Masomo ya Misa ya Kanisa Katoliki

MASOMO YA MISA, MACHI 25, 2022: IJUMAA, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

MASOMO YA MISA, MACHI 25, 2022
IJUMAA, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

SHEREHE YA KUPASHWA HABARI YA KUZALIWA BWANA

 

SOMO 1

Isa. 7:10 – 14
Bwana alisema na Ahazi akinena, Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana. Naye akasema, Sikilizeni sana, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 40:6 – 10 (K) 7 , 8

(K) Tazama, nimekuja, Ee Bwana, kuyafanya mapenzi yako.

Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)

Katika gombo la chuo nimeandikiwa
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)

Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)

Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;
Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha fadhili zako wala kweli yako
Katika kusanyiko kubwa. (K)

SOMO 2

Ebr. 10:4 – 10
Haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) niyafanye mapenzi yako, Mungu.
Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.

Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO

Yn. 1:14

Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukaona utukufu wake.

INJILI

Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye ju, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MACHI 22, 2022: JUMATANO, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

SOMO 1 – Kumb. 4:1, 5-9

Musa aliwaambia makutano: Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mmzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu.Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwmingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi,5 mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia⁵ amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.

Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI – Zab. 147:12-13, 15-16, 19-20 (K) 12(K)

Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;

Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,Amewabariki wanao ndani yako. (K)

Huipeleka amri yake juu ya nchi,Neno lake lapiga mbio sana.

Ndiye atoaye theluji kama sufu,Huimwaga barafu yake kama majivu. (K)

Humhubiri Yakobo neno lake,Na Israeli amri zake na hukumu zake.

Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)

SHANGILIO

Mbegu neno la Mungu, mpanzi lakini ni Kristu; Yeyote ampataye, ataishi milele.

INJILI – Mt. 5:17-19

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msidhani kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka hata yote yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme mbinguni.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, APRILI 1, 2023: JUMAMOSI, JUMA LA 5 LA KWARESIMA

SOMO 1

Eze. 37:21 – 28

Bwana Mungu asema hivi: Tazama, nitawatwaa wana wa Israeli toka kati ya mataifa walikokwenda, nami nitawakusanya pande zote, na kuwaleta katika nchi yao wenyewe; nami nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi hiyo, juu ya milima ya Israeli; na mfalme mmoja atakuwa mfalme wao wote; wala hawatakuwa tena mataifa mawili, wala hawatagawanyikana kuwa falme mbili tena, hata milele. Wala hawatajitia uchafu tena kwa vinyago vyao, wala kwa vitu vyao vichukizavyo, wala kwa makosa yao mmojawapo; lakini nitawaokoa, na kuwatoa katika makao yao yote, ambayo wamefanya dhambi ndani yake, nami nitawatakasa; basi watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja; nao wataenenda katika hukumu zangu, na kuzishika amri zangu, na kuzitenda. Nao watakaa katika nchi niliyompa Yakobo, mtumishi wangu, walimokaa baba zenu; nao watakaa humo, wao na watoto wao, na watoto wa watoto wao, milele; na Daudi, mtumishi wangu, atakuwa mkuu wao milele. Tena nitafanya agano la Amani pamoja nao; litakuwa agano la milele pamoja nao; naami nitaweka na kuwazidisha, na patakatifu pangu nitapaweka katikati yao milele. Tena maskani yangu itakuwa pamoja nao; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Na mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, mimi niwatakasaye Israeli, patakatifu pangu patakapokuwa katikati yao milele.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Yer. 31:10 – 13 (K) 10

(K) Bwana anatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Lisikieni neno la Bwana, enyi mataifa,

Litangazeni visiwani mbali;

Mkaseme: Aliyemtawanya Israeli atamkusanya,

Na kumlinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo,

Amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye. (K)

Watakuja na kuimba katika mlima Sayuni.

Wataukimbilia wema wa Bwana,

Nafaka, na divai, na mafuta,

Na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe. (K)

Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,

Na vijana na wazee pamoja;

Maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,

Nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao. (K)

SHANGILIO

Zab. 95:8 , 9

Leo msifanye migumu mioyo yenu, lakini msikie sauti yake Bwana.

INJILI

Yn. 11:45 – 57

Wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Maria, na kuyaona yale aliyoyafanya Yesu, wakamwamini. Lakini wengine wakaenda zao kwa Mafarisayo, wakawaambia aliyoyafanya.

Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi. Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja watamuondolea mahali petu na taifa letu. Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui neno lolote; wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima. Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa hilo, wala si kwa ajili ya taifa hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili waawe wamoja. Basi tangu siku ile walifanya shauri la kumwua.

Kwa hiyo Yesu hakutembea tena kwa wazi katikati ya Wayahudi; bali alitoka huko, akaenda mahali karibu na jangwa, mpaka mji uitwao Efraimu; akakaa huko pamoja na wanafunzi wake.

Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; na wengi wakakwea toka mashambani kwenda Yerusalemu kabla ya Pasaka, ili wajitakase. Basi wao wakamtafuta Yesu, wakasemezana hali wamesimama hekaluni, Mwaonaje? Haji kabisa sikukuu hii? Na wakuu wa makuhani wa Mafarisayo walikuwa wametoa amri ya kwamba mtu akijua alipo, alete habari, ili wapate kumkamata.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo

JUMAPILI YA 19 YA MWAKA A: MASOMO YA MISA AGOSTI 13, 2023

Somo la Kwanza

1Fal 19:9, 11-13

Eliya alifika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia. Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunjavunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi: na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu.

Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi vake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango.

NENO LA BWANA…….

Wimbo wa Katikati

Zab 85:8-13

Nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawambia watu wake amani.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.

(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.

Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni.

(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.

Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbelc zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.

(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.

Somo la Pili

Rum 9:1-5

Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu.

Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili.

Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.

NENO LA BWANA…..

Shangilio

Lk 19:38

Aleluya, aleluya,
Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana;
Aleluya.

Somo la Injili

Mt 14:22-33

Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambe. wakati yeye alipokuwa akiwaaga makutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.

Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea. akienda kwa miguu juu ya bahari.

Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli, wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu akanena, akawaambia, Jipeni movo; ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo.

Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe akisema, Bwana, niokoe.

Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia wakisema, Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.

NENO LA BWANA……….

MASOMO YA MISA, MARCHI 16, 2022: JUMATANO, JUMA LA 2 LA KWARESIMA

SOMO 1

Yer. 18-18-20

Waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yoyote.

Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili nisema mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 31:4-5, 13-15 (K) 16

(K) Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana.

Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,

Maana Wewe ndiwe ngome yangu.

Mikononi mwako naiweka roho yangu;

Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)

Maana nimesikia masingizio ya wengi;

Hofu ziko pande zote.

Waliposhauriana juu yangu,

Walifanya hila wauondoe uhai wangu. (K)

Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,

Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.

Nyakati zangu zimo mikononi mwako;

Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)

SHANGILIO

Lk. 8:15

Heri wale walishikao neno la Mungu katika moyo wao mwema na unyofu, na wazaao matunda katika uvumilivu.

INJILI

Mt. 20:17-28

Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.

Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza. Akawaambia, Hakika mtakinywa kikombe change; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.

Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MEI 21, 2023:
DOMINIKA YA 7 YA PASAKA
SHEREHE YA KUPAA BWANA

MWANZO:
Mdo. 1:11

Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Atakuja vivyo hivyo mlivyomwona akienda zake mbinguni, Aleluya.

SOMO 1

Mdo. 1:1-11

Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha, hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu. Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohane alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache.

Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.

Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 47 : 1-2, 5-6, 7-8, (K) 5

(K) Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti ya baragumu. au: Aleluya

Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe,
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote. (K)

Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Mwimbieni Mungu, naam, imbeni;
Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. (K)

Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili.
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu. (K)

SOMO 2

Efe 1 : 17-23

Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO

Mt. 28:19-20

Aleluya, aleluya,
Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote.
Aleluya.

INJILI

Mt. 28:16-20

Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JUNI 04, 2023: SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU – Jumapili baada ya Pentekoste

MWANZO:

Asifiwe Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu; kwasababu ametufanyizia huruma yake.

SOMO 1

Kut. 34 : 4-6, 8-9

Musa aliinuka na mapema asubuhi, naye akakwea katika mlima wa Sinai, kama Bwana alivyomwamuru, akazichukua hizo mbao mbili za mawe mkononi mwake.

Bwana akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la Bwana. Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu. Akasema, Ikiwa sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu

WIMBO WA KATIKATI

Dan. 3:52-56. (K) 52

(K) Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu:

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako;

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi;

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

SOMO 2

2 Kor. 13 :11-14

Hatimaye, ndugu, kwaherini; mtimilike, mfariji- ke, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Sali- mianeni kwa busu takatifu. Watakatifu wote wawasalimu. Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu. na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANG1LIO

Ufu. 1 :8

Aleluya, Aleluya,

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, Mungu ambaye yupo, aliyekuwako, na atakayekuja.

