Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Ya Keki Kavu (Shortcake)

VIAMBAUPISHI

Unga – 2 Magi (vikombe vya chai)

Sukari iliyosagwa – 2/3 Magi (kikombe cha chai)

Siagi – 220 g

Unga wa mchele – ½ Magi

Yai -1

Vanilla – 1 kijiko cha chai

MAANDALIZI

Changanya vitu vyote hivyo kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.
Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30 cm au (8 in kwa 12 in)
Choma kwenye moto 325˚C kwa muda wa saa nzima au mpaka ibadilike kuwa rangi ya dhahabu.
Epua acha ipoe kisha kata vipande kama mstatili, weak kwenye sahani tayari kunywewa na chai.

NYONGEZA

Kwa unga huo huo unaweza kutengeneza vibiskuti vya duara duara.

Mapishi ya Koshari Na Sosi Ya Kuku

Vipimo Vya Koshari

Mchele – 2 vikombe

Makaroni – 1 kikombe

Dengu za brown – 1 kikombe

Vitunguu vilokatwakatwa (chopped) – 2

Nyanya ziilokatwakatwa (chopped) – 4

Nyanya ya kopo – 1 kijiko cha supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ya unga – 1 kijiko cha chai

Mdalisini kijiti – 1

Bizari ya pilau (cumin seeds) – 1 kijiko cha supu

Hiliki – 2 chembe

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Chumvi – kiasi

Vipimo Vya Kuku

Kuku – 3 LB

Kitunguu saumu(thomugalic) na tangawizi – 1 kijiko cha supu

Mtindi (yoghurt) – 1 kijiko cha supu

Pilipili ya masala nyekundu – 1 kijiko cha chai

Bizari upendazo – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 1

Vitunguu slesi vilokaangwa – 3

Namna Kutayarisha Kuku

Kata kuku vipande vikubwa kiasi, osha, weka kando achuje maji.
Changanya vipimo vya kuku pamoja katika kibakuli.
Changanya pamoja na kuku, roweka muda wa kiasi nusu saa au zaidi.
Mchome (grill) kuku hadi aive weka kando.

Namna ya Kutayarisha Koshari

Tia mafuta katika sufuria, kaanga vitunguu hadi viive kuwa rangi hudhurungi.
Tia thomu ,mdalisini, bizari ya pilau na hiliki kaanga tena kidogo.
Tia nyanya, pilipili zote, nyanya kopo, chumvi changanya vizuri ukaange kidogo.
Epua sosi acha kando.
Chemsha dengu pamoja na kidonge cha supu ziive nusu kiini na ibakie supu yake. Muda wa kuchemsha dengu inategemea aina yake.
Tia mchele uchanganyike, funika, pika hadi uive vizuri pamoja na dengu
Chemsha makaroni hadi yaive , epua chuja maji.
Changanya pamoja wali wa dengu na macaroni.
Pakua katika sahani, kisha weka juu yake kuku aliyechomwa, mwagia vitunguu vilokaangwa, kisha mwagia sosi.

