Wewe ni mshindi: Mambo yakuzingatia ili uweze kushinda chochote katika maisha

Mshindi ni mtu aliyeshinda, Hivyo wewe ni mshindi kwa kuwa umeshinda, kuwa hai leo ni ushindi, kuwa na Mungu mpaka sasa huo ni Ushindi, kuweza kujifunza semina na kufuatilia mafundisho kama haya wewe ni mshindi.
Ebu jiulize ni watu wangapi ulikuwa unawafahamu leo hawapo duniani? Wewe umeshinda Mungu kakuweka duniani ili uendelee kushinda.

KWANINI WEWE NI MSHINDI

Wanasayansi wanasema wakati ujauzito wa binadamu unatungwa kunakua na mamilioni ya mbegu za kiume ambazo zinakua zinatoka ili kwenda kurutubisha yai ili azaliwe mtoto. Na kwa kawaida inatakiwa mbegu moja tu kati ya hizo milioni. Hivyo basi wewe ni mmoja wa pekee kati ya mbegu za kiume millioni moja zilizotoka siku ile ulipotungwa tumboni mwa mama yako.

JIPIGIE MAKOFI SEMA MIMI NI MSHINDI

Kabla hujazaliwa ingewezekana ujauzito wako ukaharibika, Ingewezekana labda ujauzito wako ungetolewa, lakini haikuwa hivyo ukatoka salama. Na ulipozaliwa kuna watoto wengi tunasikia wanafariki wakati wa kujifungua lakini hukuwa wewe. Tunasikia pia magonjwa mbalimbali yanaua watoto lakini hukuwa wewe. Umeyashinda yote hayo hivyo wewe ni MSHINDI usijidharau kwa hali uliyonayo sasa wewe ni mshindi. Kuwepo kwako hai leo ni kwa sababu maalumu.

Umekwenda shule, umekua ,wako waliokufa kwa ajali lakini wewe upo hai bado Mungu ana kusudi na wewe.

Usijidharau nipo hapa Leo kukonyesha jinsi wewe ulivyo wa thamani mbele za Mungu. Wako wenzako wamepitia hatari ngumu na mateso hadi wakafikia kujinyonga, kunywa sumu, kujiua, lakini wewe upo hai. Wewe ni mshindi.
Upo duniani sasa ili uendelee kushinda.

Umezaliwa na uwezo wa kipekee sana ndani yako unaokuwezesha wewe kushinda kila siku na ukiweza kuutambua uwezo huo ushindi ni lazima. Kabla ya kutambua uwezo huo lazima utambue kwanini wewe umezaliwa! Ulizaliwa kwa kusudi gani? Ili uelewe kwanini Mungu amekuacha hai mpaka sasa ni ili ulitimize kusudi lake.

Hayo Yote niliyokwambia yanaweza yasiwe na maana sana kwasababu yameshapita sasa nakwenda kuzungumza namna ya kuendelea kutengeneza ushindi mwingine kila siku kupitia kwenye kusudi lako!

UFANYEJE UENDELEE KUSHINDA?

Haijalishi hali gani unapitia sasa upo hai leo kwa sababu maalumu na ni ili uweze kuendelea kua mshindi kwa kuifanya dunia kuwa mahali bora zaidi kuliko ulivyoikuta. Hii dunia haikua hivi miaka 10 iliyopita ni watu wachache wametumia uwezo Mungu aliweka ndani yao na kuvumbua mambo mengi na ya ajabu tunayoyaona sasa. Ni nafasi yako wewe kutumia nafasi hii ya kuwa hai leo kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi naamini wewe una nafasi kubwa sana.

“You were born to win, but to be a winner, you must plan to win, prepare to win, and expect to win.” – Zig Ziglar

Zig Ziglar anasema ulizaliwa kushinda kama tulivyoelezana hapo awali, lakini ili uendelee kua mshindi, lazima ujipange kushinda, ujiandae kushinda, na utarajie kishinda

Timu ya mpira inapochukua kombe sio mwisho wa mchezo wanakwenda kujinoa zaidi ili waweze kushinda tena na tena. Wewe unajiandaa vipi na kuendelea kushinda?
Vipo Vitu vichache vya Muhimu unatakiwa uwe unavifanya ili kushinda kila siku.

(a)Jitambue.

Ili uendelee kushinda kila siku lazima ujitambue wewe ni nani! Najua unatambua kwamba wewe ni jinsia gani. Lakini kujua hivyo tu haitoshi.
Kwanini ulizaliwa mwanamke/mwanaume, mtu mweusi tena Tanzania na sio nchi nyingine?
Ukitambua hivyo lazima ukubali na uanze kufanyia kazi na uendelee kushinda kila siku, Tambua kusudi la wewe kuzaliwa na kwanini ukazaliwa kipindi hiki na sio wakati mwingine.

(b) Usiangalie nyuma.

Haijalishi umepitia maisha ya namna gani umezaliwa kwenye mazingira ya namna gani, wewe jua kusudi la Mungu ndani yako na ulifanyie kazi, haijalishi jana umefanya vibaya kiasi gani, haijalishi pia ulifanya vizuri kiasi gani angalia mbele angalia kule unakokwenda.
Kule unakokwenda kuna maana zaidi ya unakotokea. Pia huwezi kwenda mbele huku umeangalia nyuma utajikwaa. Haijalishi ulikosea mara ngapi, umeua, umeachwa, umefeli, huna kazi, umefukuzwa, una madeni, usiyaangalie hayo.
Kama umeshajitambua liangalie kusudi na songa mbele.
“Adui wa mafanikio yako ya leo ni mafanikio yako ya jana, Adui wa mafanikio yako ya kesho ni mafanikio ya leo”

(c) Jua unapokwenda.

