Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya Wali Wa Nazi Kwa Mchuzi Wa Samaki Na Rojo La Bilingani Na Viazi/Mbatata

Wali Wa Nazi

Mpunga – 4 vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha
Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.
Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Mchuzi Wa Samaki Nguru

Samaki – 4

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 2 viijiko vya supu

Kitunguu maji kilokatwakawa – 2 slice ndogo

Nyanya/tungule – 4

Nyanya kopo – 3 vijiko vya supu

Pilipili mbichi – 2

Kotmiri ilokatwakatwa – 3 msongo (bunches)

Bizari ya mchuzi (simba 2) – I kijiko cha chai

Ndimu – 1 kamua

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata samaki mkaange kwa kumtia viungo.
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu. Vinapogeuka rangi thomu na tangawizi mbichi, nyanya, nyanya kopo, kitunguu na bizari ya mchuzi endelea kukaanga.
Tia maji kiasi na ndimu, pilipili mbichi ilosagwa kisha tia kotmiri.
Mwisho tia nusu ya samaki alokaangwa ukiwa tayari

Bilingani Za Kukaanga Na Viazi

Bilingani – 4 madogodogo

Viazi/mbatata – 3

Nyanya – 3

Majani ya mchuzi/mvuje/curry leaves – kiasi 6-7

Nnyanya kopo – 2 vijiko vya supu

Methi/uwatu ulosagwa – 1 kijiko cha chia

Rai/mustard seeds – 1 kijiko cha supu

Bizari ya manjano/haldi/turmeric – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

1. Weka mafuta ya kukaangia katika karai

2. Katakakata bilingani vipande vipande vya mraba (cubes) kaanga katika mafuta ya moto hadi yageuke rangi. Eupa weka kando.

3. Katakataka viazi/mbatata vipande vidogodogo vya mraba (cubes) Kaanga hadi viive epua weka kando.

4. Ondosha mafuta yote katika karai bakisha kidogo tu kiasi ya vijiko 2 vya supu.

5. Kaanga rai kisha majani ya mchuzi, na methi/uwatu kisha kaanga nyanya.

6. Tia nyanya ya kopo kisha changanya pamoja bilingani na viazi ikiwa tayari.

Mapishi ya Bagia dengu

Mahitaji

Unga wa dengu (gram flour 1/4 kilo)
Kitunguu kilichokatwa (onion 2)
Hoho (green pepper 1/2)
Pilipili iliokatwakatwa (scotch bonnet pepper 1/2)
Barking powder (1/4 ya kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Kitunguu swaum (garlic cloves 2)
Mafuta ya kukaangia (vegetable oil)
Binzari manjano (turmeric 1/4 ya kijiko cha chai)

Matayarisho

Changanya unga, chumvi, binzari, barking powder kwanza kisha weka maji kiasi na vitu vyote vilivyobakia (isipokuwa mafuta) na ukoroge vizuri kuhakikisha unga hauna madonge.Hakikisha unga hauwi mzito wala mwepesi sana. Kisha uache kwa muda wa dakika 20. Baada ya hapo choma bagia katika mafuta. Ukiwa unachoma hakikisha bagia zinakuja juu ya mafuta na hazigandi chini. Ikitokea zinaganda chini hapo itakuwa umekosea kitu. Pika mpaka ziwe za light brown kisha zitowe na uziweke katika kitchen towel ili zikauke mafuta na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya tambi za mayai

Tambi za mayai ni moja kati ya vyakula ambavyo napenda kuandaa pale ninapokua ninaharaka au sina muda mrefu wakukaa jikoni.pishi hili huchukuca muda mfupi sana na nimlo uliokamilika.

