Dondoo za Urembo na Mitindo

Faida za kuogea maji ya Moto

Watu wengi hupendelea kutumia maji ya moto kuoga pale hali ya hewa inapobadilika na kuwa ya baridi au wakati mwingine mtu anaumwa hivyo anatumia maji ya moto.
Sehemu kama Dar es Salaam ni mara cheche utakuta wakazi wake wanaogea maji ya moto kutokana na hali ya joto katika jiji hilo.

Lakini kwa ajili ya urembo na afya ya ngozi, maji ya moto yanatajwa kuwa ni kitu muhimu sana kama vilivyo vipodozi vingine vinavyoisaida ngozi yako kuwa nyororo.

Hizi hapa ni baadhi ya faida zitokanazo na matumizi ya maji ya moto angalau mara tatu kwa wiki

Kulainisha na kutunza ngozi

Maji ya moto husaidia kulainisha ngozi yako tofauti na ukitumia maji ya baridi. Maji ya moto hasa yaliyo katika jakuzi ambapo utatumia muda mrefu kidogo ngozi yako ikiwa kwenye maji, husaidia kuilainisha ngozi yako na kuiweka katika hali nzuri.

Usingizi

Kama huwa unapata matatizo kupata usingizi usiku, amka oga kwa kutumia maji ya moto kwani husaidia kulainisha misuli ya mwili wako na itakaa sawa na utaweza kupata usinngizi.

Kukuweka katika hali nzuri

Kuna wakati mwingine mtu hujisikia uchovu wa mwili na kutotaka kufanya chochote (Off mood). Ukioga kwa maji ya moto yatakusaida kukuondolea uchovu na utajisikia mwenye nguvu na upo tayari kukabiliana na changamoto za siku.

Kuchangamsha ubongo

Unapooga kwa kutumia maji ya moto husaidia kuchangamsha ubongo na kuufanya uweze kufanyakazi kwa ufanisi na kwa haraka zaidi.

Kushusha shinikizo la damu

Ukiachanna na masuala ya urembo, kuoga maji ya moto kunatajwa kuwa ni njia ya haraka ya kusaidia kushusha shinikizo la damu. Tafiti zinaonyesha kuwa mtu mwenye shinikizo la damu la kupanda, akioga kwa maji ya moto husaidia kushusha.

Kusaidia mzunguko wa damu

Ukioga kwa kutumia maji ya moto husaidia kusisimu na kuitanua mishipa ya damu hivyo kuwezesha damu kuwa na mzunguko mzuri mwilini.

Licha ya kuwa maji ya moto ni mazuri kiafya, unashauriwa kuto oga kwa maji ya moto sana kwani huathiri ngozi.

Madhara ya Uvaaji wa Wigi au nywele Bandia

Katika miongo kadhaa iliyopita, uvaaji wa wigi umekuwa fasheni katika sekta ya urembo na hutumika hususani na wanawake. Ingawa uvaaji wa wigi huwafanya wanawake hao kuonekana mithili ya mtu aliyevaa kofia ngumu (helmet), lakini yaonekana ni mapendeleo ya wengi.

Wanaume wengi hujiuliza , “Ni kwanini kina mama hupendelea kuvaa wigi na kusuka nywele za bandia?, wakati hupendeza na kuwa warembo zaidi wakiwa na nywele zao za asili”?

Wigi huvaliwa zaidi na kinamama wenye asili ya Afrika au Wamarekani wa asili ya Afrika. Lakini tukiangalia moja ya chimbuko hasa la uvaaji wigi ni ubaguzi uliokuwepo wakati wa utumwa ambapo wale wenye ngozi nyeupe na nywele shombeshombe walipewa kazi za ndani na wale wasio na ngozi nyeupe na nywele zisizo shombeshombe walifanyishwa kazi ngumu za mashambani.

Watumwa waliopelekwa barani Amerika hawakuweza kuzihudumia nywele zao kutokana na hali ngumu, na mabwenyenye waliwashusha hadhi na kuwavunja moyo kwa kuwaambia hawakuwa na nywele bali ni “manyoya”.

Lakini sababu nyingine inayodhaniwa kuwaathiri wanawake wa asili ya Afrika ni fikra kuwa mwanamke mwenye nywele ndefu pengine hadi mgongoni ni mrembo zaidi. Pia siku hizi warembo na wanaoshiriki katika mashindano ya urembo hujaribu kurefusha nywele zao ili kuwa na viwango na aina za mitindo ya ughaibuni.

Pamoja na kuwa wanawake wanajaribu kuwa warembo kwa uvaaji wa wigi, zifuatazo ni baadhi ya hasara au madhara kiafya ya uvaaji wigi na usukaji wa nywele za bandia.

Uvaaji wa wigi au nywele za bandia waweza kukusababishia mzio (allergy), endapo malighafi au kemikali zilizotumika kutengeneza wigi hiyo zitasisimua mfumo wa kinga ya mwili wa mvaaji.

Kupata m-ba ni tatizo jingine kutokana na uvaaji wigi, hii hutokana na kukosekana kwa hewa ya kutosha ya Oksijeni katika ngozi ya kichwa (scalp hypoxia) na katika tishu za shina la nywele. Kwa hiyo kama utaamua kuvaa wigi uhakikishe imetengenezwa kwa viwango vya ubora unaotakiwa na inapitisha hewa ya kutosha ya Oksijeni.

Pia waweza kunyonyoka nywele hata kama una nywele nzuri zenye afya, na kama utachagua kuvaa wigi na unataka kuepuka madhara hakikisha kuwa nywele zako ni safi, usilazimishe kuvaa wigi iliyo ndogo na yenye kubana sana, hakikisha unapata muda wa kupata hewa na nywele zako zinapakwa mafuta kuepuka ukavu wa ngozi ya kichwa na nywele kukatika .

Maumivu ya kichwa ni tatizo ambalo laweza kusababishwa na uvaaji wigi au usukaji wa nywele bandia. Wigi iliyo ndogo husababisha mkandamizo kichwani na kusababisha maumivu ya kichwa ya mara kwa mara.

Upotevu wa muda na fedha ni dhahiri kwa kuwa ufumaji wa nywele za bandia waweza kuchukua muda mrefu, itamlazimu mvaaji wigi kubadili kwa kununua mpya kila baada ya muda fulani au kuwa na wigi nyingi kwa ajili kubadili kulingana na fasheni.

Harufu mbaya huweza kujitokeza endapo mba na jasho vitachanganyikana na hupelekea uwepo wa bakteria au fangasi na kusababisha muwasho mkali, hii yaweza kumkosesha raha mvaaji wigi na mwenye kufuma nywele za bandia hasa pale anapokuwa katika majumuiko ya kijamii.Kama utachagua kuvaa wigi hakikisha nywele zako zinasafishwa na shampoo au sabuni, zinakaushwa vizuri na kupakwa mafuta.

Endapo mwanamama atachagua kuvaa wigi,asisahau kuwa nywele zake za asili zinahitaji matunzo,na azingatie wakati wa kununua wigi au nywele za bandia, ahakikishe ananunua yenye ubora unaotakiwa ili kuepuka madhara ya kiafya anayoweza pata kutokana na uvaaji wigi au anapofuma nywele za bandia.

