Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Jinsi ya kutengeneza Pilau Ya Kuku

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 vikombe

Kuku – ½

Viazi – 4

Vitunguu – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 2 vijiko vya supu

Binzari ya pilau nzima – 1 Kijiko cha chakula

Binzari ya pilau – ½ kijiko cha chai

Pilipili manga nzima – ½ kijiko cha chai

Karafuu nzima – 8

Iliki nzima – 6

Mdalasini nzima – 5 vijiti

Pilipili mbichi iliyosagwa – 2

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kupikia – ¼ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika:

Osha mchele na roweka kwa muda kutegemea na aina ya mchele.
Kata kuku vipande upendavyo, safisha kisha mchemshe kwa chumvi, pilipili iliyosagwa, thomu na tangawizi.
Akiwiva kuku, mtoe weka kando, bakisha supu katika sufuria.
Katika sufuria, kaanga vitunguu hadi vigeuke rangu ya hudhurungi.
Tia thomu na tangawizi na binzari zote kaanga kidogo
Kisha tia viazi kanga kidogo kisha tia kisha tia vipande vyako vya kuku na supu acha ichemke kidogo kisha tia maji ukisie kutokana na mchele unaotumia.
Mwisho tia mchele koroga uchanganye na vitu vyote acha ichemke kiasi kisha funika na punguza moto mpaka uive (huku ukiugeuzageuza)
Ukishakuwa tayari pakua kwenye sahani tayari kwa kula na salad na pilipili.

Jinsi ya kupika Mitai

VIAMBAUPISHI

Unga wa ngano 1 1/2 Kikombe

Baking powder 1 Kijiko cha chai

Baking soda ¼ Kijiko cha chai

Chumvi ½ kijiko cha chai

Sukari 1 kijiko cha supu

Hamira 1/2 Kijiko cha supu

Yai 1

Maziwa ½ Kikombe

Mafuta ya kukaangia

VIAMBAUPISHI:SHIRA

Sukari 1 Kikombe

Maji ½ Kikombe

Iliki au Mdalasini ¼ kijiko cha chai (ya unga)

MAANDALIZI NA JINSI YA KUPIKA

1. Kwenye bakuli, changanya pamoja unga, baking powder, baking soda, chumvi, sukari na hamira.

2. Katika kibakuli, piga mayai na maziwa pamoja.

3. Changanya mchanganyiko wa mayai na wa unga ; na ukande kama unga wa maandazi.

4. Ikisha fura, sukuma unga kama wa maandazi na ukate mitai .

5. Pasha moto mafuta na uchome hadi iwe rangi ya dhahabu, upande zote mbili.

6. Ipikie shira lakini isiwe nzito .

7. Tia mitai na upepete hadi sukari ienee kote na zitakuwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Wali Wa Kichina Wa Kamba Na Kuku

MAHITAJI

Mchele wa pishori (basmati) – 4

Nyama ya kuku bila mafupa – 1 Lb

Kamba saizi kubwa – 1Lb

Mchanganyiko wa mboga – njegere, karoti,

mahindi, maharage ya kijani (spring beans) – 2 vikombe

Figili mwitu (Cellery) – 2 mche

Vitunguu vya majani (spring onions) – 4-5 miche

Kebeji – 2 vikombe

Pilipili ya unga nyekundu – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ya unga – 1 kijiko cha chai

