Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Jinsi ya kupika Mkate

Mahitaji

Unga wa ngano ( self risen flour) kikombe 1 na 1/2
Hamira (yeast) 1 kijiko cha chai
Sukari (sugar) 1 kijiko cha chakula
Chumvi (salt) 1/2 kijiko cha chai
Siagi iliyoyeyushwa (melted butter) 1 kijiko cha chakula
Maji ya uvuguvugu ( warm water) kiasi

Matayarisho

Changanya vitu vyote katika bakuli kubwa kisha aanza kukanda mpaka upate donge laini.Baada ya hapo liweke hilo donge kwenye bakuli la plastic na weke katika sehemu yenye joto ili unga uumuke. Hakikisha unga unaumuka zaidi (yani unaji double size) unaweza kuchukua kama saa 1 na nusu hivi. Baada ya hapo ukande tena na uache uumuke tena kwa mara ya pili, Ukisha umuka pakaza butter katika baking tin (chombo cha kuokea) na upakaze mkate butter kwa juu,kisha uoke katika oven kwa muda wa dakika 30 (katika moto wa 200C) (hakikisha juu na chini unakuwa wa brown Na hapo mkate wako utakuwa tayari

Jinsi ya kupika Mboga Za Majani Makavu (Aina Yoyote)

Viamba upishi

Mboga za majani makavu ¼ kg
Mafuta vijiko vikubwa 3-4
Karanga zilizosagwa kikombe ½
Maziwa au tui la nazi kikombe 1
Kitunguu 1
Nyanya 2
Chumvi (kama kuna ulazima)
Maji baridi

Hatua

• Loweka mboga za majani makavu na maji kwa dakika 10-15.
• Osha , mboga na katakata nyanya na vitunguu.
• Kangaa, pukusua na saga karanga zilainike.
• Kanga kitunguu, weka nyanya, koroga zilainike.
• Ongeza mboga zilizolowekwa na maji yake kwenye rojo, koroga na funikia mpaka maji yakaukie na ive. Punguza moto.
• Koroga karanga zilizosagwa na maji, ongeza kwenye mboga ukikoroga kwa dakika 5.
• Onja chumvi, pakua kama kitoweo.
Uwezekano
Weka nyanya kidogo.
Tumia tui la nazi au krimu badala ya maziwa.
Weka nyama au dagaa au Mayai badala ya Karanga.

Jinsi ya kupika Magimbi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Vipimo

Majimbi (Eddoes) kiasi 6 au 7

Nyama ng’ombe ½ kilos

Tangawizi ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Haldi (bizari manjano/turmeric) ½ kijiko cha chai

Tui zito la nazi vikombe 2

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha nyama kisha weka chumvi, bizari ya manjano, tangawizi mbichi, ukaushe kwanza katika sufuria kwa kukaanga kaanga.
Ikianza kukauka, weka maji funika uchemshe iwive.
Menya majimbi ukate kate na uweke katika sufuria nyengine.
Mimina supu na nyama katika majimbi uchemshe yawive majimbi.
Mwisho weka tui zito la nazi uchanganye vizuri kisha weka katika moto kidogo tu bila kufunika yakiwa tayari.

Jinsi ya kupika Mishkaki ya kuku

Kidali cha kuku 1 kikubwa
Swaum,tangawizi 1 kijiko cha chai
Limao 1/2
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Curry powder 1/2 kijiko
Paprika 1/2 kijiko cha chai
Hoho jekundu 1/2
Hoho la njano 1/2
Kitunguu 1/2
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Katakata kuku ktk vipande vya mishkaki ya kawaida kisha vimarinate na vitu vyote, kasoro hoho na kitunguu.Ni vizuri kuziacha either usiku mzima au kwa masaa machache ili spice ziingie vizuri. Baada ya hapo katakata hoho na vitunguu vipande vya wastani kiasi. Baada ya hapo Taarisha vijiti vya mishkaki kisha tunga nyama pamoja na hoho na vitunguu kisha nyunyuzia mafuta na kisha uzichome kama mishkaki ya kawaida. Itakapoiva itakuwa tayari kwa kuliwa na chochote upendacho kama ndizi za kuchoma, viazi na n.k.

