Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Maini ya ng’ombe

Mahitaji

Maini (Cow liver) 1/4 kilo
Vitunguu (chopped onion) 2
Nyanya (chopped tomato) 1
Kitunguu swaum/tangawizi (ginger /garlic paste) 1 kijiko cha chai
Mafuta ya kupikia
Chumvi
Coriander
Curry powder 1 kijiko cha chai
Limao (lemon) 1/4
Pilipili (scotch bonnet ) 1

Matayarisho

Safisha maini na ukate vipande vidogovidogo na uweke pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu kidogo(visiwe vya brown) kisha tia ginger/ garlic paste,carry powder kaanga kidogo kisha tia nyanya. Kaanga nyanya mpaka zitoe mafuta kisha tia chumvi, pilipili na vimaji kidogo. Acha vichemke kidogo kisha tia maini na uyapike mpaka yaive. Malizia kwa kukamulia limao na kutia coriander kisha ipua na hapo yatakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Ndizi mzuzu

Mahitaji

Ndizi tamu (plantain) 3-4
Tui la nazi (coconut milk) kikombe 1 cha chai
Sukari (sugar) 1/4 ya kikombe cha chai
Hiliki (Ground cardamon) 1/4 ya kijiko cha chai
Chumvi (salt) 1/4 ya kijiko cha chai

Matayarisho

Menya ndizi kisha zikwangue utomvu wote. Baada ya hapo zikate kati (kiurefu) na kisha kata tena kati katika kila ndizi vitoke vipande 4. baada ya hapo toa moyo wa katikai wa ndizi. Zioshe na kisha zikaushe maji na uziweke kwenye sufuria ya kupikia. Baada ya hapo tia tui la nazi, sukari, chumvi na hiliki. Ziinjike jikono na uziache zichemke uku ukiwa unalikoroga tui ili lisikatike. Baada ya dakika 10 tui la nazi litakuwa limepungua na kubaki kidogo na hapo ndizi zitakuwa zimeshaiva. Ziache zipoe na zitakuwa tayari kwa kuliwa. Zinaweza kuliwa kama mlo (main meal) au kitinda mlo (dissert) au mlo wa pembeni (side dish) haswa kwa futari.

Madhara ya soda

Soda ni kiburudisho ambacho si muhimu sana kwa afya.

Aina nyingi za soda zina kafeini ambayo huzuia usharabu (ufyonzwaji) wa madini ya chuma mwilini hasa yatokanayo na vyakula vya mimea Hata hivyo soda zinaweza kutumika kwa kiasi kidogo kama kiburudisho, ila tunapotaka ubora zaidi wa afya zetu inafaa kupunguza matumizi ya soda na badala yake kutumia vinywaji vyenye virutubishi muhimu kama vile maji ya matunda, maziwa, madafu au asusa kama vile matunda, karanga na aina mbalimbali za mboga mfano karoti.

Hii inasaidia pia kutumia fedha kidogo tuliyo nayo kwa vyakula muhimu, hasa ukizingatia badala ya soda moja unaweza kupata mayai matatu au nusu lita hadi lita moja ya maziwa.

Madhara ya nyama nyekundu kwa mtu mwenye VVU

Kuna nyama za aina mbili, nazo ni nyama nyeupe na nyama nyekundu.

Nyama nyeupe

Hizi ni nyama zitokanazo na samaki, kuku, ndege wa aina zote, bata, wadudu

Nyama nyekundu

Hutokana na ng’ombe, mbuzi, kondoo,nguruwe na wanyama wa porini.

Nyama ina virutubishi vingi muhimu kwa afya ya binadamu kama protini, vitamini na madini. Madini ya chuma yanayopatikana kwenye nyama ni rahisi sana kusharabiwa (kufyonzwa) mwilini na ni muhimu kwa kuongeza wekundu wa damu.
Uwezo wa miili ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kuyeyusha chakula na kusharabu (kufyonza) virutubishi hupungua. Utumiaji wa nyama nyekundu kwa wingi unaweza kuwaletea matatizo hasa katika uyeyushwaji tumboni kwani nyama nyekundu si rahisi kuyeyushwa ukilinganisha na nyama nyeupe.

