Dondoo za Urembo na Mitindo

Jinsi ya Kujaza nywele kwa njia za Asili

Zingatia mambo haya yafuatayo;

  1. Chukua parachichi kubwa moja, asali vijiko vitatu na kiini cha yai.
  2. Osha nywele zako kwa shampoo na uzikaushe.
  3. Ponda ponda parachichi mpaka lilainike kabisa. Chukua vijiko vitatu vya asali na kiini cha yai kisha changanya yote kwa pamoja.
  4. Paka mchanganyiko huo kaa nao kwa muda wa dakika 15 kisha osha.
  5. Fanya hivyo kwa muda wa wiki moja hadi mbili na utaweza kuona matokeo mazuri katika nywele yako

Sababu, tiba na jinsi ya kujikinga na Tatizo la uke kutoa harufu

Ni matumaini nyote mnaendelea vyema, nami alhamdulillah ala kul Hali naendelea vyema
Leo naona ni bora tukazungumzia tatizo la kutokwa na harufu mbaya ukeni maana watu wengi hudhani kuwa na harufu mbaya itokayo ukeni ni matokeo ya uchafu tu.

Ndio maana wanaume huwachamba wake zao kuwa hawajuhi kujisafisha na kufanya wanawake kuongeza jitihada katika kujisafisha ukeni, leo napenda kuzungumzia tatizo hili linalowasumbua wanawake wengi na kuwaumiza kichwa kutokana na kwamba lina athari kubwa sana kwani hufanya ndoa zao kudumaa NK,

~ Kitaalamu Hali ya mwanamke kutokwa na maji yenye rangi nyeupe au njano ni Hali ya kawaida na sio tatizo Lakini endapo maji yanatoka yapo katika Hali ya ute mzito wenye rangi nyeupe au kahawia na yanatoa harufu kali au kuwasha hapo una tatizo
~ Majimaji au ute unaoteleza kutoka sehemu za siri ni njia inayowezesha viungo vya uzazi vya mwanamke kujisafisha au kutoa uchafu wa seli zilizokufa na mabaki ya damu ya hedhi nnje ya mwili pia huvikinga viungo vya uzazi dhidi ya maaambukizi ya bacteria
~ Kwa kawaida huwa hayatoi harufu na huwa hayawashi na huwa na rangi nyeupe au njano pia huwa na asidi ya LACTIN ambayo huzuia bacteria kuzaliana
~ Mwanamke hutoa kiasi cha grams 2 za seli zilizokufa kutoka kwenye mji wa kizazi na grams 3 za ute mwepesi kila siku, kiwango hicho kinaweza kuongezeka au kupungua kutegemeana na mzunguko wa hedhi pia Kuna wakati ute huwa mwepesi na unaovutika na Kuna wakati pia huwa mzito wa rangi ya njano hautoi harufu

VISABABISHI VYA TATIZO HILI

Sababu za kutokwa na uchafu ukeni una vyanzo vingi sana vifuatavyo ni vyanzo vya tatizo hili

1. BACTERIA VAGINOSIS

Chanzo halisi cha ugonjwa huu hakijafanikiwa kuwa wazi,kinachotokea ni kuongezeka kwa ghafla kwa idadi ya ya bacteria hawa na kubadilisha uwiano wa kawaida katika mazingira ya uke, wanawake wenye wapenzi wengi na wanaofanya mapenzi kwa njia ya mdomo Wana hatari ya kupata tatizo hili

2. TRICHOMONAS

Maambukizi haya hutokana na Aina ya protozoa wa seli moja, trichomonas mara nyingi huambukizwa kwa njia ya ngono, protozoa huyo huweza kukaa kwenye unyevu unyevu kwa Muda wa saa 24 Bila kufa hivyo kufanya taulo na chupi zisizokauka kuwa chanzo kingine cha tatizo hili

3. YEAST INFECTION

Kwa kawaida Kuna kiwango kidogo cha yeast (candida albicans) katika uke, huwa tunasema Kuna maambukizi pale kiwango kinapozidi Hali ambayo inatokana na kubadilika kwa Hali ya hewa ukeni (Change in the PH balance of vagina)

Maambukizi ya yeast hayatokani na tendo la ndoa.

Mambo ambayo huchangia tatizo hili ni:

  1. MATUMIZI YA DAWA ZA KUZUIA MIMBA,
  2. MAWAZO,
  3. UJAUZITO,
  4. KISUKARI
  5. MATUMIZI YA ANTIBIOTICS

4. VAGINAL OR CERVICAL CANCER,

Mtu anapokua na kansa ya uke, hutokwa na maji ya harufu mbaya, hivyo ni heri uwe unafanya check up ili kujua Afya yako na kwakuwa cancer ya kizazi inapona hivyo ni vema ukatambua mapema uanze tiba

5. SEXUAL TRANSMITTED DESEAS (STDs)

Kuna baadhi ya magonjwa kama vile KASWENDE NA KISONONO yanasababishwa na ngono na kuwa chanzo cha tatizo hili.

6. POOR HYGIENE

Tatizo la kutokwa na maji wakati mwingine husababishwa na muhusika kua mchafu yan mtu unaoga kwa siku mara moja, chupi moja ndio hiyo hiyo mwaka mzima, pads unakaa nayo saa 24, ukienda kukojoa ujitawadhi na maji masafi hivyo unategemea utakua salama kweli??? Zingatia usafi mrembo

DALILI ZA TATIZO HILI

Kutokwa na uchafu ukeni unaoambatana na kuwashwa au kutokewa na vipele, hii hutokana na kuharibika kwa uwiano wa bacteria hivyo kuwa na madhara na uchafu hutoka wa aina tofauti hapa chini nitaelezea kila Aina ya uchafu na dalili zake.

1. UCHAFU WENYE RANGI YA KAHAWIA AU DAMU

Huu uchafu huonyesha dalili ya kuwa mzunguko wako wa hedhi umevulugika na wakati mwingine ni dalili ya kansa ya kizazi, mwanamke anayepata tatizo hili hutoa damu nyingi kuumwa sana nyonga

2. UCHAFU WENYE RANGI YA NJANO /KIJANI WENYE HARUFU MBAYA

Endapo uchafu huo utatoka kama povu na wenye rangi ya kijani au njano na ukiambatana na harufu mbaya huwa ni dalili ya ugonjwa wa trichomonas, maambukizi ya parasite yanatokana na ngono zembe, dalili Yake nyingine ni maumivu na kuwashwa wakati wa kutoa haja ndogo.

3. UCHAFU MWEUPE MZITO KAMA JIBINI

Mara nyingi hii huwa ni dalili ya maambukizi ya fangasi(YEAST INFECTION) na dalili nyingine huwa ni kuvimba sehemu ya nje ya siri, kuwashwa na kupata maumivu makali wakati wa tendo la ndoa.

4. UCHAFU MWEUPE/KIJIVU WENYE HARUFU YA SAMAKI

Uchafu wa Aina hii ni dalili ya maambukizi ya bacteria vaginosis, mara nyingi mwenye tatizo hili husikia muwasho na maumivu sehem ya nnje ya uke.

5. MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KUEPUKA TATIZO HILI NA TIBA YAKE

Matibabu ya tatizo hili hufanyika baada ya kugundua chanzo cha tatizo na mara nyingi tiba Yake ni tiba ya dawa za antibiotics kitu ambacho si tiba nzuri zaidi kwasababu tatizo huweza kujirudia kila wakati na kusababisha matatizo zaidi hivyo tiba nzuri ni kuepuka hili tatizo kwa kufanya yafuatayo

👉EPUKA KUJIINGIZA VIDOLE MARA KWA MARA UKENI
👉EPUKA MATUMIZI YA DAWA ZA ANTIBIOTICS MARA KWA MARA
👉PUNGUZA KULA VYAKULA VYENYE SUKARI NYINGI
👉TUMIA PADS ZENYE ANIONS NI SALAMA KWA AFYA YAKO
👉SAFISHA VIZURI NGUO ZAKO ZA NDANI NA UZIANIKE JUANI NA HATA KUZIPIGA PASI
👉KUNYWA JUICE YA APPLE,STRAWBERRY, NANASI KWA WINGI
👉EPUKA KUFANYA NGONO ZEMBE
👉HAKIKISHA UNAJISAFISHA KILA UNAPOMALIZA KUJISAIDIA
👉EPUKA KUTUMIA DAWA ZA KUZUIA MIMBA
👉EPUKA KUTUMIA SABUNI AU VITU VYA MANUKATO UKENI,

NOTE:

Wanawake wengi mnapenda kutumia baadhi ya dawa kwa lengo la kuongeza vionjo kwenye mapenzi pia kufanya uke kunukia vizuri, au kukaza uke rafiki uke una harufu nzuri sana ambayo haipatkan kokote hivyo haihitaji kuwekwa pafyumu Wala kusafishwa kwa sabuni za kemikali kwani huwa panajisafisha hivyo ni heri ukaacha kutumia kwani madhara Yake hayaonekani sasa ila baada ya Muda huonekana.

Njia za kutunza nywele zako

Suala la kutunza nywele za asili wengi hutamani japokuwa ukweli kwamba kuna changamoto kadhaa, lakini kwa mtu aliye makini anao uwezo wa kupata kilicho bora katika nyewle zake. Leo tunaangazia vitu vya kufanya ili kukuza na kutunza nywele za asili.

Kwanza kabisa unapaswa kuzikubali nywele zako na kuzipenda , jambo hilo litapelekea mahusiano mazuri, kuelewa tatizo la nywele zako na kuanza kuchukua hatua taratibu ya kuzipatia uvumbuzi tatizo hilo.

Pili, unapaswa kufanya usafi wa kina wa ngozi na nywele zenyewe kwasababu endapo nywele zitaachwa chafu, basi ule uchafu unaziba matundu ya nywele na kuzuia njia kama vile ambavyo matundu ya uso yakiziba unapata chunusi.

Tatu, ni kulinda unyevu wa nywele . pale zinapooshwa, yale mafuta asilia ya kuzilinda huondoka na uchafu. Nywele inabaki ikiwa na udhaifu fulani maana haiwezi hata kushikilia hayo maji yaliyoo vizuri na zikikauka zinakuwa kavu sana. Ni vizuri kabla hazijakauka vizuri, zikafanyiwa ‘condition’ , kwa zile nywele ambazo ni nyepesi na chache pia kuna bidhaa zinasaidia kutunza vizuri unyevu na hivyo kuwa na afya nzuri.

Hatua nyingine ni ya kupaka mafuta kichwani, kwani mafuta yana umuhimu mno katika ukuaji wa nywele na mafuta mazuri ni ya nazi ambayo yamewafaa baadhi ya watumiaji wengi .

Njia nyingine ni ya kuzichambua vizuri nyele kabla ya kuzichana, hapa mtu anatakiwa kuwa na subira na nywele zake , asifanye pupa kuzichana na ikiwezekana aziloweshe maji kidogo halafu ndipo azichane kwa chanuo kubwa lenye upana wa kutosha (wide toothed comb) ili kuzipa afya na kuepuka kujiumiza wakati wa kuzichana.

Pia mtu anayetunza nywele za asili anatakiwa kupunguza matumizi ya vitu vyenye moto katika nywele zake kama vile pasi ya nywele na vingine kama hivyo. Nywele zinatakiwa zichanwe kawaida na ziachwe zikauke zenyewe kwa hewa bila kuzilazimisha.

Jinsi ya Kujiremba Macho

Kuna urembo mbalimbali wa macho kulingana na taste ya mtu na mapendeleo yake . Leo nitazungumzia “smoky eyes” au macho yaliyapambwa kwa eye liner, mascara na eye shadows zenye rangi nyeusi, grey au za mng’aro.

Jinsi ya kuremba jicho:

Hakikisha uso na ngozi inayozunguka jicho ni safi kabla ya kuanza urembo wowote usishawishike kupaka vipodozi juu ya ngozi chafu haitakaa vizuri make up yako. Safisha kwa kutumia face towel iliyochovywa kwenye maji ya moto(huwa naona ni rahisi kwangu hasa kama kitambaa nitumiacho ni cheupe ni rahisi kujua kuwa u msafi au la kwa kuangalia kitambaa) kamwe usioshe uso wako kwa sabuni au maji ya moto. Ngozi ya uso iko rahisi kudhulika ikipata msukosuko kidogo. Sabuni huwa na kemikali nyingi na maji ya moto yanapausha uso. kama utalazimika kutumia sabuni osha uso kwa maji ya baridi kwa muda kiasi ili kuondoa kemikali zitakazokuwa zimeachwa.

Tayarisha kope/eye lids zako kwa kupaka wanja mweusi kwa uangalifu au eyeliner ya dark colour kama ni mtu anayejiamini unaweza tumia rangi yoyote ile sababu si wote wanaweza paka rangi ya njano au kijani na wakawa confident na muonekano wao.

Kwa matokeo mazuri uwe na eye shadow za aina mbili moja ya rangi iliyokolea na nyingine iliyo light. Anza na rangi iliyo light paka kwa uangalifu kuelekea kona ya nyusi kama picha hapo chini.

Endelea kama unapenda ming’ao machoni(hususani kwa sherehe) unaweza kupaka juu ya kope zako ila hakikisha hufiki mbali sana karibu na nyusi . Kisha malizia na darker colour kama picha ya kulia inavyoonyesha anzia kona ya kushoto ya jicho kwenda kulia kwa kiasi upendacho.

-Linganisha macho yako yote kama yana muonekano sawa kisha unaweza kuongezea mascara kwa juu ya nyusi ikiwa ni mpenzi.

Namna ya kuondoa Mikunjo ya ngozi

MIKUNJO katika ngozi ni miongoni mwa matatizo yanayowakabili wanawake wengi.
Tofauti na mikunjo ya uzee, mikunjo hii hutokana na kuchoka kwa ngozi kunakosababishwa na mambo mablimbali.
Katika kupambana na tatizo hilo, wadau wa urembo wa asili wamegundua njia mbalimbali zinazoweza kutumika kutatua tatizo hili.

Wadau hao wanashauri kumwona mtaalamu wa afya kwa ushauri zaidi wa matumizi ya njia hizo za asili kabla ya kuanza kutumia njia za asili kwani hata kama ni vipodozi asilia, haina maana kama ni salama kwa watu wote.

Kwa mujibu wa wadau hao, unaweza kutumia viungo vinavyopatikana jikoni kwako kupambana na mikunjo katika ngozi. Baadhi ya viungo hivyo ni pamoja na:

Karoti
Tumia juisi ya karoti kwa kupaka katika ngozi yako, hasa katika maeneo yaliyoathirika.
Karoti ina virutubisho muhimu kwa ngozi yako. Pia ina uwezo mkubwa wa kuondoa sumu ndani ya ngozi.