Mapishi na Viazi Vitamu: Vitamu na Vyenye Lishe

Mapishi ni kitu ambacho kinaweza kuwa raha na pia kuwa na manufaa kwa afya yetu. Na leo, kama AckySHINE, ningependa kuzungumzia kuhusu mapishi ya viazi vitamu na jinsi yanavyokuwa vitamu na vyenye lishe. Viazi vitamu ni chakula chenye lishe kubwa na ladha tamu ambacho kinaweza kuboresha mlo wako na kukupa nguvu na virutubisho muhimu.

Hapa chini nimeorodhesha pointi 15 ambazo zinaonyesha umuhimu wa kula viazi vitamu:

  1. Viazi vitamu ni chanzo kikubwa cha wanga ambacho kinaweza kukupa nishati ya kutosha kwa siku nzima. 🥔

  2. Pia, viazi vitamu vina kiwango kikubwa cha nyuzinyuzi ambazo zinaweza kuboresha umeng’enyaji wa chakula na kusaidia katika mmeng’enyo wa chakula. 🍠

  3. Viazi vitamu vina kiwango kikubwa cha vitamini A ambayo inasaidia kuimarisha afya ya macho. 🌟

  4. Pia, viazi vitamu vina kiwango kikubwa cha vitamini C ambayo inasaidia kuimarisha kinga ya mwili. 🍊

  5. Kwa kuwa viazi vitamu ni chanzo cha wanga, yanaweza kuwa chaguo bora kwa watu wenye kisukari, kwani wanga wao hutolewa taratibu na kusaidia kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu. 💪🏽

  6. Viazi vitamu ni chakula chenye kalori chache ambacho kinaweza kusaidia katika kupunguza uzito. Kwa mfano, unaweza kuandaa chips za viazi vitamu zilizopikwa kwa kutumia mafuta kidogo badala ya kuzipika kwa kuzama kwenye mafuta. 🍟

  7. Pia, viazi vitamu vina kiwango cha juu cha potasiamu ambayo inasaidia kudumisha afya ya moyo na shinikizo la damu. 💓

  8. Kwa kuwa viazi vitamu vina nyuzinyuzi nyingi, yanaweza kusaidia katika kusawazisha viwango vya kolesterolini mwilini na kusaidia katika afya ya moyo. 🌿

  9. Viazi vitamu ni chanzo kizuri cha madini ya chuma ambayo ni muhimu kwa afya ya damu na inaweza kusaidia katika kuzuia upungufu wa damu. 🌈

  10. Akishine anashauri kutumia viazi vitamu katika mapishi mbalimbali kama vile maini ya viazi vitamu, supu ya viazi vitamu au hata keki ya viazi vitamu. Unaweza kuchanganya na viungo mbalimbali kwa ladha tofauti. 🍲

  11. Viazi vitamu vinaweza kuwa chaguo bora kwa watoto, kwani ni chakula chenye ladha tamu ambacho kinaweza kuwafanya kuwa na hamu ya kula. Unaweza kuwafundisha watoto kula viazi vitamu kwa njia ya kuvutia kama kuandaa chips za viazi vitamu ambazo zimepikwa kwa njia ya afya. 🎈

  12. Pia, viazi vitamu ni chanzo kizuri cha asidi folic ambayo ni muhimu kwa afya ya wanawake wajawazito na inaweza kusaidia kuzuia kasoro za kuzaliwa kwa watoto. 🤰🏽

  13. Viazi vitamu ni chakula chenye mchango mkubwa kwa afya ya utumbo, kwani nyuzinyuzi zake zinasaidia katika kuimarisha utendaji kazi wa utumbo na kuzuia matatizo kama vile kuvimbiwa. 🚽

