Dondoo za Urembo na Mitindo

Faida za kuoga maji ya Baridi

Watu wengi hupenda kuogea maji ya moto, hii ni kutokana na kuogopa baridi au sababu za kimazoea tu. Ingawa mara nyingi umekuwa ukisisitiziwa kuwa maji moto yana manufaa mengi, lakini hata maji ya baridi nayo yana manufaa yake.

Je uko tayari kuongeza maarifa au hata kubadili mtazamo wako? Karibu nikushirikishe faida za kuogea maji ya baridi.

Huongeza utayari katika mwili.

Maji ya baridi hukufanya uchangamke, hili ni tofauti na maji ya moto. Mara nyingi mtu anapoogea maji ya baridi hasa baada ya kuamka humfanya awe katika hali nzuri ya kuwa tayari kuendelea na majukumu yake.

Kumbuka hata wakati wa kuogea maji baridi kasi ya upumuaji hubadilika na kukufanya kuongeza kiasi cha oksijeni kinachoingia mwilini.

Hulainisha ngozi na nywele

Maji moto huchubua ngozi na nywele, hasa kwa kuondoa mafuta laini yanayolinda ngozi na nywele na kuvifanya viwe vikavu sana.

Kwa kuogea maji ya baridi, ngozi na nywele zako havitapaushwa bali vitasafiwa na kuachwa katika hali nzuri ya kupendeza.

Huboresha kinga mwili

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Thrombosis Research Institute, ulibainisha kuwa watu wanaoogea maji ya baridi wanaongeza uzalishaji wa seli nyeupe za damu.

Utafiti huu unaeleza kuwa kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha metaboli mwili unapojaribu kujipasha moto, ndipo seli hizi nyeupe ambazo hupambana na maradhi zinapozalishwa.

Huhamasisha kupunguza uzito

Kupunguza uzito? Ndiyo kupunguza uzito. Baada ya binadamu kula vyakula, kiasi fulani huhifadhiwa mwilini kama mafuta. Baadhi ya mafuta haya huyeyushwa na kutumiwa kuupasha mwili joto.

Hivyo kuogea maji ya baridi kutawezesha aina fulani ya mafuta kuyeyushwa ili kuzalisha joto mwilini, jambo ambalo litapelekea kupungua kwa uzito.

Huchangia katika afya ya misuli

Wanamichezo wanafahamu kuwa kuogea maji baridi baada ya michezo au mazoezi huwafanya wajisikie vizuri mapema. Hili ni kutokana na maji baridi kuhamasisha mzunguko wa damu ambao huiwezesha misuli kujijenga tena upya vyema.

Huondoa msongo wa mawazo

Utafiti uliofanyika kwenye chuo cha tiba Virginia, ulibaini kuwa kuogea maji baridi huzalisha kemikali ya noradrenaline ambayo husaidia kukabili msongo wa mawazo.

Hukusaidia kulala vyema

Je umeshawahi kuogea maji baridi ukiwa umechoka sana au umefanya kazi ngumu? Kama umeshawahi kuogea maji baridi ni wazi kuwa ulijisikia vizuri na ukalala vizuri pia.

Hili ni tofauti na maji ya moto kwani badala ya kukupooza na kukufanya ulale vyema yatakufanya uchemke na kuchoka zaidi.

Naamini umepata maarifa juu ya faida za kuogea maji baridi. Naamini sasa hakuna haja ya kuongeza foleni za maji jikoni wakati unaweza kuogea maji ya baridi na ukapata manufaa yaliyoelezwa hapa.

Jinsi ya Kuondoa Makovu Mwilini

Makovu sio kidonda naomba hili uelewe, ila makovu ni alama ya majeraha ambayo yamebaki kwenye ngozi baada ya kupona majeraha.
Kuna baadhi ya watu husumbuliwa na shida ya kuwa na makovu sehemu mbalimbali ya mwili.
Hivyo kama wewe ni miongoni mwao maandishi haya yanakuhusu sana.

Zifuatazo ndizo mbinu za kuondoa makovu mwilini.

1. Tango

Unachotakiwa kufanya ni; Pondaponda tango na kisha kutumia mchanganyiko wake kwa kupaka juu ya kovu. Hii husaidia sana kulainisha makovu na ikiwa utatumia kwa muda mrefu huondoa makovu pia.

2. Aloe vera.

Unachotakiwa kufanya ni; kata majani hayo na utumie utomvu wake kupaka katika makovu kisha mara baada ya muda Fulani utaona mabadiliko na itapunguza na kuondoa makovu.

3. Asali

Unachotakiwa kufanya; Paka asali juu ya kovu na kuiacha usiku kucha. Rudia mara kwa mara kupaka asali hadi pale kovu litakapotoweka.

Namna ya kuvaa vizuri kwa mwanamme upendeze na kuwa mtanashati

Nimeona leo nitoe darasa kidogo kuhusu mavazi sababu na mimi ni kipaumbele changu katika maisha.

1.Epuka kuvaa marangirangi

Wakati unamatch mavazi jitahidi kupunguza idadi ya rangi, rangi 3 tu zinatosha kukutoa bomba.

2. Vaa kulingana na mazingira/sehemu

Mtu mjanja anajua kubadilika kulingana na mazingira, sio kuvaa jezi la Man utd lenye jina la Wazza kwenye sherehe

3. Masharti ya kuchomekea

-Marufuku kuvaa oversize/undersize
-Usivae mlegezo
-Hakikisha singlet haionekani
-Usivae mkanda mrefu
-Usivae makubanzi/sandals

4. Kama umevaa pensi /kaptula.

-Hakikisha unavaa soksi fupi zisizoonekana
-Piga raba au makubanzi/sandals bila soksi
-Haipendezi kuchemekea

5. Usivae shati jeupe kama la mwanafunzi

Shati nyeupe ni nzuri kama unaijulia wakati unanunua hakikisha ina urembo wa aina yoyote ile au ni ya kimtindo sio kuvaa shati la shule

6. Hakikisha una suruali nyeusi

Mwanaume yoyote yule wa kijanja anajua umuhimu wa suruali nyeusi sababu inamatch mashati ya rangi nyingi.