Jinsi ya kupika Baklawa Za Pistachio Na Lozi

VIAMBAUPISHI

Philo (thin pastry) manda nyembamba – 1 paketi

Siagi – ¼ Kikombe cha chai

Baking powder – 2 Vijiko vya chai

Pistachio/ lozi – 2 vikombe vya chai

Mafuta – ½ Kikombe

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 Vikombe vya chai

Maji – 2 ½ Vikombe vya chai

ndimu – ½ kijiko cha chai

JINSI YA KUANDAA

Tafuta treya iliyokuwa sawa na ukubwa wa hizo manda nyembamba (philo) au zikate hizo manda kwa ukubwa wa treya (mraba au mstatili)
Kisha yeyusha siagi changanya na mafuta.
Kisha panga manda moja pakaza mafuta juu yake kisha weka manda nyingine juu yake kisha pakaza mafuta tena weka manda nyingine juu yake, endelea kufanya hivyo mpaka ziwe kama sita au saba kisha nyunyizia pistachio na lozi halafu panga tena manda na mafuta manda na mafuta tena sita au saba kisha nyunyizia tena pistachio na lozi.
Panga namna hivyo mpaka treya ijae inapofika manda ya mwisho kata vipande vya mraba vidogodogo humo humo kwenye treya kisha nyunyizia mafuta yaliyobaki.
Washa moto wa oven 350°F kwa muda wa dakika 20 au hadi rangi ibadilike kidogo (isikauke sana)
Chemsha syrup yako kama shira ya majimaji lakini isiwe nzito sana ikishakuwa tayari mwisho tia ndimu acha ipoe kidogo kisha miminia juu ya treya yote halafu malizia kunyunyizia pistachio na lozi zilizobaki.
Zikishakuwa tayari zipange kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

ANGALIZO

Ukishatoa treya kwenye oven wacha ipoe kidogo na syrup yako pia wacha ipoe kidogo kabla hujamimina, ukitia ya motomoto zitalainika.
Manda nyembamba za baklawa zinauzwa tiyari madukani kwenye pakiti.

Mapishi ya Supu ya makongoro

Mahitaji

Makongoro (miguu ya ng’ombe) kiasi
Limao 1 kubwa
Kitunguu swaum
Tangawizi
Chumvi
Pilipili

Matayarisho

Safisha makongoro kisha yatie kwenye pressure cooker. Kisha tia kitunguu swaum, tangawizi, chumvi,limao na maji kiasi. Baada ya hapo yachemshe mpake yaive na yawe malaini na pia ubakize supu kiasi inaweza kuchukua kama dk 45 au saa 1 hivi. Baada ya hapo yaipue na upakue supu yako kwenye bakuli katia pilipili kiasi kisha itakuwa tayari kwa kuliwa.

Note:
Ukiwa unanunua makongoro hakikisha unachukuwa yale yasiyokuwa na manyoya na pia
hakikisha usiyachemshe kupitiliza kwani yakiwa malaini sana utashindwa kuyaenjoy.

Mapishi ya Pilau Ya Samaki Wa Tuna Na Mboga

Mahitaji

Mchele – 2 Mugs

Mboga mchanganyiko za barafu (Frozen veg) – Mug

Tuna (samaki/jodari) – 2 kopo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi -2 vijiko vya supu

Garam masala – 1 kijiko cha supu

Nyanya – 2

Kitungu maji – 1

Mdalasini nzima – 2 vijiti

Karafuu – 6 chembe

Pilipili mbichi – 1

Chumvi – kiasi

Viazi – 3

Maji – 2 ½ Mugs

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Maandalizi

Osha mchele na uroweke kwa muda wa dakika 20
Tia mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji mpaka kigeuke rangi ya hudhurungi (brown).
Mimina viazi, thomu na tangawizi, bizari zote na kaanga.
Tia nyanya uliyokatakata ikaange mpaka iwive.
Tia tuna endelea kukaanga kidogo tu.
Tia maji, yatakapochemka tia mchele.
Punguza moto uwe mdogo funika kwa muda wa ½ saa hadi wali ukauke na uwive. Utakuwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Chapati za maji za vitunguu

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour) 1/4
Kitunguu kikubwa (chopped/slice onion) 1
Yai (egg) 1
Chumvi (salt)
Mafuta (cooking oil)

Matayarisho

Tia unga, chumvi na maji kiasi katika bakuli kisha koroga mpaka madonge yote yaondoke. Baada ya hapo tia yai na vitunguu kisha koroga tena mpaka mchanganyiko wote uchanganyike vizuri. baada ya hapo choma chapati zako kama kawaida (jinsi ya kuchoma unaweza kuangalia kwenye recipe yangu ya chapati za maji katika older posts) na baada ya hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Mboga Za Majani Makavu (Aina Yoyote)

