Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Madhara ya nyama nyekundu kwa mtu mwenye VVU

Kuna nyama za aina mbili, nazo ni nyama nyeupe na nyama nyekundu.

Nyama nyeupe

Hizi ni nyama zitokanazo na samaki, kuku, ndege wa aina zote, bata, wadudu

Nyama nyekundu

Hutokana na ng’ombe, mbuzi, kondoo,nguruwe na wanyama wa porini.

Nyama ina virutubishi vingi muhimu kwa afya ya binadamu kama protini, vitamini na madini. Madini ya chuma yanayopatikana kwenye nyama ni rahisi sana kusharabiwa (kufyonzwa) mwilini na ni muhimu kwa kuongeza wekundu wa damu.
Uwezo wa miili ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kuyeyusha chakula na kusharabu (kufyonza) virutubishi hupungua. Utumiaji wa nyama nyekundu kwa wingi unaweza kuwaletea matatizo hasa katika uyeyushwaji tumboni kwani nyama nyekundu si rahisi kuyeyushwa ukilinganisha na nyama nyeupe.

Hata hivyo katika nchi yetu watu walio wengi wanatumia nyama kwa kiasi kidogo sana na mara chache. Si vyema watu hawa waache kabisa nyama nyekundu. Jambo la muhimu ni kutumia njia mbalimbali ili kuifanya nyama hii iyeyushwe kwa urahisi tumboni.

Namna ya kusaidia uyeyushwaji ni pamoja n a : –

• Kutafuna vizuri au kutumia nyama ya kusaga (kwa wanaoipata).
• Kupika nyama na viungo vinavyosaidia kulainisha kama vile papai bichi, limao, vitunguu saumu n.k.
• Kula nyama pamoja na papai

Kwa hiyo, kwa anayepata nyama nyekundu kwa wingi, kupunguza kiasi cha nyama hiyo na kuongeza kiasi cha nyama nyeupe. Na kwa yule asiyepata nyama nyeupe, apatapo nyama nyekundu asiache kutumia kwani ina umuhimu mwilini mwake.

Jinsi ya kuandaa Biriani Na Sosi Ya Nyama Ya Mbuzi

Mahitaji

Nyama Ya Mbuzi – 1 Kilo

Mchele – 4 Magi

Vitunguu – 3

Nyanya – 2

Nyanya kopo – 3 vijiko vya chai

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 2 vijiko vya supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Garam Masala (mchanganyiko wa bizari) – 2 vijiko vya supu

Hiliki – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta – ½ kikombe

Zaafarani au rangi za biriani za kijani na manjano/orenji

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Sosi Ya Nyama

Changanya nyama na thomu, pilipili, chumvi na nusu ya garam masala. Tia katika treya ya oveni uipike nyama (Bake) hadi iwive. Au iwivishe kwa kuichemsha.
Katika kisufuria kingine, tia mafuta (bakisha kidogo ya wali) kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi, kisha tia nyanya, nyanya kopo, bizari zote nyingine zilizobakia.

Namna Ya Kupika Wali

Mchele – 4 magi

Mdalasini – 1 kijiti

Hiliki – 3 chembe

Kidonge cha supu – 1

Chumvi

Osha na roweka mchele wa basmati.
Tia maji katika sufuria uweke jikoni. Tia kidonge cha supu, mdalasini, hiliki na chumvi .
Yakichemka maji tia mchele, funika upike hadi nusu kiini kisha uchuje kwa kumwaga maji.
Tia mafuta kidogo katika mchele na zaafarani iliyorowekwa au rangi za biriani kisha rudisha mchele katika sufuria ufunike na upike hadi uwive.
Pakua wali katika sahani kisha mwagia sosi ya nyama juu yake, pambia kwa kukatika nyanya, pilipili mboga na figili mwitu (Celery) au mboga yoyote upendayo.

Jinsi ya kupika Biskuti Ya Keki Kavu kwa kizungu Shortcake

Viamba upishi

Unga 2 Magi (vikombe vya chai)

Sukari iliyosagwa 2/3 Magi (kikombe cha chai)

Siagi   220 g

Unga wa mchele ½ Magi

Yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya vitu vyote hivyo kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.

2. Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30 cm au (8 in kwa 12 in)

3. Choma kwenye moto 325˚C kwa muda wa saa nzima au mpaka ibadilike kuwa rangi ya dhahabu.

4. Epua acha ipoe kisha kata vipande kama mstatili, weak kwenye sahani tayari kunywewa na chai.

Jinsi ya kuandaa Pilau ya sosi ya soya, nyama na mboga

Mahitaji

Nyama isiyokuwa na mifupa – 1 ½ Lb(ratili)
Mchele wa Basmati (rowanisha) – 3 Magi
Vitunguu maji – 2
Mchanganyiko wa mboga za barafu – 1 Magi
(karoti, mahindi, njegere)
Pilipili Mbichi – 3
Pilipili mboga kijani na nyekundu – 1
Pilipili manga – ½ kijiko cha chai
Chumvi – Kiasi
Sosi ya soya (soy sauce) – 5 Vijiko vya supu
Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 Kijiko cha supu
Mchanganyiko wa bizari (garam masala) – 1 Kijiko cha supu
Kotmiri iliyokatwa – ½ Kikombe
Mafuta ya kukaangia – Kiasi

Namna Ya Kutaarisha

Ndani ya sufuria, tia mafuta yakipata moto kaanga vitunguu mpaka ziwe rangi ya hudhurungi.
Kisha tia nyama iliyokatwa vipande vidogo vidogo pamoja na maji ya kiasi na viungo vyote isipokuwa mchele, mboga zote na kotmiri. chemsha mpaka nyama iwive na maji yakauke.
Halafu changanya na mboga na iwache kwa muda wa dakika kumi kisha tia kotmiri na umimine kwenye bakuli au treya ya oveni na uweke kando.
Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja, kisha umwagie juu ya ile treya ya nyama.
Nyunyizia mafuta na sosi ya soya na ipike katika oveni moto wa 350° kwa muda wa dakika 20 hivi.
Ukishawiva, uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Kidheri – Makande

Mahitaji

Nyama (kata vipande vidogodogo) – ½ kilo

Maharage – 3 vikombe

Mahindi – 2 vikombe

Kitunguu – 1

Nyanya – 2

Kabichi lililokatwa – 2 vikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha chai

Vidonge vya supu – 2

Chumvi – kiasi

Mafuta -1au 2 vijiko vya chakula

Namna Yakutayarisha

Chemsha mahindi mpaka yawive na maji yakauke kiasi.
Chemsha maharage pembeni nayo mpaka yawive na maji yakaukie kiasi.
Tia mafuta kwenye sufuria anza kukaanga vitunguu , thomu na vidonge vya supu koroga kiasi.
Kisha mimina nyama iliyokatwa vipande acha ikaangike kidogo na chumvi.
Nyama ikishakaangika tia nyanya funika kwa moto mdogo mpaka nyama iwive.
Kisha mimina mahindi na maharage yaliyochemshwa na maji yake kiasi koroga mpaka ichanganyike na mwisho mimina kabichi funikia mpaka kabichi iwive onja chumvi kama imekolea
Halafu malizia kukoroga mpaka ichanganyike na ikaukie kisha pakua kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Biriyani Ya Nyama Ng’ombe

Viambaupishi Vya Masala

Nyama vipande – 3 LB

Mtindi – ½ kopo

Kitunguu (thomu/galic) – 1½ kijiko cha supu

Tangawizi – 1½ kijiko cha supu

Nyanya – 2

Pilipili mbichi – kiasi

Nyanya kopo – 4 vijiko vya supu

Vidonge supu – 2

Pilipili nyekundu paprika – kiasi

Bizari zote saga – 2 vijiko vya supu

Viazi – 4

Mafuta – 2 mug

Samli – ½ kikombe

Vitungu – 6

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika masala

Kwenye sufuria tia nyama, saga nyanya na thomu, pilipili mbichi, tangawizi. Mimina kwenye nyama na mtindi, tia na nyanya kopo, bizari paprika, vidonge vya supu, chumvi kisha changanya vyote pamoja weka motoni.
Katika sufuria nyengine tia mafuta na samli kaanga vitungu mpaka viwe rangi ya hudhurungi toa weka pembeni.
Kanga viazi weka pembeni.
Chukua mafuta kidogo uliyokangia tia kwenye nyama acha katika moto wa kiasi mpaka nyama iwive na maji ya punguke.
Tia viazi na vitunguu vivunje vunje tia ndani ya nyama acha moto mdogo.

