Dondoo za Mapishi na Lishe

LISHE BORA KWA WATU WENYE AFYA NZURI

โ€ข Kula chakula bora kunamaanisha kula vyakula aina tofauti ya vyakula kila siku kama vile matunda, mboga, maziwa na aina ya vyakula vyenye asili ya nyama wa kufuga kama kuku, mbuzi, ngombe, samaki na na vyakula vya nafaka.

โ€ข Lishe bora linamaanisha pia kula chakula ambacho hakina mafuta mengi, sukari au chumvi nyingi

โ€ข Zingatia angalau vyakula vya nafaka kama vile mtama, mahindi, mchele, ngano, wimbi, ndegu, njegere. n.k

โ€ข Ni bora kula matunda mengi kama โ€˜maembe, ndizimbivu, papai, pera, chungwa, ubuyu, nanasi, pesheni, zambarauโ€ na mbogamboga kama vile โ€œmchicha, majani ya mboga, karoti, nyanya chungu, nyanya, mkunde, biringanyaโ€ mara tano kwa siku.

โ€ข Kama mboga na matunda hazipatikani ni bora kununua zile ambazo zimehifadhiwa tayari kwenye mikebe au zile ziko kwenye jokofu (friji).

โ€ข Punguza kula vyakula ambavyo vinapikwa kwa mafuta mengi na chumvi nyingi

โ€ข Lishe bora hukusaidia wewe na jamii yako kuishi vyema, kuwa na afya bora, kufanya kazi vizuri na kwa bidii, shuleni na hata kucheza.

Mapishi ya Wali Wa Mboga Na Mchuzi Wa Kuku wa Tanduri

Vipimo vya Wali:

Mchele basmati – 3 magi (kikombe kikubwa)

Mchanganyiko wa mboga za barafu

(Frozen vegetables) – 1 ยฝ mug

Chumvi – kiasi

Mafuta – 3 vijiko vya chakula

Kitungu maji (kilichokatwa) – 1

Bizari ya pilau (nzima) – 1 kijiko cha chakula

Namna Ya kutayarisha na kupika:

Osha mchele uroweke kwenye maji muda wa dakika 20.
Chemsha maji kwenye sufuria kama magi 6.
Tia chumvi.
Yakisha kuchemka unatia mchele, chemsha usiive sana, uive nusu kiini. Mwaga maji na kuchuja wali.
Unamimina Yale mafuta kwenye sufuria unakaanga bizari ya pilau kidogo na kitunguu kabla ya kugeuka rangi ya hudhurungi (brown).
Tia mchanganyiko wa mboga za barafu.,
Mimina wali, changanya vizuri, ufunike na uweke katika moto mdogo kwa dakika 20.
Pakua tayari kwa kuliwa.

Vipimo Vya Mchuzi

Kuku – 2 Ratili (LB)

Chumvi – Kiasi

Mafuta – ยผ Kikombe

Nyanya Kata vipande – 4

Nyanya kopo – 2 vijiko wa chakula

Tangawizi – 1 kijiko ya chakula

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko ya chakula

Tanduri masala – 1 kijiko cha chakula

Kotmiri liliyokatwa – 3 vijiko vya chakula

Pilipili mbichi – 2

Pili masala – 1 kijiko cha chakula

Garam masala – ยฝ kijiko cha chakula

Bizari manjano – ยฝ kijiko cha chakula

Mtindi – 3 vijiko vya chakula

Pilipili boga (kata vipande virefu) – 1

Ndimu – 2 vijiko vya chakula

Namna ya kutayarisha na kupika:

Kwenye bakuli tia kuku na changanya vitu vyote pamoja isipokua mafuta.
Tia mafuta kwenye sufuria yakisha kupata moto mimina kuku umpike kwa muda ยฝ saa kwa moto kiasi.
Pakua kuku kwenye bakuli au sahani na ukate vitunguu maji duara na umpambie. Tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Kabichi

Mahitaji

Kabichi 1/2 kilo
Nyanya ya kopo 1/2
Kitunguu 1
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Kwanza kabisa bandua magada ya juu ya kabichi, kisha ioshe na uikaushe maji baaba ya hapo katakata kabichi (inapendeza zaidi kama ikikatwa nyembamba) kisha saga pamoja nyanya na kitunguu. Baada yahapo tia katika sufuria ya kupikia, ipike mpaka maji yote yatakapokauka kisha tia chumvi, curry powder na mafuta pika kwa muda kiasi kisha tia kabichi na upunguze moto. Pika mpaka kabishi itakapoiva kisha ipua na itakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuila kwa wali au ugali.