Hata hivyo katika nchi yetu watu walio wengi wanatumia nyama kwa kiasi kidogo sana na mara chache. Si vyema watu hawa waache kabisa nyama nyekundu. Jambo la muhimu ni kutumia njia mbalimbali ili kuifanya nyama hii iyeyushwe kwa urahisi tumboni.

Namna ya kusaidia uyeyushwaji ni pamoja n a : –

• Kutafuna vizuri au kutumia nyama ya kusaga (kwa wanaoipata).
• Kupika nyama na viungo vinavyosaidia kulainisha kama vile papai bichi, limao, vitunguu saumu n.k.
• Kula nyama pamoja na papai

Kwa hiyo, kwa anayepata nyama nyekundu kwa wingi, kupunguza kiasi cha nyama hiyo na kuongeza kiasi cha nyama nyeupe. Na kwa yule asiyepata nyama nyeupe, apatapo nyama nyekundu asiache kutumia kwani ina umuhimu mwilini mwake.

Jinsi ya kupika Wali Wa Kichina wa mboga mboga Na Mayai

Viambaupishi

  1. Mchele (Basmati) – 3 vikombe
  2. Mbogamboga za barafu (karot, njegere, spring beans na mahindi) – 1 kikombe
  3. Kuku Kidari – 1 LB (ratili)
  4. Mayai – 2 mayai
  5. Vitunguu (vikubwa) – 2 au 3 vidogo
  6. Pili pili manga – 1 kijiko cha chai
  7. Paprika – 1 kijiko cha chai
  8. Chumvi – Kiasi
  9. Mafuta – 1/3 kikombe cha chai
  10. Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha supu
  11. Tangawizi – 1 kijiko cha chai
  12. Kidonge cha supu – 1
  13. Soy sauce – 2 vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Kuku

Kata kidari cha kuku vipande vidogo vidogo vya kiasi.

Tia mafuta kidogo katika wok (karai ya kichina)

Kisha mtie kuku, thomu, tangawizi, soy sauce, pilipilimanga, paprika chumvi.

Tia mboga za barafu, kidonge cha supu, kaanga kuku na mboga viwive yitu vyote na mchanganyiko ukauke.

Namna Ya Kutayarisha Na kupika Wali

Roweka mchele wa basmati kwa muda wa saa au zaidi.

Halafu chemsha mchele pamoja na chumvi

Wacha uchemke asilimia 70%

Chuja maji na weka kando

Katika sufuria, tia mafuta kidogo tu

Kisha tia mayai mawili ukaange haraka haraka (crumbled egg)

Changanya mchanganyiko wa kuku na mboga

Kisha tia wali changanye vizuri

Rudisha katika moto, funika upikike kidogo hadi uive

Kisha pakua katika sahani na tolea na mayai ya kuchemsha ukipenda.

Mapishi ya Half cake (Keki)

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) kikombe 1na 1/2
Sukari (sugar) 1/4 kikombe
Barking powder 1/2 kijiko cha chai
Magadi soda (bicarbonate soda) 1 kijiko cha chai
Mafuta 2 vijiko vya chai
Mafuta ya kukaangia
Maji ya uvuguvugu kiasi

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote (kasoro mafuta ya kuchomea) kisha ukande (hakikisha unakuwa mgumu) Baada ya hapo sukuma na ukate shape uipendayo (hakikisha unakata vipande vinene kiasi na sio kama mandazi) Baada ya hapo ziweke sehemu yenye joto na uache ziumuke. Zikisha umuka zikaange katika moto mdogo ili ziive mpaka ndani. Zikisha iva zitoe na uziweke katika kitchen towel ili zichuje mafuta. Ziache zipoe na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Mboga Za Majani Makavu (Aina Yoyote)

Viamba upishi

Mboga za majani makavu ¼ kg
Mafuta vijiko vikubwa 3-4
Karanga zilizosagwa kikombe ½
Maziwa au tui la nazi kikombe 1
Kitunguu 1
Nyanya 2
Chumvi (kama kuna ulazima)
Maji baridi

Hatua

• Loweka mboga za majani makavu na maji kwa dakika 10-15.
• Osha , mboga na katakata nyanya na vitunguu.
• Kangaa, pukusua na saga karanga zilainike.
• Kanga kitunguu, weka nyanya, koroga zilainike.
• Ongeza mboga zilizolowekwa na maji yake kwenye rojo, koroga na funikia mpaka maji yakaukie na ive. Punguza moto.
• Koroga karanga zilizosagwa na maji, ongeza kwenye mboga ukikoroga kwa dakika 5.
• Onja chumvi, pakua kama kitoweo.
Uwezekano
Weka nyanya kidogo.
Tumia tui la nazi au krimu badala ya maziwa.
Weka nyama au dagaa au Mayai badala ya Karanga.

