Dondoo za Urembo na Mitindo

Jinsi ya Kutumia Papai na Asali kuondoa Madoa Usoni

KUMEKUWA na sababu mbalimbali zinazofanya watu kutokuwa na ngozi zisizokubalika.Mbali na hali ya hewa pia matumizi ya pombe na sigara hata matumizi ya cream kali ambazo zimekuwa zikitumiwa na watu bila kujua madhara yake kumechangia kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.

Ngozi kwa kawaida inatakiwa ijitengeneze yenyewe na si kuitengeneza kwa vipodozi kama wengi wanavyodhani. Ulaji wa matunda na mboga za majani kwa wingi kunywa glasi nane za maji kwa siku ni njia nzuri kama unataka kuwa na ngozi nzuri isiyo na madoa wala ukavu ambao haupendezi.

Wengi wanaacha kula mbogamboga na matunda kwa wingi hata kutokunywa maji ya kutosha na badala yake wamekuwa akitegemea kuwa na ngozi nzuri jambo ambalo ni gumu.Mara kadhaa tumeshuhudia watu wanaopaka cream kali wakiwa kama wameungua usoni huku uso na mwili ukionekana kuwa makavu jambo ambalo linaashiria kuwa kupaka cream si suruhisho la kuwa na ngozi nzuri.

Kuna watu wamekuwa na ngozi za asili na hata unapowauliza baadhi yao hawajawahi kupaka cream hata siku moja na bado wana ngozi nzuri zinazovutia hao wamekuwa wakila kwa ajili ya kuhakikisha wanatengeneza ngozi zao kutoka ndani.

Pia wengi wanaharibu ngozi zao na kuwa na madoa kutokana na kutumia make up kwa muda mrefu na hata anapogundua kuwa ana tatizo la madoa amekuwa akijaribu kutumia cream nyingine kwa ajili ya kumaliza tatizo hilo jambo ambali linazidisha madhara kwenye ngozi.

Unaweza kutibu ngozi yenye madoa usoni pia mashavuni kwa kujitibu na juisi ya limao.

Namna ya kufanya

Chukua limao lioshe na kisha likamue na kuchuja mbegu zake. Weka juisi hiyo kwenye kikombe na kisha tafuta kitambaa laini kichovye kwenye juisi ya limao na dondoshea juisi ya limao kwenye sehemu zenye tatizo.

Kaa kama dakika tano kisha usha uso kwa maji safi.Pia unaweza kuchanganya na asali mbichi na maji ya limao husaidia pia kuondoa madoa usoni.

Limao lina sifa kubwa ya kuzuia harufu pia unaweza kulitumia katika kuondoa harufu kali ya jasho mwilini na husaidia kuondoa weusi kwenye kwapa, chini ya macho, mapajani pia.

Chukua kipande cha limao weka sukari kidogo, sugua.Unatakiwa kutumia kwenye kwapa ambalo ni safi, vizuri kutumia njia hii kabla na baada ya kuoga.

Jinsi ya Kutumia Bamia kuondoa chunusi Usoni

Wiki hii kwenye urembo tutaongelea mboga aina ya bamia jinsi inavyotibu chunusi na kuziondoa moja kwa moja. Mbali na chunusi, pia husababisha ngozi kuteleza na kuwa nyororo.

JINSI YA KUFANYA

Chukua bamia zikatekate vipande, ziweke kwenye brenda kisha chukua limao kipande na maji kidogo, weka kwenye brenda kisha saga. Baada ya kupata mchanganyiko wako upake usoni mpaka kwenye shingo, acha kwa muda likauke kisha bandua kama unavyoondoa maski nyingine usoni.

FANYA HIVI SIKU TATU KWA WIKI ITAKUSAIDIA KUONDOA CHUNUSI.

Jinsi ya kuvaa viatu mbalimbali inavyotakiwa na ili upendeze

Viatu ni kinga kwa ajili ya kuhifadhi miguu. Vile vile viatu ni vazi ambalo linaongeza urembo na nakshi kwa mvaaji. Viatu vipo vya aina mbalimbali na vinavaliwa kulingana na mahali na mavazi yanayoambatana navyo. Tuangalie baadhi ya aina za viatu na wapi hasa na vipi vikitumika vinapendeza zaidi.

1.Viatu vya ngozi vya kufunika

Viatu vya kufunika vipo virefu sana, vyenye urefu wa wastani na vifupi kabisa. Mara nyingine haviwi vya ngozi kabisa bali ni kama vina plastiki na pia vingine huwa na uwazi mdogo kwa mbele.Viatu virefu zaidi mara hupendeza zaidi kuvaliwa kwenye sherehe na kanisani. Unaweza kuvaa kazini kama kazi yako haikulazimu kutembea tembea maana vitachosha miguu yako na kupunguza ufanisi.

Viatu vyenye urefu wa wastani unaweza kuvaa popote iwe kazini, kanisani, kwenye sherehe n.k. Viatu vya chini kabisa vinakuwa vyenye matumizi zaidi wakati unamatembezi mengi. Havifai sana kuvaa kwenye sherehe za usiku hasa kama unavaa nguo maalumu ya usiku. Vinafaa sana kwa mjamzito hasa katika miezi ya mwisho.