Benson Chonya

Jinsi ya kutunza kucha kujiepusha na maradhi shambulizi ya Kucha

Mikono, viganja na vidole ni kati ya sehemu muhimu katika mwili wa msichana. Mikono hutumika kufanya shughuli nyingi za nyumbani, shuleni na sehemu mbalimbali katika maisha kuanzia kutandika kitanda, kupika, kufanya usafi, kuandika, kujiremba pamoja na majukumu mengine mengi.

Mikono isipotunzwa vizuri ni rahisi sana kuharibika, kupoteza mvuto wake wa asili na kuharibu afya ya kucha. Hitaji la urembo wakati mwingine humsukuma msichana katika matumizi ya vipodozi vya kupaka kwenye kucha zake ili kukamilisha urembo wake.

Urembo wa vidole na kucha sio lazima ufanyike katika saluni au kwa wataalamu wa kupamba kucha, msichana anaweza kushughulikia afya na urembo wa vidole na kucha zake kwa gharama nafuu na kwa muda ambao mwenyewe anaona unafaa kufanya hivyo hata akiwa nyumbani.

Hii pia itamsaidia Msichana kuchagua vipodozi salama kwa afya ya kucha zake na mwili kwa ujumla. Ni jambo la muhimu kufahamu kuwa baadhi ya vipodozi vinavyotumika katika urembo wa kucha, vina rangi na sumu zisizofaa kwa afya. Sumu kama vile ‘Formaldehyde na Toluene’ zinazopatikana katika baadhi ya rangi za kucha zina madhara kwa afya ya msichana.

Ni kweli kuwa kucha nzuri huongeza urembo, mvuto na furaha ya msichana lakini pia ni busara kukumbuka kuwa afya ni muhimu kuliko urembo na uzuri. Afya ya mwili na kucha za msichana kwa ujumla hutegemea chakula bora chenye protein, madini na vitamini na siyo rangi na vipodozi.

Upungufu wa vitamini A, B Complex, proteni, madini ya chuma na chokaa (kalishiamu) mwilini husababisha kucha zipoteze afya yake ya asili. Kucha ambazo hazina afya zinaweza kuoza, kukauka, kupinda, kupasuka au kuwa na umbo kama kijiko. Magonjwa ya kuvu (fungus), na baadhi ya dawa za kupunguza makali ya virusi pia huharibu afya ya kucha. Mojawapo ya athari za dawa za kupunguza makali ya VVU aina ya Zidovudine (ZDV) ni kucha kuwa na rangi nyeusi.

Kwa ajili ya afya bora ya kucha msichana anashauriwa kula mboga za majani, maharage, korosho, asali na matunda kwa wingi kila siku. Usafi wa kucha kila siku kwa kuziosha kwa maji ya uvuguvugu na sabuni laini pamoja na brashi ndogo ya mikono huimarisha afya ya kucha. Kucha pia zinaweza kusafishwa kwa maji ya mmea wa mshubiri (Aloevera), kitunguu saumu kilichopondwa pondwa au kitunguu maji kisha viganja na vidole vikaushwe vizuri na kupaka losheni.

Kucha za msichana zinatakiwa zisiwe ndefu ili kuepuka utunzaji wa vimelea vinavyosababisha magonjwa na kurahisisha utunzaji na usafi wa kucha. Kucha ndefu zinaweza kuwa chanzo cha hatari kwa afya ya msichana na familia yake hasa pale msichana anapohusika na uandaaji wa chakula cha familia. Katika familia nyingi, hasa familia za kiafrika wasichana ndio wanaobeba wajibu na majukumu ya kuandaa chakula cha familia.

Kwa afya nzuri ya kucha, msichana anashauriwa kukata kucha zake ili ziwe fupi kadri anavyotaka kwa kutumia ‘nail cutter’ au mkasi mdogo au wembe mpya ambao haujatumiwa na mtu mwingine. Kuchangia nyembe za kukatia kucha si salama kwani kunaweza kuwa njia mojawapo ya kusambaza vimelea vya magonjwa hatari ya kuambukiza kama vile virusi vinavyosababisha UKIMWI na ugonjwa wa homa ya ini.

Ni vizuri kulainisha ncha za kucha baada ya kuzikata kwa kutumia tupa ya kucha (nail file) na kuzisugua kuelekea upande mmoja ili kuepuka kucha zisivunjike au zisisababishe michubuko ya ngozi wakati wa kujikuna. Kusugua kucha kwa kwenda mbele na nyuma kunaweza kusababisha kucha zivunjike kwa urahisi na haraka.

Kwa afya njema ya kucha, msichana pia anashauriwa asifungue pini za barua au kukwangua vocha za simu kwa kutumia kucha. Kucha zisikatwe kwa kutumia meno na zisilowekwe kwenye maji kwa muda mrefu hasa pale maji hayo yanapokuwa na kemikali au sabuni.

Kwa ajili ya afya njema ya kucha za miguuni, ni muhimu kuhakikisha kuwa, viatu kabla ya kuvaliwa vinakuwa vikavu na safi kabisa. Viatu visipotumiwa pia vihifadhiwe sehemu kavu isiyo na vumbi, maji au unyevunyevu ili kuepusha visiwe makazi ya kuvu (fungus)

Mambo ya Msingi kujua kuhusu uvaaji wa Tai

Kuna mambo mengi ya kufanya ili tuwe watu wa kuvutia kila wakati.Mpangilio wa mavazi hufanya mtu kuonekana maridadi.

Kama wewe ni mvaaji wa tai unapovaa unazingatia mambo yapi? Na je unafunga tai yako kwa namna inayokubalika?

Wengine huwa hawafahamu jinsi ya kufunga tai na hivyo kuleta mushkeri wakati wa kuvaa tai na kusababisha tai kukaa upande. Unapoamua kuvaa tai na shati ambalo halijanyooshwa ambalo linakuwa kwenye mikunjo au kuvaa tai na ndala unakuwa umeua maananzima na kulivunjia heshima vazi hili.

Tai ni vazi lawatu walio maridadi kama huwezi kuwa maridadi basi vazi hili halikufai kabisa.
Unapovaa taa unatakiwa kuzingatia aina ya umbo lako kama wewe ni mnene vaa tai inayoendana na mtu mnene na kama wewe ni mwembamba basi vaa tai inayoendana na mtu mwembamba.

Kuna wengine huvaa tai zinazofika magotini na kuwa kichekesho anapopita mtaani
Tai ni vazi ambalo huongeza heshima na hadhi ya mvaaji cha muhimu ni jinsi gani unavaa tai yako na ikiwezekana jaribu kumechisha tai na suruali kwa vile ili tai upendeze ni laima iendane na nguo unayovaa.

Ni vyema ukahakikisha kuwa unakuwa na tai zenye rangi tofauti ambazo zitaendana na nguo unazovaa.

Jinsi ya kufanya ili uwe na umbo dogo la kuvutia

Unaweza kujiuliza, hivi inawezekanaje kuwa na umbo dogo la aina hii? Ukweli ni kwamba inawezekana, lakini inahitaji kazi ya ziada kufikia kwenye lengo hilo.

Unalifahamu umbile la sifuri au saizi zero?

Kwa wale wanaojali maumbo ya kupendeza saizi zero linatafsiriwa ni kuwa na kiuno kisichozidi inchi 23, nyonga 32 na kifua 31. Kikubwa unachotakiwa kuzingatia ni mazoezi na ulaji wako, kwa kuwa mwangalifu katika kiasi cha kalori unachoingiza mwilini kila siku.