Namna ya kutengeneza Visheti Vya Nazi Na Njugu (Sudani)

VIAMBAUPISHI

Unga – 3 mug za chai

Samli – ½ mug ya chai

Maziwa – 1¼ mug ya chai

Baking powder – 2 vijiko vya chai

VIAMBAUPISHI VYA MJAZO

Njugu zilizomenywa vipande vipande – 2 vikombe cha chai

Sukari – ½ kikombe cha chai

Iliki – 1 kijiko cha chai

Nazi iliyokunwa – 2 vikombe vya chai

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 vikombe vya chai

Maji – 1 kikombe cha chai

Ndimu – 1

JINSI YA KUVIANDAA

1-Changanya unga na samli kisha tia baking powder na maziwa. Ukande ulainike kisha

uwache kama dakika 5 uumuke.

2-Kwenye bakuli nyingine changanya njugu, sukari na iliki.

3-Kata madonge madogo dogo sukuma kila donge duara jembamba, kisha tia kijiko cha mchanganyiko wa njugu juu yake ifunikie juu yake na ibane pembeni.

4-Panga kwenye treya isiyoganda (non stick) kisha choma kwenye oven kwa moto wa chini

(bake) 350° C kwa dakika kama 15-20.

5-Chemsha maji na sukari katika sufuria ndogo kisha tia ndimu acha ichemke mpaka inatenate unapoigusa.

6-Kwenye sahani ya chali mimina nazi iliyokunwa.

7-Vibiskuti vikiwa tayari vya motomoto chovea kwenye shira kisha zungushia katika nazi iliyokunwa,

panga kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Pilau Ya Samaki Wa Tuna Na Mboga

Mahitaji

Mchele – 2 Mugs

Mboga mchanganyiko za barafu (Frozen veg) – Mug

Tuna (samaki/jodari) – 2 kopo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi -2 vijiko vya supu

Garam masala – 1 kijiko cha supu

Nyanya – 2

Kitungu maji – 1

Mdalasini nzima – 2 vijiti

Karafuu – 6 chembe

Pilipili mbichi – 1

Chumvi – kiasi

Viazi – 3

Maji – 2 ½ Mugs

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Maandalizi

Osha mchele na uroweke kwa muda wa dakika 20
Tia mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji mpaka kigeuke rangi ya hudhurungi (brown).
Mimina viazi, thomu na tangawizi, bizari zote na kaanga.
Tia nyanya uliyokatakata ikaange mpaka iwive.
Tia tuna endelea kukaanga kidogo tu.
Tia maji, yatakapochemka tia mchele.
Punguza moto uwe mdogo funika kwa muda wa ½ saa hadi wali ukauke na uwive. Utakuwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Pilau Ya Kuku Kwa Mchele Mpya

Mahitaji

Mchele – 1 kilo

Kuku – 1

Vitunguu – 3

Viazi/mbatata – 5

Jira/bizari ya pilau nzima – 3 vijiko vya supu

Mdalasini – 1 kijiti

Pilipili manga – 1 kijiko cha supu

Hiliki – 3 chembe

Karafuu – 5 chembe

Kitunguu saumu(thomu/galic) kilosagwa – 3 vijiko vya supu

Tangawizi mbichi ilosagwa – 3 vijiko vya supu

Mafuta ya kupikia – ½ kikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Baada ya kumsafisha kuku na kumkatakata, mchemshe kwa chumvi na ndimu, kijiko kimoja cha kitunguu thomu/somu na tangawizi yote..
Menya viazi, katakata vipande vya kiasi.
Katakata vitunguu maji kisha kaanga kwa mafuta katika sufuria ya kupikia pilau.
Tia bizari zote isipokuwa hiliki.
Saga hiliki kisha tia pamoja na kitunguu thomu/somu ukaange kidogo.
Mimina kuku na supu yake ikichemka kisha tia mchele na viazi.
Koroga kisha acha katika moto mdogomdogo wali uwive kama kawaida ya kupika pilau.