Vipimo Vya Wali

Mchele – 5 mug

Maji – kiasi

Chumvi – kiasi

Mafuta uliyokaanga vitungu – kiasi

Rangi ya biriani – ¼ kijiko cha chai

*Zafarani – ½ kijiko cha chai

*roweka rangi na zafarani

Namna Ya Kutarisha Na Kupika Wali

Osha mchele roweka muda wa saa.
Chemsha maji kama magi 10 hivi na chumvi tia mchele.
Uache uchemke ukishaiva kiini nusu, mwaga maji chuja.
Mimina juu ya nyama tia rangi na mafuta kwa juu funika.
Aacha kidogo katika oveni kwa muda wa dakika 20 hivi kisha epua ikiwa tayari.

Mapishi ya tambi za kukaanga

Kupika tambi ni kama ifuatavyo

VIAMBA UPISHI

Tambi pakti moja

Sukari ¾ kikombe cha chai

Mafuta ½ kikombe cha chai

Iliki kiasi

Maji 3 Vikombe vya chai

Vanilla / Arki rose 1-2 Tone

Zabibu Kiasi (Ukipenda)

JINSI YA KUPIKA TAMBI ZAKO

1. Zichambue tambi ziwe moja moja.

2. Mimina mafuta kwenye sufuria yakisha pata moto mimina
tambi,zigeuzegeuze mpaka zibadilike rangi na kuwa brown.

3. Punguza mafuta kwa kuyachuja na zirudishe jikoni.

4. Nyunyizia iliki zilizosagwa koroga kidogo na mimina maji na tia arki
na acha zichemke mpaka maji yakikaribia kukauka mimina sukari
koroga kidogo na punguza moto.
5. Kisha tia zabibu ukipenda, zifunike ili zikaukie vizuri.

6. Zikishakauka pakua kwenye sahani tayari kwa kuliwa

Kidokezi: Itategemea na aina za Tambi unazopika kwa kukisia maji, kama utaona hazijaiva unaweza kuongeza maji kidogo.

Namna ya kupika Vitumbua

Vitumbua ni aina ya vitafunwa vya chai ambavyo hutengenezwa kwa kutumia unga wa mchele. Kiasili vitumbua ni chakula ambacho hupendelewa sana na watu wa pwani. Na mara nyingi wamekuwa wakipika kwa kuchanganya na nazi ili kuvifanya view na ladha nzuri zaidi

Mahitaji:

Unga wa mchele ½ kg
Sukari vijiko 4 vya mezani
Tui bubu la nazi
Mafuta ya kupikia
Unga wa hiliki ½ kijiko cha chai
Hamira kijiko 1 cha chai
Chuma cha vitumbua

Maandalizi:

Chukua unga wa mchele na weka kwenye bakuli au sufuria ya kilo moja
Weka hamira kisha weka sukari kisha miminia tui katika mchanganyiko wako
Weka hiliki koroga hadi view uji mzito
Acha uji huo kwa muda wa saa moja hadi uumuke, mara nyingi kuumuka kunategemea na hali ya hewa,
Baada ya hapo weka mafuta kijiko kimoja cha chakula kila kishimo acha yapate moto Kisha kaanga virumbua vyako

Madhara ya kula yai bichi

Yai bichi linaweza kuwa na vijidudu viitwavyo kwa kitaalamu “SALMONELLA” vinavyoweza kusababisha tumbo kuuma, kichefuchefu na pia kuharisha.
Vijidudu ya “Salmonella” vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa watoto, wazee na wale wenye hali dhaifu ya kimwili kama wagonjwa wa UKIMWI.

Pia yai bichi lililowazi linaweza kuwa zalio zuri la vimelea vya maradhi mbalimbali. Inashauriwa kupika yai mpaka liive kabisa, na kuhakikisha kwamba hakuna ute unaoteleza.