Si hivyo tu, karoti inaweza kuondoa kabisa tatizo la mikunjo ya
ngozi hasa sehemu za pembeni ya macho, shingo na maeneo kama hayo.
Namna ya kufanya

Chukua karoti, saga kwenye mashine kisha kamua ili kupata juisi yake.
Tumia pamba kupaka katika maeneo yaliyoathirika, fanya hivyo mara kwa mara, itakusaidia kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo hilo.

Maziwa
Maziwa yana virutubisho vinavyochochea kunawiri kwa ngozi. Pia yana chembechembe za ‘Alfa-Hydroxide Acid’ ambazo zina uwezo mkubwa kuondoa seli zilizokufa mwilini.

Yote haya husaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tatizo la mikunjo katika ngozi.

Unachotakiwa kufanya
Kuchukua maziwa kiasi na chovya pamba ndani yake, kisha paka maeneo yaliyoathirika.

Aloe Vera
Jeli ya Alovera ndiyo hasa inayotakiwa katika zoezi hili. Chukua jani lake na kisha likate ili kupata utomvu wake.

Chukua utomvu au jeli hiyo kama wengine wanavyoita na kisha pakaa sehemu iliyoathirika, itapunguza ama kuondoa kabisa tatizo hilo.

Parachichi
‘Mask’ ya Parachichi husaidia kuifanya ngozi iwe na mng’ao. Siyo hivyo tu, bali huchangia kwa kiasi kikubwa pia kuifanya ngozi iwe laini na nyororo.

Unachotakiwa kufanya
Chukua parachichi liloiva vizuri, kisha saga hadi lilainike.

Baada ya hapo pakaa sehemu iliyoathirika na acha kwa muda wa dakika 10, kisha osha sehemu hiyo uikaushe.

Papai
Mask ya Papai pia husaidia kuondoa tatizo hili.

Unachotakiwa kufanya
Chukua kipande cha papai kilichoiva na kuchanganya na kijiko kimoja cha unga wa ngano.

Pakaa sehemu iliyoathirika na kaa nayo kwa muda usiopungua dakika kumi. Mbali na kupaka pia unaweza ukatumia kula kwani lina vitamin E kwa wingi, ambavyo ni muhimu katika ukuaji wa ngozi.

Danzi
Juisi ya tunda hili husaidia katika uzalishaji wa sehemu ya juu ya ngozi ‘collagen’. Danzi lina kiwango kikubwa cha vitamini C. Na kwa kawaida aina hii ya vitamin husaidia kuchochea ukuaji wa ‘collagen’, hivyo kuifanya ngozi yako kunawiri.

Maji
Kunywa maji mengi kwani husaidia kuifanya ngozi yako iwe na unyevu muda wote.
Ikiwa utazingatia zoezi hili mikunjo kati ngozi yako itakuwa ni historia.

Jinsi ya kutunza kucha kujiepusha na maradhi shambulizi ya Kucha

Mikono, viganja na vidole ni kati ya sehemu muhimu katika mwili wa msichana. Mikono hutumika kufanya shughuli nyingi za nyumbani, shuleni na sehemu mbalimbali katika maisha kuanzia kutandika kitanda, kupika, kufanya usafi, kuandika, kujiremba pamoja na majukumu mengine mengi.

Mikono isipotunzwa vizuri ni rahisi sana kuharibika, kupoteza mvuto wake wa asili na kuharibu afya ya kucha. Hitaji la urembo wakati mwingine humsukuma msichana katika matumizi ya vipodozi vya kupaka kwenye kucha zake ili kukamilisha urembo wake.

Urembo wa vidole na kucha sio lazima ufanyike katika saluni au kwa wataalamu wa kupamba kucha, msichana anaweza kushughulikia afya na urembo wa vidole na kucha zake kwa gharama nafuu na kwa muda ambao mwenyewe anaona unafaa kufanya hivyo hata akiwa nyumbani.

Hii pia itamsaidia Msichana kuchagua vipodozi salama kwa afya ya kucha zake na mwili kwa ujumla. Ni jambo la muhimu kufahamu kuwa baadhi ya vipodozi vinavyotumika katika urembo wa kucha, vina rangi na sumu zisizofaa kwa afya. Sumu kama vile ‘Formaldehyde na Toluene’ zinazopatikana katika baadhi ya rangi za kucha zina madhara kwa afya ya msichana.

Ni kweli kuwa kucha nzuri huongeza urembo, mvuto na furaha ya msichana lakini pia ni busara kukumbuka kuwa afya ni muhimu kuliko urembo na uzuri. Afya ya mwili na kucha za msichana kwa ujumla hutegemea chakula bora chenye protein, madini na vitamini na siyo rangi na vipodozi.

Upungufu wa vitamini A, B Complex, proteni, madini ya chuma na chokaa (kalishiamu) mwilini husababisha kucha zipoteze afya yake ya asili. Kucha ambazo hazina afya zinaweza kuoza, kukauka, kupinda, kupasuka au kuwa na umbo kama kijiko. Magonjwa ya kuvu (fungus), na baadhi ya dawa za kupunguza makali ya virusi pia huharibu afya ya kucha. Mojawapo ya athari za dawa za kupunguza makali ya VVU aina ya Zidovudine (ZDV) ni kucha kuwa na rangi nyeusi.

Kwa ajili ya afya bora ya kucha msichana anashauriwa kula mboga za majani, maharage, korosho, asali na matunda kwa wingi kila siku. Usafi wa kucha kila siku kwa kuziosha kwa maji ya uvuguvugu na sabuni laini pamoja na brashi ndogo ya mikono huimarisha afya ya kucha. Kucha pia zinaweza kusafishwa kwa maji ya mmea wa mshubiri (Aloevera), kitunguu saumu kilichopondwa pondwa au kitunguu maji kisha viganja na vidole vikaushwe vizuri na kupaka losheni.

Kucha za msichana zinatakiwa zisiwe ndefu ili kuepuka utunzaji wa vimelea vinavyosababisha magonjwa na kurahisisha utunzaji na usafi wa kucha. Kucha ndefu zinaweza kuwa chanzo cha hatari kwa afya ya msichana na familia yake hasa pale msichana anapohusika na uandaaji wa chakula cha familia. Katika familia nyingi, hasa familia za kiafrika wasichana ndio wanaobeba wajibu na majukumu ya kuandaa chakula cha familia.

Kwa afya nzuri ya kucha, msichana anashauriwa kukata kucha zake ili ziwe fupi kadri anavyotaka kwa kutumia ‘nail cutter’ au mkasi mdogo au wembe mpya ambao haujatumiwa na mtu mwingine. Kuchangia nyembe za kukatia kucha si salama kwani kunaweza kuwa njia mojawapo ya kusambaza vimelea vya magonjwa hatari ya kuambukiza kama vile virusi vinavyosababisha UKIMWI na ugonjwa wa homa ya ini.

Ni vizuri kulainisha ncha za kucha baada ya kuzikata kwa kutumia tupa ya kucha (nail file) na kuzisugua kuelekea upande mmoja ili kuepuka kucha zisivunjike au zisisababishe michubuko ya ngozi wakati wa kujikuna. Kusugua kucha kwa kwenda mbele na nyuma kunaweza kusababisha kucha zivunjike kwa urahisi na haraka.