Sosi ya soya – 3 vijiko vya supu

Mafuta – 1/4 kikombe

Chumvi – kiasi

MAPISHI

Osha na roweka mchele.
Tia kamba chumvi na pilipili nyekundu ya unga. Tia mafuta vijiko viwili katika kikaango (frying pan), kaanga kamba kidogo tu, weka kando.
Katakata kuku vipande vidogo vidogo, tia chumvi na pilipili manga. Kaanga kaTika kikaango (ongeza mafuta kidogo) Weka kando.
Katika karai, tia mafuta kidogo kama vijiko vitatu vya supu, tia kamba na kuku, tia mboga za mchanganyiko, sosi ya soya na chumvi, kaanga kidogo. (Kama mboga sio za barafu) itabidi uchemshe kidogo.
Katakata kebeji, figili mwitu (cellery) na vitunguu vya majani (spring onions) utie katika mchaganyiko. acha kwa muda wa chini ya dakika moja katika moto.
Chemsha mchele, tia mafuta kidogo au siagi, chumvi upikie uive nusu kiini, mwaga maji uchuje.
Changanya vyote na wali rudisha katika sufuria au bakuli la oveni, funika na upike kwa moto wa kiasi kwa muda wa dakika 15-20 takriban.
Epua na upakue katika sahani ukiwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Samaki wa kuokwa

Mahitaji

Mackerel 2
Kitunguu swaum na tangawizi (ginger and garlic paste) 1 kijiko cha cha kula
Pilipili iliyo katwakatwa (chopped scotch bonnet ) 1/2
Limao (lemon) 1/2
Chumvi (salt) kiasi
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Coriander powder 1/2 kijiko cha chai
Mafuta 1 kijiko cha chai

Matayarisho

Safisha samaki kisha wakaushe maji ( ukipenda unaweza kuwakata kati au ukawapika wazima) Baada ya hapo wakate mistari kila upande ( ili spaces ziweze kuingia ndani) kisha waweke kwenye bakuli na utie spice zote. Wachanganye vizuri kisha waweke frijini na uwaache wamarinate kwa muda wa masaa 3. Baada ya hapo washa oven kisha wapakaze mafuta na uwafunge kwenye foil na uwatie kwenye oven kwa muda wa dakika 20. Baada ya hapo fungua foil na uwaache kwenye oven kwa muda wa dakika 10 ili wapate kukauka kidogo. Na hapo watakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuwala kwa kitu chochote upendacho.

Mapishi ya Wali maharage,mchuzi wa samaki na spinach

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Maharage yaliyochemshwa (boiled red kidney beans 1 kikombe cha chai)
Samaki waliokaangwa ( 2 fried fish)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2 ya tin)
Vitunguu vilivyokatwa (onion 2)
Kitunguu swaum (garlic 3 cloves)
Tangawizi (ginger kiasi)
Limao (lemon 1/2)
Chumvi (salt)
Pilipili (scotch bonnet pepper 2)
Mafuta (vegetable oil)
Spinach
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)

Matayarisho

Saga nyanya, kitunguu, tangawizi na kitunguu swaum pamoja. Tia kwenye sufuria na upike mpaka maji yakauke kisha tia curry powder, mafuta na chumvi na upike tena mpaka mchanganyiko uive kisha tia samaki na limao na maji kiasi na uache uchemke kiasi. Na hapo mchizi utakuwa tayari.
Osha na uzikate spinach kisha kaanga kitunguu na mafuta kiasi (hakikisha visiwe vya brown kisha tia spinach na chumvi. zipike kwa muda wa dakika 3-4 na hapo zitakuwa tayari zimeshaiva.
Wali: Chemsha maji kiasi kisha tia, chumvi, pilipili nzima(isikatwe) mafuta na tui la nazi. Baada ya hapo koroga na utie mchele na maharage na ufunike uache uchemke mpaka maji yakauke. Kisha geuza na ufunike tena na uuache mpaka uive. Baada ya hapo chakula chako kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Namna ya kutengeneza Visheti Vya Nazi Na Njugu (Sudani)

VIAMBAUPISHI

Unga – 3 mug za chai

Samli – ½ mug ya chai

Maziwa – 1¼ mug ya chai

Baking powder – 2 vijiko vya chai

VIAMBAUPISHI VYA MJAZO

Njugu zilizomenywa vipande vipande – 2 vikombe cha chai

Sukari – ½ kikombe cha chai

Iliki – 1 kijiko cha chai

Nazi iliyokunwa – 2 vikombe vya chai

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 vikombe vya chai

Maji – 1 kikombe cha chai

Ndimu – 1

JINSI YA KUVIANDAA

1-Changanya unga na samli kisha tia baking powder na maziwa. Ukande ulainike kisha

uwache kama dakika 5 uumuke.