Kama ni yai la kuchemsha, lichemshwe kwa dakika kumi zaidi baada ya maji kuchemka. Pia ni muhimu kuhakikisha kwamba vyombo vilivyotumika k u k o rogea yai bichi vinaoshwa kwa maji na sabuni kabla ya kuvitumia tena kwa matumizi mengine ili kuepuka maradhi.

Jinsi ya kuandaa Ndizi Mbichi Za Supu Ya Nyama Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi mbichi – Kisia

Nyama ng’ombe – ½ kilo

Pilipili ya kusaga – 1 kijiko cha chai

Tangawizi ya kusaga – 2 vijiko vya supu

Thomu (garlic/saumu) – 1 kijiko cha supu

Bizari mchuzi – 1 kijiko cha chai

Nazi ya unga (ukipenda kuongezea) – 2 vijiko cha supu

Chumvi – Kiasi

Ndimu – 1 kamua

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama ng’ombe katika sufuria, tia tangawizi, thomu, pilipili mbichi, bizari, chumvi. Roweka kidogo ukipenda kisha ikaushe yenyewe kwa maji yake
Ongezea maji ya kiasi yasizidi mno, kisha funika na chemsha.
Menya ndizi, ukatekate.
Nyama ikikaribia kuiva, weka ndizi uendelee kupika mpaka viive vyote.
Tia nazi ya unga kidogo tu ukipenda. Koleza kwa bizari mchuzi, pilipili, na ndimu
Epua mimina katika chombo cha kupakulia zikiwa tayari.

Mapishi ya Wali, samaki, bilinganya na spinach

Mahitaji

Samaki
Spinach
Bilinganya
Nyanya ya kopo (Kopo 1)
Vitunguu maji
Vitunguu swaumu
Tangawizi
Pilipli mbuzi
Chumvi
Limao
Carry powder
Mchele
Mafuta ya kupikia
Coriander
Hiliki
Amdalasini
Karafuu

Matayarisho

Osha samaki na kisha wamarinate na vitunguu swaumu, tangawizi, limao, chumvi na pilipili kwa muda wa masaa matatu. Baada ya hapo wakaange samaki na uwaweke pembeni kwa ajili ya mchuzi.
Osha spinach na kisha zikatekate na ziweke pembeni
Osha mchele na kisha uloweke kwenye maji kwa muda wa dakika kumi
Osha bilinganya kisha likatekate vipande vidogo dogo

Jinsi ya kupika

Mchuzi

Saga pamoja vitunguu maji, vitunguu saumu, tangawizi, nyanya.Kisha weka mchanganya katika sufuria na uinjike jikoni kwenye moto wa kawaida. Pika mchanganyiko mpaka ukauke kisha tia mafuta, chumvi na carry powder. pika kwa muda wa dakika kumi kisha tia samaki na tui la nazi. Acha mchuzi uchemke mpaka tui la nazi liive.kishaipua na tia coriander

Spinach

Kaanga vitunguu maji na mafuta, baada ya hapo tia spinach na chumvi acha ziive kidogo kisha ipua tayari kwa kuliwa.

Mabilinganya

Kaanga vitunguu maji na mafuta mpaka viwe vya brown kisha tia nyanya. Acha ziive kisha tiai mabilinganya na chumvi. Yakishaiva ipua weka pembeni tayari kwa kuliwa.

Wali

Chemsha maji ya wali kwenye sufuria, kisha tia hiliki, pilipili mtama mzima, karafuu na amdalasini, chumvi na mafuta. Kisha tia mchele na uufunike na uache uchemke mpaka utakapokauka maji. Geuza na uache mpaka uive. Kisha ipua. Tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Mitai

VIAMBAUPISHI

Unga wa ngano – magi 2 (vikombe vikubwa)

Hamira kijiko 1 cha chai

Sukari Vijiko 2 vya supu

Maziwa ¾ Magi

Siagi Vijiko 2 vya supu

Mafuta ya kukaangia kiasi

VIAMBAUPISHI:SHIRA

Sukari ¾ Kikombe

Maji ¾ Kikombe

Illiki ya unga kiasi

Zafarani kiasi

JINSI YA KUPIKA

Katika bakuli, changanya vipimo vyote pamoja na ukande unga usiwe mgumu wala laini sana uwe kiasi.
Kisha fanya donge moja na iache pahali penye joto mpaka iimuke.
Halafu weka mafuta ya kukaangia kwenye moto.
Sukuma donge hadi liwe duara sio nyembamba sana, kisha katakata kama maandazi.
Mafuta ya kisha pata moto choma mittai hukuunazigeuza hadi ziwive na kugeuka rangi.
Katika sufuria tia vipimo vya shira na iache ichemke isiwe nzito sana.
Mimina mitai kwenye shira na uzipepete, kisha weka kwenye sahani na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Biskuti Za Kuchoveya Chokoleti