Aleluya.

INJILI

Yn. 3:16-18

Yesu alimwambia Nikodemu: Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhu- kumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MACHI 28, 2022: JUMATATU: JUMA LA 4 LA KWARESIMA

SOMO 1

Isa. 65:17-21

 

Bwana asema: Tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni. Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.

Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza. Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa. Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 30:1, 3-5, 10-12 (K) 1

 

(K) Nitakutukuza, ee Bwana, kwa maana umeniinua.

 

Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,

Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.

Umeniinua nafsi yangu,

Ee Bwana, kutoka kuzimu.

Umenihuisha na kunitoa

Miongoni mwao washukao shimoni. (K)

 

Mwimbieni Bwana zaburi,

Enyi watauwa wake.

Na kufanya shukrani.

Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.

Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,

Katika radhi yake mna uhai.

Huenda kilio huja kukaa usiku,

Lakini asubuhi huwa furaha. (K)

 

Ee Bwana, usikie, unirehemu,

Bwana, uwe msaidizi wangu.

Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;

Ulinivua gunia, ukanivika furaha.

Ee Bwana, mungu wangu,

Nitakushukuru milele. (K)

 

SHANGILIO

Eze. 33:11

 

Sikufurahii kufa kwake mtu mwovu, asema Bwana, bali aiache njia yake mbaya, akaishi.

 

INJILI

Yn. 4:43-54

 

Baada ya siku mbili hizo Yesu aliondoka huko, akaenda Galilaya. Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe. Basi alipofika Galilaya, Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu.

Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa kufani. Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa? Yule diwani akamwambia, Bwana, ushuke asijakufa mtoto wangu. Yesu akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia. Hata alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai. Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa hajambo; nao wakamwambia, jana, saa saba, homa ilimwacha. Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile alipoambiwa na Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake.

Hiyo ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu, alipokuwa ametoka Uyahudi kufika Galilaya.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MEI 24, 2023: JUMATANO YA 7 YA PASAKA

SOMO 1

Mdo 20 : 28-38

Paulo aliwaambia wakuu wa kanisa ya Efeso: Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi. Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote. Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu, wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 68:28-29, 32-35 (K) 32

(K) Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu.
Au: Aleluya.

Ee Mungu, uziamuru nguvu zako;
Ee Mungu, uwe hodari uliyetufanyia makuu.
Kwa ajili ya hekalu lako Yerusalemu
Wafalme watakuletea hedaya. (K)

Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu,
Msifuni Bwana kwa nyimbo.
Apandaye mbingu za mbingu za tangu milele;
Aitoa sauti yake, sauti ya nguvu.
Mhesabieni Mungu nguvu; (K)

Enzi yake i juu ya Israeli;
Na nguvu zake zi mawinguni.
Mungu ni mwenye kutisha Kutoka patakatifu pako.
Ndiye Mungu wa Israeli;
Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo.
Na ahimidiwe Mungu. (K)

SHANGILIO

Yn. 14 : 26

Aleluya, aleluya,
Roho Mtakatifu atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
Aleluya.

INJILI

Yn. 17:11-19

Siku ile, Yesu alisali akisema: Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.

Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.

Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

MASOMO YA MISA, MACHI 19, 2022: JUMAMOSI, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

SHEREHE YA MT. YOSEFU, MUME WA BIKIRA MARIA

SOMO 1

2Sam. 7: 4 – 5, 12 – 14, 16

Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema, Enenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, Bwana asema hivi, siku zako zitakapo timia, ukalala na Baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake.

Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu, akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 89:1 – 4, 26, 28 (K) 36(K)

Wazao wake watadumu milele.

Fadhili za Bwana nitaziimba milele;Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.

Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)

Nimefanya agano na mteule wangu,Nimemwapia Daudi, mtumishi wangu.Wazao wako nitawafanya imara milele,Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. (K)

Yeye ataniita, Wewe baba yangu,Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.

Hata milele nitamwekea fadhili zangu,Na agano langu litafanyika amini kwake. (K)

SOMO 2

Rum. 4:13, 16 – 18, 22

Ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa Imani. Kwa hiyo ilitoka katika Imani, iwe njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila kwa wale wa Imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote; (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ilia pate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO

Zab. 84:5

Heri wakaao nyumbani mwako, Ee Bwana.

