Dondoo za Urembo na Mitindo

Mavazi ya Ofisini kwa Wadada

Wengi wetu tunashindwa kutofautisha mavazi ya sehemu husika mfano Ofisini, michezoni, na yale ya usiku na sehemu nyinginezo leo nitagusia vazi la ofisini kwa akina dada.

Unapotaka kuvaa vazi ,lazima uangalie vazi unalolivaa mda gani na mahala unapokwenda,siyo vazi la kutokea usiku au la kimichezo unalivaa ofisini,utakuwa kichekesho mbele za watu hata kwa wafanyakazi wenzio.

Mavazi ya kiofisi yanaeleweka lakini hasa kwa mwanamke basi vaa sketi fupi au ndefu na blauzi ya heshima iliyofunika kitovu chako, au suti ya heshima na koti na hata suruali ambayo haijakubana sana inafaa sana kwa ofisi.

Kama utapendelea kuvaa gauni basi angalia mkao wa hilo gauni ukoje maana mara nyingi gauni huwa halipendezi kuwa vazi la ofisini bali vazi la jioni.

Tiba mbadala ya chunusi na vipele usoni

Kuna idadi kubwa ya watu wanao kabiliwa na tatizo la vipele vya usoni ( Chunusi ). Kuwa na chunusi ni jambo lenye karaha sana, kwani linakufanya upoteze mvuto wako wa asili na hivyo kukukosesha raha.

Zipo njia mbalimbali za asili zinazo weza kutumika kutibu tatizo la chunusi na vipele vya usoni.

Ifuatayo ni miongoni mwa njia bora kabisa na ya uhakika itakayo kusaidia kuondokana na tatizo la Chunusi au vipele kwenye uso.

Komamanga: Maganda Ya Mkomamanga yaliyosagwa, yakichanganywa na habbat sodah ya unga, hutengeneza dawa nzuri ya asili ya kuondoa tatizo la vipele vya usoni ( chunusi )

Habbat Soda: Hii ni Habbat Sodah Ya Mbegumbegu. Habbat Sodah iliyosagwa ndio inayo hitajika katika kutengeneza dawa ya asili ya kuondoa tatizo la vipele vya usoni ama chunusi.

MAHITAJI:

Habbat Sawdah ya Unga iliyo sagwa.
Nusu kikombe ya maganda ya komamanga yaliyo sagwa.
Nusu kikombe ya siki ya tofaha(apple )

MATAYARISHO NA MATUMIZI

Changanya na pasha moto kwa dakika mbili kikombe kimoja cha Habbat-Sawdaa iliyosagwa, ½ (nusu)
kikombe cha maganda ya komamanga yaliyosagwa, na ½ (nusu) kikombe cha siki ambayo inatokana na juisi ya tofaha (apple).

Paka katika sehemu inayotakiwa kabla ya kwenda kulala kila siku usiku mpaka vipele (chunusi) vitakapoondoka. Mchanganyiko unaweza kukaa mpaka wiki tatu na ni lazima uwekwe katika hali ya ubarid.

Matumizi ya Papai Katika Urembo

Tunda la kitropiki la papai lina vitamini C na E likiwa na siri kubwa ya urembo na hutumika kutengeneza facial za aina mbalimbali.
Papai limekuwa likitumiwa kama njoia boya ya kutunza uso wako na kumfanya mtu kuwa na ngozi ya asili.

Bidhaa ambazo zimekuwa zikitengenezwa kwa kutumia tunda la papai ni pamoja na sabuni, lotion, tona, moisturiza, facial peels na nyingine nyingi.

Ukitumia facial mask ya papai utakuwa na sura nzuri ya asili na kukupa uonekanaji mzuri wa uso wako. Facial mask hii huweza hutumika kwa watu wa umri na aina yoyote ya ngozi.

Facial mask ya papai ina nguvu ya kung’arisha uso wako.
Pia inasaidia ngozi ambayo imeshaanza kupatwa na makunyanzi kutokana na umri kuonekana ya kuvutia kwani pia imekuwa ikiondoa chunusi na makunyanzi pia.

Ni rahisi kutengeneza facial mask ya papai na ukitumia itakusaidia katika kukabiliana na ngozi iliyoanza kuchoka, kung’arisha ngozi.

Kuna na njia nzuri za kuhakikisha kuwa, tunakuwa na nyuso nzuri zenye kupendeza na kuvutia ikiwemo kutumia vitu vya asili pamoja na matunda ya aina mbalim ambayo husaidia zaidi katika kuimarisha ngozi.

Mask ya mchanganyiko wa papai yai na yai ni nzuri katika kuhakikisha kuwa unakuwa na ngozi nzuri na nyororo.

Njia hii pia husaidia hata wale wenye nyuso za mafuta ambao wamekuwa wakisumbuliwa na chunusi mara kwa mara kwa kufanya ngozi kuwa kavu.

Unaweza kutengeneza aina hii ya mask kwa kufanya yafuatayo:-
Chukua papai likate kasha toa mbegu na kasha lisage kwa kutumia blenda ya kuondaponda kwenye kibakuli kwa kutumia kitukama mchi mdogo wa kinu.

Kisha weka mchanganyiko huo kwenye chombo ulichokichagua kama kikombe au bakuli.
Vunja yai na koroga kuhakikisha kuwa mchanganyiko huo umechanganyika vizuri.
Safisha uso wako kwa kutumia cleanser au maji ya vuguvugu na uondoeuchafu wote ulioganda usoni.

  • Kisha paka mask kuzunguka uso wako, na unapopaka hakikisha kuwa,
  • mchanganyiko huo haugusi macho yako.
  • Osha uso wako baada ya dakika 15 kwa kutumia maji ya vuguvugu.
  • Jifute kwa kutumia taulo safi
  • Unaweza kupaka losheni, tona au moisturiza.

