Masomo ya Misa ya Kanisa Katoliki

MASOMO YA MISA, JUNI 18, 2023: JUMAPILI, JUMA LA 11 LA MWAKA

SOMO 1 

Kut. 19 :2-6

Waisraeli walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. Musa akapanda kwa Mungu, na Bwana akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya: Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi. Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI 

Zab. 100 :2-3, 5 (K) 3

(K) Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.

Mtumikieni Bwana kwa furaha;

Njoni mbele zake kwa kuimba. (K)

Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;

Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;

Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)

Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;

Rehema zake ni za milele;

Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)

SOMO 2 

Rum. 5 : 6-11

Wapendwa, hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake veye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake, zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, am have kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANG1LIO 

Yn. 15 :15

Aleluya, aleluya, Ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.

Aleluya.

INJILI 

Mt. 9:36-10:8

Yesu alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza

magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti. Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, APRILI 5, 2022: JUMANNE JUMA LA 5 LA KWARESIMA

SOMO 1

Hes. 21:4-9

Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.

Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi, Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo, ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 102:1-2, 15-20 (K) 1

(K) Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, kilio changu kikufikie.

Ee Bwana, usikie kuomba kwangu,

Kilio change kikufikie,

Usinifiche uso wako siku ya shida yangu,

Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi. (K)

Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana,

Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;

Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,

Atakapoonekana katika utukufu wake,

Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,

Asiyadharau maombi yao. (K)

Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,

Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.

Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,

Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi,

Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,

Na kuwafungua walioandikiwa kufa. (K)

SHANGILIO

Yn. 8:12

 

Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, yeye anifuataye, atakuwa na nuru ya uzima.

INJILI

 

Yn. 8:21-30

 

Yesu aliwaambia Mafarisayo: Mimi naondoka, nanyi mtanitafuta; nanyi mtakufa katika dhambi yenu; mimi niendako ninyi hamwezi kuja.

Basi, Wayahudi wakasema, Je! Atajiua! Kwa kuwa asema, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja?

Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.

Basi wakamwambia, U nani wewe? Yesu akawaambia, Hasa neno lilo hilo ninalowaambia. Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu; lakini yeye aliyenipeleka ni kweli, nami niliyoyasikia kwake ndiyo ninenayo katika ulimwengu.

Wala hawakutambua ya kuwa anawatajia Baba. Basi Yesu akawaambia, Mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo. Naye aliyenipeleka yu pamoja nami; hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo.

Naye alipokuwa akisema hayo, wengi walimwamwini.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MEI 24, 2023: JUMATANO YA 7 YA PASAKA

SOMO 1

Mdo 20 : 28-38

Paulo aliwaambia wakuu wa kanisa ya Efeso: Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi. Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote. Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu, wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 68:28-29, 32-35 (K) 32

(K) Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu.
Au: Aleluya.

Ee Mungu, uziamuru nguvu zako;
Ee Mungu, uwe hodari uliyetufanyia makuu.
Kwa ajili ya hekalu lako Yerusalemu
Wafalme watakuletea hedaya. (K)

Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu,
Msifuni Bwana kwa nyimbo.
Apandaye mbingu za mbingu za tangu milele;
Aitoa sauti yake, sauti ya nguvu.
Mhesabieni Mungu nguvu; (K)

Enzi yake i juu ya Israeli;
Na nguvu zake zi mawinguni.
Mungu ni mwenye kutisha Kutoka patakatifu pako.
Ndiye Mungu wa Israeli;
Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo.
Na ahimidiwe Mungu. (K)

SHANGILIO

Yn. 14 : 26

Aleluya, aleluya,
Roho Mtakatifu atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
Aleluya.

INJILI

Yn. 17:11-19

Siku ile, Yesu alisali akisema: Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.

Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.

Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

MASOMO YA MISA, JUMAPILI, AGOSTI 27, 2023: JUMA LA 21 LA MWAKA

SOMO I

Isa. 22:19-23

Bwana, Bwana wa majeshi, asema hivi: Nami nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo. Na itakuwa katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia; nami nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nvumba ya Yuda. Na ufunguo wa nvumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga. Nami nitamkaza kanta msumari mahali palipo imara; naye atakuwa kiti cha utukufu kwa nyumba ya baba yake.