  14. Kwa kuwa viazi vitamu vina kiwango kikubwa cha vitamini E, vinaweza kusaidia katika kudumisha afya ya ngozi na kusaidia katika kupunguza madhara ya kuzeeka. 🌺

  15. Na mwisho kabisa, viazi vitamu vinaweza kuwa chaguo bora kwa watu wenye mlo wa mboga, kwani ni chakula chenye ladha nzuri na kinaweza kufanywa kuwa chakula kamili kwa kuongeza viungo mbalimbali kama vile mboga za majani, nyanya au hata kuku wa kukaanga. 🥗

Kwa ufupi, viazi vitamu ni chakula chenye ladha tamu na muhimu kwa afya yetu. Kama AckySHINE, nakushauri kuwapa kipaumbele kwenye mlo wako na kujumuisha katika mapishi yako. Unaweza kujaribu mapishi mbalimbali na kubuni ladha tofauti kwa kutumia viazi vitamu. Je, unapenda viazi vitamu? Ni mapishi gani unayopenda kufanya na viazi vitamu? Napenda kusikia maoni yako! 🍽️😊

Mapishi ya Chicken Satay

Mahitaji

Kidali cha kuku 1 (chicken breast)
Kitunguu maji 1/2 (onion)
Kitunguu swaum/tangawizi (garlic and ginger paste) 1 kijiko cha chai
Limao ( lemon)1/4 kijiko cha chai
Curry powder 1/4 kijiko cha chai
Pilipili ya unga kidogo (Chilli powder)
Coriander powder 1/4 kijiko cha chai
Soy sauce 1kijiko cha chai
Mafuta 2 vijiko vya chai.
Chumvi kiasi (salt)
Vijiti vya mishkaki

Matayarisho

Osha kidali kisha kikaushe maji na kitchen towel na ukate vipande(cubes) vidogodogo na uweke pembeni. Baada ya hapo changanya vitu vyote (kasoro vijiti )na utie vimaji kidogo kisha visage katika breda kupata paste nzito. Baada ya hapo changanya hiyo paste na kuku na uache zimarinate kwa muda wa saa moja. Baada ya hapo zitunge kuku katika vijiti vya kuchomea na uzichome katika oven mpaka ziive (inaweza kuchukua kama dakika 10). Baada ya hapo chicken satay yako itakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Ndizi na Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi mbichi – 10-12

Nyama ng’ombe – 1 kilo moja

Kitunguu maji – 2

Nyanya/tungule – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 7

Tangawizi mbichi – 1 kipande

Ndimu – 2 kamua

Chumvi – kiasi

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi – 3 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Saga kitunguu thomu na tangawiz mbichi.
Weka nyama katika sufuria tia kijiko kimoja cha kitunguu thomu na tangawizi, chumvi na ndimu kisha chemsha hadi iive.
Menya ndizi ukatekate
Weka mafuta katika sufuria tia kitunguu maji kilokatwakatwa ukaange kidogo tu kisha tia nyanya/tungule uendelea kukaanga.
Tia tangawizi na thomu ilobakia.
Tia ndizi, kaanga kidogo kisha tia supu ya nyama na nyama yake.
Ziache ndizi ziive zikiwa tayari tia tui la nazi zikiwa tayari.

Jinsi ya kupika mboga ya majani ya mashona nguo

Viamba upishi

Mashonanguo mkono 1
Tui la nazi kikombe 1
Karanga zilizosagwa kikombe ½
Mafuta vijiko vikubwa 4
Kitunguu 1
Nyanya ndogo 2
Chumvi kiasi