Unatakiwa kuwa mwadilifu katika uchaguaji wako wa chakula, haimaanishi ukae na njaa. Inawezekana ikawa ni vigumu kuelewa makala haya.

Kinachosisitizwa katika mpango huu, ni kuwa waangalifu katika upangiliaji wa vyakula. Aina hii ya mpangilio wa ulaji inafahamika zaidi kitaalamu kama ‘crash diet’ Kula kiasi cha kalori 400- 500 kwa siku. Lakini unatakiwa kufanya mazoezi angalau kwa saa mbili kwa siku, ili kupunguza mara mbili ya kiasi cha mafuta uliyokula katika siku hiyo.

Kunywa maji kwa wingi:

Kwa kunywa kiasi kikubwa cha maji itakusaidia kurahisisha umeng’enyaji wa chakula mwilini. Ni vyema mwili wako ukawa na maji ya kutosha ikiwa umeingia kwenye mpango huu wa ulaji Kula mboga za kijani: Zina Vitamini, protini na virutubisho vingine kwa wingi ambavyo ni muhimu kwa afya. Kama ilivyoainisha awali, utaratibu huu hauhamasishi kukaa na njaa, bali kula vyakula vilivyo bora kiafya.

Kula vyakula visivyokobolewa.

Mara nyingi vyakula vya aina hii, huwa na virutubisho muhimu na vinavyohitajika katika ustawi wa mwili.

Punguza wanga katika mlo wako.

Badala yake unaweza kula protini na kuingiza vyakula kama mayai na samaki kwenye mlo wako.

Epuka kula vyakula vya mtaani.

Vyakula kama chips, mihogo ya kukaanga na jamii yake vinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzito wa mwili na pia hulifanya zoezi la umeng’enywaji wa chakula tumboni kuwa gumu.

Kula supu za mbogamboga;

Supu kama ya kabichi licha ya kujaza tumbo, husaidia katika kurahisisha mfumo wa umeng’enyaji chakula tumboni.

Kula saladi na matunda kwa wingi.

Hii itasaidia kukuweka sawa kiafya.

Jizuie kula vyakula vyenye sukari nyingi na hata vile vya mtaani unavyohisi vinaweza kukwamisha mpango wako wa kupungua.

Lakini pamoja na yote jipe mazoezi ya kutosha kama kukimbia, kuruka kamba au mazoezi ya kupunguza tumbo na maziwa

Jinsi ya Kutumia Bamia kuondoa chunusi Usoni

Wiki hii kwenye urembo tutaongelea mboga aina ya bamia jinsi inavyotibu chunusi na kuziondoa moja kwa moja. Mbali na chunusi, pia husababisha ngozi kuteleza na kuwa nyororo.

JINSI YA KUFANYA

Chukua bamia zikatekate vipande, ziweke kwenye brenda kisha chukua limao kipande na maji kidogo, weka kwenye brenda kisha saga. Baada ya kupata mchanganyiko wako upake usoni mpaka kwenye shingo, acha kwa muda likauke kisha bandua kama unavyoondoa maski nyingine usoni.

FANYA HIVI SIKU TATU KWA WIKI ITAKUSAIDIA KUONDOA CHUNUSI.

Utengenezaji wa Makalio ni Hatari na Hutakiwi kufanya

Mwanamke wa miaka mitatu amefariki baada ya kuripotiwa kuelekea Uturuki kwa aina ya upasuaji kwa jina Brazilian Butt Lift [uongezaji wa makalio}.

Ni kwa nini upasuaji huu ni maarufu mbali na kwamba ni hatari kufanyiwa upasuaji huo ughaibuni.

Leah Cambridge kutoka Leeds alipatikana na mishtuko mitatu ya moyo baada ya kudungwa sindano ya ganzi katika kliniki moja katika mji wa Izmir, mwenzake Scott Franks aliambia gazeti la the sun.

Anaeleweka kufanyiwa BBL ama upasuaji wa kuongeza makalio ambapo mafuta kutoka katika tumbo hutiwa katika makalio.

‘Mrembo huyo alikubali kufanya upasuaji ughaibuni ambapo ni bei nafuu ikilinganishwa na Uingereza baada ya kukerwa na mafuta mengi katika sehemu yake ya tumbo baada ya kupata watoto’, alisema bwana Frank.

Majirani wake wamemtaja kuwa mtu anayevutia, wakiongezea kuwa wanaamini alielekea kufanyiwa upasuaji huo mwezi uliopita bila kumshauri mpenziwe.

Na bi Cambridge sio mwanamke wa kwanza Muingereza ambaye hamu yake ya kuwa na makalio ya kuvutia yalimwangamiza akiwa ughaibuni.

Joy Williams alifanyiwa upasuaji wa kuongeza makalio yake mjini Bangkon nchini Thailand mnamo mwezi Octoba 2014.

Vidonda vyake vilipata maambukizi na mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 24 kutoka mjini London , alifariki akidungwa sindano ya ganzi.

Miaka mitatu kabla , Claudia Aderotimi mwenye umri wa miaka 20 , kutoka Hackney , mashariki mwa London alifariki kutokana na matibabu ya kujiongeza makalio yake katika hoteli moja nchini Marekani.

Upasuaji wa kuongeza makalio hauonekani kuwa hatari zaidi ya aina nyengine zozote za upasuaji, kulingana na daktari wa upasuaji wa urembo Bryan Mayou.

‘Hatari yake ni upasuaji huo kufanywa na madaktari ambao hawajahitimu, nje ya kliniki bila kuwa na maelezo ya jinsi ya kujichunga baada ya matibabu hayo kufanywa’, anasema bwana Mayou, mwanachama wa muungano wa madaktari wa upasuaji nchini Uingereza.

Iwapo mafuta yataingizwa katika tishu ya sehemu ya makalio kuna hatari ya kuingiza mafuta hayo katika mishipa mikubwa ya damu.

Mafuta hayo yanaweza kupita katika mishipa ya damu , kuingia katika mapafu kabla ya kusababisha kifo.

Bwana Frank aliambia gazeti la The sun : Leah alikuwa amedungwa sindano ya ganzi akakumbwa na matatizo baada ya mafuta kuingia katika mishipa yake ya damu hatua iliofanya viwango vyake vya oxygen katika damu kushuka .

Hali yake iliimarishwa lakini alikumbwa na mishtuko mitatu ya moyo na hawakuwa na la kufanya.

‘Madaktari wa upasuaji kutoka jamii za kimataifa wameunda jopo kuchunguza kuripoti kuhusu utaratibu huo”, anasema Mayou.

‘Viwango vya vifo vinavyotokana na utaratibu huo ni kisa kimoja kati ya 3000 huku vifo vyote vilivyochunguzwa vikihusisha mafuta yaliopatikana ndani ya mishipa ya misuli ya makalio’, anasema.

Ni mtindo wa kisasa, miaka kadhaa iliopita kila mtu alipendelea kuwa mwembamba na walikuwa wakisema kuwa wanataka kufanyiwa upasuji ili kufanya makalio yao kuwa madogo.

‘Na hiyo ndio mbinu ambayo inaweza kutumika iwapo mtindo mpya wa kuongeza makalio utakwisha na mwathiriwa anataka makalio yake kurudishwa yalivyokuwa’, anasema.