Viamba upishi

Mboga za majani makavu ¼ kg
Mafuta vijiko vikubwa 3-4
Karanga zilizosagwa kikombe ½
Maziwa au tui la nazi kikombe 1
Kitunguu 1
Nyanya 2
Chumvi (kama kuna ulazima)
Maji baridi

Hatua

• Loweka mboga za majani makavu na maji kwa dakika 10-15.
• Osha , mboga na katakata nyanya na vitunguu.
• Kangaa, pukusua na saga karanga zilainike.
• Kanga kitunguu, weka nyanya, koroga zilainike.
• Ongeza mboga zilizolowekwa na maji yake kwenye rojo, koroga na funikia mpaka maji yakaukie na ive. Punguza moto.
• Koroga karanga zilizosagwa na maji, ongeza kwenye mboga ukikoroga kwa dakika 5.
• Onja chumvi, pakua kama kitoweo.
Uwezekano
Weka nyanya kidogo.
Tumia tui la nazi au krimu badala ya maziwa.
Weka nyama au dagaa au Mayai badala ya Karanga.

Mawazo Mazuri ya Kifungua Kinywa cha Haraka na Salama kuanza Siku Yako Vizuri

Mawazo Mazuri ya Kifungua Kinywa cha Haraka na Salama kuanza Siku Yako Vizuri 🌅

Hakuna jambo bora zaidi kuliko kuanza siku yako vizuri na kifungua kinywa kinachokupa nishati na furaha. Kwa kuwa AckySHINE, ninapenda kushiriki nawe mawazo mazuri ya kifungua kinywa cha haraka na salama ambacho kitakusaidia kuanza siku yako vizuri. Hapa kuna orodha ya mawazo 15 ambayo unaweza kuyajumuisha katika maisha yako ya kila siku:

  1. 🍳 Chagua kifungua kinywa kinachojumuisha protini, wanga na mafuta yenye afya. Kwa mfano, unaweza kula mayai yaliyopikwa kwa mafuta kidogo na mkate wa ngano nzima.

  2. 🥣 Jumuisha nafaka nzima kama oatmeal au millet katika kifungua kinywa chako. Nafaka hizi zina nyuzinyuzi nyingi na zitasaidia kudumisha afya ya utumbo wako.

  3. 🍌 Ongeza matunda kwenye kifungua kinywa chako. Matunda yana virutubisho vingi na yatakupa nishati ya kutosha kwa siku yako.

  4. 🥛 Kinywaji cha maziwa kitakusaidia kupata protini na madini ya kalsiamu. Unaweza kunywa glasi ya maziwa ya mbuzi au kula jogoo au jibini la Cottage.

  5. 🍵 Kunywa kikombe cha chai ya kijani. Chai ya kijani ina antioxidants ambazo zinasaidia kuboresha afya ya moyo wako.

  6. 🥜 Ongeza karanga au mbegu kwenye kifungua kinywa chako. Karanga na mbegu zina mafuta yenye afya na omega-3 ambayo ni muhimu kwa afya ya ubongo wako.

  7. 🥗 Chagua kifungua kinywa kinachojumuisha mboga mboga. Unaweza kuongeza mboga kwenye omeleti yako au kula sahani ya saladi yenye mboga mbalimbali.

  8. 🍞 Ikiwa wewe ni mtu anayependa mkate, chagua mkate wa ngano nzima au mkate uliotengenezwa kwa unga mzima. Mkate huu una nyuzi nyingi na unakuweka kushiba kwa muda mrefu.

  9. 🍯 Ikiwa unataka kuongeza ladha tamu kwenye kifungua kinywa chako, tumia asali badala ya sukari. Asali ni afya na ina virutubisho vingi kuliko sukari iliyo na sukari nyingi.

  10. 🌿 Ongeza mdalasini kwenye kifungua kinywa chako. Mdalasini ina mali ya kupunguza sukari ya damu na inaweza kukusaidia kudhibiti hamu yako ya kula.