7. Saa

-Kama umevaa jeans/kadet unaruhusiwa kuvaa saa ya aina yoyote
-Kama umevaa suti/suruali ya kitambaa epuka kuvaa saa ya mkanda wa plastic.

8. Miwani

Duh hapa pagumu kidogo lakini cha msingi zingatia muundo wa kichwa chako pamoja na aina ya macho uliyonayo na aina ya pamba ulizovaa pia.Sio umepiga jeans kali,kichwa kama madenge na macho kama bundi kisha unapiga miwani ndogo ya njano,ni

9. Vaa kofia za kijanja

Kofia pia huongeza mvuto,chagua kofia kulingana na aina ya kichwa na mavazi uliyovaa,haipendezi kuvaa suti na kapelo.Kanzu sharti ivaliwe na barakashia ndo utaeleweka la sivyo ni sawa na kuvaa dera tu

10. Mkanda

-Usivae mkanda mrefu km vile umefunga nyoka kiunoni
-Mikanda ya vitambaa au madoidoi inafaa kuvaliwa na jeans/kadeti/kaptula
-Jitahidi mkumatch rangi ya mkanda na viatu kama umevaa nguo za kuchomekea
-Zingatia upana wamkanda na rux za nguo yako

11.Tupia cheni za ukweli

Mikufu ya kiume pia huongeza mvuto
-Kama umevaa nguo za kuchomekea au suti itapendeza ukivaa cheni ndogo ambayo haitokezi nje ya shati
-Kama umepiga pamba za kishua mfano T.shirt na jeans hapa tupia cheni kubwa lakini hata cheni ndogo zinakubali

12.Uvaaji wa Tai

-Vaa kulingana na urefu wako
-Kama wewe mwembamba inapendeza kuvaa tie nyembamba
-Jitahidi kumatch tie na rangi ya shirt/suruali
-Hakikisha tie yako imefungwa vizuri shingoni

13.T.shirt na Jeans

Wanaume wajanja wa mjini hupenda kupiga t shirt na jeans na chini kutupia raba Kali…..Vazi hili lina mvuto wa aina yake hasa likivaliwa kitaani na sehemu za mitoko kama vile kwenye Club za starehe.

14. Vaa viatu kijanja

Hapa pia Kuna changamoto
-Usivaa suruali ya kitambaa na Raba
-Usivae suruali ya kuchomekea na makubanzi
-Ukipiga jeans unaweza kumatch t.shirt/shirt na rangi ya viatu
-Ukivaa suti yakupasa upige kiatu kikali ….ulikosea itakuwa sawa na Toyota Mark X yenye matairi ya Fuso !!!

Jinsi ya kuchagua rangi sahihi wakati wa Kujipodoa

YAPO mambo mabalimbali katika tasnia ya urembo hasa katika vipodozi yanayopaswa kuzingatiwa katika kuboresha muonekano wa mtu.
Moja ya mambo hayo ni ujuzi na uelewa wa kutumia rangi katika kujipodoa kwani ni wanawake wachache wenye ujuzi huu.
Katika makala hii, nitakuelezea namna ya kuchanganya na kutofautisha rangi za vipodozi, lengo likiwa ni kuboresha muonekano wako.

Uchanganyaji wa rangi za vipodozi ni muhimu sana kwani katika kujipodoa, rangi zote za vipodozi unavyopaka zinatakiwa zioane ili kuleta muonekano ulio sawa na wa kueleweka.

Kwanza kabisa unatakiwa uwe makini katika kuoanisha rangi za vipodozi pamoja na rangi ya ngozi yako, hivyo katika hili unatakiwa kuwa na ujuzi maalumu ili usije ukafanya makosa na kuharibu muonekano wako.

Pia inabidi ufahamu hatua za upakaji vipodozi ili usije ukafanya vipodozi vingine visionekane katika uso wako.

Namna ya kuoanisha na kutofautisha rangi

Siku zote vipodozi vyako lazima viendane na mavazi yako ili kuleta maana zaidi kwa mfano, mara nyingi rangi ya mdomo ‘lipstick’ huendana na vazi lako wakati shedo ‘eye shadow’ zinatofautiana.

Kwa nguo za pinki

Katika mavazi haya, unatakiwa kupaka rangi ya mdomo yenye rangi ya pinki ambayo itaendana sawasawa na mavazi yako huku ukichanganya na shedo ‘eyeshadow’, inaweza kuwa ya rangi ya bluu ili kuitofautisha na mavazi yako, hapo utakuwa sawa katika kanuni za urembo.

Vazi la kijani

katika vazi hili unatakiwa kupaka rangi ya mdomo yenye rangi ya kahawia huku ukichanganya na shedo ya rangi ya kijani au kahawia iliyoingiliana na pinki au rangi ya machungwa.

Kwa vazi la njano au kahawia

Katika vazi hili unatakiwa kupaka ‘lipstick’ ya rangi ya kahawia iliyokolea, kwa upande wa shedo waweza kupaka ya rangi ya dhahabu.

Kwa vazi la bluu

Katika vazi hili unatakiwa kupaka ‘lipstick’ yenye rangi ya pinki huku ukipaka shedo ya rangi ya bluu kwa mtindo huu utakuwa mwenye kuvutia siku zote.

Umuhimu wa kuvaa soksi

Miguu ni sehemu mojawapo inayotoa jasho sana hivvo ni vema kuiweka mikavu kuzuia ukuaji wa bacteria au fungus.Wakaka tunajua umuhimu wa soksi au tunavaa bila kujua na wengine hatuvai? Hii ni kwa wadada pia wanaovaa viatu kama raba au hata nyumbani. Ni vema sana kufahamu kwanini tunavaa soksi na mda mwingine soksi gani tuvae.

1. KUZUIA MAGONJWA YA NGOZI MIGUUNI.

Tumia sekunde tatu tu kuvaa soksi na ujikinge na maradhi haya ya fungus na bacteria, kama sio mpenzi was soksi nashauri ufikirie tena maamuzi yako ya kutovaa soksi.

2. EPUKA HARUFU MBAYA YA MIGUU

Image result for atletes foot
Kwa kweli hii ni kero kwako na wanaokuzunguka.Usipovaa soksi jasho lote la miguu litaenda kwenye viatu na ivo viatu kutoa harufu.Soksi hunyonya lile jasho na huzuia harufu iyo. Aya basi tushtuke aibu hii ya nini katika karne ya watanashati sisi.Tuvae soksi na kubadili kila siku.