Hakikisha umetambua unapokwenda kama tayari umeshajitambua na umeacha kuangalia nyuma hakikisha sasa unajua unapoelekea. Kuwa na Maono, ndoto kubwa na kua na viongozi wanaokufundisha uelekee kwenye maono yako.Ukijua unapokwenda huwezi kupotea, Ukijua unapokwenda huwezi kufanya mambo ya ajabu ajabu, ukijua unapokwenda huwezi kuchukuliwa na kila mtu hovyo hovyo, Ukijua unapokwenda lazima utajisitiri, Biblia inasema pasipo maono watu huacha kujizuia.
Kama huna maono kulijua kusudi hakuna maana, kama huna maono utadondoka kila siku.

(d)Jifunze Kila Siku.

Umeshajitambua, ukaacha kuangalia nyuma, ukajua unapokwenda kwa kuwa na maono na ndoto kubwa, sasa huwezi kuvifikia vyote hivyo bila kujifunza. Huwezi kwenda kuwa mtu mkuu kwa ufahamu huo ulio nao sasa hivi, Inawezekana umesoma vyuoni una Degree au Masters lakini hiyo haionyeshi vyema kwamba wewe umesoma unajua kila kitu unaweza kuyabeba maono makubwa.
Soma vitabu vya uongozi, vitabu vya kuhamasiha jiendeleze binafsi, Jifunze kwa kupitia watu unaokutana nao kila siku, Jiunge na magroup kama ya whatsapp na ujifunze Makala kama hizi.

USHINDI UTAKUA WAKO KILA SIKU

“adui mkubwa wa kujifunza ni kujua” unapojiona wewe unajua kila kitu umesoma sana huwezi kujifunza kwa mtu mwingine alieko chini yako unakosea sana na hutaweza kufika popote kubali kujifunza kwa kila mtu haijalishi ni nani. Ushindi ni wako Na naamini kabisa kupitia makala hii kutatoka watu wakubwa sana katika Historia ya nchi hii na dunia.

(e) Jitengenezee tabia za Kushinda.

Unajitengenezeaje Tabia za kushinda? Jiambie maneno ya kushinda,huonagi wachezaji huwa wakiwa kwenye mazoezi wanashangilia kama vile tayari wana ushindi?
Jiambie maneno ya kujihamasisha mwenyewe. Mimi ni mshindi nimezaliwa kushinda, Siziogopi changamoto, mimi ni wa thamani, Unaweza kuandika maneno mazuri ya kukuhamasisha ukutani ili unapolala na uamkapo asubuhi uyaone na kuyasoma.
Washindi wana amka mapema. Washindi wanajua ndoto zao vizuri. Hakikisha kile unachokitaka kimekaa kwenye akili yako yaani hata ukishtuliwa usingizini leo unakuwa na uwezo wa kukisema.
Anza kufanyia kazi yale unayojifunza kila siku.

(F) Usiogope Kushindwa.

Usiziangalie changamoto na kukata tamaa. Zitumie changamoto kama shule jifunze kwa kupitia hizo na utaendelea kushinda kila siku.
Changamoto zinakuja kwasababu njia unayoiendea ni nyembamba hujawahi kuipita kabla. Na pia bado uwezo wako haujakuwa vya kutosha tumia changamoto kama njia za kukuza uwezo wako ili siku moja ufikie kule unakotaka ukiwa imara na usitetereke.

(g) Fanya vitu unavyoviogopa.

Usikubali kila siku unafanya vitu vile vile. Hakikisha kila siku kuna kitu kipya umefanya. Hii itakuongezea wewe uwezo wa kushinda na ujasiri wa kupita sehemu za mbele zaidi.
Hakikisha inapokua jioni umeangalia ni vitu gani vipya umefanya. Ni hatua gani umepiga katika malengo yako. Ni kitu gani kipya umejifunza. Usikubali unakutana na mtu anakupita hivi .Hujaongeza kitu chochote kwenye ufahamu wako au yeye hajajifunza kitu kutoka kwako. Wewe una kitu cha pekee sana ndani yako ambacho Mungu kakiweka kwa ajili ya wengine.

(h) Fanya na fuatilia zaidi vitu vinavyoongeza thamani kwako, kwa wengine, kwenye roho yako, kwenye mahusiano yako, kwenye maono na malengo yako na kwenye kusudi lako.

Ukifanya nje ya hapo utakua unapoteza muda bure. usikubali kupoteza siku yako bure. Kumbuka tumepewa masaa 24 tu ya kuishi yatumie vyema masaa hayo.

UKIWEZA KUFUATILIA HAYA USHINDI NI WAKO KILA SIKU, NI MAMBO MADOGO MADOGO UTAPITIA TU NA YANAREKEBIKA.

“Hakuna kiumbe kingine kitakachozaliwa tena kifikiri kama wewe, kitembee kama wewe, kiongee kama wewe, Hakuna tena, wewe ni wa pekee sana usijidharau tumia upekee huo kufanya mambo makubwa katika dunia hii usikubali kuondoka hivi hivi.”

“Hamu Yangu Ni Kuona Unafanikiwa”.

Melkisedeck Leon Shine

Editor: Melkisedeck Leon Shine. About Me | Contact Me | LinkedIn | TikTok | WhatsApp

Read and Write Comments

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Shopping Cart