SALA YA MATUMAINI
Mungu wangu,
natumaini kwako nitapewa kwa njia ya Yesu Kristu,
neema zako duniani na utukufu mbinguni,
kwani ndiwe uliyeagana hayo nasi,
nawe mwamini. Amina
Mungu wangu,
natumaini kwako nitapewa kwa njia ya Yesu Kristu,
neema zako duniani na utukufu mbinguni,
kwani ndiwe uliyeagana hayo nasi,
nawe mwamini. Amina
Roho ya Kristo unitakase
Mwili wa Kristo uniokoe
Damu ya Kristo unifurahishe
Maji ya ubavu wake Kristo yanioshe
Mateso ya Kristo nguvu yanizidishie
Ee Yesu mwema unisikilize
Katika madonda yako unifiche
Usikubali nitengwe nawe
Na adui mwovu unikinge
Saa ya kufa kwangu uniite
Uniamuru kwako nije
Na watakatifu wako nikutukuze
Milele na milele.
Amina.
Ee Yosef mwenye heri, tunakimbilia kwako, katika masumbuko yetu, na kishaomba shime ya Mchumba wako Mtakatifu, tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako. Kwa ajili ya mapendo uliyompenda nayo Bikira Mtakatifu, Mzazi wa Mungu, na kwa ajili ya tunza ya Baba, uliyomtunza nayo Mtoto Yesu, tunakuomba sana, utuangalie kwa wema, sisi tuliokuwa fungu lake Yesu Kristo, tuliokombolewa kwa damu yake, utusimamie katika masumbuko yetu, kwa enzi na shime yako.
Ee Mlinzi amini wa Jamaa Takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristo, ee Baba uliyetupenda mno, utuepusha na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji,utusimamie huko juu mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwokoa Mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa, na leo hivi, ulikinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida yote, mtunze daima kila mmoja wetu, tupate mfano wako, tusaidie kwa msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupokelewa mbinguni makao ya raha milele. Amina
Kwa njia ya Maji haya ya Baraka,
na kwa njia ya Damu yako azizi,
na kwa maombezi ya Moyo Safi wa Maria,
unioshe na uovu wangu wote na uwasaidie roho zinazoteseka toharani. Amina.
Ee Mtukufu Mt. Yosefu, ulichaguliwa na Mungu kuwa Baba Mlishi wa Yesu, mchumba safi kabisa wa Maria Bikira Milele, na mkubwa wa Familia Takatifu. Umechaguliwa na Mwakilishi wa Kristu kama Msimamizi wa kimbingu na mlinzi wa Kanisa alilolianzisha Kristu. Ndiyo maana ninakuomba kwa matumaini makuu usaidizi wako wenye nguvu kwa ajili ya Kanisa zima duniani.
Mlinde kwa namna ya pekee, kwa upendo wa kikweli wa ki-baba, Baba Mtakatifu na Maaskofu wote na Mapadre wenye ushirika na Kiti cha Petro. Uwe mlinzi wao wote wanaotumikia wokovu wa wanadamu kati ya majaribu na mahangaiko ya maisha haya, na utujalie kwamba watu wote wa dunia hii wamfuate Kristu na Kanisa alilolianzisha.
Mpendwa Mtakatifu Yosefu, ukubali majitoleo ya nafsi yangu ambayo sasa ninafanya. Ninajiweka wakfu kwako kwa ajili ya utumishi wako, ili daima wewe uwe baba yangu, mlinzi wangu, na kiongozi wangu katika njia ya wokovu. Unijalie usafi mkuu wa moyo na matamanio makuu ya maisha ya kiroho. Unijalie ili matendo yangu yote, kwa mfano wako, yawe kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, pamoja na Moyo wa kimungu wa Yesu, moyo safi wa Maria, na moyo wako wa ki-baba. Uniombee, nami nishiriki kifo chako cha furaha na kitakatifu.
Amina.
Ee Bikira Maria uliyekingiwa dhambi ya asili, utuombee sisi wenye kukimbilia kwako, uwaombee na wale wasioukimbilia kwako, hasa maadui wa Kanisa Takatifu, na wale waliokabidhiwa kwako. Amina.