2-Kwenye bakuli nyingine changanya njugu, sukari na iliki.

3-Kata madonge madogo dogo sukuma kila donge duara jembamba, kisha tia kijiko cha mchanganyiko wa njugu juu yake ifunikie juu yake na ibane pembeni.

4-Panga kwenye treya isiyoganda (non stick) kisha choma kwenye oven kwa moto wa chini

(bake) 350° C kwa dakika kama 15-20.

5-Chemsha maji na sukari katika sufuria ndogo kisha tia ndimu acha ichemke mpaka inatenate unapoigusa.

6-Kwenye sahani ya chali mimina nazi iliyokunwa.

7-Vibiskuti vikiwa tayari vya motomoto chovea kwenye shira kisha zungushia katika nazi iliyokunwa,

panga kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Muhogo Wa Nazi Na Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Muhogo – 3

Tui La Nazi – 2 vikombe

Chumvi – kiasi

Pilipili mbichi – 2

Mafuta – 1 kijiko moja

Kitunguu maji – 1 kidogo

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chambua muhogo ukatekate au tumia iliyo tayari.
Chemsha muhogo katika sufuria kwa maji kidogo na chumvi, funika uive muhogo.
Karibu na kukauka maji tia tui, kitunguu maji ulichokatakata na pilipili mbichi.
Unaupika moto mdogo mdogo hadi ukauke tayari kuliwa na samaki au kitoweo chochote kingine

Jinsi ya kupika Visheti Vya Kastadi Vya Shepu Ya Kombe

Viamba upishi

Unga wa ngano 1 Kilo

Siagi ¼ kilo

Mayai 2

Kastadi (custard) 3 vijiko vya supu

Baking powder 1 kijiko cha chai

Maziwa 1 ½ gilasi

Mafuta Ya kukaangia kiasi katika karai

Maandalizi na upikaji

Weka unga katika bakuli kubwa kisha changanya na unga wa kastadi na baking powder.
Tia siagi uchanganye vizuri.
Tia mayai, kisha maziwa ya baridi uchanganye vizuri usiukande sana.
Fanya madonge kisha kata vipande vidogovidogo kisha ubonyeze kwa kidole uvikwaruze kwenye chujio lenye tundu itokee shepu (design) yake.

5- Tia mafuta katika karai yakipata moto, kaanga visheti hadi viive. Usiache hadi vikageuka rangi sana.

6- Eupua, weka katika sufuria au chombo kikubwa kusubiri shira.

Vipimo Vya Shira

Sukari ½ kilo

Hiliki ilosagwa 1 kijiko cha chai

‘arki (rose flavor) 5 matone

Maji 1 gilasi

Namna Ya Kutyarisha

Changanya sukari na maji uipike hadi iwe nzito.
Ukiona mapovu yanatoka tia hilik na ‘arki .
Mwagia katika visheti uchanganye vizuri hadi vishike na sukari.

Jinsi ya kupika Biskuti Nyembamba (Wafer Bar) Za Chokoleti Na Njugu

MAHITAJI

Wafer Powder/gram wafer (unga wa biskuti uliosagwa wa tayari) – vikombe 2

Maziwa ya Mgando Matamu ya Kopo – 2 vikombe

Nazi iliyokunwa – ½ Kikombe

Chokoleti vipande vipande – 1 Kikombe

Njugu vipande vipande – ½ Kikombe

Siagi – 227 g

MAPISHI

Yeyusha siagi motoni kisha changanya na unga wa wafer acha kidogo motoni
Mimina katika treya unayochomea itandaze vizuri, kisha mimina maziwa juu yake pamoja na njugu vipande , nazi iliyokunwa na vipande vya chokoleti.
Choma (bake) kwenye oveni kwa moto wa 350ºC kwa dakika 20.
Katakata tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Nazi Wa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia, Mboga Ya Matembele Na Samaki Wa Kukaanga

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4

Maji – 6 kiasi kutegemea na aina ya unga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka maji katika moto.