3. LAINISHA NGOZI YA MIGUU YA YAKO

Nani hapendi miguu soft?? wadada kutwa kusugua miguu saloon.Simple ukirud nyumban kama sakafu ni ngumu vaa soksi zako nyepesi safi miguu iwe laini.Baadhi ya viatu pia vina surface ngumu kwa chini (wakaka) ukiweka soksi zako safi hamna maneno.

4. KUPUNGUZA MAUMIVU MIGUUNI

Hii hasa kwa watoto wadogo ..tuwazoeze mapema kuvaa soksi.Mtoto anatembea ndani Mara akanyage maji mara vitu vya ncha Kali….Pia kuna viatu ukivaa bila soksi lazima upate maumivu na kupata zile sugu nyeusi.

5. KUPATA JOTO NYAKATI ZA BARIDI

Wale was mikoa iliyo na baridi kwa sasa naamini tuna soksi za kutosha za miguuni na mikono.Kama kuna sehemu inayongoza kutoa joto ni miguuni na mikononi.Basi vaa soksi ili kuzuia joto lisipotee.

6. MVUTO

Ili sio geni, mi mtu akivaa viatu bila soksi kwa kweli napunguza maksi za utanashati…wengine wanasema kuna viatu vya kutovaa soksi. .hakuna kitu kama icho kuna soksi ndogo ambazo hazionekani kwa juu zimejaa tele madukani tutafte.Ebu mtu kavaa kiatu chake safi akiweka na soksi safi inaonekana mvuto lazima uwepo….Nani hapendi kuvutia??basi sote tunapenda tuvae soksi

Siandiki mengi sana, soksi sio jambo geni, tubadilike tujijali,.Ok unavaa soksi Je?unavaa soksi pea moja mara ngapi, unafua na kukausha vizuri maana soksi mbichi ni janga jingine la uchafu na maradhi.Kitu kingine ujue aina ya soksi nyakati za joto usivae soksi ambazo ni nzito sana vaa nyepesi, ambazo ni nzito vaa nyakati za baridi. Na soksi za watoto tununue ambazo hazibani sana.

Vyakula vya Kukuza nywele na kuzifanya ziwe na Afya

Kuwa na nywele zenye afya nzuri ni muhimu kwa wote bila kujali jinsi, hali hii husababisha wengi kutumia madawa ya aina mbalimbali ya kuhakikisha nywele zao zinastawi na kuwa na muonekano mzuri.
Kwa bahati mbaya, wengi waliotumia madawa yanayotengenezwa kwa kemikali hujikuta katika wakati mgumu siku za usoni wakikabiliwa na matatizo ya nywele kukatika na hata kupata madhara katika ngozi ya kichwa.

Njia bora na salama zaidi ya kustawisha nywele, kuzifanya ziwe na mvuto wa aina yake bila kujali wewe ni mtu wa asili ya bara Asia, Afrika au Marekani, ni kula vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa afya ya nywele.

Vifuatavyo ni sehemu ya vyakula ambavyo hupatikana kirahisi barani Afrika na kwa bei nafuu, ambavyo vitakupa afya bora zaidi ya nywele zako.

1. Yai

Nywele za binadamu zina protini ambayo zimeumbiwa. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa zina protini ya kutosha, na hilo hufanyika kupitia vyakula. Protini ni nguzo kuu ya nywele za binadamu, na yai ni moja kati ya vyakula vyenye utajiri mkubwa wa protini. Hakikisha unakula yai angalau mara tatu kwa wiki.

2. Spinachi

Nywele zinahitaji madini ya chuma ili ziweze kuwa katika hali nzuri ya afya. Kukosekana kwa madini ya chuma husababisha nywele kunyonyoka. Mwili unapokosa madini ya chuma, hewa ya oxygen na virutubisho hushindwa kufika vizuri kwenye mizizi ya nywele hivyo hufanya nywele kuwa dhaifu na zisizo na muonekano mzuri.

Mboga za majani aina ya spinachi ni suluhisho, kwakuwa zina madini ya chuma kwa wingi ambayo seli za nywele huhitaji.

3. Jamii ya Machungwa, Limao

Mwili wa binadamu huhitaji vitamini C ambayo husaidia kuhuisha utendaji wa madini ya chuma. Hivyo, unapaswa kuongeza matunda ya jamii ya ‘citrus’, kama vile machungwa, chenza, balungi na limao. Pia, unaweza kutumia na asali pamoja.

Vitamini C husaidia katika ukuaji wa nywele kusaidia usambaaji wa virutubisho na ukuaji wa haraka wa nywele.

4. Karoti

Ni muhimu sana kuhakikisha unakunywa juice ya karoti kila siku, kama unataka nywele zako zikue haraka zikiwa na mwonekano mzuri wenye afya. Vitamini A inayopatikana kwenye karoti ni muhimu sana kwa ukuaji wa seli za nywele. Kumbuka nywele zina tishu ambazo hukua haraka zaidi katika mwili.

Karoti ina mafuta asili yanayofahamika kama ‘sebum’ na mizizi ambayo husaidia kukuza nywele kwa haraka.

5. Parachichi

Tunda aina ya parachichi lina kazi nyingi sana mwilini kama matunda mengine, lakini hili ni tunda la kipekee amnbalo lina utajiri wa vitamini E ambayo husaidia mzunguko wa damu na katika hilo husaidia mfumo wa ukuaji wa nywele kwa haraka.

Tunda hili husaidia kuhuisha na kurekebisha mafuta na kiwango cha PH (inayosafisha kemikalii mwilini) ambavyo kama vitazidi kwenye mwili vinaweza kusababisha kusimama kwa ukuaji wa nywele, yaani nywele hudumaa.

Kwa faida zaidi, vitamin E inayopatikana kwenye parachichi kwa wingi husaidia zaidi afya ya moyo wa binadamu na zaidi ngozi. Hakikisha unapata tunda hili kadiri iwezekanavyo.