Ewe Mtakatifu Yuda Tadei,/ mtume mtukufu na shahidi wa Kristo,/ umesifika pote kwa wepesi wako wa kutoa misaada/ kwa wanaokukimbilia katika matatizo yao mazito./ Pia ni mwombezi wa waliopondeka moyo./
Mimi ni mmoja wa hao./ Nakujia na moyo uliojaa shida na matatizo./ Nakusihi kwa moyo wote/ unisaidie kwa maombezi yako yenye nguvu/ kufikia utatuzi unaofaa kadiri ya mapenzi ya Mungu./ Maisha yangu yamejaa misalaba,/ siku kwa siku matatizo hayapungui./ Moyo wangu umekuwa bahari ya siki chungu sana./ Mapito yangu nayaona yamejaa miiba mikali./ Roho yangu imezama katika dimbwi la machozi na kite./ Nafsi yangu imezingirwa na giza nene./ Ghasia na kukatishwa tamaa ya kuishi/ hunyemelea roho yangu./ Maongozi ya Mungu na imani naviona vinanitoka kidogo kwa kidogo./
Nikielemewa na mawazo kama hayo/ najikuta sina nguvu za kuishi,/ na maisha kwangu ni msalaba mzito/ ninaouogopa hata kuunyakua./ Wewe unaweza kabisa kunitoa katika balaa hili./ Sitaacha kukusihi/ hadi hapo utakaponisaidia/ au kunijulisha mapenzi ya Mungu kwangu./ Natangulia kutoa shukrani kwa jibu liwalo lote.
Ewe Mungu Mwenyezi, sisi kama familia tunakushukuru kwa zawadi ya Mama Kanisa Katoliki ambaye siku zote hutupatia malezi bora kwa ajili ya wokovu wetu. Kanisa halichoki kutuhimiza tutafakari na kuishi utakatifu wa familia ya Nazareti ya Yesu, Maria na Yosefu. Familia hii iliishi upendo uliojengwa kwa fadhila za imani, uaminifu, utii, uvumilivu na upole hata wakawa watakatifu. Tunapoadhimisha mwaka wa Familia, tunaiweka mbele yetu familia ya Nazareti iwe dira, baraka na mfano kwa familia zetu.
Tunakushukuru Baba kwa ajili ya familia zote zinazojitahidi kuishi fadhila hizo za Familia takatifu na tunakuomba uzidi kuwaimarisha wanandoa ili tupate kwao mifano mingi na bora ya kuigwa. Ee Bwana, tunaomba Roho Mtakatifu atuangazie tuweze: kutambua familia kuwa Kanisa la nyumbani na shule ya imani na upendo; kuimarisha familia kwa sala, sakramenti na tunu za kiinjili na kushirikiana kwa heshima katika familia kwa usitawi wa roho na wa mwili kwa wanafamilia wote.
Tunaziombea familia zetu na Jumuiya Ndogondogo za Kikristo ziwe bustani bora na salama za kuchipusha na kulea miito mitakatifu ya Ndoa, Utawa na Upadre. Tunawaombea vijana na watoto wetu Uchaji wa Mungu ili wawe na bidii ya kujitunza kwa kushika amri za Mungu na kuishi fadhila za kiinjili, wawe na roho ya kimisionari yaani walipende Kanisa na kuwa na moyo wa kueneza ufalme wako kwa matendo ya imani. Baba wa huruma, tunakukabidhi familia zenye misukosuko ya mafarakano, ulevi, ubinafsi, uregevu-dini, uvivu, ushirikina, hofu, magonjwa sugu na mengineyo yenye kuleta huzuni; kwa hisani yako uwape neema, mwanga na nguvu za kuanza maisha mapya yenye amani, waweze kufurahia upatanisho na uponyi wa pendo lako la kibaba kati yao.
Tunaomba toba na msamaha kwa ukatili, manyanyaso na hata mauaji katika familia zetu na uwaponye wote waliojeruhiwa kwa maneno, matendo na makwazo ya aina yeyote. Aidha tunakuomba uwe kitulizo na faraja kwa wagonjwa na wazee, pia tegemeo la yatima na wajane. Wenye matatizo ya kiafya au ya kijamii wasikate tamaa bali waunganishe hali zao na msalaba wa Mwanao na kukutumaini wewe Mweza yote. Jamii iwajibike nao kwa kuzijali haki zao na kuwapa misaada wanayohitaji.