Kwa afya njema ya kucha, msichana pia anashauriwa asifungue pini za barua au kukwangua vocha za simu kwa kutumia kucha. Kucha zisikatwe kwa kutumia meno na zisilowekwe kwenye maji kwa muda mrefu hasa pale maji hayo yanapokuwa na kemikali au sabuni.

Kwa ajili ya afya njema ya kucha za miguuni, ni muhimu kuhakikisha kuwa, viatu kabla ya kuvaliwa vinakuwa vikavu na safi kabisa. Viatu visipotumiwa pia vihifadhiwe sehemu kavu isiyo na vumbi, maji au unyevunyevu ili kuepusha visiwe makazi ya kuvu (fungus)

Jinsi ya kuondoa weusi kwenye magoti na viwiko vya mikono

Ngozi nyeusi katika magoti na nyuma ya mikono hutokana na mkusanyiko wa cells zilizokufa, na hata unavyoweka pressure kwenye magoti na vipepsi vya mikono yako. Kama ukiwa unaweka mikono kwenye meza ukiwa kazini, ule msuguano unafanya ngozi iwe nyeusi.

Kama una magoti myeusi na nyuma ya mikono pia ni peiusi, tumia hizi njia asili kuweza kuondoa weusi huo:

Tumia Aloe Vera Juice.

Juice ya Aloe Vera inasaidia kuondoa weusi, all you have to do ni kupaka juice hiyo kwenye sehemu yenye weusi na uache kwa nusu saa kisha nawa na upake moisturizer. Rudia kufanya hivi mara mbili kila siku.

Tumia Binzari Manjano, Asali na Maziwa.

Changanya vyote hivi utapata mchanganiko mzito, paka kwenye magoti na kwenye mikono yako palipo na weusi. Kaa nayo kwa dakika 30, nawa na paka moisturizer. Rudia hii kila siku kwa wiki 3-4, utapata matokeo mazuri.

Tumia Ndimu.

Chukua pamba na uitumie kupaka juice ya ndimu katika sehemu zenye weusi. Au unaweza kuikata tu ndimu na kuipaka directly kwenye sehemu zenye weusi. Kaa nayo kwa lisaa 1 kisha nawa. Rudia hivi kila siku hadi weusi utakapopotea.

Tumia Olive Oil na Sukari.

Changanya vizuri, hii itakuwa kama exfoliation/scrub kwa ajili ya magoti na mikono. Paka katika hizo sehemu zenye weusi kisha kuwa kama una-massage polepole. nawa kwa maji ya uvuguvugu kisha paka moisturizer.

Mavazi Mazuri kwa wanawake wanene

Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiangaika kupata aina ya nguo za kuvaa tena hasa wanawake wanene, kutokana na maumbo yao wanaona ni kazi sana kutafuta nguo, wengine hukosa hata uhuru wa kutoka out na watu wao wa karibu kwa sababu tu wanakosa nguo.Wengi ujikuta wakichagua nguo pana pana ili kuficha maumbo yao, lakini kumbe unaweza kuwa huru sana na mwili wako.

Zifuatazo ni badhi ya tips zinazoweza kukusaidi kuchagua nguo za kuvaa kwa mwanamke mnene.Inawezekana nguo hizi unazo ndani lakini unashindwa kuzipangilia;

1. Kabla ya kuchagua nguo ni lazima kujua mwili wako una unene wa aina gani,ikiwa wewe ni mnene na unatumbo kubwa basi ni bora kuvaa gauni maana gauni uweza kukuweka vizuri na pia ni mazuri hasa kwa watu wanene.

2. Lakini pia kama wewe ni mnene na umebahatika kuwa na maziwa makubwa, ni vizuri kupendelea kuvaa nguo zenye v-shape, siri ya nguo hizi ni kwamba huwa na tabia ya kuficha ukubwa wa maziwa na kufanya uwe maridadi zaidi ila zingatia kuchagua brazia nzuri kuikaa blauzi yako sawia.

3. Kwa mwanamke mwenye hipsi anashauriwa kuvaa nguo zinakazo mfanya hasionyeshe sana hipsi zake tofauti ya yule hasiekuwa na hipsi , maana yeye anatakiwa kuvaa nguo itakavyo onyesha hipsi zake , hata hivyo kwa wanawake wanene wenye hipsi hawana haja ya kujibana sana kwa sababu hipsi huweza kujitokeza zenyewe tu.

4. Lakini pia kuchagua rangi ya nguo nzuri pia husaidia kupunguza au kuongeza umbile la mtu, kuna rangi huweza kukufanya ukawa mnene sana au mwembamba sana,kwa mfano nguo zenye mistari ya kulala sio nzuri kwa watu wanene maana hutanua miili yao.Lakini pia rangi za giza hupunguza muonekano wa unene ilihali rangi za mwanga huangaza na kufanya mtu aonekane sana.

Zingaia:

-Ni bora zaidi katika kuchagua rangi nguo za rangi nyeusi na nyeupe iliyochanganywa ni nzuri zaidi inafanya muonekano wa mtu uonekane maridadi zaidi.

-Lakini pia jitahidi kuvaa viatu vinavyoendana na mwili wako ,sio lazima kuvaa kiatu kirefu wakati mwili wako hauimili mikikimikiki ya kiatu kirefu, flatshoes pia hupendeza zaidi kwa mtu mnene .

Namna ya kuvaa vizuri kwa mwanamme upendeze na kuwa mtanashati

Nimeona leo nitoe darasa kidogo kuhusu mavazi sababu na mimi ni kipaumbele changu katika maisha.

1.Epuka kuvaa marangirangi

Wakati unamatch mavazi jitahidi kupunguza idadi ya rangi, rangi 3 tu zinatosha kukutoa bomba.

2. Vaa kulingana na mazingira/sehemu

Mtu mjanja anajua kubadilika kulingana na mazingira, sio kuvaa jezi la Man utd lenye jina la Wazza kwenye sherehe

3. Masharti ya kuchomekea

-Marufuku kuvaa oversize/undersize
-Usivae mlegezo
-Hakikisha singlet haionekani
-Usivae mkanda mrefu
-Usivae makubanzi/sandals

4. Kama umevaa pensi /kaptula.

-Hakikisha unavaa soksi fupi zisizoonekana
-Piga raba au makubanzi/sandals bila soksi
-Haipendezi kuchemekea

5. Usivae shati jeupe kama la mwanafunzi

Shati nyeupe ni nzuri kama unaijulia wakati unanunua hakikisha ina urembo wa aina yoyote ile au ni ya kimtindo sio kuvaa shati la shule

6. Hakikisha una suruali nyeusi

Mwanaume yoyote yule wa kijanja anajua umuhimu wa suruali nyeusi sababu inamatch mashati ya rangi nyingi.

7. Saa

-Kama umevaa jeans/kadet unaruhusiwa kuvaa saa ya aina yoyote
-Kama umevaa suti/suruali ya kitambaa epuka kuvaa saa ya mkanda wa plastic.