Kwa nini watu wanapendelea sana kuwa na makalio makubwa ? ni kutokana na utamaduni maarufu wa kushabikia maungo yanayovutia.

Watu maarufu kama vile Kim Kardashian , Kylie Jenner na Cardi B wana umaarufu mkubwa katika mitandao ya kijmaii ambapo huchapisha picha zao wakionyesha makalio yao yalio mviringo.

Jenner alichapisha katika blogi yake ambapo alisifu maumbile yake na uzani ulioongezeka.

”Sijaongezewa makalio. Unajua, nilikuwa na uzani wa 120 [lbs]. Nilikuwa mwembamba sana. Sasa nianelekea 136Ibs , lakini ni sawa napendelea uzani nilionao”.

Hatahivyo, Cardi B amefichua kwamba kabla ya kuingia katika fani ya muziki aliongezewa makalio huko mjini New York na kifaa alichowekewa ndani kilivuja kwa siku tano baadaye.

Katika mahojiano alisema kuwa alilipa takriban $800 (£564) kwa upasuaji huo baada ya kuwaona wachezaji densi wanzake walio uchi katika vilabu vya burudani walio na makalio makubwa wakipata fedha nyingi kumliko.

Chloe Simms, ambaye ni nyota wa kipindi cha runinga cha The Only Way Is Essex, amekuwa wazi kuhusu makalio yake aliyoongezewa baada ya kulalamika katika kipindi hicho kwamba alikuwa hana makalio.

Mambo ya Kuzingatia ili uwe mrembo siku zote

Katika Jamii nyingi duniani, dhana ya urembo imekuwa na mitazamo tofauti kwa watu wengi. Kila mmoja anautafakari urembo kwa namna yake kulingana na malezi na tamaduni za mahali husika. Wako wanaoamini kuwa mrembo ni lazima awe na ngozi nyeupe, wengine hudhani kuwa ili kuonekana mrembo, lazima uwe na nywele ndefu, lakini pia wapo wanaodhani kwamba ili uwe mrembo ni lazima uwe na umbo namba nane na wapo wanaojua urembo ni kuwa mwembamba (kimbaumbau au Miss) au kuwa mrefu na wapo wanaoamini urembo ni kuwa mnene.

Hiyo yote ni mitazamo tu, lakini tafsiri halisi kutoka kwa wataalamu wa urembo ni kwamba; urembo ni hali ya kuwa na afya bora.

Je, Mpenzi msomaji ulikuwa unajua hili? Nakuomba Kabla hujafanya chochote kuhusu afya yako, unatakiwa kuamini kwamba wewe ni mrembo. Ikiwa utasimama katika hilo ni kweli utakuwa mrembo siku zote. Basi ili kubaki kuwa mrembo tujifunze haya machache leo ya kufanya:

1. SAFISHA NGOZI YAKO:

Hakikisha ngozi yako inakuwa safi muda wote. Unaweza kutumia njia mbalimbali kama vile kuondoa ngozi zilizokufa mara kwa mara. Kuondoa mafuta yaliyogandamana katika ngozi kwa kufanyia masaji ngozi yako ili kurahisisha mzunguko wa damu yako.
Ikiwa hili litafanyika kwa umakini ni wazi kuwa matatizo ya kuwa na chunusi au weusi katika ngozi yako havitakuwepo kwako.

2. SAFISHA NYWELE ZAKO:

Tumia bidhaa za nywele, ambazo zinaendana na nywele zako na hakikisha unazingatia mambo muhimu katika uboreshaji wa nywele zako.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kutokutumia vifaa vinavyounguza vywele.

Epuka kuosha nywele kwa maji ya moto, pia kuchana nywele zikiwa na maji, kwani unaweza kusababisha kukatika kwa nywele zako.

3. USIPAKE VIPODOZI MARA KWA MARA:

Tumia vipodozi pale inapobidi, usipendelee kutumia vipodozi mara kwa mara kwani wakati mwingine matumizi ya mara kwa mara ya vipodozi, husababisha madhara katika ngozi yako, hasa unapotumia bila kufuata maelekezo ya wataalamu.

4. PATA USINGIZI WA KUTOSHA:

Hakikisha unapata usingizi wa kutosha kila siku. Kwa mujibu wa wataalamu, unatakiwa kulala si chini ya saa nane kila siku. Ikiwa utapata usingizi wa kutosha ni wazi kuwa macho yako yataonekana yenye nuru siku zote. Pia utazidi kuonekana kuwa mrembo zaidi.

5. FANYA MAZOEZI YA VIUNGO:

Hakikisha mazoezi yanakuwa sehemu ya maisha yako, hii itasaidia kukufanya uonekane siyo tu mrembo, bali pia mwenye kujiamini.

6. SAFISHA MENO YAKO:

Usafi wa meno pia ni miongoni mwa mambo ya kuzingatia unapoamua kuboresha urembo wako. Hakikisha unapiga mswaki walau mara mbili kwa siku kila siku au kila baada ya kula.

Haya yameorodheshwa na wataalamu mbalimbali kuwa ni mambo yanayochangia urembo wa asili na mvuto wa ngozi na mwili.

Namna nzuri ya kutunza Hips na Makalio

KUNA kitu ambacho wengi wetu huwa hawakifikirii nacho ni makalio. Makalio yetu ndiyo yanatoa shepu fulani kwa mwanamke katika vivazi na ukiyaachia ovyo yanaweza kukuletea mushkeli na kama ukiyatengeneza kama yale makalio yanayosifiwa sana na watu wa Televisheni ya Jeniffer Lopez hayawezi kufua dafu.

Wanawake wengi kwa sasa wanakwenda kuboresha makalio yao ili kuyapatia ukubwa unaostahili kwa jinsi wao wanavyopenda.

Tatizo hili halipo hapa nchini lakini wapo walionituipia swali sasa inabidi nikiri kuwa lipo sana marekani na mpasuaji wa masuala ya urembo wa Miani Dk Costantino Mendieta amethibitisha.
Katika fasihi yake mtaalam huyo amezungumzia sana utunzaji wa makalio kwa kuyagawa katika madaraja manne.

Anasema makalio daraja la kwanza ndiyo yanayotakiwa sana > Ni kama vile umechukua moyo halafu ukaugeuza chini juu haya ndiyo dizaini ambayo Marekani wanalilia sana. Watu wa huko wanajimwaga katika majumba ya upasuaji kupata shepu hiyo adimu.

Hatua hizo ni kama ifuatavyo.

1.fanya masaji na losheni zinazoimarisha na kutengeneza ngozi mwororo katika mapaja yako ukianzia chini ya makalio mara mbili kwa siku.

2.Ondoa miinuko midogo midogo isiyotakiwa ni yako kwa kuskrabu mara mbili au tatu kwa wiki ukitumia salt scrub.

3.Pamoja na matatizo ya michuchumio, ivae ili kukupa nafasi ya kutembea kwa miondoko ya twiga inayotoa nafasi nzuri kwa makalio kuwa na mvuto.

4.tafuta namna nzuri ya kuficha michirizi ya kunyooka kwa misuli ya mwili.