INJILI

Mt. 1:16, 18 – 21, 24

Yakobo alimzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa yesu aitwaye Kristo.Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akimchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MACHI 18, 2022: IJUMAA, JUMA LA 2 LA KWARESIMA

SOMO 1

Mwa. 37:3-4, 12-13, 17-28

 

Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, na hawakuweza kusema naye kwa amani.

Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao.

Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shuri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula.

Wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yenu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali.

Wakapita wafanyabiashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 105:16-21 (K) 5

 

(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.

 

Akaiita njaa iijilie nchi,

Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.

Alimpeleka mtu mbele yao,

Yusufu utumwani. (K)

 

Walimwumiza miguu yake kwa pingu,

Akatiwa katika minyororo ya chuma.

Hata wakati wa kuwadia neno lake,

Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)

 

Mfalme alituma watu akamfungua,

Mkuu wa watu akamwachia.

Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,

Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)

 

SHANGILIO

Yn. 3:16

 

Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee; Kila mtu amwaminiye huwa na uzima wa milele.

 

INJILI

Mt. 21:33-43; 45-46

 

Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza, wakawatenda vile vile.

Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Ataangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake.

Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa, linguine lenye kuzaa matunda yake.

Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata waliogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

 

MASOMO YA MISA, JUMAPILI, JULAI 2, 2023: DOMINIKA LA 13 LA MWAKA

MWANZO

Zab. 47:2

Enyi watu wote, pigeni makofi, mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe.

SOMO 1 

2 Fal 4:8-11,14-16

Ilikuwa siku moja, Elisha alikwenda Shunemu; na huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo; nave akamshurutisha aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula.

Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu w’a Mungu. Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa na itakuwa, atujiapo, ataingia humo.

Ikawa siku moja akafikia huko, akaingia katika chumba kile akalala. Akasema, Basi, atendewe nini? Gehazi akajibu, Hakika hana mwana, na mumewe ni mzee. Akamwambia, Kamwite. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mlangoni. Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI 

Zab. 89 : 1-2, 15-18 (K) 1(K)

Fadhili za Bwana nitaziimba milele. Fadhili za Bwana nitaziimba milele; Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako. Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)

Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe, Ee Bwana, kuenenda katika nuru ya uso wako. Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa,Na kwa haki yako hutukuzwa. (K)

Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe, Na kwa radhi yako pern be yetu itatukuka.

Maana ngao yetu ina Bwana,Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli. (K)

SOMO 2 

Rum. 6:3-4,8-11

Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katikawafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.

Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye; tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena, wala mauti haimtawali tena. Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu. Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi, na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO 

Mt. 11:25

Aleluya, aleluya, 
Nakushukuru, Baba, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. 
Aleluya.


INJILI 

Mt. 10:37-42


Yesu aliwafundisha mitume wake hivi: Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.

Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeave nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki.

Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia. haitampotea kamwe thawabu yake.

Neno la Bwana……..Sifa kwako Ee Kristo

MASOMO YA MISA, JUNI 11, 2023: SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA BWANA WETU YESU KRISTU

SOMO 1

Kum. 8:2-3;14-16

Musa aliwaambia makutano: Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako, aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu, kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. Basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 147:12-15,19-20 (K) 12

(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;

Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.

Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,

Amewabariki wanao ndani yako. (K)

Ndiye afanyaye amani mipakani mwako,

Akushibishaye kwa unono wa ngano.

Huipeleka amri yake juu ya nchi,

Neno lake lapiga mbio sana. (K)

Humhubiri Yakobo neno lake,

Na Israeli amri zake na hukumu zake.

Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,

Wala hukumu zake hawakuzijua.

aleluya. (K)

SOMO 2

1Kor. 10:16-17

Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANG1LIO

Yn. 6:51

Aleluya, aleluya,

Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; asema Bwana; mtu akila chakula hiki, ataishi milele.

Aleluya.

INJILI

Yn. 6:51-58

Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JUMAPILI, AGOSTI 20, 2023: JUMA LA 20 LA MWAKA 

SOMO I

Isa. 56:1, 6-7

Bwana asema hivi, Shikeni hukumu, mkatenda haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.

Neno la Bwana…Tumshukuru Mungu

WIMBO WA KATIKATI 

Zab. 67:1-2, 4-5, 7 (K) 5

(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, 
Watu wote na wakushukuru.