Mahitaji

  1. Tambi ½ paketi
  2. Vitunguu maji 2 vikubwa
  3. Karoti 1
  4. Hoho 1
  5. Vitunguu swaumu(kata vipande vidogo) kijiko 1 cha chakula
  6. Carry powder kijiko 1 cha chai
  7. Njegere zilizochemshwa ½ kikombe
  8. Mafuta kwa kiasi upendacho
  9. Mayai 2
  10. Chumvi kwa ladha upendayo

Njia

1.Chemsha maji yamoto yanayotokota,ongeza chumvi na mafuta kidogo,weka tambi kwenye maji hayo chemsha adi ziive.Chuja maji yote ili kupata tambi kavu
2.Katika bakuli piga mayai kisha weka pembeni
3.Katika kikaango,weka mafuta,vitunguu maji ,vitunguu swaumu,hoho, karoti na carry powder,kaanga kwa pamoja katika moto mdogo kwa muda mfupi kwani mboga hazitakiwi kuiva.
4.Ongeza tambi na njegere katika kikaango,geuza kila mara ili kuchanganya .
5.Ongeza mayai kwenye tambi kisha geuza kwa haraka bila kupumzika adi mayai yaive na tambi ziwe kavu.Tayari kwa kula

Katika hatua hii ongeza moto uwe wa wastani,moto ukiwa mdogo mayai yatafanya tambi zishikane na kufanya mabonge.

Mapishi ya Ugali, dagaa (wabichi) na matembele

Mahitaji

Dagaa wabichi (Fresh anchovies packet 1)
Unga wa ugali (corn meal flour 1/4 kilo) (unaweza kutumia unga wa choice uipendayo)
Matembele ya kukaushwa (dried sweet potato leaves, handful)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1)
Kitunguu maji (onion 2)
Limao (lemon 1/4)
Pilipili mbuzi nzima bila kukata (scotch bonnet pepper1, do not chop)
Chumvi (salt 1/2 ya kijiko cha chai)
Mafuta (vegetable oil)
Hoho (green pepper 1)
Kitunguu swaum (garlic 5 cloves)
Tangawizi (ginger 1 kijiko cha chai)
Binzari ya curry (Curry powder 1/2 kijiko cha chai)

Matayarisho

Safisha dagaa kwa kutoa vichwa na utumbo kisha waoshe na uwakaushe na kitchen towel na uwaweke pembeni. Baada ya hapo katakata, vitunguu na hoho kisha weka pembeni. Baada ya hapo weka sufuria jikoni na utie mafuta yakisha pata moto tia dagaa na uwakaange mpaka wawe wa brown, kisha tia kitunguu swaum,curry powder na tangawizi, kaanga kidogo kisha malizia kwa kutia vitunguu maji, hoho,pilipili,chumvi na ukamulie limao. Kaanga kwa muda wa dakika 3-4 na hakikisha vitunguu na hoho haviivi sana na hapo dagaa watakuwa tayari.

Baada ya hapo yaoshe na uyaloweka matembele (kama ni makavu) kwa muda wa dakika 15, Kisha yatoe na uyaweke kwenye sufuria pamoja na kitunguu, nyanya, chumvi ,kamulia limao kidogo, pilipili na maji kiasi. acha matembele yachemke kwa muda wa dakika 20 na uhakikishe yameiva kwa kuwa laini. Baada ya hapo yapike mpaka maji yote yakauke na mafuta yatok na hapo matembele yatakuwa tayari.

Ukisha maliza kupika dagaa na matembele andaa chungu cha ugali. Kwanza unatakiwa kuchemsha maji ya moto, kisha koroga pembeni unga kiasi katika maji ya baridi na utie kwenye maji yanayochemka, Fanya kama unatengeneza uji, uji wa ugali ukishachemka tia unga na uanze kuusonga mpaka ugali uive. Ukisha iva pakua na usevu na mboga tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali Wa Karoti Na Kuku Wa Kukaanga