2.Viatu vya wazi virefu

Viatu hivi vipo vya aina mbili, vyenye rangi za mng’ao na ambavyo ni mahususi kwa sherehe za usiku na vyenye rangi ngumu ambavyo waweza kuvaa kazini au kanisani. Viatu hivi vinapendeza kuvaliwa na nguo yoyote ila ikiwa ya urefu wa wastani ni nzuri zaidi maana huwezesha kuonekana urembo na uzuri wote wa kiatu. Viatu hivi vinakuja katika mitindo mbalimbali na unachagua ule ambao wewe unaupendelea zaidi mfano vyenye visigino vyembamba, visigino vinene au aina ya ‘wedges’.

3.Viatu vya wazi vifupi

Viatu hivi ni vizuri sababu vinawezesha miguu kupumua na ku’relax’. Viatu hivi vipo vya aina tofauti tofauti na vinafaa sana kuvaliwa kwa matembezi ya jioni, wakati wa safari ndefu, wakati ukiwa na mizunguko mingi na pia hata kazini au kanisani pale unapokuwa umevaa nguo za kawaida (casual). Havivutii sana kuvaliwa na suti au nguo ya usiku. Pia mara nyingi viatu vya chini hupendezea kuvaliwa na nguo ndefu( hasa casual) na viatu virefu hupendeza zaidi kwa nguo yenye urefu wa wastani.

4.Viatu vya muda maalumu

Hivi ni viatu ambavyo vinavaliwa wakati wa kazi maalumu kama wakati wa kazi za mashambani, mgodini, wakati wa michezo au wakati wa baridi kali.

Ni vyema na inapendeza kama unauwezo uwe na viatu vya aina mbalimbali angalau aina tatu. Mfano viatu vyeusi vya urefu wa wastani, viatu vya usiku vya wazi, viatu vya chini vya kufunika na vya wazi.

Madhara ya Kujichubua

Katika baadhi ya sehemu duniani watu wanaamini kuwa ngozi angavu huashiria uzuri, utajiri na uwezo(kifedha) alionao mtu.Katika baadhi ya sehemu watu wenye ngozi nyeusi huchukuliwa kuwa wapo chini ya kiwango, hii hupelekea watu hawa kutumia ving´arisha ngozi kama krimu, vidonge au nyenzo zingine kubadilisha ngozi zao.

Tafiti zinaonyesha kwamba wavulana na wasichana hupendelea kutumia bidhaa zinazong´arisha ngozi ili waweze kupata hadhi nzuri katika kundi la familia zao, na jamii. Kwa kweli,hata matangazo yanayoonyeshwa kwenye televisheni mbalimbali huonyesha kitu hiki. Mambo hayo yote huwa na athari kubwa juu ya mawazo ya vijana wa kiume na wakike ambayo hupelekea kuwafanya wachague chochote wanachomudu kati ya krimu au vidonge.

Madhara ya kujichubua ni yapi?
Mtu anaeyejichubua anaweza kupata kansa ya ngozi, chunusi, uvimbe katika ngozi, ngozi kuwa nyembamba,Kuongezeka kwa hamu ya kula na uzito,kutokwa na mabaka, pumu, kupata watoto wenye kasoro, kupata matatizo ya akili, kuharibika kwa ini, kuharibika kwa mishipa ya fahamu pamoja na figo kutokana na kiwango kikubwa cha zebaki(mercury) kilichomo katika krimu,Osteoporosis(kupungua kwa uzito wa mifupa ambapo huongeza hatari ya kuvunjika kwa mifupa)

Baadhi ya madhara haya huonekaa mara moja na mengine hujitokeza kadri mtu anavyotumia ving´arisha ngozi.

Faida na namna ya kutumia mafuta ya Zaituni Olive Oil kwenye nywele

Faida ya Mafuta Ya Zaituni Olive Oil kwenye nywele.

1. Yanasaidia kufanya mzunguko wa damu kufanya kazi vizuri kwenye ngozi ya kichwa na kupenyeza hadi kwenye shina ya nywele kisha kuifanya nywele inayoota kuwa imara

2. Yanasaidia kupambana na mba kwenye ngozi ya kichwa

3. Yanasaidia uzalishwaji wa mzizi au shina ya nywele

4. Yanasaidia uzalishwaji wa melanin ambayo inafanya kazi ya kutoa rangi ya nywele inayotakiwa.

5. Yanasaidia kuifanya nywele isiwe kavu sana.

NAMNA YA KUZIHUDUMIA NYWELE:

Unaweza kuchanganya na Mdalasini pamoja na Asali.

1. Olive oil vijiko 2 vya chakula

2. Asali kijiko 1 cha chakula

3. Mdalasini kijiko 1 cha chai

Pasha moto olive oil kisha changanya vyote kwa pamoja pakaa kwenye nywele acha kwa muda wa dakika 20 kisha osha nywele zako na upakae mafuta zikishakauka.

Ninashauri utumie mafuta haya kwenye nywele na ngozi ni mazuri sana. Ukiwa na mba pakaa kwenye ngozi mba itaisha na muwasho utaondoka.