Mapishi ya Viazi vya nyama

Mahitaji

Viazi (potato) 1 kilo
Nyama ya ng’ombe 1/2 kilo
Nyanya ya kopo iliyosagwa 1/2 tin
Vitunguu maji 2
Tangawizi/ swaum 1 kijiko cha chai
Hoho 1
Curry powder 1 kijiko cha chai
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/2
Chumvi
Coriander
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Safisha na katakata nyama ktk vipande vidogovidogo kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu mpaka viwe vya brown kisha tia nyama, swaum/ tangawizi, chumvi na limao. Ichanganye vizuri kisha funika na uipike mpaka iive na maji yote yakauke yani yabaki mafuta tu. Baada ya hapo tia viazi vilivyokatwa vipande vya wastani vikaange kwa muda wa dakika 10 kisha tia pilipili na curry powder na nyanya. Funika na punguza moto.Pika mpaka nyanya iive vigeuze kisha tia vimaji kidogo vya kuivishia viazi. Viazi vikikaribia kuiva(hakikisha vinabaki na rojo kidogo) tia hoho na upike kwa muda wa dk 5 kisha malizia kwa kutia coriander. Changanya vizuri kisha ipua na viazi vyako vitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Boga La Nazi

Vipimo

Boga la kiasi – nusu yake

Tui zito la nazi 1 ½ gilasi

Sukari ½ kikombe

Hiliki ½ kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Menya boga kisha katakata vipande vya kiasi.
Weka katika sufuri tia maji kiasi ya kuchemshia na kuwiva bila ya kubakia maji mengi.
Changanya tui na sukari na hiliki kisha mimina juu ya boga wacha katika moto dakika chache tu bila ya kufunika.
Epua mimina katika chombo likiwa tayari.

Mapishi ya Kabichi

Mahitaji

Kabichi 1/2 kilo
Nyanya ya kopo 1/2
Kitunguu 1
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Kwanza kabisa bandua magada ya juu ya kabichi, kisha ioshe na uikaushe maji baaba ya hapo katakata kabichi (inapendeza zaidi kama ikikatwa nyembamba) kisha saga pamoja nyanya na kitunguu. Baada yahapo tia katika sufuria ya kupikia, ipike mpaka maji yote yatakapokauka kisha tia chumvi, curry powder na mafuta pika kwa muda kiasi kisha tia kabichi na upunguze moto. Pika mpaka kabishi itakapoiva kisha ipua na itakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuila kwa wali au ugali.

Mapishi ya Kuku wa kukaanga

Mahitaji

Miguu ya kuku (chicken legs) 10
Kitunguu swaum na tangawizi (ginger & garlic paste) 1 kijiko cha chakula
Limao (lemon) 1
Pilipili iliyosagwa (ground scotch bonnet) 1/2
Giligilani iliyokatwakatwa (chopped coriander) kiasi
Chumvi (salt) kiasi
Mafuta ya kukaangia (veg oil)

Matayarisho

Safisha kuku kisha mtie kwenye sufuria na viungo vyote (kasoro mafuta na giligilani) kisha mchemshe mpaka aive na umkaushe supu yote. Baada ya hapo mkaange katika mafuta mpaka awe wa brown kisha mtoe na uweke katika kitchen towel ili kuchuja mafuta. Baada ya hapo weka katika sahani na umwagie giligilani kwa juu. Na hapo kuku wako atakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Muhogo Wa Nazi Na Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Muhogo – 3

Tui La Nazi – 2 vikombe

Chumvi – kiasi

Pilipili mbichi – 2

Mafuta – 1 kijiko moja

Kitunguu maji – 1 kidogo

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chambua muhogo ukatekate au tumia iliyo tayari.
Chemsha muhogo katika sufuria kwa maji kidogo na chumvi, funika uive muhogo.
Karibu na kukauka maji tia tui, kitunguu maji ulichokatakata na pilipili mbichi.
Unaupika moto mdogo mdogo hadi ukauke tayari kuliwa na samaki au kitoweo chochote kingine