Hivi ni baadhi tu ya vyakula na matunda kwa ukuaji mzuri wa nywele zako. Kama unatumia vizuri mlo wako, utakuwa adimu sana kutumia mafuta yenye kemikali ambayo yanaweza kukuletea madhara mabaya.

Jinsi ya kutunza kucha kujiepusha na maradhi shambulizi ya Kucha

Mikono, viganja na vidole ni kati ya sehemu muhimu katika mwili wa msichana. Mikono hutumika kufanya shughuli nyingi za nyumbani, shuleni na sehemu mbalimbali katika maisha kuanzia kutandika kitanda, kupika, kufanya usafi, kuandika, kujiremba pamoja na majukumu mengine mengi.

Mikono isipotunzwa vizuri ni rahisi sana kuharibika, kupoteza mvuto wake wa asili na kuharibu afya ya kucha. Hitaji la urembo wakati mwingine humsukuma msichana katika matumizi ya vipodozi vya kupaka kwenye kucha zake ili kukamilisha urembo wake.

Urembo wa vidole na kucha sio lazima ufanyike katika saluni au kwa wataalamu wa kupamba kucha, msichana anaweza kushughulikia afya na urembo wa vidole na kucha zake kwa gharama nafuu na kwa muda ambao mwenyewe anaona unafaa kufanya hivyo hata akiwa nyumbani.

Hii pia itamsaidia Msichana kuchagua vipodozi salama kwa afya ya kucha zake na mwili kwa ujumla. Ni jambo la muhimu kufahamu kuwa baadhi ya vipodozi vinavyotumika katika urembo wa kucha, vina rangi na sumu zisizofaa kwa afya. Sumu kama vile ‘Formaldehyde na Toluene’ zinazopatikana katika baadhi ya rangi za kucha zina madhara kwa afya ya msichana.

Ni kweli kuwa kucha nzuri huongeza urembo, mvuto na furaha ya msichana lakini pia ni busara kukumbuka kuwa afya ni muhimu kuliko urembo na uzuri. Afya ya mwili na kucha za msichana kwa ujumla hutegemea chakula bora chenye protein, madini na vitamini na siyo rangi na vipodozi.

Upungufu wa vitamini A, B Complex, proteni, madini ya chuma na chokaa (kalishiamu) mwilini husababisha kucha zipoteze afya yake ya asili. Kucha ambazo hazina afya zinaweza kuoza, kukauka, kupinda, kupasuka au kuwa na umbo kama kijiko. Magonjwa ya kuvu (fungus), na baadhi ya dawa za kupunguza makali ya virusi pia huharibu afya ya kucha. Mojawapo ya athari za dawa za kupunguza makali ya VVU aina ya Zidovudine (ZDV) ni kucha kuwa na rangi nyeusi.

Kwa ajili ya afya bora ya kucha msichana anashauriwa kula mboga za majani, maharage, korosho, asali na matunda kwa wingi kila siku. Usafi wa kucha kila siku kwa kuziosha kwa maji ya uvuguvugu na sabuni laini pamoja na brashi ndogo ya mikono huimarisha afya ya kucha. Kucha pia zinaweza kusafishwa kwa maji ya mmea wa mshubiri (Aloevera), kitunguu saumu kilichopondwa pondwa au kitunguu maji kisha viganja na vidole vikaushwe vizuri na kupaka losheni.

Kucha za msichana zinatakiwa zisiwe ndefu ili kuepuka utunzaji wa vimelea vinavyosababisha magonjwa na kurahisisha utunzaji na usafi wa kucha. Kucha ndefu zinaweza kuwa chanzo cha hatari kwa afya ya msichana na familia yake hasa pale msichana anapohusika na uandaaji wa chakula cha familia. Katika familia nyingi, hasa familia za kiafrika wasichana ndio wanaobeba wajibu na majukumu ya kuandaa chakula cha familia.

Kwa afya nzuri ya kucha, msichana anashauriwa kukata kucha zake ili ziwe fupi kadri anavyotaka kwa kutumia ‘nail cutter’ au mkasi mdogo au wembe mpya ambao haujatumiwa na mtu mwingine. Kuchangia nyembe za kukatia kucha si salama kwani kunaweza kuwa njia mojawapo ya kusambaza vimelea vya magonjwa hatari ya kuambukiza kama vile virusi vinavyosababisha UKIMWI na ugonjwa wa homa ya ini.

Ni vizuri kulainisha ncha za kucha baada ya kuzikata kwa kutumia tupa ya kucha (nail file) na kuzisugua kuelekea upande mmoja ili kuepuka kucha zisivunjike au zisisababishe michubuko ya ngozi wakati wa kujikuna. Kusugua kucha kwa kwenda mbele na nyuma kunaweza kusababisha kucha zivunjike kwa urahisi na haraka.

Kwa afya njema ya kucha, msichana pia anashauriwa asifungue pini za barua au kukwangua vocha za simu kwa kutumia kucha. Kucha zisikatwe kwa kutumia meno na zisilowekwe kwenye maji kwa muda mrefu hasa pale maji hayo yanapokuwa na kemikali au sabuni.

Kwa ajili ya afya njema ya kucha za miguuni, ni muhimu kuhakikisha kuwa, viatu kabla ya kuvaliwa vinakuwa vikavu na safi kabisa. Viatu visipotumiwa pia vihifadhiwe sehemu kavu isiyo na vumbi, maji au unyevunyevu ili kuepusha visiwe makazi ya kuvu (fungus)

Tiba mbadala ya chunusi na vipele usoni

Kuna idadi kubwa ya watu wanao kabiliwa na tatizo la vipele vya usoni ( Chunusi ). Kuwa na chunusi ni jambo lenye karaha sana, kwani linakufanya upoteze mvuto wako wa asili na hivyo kukukosesha raha.

Zipo njia mbalimbali za asili zinazo weza kutumika kutibu tatizo la chunusi na vipele vya usoni.

Ifuatayo ni miongoni mwa njia bora kabisa na ya uhakika itakayo kusaidia kuondokana na tatizo la Chunusi au vipele kwenye uso.

Komamanga: Maganda Ya Mkomamanga yaliyosagwa, yakichanganywa na habbat sodah ya unga, hutengeneza dawa nzuri ya asili ya kuondoa tatizo la vipele vya usoni ( chunusi )

Habbat Soda: Hii ni Habbat Sodah Ya Mbegumbegu. Habbat Sodah iliyosagwa ndio inayo hitajika katika kutengeneza dawa ya asili ya kuondoa tatizo la vipele vya usoni ama chunusi.