Mambo ya Kuzingatia ili uwe na ngozi laini

Takribani kila mtu angependa kuwa na ngozi laini, au hata laini zaidi. Watu wengi wamekuwa wakiitafuta ngozi nzuri au kujitahidi kuitunza ili isiharibike. Lakini je, wamefanikiwa?
Wachache hufanikiwa na wengi hushindwa. Na hata hao waliofanikiwa wengi wao hutumia vipodozi vikali ambavyo vingi huchubua na kuharibu ngozi zao na kuwaletea madhara makubwa sana baadae.

Vipi wewe, ungependa kuwa na ngozi nzuri bila kuidhuru afya yako? Karibu somo la leo ili uweze kuwa na ngozi nzuri bila kuidhuru afya yako.

Ngozi laini ni nzuri na inaongeza mvuto wa mwili. Ulaini wa ngozi hupotezwa na mambo mbalimbali kama vile seli za ngozi kupungukiwa na maji na kuanza kusinyaa na kunyauka, seli za ngozi kujeruhiwa, na seli za ngozi kufa. Matokeo yake ni michirizi, makunyanzi, makovu, chunusi, madoa, ngozi kufubaa na kuzeeka.

Kuifanya ngozi kuwa laini unahitaji kuupatia mwili virutubisho vyote vya kujenga mwili vizuri na kunywa maji ya kutosha ili seli zisikauke, kusinyaa wala kunyauka. Kula mlo kamili, matunda mengi na kunywa maji ya kutosha.

Pia unahitaji kuepuka jua kali ambalo litaunguza ngozi, kuikausha na kuifanya iwe na makunyanzi na vitu vingine vinavyoota kwenye ngozi kutokana na jua.

Tumia vipodozi vizuri vinavyosaidia ngozi kuwa laini bila kuidhuru. Hapa kuna vipodozi vya aina mbali mbali na vinavyofanya kazi kwa njia mbali mbali. Vipodozi vya muhimu ni

  1. Vipodozi vya kuongeza unyevu au maji kwenye (seli za) ngozi
  2. Kwa kiingereza vinaitwa “Moisturizers”. Hivi hufanya kazi ya kufunika ngozi na kuzuia maji yasipotee kutoka kwenye ngozi, na pia husaidia kuongea maji kuingia kwenye seli za ngozi. Vipo katika mtindo wa sabuni, mafuta na losheni.
  3. Vipodozi vya kusaidia kuongeza kasi ya kuzalishwa kwa seli mpya za ngozi
  4. Hivi husaidia kuzalisha seli mpya za ngozi ambazo zitaleta ngozi mpya na nzuri na kuondoa ile ya zamani iliyochoka na kuzeeka. Mifano ni losheni na krimu zenye Vitamini A na Vitamini E.
  5. Vipodozi vya kusaidia kuondoa uchafu na seli (ngozi) zilizozeeka au kufa

Tumia sabuni zenye uwezo mkubwa wa kuondoa uchafu kutoka kwenye ngozi, na ukiweza tumia “face wash” au “facial cleansers”. Hivi husaidia kusafisha kabisa ngozi na kuondoa uchafu.

Kwa upande wa seli zilizokufa na kubaki juu ya ngozi tumia “scrub”. Scrub hufanya kazi kwa kuondoa seli zilizoharibika na zilizokufa na kuacha seli changa na ngozi nzuri.

USHAURI:

  1. Pata ushauri wa kulainisha na kupendezesha ngozi yako kutoka kwa wataalam wanaojua vizuri afya, urembo na vipodozi. Utashauriwa vizuri jinsi ya kufanya, vipodozi vya kutumia na jinsi ya kuvitumia vizuri kwa matokeo mazuri zaidi. Epuka wauza vipodozi wasio waaminifu au wasiovijua vizuri vipodozi, maana wanaweza kukupa vipodozi vya tofauti na mahitaji yako au vipodozi vinavyodhuru afya yako.
  2. Safisha ngozi yako vizuri, kila siku. Hakikisha unaondoa uchafu na vijidudu vyote vinavyotua na kukaa juu ya ngozi yako. Ondoa vumbi, seli zilizokufa, mafuta ya ziada, jasho nk Lala na pumzisha ngozi yako kiasi cha kutosha ili iweze kujitengeneza na kuwa nzuri. Ipumzishe kila siku kwa matokeo mazuri zaidi. Pata usingizi wa kutosha na ulio bora
  3. Tumia vipodozi vizuri vyenye uwezo wa kukupa matokeo mazuri unayoyataka na visivyodhuru afya yako. Pata ushauri mzuri kutoka kwa wataalam ili uweze kufanikisha hili vizuri. Tumia vipodozi vinavyoendana na ngozi yako. Kama ngozi yako ni kavu tumia vipodozi ambavyo ni maalum kwa ajili ya ngozi kavu, na kama ngozi yako ni ya mafuta basi tumia vipodozi ambavyo ni mahususi kwa ajili ya ngozi ya mafuta.
  4. Usitumie vipodozi vinavyoharibu ngozi na kuihatarisha ngozi yako. Epuka vipodozi vyote visivyo salama na vile visivyoendana na ngozi yako.
  5. Jihadhari na michubuko au majeraha mengine yoyote yatakayoweza kuharibu ngozi yako. Hii ni kwa sababu michubuko na majeraha hayo yatakuharibia uzuri wa ngozi yako na pia yatakuachia makovu baada ya kupona
  6. Kuwa na furaha, amani na tabasamu itakusaidia pia kuwa na ngozi nzuri, hususan ngozi ya usoni.