Viambaupishi

Unga 300gm

Siagi 225gm

Icing Sugar 60gm

Chokoleti iliyokoza (Dark Chocolate) 225gm

Vanilla 2 kijiko cha chai

Yai 1

Baking Powder ½ kijiko cha chai

Njugu za vipande ½ kikombe cha chai

Njugu zilizosagwa ¼ kikombe cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Piga sukari na siagi katika mashine ya keki mpaka iwe laini

2. Kisha mimina yai na vanilla koroga vizuri

3. Mwisho mimina unga na baking powder polepole mpaka ichanganyike.

4. Kata kata umbo (shape) lolote unavyopenda (kama nyota, pembetatu,duara, kopa n.k)

5. Panga kwenye treya na choma kwa moto wa 350°C , vikibadilika rangi kidogo tu vitoe

6. Yayusha chokoleti tia kwenye bakuli ndogo.

7. kisha paka kwa kijiko au chovyea upande mmoja mmoja wa biskuti kisha nyunyizia njugu za kipande na njugu ya unga.

8. Panga kwenye sahani tiyari kunywewa na chai ya maziwa au kahawa.

Mapishi ya Sponge keki

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) 100g
Sukari (sugar) 100g
Siagi isiyokuwa na chumvi (unsalted butter) 100g
Mayai (eggs) 2
Vanila 1 kijiko cha chai
Chumvi pinch
Warm water 3 vijiko vya chakula

Matayarisho

Kwanza washa oven moto wa 200 C. Baada ya hapo saga butter na sukari mpaka viwe laini kisha tia mayai na uendelee kusaga mpaka vichanganyike vizuri kisha tia unga, vanila, chumvi na na maji na usage mpaka upate uji usiokuwa mzito sana au mwepesi sana. Baada ya hapo utie kwenye baking tin na u bake kwa muda wa dakika 25 na mpaka cake yako iive yani juu na chini iwe ya brown na ukidumbukiza kijiti katikati kinatoka kikiwa clean. Baada ya hapo itoe kwenye tin na uiache ipoe. Ikisha poa itakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Bisikuti Za Kaukau Na Kahawa (Cocoa Coffee Biscuits)

MAHITAJI

Maji baridi – kikombe 1

Biskuti za kawaida – paketi 2

Kaukau (cocoa) – vijiko 3 vya kulia

Kahawa ya unga – kijiko 1 cha kulia

Njugu mchanganyiko zilokatwakatwa – kikombe 1

Sukari – kiasi upendavyo

MAANDALIZI

Changanya maji na kaukau na kofi na sukari
Katakata biskuti kisha tia paketi moja na nusu uchanganye vizuri.
Kisha nusu ya biskuti zilobakia katakata vipande vikubwa na weka juu ya mchanganyiko, kisha changanya kidogo tu.
Weka katika foil paper na zungusha (roll)
Kisha fungua umwagie njugu au mkassaraat zilosagwa
Kisha roll katika foil paper na uweke katika freezer mpaka igande
Kisha kata kata slices na iko tayari

Mawazo ya Chakula cha Mchana cha Dakika 20 kwa Siku zenye Shughuli Nyingi

Mawazo ya Chakula cha Mchana cha Dakika 20 kwa Siku zenye Shughuli Nyingi

Leo, nataka kuzungumzia kuhusu mawazo ya chakula cha mchana cha dakika 20 kwa siku zenye shughuli nyingi. Kama AckySHINE, ninaelewa jinsi wakati unavyoweza kuwa mdogo sana wakati wa mchana, hasa ikiwa una shughuli nyingi za kufanya. Lakini hii haimaanishi kuwa unapaswa kusahau kuhusu lishe bora na kupendeza kwenye chakula chako cha mchana. Hapa nitakupa mawazo kadhaa ya chakula cha mchana cha dakika 20 ambacho kitakufanya uhisi kuridhika na kuwa na nguvu kwa shughuli zako zote.

