Je, karama ni zile za kushangaza tu?
Hapana, karama si zile za kushangaza tu, tena zile muhimu zaidi si hizo, bali zile zinazojenga zaidi Kanisa, kama zile za uongozi:
โMungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lughaโ (1Kor 12:28).
โBasi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia, kwa bidii; mwenye kurehemu, kwa furahaโ (Rom 12:6-8).
Karama nyingine muhimu zinatuwezesha kufanya nini?
Karama nyingine muhimu zinatuwezesha kuishi kwa useja kama Yesu na Paulo, au kwa ndoa:
โNipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi. Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane; ni heri wakae kama mimi nilivyoโ (1Kor 7:7-8).
โSi wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwaโ (Math 19:11).
Tunavyoona katika historia ya watawa, mara nyingi karama ya useja inaendana na nyingine katika maisha ya sala, ya kijumuia na ya kitume. Hivyo Filipo โalikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiriโ (Mdo 21:9).
Karama zinagawiwa vipi?
Karama zinagawiwa na Roho Mtakatifu jinsi anavyotaka, si kwa sifa au faida ya binafsi, bali kwa ustawi wa taifa la Mungu.
โKazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeyeโฆ Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?โฆ Kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisaโฆ Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amaniโ (1Kor 12:11,29-30; 14:12,33). Kwa ajili hiyo mitume walipambanua na kuratibu karama katika ibada na katika maisha ya jumuia zisije zikavuruga Kanisa.
Karama za kushangaza zina hatari gani?
Karama za kushangaza zina hatari mbalimbali, hasa zikitiwa maanani mno. Hapo ni rahisi zilete majivuno, kijicho na mafarakano.
โIkiwa kwenu kuna husuda na fitina, je, si watu wa tabia ya mwili ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?โฆ Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi. Naam, laiti mngemilikiโฆ Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asiangukeโ (1Kor 3:3; 4:8; 10:12).
Katika mambo yasiyothibitika ni rahisi kudanganyika kuwa yametoka kwa Mungu, kumbe sivyo. Kisha kudanganyika ni vigumu kuachana nayo hata yakiwa na madhara kwa mhusika au kwa Kanisa.
โWapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea dunianiโ (1Yoh 4:1).
Tunda la kuongozwa na Roho Mtakatifu ni lipi?
Tunda la kuongozwa na Roho Mtakatifu ni umoja wa Kanisa unaotokana na ustawi wa upendo na vipaji ndani ya waamini.
โWote walijaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho mojaโ (Mdo 4:31-32).
โTunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheriaโ (Gal 5:22-23).
โLakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi, ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi; tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafikiโ (Yak 3:14-17).
Madhehebu yanapozidi kufarakana ni lazima tujiulize kama kweli ni kazi ya Roho Mtakatifu.
Recent Comments