Tia unga kidogo katika kibakuli, koroga ufanye uji.

Maji yakichemka tia kwenye maji uwe uji.

Ujii ikiiva punguza kidogo tia unga kidogokidogo na usonge ugali. Ikiwa unga ni mgumu utaongeza maji ya ule uji ulopunguza usonge hadi uive ukiwa tayari.

Vipimo Vya Mchuzi Wa Nazi Kwa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia

Nyanya chungu/mshumaa/Ngogwe – 7

Bamia – 10

Kitunguu maji – 2

Nyanya/tungule – 2

Tui la nazi jepesi – 2 viwili

Tui la nazi zito – 2

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 mbili kamua

Bizari manjano/haldi/turmeric – ½ kijiko cha chai

Pilipili mbuzi – 3

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata kitunguu maji na nyanya vipande vidogodogo sana kisha weka katika sufuria.

Iache ichemke kwa maji yake ya nyanya, ikishachemka tia maji kidogo kama robo kikombe.

Tia nyanya chungu, bamia na koleza ndimu, chumvi.

Iache ichemke. Inapokuwa tayari imeiva tia tui jepesi endelea kuacha katika moto huku unakoroga kidogo kidogo.

Tui jepesi likipungua kiasi chake, tia tui zito, kisha usiachie mkono koroga ikichemka kidog kiasi cha kuiva tui mchuzi tayari.

Vipimo Vya Mboga Ya Matembele

Matembele – 5 mafungu

Mafuta – ¼ kikombe

Kitunguu maji kilokatwakatwa – 1

Nyanya/tungule – 4

Chumvi – 1

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Punguza miche ya matembele kwa kuikata ncha kisha osha majani yake. Acha yachuje maji .
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji na nyanya hadi viivie.
Tia mboga, Iache ichemke kwa maji yake hadi iive. Ukiona bado haikuiva tia maji kidogo tu.
Ukipenda unatia ndimu kiasi cha kipande kimoja ukamue .

Samaki Wa Nguru Wa Kukaanga

Samaki Wa Nguru – 4 vipande

Kitunguu saumu(thom/galic) na tangawizi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi – 4

Ndimu – 2 kamua

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Mwoshe samaki kisha mtie kitunguu thomu, tangawizi ilosagwa, chumvi, pilipilimbichi ilosagwa, ndimu na bizari ya samaki.
Mwache akolee viungo kwa muda kidogo.
Makaange katika mafuta hadi aive akiwa tayari.

Mapishi ya wali wa hoho nyekundu

Mahitaji

Pilipili hoho (Red pepper 3)
Cougette 1
Kitunguu (onion 1)
Uyoga (mashroom 1 kikombe cha chai)
Carrot 1
Nyanya (fresh tomato 1)
Nyanya ya kopo iliyosagwa (tomato paste 3 vijiko vya chai)
Giligilani (fresh coriander)
Binzari manjano (Turmaric 1/2 ya kijiko cha chai)
Curry powder 1/2 ya kijiko cha chai
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Kata hoho kati na utoe moyo wake kisha ziweke pembeni, Kisha katakata cougette, kitunguu, uyoga, carrot, nyanya katika vipande vidogo vidogo, Weka sufuria jikoni na uanze kupika uyoga kwa muda wa dakika 5, kisha weka curry powder, turmaric na chumvi na kaanga kidogo kisha weka vegetable zilizobakia pamoja na nyanya ya kusaga pamoja na giligilani. Zikaange kwa muda wa dakika 5 kisha zitie kwenye hoho na kisha uzibake kwa muda wa dakika 20 na hapo zitakuwa tayari kuseviwa na wali.
Wali: angalia katika recipe zilizopita

