Nukuu za Dini

Toba, msamaha na Baraka

Inashangaza kwa sasa watu wengi hawapendi kuambiwa kuhusu kutubu dhambi zao bali wanataka waambiwe watabarikiwa. Kama vile wewe huwezi kumvika mwanao nguo nzuri kabla ya kumuogesha vivyo hivyo na Mungu hawezi kukubariki kabla ya kukutakasa. Unapotubu unasamehewa na kutakaswa dhambi zako kisha unakua umefungua milango ya baraka. Huwezi kubarikiwa bila kutubu kweli.

Maana ya kubarikiwa

Kubarikiwa ni Kutokutindikiwa na kuwa na matumaini ya siku zijazo. Kubarikiwa ni kuwa na amani, furaha, na matumaini katika maisha ya sasa na yajayo. Kubarikiwa sio kuwa na mali nyingi. Yesu hajawahi kumwambia mtu kuwa utakua tajiri sana kwa kuwa umebarikiwa wala hajawahi kumuahidi kumpa mtu utajiri. Unaweza ukawa na mali nyingi lakini zikakufanya ukakosa Amani, furaha na matumaini ya siku zijazo. Ndiyo maana Mungu anatupa kulingana na vile tunavyohitaji ili visiwe mtego kwetu.

Upendo mkuu wa Yesu

Fikiria umenunua zawadi nzuri ya gharama sana na unataka kumpa mtu umpendaye sana. Akipokea zawadi yako unafurahi sana, akikataa kuipokea zawadi inaumiza sana, lakini inaumiza zaidi akiipokea kisha akaitupa mbele yako na kuona haina maana. Hiki ndicho kinachotokea kwa Yesu. Yesu yupo kwa ajili ya kutupa zawadi ya Wokovu alyogharamia kwa uhai wake. Tunapoipokea tunamfurahisha sana, tukiikataa tunamhuzunisha na tunapoipokea na kuiacha baadae tunamhuzunisha kwelikweli.

Mawazo ya Mungu tunapokua na shida na mateso

Mawazo ya Mungu ni makuu. Mungu anatuwazia mema daima. Hata unapopitia shida na matatizo katika maisha nia ya Mungu inabaki kuwa njema ya Kukuonyesha ukuu wake na kukuwezesha kumjua yeye. Pengine usingejua matendo ya Mungu bila kupitia shida na changamoto katika maisha. Mungu hapendi upate shida bali anaruhusu hayo ili upate faida ya kumjua na kujua uwezo wake. Hata Yesu ilibidi apitie mateso na kifo ili uwezo wa Mungu udhihirike baada ya kufufuliwa. Amini kuwa kuna mema mbele yako baada ya mateso haya ya sasa.

Kutubu na Kusamehewa dhambi

Usiogope wala usisite kutubu na kuomba msamaha kwa Mungu. Uwe na Amani na Matumaini katika Huruma ya Mungu itokayo katika Upendo wake wa Mfano wa baba awapendavyo wanawe. Mungu anasubiri kukupokea kwenye mikono yake Ili akutunze kama mtoto wake kama utatubu na kumrudia yeye. Amua kumwendea leo! Anakungoja ni wewe tuu…

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About