8. Miwani

Duh hapa pagumu kidogo lakini cha msingi zingatia muundo wa kichwa chako pamoja na aina ya macho uliyonayo na aina ya pamba ulizovaa pia.Sio umepiga jeans kali,kichwa kama madenge na macho kama bundi kisha unapiga miwani ndogo ya njano,ni

9. Vaa kofia za kijanja

Kofia pia huongeza mvuto,chagua kofia kulingana na aina ya kichwa na mavazi uliyovaa,haipendezi kuvaa suti na kapelo.Kanzu sharti ivaliwe na barakashia ndo utaeleweka la sivyo ni sawa na kuvaa dera tu

10. Mkanda

-Usivae mkanda mrefu km vile umefunga nyoka kiunoni
-Mikanda ya vitambaa au madoidoi inafaa kuvaliwa na jeans/kadeti/kaptula
-Jitahidi mkumatch rangi ya mkanda na viatu kama umevaa nguo za kuchomekea
-Zingatia upana wamkanda na rux za nguo yako

11.Tupia cheni za ukweli

Mikufu ya kiume pia huongeza mvuto
-Kama umevaa nguo za kuchomekea au suti itapendeza ukivaa cheni ndogo ambayo haitokezi nje ya shati
-Kama umepiga pamba za kishua mfano T.shirt na jeans hapa tupia cheni kubwa lakini hata cheni ndogo zinakubali

12.Uvaaji wa Tai

-Vaa kulingana na urefu wako
-Kama wewe mwembamba inapendeza kuvaa tie nyembamba
-Jitahidi kumatch tie na rangi ya shirt/suruali
-Hakikisha tie yako imefungwa vizuri shingoni

13.T.shirt na Jeans

Wanaume wajanja wa mjini hupenda kupiga t shirt na jeans na chini kutupia raba Kali…..Vazi hili lina mvuto wa aina yake hasa likivaliwa kitaani na sehemu za mitoko kama vile kwenye Club za starehe.

14. Vaa viatu kijanja

Hapa pia Kuna changamoto
-Usivaa suruali ya kitambaa na Raba
-Usivae suruali ya kuchomekea na makubanzi
-Ukipiga jeans unaweza kumatch t.shirt/shirt na rangi ya viatu
-Ukivaa suti yakupasa upige kiatu kikali ….ulikosea itakuwa sawa na Toyota Mark X yenye matairi ya Fuso !!!

Matumizi ya Papai Katika Urembo

Tunda la kitropiki la papai lina vitamini C na E likiwa na siri kubwa ya urembo na hutumika kutengeneza facial za aina mbalimbali.
Papai limekuwa likitumiwa kama njoia boya ya kutunza uso wako na kumfanya mtu kuwa na ngozi ya asili.

Bidhaa ambazo zimekuwa zikitengenezwa kwa kutumia tunda la papai ni pamoja na sabuni, lotion, tona, moisturiza, facial peels na nyingine nyingi.

Ukitumia facial mask ya papai utakuwa na sura nzuri ya asili na kukupa uonekanaji mzuri wa uso wako. Facial mask hii huweza hutumika kwa watu wa umri na aina yoyote ya ngozi.

Facial mask ya papai ina nguvu ya kung’arisha uso wako.
Pia inasaidia ngozi ambayo imeshaanza kupatwa na makunyanzi kutokana na umri kuonekana ya kuvutia kwani pia imekuwa ikiondoa chunusi na makunyanzi pia.

Ni rahisi kutengeneza facial mask ya papai na ukitumia itakusaidia katika kukabiliana na ngozi iliyoanza kuchoka, kung’arisha ngozi.

Kuna na njia nzuri za kuhakikisha kuwa, tunakuwa na nyuso nzuri zenye kupendeza na kuvutia ikiwemo kutumia vitu vya asili pamoja na matunda ya aina mbalim ambayo husaidia zaidi katika kuimarisha ngozi.

Mask ya mchanganyiko wa papai yai na yai ni nzuri katika kuhakikisha kuwa unakuwa na ngozi nzuri na nyororo.

Njia hii pia husaidia hata wale wenye nyuso za mafuta ambao wamekuwa wakisumbuliwa na chunusi mara kwa mara kwa kufanya ngozi kuwa kavu.

Unaweza kutengeneza aina hii ya mask kwa kufanya yafuatayo:-
Chukua papai likate kasha toa mbegu na kasha lisage kwa kutumia blenda ya kuondaponda kwenye kibakuli kwa kutumia kitukama mchi mdogo wa kinu.

Kisha weka mchanganyiko huo kwenye chombo ulichokichagua kama kikombe au bakuli.
Vunja yai na koroga kuhakikisha kuwa mchanganyiko huo umechanganyika vizuri.
Safisha uso wako kwa kutumia cleanser au maji ya vuguvugu na uondoeuchafu wote ulioganda usoni.

  • Kisha paka mask kuzunguka uso wako, na unapopaka hakikisha kuwa,
  • mchanganyiko huo haugusi macho yako.
  • Osha uso wako baada ya dakika 15 kwa kutumia maji ya vuguvugu.
  • Jifute kwa kutumia taulo safi
  • Unaweza kupaka losheni, tona au moisturiza.

Husaidia kutunza ngozi na kuondoa vipele na uchafu ulioganda usoni.
Hii ni njia rahisi ya kutengeneza uso isiyo na gharama.

Madhara ya kuvaa miwani ya Urembo maarufu kama miwani ya Jua

Miwani za urembo maarufu kama miwani za jua zimetajwa kuwa na madhara kwa watumiaji wake kutokana na watu kutofahamu saizi za namba ambazo wanapaswa kuzivaa kabla ya kununua.

Akifafanua kwenye kipindi cha Supamix kinachorushwa East Africa Redio, Daktari Ningwa wa Upasuaji wa macho kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dk.Neema Daniel Kanyaro amesema watu wengi amekuwa wakivaa miwani pasipokjua kwamba zinaweza kuwasababishia matatizo ya kuona.

Dk. Kanyaro amesema kwamba watu wamekuwa wakivaa miwani za jua kama urembo pasipo kwenda kupima kujua ni aina gani ya miwani wanazotakiwa kuzitumia lakini pia bila kujua kama miwani hizo zina namba ambazo kila mtu ana namba kutokana na uono wake.

“Miwani ni dawa lakini usivae bila kupima kwani inaweza kukusababishia matatizo ikiwemo uoni hafifu. Unaweza kukuta unavaa miweani nyeusi lakini kumbe siyo namba yako. Kama hujijui unaweza kuta ukitazama unaona giza kumbe umeshaua macho kwa urembo” amesema.

Akizungumzia kuhsu presha ya macho Dk. Kanyaro amesema kwamba ugonjwa huo hauna dalili za moja kwa moja bali ni lazima kupima na huathiri watu wa rika zote.

Madhara ya Uvaaji wa Wigi au nywele Bandia

Katika miongo kadhaa iliyopita, uvaaji wa wigi umekuwa fasheni katika sekta ya urembo na hutumika hususani na wanawake. Ingawa uvaaji wa wigi huwafanya wanawake hao kuonekana mithili ya mtu aliyevaa kofia ngumu (helmet), lakini yaonekana ni mapendeleo ya wengi.

Wanaume wengi hujiuliza , “Ni kwanini kina mama hupendelea kuvaa wigi na kusuka nywele za bandia?, wakati hupendeza na kuwa warembo zaidi wakiwa na nywele zao za asili”?

Wigi huvaliwa zaidi na kinamama wenye asili ya Afrika au Wamarekani wa asili ya Afrika. Lakini tukiangalia moja ya chimbuko hasa la uvaaji wigi ni ubaguzi uliokuwepo wakati wa utumwa ambapo wale wenye ngozi nyeupe na nywele shombeshombe walipewa kazi za ndani na wale wasio na ngozi nyeupe na nywele zisizo shombeshombe walifanyishwa kazi ngumu za mashambani.

