Sala ni ufunguo
Sala ni ufunguo wa kufungulia mema na kufungia Mabaya. Tusali ili tufungue mema katika maisha yetu na tufunge mabaya katika maisha yetu.
Sala ni ufunguo wa kufungulia mema na kufungia Mabaya. Tusali ili tufungue mema katika maisha yetu na tufunge mabaya katika maisha yetu.
Usiache kusali na kutenda mema kwa kuwa huwezi jua ni watu wangapi wanategemea sala na matendo yako mema. Kumbuka Mungu alimwambia Abraham kama akikuta Wacha Mungu wengi hataiharibu Sodoma na Gomora. Vivyo hivyo Inawezekana wapo watu wengi wanaonufaika na Sala na matendo yako, hasa watu wako wa karibu uwapendao. Unapokuwa mtu wa Sala na mcha Mungu unabarikiwa wewe na wale wa karibu yako. KAMWE USIACHE KUMCHA MUNGU NA KUSALI. Ukiwa mregevu ni sawa na unakata Mnyororo wa Baraka za Mungu kwako na wenzako.
Mungu anasubiri sala zako kila siku. Anasubiri sala zako akujibu ili uone utukufu wake. Anasubiri sala zako ili akuze mahusiano yake na wewe. Sali daima kwani Mungu yupo milele kukusikiliza na kukuhudumia.
Sala yoyote ili iwe SALA lazima itolewe kwa Imani, Upendo, Unyenyekevu na kwa Matumaini. Sala kama hii ndiyo ipendezayo mbele ya Mungu.
Sala ni kama chakula cha Roho, Bila sala roho inakufa. Tusali daima ili roho zetu ziwe hai siku zote.
Kama vile Baba anavyotamani mwanae akue katika maadili na aelekee katika njia nyoofu. Ndivyo na Mungu anavyotamani uachane na dhambi na kumfuata yeye.
Sala siyo maneno mazuri, bali sala ni NIA ya Upendo iliyobebwa na maneno mazuri. Tusali kwa kunuia kutoka moyoni na sio kwa kunena maneno tuu mdomoni.
Kwa njia ya sala Binadamu anampa Mungu Utukufu, Mungu anampa Binadamu Wokovu na Neema.
Mungu ni mwema sana tunapokua wadhambi anapotuadhibu haimaanishi kuwa anatuchukia. Inamaanisha kuwa anatuonya na hapendi turudie makosa.
Hakuna Binadamu anayemchukia Mungu kama hajichukii yeye mwenyewe na wale wanaomzunguka. Huwezi kusema humtaki Mungu kama hujichukii mwenyewe na wale waliokuzunguka vivyo hivyo huwezi kusema Unampenda Mungu kama hupendi wengine waliokuzunguka.
Upendo wa Mungu hauna kikomo. Mama anaweza kumchoka na kumtelekeza mwanae lakini Mungu kamwe hamchoki mtu.
Hakuna Maisha ya Kikristo bila Kusali. Kama kuna Mkristo anaishi bila kusali huyo siyo Mkristo bali Mkristo mfu. Sala ndiyo uhai wa Mkristo. Hakuna Njia nyingine yoyote ya kumfikia Mungu isipokua sala.
Mungu ni mwenye Hekima, anajibu Sala zetu kwa kutupa kile tunachohitaji na chenye kutufaa na Sio kutupa kile tunachokitaka na kukitamani kwa kuwa anatupenda na kututakia mema.
Kama yalivyo maisha ya kimwili, maisha ya kiroho pia yanahitaji mipango. Kila siku panga utafanya nini kiroho, mfano unaweza kupanga sala, kusaidia masikini, kuwa mpole au mwema. Vivyo hivyo kila wiki, kila mwezi na kila mwaka mpya panga cha kufanya kiroho naye Mungu atakubariki na kukupangia zaidi. Huwezi kufanikiwa kiroho kama hujui unafanya nini kiroho.
Uhuru Na Amani Ya Moyoni hupatikana kwa kusali wala sio kwa kusoma vitabu na kujua sana Mambo mengi.
Uwe na maono au ndoto ya mambo unayotaka kufanya maishani naye Mungu atakubariki na kujidhihirisha katika ndoto zako.
Sala ndiyo chimbuko la fadhila. Kwa njia ya sala tunapata fadhila za Kimungu na Neema za Mungu. Asaliye daima hujazwa neema na fadhila.
Fikiria umenunua zawadi nzuri ya gharama sana na unataka kumpa mtu umpendaye sana. Akipokea zawadi yako unafurahi sana, akikataa kuipokea zawadi inaumiza sana, lakini inaumiza zaidi akiipokea kisha akaitupa mbele yako na kuona haina maana. Hiki ndicho kinachotokea kwa Yesu. Yesu yupo kwa ajili ya kutupa zawadi ya Wokovu alyogharamia kwa uhai wake. Tunapoipokea tunamfurahisha sana, tukiikataa tunamhuzunisha na tunapoipokea na kuiacha baadae tunamhuzunisha kwelikweli.
Upendo wa Mungu hauna mwisho. Mtu anaweza akaacha kukupenda na kukusahau kabisa lakini kamwe Mungu haachi kumpenda Mtu wala hamsahau Mtu.
Sala sio maneno mengi au maneno ya kurudiarudia. Sala ni maneno au hata neno moja la kimapendo litamkwalo kwa imani na kwa nia thabiti.
Recent Comments