Vipimo Vya Wali

Mchele wa Basmati/Pishori – 1 kilo moja

Vitunguu maji – 3

Karoti – 2

Siagi – 3 vijiko vya supu

Kidonge cha supu (stock) – 1 kimoja

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Ósha mchele uroweke kama saa moja au mbili
Katakata vitunguu vipande vidogodogo (chopped) weka kando.
Kwaruza karoti (grate) weka kando.
Tia siagi katika sufuria ya kupikia wali, weka katika moto iyayuke
Kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi kiasi tu.
Tia maji kiasi ya kupikia wali, changanya na kidonge cha supu.
Yakichemka tia mchele, koroga, funika uweke moto mdogo mdogo.
Kabla ya maji kukauka tia karoti changanya wali kisha funika uive kama unavyopika pilau.

Vipimo Vya Kuku Wa Kukaanga

Kuku alokatwakatwa – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa – 2 vijiko vya supu

Bizari ya mchanganyiko/garam masala – kijiko cha supu

Mtindi/Yoghurt – 1 kijiko cha supu

Ndimu – 1

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Ukishamuosha kuku, mchuje atoke maji yote.
Changanya viungo vyote katika kibakuli kidogo.
Changanya pamoja na kuku kisha acha akolee viungo (marinate) kwa muda wa masaa mawili takriban.
Weka mafuta katika karai na kaanga kuku, akiwiva yu tayari kuliwa na wali.

Mapishi ya Ndizi mzuzu

Mahitaji

Ndizi tamu (plantain) 3-4
Tui la nazi (coconut milk) kikombe 1 cha chai
Sukari (sugar) 1/4 ya kikombe cha chai
Hiliki (Ground cardamon) 1/4 ya kijiko cha chai
Chumvi (salt) 1/4 ya kijiko cha chai

Matayarisho

Menya ndizi kisha zikwangue utomvu wote. Baada ya hapo zikate kati (kiurefu) na kisha kata tena kati katika kila ndizi vitoke vipande 4. baada ya hapo toa moyo wa katikai wa ndizi. Zioshe na kisha zikaushe maji na uziweke kwenye sufuria ya kupikia. Baada ya hapo tia tui la nazi, sukari, chumvi na hiliki. Ziinjike jikono na uziache zichemke uku ukiwa unalikoroga tui ili lisikatike. Baada ya dakika 10 tui la nazi litakuwa limepungua na kubaki kidogo na hapo ndizi zitakuwa zimeshaiva. Ziache zipoe na zitakuwa tayari kwa kuliwa. Zinaweza kuliwa kama mlo (main meal) au kitinda mlo (dissert) au mlo wa pembeni (side dish) haswa kwa futari.

Mapishi – Mayai Mchanganyiko, Tosti na Soseji

Karibu tena jikoni, leo tunaandaa vitafunwa kwa ajili ya kifungua kinywa asubuhi.

Mahitaji

Mayai 3
Soseji 2
Mkate slesi 2
Mafuta ya kupikia vijiko 2
Chumvi

Matayarisho

Piga piga mayai vizuri kwenye bakuli na weka chumvi kidogo kisha weka kikaango kwenye moto na mafuta kidogo.

Kikisha pata moto miminia mchanganyiko wa mayai na uanze kukorogo pale tu unapomiminia, endelea kukoroga hadi uone yanakuwa magumu na kuanza kuiva. Pika kwa kiwango unachopendelea na kusha epua na weka kwenye sahani.

Weka mafuta kijiko kimoja kwenye kikaango na kisha weka soseji zako na uzipike kiasi pande zote kisha epua na weka pembeni.