  1. 🥗 Saladi yenye afya: Andaa saladi yenye mboga mbalimbali kama vile letusi, nyanya, pilipili, karoti, na matango. Ongeza kuku wa kuchoma uliyebaki kutoka kwenye chakula cha jioni cha jana ili kuongeza protini. Pamba na vijiko vichache vya dressing ya saladi.

  2. 🍲 Supu ya mboga: Pika supu ya mboga kwa kutumia mboga uliyopenda kama vile karoti, viazi, na kabichi. Ongeza viungo kama vile vitunguu, nyanya, na pilipili kwa ladha zaidi. Supu ya mboga ni njia nzuri ya kupata virutubisho vyote muhimu kwa haraka.

  3. 🍱 Sushi ya kujitengenezea: Andaa sushi ya kujitengenezea kwa kutumia mchele uliopikwa, tangawizi, na mchuzi wa soya. Weka mboga ulizopenda kama vile karoti, matango, au avokado kwenye sushi yako. Hii ni chaguo nzuri kwa watu ambao wanapenda vyakula vya Kijapani.

  4. 🥪 Sandwich ya kujitengenezea: Tengeneza sandwich yako mwenyewe kwa kutumia mkate kamili, nyama ya kukaanga, na mboga kama vile lettuce na nyanya. Unaweza pia kuongeza viungo vingine kama vile mayonnaise au mchuzi wa haradali kwa ladha zaidi.

  5. 🍛 Nafaka na mboga: Pika nafaka ya haraka kama vile quinoa au mchele mweupe. Ongeza mboga uliyopenda kama vile maharage ya kijani, karoti, au pilipili. Hii ni chaguo nzuri kwa watu ambao wanapenda chakula cha kitamu na cha kusitawisha.

  6. 🍝 Pasta isiyo na nyama: Pika pasta isiyo na nyama kwa kutumia spageti au tagliatelle. Ongeza mboga kama vile broccoli, nyanya, na vitunguu kwa ladha zaidi. Pamba na mchuzi wa nyanya na viungo vingine kama vile bizari au pilipili kwa ladha zaidi.

  7. 🌮 Tacos za mboga: Tengeneza tacos za mboga kwa kutumia nyanya, pilipili, na vitunguu vilivyosonga. Ongeza mboga uliyopenda kama vile avokado au maharage. Pamba na mchuzi wa guacamole na juisi ya limao kwa ladha zaidi.

  8. 🥦 Stir-fry ya mboga: Pika stir-fry ya mboga kwa kutumia mboga kama vile kabichi, karoti, na pilipili. Ongeza viungo kama vile vitunguu na tangawizi kwa ladha zaidi. Pamba na mchuzi wa soya na kitunguu saumu kwa ladha zaidi.

  9. 🍠 Mkate wa viazi: Pika viazi vitamu na utumie kama mkate badala ya mkate wa kawaida. Ongeza nyama ya kukaanga au mboga kama vile avocado na nyanya kwenye mkate wako wa viazi. Hii ni chaguo nzuri kwa watu ambao wanataka chakula cha mchana chenye afya na ladha ya kipekee.

  10. 🍲 Chapati ya mboga: Pika chapati ya mboga kwa kutumia unga wa ngano, mboga iliyosagwa, na viungo kama vile pilipili na kitunguu. Tumia chapati hizi kama msingi wa sahani yako ya mboga kwa ladha na mlo kamili.

  11. 🥕 Mchanganyiko wa mboga: Kata mboga uliyopenda kama vile karoti, pilipili, na vitunguu katika vipande vidogo. Changanya na mchuzi wa soya au mchuzi mwingine wa ladha na pika kwa muda mfupi. Tumia mchanganyiko huu kama msingi wa sahani yako ya mboga.

  12. 🌯 Burrito ya mboga: Tengeneza burrito ya mboga kwa kutumia tortilla, mboga uliyosonga, na mchuzi wa nyanya. Ongeza viungo vingine kama vile pilipili na tangawizi kwa ladha zaidi. Hii ni chaguo nzuri kwa watu ambao wanapenda vyakula vya Mexiko.