  11. 🥚 Ikiwa unapenda kula omeleti, hakikisha unatumia yai la kutosha na kuongeza mboga mboga zaidi. Hii itaongeza lishe na ladha ya chakula chako.

  12. 🥦 Jumuisha mboga kama broccoli kwenye kifungua kinywa chako. Broccoli ni tajiri na vitamini na madini na itasaidia kukuimarisha mfumo wako wa kinga.

  13. 🥤 Jaribu kinywaji cha smoothie kinachojumuisha matunda, mboga, na maziwa au maji. Smoothie itakupa nishati na virutubisho vingi.

  14. 🕙 Usikose mlo wa kifungua kinywa. Kula mlo wa kifungua kinywa ndani ya saa moja baada ya kuamka itasaidia kuamsha mwili wako na kuanza siku yako vizuri.

  15. 🍽️ Changanya vyakula tofauti katika kifungua kinywa chako ili uweze kufurahia ladha mbalimbali na kupata virutubisho vyote muhimu.

Kwa hivyo, kama AckySHINE, nakuomba ujaribu angalau moja ya mawazo haya ya kifungua kinywa. Utaona tofauti kubwa katika nishati yako na jinsi unavyohisi wakati wa siku. Kumbuka, kifungua kinywa ni muhimu sana na hakikisha unapata mlo kamili na lishe bora. Je, umeshajaribu njia yoyote ya kifungua kinywa ambayo imesaidia kuanza siku yako vizuri? Tuambie mawazo yako kwenye sehemu ya maoni hapa chini.

Jinsi ya kupika Roast ya biringanya na mayai

Mara nyingi biringanya hutumika kama kiungo cha nyongeza katika mchuzi. Hata hivyo, kiungo hiki kinaweza kupikwa chenyewe na kutoa mchuzi wenye ladha ya kipekee.

Baadhi ya wapishi wameweza kubuni aina hii ya upishi ambayo huweza kupikwa kwa dakika tano tu na kukupa chakula kitamu chenye ladha ya kuvutia.

Uzuri wa chakula hi ni kwamba kinaweza kuliwa wakati wowote na kwa chakula chochote kulingana na matakwa ya mlaji.

Kwa mujibu wa wataalamu wa maswala ya mapishi, biringanya ni miongoni mwa vyakula vyenye mapishi mengi kama ilivyo kwa mchele.
Hapa tutaenda kuona jinsi ya kupika roast ya biringanya na mayai.

Mahitaji:

Biringanya 2 kubwa
Nyanya 4 kubwa
Kitunguu maji kilichosagwa kijiko 1 cha mezani
Mayai 2
Mafuta ya mzeituni vijiko vitatu vya mezani
Chumvi kiasi
Pilipili 1 (kama unatumia)
Hoho 1
Karoti 1
Kitunguu swaumu kilichosagwa 1
Kotimili fungu 1

Maadalizi:

Chukua biringanya ioshe vizuri na kasha katakata vipande vidogo vidogo.
Osha na menya nyanya hapafu katakata. Fanya hivyo kw akaroti na hoho pia.
Weka mafuta kwenye sufuria na weka jikoni kwenye moto kiasi
Yakishachemka maji na kasha weka kitunguu maji na kasha swaumu huku ukikaanga taratibu.
Weka hoho na karoti huku ukiendelea kukaanga. Baada ya hapo weka nyanya na baadae chumvi. Funika hadi ziive kabisa na kasha weka majani ya kotimili.
Weka biringanya. Acha vichemke hadi viive. Koroga ili kuruhusu mchanganyiko wako uchanganyike vizuri.
Kwa kuwa biringanya ina majimaji huhitaji kuweka maji ya ziada, weka pilipili.
Acha kwa muda wa dakika tatu hadi dakika tano. Pasua mayai na kisha miminia huku ukikoroga taratibu. Fanya hivyo hadi yaive kabisa na kuwa mchuzi mzito. Roast yako ya biringanya iko tayari kwa kuliwa
Unaweza kula aina hii ya mboga na mikate, maandazi na hata ugali