Husaidia kutunza ngozi na kuondoa vipele na uchafu ulioganda usoni.
Hii ni njia rahisi ya kutengeneza uso isiyo na gharama.

Vyakula vya Kukuza nywele na kuzifanya ziwe na Afya

Kuwa na nywele zenye afya nzuri ni muhimu kwa wote bila kujali jinsi, hali hii husababisha wengi kutumia madawa ya aina mbalimbali ya kuhakikisha nywele zao zinastawi na kuwa na muonekano mzuri.
Kwa bahati mbaya, wengi waliotumia madawa yanayotengenezwa kwa kemikali hujikuta katika wakati mgumu siku za usoni wakikabiliwa na matatizo ya nywele kukatika na hata kupata madhara katika ngozi ya kichwa.

Njia bora na salama zaidi ya kustawisha nywele, kuzifanya ziwe na mvuto wa aina yake bila kujali wewe ni mtu wa asili ya bara Asia, Afrika au Marekani, ni kula vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa afya ya nywele.

Vifuatavyo ni sehemu ya vyakula ambavyo hupatikana kirahisi barani Afrika na kwa bei nafuu, ambavyo vitakupa afya bora zaidi ya nywele zako.

1. Yai

Nywele za binadamu zina protini ambayo zimeumbiwa. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa zina protini ya kutosha, na hilo hufanyika kupitia vyakula. Protini ni nguzo kuu ya nywele za binadamu, na yai ni moja kati ya vyakula vyenye utajiri mkubwa wa protini. Hakikisha unakula yai angalau mara tatu kwa wiki.

2. Spinachi

Nywele zinahitaji madini ya chuma ili ziweze kuwa katika hali nzuri ya afya. Kukosekana kwa madini ya chuma husababisha nywele kunyonyoka. Mwili unapokosa madini ya chuma, hewa ya oxygen na virutubisho hushindwa kufika vizuri kwenye mizizi ya nywele hivyo hufanya nywele kuwa dhaifu na zisizo na muonekano mzuri.

Mboga za majani aina ya spinachi ni suluhisho, kwakuwa zina madini ya chuma kwa wingi ambayo seli za nywele huhitaji.

3. Jamii ya Machungwa, Limao

Mwili wa binadamu huhitaji vitamini C ambayo husaidia kuhuisha utendaji wa madini ya chuma. Hivyo, unapaswa kuongeza matunda ya jamii ya ‘citrus’, kama vile machungwa, chenza, balungi na limao. Pia, unaweza kutumia na asali pamoja.

Vitamini C husaidia katika ukuaji wa nywele kusaidia usambaaji wa virutubisho na ukuaji wa haraka wa nywele.

4. Karoti

Ni muhimu sana kuhakikisha unakunywa juice ya karoti kila siku, kama unataka nywele zako zikue haraka zikiwa na mwonekano mzuri wenye afya. Vitamini A inayopatikana kwenye karoti ni muhimu sana kwa ukuaji wa seli za nywele. Kumbuka nywele zina tishu ambazo hukua haraka zaidi katika mwili.

Karoti ina mafuta asili yanayofahamika kama ‘sebum’ na mizizi ambayo husaidia kukuza nywele kwa haraka.

5. Parachichi

Tunda aina ya parachichi lina kazi nyingi sana mwilini kama matunda mengine, lakini hili ni tunda la kipekee amnbalo lina utajiri wa vitamini E ambayo husaidia mzunguko wa damu na katika hilo husaidia mfumo wa ukuaji wa nywele kwa haraka.

Tunda hili husaidia kuhuisha na kurekebisha mafuta na kiwango cha PH (inayosafisha kemikalii mwilini) ambavyo kama vitazidi kwenye mwili vinaweza kusababisha kusimama kwa ukuaji wa nywele, yaani nywele hudumaa.

Kwa faida zaidi, vitamin E inayopatikana kwenye parachichi kwa wingi husaidia zaidi afya ya moyo wa binadamu na zaidi ngozi. Hakikisha unapata tunda hili kadiri iwezekanavyo.

Hivi ni baadhi tu ya vyakula na matunda kwa ukuaji mzuri wa nywele zako. Kama unatumia vizuri mlo wako, utakuwa adimu sana kutumia mafuta yenye kemikali ambayo yanaweza kukuletea madhara mabaya.

Njia za kutunza nywele zako

Suala la kutunza nywele za asili wengi hutamani japokuwa ukweli kwamba kuna changamoto kadhaa, lakini kwa mtu aliye makini anao uwezo wa kupata kilicho bora katika nyewle zake. Leo tunaangazia vitu vya kufanya ili kukuza na kutunza nywele za asili.

Kwanza kabisa unapaswa kuzikubali nywele zako na kuzipenda , jambo hilo litapelekea mahusiano mazuri, kuelewa tatizo la nywele zako na kuanza kuchukua hatua taratibu ya kuzipatia uvumbuzi tatizo hilo.

Pili, unapaswa kufanya usafi wa kina wa ngozi na nywele zenyewe kwasababu endapo nywele zitaachwa chafu, basi ule uchafu unaziba matundu ya nywele na kuzuia njia kama vile ambavyo matundu ya uso yakiziba unapata chunusi.

Tatu, ni kulinda unyevu wa nywele . pale zinapooshwa, yale mafuta asilia ya kuzilinda huondoka na uchafu. Nywele inabaki ikiwa na udhaifu fulani maana haiwezi hata kushikilia hayo maji yaliyoo vizuri na zikikauka zinakuwa kavu sana. Ni vizuri kabla hazijakauka vizuri, zikafanyiwa ‘condition’ , kwa zile nywele ambazo ni nyepesi na chache pia kuna bidhaa zinasaidia kutunza vizuri unyevu na hivyo kuwa na afya nzuri.

