapa ndipo watu wengi wanashindwa.
Mtumainie Mungu kwa maana Mungu hawatupi wale wamtumainiao na kumgoja. Mkono wake upo tayari kwa ajili ya kuwaokoa wale wanaomwelekea.
Kwa kawaida kwenye maisha unapofikia Hatua unaona Mungu hayupo kabisa na wewe basi ujue huo ndio wakati ambao Mungu yupo karibu na wewe zaidi.
Njia pekee ya Kumrudia Mungu tunapoanguka dhambini ni Njia ya Toba ya kweli ikiambatana na kukiri makosa na kusamehewa. Mara nyingi tunapotubu tunasahau dhambi za mawazo na kukumbuka za matendo tuu. Dhambi ya Mawazo pia ni dhambi yapaswa toba na maondoleo.
Mungu ni mwenye Hekima, anajibu Sala zetu kwa kutupa kile tunachohitaji na chenye kutufaa na Sio kutupa kile tunachokitaka na kukitamani kwa kuwa anatupenda na kututakia mema.
Mungu ni mwenye Huruma na Upendo na Anataka watu wote waokolewe naye. Mungu hayupo kwa ajili ya kukuhukumu bali kwa ajili ya kukuhurumia na kukurehemu.
Sala sio kitu cha muhimu kufanya wakati wa shida tuu. Sala ni kitu cha muhimu zaidi kila siku katika Maisha kuwe na shida au kusiwe na shida.
Kila jambo lina Mkono wa Mungu juu yake hata kama limefanyika bila kupangwa au kukusudiwa. Mbele ya Mungu hakuna kitu kinachofanyika kwa Ajali au bahati mbaya.
Usiogope wala usisite kutubu na kuomba msamaha kwa Mungu. Uwe na Amani na Matumaini katika Huruma ya Mungu itokayo katika Upendo wake wa Mfano wa baba awapendavyo wanawe. Mungu anasubiri kukupokea kwenye mikono yake Ili akutunze kama mtoto wake kama utatubu na kumrudia yeye. Amua kumwendea leo! Anakungoja ni wewe tuu…
Mungu anamjibu mtu sala zake kutokana na anachonuia.
Hakuna sala yeyote itolewayo kwa unyenyekevu wa kweli katika imani, matumaini na mapendo inayopita bure mbele ya Mungu. Mungu hamtupi mwenye unyoofu wa moyo.
Recent Comments