Anachokiangalia Mungu
Mungu haangalii matemdo ya mtu ya nje tuu, bali anaangalia ndani kabisa mawazo ya mtu na nia yake. Nia ya mtu ndiyo inayoonyesha mtu alivyo.
Mungu haangalii matemdo ya mtu ya nje tuu, bali anaangalia ndani kabisa mawazo ya mtu na nia yake. Nia ya mtu ndiyo inayoonyesha mtu alivyo.
Mtumainie Mungu kwa maana Mungu hawatupi wale wamtumainiao na kumgoja. Mkono wake upo tayari kwa ajili ya kuwaokoa wale wanaomwelekea.
Sala ni Hazina. Kusali ni muhimu sana. Sala unayosali leo inaweza kukusaidia hata miaka kumi ijayo au ikasaidia watoto wa watoto wako. Mungu ni mwenye fadhila na anakumbuka yote. Mwombe Mungu akulinde ukiwa mzima ili uwapo hatarini akukumbuke hata kabla hujamwomba.
Usiache kusali na kutenda mema kwa kuwa huwezi jua ni watu wangapi wanategemea sala na matendo yako mema. Kumbuka Mungu alimwambia Abraham kama akikuta Wacha Mungu wengi hataiharibu Sodoma na Gomora. Vivyo hivyo Inawezekana wapo watu wengi wanaonufaika na Sala na matendo yako, hasa watu wako wa karibu uwapendao. Unapokuwa mtu wa Sala na mcha Mungu unabarikiwa wewe na wale wa karibu yako. KAMWE USIACHE KUMCHA MUNGU NA KUSALI. Ukiwa mregevu ni sawa na unakata Mnyororo wa Baraka za Mungu kwako na wenzako.
Kwa kawaida kwenye maisha unapofikia Hatua unaona Mungu hayupo kabisa na wewe basi ujue huo ndio wakati ambao Mungu yupo karibu na wewe zaidi.
Usifadhaike moyoni pale unapokuwa katika matatizo au unapopitia changamoto katika maisha. Kumbuka kuwa Mungu yupo, anayaona hayo na anataka kukusaidia, ni wewe tuu kumpa nafasi ya kukusaidia. Hatumpi Mungu nafasi pale tunapozani tunaweza wenyewe.
Jifunze na jijengea tabia ya kumsikiliza Mungu rohoni mwako unaposali. Sala ni mazungumzo ya Mungu na mwanadamu. Mazungumzo yanahusisha kuongea na kusikiliza.
Sala za kila siku katika maisha ndiyo hazina kubwa na msaada hasa wakati wa kufa. Adumuye katika sala Mungu hatomwacha saa ya mwisho. Tusali, tusali, tusali daima…
Mungu anaporuhusu ukaingia katika majaribu na mateso hana nia ya kukutesa bali anataka kukuimarisha. Mungu ni mwema kila wakati.
Sala ndiyo chimbuko la fadhila. Kwa njia ya sala tunapata fadhila za Kimungu na Neema za Mungu. Asaliye daima hujazwa neema na fadhila.
Upendo wa Mungu hauna kikomo. Mama anaweza kumchoka na kumtelekeza mwanae lakini Mungu kamwe hamchoki mtu.
Kutubu ndio njia pekee ya kumrudia Mungu. Toba ya kweli ndiyo iletayo maondoleo ya dhambi. Ukiondolewa dhambi unaimarishwa na kufanywa mya. Tubu usamehewe na kufanywa mpya.
Kama yalivyo maisha ya kimwili, maisha ya kiroho pia yanahitaji mipango. Kila siku panga utafanya nini kiroho, mfano unaweza kupanga sala, kusaidia masikini, kuwa mpole au mwema. Vivyo hivyo kila wiki, kila mwezi na kila mwaka mpya panga cha kufanya kiroho naye Mungu atakubariki na kukupangia zaidi. Huwezi kufanikiwa kiroho kama hujui unafanya nini kiroho.
Mungu anamjibu mtu sala zake kutokana na anachonuia.
Unapo mwomba Mungu Usisahau Kushukuru. Kushukuru ni kuomba mara ya pili. Utazidishiwa kile ulichokiomba na kupewa hata usichokiomba kwa shukrani yako.
Kwa njia ya sala Binadamu anampa Mungu Utukufu, Mungu anampa Binadamu Wokovu na Neema.
Mungu ni Mwaminifu Sana na mwenye mipango na subira katika kila kitu hasa Sala na maombi yetu kwake. Tunaposali leo Mungu anatusikia na kujibu leo, kesho au hata miaka kumi ijayo. Inawezekana hata baraka zako za leo ni majibu ya Sala zako miaka kumi iliyopita. Sali bila kuchoka kwani hujui Sala zako zitakusaidia lini. Usitegemee majibu ya Sala zako wakati huo huo, amini katika uaminifu wa Mungu kwani anajua lini ni siku sahii ya kukujibu.
Sala sio kitu cha muhimu kufanya wakati wa shida tuu. Sala ni kitu cha muhimu zaidi kila siku katika Maisha kuwe na shida au kusiwe na shida.
Upendo wa kweli hauambatani na chuki. Huwezi kusema una Upendo wakati kuna watu wengine unawapenda na wengine unawachukia. Ni sawa na kusema kitambaa ni cheupe lakini kina madoa doa, maana yake sio cheupe.
Uwe na maono au ndoto ya mambo unayotaka kufanya maishani naye Mungu atakubariki na kujidhihirisha katika ndoto zako.
Recent Comments