Watumwa waliopelekwa barani Amerika hawakuweza kuzihudumia nywele zao kutokana na hali ngumu, na mabwenyenye waliwashusha hadhi na kuwavunja moyo kwa kuwaambia hawakuwa na nywele bali ni “manyoya”.

Lakini sababu nyingine inayodhaniwa kuwaathiri wanawake wa asili ya Afrika ni fikra kuwa mwanamke mwenye nywele ndefu pengine hadi mgongoni ni mrembo zaidi. Pia siku hizi warembo na wanaoshiriki katika mashindano ya urembo hujaribu kurefusha nywele zao ili kuwa na viwango na aina za mitindo ya ughaibuni.

Pamoja na kuwa wanawake wanajaribu kuwa warembo kwa uvaaji wa wigi, zifuatazo ni baadhi ya hasara au madhara kiafya ya uvaaji wigi na usukaji wa nywele za bandia.

Uvaaji wa wigi au nywele za bandia waweza kukusababishia mzio (allergy), endapo malighafi au kemikali zilizotumika kutengeneza wigi hiyo zitasisimua mfumo wa kinga ya mwili wa mvaaji.

Kupata m-ba ni tatizo jingine kutokana na uvaaji wigi, hii hutokana na kukosekana kwa hewa ya kutosha ya Oksijeni katika ngozi ya kichwa (scalp hypoxia) na katika tishu za shina la nywele. Kwa hiyo kama utaamua kuvaa wigi uhakikishe imetengenezwa kwa viwango vya ubora unaotakiwa na inapitisha hewa ya kutosha ya Oksijeni.

Pia waweza kunyonyoka nywele hata kama una nywele nzuri zenye afya, na kama utachagua kuvaa wigi na unataka kuepuka madhara hakikisha kuwa nywele zako ni safi, usilazimishe kuvaa wigi iliyo ndogo na yenye kubana sana, hakikisha unapata muda wa kupata hewa na nywele zako zinapakwa mafuta kuepuka ukavu wa ngozi ya kichwa na nywele kukatika .

Maumivu ya kichwa ni tatizo ambalo laweza kusababishwa na uvaaji wigi au usukaji wa nywele bandia. Wigi iliyo ndogo husababisha mkandamizo kichwani na kusababisha maumivu ya kichwa ya mara kwa mara.

Upotevu wa muda na fedha ni dhahiri kwa kuwa ufumaji wa nywele za bandia waweza kuchukua muda mrefu, itamlazimu mvaaji wigi kubadili kwa kununua mpya kila baada ya muda fulani au kuwa na wigi nyingi kwa ajili kubadili kulingana na fasheni.

Harufu mbaya huweza kujitokeza endapo mba na jasho vitachanganyikana na hupelekea uwepo wa bakteria au fangasi na kusababisha muwasho mkali, hii yaweza kumkosesha raha mvaaji wigi na mwenye kufuma nywele za bandia hasa pale anapokuwa katika majumuiko ya kijamii.Kama utachagua kuvaa wigi hakikisha nywele zako zinasafishwa na shampoo au sabuni, zinakaushwa vizuri na kupakwa mafuta.

Endapo mwanamama atachagua kuvaa wigi,asisahau kuwa nywele zake za asili zinahitaji matunzo,na azingatie wakati wa kununua wigi au nywele za bandia, ahakikishe ananunua yenye ubora unaotakiwa ili kuepuka madhara ya kiafya anayoweza pata kutokana na uvaaji wigi au anapofuma nywele za bandia.

Benson Chonya

Namna ya uvaaji wa mavazi mbalimbali kwa wanaume

Wanaume wanajali mavazi yao pia, sio wanawake tu. Ila, mwanaume anabidi aelewe kwamba badala ya kufuata mitindo, kupendeza kwenye tukio lolote kuna nguo ambayo utaihitaji. Nguo hizi ni kama:

1. T-Shirt ya Pamba

Ukitaka t-shirt itakayo dumu kwa muda mrefu, nunua t-shirt zilizotengenezwa kwa pamba tu. Pia, kuwa na t-shirt kadhaa zenye rangi tofauti, zikiwemo:

Za rangi ya kawaida kama Nyeupe, nyeusi, rangi ya kijivu
Za rangi kali kama Njano, bluu nyepesi na kijani
Uzuri wa t-shirt ni kwamba zinaweza kuvaliwa na chochote kile. Kwa hiyo, kuwa na aina nyingi kabatini.

2. Polo Shirts

Mwanaume yoyote anatakiwa kuwa na Polo Shirt (t-shirt zenya kola) kadhaa. Zinafaa sana kuvaliwa kazini kwenye siku za Ijumaa au weekend.

3. Mashati ya kawaida

Mashati ya kawaida, ya mikono mirefu au mifupi, ni mazuri kuvaa na jinzi na viatu au raba. Pia, zipo za aina na rangi tofauti kwa hiyo tafuta itakayokufaa.

4. Mashati ya shughuli/sherehe rasmi

Kutegeamea na ajira yako, shati ya aina hii inaweza ikawa nguo utakayoishia kuvaa kuliko zote. Kwa hiyo, lazima uwe nazo za kutosha za aina mbalimbali.

Pia hata kama huzihitaji kwa kila siku, utazihitaji kwa sherehekama harusi au mkutano mkubwa wa kikazi.

Muhimu kuliko vyote ni kuhakikisha unajua saizi yako na kwamba unavaa shati linalo kutosha vizuri kabisa. Zaidi ya hapo, fikiria tai utakayoivalia.

5. Bukta

Kwa kuzingatia joto lote la Tanzania, bukta ni muhimu.

Kuna aina nyingi za bukta na zenye rangi tofauti. Zinaendena na polo shirt pamoja na viatu vya kawaida. Ni mazuri kuvaa kwenye wikiendi ukiwa umetulia na washkaji.

6. Suruali za kawaida

Suruali za aina hii zina faraja na zinavaliwa kwenye mazingira mbalimbali. Pia, kama polo shirt zinapatikana kwa rangi nyingi kwa hiyo zinaweza kuvaliwa na mashati, viatu, kodia n.k za ain nyingi.

7. Jinzi

Jinzi zinaweza kuvaliwa kokote, siku yoyote.

Iwe ijumaa kazini au jumamosi usiku, hata kazini kwenye siku ya kazi (kutegemea na masharti ya kazini kwako), jinzi zitavaliwa tu. Zipo za aina nyingi, rangi tofauti na zinavaliwa na chochote kile.

Ila, ni muhimu kujua saizi yako ile upendeza unavyostahili. Pia, jinzi zenye ubora zitakuwa na bei zaidi ila bora ununue jinzi yenye ubora itakayodumu kwa miaka kuliko jinzi isiyo na ubora itakyodumu kwa miezi.

8. Koti la suti

Mwanaume yoyote anatakiwa kuwa na koti za suti za rangi ya bluu na kijivu kabatini. Rangi hizi zinaendana na sherehe rasmi na zisizo rasmi, na zinavaliwa na aina mbalimbali ya mashati na viatu.

Ila, muhimu zaidi ya rangi ni saizi. Hakikisha unajua saizi yako na kwamba koti zinakutosha vizuri.