Tunakuomba ubariki miradi na kazi zetu ili familia zipate usitawi na maendeleo; na utujalie hekima ya kukushukuru kwa maisha ya haki, amani na ukarimu na mwisho tukaimbe sifa zako pamoja na familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefuna jeshi lote la mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
Baba yetuโฆ โฆ..Salamu Mariaโฆ.โฆAtukuzwe Babaโฆโฆโฆ
Malaika wa Mungu Mlinzi wangu mpenzi,
Ambaye upendo wake unanifanya niwepo hapa,
Uwe nami leo hii,
Kuniangaza na kunilinda,
Kunitawala na kuniongoza.
Amina.
Kumheshimu Mungu wangu, Namtolea roho yangu, Nifanye kazi nipumzike, Amri zake tu nishike, Wazo neno tendo lote, Namtolea Mungu pote, Roho, mwili chote changu, pendo na uzima wangu, Mungu wangu nitampenda, Wala dhambi sitatenda, Jina lako nasifia, Utakalo hutimia, Kwa utii navumilia, Teso na matata pia, Nipe Bwana neema zako, Niongezee sifa yako, Amina.
Ee Yesu Kristu,/ Bwana wangu na Mungu wangu/ ambaye ninasadiki kuwa upo hapa/ katika Sakramenti Takatifu ya Altare;/ pokea kitendo hiki cha kukuangukia kifudi fudi/ kama ishara ya tamaa niliyonayo ya kukuabudu Wewe/ bila kuchoka/ na kukushukuru kwa mapendo yako makubwa/ yasiyo na kipimo/ ambayo Moyo wako Mtakatifu sana/ unawaka katika Sakramenti Takatifu hii./ Siwezi kukushukuru vizuri zaidi/ kuliko kama ningetolea kwako/ matendo yangu yote ya kukuabudu/ unyenyekevu wangu/ uvumilivu na mapendo/ ambayo huu Moyo Mwabudiwa ulifanya,/ bado unafanya/ na utaendelea kufanya katika uzima wa milele mbinguni./ Ninaahidi kupitia Moyo huu,/ nitakupenda,/ nitakutukuza,/ na nitakuabudu kama nitakavyoweza./ Ninajiunganisha na hii Sadaka Takatifu/ ambayo unatoa kwa Baba Mungu/ na ninatolea kwako utu wangu./ Ninakuomba kuangamiza ndani yangu/ dhambi zote pamoja na majeraha yake/ na usikubali kunitenga nawe milele./ Amina.
(Na Mt. Margareta Maria Alakoki)
Ee Yesu Mfungwa wa Upendo wa Mungu,/ ninapofikiri Upendo wako na jinsi ulivyojitolea kwa ajili yangu,/ nashindwa kuelewa./ Unaficha Ukuu wako usiofahamika/ na kujidhihirisha kwa ajili yangu mimi mnyonge./ Ee Mfalme wa utukufu,/ unaficha uzuri wako,/ lakini jicho la moyo wangu/ linapenya pazia na kuona Majeshi ya Malaika/ wakikuimbia kwa heshima bila kukoma/ na nguvu zote mbinguni zikikusifu bila mwisho zikisema:/ โMtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu..โ/
Ni nani awezaye kufahamu Upendo wako/ na huruma yako isiyo na kipimo kwa ajili yetu!/ Ee Mfungwa wa Upendo,/ nafungia moyo wangu masikini/ kwenye Tabarnakulo hii/ ili niweze kukuabudu usiku na mchana bila mwisho./ Najua hakuna kizuizi/ na hata kama naonekana kukaa mbali,/ lakini moyo wangu u pamoja nawe/ katika ibada hii./ Hakuna kinachoweza kuzuia upendo wangu kwako./ Kwangu hakuna kizuizi chochote./
Ee Utatu Mtakatifu,/ Mungu Mmoja usiyegawanyika,/ utukuzwe kwa zawadi yako hii kuu/ na agano hili la huruma!/