Jinsi ya kupika Biskuti Ya Keki Kavu kwa kizungu Shortcake

Viamba upishi

Unga 2 Magi (vikombe vya chai)

Sukari iliyosagwa 2/3 Magi (kikombe cha chai)

Siagi โ€… 220ย g

Unga wa mchele ยฝ Magi

Yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya vitu vyote hivyo kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.

2. Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30ย cm au (8 in kwa 12 in)

3. Choma kwenye moto 325หšC kwa muda wa saa nzima au mpaka ibadilike kuwa rangi ya dhahabu.

4. Epua acha ipoe kisha kata vipande kama mstatili, weak kwenye sahani tayari kunywewa na chai.

Jinsi ya kutengeneza Visheti Vyeupe Na Vya Kaukau

VIAMBAUPISHI

Unga – 4 Vikombe vya chai

Siagi – 1 Kikombe cha chai

Hiliki ยฝ Kijiko cha chai

VIAMBAUPISHI:SHIRA

Sukari – 2 Vikombe vya chai

Maji – 1 Kikombe cha chai

Vanilla ยฝ Kijiko cha chai

(cocoa ukipenda kugawa visheti aina mbili) 2 Vijiko vya chai.

JINSI YA KUTENGENEZA

Tia unga kwenye bakuli pamoja na siagi na hiliki.
Changanya vizuri isiwe na madonge.
Tia maji baridi vikombe viwili kasoro vya chai changanya ukiona bado ongeza maji kidogo, iwe kama chapati usikande uchanganye tu.
Halafu utakata sampuli unayopenda mwenyewe.
Unaweka karai ya mafuta yakisha kupata moto unaanza kuchoma moto usiwe mkali sana, kiasi, baadae unaweza kuongeza moto na vikaange hadi viwe rangi ya dhahabu, kisha viepue vichuje mafuta. .
Ukipenda gawa visheti sehemu mbili, na shira pia igawe sehemu mbili
Changanya nusu ya visheti kwa shira nyeupe.
Nusu ya shira nyingine ibandike tena motoni na tia cocoa vijiko viwili vidogo vya chai.
Inapochanganyika cocoa vizuri changanya nusu ya visheti ulivyogawa kupata visheti vya shira ya cocoa.

Mapishi ya mboga ya mnavu

Viamba upishi

Mnavu mkono 1
Kitungu 1
Karoti 2
Maziwa kikombe 1
Mafuta vijiko viubwa 4
Karanga zilizosagwa kikombe 1
Chumvi kiasi ยฝ

Hatua

โ€ข Chambua mnavu, osha na katakata.
โ€ข Menya, osha na katakata kitunguu.
โ€ข Osha, menya na kwaruza karoti.
โ€ข Kaanga karanga, ondoa maganda na saga zilainike.
โ€ข Kaanga vitunguu na karoti mpaka zilainike ukikoroga.
โ€ข Weka mnavu na chumvi koroga sawa sawa, funika kwa dakika 5-10 (kama ni kavu weak maji kidogo).
โ€ข Changanya maziwa na karanga, ongeza kwenye mnavu ukikoroga kisha punguza moto kwa dakika 5.
โ€ข Onja chumvi na pakua kama kitoweo.
Uwezekano
Weka nyanya kidogo.
Tumia tui la nazi au krimu badala ya maziwa.
Weka nyama au dagaa au Mayai badala ya Karanga.