Hatua nyingine ni ya kupaka mafuta kichwani, kwani mafuta yana umuhimu mno katika ukuaji wa nywele na mafuta mazuri ni ya nazi ambayo yamewafaa baadhi ya watumiaji wengi .

Njia nyingine ni ya kuzichambua vizuri nyele kabla ya kuzichana, hapa mtu anatakiwa kuwa na subira na nywele zake , asifanye pupa kuzichana na ikiwezekana aziloweshe maji kidogo halafu ndipo azichane kwa chanuo kubwa lenye upana wa kutosha (wide toothed comb) ili kuzipa afya na kuepuka kujiumiza wakati wa kuzichana.

Pia mtu anayetunza nywele za asili anatakiwa kupunguza matumizi ya vitu vyenye moto katika nywele zake kama vile pasi ya nywele na vingine kama hivyo. Nywele zinatakiwa zichanwe kawaida na ziachwe zikauke zenyewe kwa hewa bila kuzilazimisha.

Jinsi ya Kutumia Papai na Asali kuondoa Madoa Usoni

KUMEKUWA na sababu mbalimbali zinazofanya watu kutokuwa na ngozi zisizokubalika.Mbali na hali ya hewa pia matumizi ya pombe na sigara hata matumizi ya cream kali ambazo zimekuwa zikitumiwa na watu bila kujua madhara yake kumechangia kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.

Ngozi kwa kawaida inatakiwa ijitengeneze yenyewe na si kuitengeneza kwa vipodozi kama wengi wanavyodhani. Ulaji wa matunda na mboga za majani kwa wingi kunywa glasi nane za maji kwa siku ni njia nzuri kama unataka kuwa na ngozi nzuri isiyo na madoa wala ukavu ambao haupendezi.

Wengi wanaacha kula mbogamboga na matunda kwa wingi hata kutokunywa maji ya kutosha na badala yake wamekuwa akitegemea kuwa na ngozi nzuri jambo ambalo ni gumu.Mara kadhaa tumeshuhudia watu wanaopaka cream kali wakiwa kama wameungua usoni huku uso na mwili ukionekana kuwa makavu jambo ambalo linaashiria kuwa kupaka cream si suruhisho la kuwa na ngozi nzuri.

Kuna watu wamekuwa na ngozi za asili na hata unapowauliza baadhi yao hawajawahi kupaka cream hata siku moja na bado wana ngozi nzuri zinazovutia hao wamekuwa wakila kwa ajili ya kuhakikisha wanatengeneza ngozi zao kutoka ndani.

Pia wengi wanaharibu ngozi zao na kuwa na madoa kutokana na kutumia make up kwa muda mrefu na hata anapogundua kuwa ana tatizo la madoa amekuwa akijaribu kutumia cream nyingine kwa ajili ya kumaliza tatizo hilo jambo ambali linazidisha madhara kwenye ngozi.

Unaweza kutibu ngozi yenye madoa usoni pia mashavuni kwa kujitibu na juisi ya limao.

Namna ya kufanya

Chukua limao lioshe na kisha likamue na kuchuja mbegu zake. Weka juisi hiyo kwenye kikombe na kisha tafuta kitambaa laini kichovye kwenye juisi ya limao na dondoshea juisi ya limao kwenye sehemu zenye tatizo.

Kaa kama dakika tano kisha usha uso kwa maji safi.Pia unaweza kuchanganya na asali mbichi na maji ya limao husaidia pia kuondoa madoa usoni.

Limao lina sifa kubwa ya kuzuia harufu pia unaweza kulitumia katika kuondoa harufu kali ya jasho mwilini na husaidia kuondoa weusi kwenye kwapa, chini ya macho, mapajani pia.

Chukua kipande cha limao weka sukari kidogo, sugua.Unatakiwa kutumia kwenye kwapa ambalo ni safi, vizuri kutumia njia hii kabla na baada ya kuoga.

Namna ya uvaaji wa mavazi mbalimbali kwa wanaume

Wanaume wanajali mavazi yao pia, sio wanawake tu. Ila, mwanaume anabidi aelewe kwamba badala ya kufuata mitindo, kupendeza kwenye tukio lolote kuna nguo ambayo utaihitaji. Nguo hizi ni kama:

1. T-Shirt ya Pamba

Ukitaka t-shirt itakayo dumu kwa muda mrefu, nunua t-shirt zilizotengenezwa kwa pamba tu. Pia, kuwa na t-shirt kadhaa zenye rangi tofauti, zikiwemo:

Za rangi ya kawaida kama Nyeupe, nyeusi, rangi ya kijivu
Za rangi kali kama Njano, bluu nyepesi na kijani
Uzuri wa t-shirt ni kwamba zinaweza kuvaliwa na chochote kile. Kwa hiyo, kuwa na aina nyingi kabatini.

2. Polo Shirts

Mwanaume yoyote anatakiwa kuwa na Polo Shirt (t-shirt zenya kola) kadhaa. Zinafaa sana kuvaliwa kazini kwenye siku za Ijumaa au weekend.

3. Mashati ya kawaida

Mashati ya kawaida, ya mikono mirefu au mifupi, ni mazuri kuvaa na jinzi na viatu au raba. Pia, zipo za aina na rangi tofauti kwa hiyo tafuta itakayokufaa.

4. Mashati ya shughuli/sherehe rasmi

Kutegeamea na ajira yako, shati ya aina hii inaweza ikawa nguo utakayoishia kuvaa kuliko zote. Kwa hiyo, lazima uwe nazo za kutosha za aina mbalimbali.