Hatua

• Chambua mashona nguo mateke, osha na katakata.
• Menya osha na katakata kitunguu.
• Osha, menya na katakata nyanya.
• Kaanga karanga, ondoa maganda na saga zilainike.
• Kuna nazi na chuja tui.
• Kanga kitunguu, weka nyanya na koroga mpaka zilainike.
• Weka mashona nguo na chumvi kisha koroga sawa sawa,
funikiakwa dakika 5 -10.
• Changanya tui la nazi na karanga, ongeza kwenye hizo mboga
ukikoroga kwa dakika 5, punguza moto ili ziive taratibu.
• Onja chumvi na pakua kama kitoweo.
Uwezekano
Changanya mnavu, mgagani, mashonanguo kidogo ki¬dogo au
mboga nyingme.
Tumia maziwa au krimu badala ya tui la nazi.
Weka nyama au dagaa au samaki au mayai badala ya – karanga.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4 vikombe

Maji – 6 kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria wacha yachemke hasa

Tia unga kidogo kidogo huku ukikoroga mpaka ukamatane

Punguza moto huku ukiendelea kuusonga

Endelea kusonga kwa dakika kadhaa mpaka uanze kuchambuka

Kisha mimina kwenye bakuli au sahani na itakuwa tayari

Vipimo Ya Upishi Wa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma Wa Nazi

Samaki:

Samaki wa Nguru – kiasi vipande 5 – 6

Pilipili mbichi – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 5 chembe

Tangawizi mbichi – 1 kipande

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha supu

Pilipili nyekundu ya unga – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 3 kamua

Chumvi – kiasi

Ukipenda mkate samaki vipande kiasi.
Saga vipimo vyote vinginevyo katika mashine. Mchanganyiko ukiwa mzito ongezea ndimu
Changanya pamoja na samaki upake vizuri vipande vya samaki
Acha kwa muda wa nusu saa vikolee mchanganyiko
Panga samaki katika treya ya kupikia ndani ya oveni, kisha mchome (grill) samaki huku ukigeuza hadi viwive.
Epua weka kando.

Kuandaa Mchuzi:

Nyanya/tungule – 3

Kitunguu – 2

Bizari ya manjano/haldi – ¼ kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi zito – 3 vikombe

Chumvi – kiasi

Katakata vitunguu na nyanya vidogodogo (chopped) weka kando

Weka mafuta katika karai au sufuria, kaanga vitunguu hadi vianze kugeuka rangi

Tia nyanya kaanga pamoja na tia bizari ya njano/haldi .

Tia tui la nazi, chumvi koroga .

Mwishowe tia vipande vya samaki na rojo lake litakalobakia katika treya, mchuzi uko tayari

Jinsi ya kupika Biskuti Za Njugu/Matunda Makavu (Rock Cakes)

Viambaupishi

Unga 4 Vikombe

Sukari 10 Ounce

Siagi 10 Ounce

Mdalasini ya unga 2 vijiko vya chai

Matunda makavu/njugu (kama lozi,
Zabibu, maganda ya chungwa,
Cherries na kadhalika 4 ounce

Maziwa ya maji 4 Vijiko vya supu

Jinsi ya kuandaa na kupika

1) Chukua siagi na sukari koroga na mixer mpaka iwe kama cream.

2) Tia vanilla mdalasini, tia yai moja mix tena endelea kuongeza yai lingine mpaka umalize yote, changanya mpaka iwe laini kama sufi (fluffy)

3) Tia unga na baking powder na dried fruits, changanya na mwiko.

4) Chota mchanganyiko na kijiko cha soup weka kwenye treya ya kupikia tandaza na uma ili upate matundu juu ya biskuti.

5) Pika (bake) kwenye oven lenye moto wa 375 F. kwa muda wa dakika 15 hivi huku unazitazama tazama.

Jinsi ya kuishi maisha marefu (Mambo ya kuzingatia ili uishi maisha marefu)

Kuishi ukiwa na afya na kuishi maisha marefu kunawezekana kwa kubadili hali ya maisha unayoishi inayoharibu afya yako mfano uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi,kutokufanya mazoezi na kutokula matunda na mbogamboga.