Mapishi ya Kuku wa kukaanga

Mahitaji

Miguu ya kuku (chicken legs) 10
Kitunguu swaum na tangawizi (ginger & garlic paste) 1 kijiko cha chakula
Limao (lemon) 1
Pilipili iliyosagwa (ground scotch bonnet) 1/2
Giligilani iliyokatwakatwa (chopped coriander) kiasi
Chumvi (salt) kiasi
Mafuta ya kukaangia (veg oil)

Matayarisho

Safisha kuku kisha mtie kwenye sufuria na viungo vyote (kasoro mafuta na giligilani) kisha mchemshe mpaka aive na umkaushe supu yote. Baada ya hapo mkaange katika mafuta mpaka awe wa brown kisha mtoe na uweke katika kitchen towel ili kuchuja mafuta. Baada ya hapo weka katika sahani na umwagie giligilani kwa juu. Na hapo kuku wako atakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya choroko

Mahitaji

Choroko kikombe 1 na nusu
Nazi kopo 1
Kitunguu kikubwa 1
Nyanya 1/2 kopo
Swaum 1 kijiko cha chai
Curry powder 1 kijiko cha chai
Chumvi kiasi
Olive oil
Pilipili nzima

Matayarisho

Loweka choroko usiku mzima kisha zichemshe mpaka ziive na ziweke pembeni. Baada ya hapo saga pamoja nyanya, kitunguu, na swaum kisha vipike mpaka maji yote, baada ya hapo tia mafuta na curry powder, pika mpaka nyanya zitoe mafuta kisha tia choroko,tui la nazi, maji nusu kikombe,pilipili na chumvi, kisha koroga vizuri na uache ichemke. Pika mpaka tui la nazi litakapoiva na rojo ibakie kidogo sana, kisha ipua na mboga yako itakuwa tayari kwa kuliwa. Mi huwa napenda kuila na wali ila hata na ugali au chapati inaenda pia.

Mapishi ya Kachori

Mahitaji

Viazi mbatata (potato 4 vya wastani)
Nyama ya kusaga (mince beef 1 kikombe cha chai)
Kitunguu (onion 1 cha wastani)
Carrot 1
Hoho (green pepper 1/2)
Kitunguu swaum (garlic)
Tangawizi (ginger )
Binzari nyembamba (ground cumin 1/2 kijiko cha chai)
Binzari manjano (turmeric 1/2 kijiko cha chai)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Limao (lemon 1/2)
Pilipili ya unga (chilli powder 1/2 kijiko cha chai)
Giligilani (coriander kiasi)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Unga wa ngano kiasi

Matayarisho

Katakata vitunguu na hoho katika vipande vidogo vidogo na kisha kwangua carrot na uweke pembeni. Chemsha viazi na chumvi kidogo vikiiva viponde na uviweke pembeni, Baada ya hapo tia nyama limao, chumvi, kitunguu swaum na tangawizi ichemshe mpaka iive na uhakikishe maji yote yamekauka. Kisha Tia binzari zote, pilipili, curry powder, giligilani, vitunguu, hoho na carrot. Pika mchanganyiko huo kwa muda wa dakika 3 na kisha ipua. Baada ya hapo changanya na viazi kisha tengeneza maduara ya kiasi na uyaweke pembeni. Chukua unga wa ngano kiasi na uchanganye na maji kupata uji usiokuwa mzito au mwepesi sana. baada ya hapo chovya madonge katika huo uji na uyachome katika mafuta. Hakikisha zinaiva na kuwa rangi ya brown na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.Unaweza ukazisevu na chatney yoyote unayopendelea.

Mapishi ya Mandazi ya nazi

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) vikombe 2 na1/2
Sukari (sugar) 1/2 kikombe
Hamira (yeast) 1/2 kijiko cha chai
Hiliki (cardamon powder) 1/4 kijiko cha chai
Tui la nazi (coconut milk) kiasi
Baking powder 1/4 kijiko cha chai
Siagi (butter)1 kijiko cha chakula
Mafuta ya kukaagia

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote kasoro tui la nazi na mafuta ya kukaangia. Ukisha changanyika vizuri tia tui la nazi na uanze kuukanda mpaka uwe mlaini. Baada ya hapo usukume na ukate mandazi katika shape uipendayo, Kisha uyawe katika sehemu yenye joto (warm place) ili yapate kuumuka.
Yakisha uumuka yakaange katika mafuta mpaka yaive kisha ipua na uyaache yapoe tayari kwa kuliwa. (Mafuta ya kukaangia yasiwe yamoto sana kwani yatayababua mandazi na hivyo ndani hayataiva vizuri.