Mambo ya kuzingatia kama una ngozi yenye Mafuta

Ngozi yenye mafuta kwa kawaida huwa inang’ara, nene na yenye rangi iliyotitia. Mara nyingi ngozi yenye mafuta mengi sana huwa na chunusi nyingi na vipelepele na mara nyingine huwa na chunusi zenye vichwa vyeusi. Katika aina hizi za ngozi mafuta hutokana na tezi za sebaceous na kuzalisha mafuta zaidi ya kiwango kinachotakiwa. Mafuta hayo husambaa katika ngozi na kuifanya iwe na mafuta mafuta.

Mafuta katika mwili yanatengenezwa na ‘sebaceous glands’,kwa hiyo kuna baadhi ya watu wana sebaceous glands ambazo zinatengeneza mafuta kwa wingi sana na hivyo kufanya ngozi zao kung’aa kwa sababu ya hayo mafuta mengi.

Sebaceous gland zipo kwa wingi usoni(face) shingoni(neck), kifuani, kichwani na mgongoni, ndiyo maana hayo maeneo yanakuwa na mafuta kwa wingi.

Sababu zinazosababisha ngozi kuwa na mafuta:

  1. Kurithi.
  2. Lishe.
  3. Kiwango cha homoni mbalimbali mwilini.
  4. Ujauzito.
  5. Vidonge vya kuzuia mimba.
  6. Baadhi ya vipodozi.
  7. Hali ya hewa ya joto.

Namna ya kutunza ngozi zenye mafuta

Faida kubwa ya kuwa na ngozi yenye mafuta ni kuwa haizeeki kwa haraka ikilinganishwa na aina nyinginezo za ngozi. Miongoni mwa mambo yanayosaidia ili kuitunza ngozi yenye mafuta na kuiepusha na chunusi na hali isiyopendeza ni:-

Ngozi yenye mafuta inahitajia kusafishwa vyema kwa maji ya moto na sabuni ili kuzuia vinyweleo visizibwe na mafuta.

Epusha vifaa vigumu visikwaruze uso wako na kupelekea ngozi kubanduka, kwani suala hilo husababisha tezi za mafuta kufanya kazi zaidi ili kujaza sehemu iliyopotea ya mafuta.

Epuka kutumia vipodozi ambavyo huifanya ngozi yako ipoteze maji au kukauka. Kwani husababisha sehemu ya juu ya ngozi inyauke, na hivyo kusababisha mafuta kuziba vinyweleo na kupelekea kutokea vichwa vyeusi.

Jitahidi kuitunza vyema ngozi yako na kuisafisha vizuri. Jaribu kuosha uso mara mbili au tatu kwa siku. Usioshe mara nyingi kwani kufanya hivyo huufanya uso kutoa mafuta zaidi.

Chagua kile unachosafishia kwa makini, jiepushe kutumia cream nzito nzito au vifaa vugumu wakati wa kuosha uso wako. Ni bora utumie sabuni za kawaida zisizokuwa na madawa. Unaweza kutumia lotion ya kuua bacteria au sabuni zisizo na dawa nyingi (lightly medicated), au sabuni zenye madini mbalimbali. Ni bora usioshe au kutumia lotion au michanganyiko yenye alkoholi.

Tumia maji ya moto au ya vuguvugu wakati unaosha uso wako.

Wakati unapoosha uso wako, ukande kwa kutumia ncha za vidole, jiepushe kupaka sabuni moja kwa moja usoni, inaweza kuganda na kuzuia vinyweleo kuziba.

Kutumia mask za udongo (clay) na tope (mud) husaidia katika ngozi za aina hii. Ni bora utumie mask mara moja au mbili kwa wiki.

Jitahidi kutumia vipodozi vya uso ambavyo vimetengenezwa kwa ajili ya ngozi yenye mafuta.

Mavazi ya Ofisini kwa Wadada

Wengi wetu tunashindwa kutofautisha mavazi ya sehemu husika mfano Ofisini, michezoni, na yale ya usiku na sehemu nyinginezo leo nitagusia vazi la ofisini kwa akina dada.

Unapotaka kuvaa vazi ,lazima uangalie vazi unalolivaa mda gani na mahala unapokwenda,siyo vazi la kutokea usiku au la kimichezo unalivaa ofisini,utakuwa kichekesho mbele za watu hata kwa wafanyakazi wenzio.

Mavazi ya kiofisi yanaeleweka lakini hasa kwa mwanamke basi vaa sketi fupi au ndefu na blauzi ya heshima iliyofunika kitovu chako, au suti ya heshima na koti na hata suruali ambayo haijakubana sana inafaa sana kwa ofisi.