MAHITAJI:

Habbat Sawdah ya Unga iliyo sagwa.
Nusu kikombe ya maganda ya komamanga yaliyo sagwa.
Nusu kikombe ya siki ya tofaha(apple )

MATAYARISHO NA MATUMIZI

Changanya na pasha moto kwa dakika mbili kikombe kimoja cha Habbat-Sawdaa iliyosagwa, ½ (nusu)
kikombe cha maganda ya komamanga yaliyosagwa, na ½ (nusu) kikombe cha siki ambayo inatokana na juisi ya tofaha (apple).

Paka katika sehemu inayotakiwa kabla ya kwenda kulala kila siku usiku mpaka vipele (chunusi) vitakapoondoka. Mchanganyiko unaweza kukaa mpaka wiki tatu na ni lazima uwekwe katika hali ya ubarid.

Namna ya uvaaji wa mavazi mbalimbali kwa wanaume

Wanaume wanajali mavazi yao pia, sio wanawake tu. Ila, mwanaume anabidi aelewe kwamba badala ya kufuata mitindo, kupendeza kwenye tukio lolote kuna nguo ambayo utaihitaji. Nguo hizi ni kama:

1. T-Shirt ya Pamba

Ukitaka t-shirt itakayo dumu kwa muda mrefu, nunua t-shirt zilizotengenezwa kwa pamba tu. Pia, kuwa na t-shirt kadhaa zenye rangi tofauti, zikiwemo:

Za rangi ya kawaida kama Nyeupe, nyeusi, rangi ya kijivu
Za rangi kali kama Njano, bluu nyepesi na kijani
Uzuri wa t-shirt ni kwamba zinaweza kuvaliwa na chochote kile. Kwa hiyo, kuwa na aina nyingi kabatini.

2. Polo Shirts

Mwanaume yoyote anatakiwa kuwa na Polo Shirt (t-shirt zenya kola) kadhaa. Zinafaa sana kuvaliwa kazini kwenye siku za Ijumaa au weekend.

3. Mashati ya kawaida

Mashati ya kawaida, ya mikono mirefu au mifupi, ni mazuri kuvaa na jinzi na viatu au raba. Pia, zipo za aina na rangi tofauti kwa hiyo tafuta itakayokufaa.

4. Mashati ya shughuli/sherehe rasmi

Kutegeamea na ajira yako, shati ya aina hii inaweza ikawa nguo utakayoishia kuvaa kuliko zote. Kwa hiyo, lazima uwe nazo za kutosha za aina mbalimbali.

Pia hata kama huzihitaji kwa kila siku, utazihitaji kwa sherehekama harusi au mkutano mkubwa wa kikazi.

Muhimu kuliko vyote ni kuhakikisha unajua saizi yako na kwamba unavaa shati linalo kutosha vizuri kabisa. Zaidi ya hapo, fikiria tai utakayoivalia.

5. Bukta

Kwa kuzingatia joto lote la Tanzania, bukta ni muhimu.

Kuna aina nyingi za bukta na zenye rangi tofauti. Zinaendena na polo shirt pamoja na viatu vya kawaida. Ni mazuri kuvaa kwenye wikiendi ukiwa umetulia na washkaji.

6. Suruali za kawaida

Suruali za aina hii zina faraja na zinavaliwa kwenye mazingira mbalimbali. Pia, kama polo shirt zinapatikana kwa rangi nyingi kwa hiyo zinaweza kuvaliwa na mashati, viatu, kodia n.k za ain nyingi.

7. Jinzi

Jinzi zinaweza kuvaliwa kokote, siku yoyote.

Iwe ijumaa kazini au jumamosi usiku, hata kazini kwenye siku ya kazi (kutegemea na masharti ya kazini kwako), jinzi zitavaliwa tu. Zipo za aina nyingi, rangi tofauti na zinavaliwa na chochote kile.

Ila, ni muhimu kujua saizi yako ile upendeza unavyostahili. Pia, jinzi zenye ubora zitakuwa na bei zaidi ila bora ununue jinzi yenye ubora itakayodumu kwa miaka kuliko jinzi isiyo na ubora itakyodumu kwa miezi.

8. Koti la suti

Mwanaume yoyote anatakiwa kuwa na koti za suti za rangi ya bluu na kijivu kabatini. Rangi hizi zinaendana na sherehe rasmi na zisizo rasmi, na zinavaliwa na aina mbalimbali ya mashati na viatu.

Ila, muhimu zaidi ya rangi ni saizi. Hakikisha unajua saizi yako na kwamba koti zinakutosha vizuri.

9. Chupi na Soksi

Hakikisha chupi zako ni nzuri, zinakutosha na ni safi (usije ukajiaibisha). Kama zimechakaa, zitupe.

Soksi nazo ni vilevile. Ila, unahitaji kuwa na aina tofauti za soksi kwa ajili ya mavazi tofauti. Hakikisha rangi ya soksi zako zina ukali au ni nzito kidogo ya suruali yako.

10. Viatu

Kwa kawaida, viatu ni vitu vya kwanza vya mtu kuangalia akikuona, hasa na wanawake. Kwa, sio swala la kupuuzia.

Cha muhimu ni kwamba ni visafi na ziko katika hali nzuri.

Ndio, inabidi ujaribu nguo mbalimbali ila ujue kinachokupendeza. Ila, kuwa na mavazi yasiyo na mbwembwe nyingi si mbaya. Bahati nzuri, nguo tulizoorodhesha hapo juu zitakusaidia kupendeza bila kuweka juhudi saaaaana.

Jinsi ya Kuvaa hereni kwa Mpangilio kuongeza Mvuto wako

HERENI ni pambo linavoliwa masikioni na kwa kiasi kikubwa linachangia kuongeza mvuto na muonekano mzuri. Kuna aina nyingi za hereni katika tamaduni mbalimbali. Zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia vito vya thamani kama vile Dhahabu, Almasi, Shaba au Kopa.