Jinsi ya kutengeneza Wali Wa Dengu Kwa Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 Vikombe

Dengu – 2 vikombe

Viazi – 3 vikubwa

Kitunguu – 2 kubwa

Nyanya – 2

Pilipili mbichi kubwa – 3

Pilipilimanga – ยฝ kijiko cha chai

Garama Masala (bizari mchanganyiko) -1 kijiko cha chai

Supu ya vidonge (stock cubes) – 2 vidonge

Chumvi – kiasi

Mafuta – ยผ kikombe

Zaafarani – 1 kijiko cha chai

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Dengu kama sio za tayari kwenye kopo, roweka na zichemshe hadi ziwive

Maandalizi ya Masala Ya Dengu:

Zaafarani โ€“ iroweke katika maji ya dafu dafu (warm) ya chini ya robo kikombe weka kando.
Osha mchele, roweka.
Menya viazi na vitunguu, katakata vitunguu, na nyanya , weka kando.
Katakata viazi vipande vidogo vidogo kwa umbo la mchemraba (cubes).
Katika sufuria tia mafuta yakipata moto, tia viazi ukaange kidogo kwa moto mdogo mdogo hadi kukaribia kuwiva, toa weka kando.
Kaanga vitunguu hadi vigeuka rangi ya hudhurungi isiyokoza (light brown) kisha tia nyanya ukaange kidogo.
Tia vidonge vya supu (stock cubes) uvivuruge katika mchanganyiko, katakata pilipili mbichi kwa urefu tia, uendelee kukakaanga. Tia bizari, chumvi.
Zima moto, changanya dengu na viazi katika mchanganyiko huo.

Mapishi ya Wali:

Chemsha mchele kama kawaida ya kupika wali mweupe, kiini kiwe kimewiva nusu yake.
Chuja maji kisha changanya katika mchanganyiko wa dengu.
Nyunyizia zaafarani, uchanganye wali na mchanganyiko kidogo tu.
Funika acha uive katika mtoto mdogo mdogo au tia katika oveni hadi uive kama kawaida ya kupika wali.
Pakua katiha sahani na tolea na samaki yoyote wa kukaanga.

Madhara ya soda

Soda ni kiburudisho ambacho si muhimu sana kwa afya.

Aina nyingi za soda zina kafeini ambayo huzuia usharabu (ufyonzwaji) wa madini ya chuma mwilini hasa yatokanayo na vyakula vya mimea Hata hivyo soda zinaweza kutumika kwa kiasi kidogo kama kiburudisho, ila tunapotaka ubora zaidi wa afya zetu inafaa kupunguza matumizi ya soda na badala yake kutumia vinywaji vyenye virutubishi muhimu kama vile maji ya matunda, maziwa, madafu au asusa kama vile matunda, karanga na aina mbalimbali za mboga mfano karoti.

Hii inasaidia pia kutumia fedha kidogo tuliyo nayo kwa vyakula muhimu, hasa ukizingatia badala ya soda moja unaweza kupata mayai matatu au nusu lita hadi lita moja ya maziwa.