Neno la Bwana…Tumshukuru Mungu

WIMBO WA KATIKATI 

Zab. 138: 1-3, 6, 9 (K) 9

(K) Ee Bwana, fadhili zako ni za milele, 
Usiziache kazi za mikono yako.

Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,

Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu. (K)

Nitalishukuru jina lako,

Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umeikuza ahadi yako,
Kuliko jina lako lote.
Siku ile niliyokuita ulinitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)

Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu, 

Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali.
Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
Usiziache kazi za mikono yako. (K)

SOMO 2 

Rum 11: 33-36

Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani! Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana? Au ni nani aliyekuwa mshauri wake? Au ni nani aliyempa yeye kitu kwanza, naye atalipwa tena? Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.

Neno la Bwana…Tumshukuru Mungu

SHANGILIO

Mt 11: 25

Aleluya, aleluya,
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, 
kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye
hekima na akili. ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya

INJILI 

Ml 16:13-20

Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipo, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaa- mbia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia. Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikufunulia hili, bali Baba vangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu ye yote ya kwamba yeye ndiye Kristo.

Neno la Bwana…Sifa kwako, ee Kristo

 

MASOMO YA MISA, MACHI 18, 2022: IJUMAA, JUMA LA 2 LA KWARESIMA

SOMO 1

Mwa. 37:3-4, 12-13, 17-28

 

Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, na hawakuweza kusema naye kwa amani.

Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao.

Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shuri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula.

Wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yenu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali.

Wakapita wafanyabiashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 105:16-21 (K) 5

 

(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.

 

Akaiita njaa iijilie nchi,

Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.

Alimpeleka mtu mbele yao,

Yusufu utumwani. (K)

 

Walimwumiza miguu yake kwa pingu,

Akatiwa katika minyororo ya chuma.

Hata wakati wa kuwadia neno lake,

Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)

 

Mfalme alituma watu akamfungua,

Mkuu wa watu akamwachia.

Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,

Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)

 

SHANGILIO

Yn. 3:16

 

Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee; Kila mtu amwaminiye huwa na uzima wa milele.

 

INJILI

Mt. 21:33-43; 45-46

 

Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza, wakawatenda vile vile.

Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Ataangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake.

Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa, linguine lenye kuzaa matunda yake.

Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata waliogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

 

MASOMO YA MISA, MACHI 24, 2022: ALHAMISI, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

SOMO 1

Yer. 7:23-28

 

Naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru, mpate kufanikiwa. Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kw amashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele. Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku na kuwatuma. Lakini hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko baba zao. Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza; nawe utawaita; lakini hawatakuitikia. Nawe utawaambia, Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali vinywa vyao.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 95:1-2, 6-9 (K) 7

 

(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu.

 

Njoni, tumwimbie Bwana,

Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.

Tuje mbele zake kwa shukrani,

Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)

 

Njoni, tuabudu, tusujudu,

Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.

Kwa maana ndiye Mungu wetu,

Na sisi tu watu wa malisho yake,

Na kondoo za mkono wake. (K)

 

Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!

Msifanye migumu mioyo yenu;

Kama vile huko Meriba,

Kama siku ya Masa jangwani.

Hapo waliponijaribu baba zenu,

Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)

 

SHANGILIO

Zab. 51:10, 12

 

Ee Mungu, uniumbie moyo safi,

Unirudishie furaha ya wokovu wako.

 

INJILI

Lk. 11:14-23

 

Yesu alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.

 

Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

 

JUMAPILI YA 19 YA MWAKA A: MASOMO YA MISA AGOSTI 13, 2023

Somo la Kwanza

1Fal 19:9, 11-13

Eliya alifika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia. Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunjavunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi: na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu.

Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi vake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango.

NENO LA BWANA…….

Wimbo wa Katikati

Zab 85:8-13

Nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawambia watu wake amani.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.

(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.

Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni.

(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.

Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbelc zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.

(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.

Somo la Pili

Rum 9:1-5

Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu.

Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili.

Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.

NENO LA BWANA…..

Shangilio

Lk 19:38

Aleluya, aleluya,
Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana;
Aleluya.

Somo la Injili

Mt 14:22-33

Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambe. wakati yeye alipokuwa akiwaaga makutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.

Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea. akienda kwa miguu juu ya bahari.

Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli, wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu akanena, akawaambia, Jipeni movo; ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo.

Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe akisema, Bwana, niokoe.

Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia wakisema, Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.

NENO LA BWANA……….