Pia hata kama huzihitaji kwa kila siku, utazihitaji kwa sherehekama harusi au mkutano mkubwa wa kikazi.

Muhimu kuliko vyote ni kuhakikisha unajua saizi yako na kwamba unavaa shati linalo kutosha vizuri kabisa. Zaidi ya hapo, fikiria tai utakayoivalia.

5. Bukta

Kwa kuzingatia joto lote la Tanzania, bukta ni muhimu.

Kuna aina nyingi za bukta na zenye rangi tofauti. Zinaendena na polo shirt pamoja na viatu vya kawaida. Ni mazuri kuvaa kwenye wikiendi ukiwa umetulia na washkaji.

6. Suruali za kawaida

Suruali za aina hii zina faraja na zinavaliwa kwenye mazingira mbalimbali. Pia, kama polo shirt zinapatikana kwa rangi nyingi kwa hiyo zinaweza kuvaliwa na mashati, viatu, kodia n.k za ain nyingi.

7. Jinzi

Jinzi zinaweza kuvaliwa kokote, siku yoyote.

Iwe ijumaa kazini au jumamosi usiku, hata kazini kwenye siku ya kazi (kutegemea na masharti ya kazini kwako), jinzi zitavaliwa tu. Zipo za aina nyingi, rangi tofauti na zinavaliwa na chochote kile.

Ila, ni muhimu kujua saizi yako ile upendeza unavyostahili. Pia, jinzi zenye ubora zitakuwa na bei zaidi ila bora ununue jinzi yenye ubora itakayodumu kwa miaka kuliko jinzi isiyo na ubora itakyodumu kwa miezi.

8. Koti la suti

Mwanaume yoyote anatakiwa kuwa na koti za suti za rangi ya bluu na kijivu kabatini. Rangi hizi zinaendana na sherehe rasmi na zisizo rasmi, na zinavaliwa na aina mbalimbali ya mashati na viatu.

Ila, muhimu zaidi ya rangi ni saizi. Hakikisha unajua saizi yako na kwamba koti zinakutosha vizuri.

9. Chupi na Soksi

Hakikisha chupi zako ni nzuri, zinakutosha na ni safi (usije ukajiaibisha). Kama zimechakaa, zitupe.

Soksi nazo ni vilevile. Ila, unahitaji kuwa na aina tofauti za soksi kwa ajili ya mavazi tofauti. Hakikisha rangi ya soksi zako zina ukali au ni nzito kidogo ya suruali yako.

10. Viatu

Kwa kawaida, viatu ni vitu vya kwanza vya mtu kuangalia akikuona, hasa na wanawake. Kwa, sio swala la kupuuzia.

Cha muhimu ni kwamba ni visafi na ziko katika hali nzuri.

Ndio, inabidi ujaribu nguo mbalimbali ila ujue kinachokupendeza. Ila, kuwa na mavazi yasiyo na mbwembwe nyingi si mbaya. Bahati nzuri, nguo tulizoorodhesha hapo juu zitakusaidia kupendeza bila kuweka juhudi saaaaana.

Uvaaji wa Tai kulingana na Umbo lako

Kuna mambo mengi ya kufanya ili tuwe watu wa kuvutia kila wakati.Mpangilio wa mavazi hufanya mtu kuonekana maridadi. Kama wewe ni mvaaji wa tai unapovaa unazingatia mambo yapi? Na je unafunga tai yako kwa namna inayokubalika?

Wengine huwa hawafahamu jinsi ya kufunga tai na hivyo kuleta mushkeri wakati wa kuvaa tai na kusababisha tai kukaa upande. Unapoamua kuvaa tai na shati ambalo halijanyooshwa ambalo linakuwa kwenye mikunjo au kuvaa tai na ndala unakuwa umeua maananzima na kulivunjia heshima vazi hili.

Tai ni vazi lawatu walio maridadi kama huwezi kuwa maridadi basi vazi hili halikufai kabisa.
Unapovaa taa unatakiwa kuzingatia aina ya umbo lako kama wewe ni mnene vaa tai inayoendana na mtu mnene na kama wewe ni mwembamba basi vaa tai inayoendana na mtu mwembamba.

Kuna wengine huvaa tai zinazofika magotini na kuwa kichekesho anapopita mtaani
Tai ni vazi ambalo huongeza heshima na hadhi ya mvaaji cha muhimu ni jinsi gani unavaa tai yako na ikiwezekana jaribu kumechisha tai na suruali kwa vile ili tai upendeze ni laima iendane na nguo unayovaa.

Ni vyema ukahakikisha kuwa unakuwa na tai zenye rangi tofauti ambazo zitaendana na nguo unazovaa.

Jinsi ya Kujiremba Macho

Kuna urembo mbalimbali wa macho kulingana na taste ya mtu na mapendeleo yake . Leo nitazungumzia “smoky eyes” au macho yaliyapambwa kwa eye liner, mascara na eye shadows zenye rangi nyeusi, grey au za mng’aro.

Jinsi ya kuremba jicho:

Hakikisha uso na ngozi inayozunguka jicho ni safi kabla ya kuanza urembo wowote usishawishike kupaka vipodozi juu ya ngozi chafu haitakaa vizuri make up yako. Safisha kwa kutumia face towel iliyochovywa kwenye maji ya moto(huwa naona ni rahisi kwangu hasa kama kitambaa nitumiacho ni cheupe ni rahisi kujua kuwa u msafi au la kwa kuangalia kitambaa) kamwe usioshe uso wako kwa sabuni au maji ya moto. Ngozi ya uso iko rahisi kudhulika ikipata msukosuko kidogo. Sabuni huwa na kemikali nyingi na maji ya moto yanapausha uso. kama utalazimika kutumia sabuni osha uso kwa maji ya baridi kwa muda kiasi ili kuondoa kemikali zitakazokuwa zimeachwa.