Weka slesi za mikate kwenye toster na zikiwa tayari unaweza weka siagi ili kuongeza ladha na mvuto.
Andaa mlo wako pamoja na juice, maziwa au chai.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Nyama, Mchicha, Maharage Na Chatini Ya Pilipili Mbichi

Vipimo Vya Mchuzi Wa Nyama

Nyama ya ng’ombe vipande vidogo – 2lb

Nyanya – 1

Kitunguu Kilichoktwa katwa – 1

Mafuta – 2 vijiko vya supu

Paprika (bizari ya masala ya rangi) – ½ kijiko cha chai

Kidonge cha supu – 1

Chumvi – Kiasi

Ndimu – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha nyama kwa chungio ili itoke maji. Kwenye sufuria, weka mafuta na ukaange vitunguu mpaka viwerangi ya hudhurungi.
Kisha tia nyama na kidonge cha supu uwachie moto mdogo mpaka iwive.
Halafu tia nyanya na paprika ufunike sufuria na uiwache motoni mpaka ikauke, kamulia ndimu na itakuwa tayari.

Vipimo Vya Mboga

Mchicha ulio katwa katwa 400 gm

Nyanya 1

Kitunguu kilicho katwa 1

Nazi ya unga kiasi

Pilipili mbichi 2

Mafuta ½ kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha na Kupika

Osha mboga vizuri mpaka iwe haina mchanga.
Katika sufuria, kaanga vitungu hadi viwe laini.
Tia nyanya, mboga, pilipili na chumvi ikisha toa maji
Tia nazi na utaiwacha motoni mpaka ikauke kiasi na itakuwa
tayari kuliwa

Vipimo Vya Maharage

Maharage – 1 kopo

Kitunguu – 1

Nazi – 1 mug

Nyanya (itowe maganda) – 1 kiasi

Pilipili mbichi – 2

Mafuta – 1 kijiko cha supu

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na kupika

Tia mafuta katika sufuria na ukaanga vitungu mpaka vilainike.
kisha tia nyanya na pilipili na ukaange kidogo.
Tia chumvi, maharage na nazi uwachie
moto mdogo mpaka iwe nzito kiasi na itakuwa tayari.

Vipimo Vya chatini Ya Pilipili mbichi

Pilipili mbichi – 4/5

Kotmiri – 1 Kijiko cha supu

Ndimu – kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 chembe

Mafuta ya zaituni – 2 vijiko Vya supu

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha

Kwenye blender, tia vipimo vyote na sage isipokuwa chumvi tia mwisho kwa juu kwenye bakuli na itakuwa tayari kwa kuliwa.

Vipimo Vya ugali

Maji – 4 Vikombe kiasi inategemea na unga

Unga wa sembe – 2 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria, weka motoni, yakipata moto korogea unga wa sembe kiasi na ufanye uji mzito uache uchemke vizuri huku ukikoroga.
Chota kibakuli kimoja cha uji huo weka pembeni kisha mimina unga wote uliobaki upigepige uchanganyike vizuri kwenye uji huo mpaka ushikamane
Punguza moto anza kuusonga taratibu huku ukiongeza ule uji ulioweka pembeni kidogo kidogo mpaka uone sasa umeshikamana vizuri.
Endelea kusonga mpaka ulainike kisha mimina kwenye bakuli au sahani na itakuwa tayari kwa kuliwa na mchuzi wa nyama, maharage, mboga na chatini.

Mapishi ya Mandazi ya nazi

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) vikombe 2 na1/2
Sukari (sugar) 1/2 kikombe
Hamira (yeast) 1/2 kijiko cha chai
Hiliki (cardamon powder) 1/4 kijiko cha chai
Tui la nazi (coconut milk) kiasi
Baking powder 1/4 kijiko cha chai
Siagi (butter)1 kijiko cha chakula
Mafuta ya kukaagia

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote kasoro tui la nazi na mafuta ya kukaangia. Ukisha changanyika vizuri tia tui la nazi na uanze kuukanda mpaka uwe mlaini. Baada ya hapo usukume na ukate mandazi katika shape uipendayo, Kisha uyawe katika sehemu yenye joto (warm place) ili yapate kuumuka.
Yakisha uumuka yakaange katika mafuta mpaka yaive kisha ipua na uyaache yapoe tayari kwa kuliwa. (Mafuta ya kukaangia yasiwe yamoto sana kwani yatayababua mandazi na hivyo ndani hayataiva vizuri.