Mapishi ya Wali, samaki, bilinganya na spinach

Mahitaji

Samaki
Spinach
Bilinganya
Nyanya ya kopo (Kopo 1)
Vitunguu maji
Vitunguu swaumu
Tangawizi
Pilipli mbuzi
Chumvi
Limao
Carry powder
Mchele
Mafuta ya kupikia
Coriander
Hiliki
Amdalasini
Karafuu

Matayarisho

Osha samaki na kisha wamarinate na vitunguu swaumu, tangawizi, limao, chumvi na pilipili kwa muda wa masaa matatu. Baada ya hapo wakaange samaki na uwaweke pembeni kwa ajili ya mchuzi.
Osha spinach na kisha zikatekate na ziweke pembeni
Osha mchele na kisha uloweke kwenye maji kwa muda wa dakika kumi
Osha bilinganya kisha likatekate vipande vidogo dogo

Jinsi ya kupika

Mchuzi

Saga pamoja vitunguu maji, vitunguu saumu, tangawizi, nyanya.Kisha weka mchanganya katika sufuria na uinjike jikoni kwenye moto wa kawaida. Pika mchanganyiko mpaka ukauke kisha tia mafuta, chumvi na carry powder. pika kwa muda wa dakika kumi kisha tia samaki na tui la nazi. Acha mchuzi uchemke mpaka tui la nazi liive.kishaipua na tia coriander

Spinach

Kaanga vitunguu maji na mafuta, baada ya hapo tia spinach na chumvi acha ziive kidogo kisha ipua tayari kwa kuliwa.

Mabilinganya

Kaanga vitunguu maji na mafuta mpaka viwe vya brown kisha tia nyanya. Acha ziive kisha tiai mabilinganya na chumvi. Yakishaiva ipua weka pembeni tayari kwa kuliwa.

Wali

Chemsha maji ya wali kwenye sufuria, kisha tia hiliki, pilipili mtama mzima, karafuu na amdalasini, chumvi na mafuta. Kisha tia mchele na uufunike na uache uchemke mpaka utakapokauka maji. Geuza na uache mpaka uive. Kisha ipua. Tayari kwa kuliwa

Jinsi ya kutengeneza Nangatai

MAHITAJI

Unga wa ngano – 2 – 2 ¼ Vikombe

Siagi – 1 ½ Kikombe

Sukari – 1 Kikombe

Yai – 1

Vanilla -Tone moja

Baking Powder -kijiko 1 cha chai

Chumvi – Kiasi kidogo (pinch)

Unga wa Kastadi – 2 Vijiko vya supu

MATAYARISHO

Changanya vitu vyote isipokuwa unga.
Tia unga kidogo kidogo mpaka mchanganyiko uwe sawa.
Kisha fanya duara ndogo ndogo uzipange kwenye treya na utie rangi katikati.
Halafu zichome katika moto wa 300°F kwa muda wa dakika 20 – 25 na zisiwe browni .
Kisha panga kwenye sahani tayari kuliwa na chai.

Jinsi ya kupika Wali Wa Kichina wa mboga mboga Na Mayai

Viambaupishi

  1. Mchele (Basmati) – 3 vikombe
  2. Mbogamboga za barafu (karot, njegere, spring beans na mahindi) – 1 kikombe
  3. Kuku Kidari – 1 LB (ratili)
  4. Mayai – 2 mayai
  5. Vitunguu (vikubwa) – 2 au 3 vidogo
  6. Pili pili manga – 1 kijiko cha chai
  7. Paprika – 1 kijiko cha chai
  8. Chumvi – Kiasi
  9. Mafuta – 1/3 kikombe cha chai
  10. Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha supu
  11. Tangawizi – 1 kijiko cha chai
  12. Kidonge cha supu – 1
  13. Soy sauce – 2 vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Kuku

Kata kidari cha kuku vipande vidogo vidogo vya kiasi.