MASOMO YA MISA, MACHI 21, 2022: JUMATATU , JUMA LA 3 LA KWARESIMA

SOMO 1

2 Fal. 5:1-15

Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena likuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake. Mtu mmoja akaingia, akamwambia bwana wake, akasema, Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi. Mfalme wa Sahmu akasema, Haya! Basi, mimi nitampelekea mfalame wa Israeli waraka. Basi akaenda zake, akachukua mikononi mwake talanta kumi za fedha, na vipande vya dhahabu elfu sita, na mavazi kumi.

Akampelekea mfalme wa Israeli waraka ule, kusema, Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamni kwako, ili upate kumponya ukoma wake. Ikawa, mfalme wa Israeli alipousoma waraka, alirarua mavazi yake, akasema, Je! Mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni, basi, nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami.

Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sana kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.

Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema. Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia nawe utakuwa safi. Lakini Naaman akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira.

Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakisema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; naye nyama ya wmili wak eikarudi ikawa kama nyam aya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.

Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli, basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 42:1-2, 43:3-4 (K) 42:3

(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu.

Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji.

Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu. (K)

Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,

Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? (K)

Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze,

Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu

Na hata maskani yako. (K)

Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu,

Kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu. (K)

SHANGILIO

Yn. 8:12

Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, Yeye anifuataye, atakuwa na nuru ya uzima.

INJILI

Lk. 4:24-30

Yesu alifika Nazareti akawaambia makutano hekaluni: Amin, nawaambia ya kuwa, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na weny eukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakazwa ila Naamani, mtu wa Shamu.

Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipiita katikati yao, akaenda zake.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MEI, 28, 2023: SHEREHE YA PENTEKOSTE

SOMO 1

Mdo. 2:1-11

Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.


Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelani, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu

WIMBO WA KATI KATI

Zab. 104:1, 24, 29-31, 34, (K) 30

(K) Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya upya uso wa nchi. au: Aleluya.

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Dunia imejaa mali zako. (K)

Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wa nchi. (K)

Utukufu wa Bwana na udumu milele;
Bwana na ayafurahie matendo yake.
Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
Mimi nitamfurahia Bwana. (K)

SOMO 2

1 Kor. 12 :3b-7, 12-13

Hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.

Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu

SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Uje Roho Mtakatifu, uzienee nyoyo za waamini wako uwatie mapendo yako.
Aleluya.

INJILI

Yn. 20 :19-23

Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.
Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JUMAPILI, JULAI 2, 2023: DOMINIKA LA 13 LA MWAKA

MWANZO

Zab. 47:2

Enyi watu wote, pigeni makofi, mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe.

SOMO 1 

2 Fal 4:8-11,14-16

Ilikuwa siku moja, Elisha alikwenda Shunemu; na huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo; nave akamshurutisha aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula.

Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu w’a Mungu. Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa na itakuwa, atujiapo, ataingia humo.

Ikawa siku moja akafikia huko, akaingia katika chumba kile akalala. Akasema, Basi, atendewe nini? Gehazi akajibu, Hakika hana mwana, na mumewe ni mzee. Akamwambia, Kamwite. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mlangoni. Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI 

Zab. 89 : 1-2, 15-18 (K) 1(K)

Fadhili za Bwana nitaziimba milele. Fadhili za Bwana nitaziimba milele; Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako. Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)

Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe, Ee Bwana, kuenenda katika nuru ya uso wako. Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa,Na kwa haki yako hutukuzwa. (K)

Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe, Na kwa radhi yako pern be yetu itatukuka.

Maana ngao yetu ina Bwana,Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli. (K)

SOMO 2 

Rum. 6:3-4,8-11

Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katikawafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.

Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye; tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena, wala mauti haimtawali tena. Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu. Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi, na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO 

Mt. 11:25

Aleluya, aleluya, 
Nakushukuru, Baba, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. 
Aleluya.


INJILI 

Mt. 10:37-42


Yesu aliwafundisha mitume wake hivi: Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.

Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeave nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki.

Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia. haitampotea kamwe thawabu yake.

Neno la Bwana……..Sifa kwako Ee Kristo

MASOMO YA MISA, MARCHI 16, 2022: JUMATANO, JUMA LA 2 LA KWARESIMA

SOMO 1

Yer. 18-18-20

Waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yoyote.

Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili nisema mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 31:4-5, 13-15 (K) 16

(K) Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana.

Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,

Maana Wewe ndiwe ngome yangu.

Mikononi mwako naiweka roho yangu;

Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)

Maana nimesikia masingizio ya wengi;

Hofu ziko pande zote.

Waliposhauriana juu yangu,

Walifanya hila wauondoe uhai wangu. (K)

Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,

Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.

Nyakati zangu zimo mikononi mwako;

Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)

SHANGILIO

Lk. 8:15

Heri wale walishikao neno la Mungu katika moyo wao mwema na unyofu, na wazaao matunda katika uvumilivu.

INJILI

Mt. 20:17-28

Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.

Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza. Akawaambia, Hakika mtakinywa kikombe change; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.

Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, APRILI 2, 2022: JUMAMOSI: JUMA LA 4 LA KWARESIMA

SOMO 1

 

Yer. 11:18-20

 

Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao. Lakini mimi nalikuwa kama mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa; wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.

Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Bwana.

 

WIMBO WA KATIKATI

 

Zab. 7:1-2, 8-12 (K) 1

 

(K) Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe.

 

Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe,

Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.

Asije akaipapura nafsi yangu kama samba,

Akiivunja-vunja pasipokuwa na wa kuponya. (K)

 

Bwana, unihukumu mimi,

Kwa kadiri ya haki yangu,

Sawasawa na unyofu nilio nao.

Ubaya wao wasio haki na ukome,

Lakini umthibitishe mwenye haki. (K)

 

Ngao yangu ina Mungu,

Awaokoaye wanyofu wa moyo.

Mungu ni mwamuzi mwenye haki,

Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku. (K)

 

SHANGILIO

 

Lk. 15:18

 

Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.

 

INJILI

 

Yn. 7:40-52

 

Wengine katika mkutano walipoyasikia maneno ya Yesu, walisema, Hakika huyu ndiye nabii yule. Wengine walisema, Huyu ndiye Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya? Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi? Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao wakataka kumkamata, alkini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika.

Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, Mbona hamkumleta? Wale watumishi wakajibu, Hajanena kamwe mtu yeyote kama huyu anavyonena. Basi Mafarisayo wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika? Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo? Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa.

Akawaambia Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao), Je! Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo? Wakajibu, wakamwambia, Je! Wewe nawe umetoka Galilaya! Tafuta, ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JUMAPILI, AGOSTI 20, 2023: JUMA LA 20 LA MWAKA 

SOMO I

Isa. 56:1, 6-7

Bwana asema hivi, Shikeni hukumu, mkatenda haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.

Neno la Bwana…Tumshukuru Mungu

WIMBO WA KATIKATI 

Zab. 67:1-2, 4-5, 7 (K) 5

(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, 
Watu wote na wakushukuru.

Mungu na atufadhili na kutubariki,

na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulikane duniani,
wokovu wake katikati ya mataifa yote. (K)

mataifa na washangilia,

naam, waimbe kwa furaha.
Maana kwa haki utawahukumu watu,
na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)

watu na wakushukuru, Ee Mungu,

watu wote na wakushukuru.
Mungu atatubariki sisi;
miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)

SOMO 2

Rum. 11:13-15, 29-32

Nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa. Basi, naitukuza huduma iliyo yangu? Huenda nikapata kuwapatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao. Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa. Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake. Kwa maana kama ninyi zamani mlivyomwasi Mungu, lakini sasa mmepata rehema kwa kuasi kwao; kadhalika na hao wameasi sasa, ili kwa kupata rehema kwenu wao nao wapate rehema. Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote.

Neno la Bwana…Tumshukuru Mungu

SHANGILIO

Mdo. 16:14


Aleluya, aleluya,

Fungua mioyo yetu, Ee Bwana, 
Ili tuyatuze maneno ya Mwanao.
Aleluya

INJILI 

Mt. 15:21-28

Yesu aliondoka huko, akaenda kando pande za tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema, Bwana unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.

Neno la Bwana…Sifa kwako, ee Kristo

MASOMO YA MISA, MACHI 20, 2022: JUMAPILI YA 3 YA KWARESIMA

SOMO 1 – Kut. 3:1-8a, 13-15

Basi, Musa alikuwa akilichunga kunda la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu.Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali.Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n’nani? Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, Mimi niko ambaye niko, akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; Mimi niko amenituma kwenu. Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI – Zab. 103:1-4, 6-8, 11 (K) 8

(K) Bwana amejaa huruma na neema.Ee nafsi yangu umhimidi Bwana.Naam, vyote vilivyo ndani yanguVilihimidi jina lake takatifu.