Mambo yanayoweza kukusaidia kuishi maisha marefu ni kama yafuatayo

  1. Kuuandaa mwili kwa maisha marefu kwa kufanya mazoezi
  2. Kuwa makini kutambua na kutibu matatizo ya kiafya
  3. Kuepuka mazingira na kufanya kazi kwa namna au kazi zinazoweza kudhuru maisha yako. Mfano kuendesha gari bila kufuata utaratibu, kutokuvaa vifaa vya kujikinga wakati wa kazi
  4. Epuka vitu vyenye sumu vinavyoweza kudhuru afya yako na kukuletea matatizo ya kiafya kama dawa za mimea na mifugo, zitumie kama inavyotakiwa
  5. Usinywe pombe, usivute sigara wala kutumia dawa za kulevya
  6. Kula mlo kamili
  7. Usile vyakula vyenye chumvi na mafuta mengi
  8. Kunywa maji mengi ili kusafisha mwili
  9. Epuka msongo wa mawazo

Jinsi ya kutengeneza Cookies Za Tende Na Tangawizi

MAHITAJI

Unga vikombe vikombe 4

Baking soda 1 kijiko cha chai mfuto

Siagi 400 gms

Sukari ½ kikombe

Tende chambua ukatekate ifikie ¾ kikombe

Tangawizi ya unga vijiko 2 vya chai

Vanilla 1 kijiko cha chai

Yai 1

Maziwa mazito vijiko 2 vya kulia.

MAANDALIZI

Changanya siagi na sukari katika mashine usage mpaka iwe laini nyororo.
Tia yai uchanganye vizuri
Tia tende na vanilla, tangawizi uchanganye vizuri.
changanya unga na baking soda kisha, mimina kidogo kidogo huku unachanganya kwa kijiko cha ubao (mwiko).
Unga ukiwa mzito ongeza vijiko 2 vya maziwa. Fanya viduara upange katika treya uliyopakaza siagi kisha uchome (bake) katika over moto mdogo wa kiasi dakika 15 vigeuke rangi viwive.
Epua vikiwa tayari

Mapishi ya Biriani la nyama ya ng’ombe

Mahitaji

Nyama ya ng’ombe (beef 1/2 kilo)
Mchele (rice 1/2 kilo)
Vitunguu (onion 2)
Viazi (potato 2)
Vitunguu swaum (garlic 3 cloves)
Tangawizi (ginger)
Nyanya ya kopo (tomato 1/2 ya tin)
Curry powder (1/2 kijiko cha chai)
Binzari nyembamba ya kusaga (cumin 1/2 kijiko cha chai)
Binzari manjano (tarmaric 1/2 kijiko cha chai)
Mafuta (vegetable oil)
Chumvi (salt)
Rangi ya chakula (food colour)
Giligilani (fresh coriander)
Maziwa ya mgando (yogurt kikombe 1 cha chai)
Hiliki nzima (cardamon 3cloves)
Karafuu (clove 3)
Pilipili mtama nzima (black pepper 5)
Amdalasini (cinamon stick 1)

Matayarisho

Katakata nyama kisha ioshe na uiweke kwenye sufuria kisha tia kitunguu swaum, tangawizi, nyanya, curry powder, binzari zote, chumvi na maziwa ya mgando kisha bandika jikoni ichemke mpaka nyama iive na mchuzi ubakie kidogo.Baada ya hapo kaanga viazi na uweke pembeni, kisha kaanga vitunguu na mafuta mpaka viwe ya brown na kisha uvitie viazi vitunguu, na mafuta yake katika nyama. Koroga na uache uchemke kidogo kisha ipua na utie fresh coriander iliyokatwa na hapo mchuzi wako utakuwa tayari.
Baada ya hapo loweka mchele wako kwa muda wa dakika 10, kisha chemsha maji yatie chumvi, hiliki, karafuu, pilipili mtama na abdalasin na mafuta. Yakisha chemka tia mchele na uache uchemke mpaka ukauke maji yakisha kauka tia rangi ya chakula na uanze kugeuza ili ichanganyike na wali wote. Baada ya hapo ufunike na uache mpaka uive. Na baada ya hapo biriani litakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kuandaa Ndizi Mbichi Za Supu Ya Nyama Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi mbichi – Kisia