9. Chupi na Soksi

Hakikisha chupi zako ni nzuri, zinakutosha na ni safi (usije ukajiaibisha). Kama zimechakaa, zitupe.

Soksi nazo ni vilevile. Ila, unahitaji kuwa na aina tofauti za soksi kwa ajili ya mavazi tofauti. Hakikisha rangi ya soksi zako zina ukali au ni nzito kidogo ya suruali yako.

10. Viatu

Kwa kawaida, viatu ni vitu vya kwanza vya mtu kuangalia akikuona, hasa na wanawake. Kwa, sio swala la kupuuzia.

Cha muhimu ni kwamba ni visafi na ziko katika hali nzuri.

Ndio, inabidi ujaribu nguo mbalimbali ila ujue kinachokupendeza. Ila, kuwa na mavazi yasiyo na mbwembwe nyingi si mbaya. Bahati nzuri, nguo tulizoorodhesha hapo juu zitakusaidia kupendeza bila kuweka juhudi saaaaana.

Mambo ya Msingi kujua kuhusu uvaaji wa Tai

Kuna mambo mengi ya kufanya ili tuwe watu wa kuvutia kila wakati.Mpangilio wa mavazi hufanya mtu kuonekana maridadi.

Kama wewe ni mvaaji wa tai unapovaa unazingatia mambo yapi? Na je unafunga tai yako kwa namna inayokubalika?

Wengine huwa hawafahamu jinsi ya kufunga tai na hivyo kuleta mushkeri wakati wa kuvaa tai na kusababisha tai kukaa upande. Unapoamua kuvaa tai na shati ambalo halijanyooshwa ambalo linakuwa kwenye mikunjo au kuvaa tai na ndala unakuwa umeua maananzima na kulivunjia heshima vazi hili.

Tai ni vazi lawatu walio maridadi kama huwezi kuwa maridadi basi vazi hili halikufai kabisa.
Unapovaa taa unatakiwa kuzingatia aina ya umbo lako kama wewe ni mnene vaa tai inayoendana na mtu mnene na kama wewe ni mwembamba basi vaa tai inayoendana na mtu mwembamba.

Kuna wengine huvaa tai zinazofika magotini na kuwa kichekesho anapopita mtaani
Tai ni vazi ambalo huongeza heshima na hadhi ya mvaaji cha muhimu ni jinsi gani unavaa tai yako na ikiwezekana jaribu kumechisha tai na suruali kwa vile ili tai upendeze ni laima iendane na nguo unayovaa.

Ni vyema ukahakikisha kuwa unakuwa na tai zenye rangi tofauti ambazo zitaendana na nguo unazovaa.

Jinsi ya kufanya nywele zako ziwe na mvuto na kuvutia zaidi

Mwanamke unywele hasa ukiwa nao, hii ni kauli upya ambayo Muungwana blog inakupa siku ya leo. Miongoni mwa maswali ambavyo huwa tunaulizwa na wasamoaji wetu ni pamoja ni kwa jinsi gani naweza kutengeneza nywele zangu ili ziwe za kuvutia?

Basi nasi bila ya haiana yeyote ile tunakuletea somo hili maalum kwa ajili ya watu wote ambao wanatamani kujua namna ya kuzifanya nywele zako zivutie. Kwanza kabisa kuna vitu vingi vinavyoweza kufanya nywele zako zikakosa afya na mvuto, vitu kama vumbi, upepo, mvua, jua, maji na madawa tunayoweka kwenye nywele zetu pamoja na vyakula tunavyokula ni chanzo kikuu cha nywele zetu kuharibika na kukosa afya na mvuto

Hivyo zifuatazo ndizo njia ya kufanya nywele zako zivutie:

Tumia shampoo inayoendana na nywele zako

Tumia shampoo inayoendana na nywele zako, kuna nywele za aina tofauti. kuna nywele kavu, zenye mafuta, mchanganyiko, na pia kuna nywele nyepesi, laini, ngumu na nzito. zipo aina tofauti za shampoo zinazoendana na aina ya nywele zilizopo . hivyo basi ni vyema unapotaka kuosha nywele ukajua ni aina gani ya shampoo utumie, pia kwenye condition napo unatakiwa kufanya hivyo hivyo.

Usichane nywele kwa nguvu zikiwa mbichi.

Jaribu kuzichana nywele kwa kichanuo kikubwa, au jaribu kuziacha mpaka zikauke ndo uzichane. unapochana nywele mbichi tumia kitana kikubwa na chana taratibub ukianzia nyuma kuja mbele. kuchan nywele zikiwa mbichi bila kufuata utaratibu kutafanya nywele zako zikatike na ziharibike.

Kula vyakula venye protin na matunda

kula vyakula venye protin na matunda kutasaidia kuimalisha afya ya nywele zako na kuzifanya ziwe nzuri na za kuvutia.

Kata ncha za nywele zako

kukata ncha za nywele zako kunasaidia kufanya nywele zako kujizaa upya, mara nyingi seli katika ncha za nywele hufa. seli zinapokufa huzui nywele zinazozaliwa kushindwa kustawi vyema na hivyo kuzifanya nywele zako kukosa afya. japo wanawake wengi huwa hawapendi kukata ncha za nywele zao wakihofia nywele zao kuonekana fupi. lakini ukweli ni kwamba unapokata ncha za nywele zako unasaidia nywele zako kupata nafasi ya kukua vizuri na kuwa zenye afya nzuri na kuvutia.

Osha nywele zako angalau mara moja kwa wiki

kuosha nywele zako angalau mara moja kwa wiki kutasaidia kuzifanya nywele zako ziwe na afya. Hata kama uko busy sana basi jitahidi isipite wiki mbili bila kuonsha nywele zako.

Zifunge nywele zako kabla ya kulala

Unapotaka kulala hakikisha unazifunga nywele zako, unaweza kuzisuka mabutu au kuzifuna vizuri na kuzibana. kulala huki ukiwa umeziachia nywele zako hufanya nywele zikatike na kuharibika

Tumia mafuta asili

Badala ya kutumia mafuta yenye kemikali nyingi kutoka viwandani, jaribu kutumia mafuta ya asili katika kutunza nywele zako. tumia mafuta kama ya nazi au parachichi kupaka nywele zako.

Zilinde nywele zako na jua

W akati utakapokuwa unaelekea kwenye sehemu yenye jua kali, vumbi au upepo. zilinde nywele zako kwa kuzifunika na kofia, scarf au mtandio. Pia unaweza kuzipaka sunscreen.

Jinsi ya kung’arisha sura yako kwa kutumia Asali, Sukari, Maziwa, na Limao

Usafi wa uso ni moja ya mambo muhimu sana kwa mwanamke au mwanaume yeyote yule ambaye anapenda kuwa nadhifu na mwenye mvuto. Kumbuka “reception ndio kila kitu “. Unapokutana na mtu sura yako na mwonekano wa sura yako ndio kitu cha kwanza kinachomtambulisha kwamba wewe ni nani na upo kwenye hali gani.

Kuna njia nyingi za kuufanya uso wako uvutie na kupendeza. Leo tutaongelea zaidi jinsi ya kusafisha uso kwa njia ya asili. Mie hupenda kutumia njia ya asili sababu ni rahisi kupata vifaa na ni nafuu . Pia mtu anaweza kufanya kwa mazingira yoyote yale. Na matumizi ya vitu vya asili kwenye mwili husaidia kupunguza sumu mwilini kwani kutumia vipodozi vyenye kemikali husababisha miili yetu kujaaa sumu.