Jinsi ya kupika Wali Wa Sosi Ya Tuna

Viambaupishi

Sosi Ya tuna

Tuna (samaki/jodari) 2 Vikopo

Vitunguu (kata kata) 4

Nyanya zilizosagwa 5

Nyanya kopo 3 Vijiko vya supu

Viazi (vilivyokatwa vipande vidogo – cubes) 4

Dengu (chick peas) 1 kikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic)&Tangawizi iliyosagwa 1 Kijiko cha supu

Hiliki 1/4 kijiko cha chai

Mchanganyiko wa bizari 1 kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Pilipili manga 1 Kijiko cha chai

Vipande cha Maggi (Cube) 2

Wali

Mchele 3 Vikombe vikubwa (Mugs)

Mdalasini 2 Vijiti

Karafuu chembe 5

Zaafarani kiasi

*Jirsh (Komamanga kavu au zabibu kavu -raisins) 1/2 Kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Kosha Mchele na roweka.

2. Kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi (brown) chuja mafuta uweke kando.

3. Kaanga viazi, epua

4. Punguza mafuta, kaanga nyanya.

5. Tia thomu/tangawizi, bizari zote, vipande vya Maggi, nyanya kopo, chumvi.

6. Mwaga maji ya tuna iwe kavu, changanyisha kwenye sosi.

7. Tia zaafarani kidogo katika sosi na bakisha ya wali.

8. Chemsha mchele pamoja na mdalasini na karafuu.

9. Karibu na kuwiva, chuja maji utie katika chombo cha kupikia katika jiko (oven)

10. Nyunyizia zaafarani, mwagia vitunguu, viazi, na dengu juu ya wali.

11. Mwagia sosi ya tuna na pambia jirshi (au zabibu).

12. Funika wali na upike katika jiko moto wa 450º kwa muda wa kupikika wali.

* Jirsh (komamanga) kavu zioshwe vizuri kutoa vumbi au tumia zabibu kavu (raisins)

Mapishi ya Bilinganya

Mahitaji

Bilinganya 2 za wastani
Nyanya kubwa 1
Kitunguu maji 1 kikubwa
Swaum 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/4
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Parpika 1/4 kijiko cha chai
Pilipili mtama 1/4 kijiko cha chai
Curry powder1/4 kijiko cha chai
Chumvi kiasi
Coriander
Olive oil

Matayarisho

Katakata bilinganya slice nyembamba kisha ziweke pembeni. Baada ya hapo kaanga kitunguu maji mpaka kiwe cha brown kisha tia swaum na spice zote, zikaange kidogo kisha tia nyanya na chumvi kiasi. Pika nyanya mpaka iive na itengane na mafuta. Baada ya hapo tia mabilinganya na ukamulie limao kisha punguza moto na uyafunike na mfuniko usioruhusu kutoa mvuke ili yaivie na huo mvuke. Baada ya hapo yaonje kama yameiva na malizia kwa kutia fresh coriander na baada ya hapo yatakuwa tayari kwa kuliwa. kwa kawaida mi hupendaga kuyalia na wali na maharage badala ya kachumari kwahiyo nakuwa naitumia hiyo kama kachumbari

Upishi wa Afya kwa Nishati na Nguvu

Upishi wa Afya kwa Nishati na Nguvu 🥗💪

Kuhusu afya na lishe, ni muhimu sana kuzingatia upishi wa afya ili kuwa na nishati na nguvu ya kutosha kwa siku nzima. Kwa kuwa AckySHINE, mtaalamu wa lishe, nina ushauri na mapendekezo mengi kuhusu jinsi ya kuboresha upishi wako ili kuwa na afya bora. Hapa ni mambo 15 ya kuzingatia:

  1. Kula vyakula vyenye virutubisho vingi kama matunda na mboga mboga 🍎🥦. Vyakula hivi vinajaa vitamini, madini, na nyuzinyuzi ambazo ni muhimu kwa mwili wako.