5.Mazoezi yatakufanya uwe mtu tofauti zaidi pandisha ngazi kwa dakika kumi au zaidi na chukua mazoezi ya kubana makalio yako na sehemu za kiuno kwa kusukuma kwa ndani na kutulia hivyo kwa sekunde tano na kujiachia na unaweza kufanya hivyo unavyotaka.

Pia unaweza kuongeza uzuri wa makalio yako kwa kuhakikisha unakula vyema na unakula inavyostahili

Jinsi ya Kutumia Papai na Asali kuondoa Madoa Usoni

KUMEKUWA na sababu mbalimbali zinazofanya watu kutokuwa na ngozi zisizokubalika.Mbali na hali ya hewa pia matumizi ya pombe na sigara hata matumizi ya cream kali ambazo zimekuwa zikitumiwa na watu bila kujua madhara yake kumechangia kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.

Ngozi kwa kawaida inatakiwa ijitengeneze yenyewe na si kuitengeneza kwa vipodozi kama wengi wanavyodhani. Ulaji wa matunda na mboga za majani kwa wingi kunywa glasi nane za maji kwa siku ni njia nzuri kama unataka kuwa na ngozi nzuri isiyo na madoa wala ukavu ambao haupendezi.

Wengi wanaacha kula mbogamboga na matunda kwa wingi hata kutokunywa maji ya kutosha na badala yake wamekuwa akitegemea kuwa na ngozi nzuri jambo ambalo ni gumu.Mara kadhaa tumeshuhudia watu wanaopaka cream kali wakiwa kama wameungua usoni huku uso na mwili ukionekana kuwa makavu jambo ambalo linaashiria kuwa kupaka cream si suruhisho la kuwa na ngozi nzuri.

Kuna watu wamekuwa na ngozi za asili na hata unapowauliza baadhi yao hawajawahi kupaka cream hata siku moja na bado wana ngozi nzuri zinazovutia hao wamekuwa wakila kwa ajili ya kuhakikisha wanatengeneza ngozi zao kutoka ndani.

Pia wengi wanaharibu ngozi zao na kuwa na madoa kutokana na kutumia make up kwa muda mrefu na hata anapogundua kuwa ana tatizo la madoa amekuwa akijaribu kutumia cream nyingine kwa ajili ya kumaliza tatizo hilo jambo ambali linazidisha madhara kwenye ngozi.

Unaweza kutibu ngozi yenye madoa usoni pia mashavuni kwa kujitibu na juisi ya limao.

Namna ya kufanya

Chukua limao lioshe na kisha likamue na kuchuja mbegu zake. Weka juisi hiyo kwenye kikombe na kisha tafuta kitambaa laini kichovye kwenye juisi ya limao na dondoshea juisi ya limao kwenye sehemu zenye tatizo.

Kaa kama dakika tano kisha usha uso kwa maji safi.Pia unaweza kuchanganya na asali mbichi na maji ya limao husaidia pia kuondoa madoa usoni.

Limao lina sifa kubwa ya kuzuia harufu pia unaweza kulitumia katika kuondoa harufu kali ya jasho mwilini na husaidia kuondoa weusi kwenye kwapa, chini ya macho, mapajani pia.

Chukua kipande cha limao weka sukari kidogo, sugua.Unatakiwa kutumia kwenye kwapa ambalo ni safi, vizuri kutumia njia hii kabla na baada ya kuoga.

Mavazi Mazuri kwa wanawake wanene

Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiangaika kupata aina ya nguo za kuvaa tena hasa wanawake wanene, kutokana na maumbo yao wanaona ni kazi sana kutafuta nguo, wengine hukosa hata uhuru wa kutoka out na watu wao wa karibu kwa sababu tu wanakosa nguo.Wengi ujikuta wakichagua nguo pana pana ili kuficha maumbo yao, lakini kumbe unaweza kuwa huru sana na mwili wako.

Zifuatazo ni badhi ya tips zinazoweza kukusaidi kuchagua nguo za kuvaa kwa mwanamke mnene.Inawezekana nguo hizi unazo ndani lakini unashindwa kuzipangilia;

1. Kabla ya kuchagua nguo ni lazima kujua mwili wako una unene wa aina gani,ikiwa wewe ni mnene na unatumbo kubwa basi ni bora kuvaa gauni maana gauni uweza kukuweka vizuri na pia ni mazuri hasa kwa watu wanene.

2. Lakini pia kama wewe ni mnene na umebahatika kuwa na maziwa makubwa, ni vizuri kupendelea kuvaa nguo zenye v-shape, siri ya nguo hizi ni kwamba huwa na tabia ya kuficha ukubwa wa maziwa na kufanya uwe maridadi zaidi ila zingatia kuchagua brazia nzuri kuikaa blauzi yako sawia.

3. Kwa mwanamke mwenye hipsi anashauriwa kuvaa nguo zinakazo mfanya hasionyeshe sana hipsi zake tofauti ya yule hasiekuwa na hipsi , maana yeye anatakiwa kuvaa nguo itakavyo onyesha hipsi zake , hata hivyo kwa wanawake wanene wenye hipsi hawana haja ya kujibana sana kwa sababu hipsi huweza kujitokeza zenyewe tu.

4. Lakini pia kuchagua rangi ya nguo nzuri pia husaidia kupunguza au kuongeza umbile la mtu, kuna rangi huweza kukufanya ukawa mnene sana au mwembamba sana,kwa mfano nguo zenye mistari ya kulala sio nzuri kwa watu wanene maana hutanua miili yao.Lakini pia rangi za giza hupunguza muonekano wa unene ilihali rangi za mwanga huangaza na kufanya mtu aonekane sana.

Zingaia:

-Ni bora zaidi katika kuchagua rangi nguo za rangi nyeusi na nyeupe iliyochanganywa ni nzuri zaidi inafanya muonekano wa mtu uonekane maridadi zaidi.

-Lakini pia jitahidi kuvaa viatu vinavyoendana na mwili wako ,sio lazima kuvaa kiatu kirefu wakati mwili wako hauimili mikikimikiki ya kiatu kirefu, flatshoes pia hupendeza zaidi kwa mtu mnene .

Jinsi ya Kuondoa Makovu Mwilini

Makovu sio kidonda naomba hili uelewe, ila makovu ni alama ya majeraha ambayo yamebaki kwenye ngozi baada ya kupona majeraha.
Kuna baadhi ya watu husumbuliwa na shida ya kuwa na makovu sehemu mbalimbali ya mwili.
Hivyo kama wewe ni miongoni mwao maandishi haya yanakuhusu sana.

Zifuatazo ndizo mbinu za kuondoa makovu mwilini.

1. Tango

Unachotakiwa kufanya ni; Pondaponda tango na kisha kutumia mchanganyiko wake kwa kupaka juu ya kovu. Hii husaidia sana kulainisha makovu na ikiwa utatumia kwa muda mrefu huondoa makovu pia.

2. Aloe vera.

Unachotakiwa kufanya ni; kata majani hayo na utumie utomvu wake kupaka katika makovu kisha mara baada ya muda Fulani utaona mabadiliko na itapunguza na kuondoa makovu.

3. Asali

Unachotakiwa kufanya; Paka asali juu ya kovu na kuiacha usiku kucha. Rudia mara kwa mara kupaka asali hadi pale kovu litakapotoweka.