  13. 🥣 Mchuzi wa maharage: Pika mchuzi wa maharage kwa kutumia maharage ya kijani na viungo kama vile vitunguu na nyanya. Tumia mchuzi huu kama msingi wa chakula chako cha mchana kwa ladha na lishe.

  14. 🥦 Saladi ya kijani: Tengeneza saladi ya kijani kwa kutumia mboga mbalimbali za majani kama vile spinachi, kale, na letusi. Ongeza viungo kama vile avokado, quinoa, na karanga kwa ladha zaidi. Pamba na mchuzi wa limao na mafuta ya zeituni kwa ladha zaidi.

  15. 🍱 Bento ya mboga: Andaa bento ya mboga kwa kuweka mboga mbalimbali kama vile nyanya, karoti, na kabichi kwenye sehemu tofauti za sanduku la chakula. Ongeza protini kama tofu au tempeh kwa ladha zaidi. Pamba na mchuzi wa soya au mchuzi mwingine wa ladha kwa ladha zaidi.

Hizi ni baadhi tu ya mawazo ya chakula cha mchana cha dakika 20 kwa siku zenye shughuli nyingi. Kumbuka kuwa unaweza kubadilisha viungo au kuongeza viungo vyovyote unavyopenda ili kufanya chakula chako cha mchana kiwe cha kipekee na chenye ladha. Hakikisha unazingatia lishe na kula chakula kilichojaa virutubisho ili uwe na nguvu na kufanya vizuri siku nzima. Je, una mawazo yoyote mengine ya chakula cha mchana cha dakika 20? Nipatie maoni yako!

Mapishi ya Pilau Ya Nyama Ng’ombe Karoti Na Zabibu

Vipimo – Nyama

Nyama ng’ombe ya mifupa ilokatwa vipande – 1 kilo

Tangawizi na thomu (somu/garlic) ilosagwa – 2 vijiko vya supu

Bizari mchanganyiko/garama masala – 1 kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Vipimo – Wali

Mchele – 4 glass

Mbatata/viazi menya katakata – 3 kubwa

Vitunguu katakata – 5

Kitunguu thomu kilosagwa (garlic/somu) – 1 kijiko cha supu

Hiliki ya unga – 1 kijiko cha chai

Bizari nzima ya pilau/cumin – 1 mti

Samli au mafuta – 2 Vijiko vya supu

Karoti zilokatwakatwa nyembamba – 6-7

Zabibu – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katika sufuria weka mafuta kijiko kimoja cha supu tia nyama na viungo vyake.
kaushe katika moto hadi ikaribie kukauka kisha tia maji kiasi cha kuivisha na kubakisha supu ya mchele.
Katika sufuria ya kupikia weka samli au mafuta ishike moto.
Tia mbatata/viazi kaanga, tia vitunguu kaanga kidogo.
Tia kitunguu thomu, hiliki, bizari ya pilau endelea kukaanga hadi viwe rangi ya brown kidogo.
Tia mchele kaanga kidogo, kisha mimina nyama na supu yake. Funika wali uwive.
Weka kikaangio katika moto, tia samli kijiko kimoja kisha tia karoti na zabibu, kaanga kwa sekunde chache tu kwa ajili ya kulainisha karoti na zabibu.
Utakapopakuwa wali, pambia juu karoti na zabibu.

LISHE BORA KWA WATU WENYE AFYA NZURI

• Kula chakula bora kunamaanisha kula vyakula aina tofauti ya vyakula kila siku kama vile matunda, mboga, maziwa na aina ya vyakula vyenye asili ya nyama wa kufuga kama kuku, mbuzi, ngombe, samaki na na vyakula vya nafaka.

• Lishe bora linamaanisha pia kula chakula ambacho hakina mafuta mengi, sukari au chumvi nyingi

• Zingatia angalau vyakula vya nafaka kama vile mtama, mahindi, mchele, ngano, wimbi, ndegu, njegere. n.k

• Ni bora kula matunda mengi kama ‘maembe, ndizimbivu, papai, pera, chungwa, ubuyu, nanasi, pesheni, zambarau” na mbogamboga kama vile “mchicha, majani ya mboga, karoti, nyanya chungu, nyanya, mkunde, biringanya” mara tano kwa siku.