Kama utapendelea kuvaa gauni basi angalia mkao wa hilo gauni ukoje maana mara nyingi gauni huwa halipendezi kuwa vazi la ofisini bali vazi la jioni.

Jinsi ya kufanya ili uwe na umbo dogo la kuvutia

Unaweza kujiuliza, hivi inawezekanaje kuwa na umbo dogo la aina hii? Ukweli ni kwamba inawezekana, lakini inahitaji kazi ya ziada kufikia kwenye lengo hilo.

Unalifahamu umbile la sifuri au saizi zero?

Kwa wale wanaojali maumbo ya kupendeza saizi zero linatafsiriwa ni kuwa na kiuno kisichozidi inchi 23, nyonga 32 na kifua 31. Kikubwa unachotakiwa kuzingatia ni mazoezi na ulaji wako, kwa kuwa mwangalifu katika kiasi cha kalori unachoingiza mwilini kila siku.

Unatakiwa kuwa mwadilifu katika uchaguaji wako wa chakula, haimaanishi ukae na njaa. Inawezekana ikawa ni vigumu kuelewa makala haya.

Kinachosisitizwa katika mpango huu, ni kuwa waangalifu katika upangiliaji wa vyakula. Aina hii ya mpangilio wa ulaji inafahamika zaidi kitaalamu kama ‘crash diet’ Kula kiasi cha kalori 400- 500 kwa siku. Lakini unatakiwa kufanya mazoezi angalau kwa saa mbili kwa siku, ili kupunguza mara mbili ya kiasi cha mafuta uliyokula katika siku hiyo.

Kunywa maji kwa wingi:

Kwa kunywa kiasi kikubwa cha maji itakusaidia kurahisisha umeng’enyaji wa chakula mwilini. Ni vyema mwili wako ukawa na maji ya kutosha ikiwa umeingia kwenye mpango huu wa ulaji Kula mboga za kijani: Zina Vitamini, protini na virutubisho vingine kwa wingi ambavyo ni muhimu kwa afya. Kama ilivyoainisha awali, utaratibu huu hauhamasishi kukaa na njaa, bali kula vyakula vilivyo bora kiafya.

Kula vyakula visivyokobolewa.

Mara nyingi vyakula vya aina hii, huwa na virutubisho muhimu na vinavyohitajika katika ustawi wa mwili.

Punguza wanga katika mlo wako.

Badala yake unaweza kula protini na kuingiza vyakula kama mayai na samaki kwenye mlo wako.

Epuka kula vyakula vya mtaani.

Vyakula kama chips, mihogo ya kukaanga na jamii yake vinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzito wa mwili na pia hulifanya zoezi la umeng’enywaji wa chakula tumboni kuwa gumu.

Kula supu za mbogamboga;

Supu kama ya kabichi licha ya kujaza tumbo, husaidia katika kurahisisha mfumo wa umeng’enyaji chakula tumboni.

Kula saladi na matunda kwa wingi.

Hii itasaidia kukuweka sawa kiafya.

Jizuie kula vyakula vyenye sukari nyingi na hata vile vya mtaani unavyohisi vinaweza kukwamisha mpango wako wa kupungua.

Lakini pamoja na yote jipe mazoezi ya kutosha kama kukimbia, kuruka kamba au mazoezi ya kupunguza tumbo na maziwa

Madhara ya Kuvaa viatu virefu

NI wazi kuwa viatu virefu huvutia sana vinapo kuwa vimevaliwa.Tulio wengi hasa mabinti au wanawake tunaokwenda na wakati hupenda kuvaa viatu virefu ilikuongeza muonekano wa umbile lako nikiwa na maana kuwa miguu huonekana yenye kuvutia zaidi unapo kuwa umevaa viatu virefu.

Kutokana na utafiti wa kitaalamu, mwanamke ana uwezo wa kutembea wastani wa hatua 10,000 kwa siku.Visigino virefu hufanya nguvu inayotumika kutembea hatua moja kuwa kubwa kuliko kawaida, huku vikikunyima raha ya kutembea kwa uhuru kiasi kwamba wengine hufikia hatua ya kuvua na kutembea peku.

Leo hii napenda kukujuza madhara ya uvaaji wa wa viatu virefu.Kwa kawaida, miguu ya binadamu hasa visigino, vimeumbwa ili kuuzuia uzito wa mwili juu ya ardhi.Uvaaji wa viatu virefu hufanya uzito wa mwili kubebwa na kisigino, hivyo uzito wa mwili kushindwa kuhimili uzito wote.

Matokeo yake husababisha misuli na mishipa ya miguu, kiuno, mgongo na shingo kufanya kazi kubwa ya kujaribu kusawazisha uzito.Kazi ambayo kwa kawaida hufanywa na visigino.Tatizo hilo hupelekea kiuno,Miguu na mgongo kuwa katika hatari ya matatizo ya kiafya pamoja na kuteguka na kuvunjika miguu.