Tayarisha kope/eye lids zako kwa kupaka wanja mweusi kwa uangalifu au eyeliner ya dark colour kama ni mtu anayejiamini unaweza tumia rangi yoyote ile sababu si wote wanaweza paka rangi ya njano au kijani na wakawa confident na muonekano wao.

Kwa matokeo mazuri uwe na eye shadow za aina mbili moja ya rangi iliyokolea na nyingine iliyo light. Anza na rangi iliyo light paka kwa uangalifu kuelekea kona ya nyusi kama picha hapo chini.

Endelea kama unapenda ming’ao machoni(hususani kwa sherehe) unaweza kupaka juu ya kope zako ila hakikisha hufiki mbali sana karibu na nyusi . Kisha malizia na darker colour kama picha ya kulia inavyoonyesha anzia kona ya kushoto ya jicho kwenda kulia kwa kiasi upendacho.

-Linganisha macho yako yote kama yana muonekano sawa kisha unaweza kuongezea mascara kwa juu ya nyusi ikiwa ni mpenzi.

Namna ya kuondoa Mikunjo ya ngozi

MIKUNJO katika ngozi ni miongoni mwa matatizo yanayowakabili wanawake wengi.
Tofauti na mikunjo ya uzee, mikunjo hii hutokana na kuchoka kwa ngozi kunakosababishwa na mambo mablimbali.
Katika kupambana na tatizo hilo, wadau wa urembo wa asili wamegundua njia mbalimbali zinazoweza kutumika kutatua tatizo hili.

Wadau hao wanashauri kumwona mtaalamu wa afya kwa ushauri zaidi wa matumizi ya njia hizo za asili kabla ya kuanza kutumia njia za asili kwani hata kama ni vipodozi asilia, haina maana kama ni salama kwa watu wote.

Kwa mujibu wa wadau hao, unaweza kutumia viungo vinavyopatikana jikoni kwako kupambana na mikunjo katika ngozi. Baadhi ya viungo hivyo ni pamoja na:

Karoti
Tumia juisi ya karoti kwa kupaka katika ngozi yako, hasa katika maeneo yaliyoathirika.
Karoti ina virutubisho muhimu kwa ngozi yako. Pia ina uwezo mkubwa wa kuondoa sumu ndani ya ngozi.

Si hivyo tu, karoti inaweza kuondoa kabisa tatizo la mikunjo ya
ngozi hasa sehemu za pembeni ya macho, shingo na maeneo kama hayo.
Namna ya kufanya

Chukua karoti, saga kwenye mashine kisha kamua ili kupata juisi yake.
Tumia pamba kupaka katika maeneo yaliyoathirika, fanya hivyo mara kwa mara, itakusaidia kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo hilo.

Maziwa
Maziwa yana virutubisho vinavyochochea kunawiri kwa ngozi. Pia yana chembechembe za ‘Alfa-Hydroxide Acid’ ambazo zina uwezo mkubwa kuondoa seli zilizokufa mwilini.

Yote haya husaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tatizo la mikunjo katika ngozi.

Unachotakiwa kufanya
Kuchukua maziwa kiasi na chovya pamba ndani yake, kisha paka maeneo yaliyoathirika.

Aloe Vera
Jeli ya Alovera ndiyo hasa inayotakiwa katika zoezi hili. Chukua jani lake na kisha likate ili kupata utomvu wake.

Chukua utomvu au jeli hiyo kama wengine wanavyoita na kisha pakaa sehemu iliyoathirika, itapunguza ama kuondoa kabisa tatizo hilo.

Parachichi
‘Mask’ ya Parachichi husaidia kuifanya ngozi iwe na mng’ao. Siyo hivyo tu, bali huchangia kwa kiasi kikubwa pia kuifanya ngozi iwe laini na nyororo.

Unachotakiwa kufanya
Chukua parachichi liloiva vizuri, kisha saga hadi lilainike.

Baada ya hapo pakaa sehemu iliyoathirika na acha kwa muda wa dakika 10, kisha osha sehemu hiyo uikaushe.

Papai
Mask ya Papai pia husaidia kuondoa tatizo hili.

Unachotakiwa kufanya
Chukua kipande cha papai kilichoiva na kuchanganya na kijiko kimoja cha unga wa ngano.

Pakaa sehemu iliyoathirika na kaa nayo kwa muda usiopungua dakika kumi. Mbali na kupaka pia unaweza ukatumia kula kwani lina vitamin E kwa wingi, ambavyo ni muhimu katika ukuaji wa ngozi.

Danzi
Juisi ya tunda hili husaidia katika uzalishaji wa sehemu ya juu ya ngozi ‘collagen’. Danzi lina kiwango kikubwa cha vitamini C. Na kwa kawaida aina hii ya vitamin husaidia kuchochea ukuaji wa ‘collagen’, hivyo kuifanya ngozi yako kunawiri.

Maji
Kunywa maji mengi kwani husaidia kuifanya ngozi yako iwe na unyevu muda wote.
Ikiwa utazingatia zoezi hili mikunjo kati ngozi yako itakuwa ni historia.

Jinsi ya kufanya nywele zako ziwe na mvuto na kuvutia zaidi

Mwanamke unywele hasa ukiwa nao, hii ni kauli upya ambayo Muungwana blog inakupa siku ya leo. Miongoni mwa maswali ambavyo huwa tunaulizwa na wasamoaji wetu ni pamoja ni kwa jinsi gani naweza kutengeneza nywele zangu ili ziwe za kuvutia?