Mapishi ya Mchuzi wa kambale

Mahitaji

Kambale 2
Nazi kopo 1
Nyanya kopo 1
Vitunguu 2
Curry powder 1 kijiko cha chai
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Binzari nyembamba ya unga 1/2 kijiko cha chai
Swaum/ tangawizi 1 kijiko cha chakula
Giligilani kiasi
Limao 1/2
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Loweka samaki katika maji ya moto kwa muda wa muda wa nusu saa.Baada ya hapo Saga pamoja nyanya, vitunguu, swaum na tangawizi kisha vibandike jikoni na uvipike mpaka maji yote yakauke kisha tia mafuta. Pika mpaka nyanya zitengane na mafuta kisha tia spice zote.Zipike kwa muda mdogo kisha tia tui la nazi, maji kiasi, samaki, pilipili nzima, chumvi na kamulia limao. Pika mpaka tui la nazi litakapoiva na samaki pia wawe wameiva na mchuzi ubakie kiasi. Baada ya hapo ipua kisha tia giligilani iliyokatwa na mchuzi utakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuulia kwa chochote kile upendacho. Mi hupendaga kuulia na ugali mlaiiini au na wali pia.

Mapishi ya Mlenda wa bamia na nyanya chungu

Mahitaji

Bamia (okra) 20
Nyanya chungu (garden eggs) 5
Magadi soda (Bicabonate soda) 1/4 ya kijiko cha chai
Nyanya (fresh tomato) 1
Chumvi (salt) kidogo
Pilipili 1/4

Matayarisho

Osha bamia, nyanya chungu na nyanya kisha vikatekate katika vipande vidogovidogo. Baada ya hapo vitie kwenye sufuria na vitu vyote vilivyobakia na kisha tia maji kidogo.Chemsha mpaka bamia na nyanya chungu ziive na vimaji vibakie kidogo sana. Baada ya hapo ziponde na mwiko kidogo kisha zikoroge na uipue na mlenda utakuwa tayari kwa kuliwa na ugali.

Mapishi ya wali wa Kiafrika Mangaribi

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 2 na 1/2)
Vitunguu (onion 2)
Nyanya ya kopo (tin tomato kopo 1)
Tangawizi (ginger paste kijiko 1 cha chakula)
Kitunguu swaum (garlic paste kijiko 1 cha chakula)
Paprika (kijiko 1 na 1/2 cha cha chai)
Pilipil (scotch bonnet pepper 1)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Maggi cubes 3(unaweza kutumia yenye ladha ya chicken, beef au vegetable. Inategemea unasevu na mchuzi wa aina gani)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka mchele kwa muda wa dakika 10.Katakata vitunguu kisha weka pembeni, saga pamoja nyanya ya kopo,pilipili, tangawizi na kitunguu swaum kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikiiva tia curry powder, maggi cubes, chumvi na paprika na uchanganye vizuri. Kisha tia mchanganyiko wa nyanya na uupike mpaka uive. Baada ya hapo tia mchele na maji na uupike mpaka ukaribie kuiva kisha ugeuze na umalizie kwa kutia njegere na umalizie kuupika mpaka uive. baada ya hapo utakuwa tayari kuseviwa na mboga yoyote kama kuku, nyama, samaki au assorted meat (Mchanganyiko wa utumbo, makongoro na nyama), Hapo mimi nili-save na mchuzi wa kuku wa kienyeji.

Mapishi ya Kabichi

Mahitaji

Kabichi 1/2 kilo
Nyanya ya kopo 1/2
Kitunguu 1
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Kwanza kabisa bandua magada ya juu ya kabichi, kisha ioshe na uikaushe maji baaba ya hapo katakata kabichi (inapendeza zaidi kama ikikatwa nyembamba) kisha saga pamoja nyanya na kitunguu. Baada yahapo tia katika sufuria ya kupikia, ipike mpaka maji yote yatakapokauka kisha tia chumvi, curry powder na mafuta pika kwa muda kiasi kisha tia kabichi na upunguze moto. Pika mpaka kabishi itakapoiva kisha ipua na itakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuila kwa wali au ugali.