Madhara ya kuchora tattoo mwilini

Tattoo ni nini?
Hii ni uwekaji wa wino kwenye ngozi ya ndani kitaalamu kama dermis kubadilisha rangi kabisa maisha yako yote au kwa muda tu, inateemea na uwekaji..
Kwa dunia ya sasa kujichora tatoo ni kama fasheni fulani kwenye jamii, ukienda kuchora tattoo kuna uwezekano mkubwa sana isitoke maisha yako yote hivyo kwa usalama wako ni vizuri ukamuona mtaalamu wa tattoo ambaye ni maarufu na ana sifa kubwa katika shughuli hizo, anaweza kua ana gharama kubwa lakini binafsi itakusaidia.kwa sasa nchi ya marekani inaongoza kwa kua na watu wengi wenye tattoo duniani.

Hivyo kabla hujaamua kujichora tattoo basi madhara yake haya hapa..

Kansa ya ngozi; hapo mwanzoni wataalamu walikua wanasema hakuna mahusiano kati ya kansa ya ngozi na na tabia ya kujichora tattoo lakini hivi karibuni tafiti kutoka uingereza zinaonyesha kuna aina fulani za wino ambazo zinaweza kusababisha kansa zikitumika kuchora tattoo.

Allergy ya ngozi; haijalishi unaweka tattoo kwa muda au ya moja kwa moja kumetokea kesi nyingi za watu wanaopata allergy baada ya kupakwa tattoo, utafiti unaonyesha rangi nyekundu ndio inaongoza kwa kusababisha allergy hizo huku rangi zingine kama nyeusi, purple na zingine hazisababishi. mara nyingi allergy hizi huonekana mtu akikaa juani.

makovu; mwili unataambua tattoo kama adui wake hivyo hujaribu kuiondoa kwa njia mbalimbali na kwa kufanya hivyo husababisha makovu ya muda mrefu ambayo yanaweza kuleta magonjwa mengine ya ngozi.

Maambukizi ya ukimwi na ugonjwa wa hepatitis; tabia ya kurudia sindano zilezile wakati wa kuchora tattoo kunaweza kusababisha maambukizi ya virusi vya ukimwi na maambukizi ya virusi vinavyoshambulia ini kitaalamu kama hepatitis b. ugonjwa huu wa hepatitis b husababisha kansa ya ini ambayo haitibiki. ni vizuri kua makini ili uone kama sindano inayotumika kwako ni mpya.

Matatizo kipindi cha kufanya kipimo cha MRI; hichi kipimo ni cha mionzi na kirefu chake ni magnetic resonance imaging, hutumika kupima viungo vya mwili ambavyo havionekani kwa macho ndani ya mwili wa binadamu kama x ray inavyofanya. tatizo ni kwamba kipimo hiki kina sumaku kali kiasi kwamba mtu hatakiwi kuingia kwenye mtambo huo akiwa amevaa chuma chochote na hata kama kiko ndani ya mwili kitavutwa nje, sasa mara nyingi tattoo nyeusi hua imetengenezwa na compound kitaalamu kama iron oxide ambayo ina chembechembe za chuma. hii inaweza ikaleta changamoto kubwa kwenye vipimo.

Kubadilika kwa ngozi ya rangi; sehemu inayochorwa tattoo hubadilika moja kwa moja na kua na rangi tofauti, hakuna jinsi unaweza ukaitoa hiyo rangi tena, hata baada ya muda mrefu tattoo ikipungua nguvu lakini ngozi haiwezi kua kama zamani.

Hutaruhusiwa kuchangia damu; mara nyingi watu wenye tattoo hawaruhusiwi kuchangia damu kwani wana hatari ya kusambaza ugonjwa kwenda kwa mtu mwingine, kimsingi mtu aliyechora ndani ya muda mfupi ndio haruhusiwi lakini kwasababu wakati mwingine sio rahisi kutofautisha tattoo mpya na ya zamani basi hawa watu huwa hawaruhusiwi kabisa.mchezaji wa kimataifa christian ronaldo hachori tattoo kwa sababu ya hili.

Unaweza kukosa fursa mbalimbali; kuna kampuni mbalimbali duniani haziwapi watu kazi kwasababu wamechora tattoo kulingana na imani za kampuni husika lakini pia kazi yeyote ya jeshi duniani hairuhusu tattoo hivyo kama wewe unayesoma hapa umeshachora tattoo ujue kazi ya jeshi huna tena.

Tattoo huingiliana na matumizi ya dawa fulani; kama wewe unatumia dawa za kuzuia damu isingane mwilini ukichora tattoo inaweza kufanya utoke damu nyingi sana kwani dawa hizo huzuia uwezo wa mwili kukausha damu na kuponyesha vidonda.

Magonjwa ya ngozi; wakati mwingine bacteria huweza kuvamia sehemu zenye vidonda vya tattoo na kusababisha kutopona haraka, dalili huweza kua homa kali, maunivu makali na sehemu ya tattoo kuvimba.

Damu kuganda juu ya ngozi[haematoma]; hii husababishwa na kuvuja kwa damu nyingi chini ya ngozi, huonekana sana pembeni pembeni ya sehemu ambapo rangi ya tatoo imepita na huchelewesha kupona kwa kidonda.

Nini kifanyike kwa wanaopenda tattoo?

Siku hizi kuna tattoo zinachorwa juu ya ngozi kama hina na kuondoka baada ya muda fulani, hizi hazina madhara kabisa, huchorwa kwa bei ndogo na hukupa nafasi ya wewe kubadilisha tatoo za aina mbalimbali kwenye sehemu moja ya mwili.

Je tattoo inafutika?

Ni ngumu sana kuifuta tattoo na hii ni changamoto kwa watu ambao wamechora tattoo za majina au sura za wapenzi wao wa zamani. kuna kikaa kinaitwa laser ambacho kinaweza kutumika kufuta tattoo yote au sehemu ndogo tu ya tattoo. mara nyingi rangi nyeusi zinaweza kutoka ukilinganisha na rangi zingine. maumivu yanayotumiaka kuiondoa tattoo ni makali kuliko maumivu ya kuiweka na hapa kwetu tanzania siana uhakika kama huduma hii ya kuondoa tattoo ipo.

Mambo ya Kuzingatia Kama una ngozi Kavu na Kuepuka kuwa na ngozi kavu

Ngozi kavu inaweza kukufanya ukose raha kutokana na kuwasha mara kwa mara, lakini pia kupauka hii inaweza kusababisha mikunjo ya ngozi na hata kupatwa na vidonda katika ngozi. Ngozi kavu husababishwa na baridi lakini pia unaweza ukawa umezaliwa nayo tu upo hivyo. kama una ngozi ya aina hii basi haya ni mambo matatu ya kuyaepuka kufanya.

Kuoga maji ya moto kwa muda mrefu

Epuka kuoga maji ya moto mara kwa mara kunaweza kufanya yale mafuta natural yanayo moisturize mwili kukauka, ili kuepuka tatizo hili ni vyema ukatumia maji ya uvuguvugu au baridi katika kuoga au kunawa mwili wako.

kutumia vipodozi vyenye Alcohol Nyingi

Alcohol nyingi husababisha ngozi kuzidi kuwa kavu, wakati wa kwenda kununua vipodozi vyako hakikisha unasoma maelezo na kujua kiasi cha alcohol kilichopo kama ni nyingi usichukue chukua yenye kiasi kidogo.