Basi nasi bila ya haiana yeyote ile tunakuletea somo hili maalum kwa ajili ya watu wote ambao wanatamani kujua namna ya kuzifanya nywele zako zivutie. Kwanza kabisa kuna vitu vingi vinavyoweza kufanya nywele zako zikakosa afya na mvuto, vitu kama vumbi, upepo, mvua, jua, maji na madawa tunayoweka kwenye nywele zetu pamoja na vyakula tunavyokula ni chanzo kikuu cha nywele zetu kuharibika na kukosa afya na mvuto

Hivyo zifuatazo ndizo njia ya kufanya nywele zako zivutie:

Tumia shampoo inayoendana na nywele zako

Tumia shampoo inayoendana na nywele zako, kuna nywele za aina tofauti. kuna nywele kavu, zenye mafuta, mchanganyiko, na pia kuna nywele nyepesi, laini, ngumu na nzito. zipo aina tofauti za shampoo zinazoendana na aina ya nywele zilizopo . hivyo basi ni vyema unapotaka kuosha nywele ukajua ni aina gani ya shampoo utumie, pia kwenye condition napo unatakiwa kufanya hivyo hivyo.

Usichane nywele kwa nguvu zikiwa mbichi.

Jaribu kuzichana nywele kwa kichanuo kikubwa, au jaribu kuziacha mpaka zikauke ndo uzichane. unapochana nywele mbichi tumia kitana kikubwa na chana taratibub ukianzia nyuma kuja mbele. kuchan nywele zikiwa mbichi bila kufuata utaratibu kutafanya nywele zako zikatike na ziharibike.

Kula vyakula venye protin na matunda

kula vyakula venye protin na matunda kutasaidia kuimalisha afya ya nywele zako na kuzifanya ziwe nzuri na za kuvutia.

Kata ncha za nywele zako

kukata ncha za nywele zako kunasaidia kufanya nywele zako kujizaa upya, mara nyingi seli katika ncha za nywele hufa. seli zinapokufa huzui nywele zinazozaliwa kushindwa kustawi vyema na hivyo kuzifanya nywele zako kukosa afya. japo wanawake wengi huwa hawapendi kukata ncha za nywele zao wakihofia nywele zao kuonekana fupi. lakini ukweli ni kwamba unapokata ncha za nywele zako unasaidia nywele zako kupata nafasi ya kukua vizuri na kuwa zenye afya nzuri na kuvutia.

Osha nywele zako angalau mara moja kwa wiki

kuosha nywele zako angalau mara moja kwa wiki kutasaidia kuzifanya nywele zako ziwe na afya. Hata kama uko busy sana basi jitahidi isipite wiki mbili bila kuonsha nywele zako.

Zifunge nywele zako kabla ya kulala

Unapotaka kulala hakikisha unazifunga nywele zako, unaweza kuzisuka mabutu au kuzifuna vizuri na kuzibana. kulala huki ukiwa umeziachia nywele zako hufanya nywele zikatike na kuharibika

Tumia mafuta asili

Badala ya kutumia mafuta yenye kemikali nyingi kutoka viwandani, jaribu kutumia mafuta ya asili katika kutunza nywele zako. tumia mafuta kama ya nazi au parachichi kupaka nywele zako.

Zilinde nywele zako na jua

W akati utakapokuwa unaelekea kwenye sehemu yenye jua kali, vumbi au upepo. zilinde nywele zako kwa kuzifunika na kofia, scarf au mtandio. Pia unaweza kuzipaka sunscreen.

Madhara ya kuvaa miwani ya Urembo maarufu kama miwani ya Jua

Miwani za urembo maarufu kama miwani za jua zimetajwa kuwa na madhara kwa watumiaji wake kutokana na watu kutofahamu saizi za namba ambazo wanapaswa kuzivaa kabla ya kununua.

Akifafanua kwenye kipindi cha Supamix kinachorushwa East Africa Redio, Daktari Ningwa wa Upasuaji wa macho kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dk.Neema Daniel Kanyaro amesema watu wengi amekuwa wakivaa miwani pasipokjua kwamba zinaweza kuwasababishia matatizo ya kuona.

Dk. Kanyaro amesema kwamba watu wamekuwa wakivaa miwani za jua kama urembo pasipo kwenda kupima kujua ni aina gani ya miwani wanazotakiwa kuzitumia lakini pia bila kujua kama miwani hizo zina namba ambazo kila mtu ana namba kutokana na uono wake.

“Miwani ni dawa lakini usivae bila kupima kwani inaweza kukusababishia matatizo ikiwemo uoni hafifu. Unaweza kukuta unavaa miweani nyeusi lakini kumbe siyo namba yako. Kama hujijui unaweza kuta ukitazama unaona giza kumbe umeshaua macho kwa urembo” amesema.

Akizungumzia kuhsu presha ya macho Dk. Kanyaro amesema kwamba ugonjwa huo hauna dalili za moja kwa moja bali ni lazima kupima na huathiri watu wa rika zote.

Jinsi ya kuvaa viatu mbalimbali inavyotakiwa na ili upendeze

Viatu ni kinga kwa ajili ya kuhifadhi miguu. Vile vile viatu ni vazi ambalo linaongeza urembo na nakshi kwa mvaaji. Viatu vipo vya aina mbalimbali na vinavaliwa kulingana na mahali na mavazi yanayoambatana navyo. Tuangalie baadhi ya aina za viatu na wapi hasa na vipi vikitumika vinapendeza zaidi.