Visigino virefu hubadili muundo wa mifupa ya miguu, hivyo hupelekea magoti na misuli ya mapaja kufanya kazi ya ziada ili kuupa mwili usawa.Kwa kuwa misuli inafanya kazi kubwa, uwezekano wa kupatwa na maumivu makali ya miguu na kushindwa kutembea katika siku za baadae huwa mkubwa zaidi. Visigino virefu husababisha maumivu ya visigino, damu kuvilia ndani ya miguu, mpangilio wa mifupa ya vidole kuvurugika, mishipa na misuli ya mapaja kuuma, neva za fahamu kufungana na kushindwa kufanya kazi yake.

Tatizo huendelea kwa vifundo vya miguu, magoti, na mifupa ya kwenye mapaja kushindwa kujivuta na kulegea na hivyo kusuguana wakati wa kutembea.

Jambo la kuzingatia kwa wale wanaopenda kuvaa viatu virefu,ni vema kama unapenda kuvaa viatu virefu hakikisha hutembei umbali mrefu kama una usafiri sio mbaya ukivaa viatu virefu,na kwa wale wanao kwenda ofisini jitahidi kuwa na viatu flati ndani ya mkoba wako ili unapokuwa umechoka unavua na kuvaa viatu vyako pia ukiwa ofisini waweza kuvua viatu virefu.

Mpenzi msomaji kama huwezi kutembelea viatu virefu nivema ukipitwa na wakati kuliko kujiabisha barabarani na kuonekana rimbukeni ikiwa wewe ni mjamzito epuka uvaaji wa viatu virefu.Usikose kujumuika nami katika safu hii ya urembo na mitindo.

Madhara ya Uvaaji wa Wigi au nywele Bandia

Katika miongo kadhaa iliyopita, uvaaji wa wigi umekuwa fasheni katika sekta ya urembo na hutumika hususani na wanawake. Ingawa uvaaji wa wigi huwafanya wanawake hao kuonekana mithili ya mtu aliyevaa kofia ngumu (helmet), lakini yaonekana ni mapendeleo ya wengi.

Wanaume wengi hujiuliza , “Ni kwanini kina mama hupendelea kuvaa wigi na kusuka nywele za bandia?, wakati hupendeza na kuwa warembo zaidi wakiwa na nywele zao za asili”?

Wigi huvaliwa zaidi na kinamama wenye asili ya Afrika au Wamarekani wa asili ya Afrika. Lakini tukiangalia moja ya chimbuko hasa la uvaaji wigi ni ubaguzi uliokuwepo wakati wa utumwa ambapo wale wenye ngozi nyeupe na nywele shombeshombe walipewa kazi za ndani na wale wasio na ngozi nyeupe na nywele zisizo shombeshombe walifanyishwa kazi ngumu za mashambani.

Watumwa waliopelekwa barani Amerika hawakuweza kuzihudumia nywele zao kutokana na hali ngumu, na mabwenyenye waliwashusha hadhi na kuwavunja moyo kwa kuwaambia hawakuwa na nywele bali ni “manyoya”.

Lakini sababu nyingine inayodhaniwa kuwaathiri wanawake wa asili ya Afrika ni fikra kuwa mwanamke mwenye nywele ndefu pengine hadi mgongoni ni mrembo zaidi. Pia siku hizi warembo na wanaoshiriki katika mashindano ya urembo hujaribu kurefusha nywele zao ili kuwa na viwango na aina za mitindo ya ughaibuni.

Pamoja na kuwa wanawake wanajaribu kuwa warembo kwa uvaaji wa wigi, zifuatazo ni baadhi ya hasara au madhara kiafya ya uvaaji wigi na usukaji wa nywele za bandia.

Uvaaji wa wigi au nywele za bandia waweza kukusababishia mzio (allergy), endapo malighafi au kemikali zilizotumika kutengeneza wigi hiyo zitasisimua mfumo wa kinga ya mwili wa mvaaji.

Kupata m-ba ni tatizo jingine kutokana na uvaaji wigi, hii hutokana na kukosekana kwa hewa ya kutosha ya Oksijeni katika ngozi ya kichwa (scalp hypoxia) na katika tishu za shina la nywele. Kwa hiyo kama utaamua kuvaa wigi uhakikishe imetengenezwa kwa viwango vya ubora unaotakiwa na inapitisha hewa ya kutosha ya Oksijeni.

Pia waweza kunyonyoka nywele hata kama una nywele nzuri zenye afya, na kama utachagua kuvaa wigi na unataka kuepuka madhara hakikisha kuwa nywele zako ni safi, usilazimishe kuvaa wigi iliyo ndogo na yenye kubana sana, hakikisha unapata muda wa kupata hewa na nywele zako zinapakwa mafuta kuepuka ukavu wa ngozi ya kichwa na nywele kukatika .

Maumivu ya kichwa ni tatizo ambalo laweza kusababishwa na uvaaji wigi au usukaji wa nywele bandia. Wigi iliyo ndogo husababisha mkandamizo kichwani na kusababisha maumivu ya kichwa ya mara kwa mara.

Upotevu wa muda na fedha ni dhahiri kwa kuwa ufumaji wa nywele za bandia waweza kuchukua muda mrefu, itamlazimu mvaaji wigi kubadili kwa kununua mpya kila baada ya muda fulani au kuwa na wigi nyingi kwa ajili kubadili kulingana na fasheni.