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,Wala usizisahau fadhili zake zote.

(K)Akusamehe maovu yako yote,Akuponya magonywa yako yote,Aukomboa uhai wako na kaburi,Akutia taji ya fadhili na rehema.

(K)

Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki,Na hukumu kwa wote wanaoonewa.Alimjulisha Musa njia zake.Wana wa Israeli matendo yake. (K)

Bwana amejaa huruma na neema,Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao. (K)

SOMO 2 – 1 Kor. 10:1-6, 10-12

Ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe na Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani.Wala msinung’unike kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu.Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO – Zab. 95:8

Msifanye migumu mioyo yenu; Lakini msikie sauti yake Bwana.

INJILI – Lk. 13:1-9

Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha Yesu habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichangaya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia.Je! Mwadahni ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamb awao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JUNI 11, 2023: SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA BWANA WETU YESU KRISTU

SOMO 1

Kum. 8:2-3;14-16

Musa aliwaambia makutano: Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako, aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu, kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. Basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 147:12-15,19-20 (K) 12

(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;

Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.

Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,

Amewabariki wanao ndani yako. (K)

Ndiye afanyaye amani mipakani mwako,

Akushibishaye kwa unono wa ngano.

Huipeleka amri yake juu ya nchi,

Neno lake lapiga mbio sana. (K)

Humhubiri Yakobo neno lake,

Na Israeli amri zake na hukumu zake.

Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,

Wala hukumu zake hawakuzijua.

aleluya. (K)

SOMO 2

1Kor. 10:16-17

Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANG1LIO

Yn. 6:51

Aleluya, aleluya,

Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; asema Bwana; mtu akila chakula hiki, ataishi milele.

Aleluya.

INJILI

Yn. 6:51-58

Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MACHI 19, 2022: JUMAMOSI, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

SHEREHE YA MT. YOSEFU, MUME WA BIKIRA MARIA

SOMO 1

2Sam. 7: 4 – 5, 12 – 14, 16

Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema, Enenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, Bwana asema hivi, siku zako zitakapo timia, ukalala na Baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake.

Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu, akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 89:1 – 4, 26, 28 (K) 36(K)

Wazao wake watadumu milele.

Fadhili za Bwana nitaziimba milele;Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.

Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)

Nimefanya agano na mteule wangu,Nimemwapia Daudi, mtumishi wangu.Wazao wako nitawafanya imara milele,Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. (K)

Yeye ataniita, Wewe baba yangu,Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.

Hata milele nitamwekea fadhili zangu,Na agano langu litafanyika amini kwake. (K)

SOMO 2

Rum. 4:13, 16 – 18, 22

Ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa Imani. Kwa hiyo ilitoka katika Imani, iwe njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila kwa wale wa Imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote; (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ilia pate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO

Zab. 84:5

Heri wakaao nyumbani mwako, Ee Bwana.

INJILI

Mt. 1:16, 18 – 21, 24

Yakobo alimzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa yesu aitwaye Kristo.Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akimchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MACHI 30, 2022, JUMATANO: JUMA LA 4 LA KWARESIMA

SOMO 1

 

Isa. 49:8-15
Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni.
Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza. Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia kuu zangu zitatukuzwa zote.
Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya sinimu. Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, naye atawahurumia watu wake walioteswa.
Bali Sayuni alisema, Yehova ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

 

Zab. 145:8-9, 13-14, 17-18 (K)

(K) Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma.

Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.
Bwana ni mwema kwa watu wote,

Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. (K)
Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Ni mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinama chini. (K)

Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu. (K)

SHANGILIO

Mt. 4:4

Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

INJILI

Yn. 5:17-30
Yesu aliwajibu Wayahudi: Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. Basi kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu.
Basi Yesu akajibu, akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile. Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizi atamwonyesha ili ninyi mpate kustaajabu. Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana ahuisha wale awatakao. Tena Baba hamhukumu mtu yeyote, bali amempa Mwana hukumu yote, ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka.
Amin, amin, nawaambia, yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.
Maana kam avile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake. Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo; kwa maana sasa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu. Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About