  2. Punguza matumizi ya chumvi na sukari. Chumvi nyingi inaweza kuongeza hatari ya shinikizo la damu, na sukari nyingi inaweza kuongeza hatari ya kisukari. Badala yake, tumia viungo asili kama vile tangawizi na mdalasini kuongeza ladha kwenye vyakula vyako. 🧂🍭

  3. Hakikisha kula protini ya kutosha kila siku kwa ajili ya ujenzi wa misuli na nishati. Chagua chanzo bora cha protini kama vile nyama ya kuku, samaki, maharage, na karanga. 🍗🐟🥜

  4. Jiepushe na vyakula vya haraka au vyakula vilivyosindikwa. Vyakula hivi mara nyingi vina kiwango kikubwa cha mafuta yasiyo na afya na sukari. Badala yake, jifunze kupika vyakula vyenye lishe nyumbani. 🍔🍟

  5. Kula milo midogo mara kwa mara badala ya milo mikubwa. Hii itasaidia kuweka kiwango cha nishati yako imara na kukufanya uhisi kujazwa na uchangamfu wote. 🍽️

  6. Punguza matumizi ya vyakula vyenye mafuta mengi na badala yake chagua vyakula vyenye mafuta yenye afya kama vile mlozi, alizeti, na avokado. Mafuta yenye afya yanasaidia mwili wako kufyonza virutubisho muhimu. 🥑

  7. Kula kabohidrati iliyo na kiwango cha chini cha glycemic index, kama vile nafaka nzima, viazi vitamu, na mchele wa kahawia. Kabohidrati hizi husaidia kudumisha kiwango cha sukari kwenye damu kisichobadilika sana. 🍚

  8. Kunywa maji ya kutosha kila siku ili kuhakikisha kuwa mwili wako unakaa unyevu na unaendelea kufanya kazi vizuri. Maji ni muhimu kwa afya na nishati. 🚰

  9. Punguza unywaji wa vinywaji vyenye sukari kama soda na vinywaji vya nishati. Badala yake, chagua vinywaji vya asili kama maji ya matunda na juisi ya matunda. 🥤🍹

  10. Hakikisha kula mlo wa asubuhi wenye lishe. Kifungua kinywa ni mlo muhimu sana kwani husaidia kutoa nishati inayohitajika kuanza siku yako. Chagua chakula kama oatmeal, mayai, na matunda. 🥣🍳🍇

  11. Epuka kula usiku sana. Kupumzika kwa muda wa saa 2-3 kabla ya kwenda kulala itasaidia kuhakikisha kuwa chakula chako kinavunjwa vizuri na kusaidia kupata usingizi mzuri. 🌙💤

  12. Tumia mbinu za upishi ambazo zinaweza kusaidia kuhifadhi virutubisho vya chakula. Kupika kwa kutumia mvuke, kuchemsha, au upishi wa haraka kwa muda mfupi husaidia kuweka virutubisho kwenye chakula chako. 💨

  13. Kuwa na mazoezi ya mara kwa mara. Mazoezi husaidia kuongeza nishati na kuimarisha afya yako kwa ujumla. Panga ratiba ya mazoezi yako na fanya mazoezi ya angalau dakika 30 kwa siku. 🏋️‍♀️🚶‍♀️

  14. Chukua muda wa kupumzika na kujitunza. Kuwa na usingizi wa kutosha, kupata massage, kufanya yoga, na kufanya mambo unayopenda husaidia kuweka akili na mwili wako katika hali nzuri. 😌🧘‍♀️

  15. Kuwa na mtazamo chanya na furahia mchakato wa kuboresha upishi wako. Kula chakula chenye afya sio tu muhimu kwa mwili wako, bali pia kwa akili yako. Furahia chakula chako na ujue kuwa unaleta mabadiliko mazuri katika maisha yako. 😄🌈

Kama AckySHINE, ningeomba kujua maoni yako juu ya upishi wa afya na nishati. Je, una mapendekezo yoyote au mbinu bora ambazo umepata kwa uzoefu wako? Je, unapataje lishe bora wakati wa kazi au shughuli za kila siku? Natumai kuwa nakupa mwongozo mzuri na kuwa na afya bora na nguvu zaidi katika maisha yako! 💪🥗🌟