Kuosha Ngozi Na Sabuni Mara Kwa Mara Na Kusugua Kwa Nguvu

Kuosha ngozi mara nyingi sana na sabuni ni njia ya mojawapo ya kupata ngozi kavu. Ngozi kavu iliyokasirika huathirika zaidi na maambukizi ya bakteria kwa sababu kuosha mara nyingi huondosha safu za kinga ya ngozi yako.

Matumizi ya Papai Katika Urembo

Tunda la kitropiki la papai lina vitamini C na E likiwa na siri kubwa ya urembo na hutumika kutengeneza facial za aina mbalimbali.
Papai limekuwa likitumiwa kama njoia boya ya kutunza uso wako na kumfanya mtu kuwa na ngozi ya asili.

Bidhaa ambazo zimekuwa zikitengenezwa kwa kutumia tunda la papai ni pamoja na sabuni, lotion, tona, moisturiza, facial peels na nyingine nyingi.

Ukitumia facial mask ya papai utakuwa na sura nzuri ya asili na kukupa uonekanaji mzuri wa uso wako. Facial mask hii huweza hutumika kwa watu wa umri na aina yoyote ya ngozi.

Facial mask ya papai ina nguvu ya kung’arisha uso wako.
Pia inasaidia ngozi ambayo imeshaanza kupatwa na makunyanzi kutokana na umri kuonekana ya kuvutia kwani pia imekuwa ikiondoa chunusi na makunyanzi pia.

Ni rahisi kutengeneza facial mask ya papai na ukitumia itakusaidia katika kukabiliana na ngozi iliyoanza kuchoka, kung’arisha ngozi.

Kuna na njia nzuri za kuhakikisha kuwa, tunakuwa na nyuso nzuri zenye kupendeza na kuvutia ikiwemo kutumia vitu vya asili pamoja na matunda ya aina mbalim ambayo husaidia zaidi katika kuimarisha ngozi.

Mask ya mchanganyiko wa papai yai na yai ni nzuri katika kuhakikisha kuwa unakuwa na ngozi nzuri na nyororo.

Njia hii pia husaidia hata wale wenye nyuso za mafuta ambao wamekuwa wakisumbuliwa na chunusi mara kwa mara kwa kufanya ngozi kuwa kavu.

Unaweza kutengeneza aina hii ya mask kwa kufanya yafuatayo:-
Chukua papai likate kasha toa mbegu na kasha lisage kwa kutumia blenda ya kuondaponda kwenye kibakuli kwa kutumia kitukama mchi mdogo wa kinu.

Kisha weka mchanganyiko huo kwenye chombo ulichokichagua kama kikombe au bakuli.
Vunja yai na koroga kuhakikisha kuwa mchanganyiko huo umechanganyika vizuri.
Safisha uso wako kwa kutumia cleanser au maji ya vuguvugu na uondoeuchafu wote ulioganda usoni.

  • Kisha paka mask kuzunguka uso wako, na unapopaka hakikisha kuwa,
  • mchanganyiko huo haugusi macho yako.
  • Osha uso wako baada ya dakika 15 kwa kutumia maji ya vuguvugu.
  • Jifute kwa kutumia taulo safi
  • Unaweza kupaka losheni, tona au moisturiza.

Husaidia kutunza ngozi na kuondoa vipele na uchafu ulioganda usoni.
Hii ni njia rahisi ya kutengeneza uso isiyo na gharama.

Jinsi ya Kuvaa hereni kwa Mpangilio kuongeza Mvuto wako

HERENI ni pambo linavoliwa masikioni na kwa kiasi kikubwa linachangia kuongeza mvuto na muonekano mzuri. Kuna aina nyingi za hereni katika tamaduni mbalimbali. Zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia vito vya thamani kama vile Dhahabu, Almasi, Shaba au Kopa.

Vilevile zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia malighafi za asili kama vile ubao, vifuu vya nazi, mfupa kioo na shanga ambazo zimekuwa zikivaliwa sana na wanawake wa kimasai. Hereni zilizotengenezwa kwa shanga zimekuwa zikiwavutia watu wengi kuvaa kutokana na nakshi zake za asili.

Mara nyingi uvaaji wa hereni unatakiwa kuzingatia aina ya nguo uliyovaa, hapo unatakiwa kucheza na rangi. Mpangilio wako wa nguo na hereni hata na viatu utakufanya uonekane maridadi muda wote.

Unapotoka kwenda katika shughuli zako, au uwapo nyumbani basi zingatia uvaaji wa hereni na nguo. Uvaaji usiozingatia mpangilio wa rangi na hereni zako huondoa ladha ya urembo na si rahisi kwa mtu mwingine kugundua umependeza.

Licha ya kuwa hapo awali hareni zilikuwa zikivaliwa na wanawake pekee lakini miaka ya hivi karibuni tunaona urembo huu unaanza kuwavutia baadhi ya wanaume hususan vijana wa mjini.

Kutokana na hilo kuna hereni ambazo zimetengenezwa maalum kwa kuvaliwa na wanaume, hizi huwa za kubana na huwa na umbo dogo ukilinganisha zile zinazopendwa kuvaliwa na wanawake.

Angalizo: Epuka kuvaa hereni zaidi ya moja katika tundu la sikio kwani kufanya hivyo kunaweza kupelekea ukubwa wa tundu kuongezeka na hatimaye nyama ya sikio kuchanika. Hereni nzito sana nazo huchangia kutokea kwa tatizo hili.

Uvaaji wa Tai na Maana yake

Wachambuzi wa mambo ya saikolojia wanasema kwamba kwa kuchukua tai na kulivaa ile rangi ndiyo itakayoweza kupeleka ujumbe wa wewe unataka nini au unataka watu wakutambue kwa namna gani.
Wakati Joshua Blue, Makamu mkuu wa shule ya Kennedy mjini Hong Kong, anapoendesha baraza la wanafunzi anavaa tai lenye rangi ya light violet ili kumpa mamlaka.

Tai la rangi ya bluish-purple anasema ni “colourful yet muted”, anaamini kwamba rangi ya bluu inawafanya wanafunzi wasiboreke wakatiw anasikiliza, anajizuia kutumia brighter purples na pinks wakati akiwa mbele ya wanafunzi.

“Huhitaji kuwa na rangi nyingi zinazong’aa kwani watoto watajivuruga,” anasema Blue mwenye umri wa miaka 35.

Hakika inaweza kuwa kama kichekesho lakini wataalamu wanasema kwamba uchaguzi wa rangi ya tai inasaidia sana kupeleka ujumbe unaotakiwa kwa wahusika. Na hii haijalishi ni mteja, mdau wafanyakazi au watoto.

“Rangi hutoa aina Fulani ya ishara,” anasema David Zyla, Mwandishi mwenye makao makuu yake New York anayeandika Color Your Style.

“Suti ile ile inaweza kubadilishwa kimtindo yaani salamu zake kwa kubadili rangi ya tai, na kila mvao ukawa na ishara na salamu tofauti.”

Baada ya kusoma maelezo yote hayo, nikuulize je sasa unaweza kufikiria unataka kuvaa tai gani katika mkutano wako ujao.Labda nikusaidie kwa namna hii.:

Rangi nyekundu

Ni rangi Inayotawala

Si bahati mbaya au kitendo cha kubahatisha kwa wanasiasa wengi kuvaa tai lenye rangi nyekundi ndani ya suti zilizo dark na mashati mepesi.