Mapishi ya Biriani

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Nyama (beef 1/2 kilo)
Vitunguu (onion 2)
Kitunguu swaum (garlic 1 kijiko cha chai)
Tangawizi (ginger 1 kijiko cha chai)
Maziwa mgando (yogurt 1 kikombe cha chai)
Hiliki nzima (cardamon 6)
Amdalasini nzima (cinamon stick 2)
Karafuu nzima (cloves 6)
Pilipili mtama nzima (black pepper 8)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Binzari manjano (turmaric 1/2 kijiko cha chai)
Binzari nyembamba nzima (cumin 1/4 kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Kaanga vitunguu mpaka viwe vya brown kisha tia nyama na uikaange kwa muda wa dakika 10. baada ya hapo tia tangawizi, kitunguu swaum, hiliki(4), amdalasini (1), karafuu (4), pilipili mtama (5), Curry powder, binzari manjano, binzari nyembamba na chumvi. Kisha koroga. Baada ya hapo tia yogurt na uipike mpaka ikauke kisha tia maji kidogo, funika na upunguze moto na uache ichemke kwa muda wa nusu saa.Baada ya hapo nyama itakuwa imeiva na mchuzi kubakia kidogo.Kwahiyo itatakiwa kuiipua.
Loweka mchele kwa dakika 10. kisha chemsha maji mengi kidogo katika sufuria kubwa. baada ya hapo tia hiliki (2) amdalamsini (1) karafuu(2) pilipili mtama (3) chumvi na mafuta kiasi. acha ichemke kidogo kisha tia mchele.Hakikisha maji yameufunika mchele kabisa na uuache uchemke kwa muda wa dakika 8 tu (kwani hautakiwi kuiva kabisa) kisha uipue na uchuje maji yote katika chujio. baada ya hapo chukua sufuria ya kuokea (baking pot kama unayoiona kweye picha) Kisha weka wali nusu na uusambaze sawia kisha weka mchuzi nyama na mchuzi wake pia utandaze na umalizie kwa kuweka leya ya wali uliobakia. Baada ya hapo ufunike na uweke kwenye oven kwenye moto wa 200ยฐC kwa muda wa nusu saa.na baada ya hapo biriani litakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kuandaa Vileja Vya Karanga

MAHITAJI

Mayai 5

Sukari 450gm (1ย lb)

Unga wa Ngano 1ย kg

Siagi 450gm (1ย lb)

Baking powder ยฝ Kijiko cha chai

Unga wa Custard Vijiko 2 vya chakula

Karanga za kusaga 250gm

Jam ยฝ kikombe

MAANDALIZI

Chukua bakuli la kiasi, weka sukari na siagi.
Changanya sukari na siagi kwa kutumia mashine ya kukorogea keki (cakemixer), mpaka sukari ichanganyike na siagi.
Vunja yai moja moja na weka kiini chake kwenye mchanganyiko wa sukari na siagi, endelea kuchanganya mpaka ichanganyike vizuri. Hifadhi ute wa mayai ndani ya kibakuli.
Mimina unga wa ngano ndani ya mchanganyiko wako huku ukichanganya Changanya unga wa custard na baking powder.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Vichovye viduara ndani ya ute wa yai kisha zimwagie unga wa karanga na kuzipanga kwenye tray ya kuchomea.
Weka dole gumba kati kati ya kila kiduara na uweke jam.
Washa jiko (oven) 350F na uchome vileja vyako kwa dakika 20.
Toa vileja vyako vipoe na uviweke ndani ya sahani tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Cookies Za Jam Ya Peach Na Raspberry

MAHITAJI

Unga kikombe 1 ยฝ

Siagi ยฝ kikombe

Sukari ยฝ kikombe

Yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jam ya peach na raspberry

MAANDALIZI

Wash oven moto wa takriban 180 โ€“ 190 Deg F
Piga siagi na sukari katika mashine mpaka iwe laini na nyororo (creamy) kisha weka yai na vanilla.
Tia unga kidogo kidogo uchanganye kwa mwiko wa mbao (wooden spoon).
Pakaza mkononi unga uchukue vidonge ubonyeze kufanya vishimo vya kuwekea jam.
Panga katika treya uliyopakaza siagi.
Tia nusu yake jam ya peach na nusu jam ya raspberry
Bake katika oven kiasi robo saa mpaka ziwive na kugeuka rangi ya brown light.
Epua vikiwa tayari

Jinsi ya kutengeneza Fagi Ya Kumumunyuka Mdomoni

VIAMBAUPISHI

Maziwa mazito matamu (condensed milk) – 2 vibati

Sukari – 1 kikombe

Samli 1 ยฝ kikombe

Vanilla 2 kifuniko cha chupa yake

Hiliki ilosagwa – 2 vijiko vya chai

Sinia kubwa ya bati Paka samli

MAANDALIZI

Changanya maziwa, sukari na samli katika sufuria isiyogandisha chakula (non-stick) uweke katika moto.
Koroga huku ikipikika hadi ianze kugeuka rangi na kuanza kuachana. Usiache mkono kuroga isije kufanya madonge.
Tia hiliki na vanilla, endelea kuipika.
Itakapogeuka rangi vizuri mimina katika sinia na haraka uitandaze kwa mwiko huku ukiuchovya katika maji na kuendelea kuitandaza hadi ikae sawa kote.
Pitisha kisu kuikataka ili ikipoa iwe wepesi kuitoa vipande.