Vilevile zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia malighafi za asili kama vile ubao, vifuu vya nazi, mfupa kioo na shanga ambazo zimekuwa zikivaliwa sana na wanawake wa kimasai. Hereni zilizotengenezwa kwa shanga zimekuwa zikiwavutia watu wengi kuvaa kutokana na nakshi zake za asili.

Mara nyingi uvaaji wa hereni unatakiwa kuzingatia aina ya nguo uliyovaa, hapo unatakiwa kucheza na rangi. Mpangilio wako wa nguo na hereni hata na viatu utakufanya uonekane maridadi muda wote.

Unapotoka kwenda katika shughuli zako, au uwapo nyumbani basi zingatia uvaaji wa hereni na nguo. Uvaaji usiozingatia mpangilio wa rangi na hereni zako huondoa ladha ya urembo na si rahisi kwa mtu mwingine kugundua umependeza.

Licha ya kuwa hapo awali hareni zilikuwa zikivaliwa na wanawake pekee lakini miaka ya hivi karibuni tunaona urembo huu unaanza kuwavutia baadhi ya wanaume hususan vijana wa mjini.

Kutokana na hilo kuna hereni ambazo zimetengenezwa maalum kwa kuvaliwa na wanaume, hizi huwa za kubana na huwa na umbo dogo ukilinganisha zile zinazopendwa kuvaliwa na wanawake.

Angalizo: Epuka kuvaa hereni zaidi ya moja katika tundu la sikio kwani kufanya hivyo kunaweza kupelekea ukubwa wa tundu kuongezeka na hatimaye nyama ya sikio kuchanika. Hereni nzito sana nazo huchangia kutokea kwa tatizo hili.

Madhara ya Kuvaa viatu virefu

NI wazi kuwa viatu virefu huvutia sana vinapo kuwa vimevaliwa.Tulio wengi hasa mabinti au wanawake tunaokwenda na wakati hupenda kuvaa viatu virefu ilikuongeza muonekano wa umbile lako nikiwa na maana kuwa miguu huonekana yenye kuvutia zaidi unapo kuwa umevaa viatu virefu.

Kutokana na utafiti wa kitaalamu, mwanamke ana uwezo wa kutembea wastani wa hatua 10,000 kwa siku.Visigino virefu hufanya nguvu inayotumika kutembea hatua moja kuwa kubwa kuliko kawaida, huku vikikunyima raha ya kutembea kwa uhuru kiasi kwamba wengine hufikia hatua ya kuvua na kutembea peku.

Leo hii napenda kukujuza madhara ya uvaaji wa wa viatu virefu.Kwa kawaida, miguu ya binadamu hasa visigino, vimeumbwa ili kuuzuia uzito wa mwili juu ya ardhi.Uvaaji wa viatu virefu hufanya uzito wa mwili kubebwa na kisigino, hivyo uzito wa mwili kushindwa kuhimili uzito wote.

Matokeo yake husababisha misuli na mishipa ya miguu, kiuno, mgongo na shingo kufanya kazi kubwa ya kujaribu kusawazisha uzito.Kazi ambayo kwa kawaida hufanywa na visigino.Tatizo hilo hupelekea kiuno,Miguu na mgongo kuwa katika hatari ya matatizo ya kiafya pamoja na kuteguka na kuvunjika miguu.

Visigino virefu hubadili muundo wa mifupa ya miguu, hivyo hupelekea magoti na misuli ya mapaja kufanya kazi ya ziada ili kuupa mwili usawa.Kwa kuwa misuli inafanya kazi kubwa, uwezekano wa kupatwa na maumivu makali ya miguu na kushindwa kutembea katika siku za baadae huwa mkubwa zaidi. Visigino virefu husababisha maumivu ya visigino, damu kuvilia ndani ya miguu, mpangilio wa mifupa ya vidole kuvurugika, mishipa na misuli ya mapaja kuuma, neva za fahamu kufungana na kushindwa kufanya kazi yake.

Tatizo huendelea kwa vifundo vya miguu, magoti, na mifupa ya kwenye mapaja kushindwa kujivuta na kulegea na hivyo kusuguana wakati wa kutembea.

Jambo la kuzingatia kwa wale wanaopenda kuvaa viatu virefu,ni vema kama unapenda kuvaa viatu virefu hakikisha hutembei umbali mrefu kama una usafiri sio mbaya ukivaa viatu virefu,na kwa wale wanao kwenda ofisini jitahidi kuwa na viatu flati ndani ya mkoba wako ili unapokuwa umechoka unavua na kuvaa viatu vyako pia ukiwa ofisini waweza kuvua viatu virefu.

Mpenzi msomaji kama huwezi kutembelea viatu virefu nivema ukipitwa na wakati kuliko kujiabisha barabarani na kuonekana rimbukeni ikiwa wewe ni mjamzito epuka uvaaji wa viatu virefu.Usikose kujumuika nami katika safu hii ya urembo na mitindo.

Matumizi ya Asali kwenye Urembo wa ngozi na Nywele

Asali hutumika kulainisha Ngozi

Asali ina asili ya kuvuta unyevu kutoka kwenye hewa na kuipa ngozi uwezo wa kuhifadhi unyevu hivyo ni faida kwa mtu mwenye ngozi kavu.

Jinsi ya kuandaa
Chukua asali mbichi kijiko kimoja cha chai kisha paka usoni, kaa nayo kwa dakika 15 hadi 20 kisha safisha uso wako.

Asali katika kusafisha ngozi, kutibu na kuzuia chunusi

Kutokana na uwezo wa asali katika kuua bacteria na kuvuta uchafu katika matundu ya ngozi asali itakusaidia kutatua tatizo la chunusi.

Jinsi ya Kuandaa
Chukua asali mbichi Kijiko kimoja cha chakula changanya na mafuta ya nazi vijiko viwili changanya mchanganyiko uwe mlaini kisha paka usoni huku ukisugua taratibu kwa kufanya kama viduara huku ukiepuka kufikisha machoni. ukimaliza kusugua uso na mchanganyiko wako osha uso wako.

Jinsi ya kuandaa kama kisafisha ngozi, exfoliator
Changanya kijiko kimoja asali na kijiko kimoja baking soda. tumia mchanganyiko huu kusugua ngozi yako. Asali inaongeza lishe na chembe chembe kuzuia madhara yanayotokana na sumu za hewani zinazozeesha ngozi. Baking soda inasaidia kusafisha matundu ya ngozi.