“Tai nyekundu inaonesha mamlaka,” anasema Mark Woodman, mchambuzi wa mambo ambaye amejifunza masuala ya huko Laurel, Maryland, Marekani. “Kuna kitu Fulani kipo ndani ya rangi nyekundu ambacho mara zote kinajitokeza kumuimarisha mtu na kumpa mvuto wa pekee.”

Ofisa Mtendaji wa JPMorgan, Jamie Dimon huvaa tai nyekundu anapozungumza na wananchi
Hata hivyo wataalamu wanasema kwamba kuna rangi nyekundu na rangi nyekundu.Nyekundu iliyokoza kwa miondoko ambayo wazungu wanasema ni burgundy, husaidia kuleta imani na matumaini wakati ile nyekundu nyepesi na pink inakuwa zaidi onesho la ubunifu na namna ulivyo kistaili.Katika miaka michache iliyopita rangi ya pink inaweza kuonesha mshikamano na wamama anasema Woodman.

Wakati unaendesha mradi au unataka kupeleka ujumbe Fulani kwa kruu yako fikiria kuvaa tai la rangi nyekundu iliyokoza ambayo inashaini.Tai la rangi nyekundi unaweza kuwa njia bora ya kuonesha mamlaka.

Royal purples

Ross Znavor, Mtendaji katika moja ya taasisi za kifedha mjini New York yeye huvaa tai la rangi ya purple na si nyekundu katika mikutano ya kibiashara,Rangi hii huonesha kujiamini na humsaidia watu kuendelea kumkumbuka.

Anasema kuvaa tai hilo kunampatia mtu mwingine kukubali kwamba wewe unaweza kushirikiana naye na kujenga uhusiano wa kudumu.

Lindsay anasema purple, kiasili ni rangi ya utiifu na utajiri na kwa sasa inaaanza kukubalika maeneo ya kazi.

Arnold Schwarzenegger huonesha kujiamini kwa kuvaa tai rangi ya purple.

“Wanaume wanaovaa mashati ya lighter purple na tai za darker purple, hutaka kutambulika haraka katika kundi bila kuleta ushawishi mwingine wa kipuuzi unaovuruga”.

Rangi nyeusi

Inawezekana huvai kila siku au kila mahali lakini ukivaa tai nyeusi katika mikutano ya watendaji, kwenye dhifa unakupa wewe hali ya muondoko mweroro wenye utanashati mkubwa , anasema Zyla.

Muigizaji sinema Leonardo DiCaprio huvaa tai nyeusi katika mikutano au maeneo ambayo ni ya kikazi zaidi.

Lakini ni kweli kuwa rangi nyeusi inakufanya kuwa na ujeuri wa aina Fulani na wengine wanasema kusema kwamba inakuwa overdressed katika mazingira mengi. “Rangi hii inafaa kutotumika kama wewe unataka kuendelea kupanda ngazi, wapandisha ngazi wanaweza kufikiria kwamba wewe ni jeuri wa aina Fulani hivi,” anasema Zyla.

Ni vyema sana kama mtu atakuwa amejipatia grey shades, anaongeza Woodman. Tai la rangi ya grey linaweza kukupa mwonekano wenye mvuto mweroro usio na jeuri na usiojinata anasema Woodman.
“Grey iko poa, iliyotulia na ya kisasa zaidi,” anasema.Ili kuifanya iwe imetulia zaidi piga tai hili na shati ambalo ni lighter, pastel-coluored. Tafadhali angalia lighter grey shades na malizia na shaini ili kukupa muonekano ambao ni polished.

Rangi ya kijani

Rangi ya kijani ina maana nyingi kuanzia kuzaliwa upya hadi rangi ya fedha kwa mataifa Fulani.Lakini cha ajabu ni rangi yenye ‘kelele’ nyingi katika maeneo ya kazi.
Wakati mwingine kijani inakuwa too much.

“Je unataka kukumbukwa akwa ajili ya tai au kama wewe binafsi?,” anauliza Woodman .Anasema kuchagua rangi ya kijani inayostahili ni kazi kubwa.Kijani inayowaka inavuruga kutokana na mwako wake na pia inakuwa na taabu sana kupata suti inayoambatana nayo au hata shati. Hata hivyo tai la light green likiwa na subtle print linaweza kuwa jema katika shati ambalo rangi yake ni neutral.
Tai ya rangi ya njano, ni tai la kiasili kwa nchi nyingi hata waingereza wanaliheshimu kwa sababu linakupa uhakika, kukuweka mng’avu na mwenye siha hasa ya kufaa.

Ni rangi inayoonesha jua, hivyo watu wengi wanaweza kuwa na kishawishi cha kuzungumza nawe kwa sababu ya ukweli kuwa ni rangi yenye mvuto wa kipekee. Kwa wengi kuvaa tai la rangi ya njano kunaonesha kwamba maisha yeye anayaangalia katika dunia chanya zaidi, anasema Eve Roth Lindsay, mshauri wa masuala ya muonekano wa Hong Kong.

Lakini kiukweli kuwa unapaswa kuwa mwangalifu usije ukafanya kosa la uasili na utamaduni wa eneo lenu inapokuja suala la rangi.

Mathalani rangi ya njano nchini india ina maananisha kwamba wewe ni mfanyabiashara wakati rangi nyeupe nchini China inamaana upo katika kipindi cha maombolezo.

Rangi ya bluu

Unahofu ya kupeleka ujumbe ambao uhuhitaji kwa kutumia tai uliyovaa yaani rangi yake?basi ni vyema ukafikiria kutumia tai ya rangi ya bluu.

Rangi hii hutumika katika matukio yote.
Rangi ya bluu ni rangi bomba kwa kuwa inawakumbusha watu anga na bahari, vitu vyenye kutuliza maisha ya binadamu anasema Lindsay.

“Rangi ya bluu hakika ni salama zaidi kuivaa,” anasema.

Bluu inaonekana dhahiri ni rangi ya nguvu ya kimataifa

Tai ya Patterned blue hutoa hali ya kutulia na kitaalamu zaidi na inaweza kutumiwa katika mikutano ya kimataifa ya kibiashara na mazingira bila kupeleka ujumbe usiotakiwa.

Tai ya subtle blue inaweza kuwa na mvuto na kujionesha undani wakati cobalt au royal blue hukufanya ujiachie ndani ya kundi kwa namna Fulani. “Bluu iliyokoza ni rangi ya marubani watukuka. Bluu bahari ni rangi inayoaminika, inayokupa imani na kiburi cha uwezo,” anasema Lindsay .

Kuwa rafiki na asili

“Kabati lako likiwa na rangi rafiki za asili kama tan, kahawia, earthy colours, salmon na njano hufaa sana kwa watu wanaojishughulisha na wengine kama wafanyabiashara (mauzo), walimu na watu wa huduma mbalimbali,” anasema Lindsay.

Hakikisha kwamba tai la rangi ya kahawia haiku pekee kwani inaweza kuonesha ugoigoi katika wajihi. Hata hivyo tai la beige linaweza kukuonesha kwamba huna matatizo, yuko huru.
Epuka kuvaa tai la rangi ya udongo na shati linalofanana nalo. Na kama unataka kujishebedua na kuonekana kweli katika eneo la kazi rangi hizi za asili achana nazo kabisa.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About