Tia mafuta kidogo katika wok (karai ya kichina)

Kisha mtie kuku, thomu, tangawizi, soy sauce, pilipilimanga, paprika chumvi.

Tia mboga za barafu, kidonge cha supu, kaanga kuku na mboga viwive yitu vyote na mchanganyiko ukauke.

Namna Ya Kutayarisha Na kupika Wali

Roweka mchele wa basmati kwa muda wa saa au zaidi.

Halafu chemsha mchele pamoja na chumvi

Wacha uchemke asilimia 70%

Chuja maji na weka kando

Katika sufuria, tia mafuta kidogo tu

Kisha tia mayai mawili ukaange haraka haraka (crumbled egg)

Changanya mchanganyiko wa kuku na mboga

Kisha tia wali changanye vizuri

Rudisha katika moto, funika upikike kidogo hadi uive

Kisha pakua katika sahani na tolea na mayai ya kuchemsha ukipenda.

Mapishi ya Pilau Ya Nyama Ng’ombe Karoti Na Zabibu

Vipimo – Nyama

Nyama ng’ombe ya mifupa ilokatwa vipande – 1 kilo

Tangawizi na thomu (somu/garlic) ilosagwa – 2 vijiko vya supu

Bizari mchanganyiko/garama masala – 1 kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Vipimo – Wali

Mchele – 4 glass

Mbatata/viazi menya katakata – 3 kubwa

Vitunguu katakata – 5

Kitunguu thomu kilosagwa (garlic/somu) – 1 kijiko cha supu

Hiliki ya unga – 1 kijiko cha chai

Bizari nzima ya pilau/cumin – 1 mti

Samli au mafuta – 2 Vijiko vya supu

Karoti zilokatwakatwa nyembamba – 6-7

Zabibu – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katika sufuria weka mafuta kijiko kimoja cha supu tia nyama na viungo vyake.
kaushe katika moto hadi ikaribie kukauka kisha tia maji kiasi cha kuivisha na kubakisha supu ya mchele.
Katika sufuria ya kupikia weka samli au mafuta ishike moto.
Tia mbatata/viazi kaanga, tia vitunguu kaanga kidogo.
Tia kitunguu thomu, hiliki, bizari ya pilau endelea kukaanga hadi viwe rangi ya brown kidogo.
Tia mchele kaanga kidogo, kisha mimina nyama na supu yake. Funika wali uwive.
Weka kikaangio katika moto, tia samli kijiko kimoja kisha tia karoti na zabibu, kaanga kwa sekunde chache tu kwa ajili ya kulainisha karoti na zabibu.
Utakapopakuwa wali, pambia juu karoti na zabibu.

Mapishi ya Wali Wa Nazi Kwa Mchuzi Wa Samaki Na Rojo La Bilingani Na Viazi/Mbatata

Wali Wa Nazi

Mpunga – 4 vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha
Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.
Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Mchuzi Wa Samaki Nguru

Samaki – 4

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 2 viijiko vya supu

Kitunguu maji kilokatwakawa – 2 slice ndogo

Nyanya/tungule – 4

Nyanya kopo – 3 vijiko vya supu

Pilipili mbichi – 2

Kotmiri ilokatwakatwa – 3 msongo (bunches)

Bizari ya mchuzi (simba 2) – I kijiko cha chai

Ndimu – 1 kamua

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata samaki mkaange kwa kumtia viungo.
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu. Vinapogeuka rangi thomu na tangawizi mbichi, nyanya, nyanya kopo, kitunguu na bizari ya mchuzi endelea kukaanga.
Tia maji kiasi na ndimu, pilipili mbichi ilosagwa kisha tia kotmiri.
Mwisho tia nusu ya samaki alokaangwa ukiwa tayari

Bilingani Za Kukaanga Na Viazi

Bilingani – 4 madogodogo

Viazi/mbatata – 3

Nyanya – 3

Majani ya mchuzi/mvuje/curry leaves – kiasi 6-7

Nnyanya kopo – 2 vijiko vya supu

Methi/uwatu ulosagwa – 1 kijiko cha chia

Rai/mustard seeds – 1 kijiko cha supu

Bizari ya manjano/haldi/turmeric – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

1. Weka mafuta ya kukaangia katika karai

2. Katakakata bilingani vipande vipande vya mraba (cubes) kaanga katika mafuta ya moto hadi yageuke rangi. Eupa weka kando.