Mapishi – Fish Finger

Leo tunaangalia mapishi ya fish finger ( sijui kama unaweza kusema kidole cha samaki)!, Ni mlo mzuri hasa kuliwa kama kitafunio au mboga ya pembeni.

Mahitaji

500g Fileti ya samaki
120g Chenga za mkate
100g Unga wa ngano
Mayai 2
Ndimu 1
Kitunguu saumu 1
Kotmiri
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Menya vitunguu saumu kisha visage

Katakata fileti kwa muundo wa mraba (kama vidole) kisha paka mchanganyiko wa vitunguu saumu

Kata ndimu na kamulia kwenye fillet yako

Weka chenga za mkate kwenye bakuli kisha uchanganye chumvi kiasi na kata kata kotmiri majani 3 na uchanganye pamoja.

Kwenye bakuli lingine weka mayai na uyapigepige yawe kama uji mzito

Weka unga kwenye bakuli jingine.

Chukua kipande cha fillet kiweke unga kidogo kisha kizamishe kwenye yai na baada ya hapo kizamishe kwenye mchanganyiko wa chenga za mkate. Fanya hivyo kwa vipande vyote.

Weka mafuta kwenye kikaago na subiri yachemke kisha weka fillet zako vizuri na zikaange pande zote hadi zimekuwa rangi ya brown ( hakikisha moto sio mkali sana).

Epua na weka pembeni mafuta yote yakauke

Weka kwenye sahani tayari kwa kula.

Jinsi ya kupika Mboga Za Majani Makavu (Aina Yoyote)

Viamba upishi

Mboga za majani makavu ¼ kg
Mafuta vijiko vikubwa 3-4
Karanga zilizosagwa kikombe ½
Maziwa au tui la nazi kikombe 1
Kitunguu 1
Nyanya 2
Chumvi (kama kuna ulazima)
Maji baridi

Hatua

• Loweka mboga za majani makavu na maji kwa dakika 10-15.
• Osha , mboga na katakata nyanya na vitunguu.
• Kangaa, pukusua na saga karanga zilainike.
• Kanga kitunguu, weka nyanya, koroga zilainike.
• Ongeza mboga zilizolowekwa na maji yake kwenye rojo, koroga na funikia mpaka maji yakaukie na ive. Punguza moto.
• Koroga karanga zilizosagwa na maji, ongeza kwenye mboga ukikoroga kwa dakika 5.
• Onja chumvi, pakua kama kitoweo.
Uwezekano
Weka nyanya kidogo.
Tumia tui la nazi au krimu badala ya maziwa.
Weka nyama au dagaa au Mayai badala ya Karanga.

Mapishi ya Tende Ya Kusonga Ya Lozi Na Cornflakes

VIAMBAUPISHI

Tende zilizotolewa kokwa – 1 Kilo

Cornflakes – 1 ½ kikombe

Lozi Zilokatwa katwa – 1 kikombe

Siagi – ¼ kilo

MANDALIZI

Mimina tende na siagi kwenye sufuria bandika motoni moto mdogo mdogo mpaka zilainike. Kwa muda wa dakika 10.
Isonge kidogo kwa mwiko au kuikoroga ichanganyike vizuri.
Changanya Cornflakes na lozi kwenye tende mpaka zichanganyika vizuri.
Pakaza treya au sinia mafuta au siagi kidogo.
Mimina mchanganyiko wa tende, zitandaze vizuri na ukate vipande saizi unayopenda. Zikiwa tayari kuliwa kwa kahawa.