• Kama mboga na matunda hazipatikani ni bora kununua zile ambazo zimehifadhiwa tayari kwenye mikebe au zile ziko kwenye jokofu (friji).

• Punguza kula vyakula ambavyo vinapikwa kwa mafuta mengi na chumvi nyingi

• Lishe bora hukusaidia wewe na jamii yako kuishi vyema, kuwa na afya bora, kufanya kazi vizuri na kwa bidii, shuleni na hata kucheza.

Mapishi ya Mihogo ya nazi na kuku

Mahitaji

Mihogo kilo 1
Kidali cha kuku 1 kikubwa
Nyanya 1 kubwa
Kitunguu maji 1 cha wastani
Swaum/tangawizi i kijiko cha chai
Nazi kopo 1
curry powder 1 kijiko cha chai
Binzari manjano 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/2
Pilipili 1
Chumvi kiasi

Matayarisho

Saga pamoja nyanya, kitunguu na swaum/ginger pamoja na vimaji kidogo. Kisha vitie kwenye sufuria isiyoshika chini na uvishemshe mpaka maji yote yakauke kisha tia mafuta na upike ktk moto mdogo mpaka viive.Baada ya hapo tia spice na uzipike kidogo kisha tia mihogo na kuku (kuku na mihogo vikatwe vipande vya wastani) vichanganye vizuri kisha tia nazi na vimaji kiasi,limao chumvi na pilipili na ufunike kisha punguza moto. Pika mpaka mihogo na kuku viive na ibaki rojo kidogo kisha ipua na mihogo yako itakuwa tayari kwa kuliwa

MAPISHI YA LADU

VIAMBAUPISHI

Unga – 6 vikombe

Samli – ½kikombe

Baking Powder – ½kijiko cha chai

Maziwa- 1 kikombe

Maji -Kisia kiasi kama unga bado mzito

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 5 vikombe

Maji – 2 1/2 vikombe

Vanilla – 2 vijiko vya chai

Rangi ya orange – 1 kijiko cha chai

Iliki ya unga – 1 Kijiko cha chai

MAANDALIZI

Changanya unga wa dengu, samli, baking powder pamoja na maziwa katika mashine ya keki (cake mixer).
Ukisha changanya angalia kama mchanganyiko wako umekua mwepesi kidogo kuliko wa keki, kama bado mzito basi ongeza maji kiasi.
Kisha weka mafuta kiasi kwenye karai,weka na samli kikombe kimoja, weka kwenye moto wa kiasi.
Mafuta yakisha pata moto, chukua kijiko kikubwa cha matundu chota mchanganyiko wako na kijiko cha kawaida tia kwenye kijiko cha matundu. Hakikisha kijiko cha matundu kiwe juu ya karai ili mchanganyiko wako uchuruzike ndani ya mafuta yalio pata moto.
Pika ndani ya mafuta mpaka iwive, ila usiache ikawa brown.
Toa mchanganyiko ulowiva tia ndani ya shira uliyo pika. Hakikisha shira iwe imepoa kabla ya kutia mchanganyiko huo.
Endelea kupika mchanganyiko wako mpaka uishe, kila ukitoa katika mafuta hakikisha unatia ndani ya shira.
Ukishamaliza wote kanda huo mchanganyiko ulokua ndani ya shira mpaka uone shira yote imekauka (yaani iwe imeingia ndani ya mchanganyiko).
Tupia zabibu kavu na lozi zilizo katwa, changanya na mkono.
Wacha mchanganyiko katika bakuli, funika na foil mpaka siku ya pili.
Siku ya pili chukua mchanganyiko kiasi katika mkono tengeneza mviringo (round).

MAANDALIZI YA SHIRA

Katika sufuria, tia sukari, maji, iliki, vanilla na rangi.
weka kwenye moto wacha ichemke mpaka itowe povu (bubbles) juu.
Kisha toa povu, wacha shira kwenye moto kama dakika 3.
Hakikisha shira yako iwe inanata kiasi kwenye vidole, lakini iwe nyepesi kidogo kuliko shira ya kaimati.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About