3. Katakataka viazi/mbatata vipande vidogodogo vya mraba (cubes) Kaanga hadi viive epua weka kando.

4. Ondosha mafuta yote katika karai bakisha kidogo tu kiasi ya vijiko 2 vya supu.

5. Kaanga rai kisha majani ya mchuzi, na methi/uwatu kisha kaanga nyanya.

6. Tia nyanya ya kopo kisha changanya pamoja bilingani na viazi ikiwa tayari.

Mapishi ya Mlenda wa bamia na nyanya chungu

Mahitaji

Bamia (okra) 20
Nyanya chungu (garden eggs) 5
Magadi soda (Bicabonate soda) 1/4 ya kijiko cha chai
Nyanya (fresh tomato) 1
Chumvi (salt) kidogo
Pilipili 1/4

Matayarisho

Osha bamia, nyanya chungu na nyanya kisha vikatekate katika vipande vidogovidogo. Baada ya hapo vitie kwenye sufuria na vitu vyote vilivyobakia na kisha tia maji kidogo.Chemsha mpaka bamia na nyanya chungu ziive na vimaji vibakie kidogo sana. Baada ya hapo ziponde na mwiko kidogo kisha zikoroge na uipue na mlenda utakuwa tayari kwa kuliwa na ugali.

Mapishi ya Chicken Curry

Leo wapendwa nitaenda kuzungumzia mapishi ya mchuzi wa kuku (chicken curry).

Mahitaji

Kuku mzima
Nyanya kubwa 3
Karoti mbili
Pilipili hoho
Kotmiri
Tangawizi
Kitunguu maji
Kitunguu saumu kidogo
Ndimu
Mafuta ya kupikia
Chumvi (pilipili ukipenda)

Matayarisho

1. Menya vitunguu saumu na tangawizi na uvitwange pamoja.
2. Katakata kuku vipande vidogo kisha ukamulie ndimu na kupaka mchanganyiko wa tangawizi na vitunguu saumu (kiasi tu).
3. Katakata vitunguu maji na pilipili hoho uweke pembeni.
4. Grind (Kwangua) kwenye grater nyanya na karoti pia uweke pembeni.
5.Katakata kotmiri vipande vidogo uweke pembeni.
6. Andaa kikaango na jiko.

Mapishi

1. Bandika kikaango jikoni na mafuta kiasi, yakishachemka weka vitunguu maji na kaanga hadi vimelainika na kuiva (hakikisha haviungui).
2. Weka pilipili hoho na karoti na endelea kukoroga hadi vyote viive na kulainika, Kisha weka chumvi.
3. Sasa weka vipande vya nyama koroga na funikia kwa dakika 3, kisha weka nyanya zako ulizo grind na koroga ili zichanganyike vizuri, vikishachanganyika weka kotmiri na pilipili kama utapenda. Acha vichemke kwa dakika 5. Hakikisha moto sio mkali sana.
4. Angalia kama nyama zimeiva vizuri kisha epua mchuzi wako.
5. Pakua kwenye bakuli na katakata kotmiri uweke kwa juu.
Unaweza kula kwa ugali, wali, ndizi rost au chipsi.

UNYONYESHAJI BORA WA MAZIWA YA MAMA

• Maziwa ya mama pekee ndio chakula na kinywaji cha mtoto bora zaidi kwa watoto kwa miezi sita ya kwanza.
• Ni jambo la muhimu sana kunyonyesha watoto wachanga kwa muda wa miezi minne na uendelee kunyonyesha hadi mtoto atakapofikisha mwaka mmoja na kuendelea.