Nyama ng’ombe – ½ kilo

Pilipili ya kusaga – 1 kijiko cha chai

Tangawizi ya kusaga – 2 vijiko vya supu

Thomu (garlic/saumu) – 1 kijiko cha supu

Bizari mchuzi – 1 kijiko cha chai

Nazi ya unga (ukipenda kuongezea) – 2 vijiko cha supu

Chumvi – Kiasi

Ndimu – 1 kamua

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama ng’ombe katika sufuria, tia tangawizi, thomu, pilipili mbichi, bizari, chumvi. Roweka kidogo ukipenda kisha ikaushe yenyewe kwa maji yake
Ongezea maji ya kiasi yasizidi mno, kisha funika na chemsha.
Menya ndizi, ukatekate.
Nyama ikikaribia kuiva, weka ndizi uendelee kupika mpaka viive vyote.
Tia nazi ya unga kidogo tu ukipenda. Koleza kwa bizari mchuzi, pilipili, na ndimu
Epua mimina katika chombo cha kupakulia zikiwa tayari.

Namna ya kupika Biskuti Za Kuchoveya Chokoleti

VIAMBAUPISHI

Unga 300gm

Siagi 225gm

Icing Sugar 60gm

Chokoleti iliyokoza (Dark Chocolate) – 225gm

Vanilla – Vijiko 2 vya chai

Yai -1

Baking Powder ½ kijiko cha chai

Njugu za vipande ½ kikombe cha chai

Njugu zilizosagwa ¼ kikombe cha chai

JINSI YA KUTAYARISHA

Piga sukari na siagi katika mashine ya keki mpaka iwe laini
Kisha mimina yai na vanilla koroga vizuri
Mwisho mimina unga na baking powder polepole mpaka ichanganyike.
Kata kata umbo (shape) lolote unavyopenda (kama nyota, pembetatu,duara, kopa n.k)
Panga kwenye treya na choma kwa moto wa 350°C , vikibadilika rangi kidogo tu vitoe
Yayusha chokoleti tia kwenye bakuli ndogo.
kisha paka kwa kijiko au chovyea upande mmoja mmoja wa biskuti kisha nyunyizia njugu za kipande na njugu ya unga.
Panga kwenye sahani tiyari kunywewa na chai ya maziwa au kahawa.

Mapishi ya Tende Ya Kusonga Ya Lozi Na Cornflakes

VIAMBAUPISHI

Tende zilizotolewa kokwa – 1 Kilo

Cornflakes – 1 ½ kikombe

Lozi Zilokatwa katwa – 1 kikombe

Siagi – ¼ kilo

MANDALIZI

Mimina tende na siagi kwenye sufuria bandika motoni moto mdogo mdogo mpaka zilainike. Kwa muda wa dakika 10.
Isonge kidogo kwa mwiko au kuikoroga ichanganyike vizuri.
Changanya Cornflakes na lozi kwenye tende mpaka zichanganyika vizuri.
Pakaza treya au sinia mafuta au siagi kidogo.
Mimina mchanganyiko wa tende, zitandaze vizuri na ukate vipande saizi unayopenda. Zikiwa tayari kuliwa kwa kahawa.

Mapishi ya Maini ya kuku

Mahitaji

Maini ya kuku 1/2 kilo
Vitunguu vikubwa 2
Hoho 1
Pilipil 1
Limao 1/2
Swaum/tangawizi 1 kijiko cha chai
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Safisha maini weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu,swaum na tangawizi pamoja (hakikisha vitunguu visiwe vya brown), kisha tia maini, curry powder, pilipili, chumvi ,hoho na limao kisha changanya vizuri na ufunike. Pika mpaka maini yaive na hakikisha yanakuwa na rojo kidogo. Baada ya hapo ipua na yatakuwa tayari kwa kuliwa na chochote upendacho kama vile chapati, chips, ugali, wali.