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Cornflakes

MAHITAJI

Unga – 1 Kikombe

Sukari ya kusaga – 3/4 Kikombe

Siagi – 125 gms

Yai – 1

Baking powder – 1/2 kijiko cha chai

Zabibu kavu – 1/2 kikombe

Cornflakes iliyovunjwa (crushed) – 2 Vikombe

Vanilla – 1 kijiko cha chai

MAANDALIZI

Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.
Tia baking powder, zabibu na unga na changanya vizuri.
Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Weka cornflakes katika sahani ya chali (flat) na zungusha viduara humo kisha upange katika sinia ya oveni.
Pika katika moto wa 350ºF kwa muda wa dakika 20-25 hadi vigeuke rangi na viwive.

Mapishi ya Pilau Ya Nafaka Na Nyama Ya Kusaga

VIAMBAUPISHI

Mchele – 3 vikombe

Nyama ya kusaga – 1 LB

Mchanganyiko wa Nafaka upendazo; maharagwe, njegere, mbaazi n.k 1 mug

Vitunguu maji kata vipande vipande – 3 vya kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi – 2 vijiko vya supu

Mafuta – ½ Kikombe

Mchanganyiko wa bizari (Garam Masala) – 2 vijiko vya chai

Vipande vya supu (Maggi cubes) – 3

Maji (inategemea mchele) – 5

Chumvi – Kiasi

MAPISHI

Osha mchele na roweka.
Weka mafuta katika sufuria na kaanga vitunguu mpaka viwe brown.
Tia Thomu na tangawizi, kaanga kidogo.
Weka nyama ya kusaga, chumvi na garam masala, endelea kukaanga mpaka nyama iwive.
Mwaga maji yaliomo katika kopo la nafaka na utie nafaka pekee humo.
Tia maji na vipande vya supu (Maggi cubes) huku unavivuruga, koroga kidogo.
Tia mchele, koroga kidogo.
Funika na pika kwa moto mdogo mpaka karibu na kukauka ukikorogoka kidogo. (kama unavyopika pilau ya kawaida)
*Epua uipike katika moto wa oven 350-400 Deg kwa muda wa dakika 15.
*Kama sufuria uliyotumia sio ya kupikia katika oven, mimina katika chombo chochote kinachotumika kwa oven kama bakuli la pyrex au treya za foil.
Pakua katika sahani na iko tayari kuliwa.

Mapishi ya Maharage na spinach

Mahitaji

Maharage yaliyochemshwa kiasi
Spinach zilizokatwa kiasi
Vitunguu maji 2
Nyanya 1/2 kopo
Swaum/Tangawizi 1 kijiko cha chakula
Curry powder 1 kijiko cha chai
Olive oil
Chumvi

Matayarisho

Kaanga vitunguu vikianza kuwa vya brown tia tangawizi/swaum kisha nyanya. Pika mpaka nyanya ziive kisha tia curry powder na chumvi. Vipike kiasi kisha tia maharage na maji kidogo kisha funika na uache vichemke. Baada ya muda tia spinach vipike pamoja na maharage mpaka ziive kisha ziipue. Baada ya hapo mboga yako itakuwa tayari kwa kuseviwa.

Jinsi ya kupika Mkate wa sinia

Mahitaji

Unga wa mchele (rice flour 2 vikombe vya chai)
Sukari (sugar 3/4 ya kikombe cha chai)
Hamira (dried yeast 3/4 kijiko cha chakula)
Hiliki (cardamon powder 1/2 kijiko cha chai)
Ute wa yai 1(egg white)
Tui la nazi (coconut milk kikombe 1 na 1/2 cha chai)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Changanya unga wa mchele, hamira, hiliki na tui la nazi pamoja katika bakuli la plastic kisha koroga vizuri. Ufunike na uwache katika sehemu ya joto mpaka uumuke.(ambayo inaweza kuchukua kama dakika 30-45. Ukisha umuka tia sukari na ute wa yai kisha ukoroge vizuri. Baada ya hapo washa oven katika moto wa 200°C kisha chukua chombo cha kuokea na ukipake mafuta na umimine mchanganyiko. Kisha utie katika oven na uoke kwa muda wa dakika 40. Hakikisha unaiva na kuwa rangi yabrown juu na chini. Na hapo mkate utakuwa tayari.