Mapishi ya Wali maharage,mchuzi wa samaki na spinach

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Maharage yaliyochemshwa (boiled red kidney beans 1 kikombe cha chai)
Samaki waliokaangwa ( 2 fried fish)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2 ya tin)
Vitunguu vilivyokatwa (onion 2)
Kitunguu swaum (garlic 3 cloves)
Tangawizi (ginger kiasi)
Limao (lemon 1/2)
Chumvi (salt)
Pilipili (scotch bonnet pepper 2)
Mafuta (vegetable oil)
Spinach
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)

Matayarisho

Saga nyanya, kitunguu, tangawizi na kitunguu swaum pamoja. Tia kwenye sufuria na upike mpaka maji yakauke kisha tia curry powder, mafuta na chumvi na upike tena mpaka mchanganyiko uive kisha tia samaki na limao na maji kiasi na uache uchemke kiasi. Na hapo mchizi utakuwa tayari.
Osha na uzikate spinach kisha kaanga kitunguu na mafuta kiasi (hakikisha visiwe vya brown kisha tia spinach na chumvi. zipike kwa muda wa dakika 3-4 na hapo zitakuwa tayari zimeshaiva.
Wali: Chemsha maji kiasi kisha tia, chumvi, pilipili nzima(isikatwe) mafuta na tui la nazi. Baada ya hapo koroga na utie mchele na maharage na ufunike uache uchemke mpaka maji yakauke. Kisha geuza na ufunike tena na uuache mpaka uive. Baada ya hapo chakula chako kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Jinsi ya kupika Mitai

VIAMBAUPISHI

Unga wa ngano 1 1/2 Kikombe

Baking powder 1 Kijiko cha chai

Baking soda ¼ Kijiko cha chai

Chumvi ½ kijiko cha chai

Sukari 1 kijiko cha supu

Hamira 1/2 Kijiko cha supu

Yai 1

Maziwa ½ Kikombe

Mafuta ya kukaangia

VIAMBAUPISHI:SHIRA

Sukari 1 Kikombe

Maji ½ Kikombe

Iliki au Mdalasini ¼ kijiko cha chai (ya unga)

MAANDALIZI NA JINSI YA KUPIKA

1. Kwenye bakuli, changanya pamoja unga, baking powder, baking soda, chumvi, sukari na hamira.

2. Katika kibakuli, piga mayai na maziwa pamoja.

3. Changanya mchanganyiko wa mayai na wa unga ; na ukande kama unga wa maandazi.

4. Ikisha fura, sukuma unga kama wa maandazi na ukate mitai .

5. Pasha moto mafuta na uchome hadi iwe rangi ya dhahabu, upande zote mbili.

6. Ipikie shira lakini isiwe nzito .

7. Tia mitai na upepete hadi sukari ienee kote na zitakuwa tayari kuliwa.

JINSI YA KUANDAA VILEJA

MAHITAJI

Unga wa mchele – 500g

Samli – 250g

Sukari – 250g

Hiliki iliyosagwa – 1/2 kijiko cha chai

Arki (rose flavour) – 1/2 kijiko cha chai

Baking powder – 1 kijiko cha chai

Mayai – 4

Maji ya baridi – 1/2 kikombe cha chai

MAANDALIZI

Saga sukari iwe laini kiasi, changanya unga wa mchele, baking powder, hiliki na sukari.
Pasha moto samli mpaka iwe nyepesi kama maji mimina kwenye ule mchanganyiko wa unga wa mchele, kisha uchanganye pamoja na arki.
Ongeza mayai yaliopigwa endelea kuchanganya mpaka unga umeanza kuchanganyika vizuri.
Ongeza maji ya baridi sana kama nusu kikombe tu ili uchanganyike vizuri.
Kata kwa design unayotaka viwe vinene visiwe kama cookies za kawaida kama ilivyo kwenye picha na ukipenda utaweka kidoto kwa kutumia zaafarani katikati ya kileja kama inavyoonesha hapo juu.
Choma kwa moto wa baina ya 300F na 350F kwa dakika 15 mpaka 20 visiwe vyekundu toa na tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About