Kila inapozidi kupoa na kukaa ndipo fagi inakauka na kumumunyuka.

Mapishi ya Wali Wa Nazi Wa Adesi, Bamia Na Mchuzi Wa Kamba

Mahitaji

Mchele – 2 vikombe

Adesi -1 ยฝ vikombe

Nazi ya unga – 1 Kikombe

Maji (inategemea mchele) – 3

Chumvi – Kiasi

Vipimo Vya Bamia:

Bamia – ยฝ kilo

Vitunguu maji – 2 vya kiasi

Nyanya iliyosagwa – 1 kubwa

Nyanya ya kopo – 2 vijiko vya chai

Pilipili manga – ยฝ kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika:

Wali wa adesi

Osha na roweka mchele na adesi .
Chuja nazi kwa vikombe 3 vya maji tia chumvi kisha weka jikoni.
Tui la nazi likishachemka tia mchele na adesi pamoja. Punguza moto, funika wali upikike kwa moto mdogo mpaka ukauke vizuri.

Bamia

Katakata bamia vipande vya kiasi/ Katakakata vitunguu weka kando.
Katika sufuria tia mafuta na kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi.
Tia nyanya ilosagwa na nyanya ya kopo na pilipili manga na chumvi.
Kisha Tia bamia punguza moto mdogo mdogo mpaka ziwive.

Vipimo: Mchuzi Wa Kamba

Kamba – 1Lb

Vitunguu vilokatwa katwa – 2

Nyanya ilokatwa katwa – 2

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 Kijiko cha chai

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 Kijiko cha chai

Bizari ya mchuzi (curry powder) – ยฝ Kijiko cha chai

Haldi โ€“ bizari ya manajano – ยฝ kijiko cha chai

Nyanya ya kopo – ยฝ Kijiko cha chai

Ndimu – 1

Chumvi – Kiasi

Mafuta ya kukaangia – 2 Vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Kaanga vitunguu kidogo hadi vilainike,
Tia nyanya, thomu na piilipili mbichi. Endelea kukaanga, tia nyanya ya kopo, chumvi, bizari zote.
Tia tia kamba na huku unakoroga mpaka wabadilike rangi na kuwiva. Kamulia ndimu na mchuzi uko tayari.

MAANA YA MANENO YANAYOTUMIKA KATIKA MASUALA YA LISHE

1. Chakula

ni kitu chochote kinacholiwa au kunywewa na kuupatia mwili virutubishi mbalimbali Chakula huupatia mwili nguvu, kuulinda na kuukinga dhidi ya maradhi mbalimbali .Mfano wa chakula ni ugali, wali, maharagwe, ndizi, viazi, mchicha, nyama, samaki.

2. Lishe

ni mchakato unaohusisha hatua mbalimbali za jinsi mwili unavyokitumia chakula kilicholiwa, hatua hizi ni kuanzia chakula kinapoliwa, jinsi mwili unavyokisaga na kukiyeyusha, umetaboli, na hatimaye virutubishi kufyonzwa na kutumika mwilini.

3. Virutubishi

ni viini vilivyoko kwenye chakula ambavyo vinauwezesha mwili kufanya kazi zake, karibu vyakula vyote huwa na kirutubishi zaidi ya kimoja ila hutofautiana kwa kasi na ubora. Kila kirutubishi kina kazi yake mwilini na mara nyingi hutegemeana ili viweze kufanya kazi yake kwa ufanisi. Hakuna chakula kimoja chenye virutubishi vya aina zote isipokuwa maziwa ya mama kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto, ni mhimu kula vyakula vya aina mbalimbali ili kuwezesha mwili kupata virutubishi mchanganyiko vinavyohitajika.

4. Mlo kamili

ni ule ambao hutokana na chakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote ya chakula na una virutubishi vyote muhimu kwa ajili ya lishe na afya bora. Mlo huu unapoliwa kwa kiasi cha kutosha kulingana na mahitaji ya mwili angalau mara tatu kwa siku huupatia mwili virutubisho vyote muhimu.