Asali inasaidia ngozi iliyoungua na jua kujirudi na kung’aa.

Jinsi ya kutumia asali katika nywele
Asali inatibu nywele kavu zilizopauka, na kulainisha ngozi kavu ya kichwa na kutibu muwasho kichwani.

Jinsi ya kufanya
Changanya kijiko kikubwa cha asali na maji ya uvuguvugu kisha paka kichwani Acha kwa muda wa saa 1 iwe kama conditioner kisha safisha nywele zako.

Unaweza kuchanganya asali kiasi cha kijiko kimoja mpk viwili katika maji vikombe vitano kisha safishia nywele zako taratibu, yaani yapitishe tu hayo maji kwenye nywele zako ambazo ni safi.

Tahadhari: Asali kwa kiasi kikubwa hupausha weusi wa nywele kutokana na Hydrogen Peroxide inayopatikana ndani ya asali.

Ni vema ukatumia asali mbichi kujihakikishia faida za asali katika mwili wako.
Iwapo unavutiwa na matumizi ya kitu cha asili katika urembo wako unaweza kuongeza kitu hicho katika kitu kingine unachotumia mfano katika steaming yako au scrub unayotumia.

Mavazi ya Ofisini kwa Wadada

Wengi wetu tunashindwa kutofautisha mavazi ya sehemu husika mfano Ofisini, michezoni, na yale ya usiku na sehemu nyinginezo leo nitagusia vazi la ofisini kwa akina dada.

Unapotaka kuvaa vazi ,lazima uangalie vazi unalolivaa mda gani na mahala unapokwenda,siyo vazi la kutokea usiku au la kimichezo unalivaa ofisini,utakuwa kichekesho mbele za watu hata kwa wafanyakazi wenzio.

Mavazi ya kiofisi yanaeleweka lakini hasa kwa mwanamke basi vaa sketi fupi au ndefu na blauzi ya heshima iliyofunika kitovu chako, au suti ya heshima na koti na hata suruali ambayo haijakubana sana inafaa sana kwa ofisi.

Kama utapendelea kuvaa gauni basi angalia mkao wa hilo gauni ukoje maana mara nyingi gauni huwa halipendezi kuwa vazi la ofisini bali vazi la jioni.

Jinsi ya kusafisha na Kutunza Kucha zako

Inashauriwa kwamba kabla ya kuchukuwa uamuzi wa kwenda kununua vifaa husika ambavyo utavitumia unapaswa kufahamu aina ya kucha ili uweze kununua vifaa vinavyoendana na kucha zako kwa lengo la kuzilinda badala ya kuvamia na kuziharibu.

Kwa kawaida kucha za mikononi na miguuni zinakabiliwa na mazingira magumu kutokana na majukumu ya kazi za kila siku hali inayochangia kuziweka katika mazingira magumu kiafya.

Mbali na kucha kukosa afya, pia kuharibu shepu yake ya awali kutokana na shughuli za kila siku katika maisha ya binadamu yeyote, hivyo ni vyema kuzikinga kucha zako na maradhi kwa kuzifanyia usafi kila siku au mara kadhaa kwa wiki ili kuzilinda zaidi.

Ili kuweza kugundua aina ya kucha zako katika kuzipangilia wakati wa kuzifanyia usafi, unapaswa kuwa makini wakati unachagua rangi ya kupaka, kuangalia muonekano wa kucha zako zilivyo ili uweze kupangalia rangi ziweze kuwa na mvuto zaidi.

Ni vyema kwa mtu anayejali afya ya kucha zake kuchukua muda mwingi kufuatilia kucha zake na kuelekeza nguvu zake katika kuhakikisha zinakuwa katika matunzo mazuri na kujitahidi kubuni mtindo ambao unaweza kuwa tofauti na wengine ambao wanapenda kuzifanya kawaida.

Hata hivyo katika kutunza kucha ziwe nzuri, vyakula ambavyo ni mlo kamili ni muhimu sana, vinginevyo utajikuta ukishauriwa na wataalamu kutumia vitamini mbalimbali kama vile vitamini A, vitamini C, Culcium, Folic Asidi, Protini na Vitamini B12.

JINSI YA KUSAFISHA KUCHA.

Wekeza vifaa vizuri vya kisasa vya kutunzia kucha.
Tumia brush ya kucha kwa kusugua chini ya kucha na kuutoa uchafu na kufikia sehemu ngumu ambapo uchafu unajilundika. Unaweza tumia mswaki ukiwa huna vifaa vya kisasa.
Tumia maji moto na sabuni ya kunawia mikono.
Anza kwa kusugua chini kabisa kwa kushikilia brush chini na sugua kuanzia nyuma kuja mbele pole pole, kisha juu ya kucha fanya hivyo kwa kuzunguka.

Toa rangi kwa kuloweka pamba kwenye polish remover na usugue kwa vidole vyenye hinna huna haja ya kuitoa. kwa vidole vya afya na nguvu vipumzishe kwa kutumia polish kila baada ya wiki kadhaa.

Loweka kucha na maji kwenye bakuli,au sinki,au kifaa cha uwezo wako hata dishi poa,kwa maji ya moto ya uvuguvugu na pitisha sabuni ya kunawia mikono.Na ni kucha tu usiloweke mkono mzima,kwa dakika tatu,sabuni kwenye maji hufanya mikono kuwa mikavu .

Suuza kwa maji ya bomba ya uvuguvugu,au yalokua kwenye chombo yaani jimwagie,kisha zifute na taulo laini.

Kisha tumia kikatio kucha kukata maana zitakua laini,au kifaa cha kuzipunguza kuweka sawa kama hauzikati.

Mambo ya msingi kwa mwanamke kuyajua unapojiremba

Kope nazo humpendezesha mwanamke kuna aina ya rangi za kupaka kwenye kope, lakini zinatofautiana. Ni vyema ukawasiliana na wataalamu wa mambo ya urembo kwa ushauri na siyo kukurupuka. Siyo umemuona fulani kapendeza na aina fulani ya rangi ya kwenye kope halafu na wewe ukakimbilia kupaka, utachekesha.