Mapishi ya Biriani

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Nyama (beef 1/2 kilo)
Vitunguu (onion 2)
Kitunguu swaum (garlic 1 kijiko cha chai)
Tangawizi (ginger 1 kijiko cha chai)
Maziwa mgando (yogurt 1 kikombe cha chai)
Hiliki nzima (cardamon 6)
Amdalasini nzima (cinamon stick 2)
Karafuu nzima (cloves 6)
Pilipili mtama nzima (black pepper 8)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Binzari manjano (turmaric 1/2 kijiko cha chai)
Binzari nyembamba nzima (cumin 1/4 kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Kaanga vitunguu mpaka viwe vya brown kisha tia nyama na uikaange kwa muda wa dakika 10. baada ya hapo tia tangawizi, kitunguu swaum, hiliki(4), amdalasini (1), karafuu (4), pilipili mtama (5), Curry powder, binzari manjano, binzari nyembamba na chumvi. Kisha koroga. Baada ya hapo tia yogurt na uipike mpaka ikauke kisha tia maji kidogo, funika na upunguze moto na uache ichemke kwa muda wa nusu saa.Baada ya hapo nyama itakuwa imeiva na mchuzi kubakia kidogo.Kwahiyo itatakiwa kuiipua.
Loweka mchele kwa dakika 10. kisha chemsha maji mengi kidogo katika sufuria kubwa. baada ya hapo tia hiliki (2) amdalamsini (1) karafuu(2) pilipili mtama (3) chumvi na mafuta kiasi. acha ichemke kidogo kisha tia mchele.Hakikisha maji yameufunika mchele kabisa na uuache uchemke kwa muda wa dakika 8 tu (kwani hautakiwi kuiva kabisa) kisha uipue na uchuje maji yote katika chujio. baada ya hapo chukua sufuria ya kuokea (baking pot kama unayoiona kweye picha) Kisha weka wali nusu na uusambaze sawia kisha weka mchuzi nyama na mchuzi wake pia utandaze na umalizie kwa kuweka leya ya wali uliobakia. Baada ya hapo ufunike na uweke kwenye oven kwenye moto wa 200°C kwa muda wa nusu saa.na baada ya hapo biriani litakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Pilau Ya Mchicha

VIPIMO

Mchele – 3 Vikombe

Mchicha

Mafuta – 1/2 kikombe

Vitunguu maji – 2 vikubwa

Nyanya – 1

Viazi – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 3 vijiko vya supu

Vidonge vya supu (Stock cubes) – 3

Jiyrah (cummin powder) – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ya unga – 1 kijiko cha chai

Hiliki ya unga – 1/2 kijiko cha chai

Mdalasini – 1 kijiti

Maji (inategemea mchele) – 5 vikombe

Chumvi

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

1. Osha na roweka mchele.

2. Osha mchicha, chuja maji na katakata.

3. Katakata vitunguu maji, nyanya.

4. Menya na kata viazi vipande ukaange pekee vitoe weka kando.

5. Katika sufuria tia mafuta na kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi.

6. Tia thomu, bizari zote, kaanga kidogo kisha nyanya.

7. Tia mchicha kaanga kidogo kisha tia mchele, maji na vidonge vya supu, chumvi.

8. Koroga kidogo kisha tia viazi ulivyovikaanga, funika na acha uchemke kidogo katika moto mdogo mdogo.

9. Kabla ya kukauka maji, mimina katika chombo cha kupikia ndani ya oven (oven proof) au katika treya za foil, funika vizuri na upike ndani ya oven moto wa 400º kwa dakika 15-20 upikike hadi uive.

10. Ukishaiva epua na tayari kuliwa na kitoweo chochote upendacho.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About