5. Ulaji unaofaa

hutokana na kula chakula mchanganyiko na cha kutosha (mlo kamili) ili kukidhi mahitaji ya mwili. Ulaji unaofaa pia huzingatia matumizi ya kiasi kidogo cha chumvi, mafuta, sukari, ulaji wa nyama nyekundu kwa kiasi kidogo. Ni muhimu kuzingatia ulaji wa mboga mboga, matunda, na vyakula vya jamii ya kunde kwa wingi ili kudumisha uzito wa mwili unaotakiwa na kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

6. Nishati- lishe

ni nguvu inayopatikana baada ya virutubishi (kabohaidreti, mafuta) kuvunjwa vunjwa mwilini. Mwili huitumia nguvu hiyo kufanya kazi mbalimbali Kama kulima, kutembea, kupumua, kuziweka seli za mwili katika hali inayotakiwa n.k.

7. Kalori au kilo kalori

ni kipimo kinachotumika kupima nishati -lishe

8. Makapi mlo

ni sehemu ya chakula ambayo mwili hauwezi kuyeyusha lakini ni muhimu katika uyeyushwaji wa chakula. Mfano wa vyakula venye makapi mlo kwa wingi ni mboga za majani, matunda( maembe, machungwa, mapera, machenza, mafenesi, unga usiokobolewa( dona) na vyakula vya jamii ya kunde.

9. Lehemu

ni aina ya mafuta yanayopatikana hasa kwenye vyakula vya asili ya wanyama na pia hutengenezwa mwilini. Lehemu inayotokana na vyakula ikizidi mwilini huleta madhara ya kiafya. Vyakula venye lehemu kwa kiasi kikubwa ni pamoja na maini, figo, mayai, nyama iliyonona kama nundu, nyama ya nguruwe yenye mafuta, mkia wa kondoo, samli, siagi, ngozi ya kuku n.k.

10. Utapiamlo

ni hali ya kupungua au kuzidi kwa baadhi ya virutubishi mwilini ambapo husababisha lishe duni au unene uliozidi.

11. Antioxidants

ni viini ambavyo vina uwezo wa kukinga seli za mwili zisiharibiwe na chembe chembe haribifu (free radicals) ambazo huweza kusababisha saratani. Viini hivyo huungana na chembechembe hizo haribifu na kuzidhibiti ili zisisababishe madhara. Mifano ya antioxidants ni pamoja na beta-carotene, lycopene, vitamin C, E, na A.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Ufuta Na Jam

VIAMBAUPISHI

Unga vikombe 2

Sukari ya kusaga 1/4 Kikombe

Siagi 250 gms

Jam kisia

Ufuta kisia

Vanilla 1 kijiko cha chai

MAPISHI

Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai, sukari na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.
Tia baking powder, na unga na changanya kwa mkono vizuri.
Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Bonyeza kila kiduara katikati kwa kidole, kisha weka jam, halafu juu yake paka mayai na unynyuzie ufuta.
Pika katika moto wa chini 350ยบF kwa muda wa dakika 20-25.
Tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Mchemsho wa ndizi na nyama

Mahitaji

Ndizi mbichi 6
Nyama ya ng’ombe (nusu kilo)
Viazi mviringo 2
Kitunguu swaum
Tangawizi
Kitunguu maji
Nyanya 1 kubwa
Mafuta (vegetable oil)
Chumvi
Limao
Pilipili

Matayarisho

Chemsha nyama na limao, kitunguu swaum, tangawizi chumvi na maji kiasi mpaka nyama iive, Hakikisha unaiacha na supu kiasi kwa ajili ya kuwekea kwenye ndizi.Kisha katakata nyanya na vitunguu na uweke pembeni .Menya ndizi na viazi kisha zichemshe pamoja na vitunguu, nyanya, maji kidogo, mafuta na uhakikishe haziivi kabisa. Baada ya hapo tia nyama na supu yake, pilipili mzima na chumvi na uache uchemke mpaka ndizi na viazi viive.Na baada ya hapo mchemsho wako utakuwa tayari kwa kuliwa

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    ๐Ÿ  Home ๐Ÿ“– Reading ๐Ÿ–ผ๏ธ Gallery ๐Ÿ’ฌ AI Chat ๐Ÿ“˜ About