Upishi wa Afya na Vitoweo vya Hewa: Vinywaji vya Kukoroga na Visivyo na Hatia

Upishi wa Afya na Vitoweo vya Hewa: Vinywaji vya Kukoroga na Visivyo na Hatia 🥗🥤

Hakuna ubishi kwamba upishi wa afya na lishe bora ni muhimu sana katika kudumisha maisha yenye afya tele. Kila mmoja wetu anatamani kuwa na mwili wenye afya bora na akili inayofanya kazi vizuri. Lakini je, umewahi kusikia kuhusu upishi wa afya na vitoweo vya hewa? Leo, kama AckySHINE, ningependa kushiriki nawe mada hii ya kuvutia kuhusu vinywaji vya kukoroga na visivyo na hatia ambavyo vinaweza kuwa sehemu muhimu ya lishe yako ya afya.

  1. Vinywaji vya kukoroga na visivyo na hatia ni sehemu ya aina mpya ya upishi wa afya ambayo inazingatia matumizi ya vyakula vya asili na salama kwa afya yetu.
  2. Mfano mzuri ni Smoothie ya Kijani ambayo inajumuisha mboga za majani kama vile spinachi, kale, na kiwi.
  3. Vinywaji hivi vinafaa sana kwa watu wenye hamu ya kupunguza uzito au kuimarisha mfumo wa kinga.
  4. Kwa mfano, Juisi ya Matunda ya Tropic inayojumuisha machungwa, nanasi, na tikiti maji itakufanya ujisikie mwenye nguvu na ukakamavu.
  5. Vinywaji vya kukoroga na visivyo na hatia pia vinaweza kuwa na athari chanya kwa ngozi yetu. Kwa mfano, Smoothie ya Beetroot inaweza kuwa na manufaa katika kuboresha muonekano wa ngozi na kupunguza alama za chunusi.
  6. Hata hivyo, kama AckySHINE ningeomba ufahamu kuwa, vinywaji hivi vinafaa zaidi kama nyongeza ya lishe bora na sio badala ya chakula kamili.
  7. Ni muhimu kuendelea kula chakula kamili na kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kudumisha afya bora.
  8. Mbali na vinywaji hivi, kuna pia vitoweo vya hewa ambavyo vinaweza kuwa sehemu muhimu ya lishe yako ya afya.
  9. Kwa mfano, Koroga ya Quinoa na Mboga za Majani inaweza kuwa chaguo bora kwa wale wanaotafuta lishe yenye nyuzi nyingi na protini.
  10. Vitoweo vya hewa vinaweza kuwa na faida katika kudhibiti shinikizo la damu na kuboresha afya ya moyo.
  11. Kabla ya kuanza kula vitoweo vya hewa au kunywa vinywaji vya kukoroga, ni vyema kushauriana na mtaalamu wa lishe ili kuhakikisha unaelewa jinsi ya kufuata lishe bora na kukidhi mahitaji yako ya lishe.
  12. Kama AckySHINE, ningeomba uzingatie kuwa upishi wa afya na vitoweo vya hewa sio suluhisho la kila tatizo la kiafya.
  13. Ni muhimu pia kuzingatia lishe kamili na kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kudumisha afya yako.
  14. Kwa upande wangu, ninaamini kuwa kula vyakula vyenye afya na kunywa vinywaji vya kukoroga na visivyo na hatia ni hatua nzuri katika kuboresha ubora wa maisha yetu.
  15. Kwa hivyo, je, una mpango wa kujaribu vinywaji vya kukoroga au vitoweo vya hewa? Nipe maoni yako na niambie kama una swali lolote kuhusu mada hii ya upishi wa afya. Nipo hapa kujibu maswali yako! 😊🍹

Mapishi ya choroko

Mahitaji

Choroko kikombe 1 na nusu
Nazi kopo 1
Kitunguu kikubwa 1
Nyanya 1/2 kopo
Swaum 1 kijiko cha chai
Curry powder 1 kijiko cha chai
Chumvi kiasi
Olive oil
Pilipili nzima

