Ee Mtukufu Mt. Yosefu, ulichaguliwa na Mungu kuwa Baba Mlishi wa Yesu, mchumba safi kabisa wa Maria Bikira Milele, na mkubwa wa Familia Takatifu. Umechaguliwa na Mwakilishi wa Kristu kama Msimamizi wa kimbingu na mlinzi wa Kanisa alilolianzisha Kristu. Ndiyo maana ninakuomba kwa matumaini makuu usaidizi wako wenye nguvu kwa ajili ya Kanisa zima duniani.
Mlinde kwa namna ya pekee, kwa upendo wa kikweli wa ki-baba, Baba Mtakatifu na Maaskofu wote na Mapadre wenye ushirika na Kiti cha Petro. Uwe mlinzi wao wote wanaotumikia wokovu wa wanadamu kati ya majaribu na mahangaiko ya maisha haya, na utujalie kwamba watu wote wa dunia hii wamfuate Kristu na Kanisa alilolianzisha.
Mpendwa Mtakatifu Yosefu, ukubali majitoleo ya nafsi yangu ambayo sasa ninafanya. Ninajiweka wakfu kwako kwa ajili ya utumishi wako, ili daima wewe uwe baba yangu, mlinzi wangu, na kiongozi wangu katika njia ya wokovu. Unijalie usafi mkuu wa moyo na matamanio makuu ya maisha ya kiroho. Unijalie ili matendo yangu yote, kwa mfano wako, yawe kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, pamoja na Moyo wa kimungu wa Yesu, moyo safi wa Maria, na moyo wako wa ki-baba. Uniombee, nami nishiriki kifo chako cha furaha na kitakatifu.
Amina.