1.Viatu vya ngozi vya kufunika

Viatu vya kufunika vipo virefu sana, vyenye urefu wa wastani na vifupi kabisa. Mara nyingine haviwi vya ngozi kabisa bali ni kama vina plastiki na pia vingine huwa na uwazi mdogo kwa mbele.Viatu virefu zaidi mara hupendeza zaidi kuvaliwa kwenye sherehe na kanisani. Unaweza kuvaa kazini kama kazi yako haikulazimu kutembea tembea maana vitachosha miguu yako na kupunguza ufanisi.

Viatu vyenye urefu wa wastani unaweza kuvaa popote iwe kazini, kanisani, kwenye sherehe n.k. Viatu vya chini kabisa vinakuwa vyenye matumizi zaidi wakati unamatembezi mengi. Havifai sana kuvaa kwenye sherehe za usiku hasa kama unavaa nguo maalumu ya usiku. Vinafaa sana kwa mjamzito hasa katika miezi ya mwisho.

2.Viatu vya wazi virefu

Viatu hivi vipo vya aina mbili, vyenye rangi za mng’ao na ambavyo ni mahususi kwa sherehe za usiku na vyenye rangi ngumu ambavyo waweza kuvaa kazini au kanisani. Viatu hivi vinapendeza kuvaliwa na nguo yoyote ila ikiwa ya urefu wa wastani ni nzuri zaidi maana huwezesha kuonekana urembo na uzuri wote wa kiatu. Viatu hivi vinakuja katika mitindo mbalimbali na unachagua ule ambao wewe unaupendelea zaidi mfano vyenye visigino vyembamba, visigino vinene au aina ya ‘wedges’.

3.Viatu vya wazi vifupi

Viatu hivi ni vizuri sababu vinawezesha miguu kupumua na ku’relax’. Viatu hivi vipo vya aina tofauti tofauti na vinafaa sana kuvaliwa kwa matembezi ya jioni, wakati wa safari ndefu, wakati ukiwa na mizunguko mingi na pia hata kazini au kanisani pale unapokuwa umevaa nguo za kawaida (casual). Havivutii sana kuvaliwa na suti au nguo ya usiku. Pia mara nyingi viatu vya chini hupendezea kuvaliwa na nguo ndefu( hasa casual) na viatu virefu hupendeza zaidi kwa nguo yenye urefu wa wastani.

4.Viatu vya muda maalumu

Hivi ni viatu ambavyo vinavaliwa wakati wa kazi maalumu kama wakati wa kazi za mashambani, mgodini, wakati wa michezo au wakati wa baridi kali.

Ni vyema na inapendeza kama unauwezo uwe na viatu vya aina mbalimbali angalau aina tatu. Mfano viatu vyeusi vya urefu wa wastani, viatu vya usiku vya wazi, viatu vya chini vya kufunika na vya wazi.

Mambo ya msingi kwa mwanamke kuyajua unapojiremba

Kope nazo humpendezesha mwanamke kuna aina ya rangi za kupaka kwenye kope, lakini zinatofautiana. Ni vyema ukawasiliana na wataalamu wa mambo ya urembo kwa ushauri na siyo kukurupuka. Siyo umemuona fulani kapendeza na aina fulani ya rangi ya kwenye kope halafu na wewe ukakimbilia kupaka, utachekesha.

Rangi ya mdomo nayo ni eneo lingine linalompendezesha mwanamke. Ukweli ni kwamba tunatofautiana sana midomo wazungu wanaita ‘Lips’ Kila mwanamke ana tofautiana midomo na mwingine kwa hiyo hata rangi ya midomo nayo inakwenda sambambana aina ya lips na rangi ya ngozi ya mwili aliyo nayo mwanamke, siyo unajisiriba rangi ya mdomo halafu unaonekana kituko. Wasiliana na wataalamu wa urembo kwa ushauri zaidi.

Kucha kwa wanawake ni eneo lingine linolatakiwa kuwekwa katika unadhifu. Kuna baadhi ya wanawake unaweza kukutana nao kucha zao zimelika aidha kwa kung’atwa au kwa kuliwa na fangasi.

Ni vyema wanawake wenye tatizo hilo kumuona mtaalamu wa ngozi kwa msaada wa tiba. Unaweza kukutana na mwanamke kucha zake zimelika na zina sharp edges kiasi kwamba akikugusa utadhani umeguswa na msasa.

Au akishika Glasi ya Kinywaji ukiangalia kucha utadhani mkono ni wa mwanaume maana kwa jinsi kucha zake zilivyo hata hafanani nazo. Kuna kucha za bandia kama mwanamke ana matatizo ya kucha basi akazinunue kusitiri aibu.

Marashi, manukato au unyunyu kama wanavyoita vijana wa mjini ni muhimu kwa wanawake lakini ni vyema nikaweka angalizo. Haipendezi kwa mwanamke anayepulizia manukato yanayonukia sana mpaka yakawakera wengine ni vyema wanawake wakajipulizia marashi yenye staha na yasiyokera.

Ngozi ya mwanamke ni bora ‘sensitive’ sana na inaakiwa ipakwe aina ya mafuta au lotion yenye virutubisho kulingana na aina ya Ngozi. Kuna wanawake wenye Ngozi ya mafuta ‘Oil Skin’ kuna wenye Ngozi mchanganyiko na kuna wale wenye ngozi kavu (Dry Skin).

Ni vyema mwanamke kujua aina ya ngozi yake ili ajie aina ya product ya ngozi anayopaswa kutumia na siyo kwa sababu umemuona mwenzio anapaka aina fulani ya losheni na wewe unakimbilia kununua. Omba ushauri kwa wataalamu wa ngozi watakusaidia. Kuna baadhi ya maduka yanyouza vipodozi wanatoa msaada huo bure kabisa.