Rangi ya mdomo nayo ni eneo lingine linalompendezesha mwanamke. Ukweli ni kwamba tunatofautiana sana midomo wazungu wanaita ‘Lips’ Kila mwanamke ana tofautiana midomo na mwingine kwa hiyo hata rangi ya midomo nayo inakwenda sambambana aina ya lips na rangi ya ngozi ya mwili aliyo nayo mwanamke, siyo unajisiriba rangi ya mdomo halafu unaonekana kituko. Wasiliana na wataalamu wa urembo kwa ushauri zaidi.

Kucha kwa wanawake ni eneo lingine linolatakiwa kuwekwa katika unadhifu. Kuna baadhi ya wanawake unaweza kukutana nao kucha zao zimelika aidha kwa kung’atwa au kwa kuliwa na fangasi.

Ni vyema wanawake wenye tatizo hilo kumuona mtaalamu wa ngozi kwa msaada wa tiba. Unaweza kukutana na mwanamke kucha zake zimelika na zina sharp edges kiasi kwamba akikugusa utadhani umeguswa na msasa.

Au akishika Glasi ya Kinywaji ukiangalia kucha utadhani mkono ni wa mwanaume maana kwa jinsi kucha zake zilivyo hata hafanani nazo. Kuna kucha za bandia kama mwanamke ana matatizo ya kucha basi akazinunue kusitiri aibu.

Marashi, manukato au unyunyu kama wanavyoita vijana wa mjini ni muhimu kwa wanawake lakini ni vyema nikaweka angalizo. Haipendezi kwa mwanamke anayepulizia manukato yanayonukia sana mpaka yakawakera wengine ni vyema wanawake wakajipulizia marashi yenye staha na yasiyokera.

Ngozi ya mwanamke ni bora ‘sensitive’ sana na inaakiwa ipakwe aina ya mafuta au lotion yenye virutubisho kulingana na aina ya Ngozi. Kuna wanawake wenye Ngozi ya mafuta ‘Oil Skin’ kuna wenye Ngozi mchanganyiko na kuna wale wenye ngozi kavu (Dry Skin).

Ni vyema mwanamke kujua aina ya ngozi yake ili ajie aina ya product ya ngozi anayopaswa kutumia na siyo kwa sababu umemuona mwenzio anapaka aina fulani ya losheni na wewe unakimbilia kununua. Omba ushauri kwa wataalamu wa ngozi watakusaidia. Kuna baadhi ya maduka yanyouza vipodozi wanatoa msaada huo bure kabisa.

Madhara ya kuvaa miwani ya Urembo maarufu kama miwani ya Jua

Miwani za urembo maarufu kama miwani za jua zimetajwa kuwa na madhara kwa watumiaji wake kutokana na watu kutofahamu saizi za namba ambazo wanapaswa kuzivaa kabla ya kununua.

Akifafanua kwenye kipindi cha Supamix kinachorushwa East Africa Redio, Daktari Ningwa wa Upasuaji wa macho kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dk.Neema Daniel Kanyaro amesema watu wengi amekuwa wakivaa miwani pasipokjua kwamba zinaweza kuwasababishia matatizo ya kuona.

Dk. Kanyaro amesema kwamba watu wamekuwa wakivaa miwani za jua kama urembo pasipo kwenda kupima kujua ni aina gani ya miwani wanazotakiwa kuzitumia lakini pia bila kujua kama miwani hizo zina namba ambazo kila mtu ana namba kutokana na uono wake.

“Miwani ni dawa lakini usivae bila kupima kwani inaweza kukusababishia matatizo ikiwemo uoni hafifu. Unaweza kukuta unavaa miweani nyeusi lakini kumbe siyo namba yako. Kama hujijui unaweza kuta ukitazama unaona giza kumbe umeshaua macho kwa urembo” amesema.

Akizungumzia kuhsu presha ya macho Dk. Kanyaro amesema kwamba ugonjwa huo hauna dalili za moja kwa moja bali ni lazima kupima na huathiri watu wa rika zote.

Namna ndizi inavyotumika katika urembo

Mbali na kulika, ndizi zina manufaa mengine, hasa katika urembo wa ngozi.
Ndizi zina virutubisho muhimu vinavyoboresha ngozi. Ndizi pia zina aina tatu za sukari zinazojulikana kama ‘sucrose’, ‘fructose’ na ‘glucose’.

Hakikisha unanawa uso wako mara tatu kwa siku. Unapofanya hivyo unaondoa uchafu.

Ndizi pia husaidia kuzuia chunusi.

Hakikisha unanawa uso kwa sabuni ambayo inaendana na ngozi yako. Ikiwa ngozi yako ni ya mafuta, hakikisha unatumia sabuni ambayo itakuacha ukiwa mkavu na kama ngozi yako ina ukavu, jioshe na sabuni itakayokufanya uwe na unyevu.

Kulainisha ngozi

Changanya asali na ndizi moja iliyopondwa na upake kwenye uso na shingo. Nawa uso kwa maji ya fufutende baada ya muda wa nusu saa. Fanya hivi angalau mara moja kwa wiki.

Kung’arisha uso

Ndizi huwa na Vitamin C ambayo husaidia kuiweka ngozi kuonekana iking’aa. Kwenye ndizi iliyopondwa, ongeza vijiko viwili vidogo vya juisi ya limau na upake kwa uso na shingo. Osha kwa maji ya fufutende baada ya dakika 20. Ni vizuri kupaka mchanganyiko huu wakati unapoenda kulala.

Kuzuia mikunjo

Ponda parachichi na ndizi pamoja. Paka kwa uso na uoshe baada ya muda. Mchanganyiko huu hulainisha ngozi ya uso na kuwa laini lakini pia upunguza ukubwa wa matundu ya ngozi ya uso wako.

Kusugulia uso (Scrubing)

Changanya ndizi na sukari kijiko kimoja, kisha paka usoni na usugue taratibu. Ndizi hulainisha ngozi kavu na sukari huondoa seli zilizokufa kwenye ngozi.

Saga ndizi moja na Oats vijiko vitatu kisha changanya na asali na maziwa. Paka usoni kwa dakika 15 kisha sugua.

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About