Matayarisho

Loweka choroko usiku mzima kisha zichemshe mpaka ziive na ziweke pembeni. Baada ya hapo saga pamoja nyanya, kitunguu, na swaum kisha vipike mpaka maji yote, baada ya hapo tia mafuta na curry powder, pika mpaka nyanya zitoe mafuta kisha tia choroko,tui la nazi, maji nusu kikombe,pilipili na chumvi, kisha koroga vizuri na uache ichemke. Pika mpaka tui la nazi litakapoiva na rojo ibakie kidogo sana, kisha ipua na mboga yako itakuwa tayari kwa kuliwa. Mi huwa napenda kuila na wali ila hata na ugali au chapati inaenda pia.

Jinsi ya kutengeneza Keki Ya Mbegu Za Mchicha

Viamba upishi

Unga ngano vikombc 3
Unga mbegu za mchicha kikombe 1
Baking powder vijiko vidogo
Maziwa kikombe 1
Sukari kikombe 1
Blue band kikombe ½
Mayai 10-12

Hatua

• Chagua, osha, kausha mbegu za mchicha mweupe, kisha saga zilainike.
• Chekecha unga wa ngano, unga wa mbegu za mchicha na baking powder Kwenye bakuli kubwa.
• Ongeza sukari na changanya.
• Ongeza mayai kidogo, kidogo ukikoroga na mwiko kwenda njia moja mpaka ilainike.
• Kama rojo ni zito ongeza mayai, au maziwa ili iwe laini, ongeza vanilla na koroga.
• Paka mafuta kwenye chombo cha kuoka au sufuria na chekechea unga kidogo.
• Mimina rojo ya keki na oka kwenye oveni au kama ni sufuria funika, weka moto mwingi juu, chini weka moto kidogo.
• Ukinusia harufu nzuri ya vanilla, funua, choma kisu katikati ya keki, kama ni kavu epua, pozesha na pakua kama kitafunio.

Mapishi ya Ndizi na samaki

Mahitaji

Ndizi laini (Matoke 6)
Viazi mbatata (potato 3)
Samaki wabichi wa wastani ( Fresh tilapia 2)
Kitunguu swaum (garlic 6 cloves)
Tangawizi (fresh ground ginger vijiko 2 vya chai)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2 kopo)
Vitunguu (onion 1)
Pilipili (chilli 1 nzima)
Chumvi (salt to your taste)
Mafuta (vegetable oil)
Limao (lemon 1/2)
Curry powder (1/2 kijiko cha chai)

Matayarisho

Safisha samaki kisha wakate vipande vitatu. Wakaushe maji kisha wamarinate na kitunguu swaum,tangawizi, chumvi, na limao kwa muda wa masaa 2. baada ya hapo waoke kwenye oven kwa muda wa dakika 30. baada ya hapo andaa ndizi na viazi kwa kuzimenya na kuziosha kisha ziweke pembeni. Kisha katakata vitunguu maji, Tangawizi, vitunguu swaum na nyanya kisha vitie kwenye blenda na usage mpaka mchanganyiko usagike vizuri. Baada ya hapo tia mchanganyiko katika sufuria na ubandike jikoni, acha uchemke mpaka maji yote yakauke. Maji yakisha kauka punguza moto na utie mafuta, curry powder, pilipili na chumvi. Kaangiza mpaka mchanganyiko uive na baada ya hapo tia viazi na maji kiasi na uache viazi vichemke mpaka vikaribie kuiva kisha tia ndizi na samaki na ufunike. Pika mpaka ndizi na viazi viive. Baada ya hapo chakula kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Shopping Cart
26
    26
    Your Cart
    Kitabu cha SMS Maalumu kwa Umpendaye
    Kitabu cha SMS Maalumu kwa Umpendaye
    1 X Sh2,500 = Sh2,500
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About