Jinsi ya kuchagua rangi sahihi wakati wa Kujipodoa

YAPO mambo mabalimbali katika tasnia ya urembo hasa katika vipodozi yanayopaswa kuzingatiwa katika kuboresha muonekano wa mtu.
Moja ya mambo hayo ni ujuzi na uelewa wa kutumia rangi katika kujipodoa kwani ni wanawake wachache wenye ujuzi huu.
Katika makala hii, nitakuelezea namna ya kuchanganya na kutofautisha rangi za vipodozi, lengo likiwa ni kuboresha muonekano wako.

Uchanganyaji wa rangi za vipodozi ni muhimu sana kwani katika kujipodoa, rangi zote za vipodozi unavyopaka zinatakiwa zioane ili kuleta muonekano ulio sawa na wa kueleweka.

Kwanza kabisa unatakiwa uwe makini katika kuoanisha rangi za vipodozi pamoja na rangi ya ngozi yako, hivyo katika hili unatakiwa kuwa na ujuzi maalumu ili usije ukafanya makosa na kuharibu muonekano wako.

Pia inabidi ufahamu hatua za upakaji vipodozi ili usije ukafanya vipodozi vingine visionekane katika uso wako.

Namna ya kuoanisha na kutofautisha rangi

Siku zote vipodozi vyako lazima viendane na mavazi yako ili kuleta maana zaidi kwa mfano, mara nyingi rangi ya mdomo ‘lipstick’ huendana na vazi lako wakati shedo ‘eye shadow’ zinatofautiana.

Kwa nguo za pinki

Katika mavazi haya, unatakiwa kupaka rangi ya mdomo yenye rangi ya pinki ambayo itaendana sawasawa na mavazi yako huku ukichanganya na shedo ‘eyeshadow’, inaweza kuwa ya rangi ya bluu ili kuitofautisha na mavazi yako, hapo utakuwa sawa katika kanuni za urembo.

Vazi la kijani

katika vazi hili unatakiwa kupaka rangi ya mdomo yenye rangi ya kahawia huku ukichanganya na shedo ya rangi ya kijani au kahawia iliyoingiliana na pinki au rangi ya machungwa.

Kwa vazi la njano au kahawia

Katika vazi hili unatakiwa kupaka ‘lipstick’ ya rangi ya kahawia iliyokolea, kwa upande wa shedo waweza kupaka ya rangi ya dhahabu.

Kwa vazi la bluu

Katika vazi hili unatakiwa kupaka ‘lipstick’ yenye rangi ya pinki huku ukipaka shedo ya rangi ya bluu kwa mtindo huu utakuwa mwenye kuvutia siku zote.

Jinsi ya kutumia maziwa ya mtindi kufanya ngozi yako kuwa laini na soft

Ulisha wahi kukaa ukajiuliza mbona kuna baadhi ya watu wana ngozi nzuri laini na soft? lakini kwako ni tofauti?

Ukawaza labda wanatumia vitu vya bei ghali ambavyo wewe huwezi ku – afford, au umesha hangaika na ma – cosmetics lakini bado ngozi yako haikubali kukaa vizuri?

Jaribu hii Home made Yogurt Cleansing, Tumia mtindi ambao hauna mafuta mengi au hauna kabisa (low fat),

Paka mtindi wako usoni fanya kama una sugua kwa muda mchache halafu uache kwa dakika 15, fanya hivi mara mbili kila siku na utapata matokeo kwa muda mchache.

Hii husaidia kuondoa cell za ngozi zilizo kufa (dead skin cells) na protein tighten the pore.

Namna ndizi inavyotumika katika urembo

Mbali na kulika, ndizi zina manufaa mengine, hasa katika urembo wa ngozi.
Ndizi zina virutubisho muhimu vinavyoboresha ngozi. Ndizi pia zina aina tatu za sukari zinazojulikana kama ‘sucrose’, ‘fructose’ na ‘glucose’.

Hakikisha unanawa uso wako mara tatu kwa siku. Unapofanya hivyo unaondoa uchafu.

Ndizi pia husaidia kuzuia chunusi.

Hakikisha unanawa uso kwa sabuni ambayo inaendana na ngozi yako. Ikiwa ngozi yako ni ya mafuta, hakikisha unatumia sabuni ambayo itakuacha ukiwa mkavu na kama ngozi yako ina ukavu, jioshe na sabuni itakayokufanya uwe na unyevu.

Kulainisha ngozi

Changanya asali na ndizi moja iliyopondwa na upake kwenye uso na shingo. Nawa uso kwa maji ya fufutende baada ya muda wa nusu saa. Fanya hivi angalau mara moja kwa wiki.

Kung’arisha uso

Ndizi huwa na Vitamin C ambayo husaidia kuiweka ngozi kuonekana iking’aa. Kwenye ndizi iliyopondwa, ongeza vijiko viwili vidogo vya juisi ya limau na upake kwa uso na shingo. Osha kwa maji ya fufutende baada ya dakika 20. Ni vizuri kupaka mchanganyiko huu wakati unapoenda kulala.

Kuzuia mikunjo

Ponda parachichi na ndizi pamoja. Paka kwa uso na uoshe baada ya muda. Mchanganyiko huu hulainisha ngozi ya uso na kuwa laini lakini pia upunguza ukubwa wa matundu ya ngozi ya uso wako.

Kusugulia uso (Scrubing)

Changanya ndizi na sukari kijiko kimoja, kisha paka usoni na usugue taratibu. Ndizi hulainisha ngozi kavu na sukari huondoa seli zilizokufa kwenye ngozi.

Saga ndizi moja na Oats vijiko vitatu kisha changanya na asali na maziwa. Paka usoni kwa dakika 15 kisha sugua.

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About