Nakuabudu,/ Bwana na Muumba uliyefichika katika Sakramenti Takatifu!/ Ee Bwana,/ nakuabudu kwa kazi zote za mikono yako/ zinazonifunulia Hekima yako kuu,/ Wema wako na Huruma yako kuu./ Uzuri uliousambaza hapa/ Uzuri ulio nao Wewe mwenyewe/ ambaye U Uzuri usioelezeka;/ na ingawaje umejificha na kusitiri uzuri wako,/ jicho langu,/ kwa mwanga wa imani linafika kwako,/ na roho yangu inapata kumtambua Muumba wake/ aliye Uzuri usiopimika,/ ulio juu ya kila uzuri,/ na moyo wangu unazama kabisa katika sala ya kukuabudu./
Bwana wangu na Muumba wangu,/ wema wako wanitia moyo wa kuongea nawe,/ Huruma yako huondoa kiambaza/ kitenganishacho Muumba na kiumbe./ Furaha ya moyo wangu,/ ee Mungu, ni kuongea na Wewe./ Yote ambayo moyo wangu unayatamni nayapata kwako./ Hapa ndipo mwanga wako unaponiangaza akili yangu/ na kuiwezesha kukujua Wewe zaidi na zaidi/ โ ndipo mikondo ya neema inapoutiririkia moyo wangu,/ ndipo roho yangu inapochota uzima wa milele./ Ee Bwana na Muumba wangu,/ licha ya mapaji yote haya,/ unajitoa mwenyewe kwangu,/ ili uweze kujiunganisha na kiumbe dhaifu na maskini./
Ee Kristu,/ nafurahi sana nionapo kwamba unapendwa/ na kwamba sifa na utukufu wako vinaongezwa/ hasa ya Huruma yako./ Ee Kristu,/ sitaacha kamwe kuutukuza wema wako na huruma yako,/ hadi dakika ya mwisho ya maisha yangu./ Kwa kila tone la damu yangu/ na kwa kila pigo la moyo wangu/ naitukuza Huruma yako./ Natamani kugeuzwa kabisa/ na kuwa utenzi wa utukufu wako./ Naomba siku ya kufa kwangu/ popote nitakapokuwa nimelala,/ pigo la mwisho la moyo wangu/ liwe utenzi mpendevu/ usifuo Huruma yako isiyo na kipimo./ Amina
(Na Mt. Faustina Kowalska).
Ee Mama mbarikiwa na Bikira mwenye uchungu, Malkia wa Mashahidi, uliyesimama chini ya msalaba na uliyemtazama Mwana wako akifa, unitazame kwa huruma ya kimama ninayekusikitikia. Kwa sababu ya upanga uliochoma moyo wako, kwa mateso ya maisha yako nakuomba uniangalie kwa wema ukasikilize maombi yangu. Nakuomba, ee Mama, uniombee daima kwa Mwana wako, najua hawezi kukuvyima wewe kitu chochote. Basi, ufanye, Moyo wa Mwanao ukubali kunijalia ombi langu hili โฆโฆโฆโฆโฆโฆโฆ(taja ombi lako).
Maana nitamkimbilia nani katika mahitaji na misiba yangu isipokuwa kwako, ee Mama wa huruma? Wewe hasa unaweza kutusaidia sisi tulio bado katika bonde la machozi kwa sababu ulishiriki mateso ya Mwanao kutukomboa. Umtolee Yesu tone moja la Damu yake takatifu. Umkumbushe ya kuwa wewe ni matumaini, furaha na maisha yetu ukanipatie jambo ninalokuomba kwa Yesu Kristo, bwana wetu. Amina.
Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria, naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Salamu Maria,โฆ.
Ndimi Mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena. Salamu Maria, โฆโฆ
Neno wa Bwana akatwaa Mwili, akakaa kwetu. Salamu Maria, โฆ..
Utuombee, ee Mzazi Mtakatifu wa Mungu, tujaliwe ahadi za Kristo.
Tuombe:
Tunakuomba ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika, kwamba, Kristo Mwanao amejifanya mtu: kwa mateso na Msalaba wake, utufikishe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu, Amina.