Mapishi mazuri ya Wali Wa Kukaanga Kwa Kidari Cha Kuku

Vipimo vya Wali:

Mchele – 3 vikombe

*Maji ya kupikia – 5 vikombe

*Kidonge cha supu – 1

Samli – 2 vijiko vya supu

Chumvi kiasi

Hiliki – 3 chembe

Bay leaf – 1

Vipimo Vya Kuku

Kidari (chicken breast) – 1Kilo

Kitunguu – 1

Tangawizi mbichi – ½ kipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 7 chembe

Pilipili mbichi – 3

Ndimu – 2

Pilipilimanga – 1 kijiko cha chai

Mdalasini – ½ kijiko cha chai

Jira/Cummin ya unga – 1 kijiko cha chai

Maji – ¼ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Wali:

Osha na roweka mchele kisha weka sufuria katika moto tia samli ipashe moto.
Tia hiliki, bay leaf, kaanga, kisha tia mchele ukaange kidogo.
Tia maji, chumvi na kidonge cha supu, upike wali kama unavyopika pilau.
*Maji kisia kwa kutegemea mchele ulivyo.
*Unaweza kutumia supu yoyote badala ya kidonge.

Kuku:

Katakata kidari cha kuku vipande vya kiasi, weka katika sufuria, tia ndimu, bizari zote, chumvi.
Katakata kitunguu vipande vidogodogo, pilipili, na kitunguu thomu (chopped), tia katika kuku.
Chuna tangawizi mbichi tia katika kuku. Changanya vitu vyote vizuri.
Tia maji kiasi ¼ kikombe tu kiasi cha kumkaushia kuku. Weka katika moto mpike huku unageuzageuza. Anapokaribia kukauka epua akiwa tayari kuliwa na wali (na saladi upendayo)

Mapishi ya Pilau Ya Samaki Wa Tuna Na Mboga

Mahitaji

Mchele – 2 Mugs

Mboga mchanganyiko za barafu (Frozen veg) – Mug

Tuna (samaki/jodari) – 2 kopo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi -2 vijiko vya supu

Garam masala – 1 kijiko cha supu

Nyanya – 2

Kitungu maji – 1

Mdalasini nzima – 2 vijiti

Karafuu – 6 chembe

Pilipili mbichi – 1

Chumvi – kiasi

Viazi – 3

Maji – 2 ½ Mugs

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Maandalizi

Osha mchele na uroweke kwa muda wa dakika 20
Tia mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji mpaka kigeuke rangi ya hudhurungi (brown).
Mimina viazi, thomu na tangawizi, bizari zote na kaanga.
Tia nyanya uliyokatakata ikaange mpaka iwive.
Tia tuna endelea kukaanga kidogo tu.
Tia maji, yatakapochemka tia mchele.
Punguza moto uwe mdogo funika kwa muda wa ½ saa hadi wali ukauke na uwive. Utakuwa tayari kuliwa.

Mapishi ya mboga ya mnavu

Viamba upishi

Mnavu mkono 1
Kitungu 1
Karoti 2
Maziwa kikombe 1
Mafuta vijiko viubwa 4
Karanga zilizosagwa kikombe 1
Chumvi kiasi ½

Hatua

• Chambua mnavu, osha na katakata.
• Menya, osha na katakata kitunguu.
• Osha, menya na kwaruza karoti.
• Kaanga karanga, ondoa maganda na saga zilainike.
• Kaanga vitunguu na karoti mpaka zilainike ukikoroga.
• Weka mnavu na chumvi koroga sawa sawa, funika kwa dakika 5-10 (kama ni kavu weak maji kidogo).
• Changanya maziwa na karanga, ongeza kwenye mnavu ukikoroga kisha punguza moto kwa dakika 5.
• Onja chumvi na pakua kama kitoweo.
Uwezekano
Weka nyanya kidogo.
Tumia tui la nazi au krimu badala ya maziwa.
Weka nyama au dagaa au Mayai badala ya Karanga.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About