Mungu na atufadhili na kutubariki,

na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulikane duniani,
wokovu wake katikati ya mataifa yote. (K)

mataifa na washangilia,

naam, waimbe kwa furaha.
Maana kwa haki utawahukumu watu,
na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)

watu na wakushukuru, Ee Mungu,

watu wote na wakushukuru.
Mungu atatubariki sisi;
miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)

SOMO 2

Rum. 11:13-15, 29-32

Nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa. Basi, naitukuza huduma iliyo yangu? Huenda nikapata kuwapatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao. Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa. Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake. Kwa maana kama ninyi zamani mlivyomwasi Mungu, lakini sasa mmepata rehema kwa kuasi kwao; kadhalika na hao wameasi sasa, ili kwa kupata rehema kwenu wao nao wapate rehema. Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote.

Neno la Bwana…Tumshukuru Mungu

SHANGILIO

Mdo. 16:14


Aleluya, aleluya,

Fungua mioyo yetu, Ee Bwana, 
Ili tuyatuze maneno ya Mwanao.
Aleluya

INJILI 

Mt. 15:21-28

Yesu aliondoka huko, akaenda kando pande za tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema, Bwana unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.

Neno la Bwana…Sifa kwako, ee Kristo

MASOMO YA MISA, MEI, 28, 2023: SHEREHE YA PENTEKOSTE

SOMO 1

Mdo. 2:1-11

Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.


Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelani, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu

WIMBO WA KATI KATI

Zab. 104:1, 24, 29-31, 34, (K) 30

(K) Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya upya uso wa nchi. au: Aleluya.

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Dunia imejaa mali zako. (K)

Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wa nchi. (K)

Utukufu wa Bwana na udumu milele;
Bwana na ayafurahie matendo yake.
Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
Mimi nitamfurahia Bwana. (K)

SOMO 2

1 Kor. 12 :3b-7, 12-13

Hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.

Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu

SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Uje Roho Mtakatifu, uzienee nyoyo za waamini wako uwatie mapendo yako.
Aleluya.

INJILI

Yn. 20 :19-23

Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.
Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JULAI 24, 2021: JUMAMOSI, JUMA LA 16 LA MWAKA

SOMO 1

Kut. 24:3-8

Musa aliwambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 50:1-2, 5-6, 14-15 (K) 14 (K)

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru. Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi, Toka maawio ya jua hata machweo yake. Tokea Sayuni,, ukamilifu wa uzuri, Mungu amemulika. (K)

Nikusanyieni wacha Mungu wangu, Waliofanya agano nami kwa dhabihu. Na mbingu zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu. (K)

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru; Mtimizie Aliye juu nadhiri zako. Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza. (K)

SHANGILIO

Zab. 8:15

Aleluya, aleluya,

Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu na kulishika.

Aleluya.

INJILI

Mt. 13:24 – 30

Yesu aliwatolea makutano mfano akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala akaja adui yake akapanda magugu katikati ya agano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, APRILI 5, 2022: JUMANNE JUMA LA 5 LA KWARESIMA

SOMO 1

Hes. 21:4-9

Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.

Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi, Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo, ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 102:1-2, 15-20 (K) 1

(K) Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, kilio changu kikufikie.

Ee Bwana, usikie kuomba kwangu,

Kilio change kikufikie,

Usinifiche uso wako siku ya shida yangu,

Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi. (K)

Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana,

Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;

Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,

Atakapoonekana katika utukufu wake,

Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,

Asiyadharau maombi yao. (K)

Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,

Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.

Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,

Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi,

Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,

Na kuwafungua walioandikiwa kufa. (K)

SHANGILIO

Yn. 8:12

 

Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, yeye anifuataye, atakuwa na nuru ya uzima.

INJILI

 

Yn. 8:21-30

 

Yesu aliwaambia Mafarisayo: Mimi naondoka, nanyi mtanitafuta; nanyi mtakufa katika dhambi yenu; mimi niendako ninyi hamwezi kuja.

Basi, Wayahudi wakasema, Je! Atajiua! Kwa kuwa asema, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja?

Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.

Basi wakamwambia, U nani wewe? Yesu akawaambia, Hasa neno lilo hilo ninalowaambia. Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu; lakini yeye aliyenipeleka ni kweli, nami niliyoyasikia kwake ndiyo ninenayo katika ulimwengu.

Wala hawakutambua ya kuwa anawatajia Baba. Basi Yesu akawaambia, Mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo. Naye aliyenipeleka yu pamoja nami; hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo.

Naye alipokuwa akisema hayo, wengi walimwamwini.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About