Mungu wangu,
nasadiki maneno yote linalosadiki na linalofundisha kanisa katoliki la Roma;
Kwani ndiwe uliyefundisha hayo,
wala hudanganyiki,
wala hudanganyi. Amina
Ee Mt. Yosefu, tunakuomba kwa ajili ya wale asio na ajira, kwa ajili ya wale wanaotaka kujipatia kipato chao na kulisha familia zao.
Wewe u Msimamizi wa wafanyakazi, tujalie kwamba pasiwepo kati yetu mtu asiye na ajira, na kwamba wale wote ambao wako tayari kufanya kazi waweze kuelekeza nguvu zao na uwezo wao katika kuwatumikia wanadamu wenzao na kujipatia kipato halali.
Wewe u Msimamizi wa familia, usiwaache wale wenye watoto wa kuwatunza na kuwalea wakose namna ya kufanya hivyo. Uwahurumie ndugu zetu waliokosa ajira na kugubikwa na umasikini kwa sababu ya magonjwa au mipango mibaya ya kijamii. Wasaidie viongozi wetu wa kisiasa na walioshika usukani katika nyanja mbalimbali za kiuzalishaji wavumbue suluhu mpya na za haki za jambo hili. Utujalie ili kila mmoja wetu apate kujipatia kipato halali na kufurahia fursa ya kushiriki kadri ya uwezo wake, katika maisha bora zaidi kwa wote. Utujalie ili wote tushiriki pamoja katika raslimali alizotujalia Mungu, na pia utujalie tuwe tayari daima kuwasaidia wale walio wahitaji kuliko sisi.
Amina.
Salamu Maria
Umejaa neema
Bwana yu nawe
Umebarikiwa kuliko wanawake wote
Na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa
Maria Mtakatifu
Mama wa Mungu
Utuombee sisi wakosefu
Sasa, na saa ya kufa kwetu.
Amina.
Ee Mt. Yosefu, ambaye ulinzi wako ni mkubwa, wenye nguvu na wa haraka mbele ya Kiti cha Enzi cha Mungu, ninakukabidhi nia na haja zangu zote. Ee Mt. Yosefu, unisaidie kwa maombezi yako yenye nguvu, na unipatie kutoka kwa Mwanao Mungu, baraka zote za kiroho, kwa njia ya Kristu Bwana wetu, ili nikishapata msaada wako wa mbinguni ningali bado hapa duniani, niweze nami kumsifu, kumwabudu na kumshukuru Mungu aliye Baba mwema kabisa kushinda wote. Ee Mt. Yosefu, sichoki kamwe kufikiri moyoni kwa upendo, jinsi Mtoto Yesu alivyokuwa amesinzia mikononi mwako. Akiwa amepumzika hivyo karibu na moyo wako, sithubutu kujongea, nisije nikamsumbua, bali nakuomba wewe umkumbatie na kumbusu kwa niaba yangu na kumwambia anipe busu lake nitakapovuta pumzi yangu ya mwisho.
Mtakatifu Yosefu Msimamizi wa wanaozimia roho; Utuombee.
Amina.
Sala hii ilipatikana katika mwaka wa hamsini wa Bwana na Mwokozi Wetu Yesu Kristu. Mnamo mwaka 1505 Baba Mtakatifu alimtumia sala hii Mfalme Charles wakati alipokuwa anaenda vitani. Yeyote atakayeisoma sala hii, au kuisikia ikisomwa, au kuibeba, hatakufa kifo cha ghafla,hatazama majini, hatadhurika kwa sumu, wala hataanguka katika mikono ya adui zake, au kuunguzwa katika moto wowote ule, au kushindwa katika vita.
Sali sala hii kwa siku tisa mfululizo, kwa kuomba jambo lolote unalolihitaji. Haijawahi kusikika kuwa sala hii imeshindwa jambo.
Baba yetu uliye mbinguni
Jina lako litukuzwe
Ufalme wako ufike
Utakalo lifanyike
Duniani kama mbinguni
Utupe leo mkate wetu wa kila siku
Utusamehe makosa yetu
Kama tunavyowasamehe
Na sisi waliotukosea
Usitutie katika kishawishi
Lakini utuopoe maovuni.
Amina.
Recent Comments