Harufu mbaya huweza kujitokeza endapo mba na jasho vitachanganyikana na hupelekea uwepo wa bakteria au fangasi na kusababisha muwasho mkali, hii yaweza kumkosesha raha mvaaji wigi na mwenye kufuma nywele za bandia hasa pale anapokuwa katika majumuiko ya kijamii.Kama utachagua kuvaa wigi hakikisha nywele zako zinasafishwa na shampoo au sabuni, zinakaushwa vizuri na kupakwa mafuta.

Endapo mwanamama atachagua kuvaa wigi,asisahau kuwa nywele zake za asili zinahitaji matunzo,na azingatie wakati wa kununua wigi au nywele za bandia, ahakikishe ananunua yenye ubora unaotakiwa ili kuepuka madhara ya kiafya anayoweza pata kutokana na uvaaji wigi au anapofuma nywele za bandia.

Benson Chonya

Jinsi ya kutumia maziwa ya mtindi kufanya ngozi yako kuwa laini na soft

Ulisha wahi kukaa ukajiuliza mbona kuna baadhi ya watu wana ngozi nzuri laini na soft? lakini kwako ni tofauti?

Ukawaza labda wanatumia vitu vya bei ghali ambavyo wewe huwezi ku – afford, au umesha hangaika na ma – cosmetics lakini bado ngozi yako haikubali kukaa vizuri?

Jaribu hii Home made Yogurt Cleansing, Tumia mtindi ambao hauna mafuta mengi au hauna kabisa (low fat),

Paka mtindi wako usoni fanya kama una sugua kwa muda mchache halafu uache kwa dakika 15, fanya hivi mara mbili kila siku na utapata matokeo kwa muda mchache.

Hii husaidia kuondoa cell za ngozi zilizo kufa (dead skin cells) na protein tighten the pore.

Vyakula vya Kukuza nywele na kuzifanya ziwe na Afya

Kuwa na nywele zenye afya nzuri ni muhimu kwa wote bila kujali jinsi, hali hii husababisha wengi kutumia madawa ya aina mbalimbali ya kuhakikisha nywele zao zinastawi na kuwa na muonekano mzuri.
Kwa bahati mbaya, wengi waliotumia madawa yanayotengenezwa kwa kemikali hujikuta katika wakati mgumu siku za usoni wakikabiliwa na matatizo ya nywele kukatika na hata kupata madhara katika ngozi ya kichwa.

Njia bora na salama zaidi ya kustawisha nywele, kuzifanya ziwe na mvuto wa aina yake bila kujali wewe ni mtu wa asili ya bara Asia, Afrika au Marekani, ni kula vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa afya ya nywele.

Vifuatavyo ni sehemu ya vyakula ambavyo hupatikana kirahisi barani Afrika na kwa bei nafuu, ambavyo vitakupa afya bora zaidi ya nywele zako.

1. Yai

Nywele za binadamu zina protini ambayo zimeumbiwa. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa zina protini ya kutosha, na hilo hufanyika kupitia vyakula. Protini ni nguzo kuu ya nywele za binadamu, na yai ni moja kati ya vyakula vyenye utajiri mkubwa wa protini. Hakikisha unakula yai angalau mara tatu kwa wiki.

2. Spinachi

Nywele zinahitaji madini ya chuma ili ziweze kuwa katika hali nzuri ya afya. Kukosekana kwa madini ya chuma husababisha nywele kunyonyoka. Mwili unapokosa madini ya chuma, hewa ya oxygen na virutubisho hushindwa kufika vizuri kwenye mizizi ya nywele hivyo hufanya nywele kuwa dhaifu na zisizo na muonekano mzuri.

Mboga za majani aina ya spinachi ni suluhisho, kwakuwa zina madini ya chuma kwa wingi ambayo seli za nywele huhitaji.

3. Jamii ya Machungwa, Limao

Mwili wa binadamu huhitaji vitamini C ambayo husaidia kuhuisha utendaji wa madini ya chuma. Hivyo, unapaswa kuongeza matunda ya jamii ya ‘citrus’, kama vile machungwa, chenza, balungi na limao. Pia, unaweza kutumia na asali pamoja.

Vitamini C husaidia katika ukuaji wa nywele kusaidia usambaaji wa virutubisho na ukuaji wa haraka wa nywele.

4. Karoti

Ni muhimu sana kuhakikisha unakunywa juice ya karoti kila siku, kama unataka nywele zako zikue haraka zikiwa na mwonekano mzuri wenye afya. Vitamini A inayopatikana kwenye karoti ni muhimu sana kwa ukuaji wa seli za nywele. Kumbuka nywele zina tishu ambazo hukua haraka zaidi katika mwili.

Karoti ina mafuta asili yanayofahamika kama ‘sebum’ na mizizi ambayo husaidia kukuza nywele kwa haraka.

5. Parachichi

Tunda aina ya parachichi lina kazi nyingi sana mwilini kama matunda mengine, lakini hili ni tunda la kipekee amnbalo lina utajiri wa vitamini E ambayo husaidia mzunguko wa damu na katika hilo husaidia mfumo wa ukuaji wa nywele kwa haraka.