Njia ya asili ya kusafisha na kupendezesha mwili ninayokueleza leo inahitaji vitu vikuu vinne : asali, sukari, maziwa, na limao.

Haijalishi aina gani ya ngozi unayo , njia hii ya asili inaweza kutumika kwa aina yoyote ile ya ngozi iwe ngozi yenye mafuta au ngozi kavu.

Kiasi cha mahitaji yanayohitajika:

  • Kijiko kimoja cha asali
  • Kijiko kimoja cha sukari
  • Kijiko kimoja cha maziwa
  • Kijiko kimoja cha limao

Utaratibu wa kusafisha uso

Weka mahitaji hapo juu kwenye chombo kilicho kisafi, changanya vitu vyako mpaka vilainike, viache kwa muda wa dakika 10 ili viweze kuchanganyikana vizuri na na sukari iweze kuyayuka vizuri.

Baada ya mchanganyiko wako kuwa tayari chukua kipande cha pamba kilicho kisafi tumia kupakia mchanganyiko wako usoni . Na kumbuka ni vizuri uso ukiwa mchafu na upaswi kuosha uso alafu ufanye zoezi hili. Baada ya kupaka mchanganyiko wako usoni kaa kwa dk 15 .

Baada ya hapo chukua maji ya uvuguvugu, kitaulo kisafi na sabuni ya kipande “vizuri kutumia sabuni ya kipande maana haina kemikali nyingi” tumia kitambaa kuoshea uso wako pamoja na sabuni.

Basi baada ya hapo umekuwa umemaliza zoezi lako la usafi wa ngozi yako
Kumbuka njia hii aina madhara yoyote na haibadilishi rangi au muonekano wa ngozi yako na unashauliwa kufanya mara kwa mara ili kukupa mvuto zaidi.

Mambo ya Kuzingatia ili uwe na ngozi laini

Takribani kila mtu angependa kuwa na ngozi laini, au hata laini zaidi. Watu wengi wamekuwa wakiitafuta ngozi nzuri au kujitahidi kuitunza ili isiharibike. Lakini je, wamefanikiwa?
Wachache hufanikiwa na wengi hushindwa. Na hata hao waliofanikiwa wengi wao hutumia vipodozi vikali ambavyo vingi huchubua na kuharibu ngozi zao na kuwaletea madhara makubwa sana baadae.

Vipi wewe, ungependa kuwa na ngozi nzuri bila kuidhuru afya yako? Karibu somo la leo ili uweze kuwa na ngozi nzuri bila kuidhuru afya yako.

Ngozi laini ni nzuri na inaongeza mvuto wa mwili. Ulaini wa ngozi hupotezwa na mambo mbalimbali kama vile seli za ngozi kupungukiwa na maji na kuanza kusinyaa na kunyauka, seli za ngozi kujeruhiwa, na seli za ngozi kufa. Matokeo yake ni michirizi, makunyanzi, makovu, chunusi, madoa, ngozi kufubaa na kuzeeka.

Kuifanya ngozi kuwa laini unahitaji kuupatia mwili virutubisho vyote vya kujenga mwili vizuri na kunywa maji ya kutosha ili seli zisikauke, kusinyaa wala kunyauka. Kula mlo kamili, matunda mengi na kunywa maji ya kutosha.

Pia unahitaji kuepuka jua kali ambalo litaunguza ngozi, kuikausha na kuifanya iwe na makunyanzi na vitu vingine vinavyoota kwenye ngozi kutokana na jua.

Tumia vipodozi vizuri vinavyosaidia ngozi kuwa laini bila kuidhuru. Hapa kuna vipodozi vya aina mbali mbali na vinavyofanya kazi kwa njia mbali mbali. Vipodozi vya muhimu ni

  1. Vipodozi vya kuongeza unyevu au maji kwenye (seli za) ngozi
  2. Kwa kiingereza vinaitwa “Moisturizers”. Hivi hufanya kazi ya kufunika ngozi na kuzuia maji yasipotee kutoka kwenye ngozi, na pia husaidia kuongea maji kuingia kwenye seli za ngozi. Vipo katika mtindo wa sabuni, mafuta na losheni.
  3. Vipodozi vya kusaidia kuongeza kasi ya kuzalishwa kwa seli mpya za ngozi
  4. Hivi husaidia kuzalisha seli mpya za ngozi ambazo zitaleta ngozi mpya na nzuri na kuondoa ile ya zamani iliyochoka na kuzeeka. Mifano ni losheni na krimu zenye Vitamini A na Vitamini E.
  5. Vipodozi vya kusaidia kuondoa uchafu na seli (ngozi) zilizozeeka au kufa

Tumia sabuni zenye uwezo mkubwa wa kuondoa uchafu kutoka kwenye ngozi, na ukiweza tumia “face wash” au “facial cleansers”. Hivi husaidia kusafisha kabisa ngozi na kuondoa uchafu.

Kwa upande wa seli zilizokufa na kubaki juu ya ngozi tumia “scrub”. Scrub hufanya kazi kwa kuondoa seli zilizoharibika na zilizokufa na kuacha seli changa na ngozi nzuri.

USHAURI:

  1. Pata ushauri wa kulainisha na kupendezesha ngozi yako kutoka kwa wataalam wanaojua vizuri afya, urembo na vipodozi. Utashauriwa vizuri jinsi ya kufanya, vipodozi vya kutumia na jinsi ya kuvitumia vizuri kwa matokeo mazuri zaidi. Epuka wauza vipodozi wasio waaminifu au wasiovijua vizuri vipodozi, maana wanaweza kukupa vipodozi vya tofauti na mahitaji yako au vipodozi vinavyodhuru afya yako.
  2. Safisha ngozi yako vizuri, kila siku. Hakikisha unaondoa uchafu na vijidudu vyote vinavyotua na kukaa juu ya ngozi yako. Ondoa vumbi, seli zilizokufa, mafuta ya ziada, jasho nk Lala na pumzisha ngozi yako kiasi cha kutosha ili iweze kujitengeneza na kuwa nzuri. Ipumzishe kila siku kwa matokeo mazuri zaidi. Pata usingizi wa kutosha na ulio bora
  3. Tumia vipodozi vizuri vyenye uwezo wa kukupa matokeo mazuri unayoyataka na visivyodhuru afya yako. Pata ushauri mzuri kutoka kwa wataalam ili uweze kufanikisha hili vizuri. Tumia vipodozi vinavyoendana na ngozi yako. Kama ngozi yako ni kavu tumia vipodozi ambavyo ni maalum kwa ajili ya ngozi kavu, na kama ngozi yako ni ya mafuta basi tumia vipodozi ambavyo ni mahususi kwa ajili ya ngozi ya mafuta.
  4. Usitumie vipodozi vinavyoharibu ngozi na kuihatarisha ngozi yako. Epuka vipodozi vyote visivyo salama na vile visivyoendana na ngozi yako.
  5. Jihadhari na michubuko au majeraha mengine yoyote yatakayoweza kuharibu ngozi yako. Hii ni kwa sababu michubuko na majeraha hayo yatakuharibia uzuri wa ngozi yako na pia yatakuachia makovu baada ya kupona
  6. Kuwa na furaha, amani na tabasamu itakusaidia pia kuwa na ngozi nzuri, hususan ngozi ya usoni.
Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About