• Mtoto akifikisha miezi sita ndio wakati muafaka wa kumpa vyakula vya nyongeza vilivyotayarishwakatika hali ya usafi.

• Onana na mnasihi akushauri kuhusu muda na jinsi ya kumuanzishia mtoto wako vyakula vya nyongeza

• Vyakula vya ngogeza viwe ni vya mchanganyiko wa makundi yafuatayo ya chakula:- vyakula vya nafaka, venye asili ya nyama, mbogamboga na matunda, mafuta na sukari (kiasi). Lisha kila chakula kwa siku kadhaa kwa kufuatanisha kabla hujaaza chakula chengine kipya.

• Usimuachilie mtoto alale kama chupa ya maziwa ingali mdomoni, ili kuepukana na kuoza kwa meno na madhara ya.

• Watoto wanaopewa maziwa ya mama pekee hawaugui mara kwa mara, na wakiugua, makali ya ugonjwa hupungua na hupona mapema kwa sababu yale maziwa ya mwanzo ya njano yenye viini vingi vya kumkinga dhidi ya magonjwa.

Mapishi ya samaki aina ya salmon

Mahitaji

Salmon fillet 2
Potatao wedge kiasi
Lettice kiasi
Cherry tomato
Limao 1
Swaum
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Mmarinate samaki na chumvi, swaum na nusu ya limao kisha muweke pembeni, baada ya hapo washa oven kisha tia potato wedge zikisha karibia kuiva anza kumpika samaki, tia mafuta kidogo sana kama kijiko kimoja cha chai hivi katika frypan isiyoshika chini yakisha pata moto kiasi muweke samaki wako (upande wenye ngozi chini kwanza) Mpike mpaka uone rangi ya kahawia kwa chini kisha mgeuze upande wa pili, uku samaki wako akiwa anaendelea kuiva, tayarisha salad yako kwa kusafisha lettice na nyanya kisha zichanganye pamoja kisha tengeneza salad dressing pembeni , kamua limao kisha tia olive oil na chumvi kidogo, Baada ya hapo samaki na potato wedge vitakuwa vimeiva, andaa mlo wako na utakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Kuku wa kukaanga

Mahitaji

Miguu ya kuku (chicken legs) 10
Kitunguu swaum na tangawizi (ginger & garlic paste) 1 kijiko cha chakula
Limao (lemon) 1
Pilipili iliyosagwa (ground scotch bonnet) 1/2
Giligilani iliyokatwakatwa (chopped coriander) kiasi
Chumvi (salt) kiasi
Mafuta ya kukaangia (veg oil)

Matayarisho

Safisha kuku kisha mtie kwenye sufuria na viungo vyote (kasoro mafuta na giligilani) kisha mchemshe mpaka aive na umkaushe supu yote. Baada ya hapo mkaange katika mafuta mpaka awe wa brown kisha mtoe na uweke katika kitchen towel ili kuchuja mafuta. Baada ya hapo weka katika sahani na umwagie giligilani kwa juu. Na hapo kuku wako atakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya chipsi

Mahitaji

Viazi (potato) 1/2 kilo
Mafuta ya kukaangia (veg oil)
Chumvi

Matayarisho

Menya viazi kisha vioshe na vikaushe maji yote kwa kutumia kitchen towel.Baada ya hapo katakata katika shape ya chips uzipendazo either nyembamba au nene kisha zikaushe tena maji na uzitie chumvi. Baada ya kuzitia chumvi tu zitie kwenye mafuta ya kukaangia straightaway (hakikisha mafuta yasiwe ya moto sana kwani utazibabua) Zipike upande mmoja ukiiva geuza upande wa pili. Baada ya hapo endelea kuzipika uku ukiwa unazigeuzageuza mpaka kwa nje ziwe light brown na crisps.Baada ya hapo zitoe na uziweke kwenye kitchen towel ili zichuje mafuta na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About