Tunda hili husaidia kuhuisha na kurekebisha mafuta na kiwango cha PH (inayosafisha kemikalii mwilini) ambavyo kama vitazidi kwenye mwili vinaweza kusababisha kusimama kwa ukuaji wa nywele, yaani nywele hudumaa.

Kwa faida zaidi, vitamin E inayopatikana kwenye parachichi kwa wingi husaidia zaidi afya ya moyo wa binadamu na zaidi ngozi. Hakikisha unapata tunda hili kadiri iwezekanavyo.

Hivi ni baadhi tu ya vyakula na matunda kwa ukuaji mzuri wa nywele zako. Kama unatumia vizuri mlo wako, utakuwa adimu sana kutumia mafuta yenye kemikali ambayo yanaweza kukuletea madhara mabaya.

Jinsi ya Kuondoa Makovu Mwilini

Makovu sio kidonda naomba hili uelewe, ila makovu ni alama ya majeraha ambayo yamebaki kwenye ngozi baada ya kupona majeraha.
Kuna baadhi ya watu husumbuliwa na shida ya kuwa na makovu sehemu mbalimbali ya mwili.
Hivyo kama wewe ni miongoni mwao maandishi haya yanakuhusu sana.

Zifuatazo ndizo mbinu za kuondoa makovu mwilini.

1. Tango

Unachotakiwa kufanya ni; Pondaponda tango na kisha kutumia mchanganyiko wake kwa kupaka juu ya kovu. Hii husaidia sana kulainisha makovu na ikiwa utatumia kwa muda mrefu huondoa makovu pia.

2. Aloe vera.

Unachotakiwa kufanya ni; kata majani hayo na utumie utomvu wake kupaka katika makovu kisha mara baada ya muda Fulani utaona mabadiliko na itapunguza na kuondoa makovu.

3. Asali

Unachotakiwa kufanya; Paka asali juu ya kovu na kuiacha usiku kucha. Rudia mara kwa mara kupaka asali hadi pale kovu litakapotoweka.

Mavazi Mazuri kwa wanawake wanene

Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiangaika kupata aina ya nguo za kuvaa tena hasa wanawake wanene, kutokana na maumbo yao wanaona ni kazi sana kutafuta nguo, wengine hukosa hata uhuru wa kutoka out na watu wao wa karibu kwa sababu tu wanakosa nguo.Wengi ujikuta wakichagua nguo pana pana ili kuficha maumbo yao, lakini kumbe unaweza kuwa huru sana na mwili wako.

Zifuatazo ni badhi ya tips zinazoweza kukusaidi kuchagua nguo za kuvaa kwa mwanamke mnene.Inawezekana nguo hizi unazo ndani lakini unashindwa kuzipangilia;

1. Kabla ya kuchagua nguo ni lazima kujua mwili wako una unene wa aina gani,ikiwa wewe ni mnene na unatumbo kubwa basi ni bora kuvaa gauni maana gauni uweza kukuweka vizuri na pia ni mazuri hasa kwa watu wanene.

2. Lakini pia kama wewe ni mnene na umebahatika kuwa na maziwa makubwa, ni vizuri kupendelea kuvaa nguo zenye v-shape, siri ya nguo hizi ni kwamba huwa na tabia ya kuficha ukubwa wa maziwa na kufanya uwe maridadi zaidi ila zingatia kuchagua brazia nzuri kuikaa blauzi yako sawia.

3. Kwa mwanamke mwenye hipsi anashauriwa kuvaa nguo zinakazo mfanya hasionyeshe sana hipsi zake tofauti ya yule hasiekuwa na hipsi , maana yeye anatakiwa kuvaa nguo itakavyo onyesha hipsi zake , hata hivyo kwa wanawake wanene wenye hipsi hawana haja ya kujibana sana kwa sababu hipsi huweza kujitokeza zenyewe tu.

4. Lakini pia kuchagua rangi ya nguo nzuri pia husaidia kupunguza au kuongeza umbile la mtu, kuna rangi huweza kukufanya ukawa mnene sana au mwembamba sana,kwa mfano nguo zenye mistari ya kulala sio nzuri kwa watu wanene maana hutanua miili yao.Lakini pia rangi za giza hupunguza muonekano wa unene ilihali rangi za mwanga huangaza na kufanya mtu aonekane sana.

Zingaia:

-Ni bora zaidi katika kuchagua rangi nguo za rangi nyeusi na nyeupe iliyochanganywa ni nzuri zaidi inafanya muonekano wa mtu uonekane maridadi zaidi.

-Lakini pia jitahidi kuvaa viatu vinavyoendana na mwili wako ,sio lazima kuvaa kiatu kirefu wakati mwili wako hauimili mikikimikiki ya kiatu kirefu, flatshoes pia hupendeza zaidi kwa mtu mnene .

Jinsi ya kufanya nywele zako ziwe na mvuto na kuvutia zaidi

Mwanamke unywele hasa ukiwa nao, hii ni kauli upya ambayo Muungwana blog inakupa siku ya leo. Miongoni mwa maswali ambavyo huwa tunaulizwa na wasamoaji wetu ni pamoja ni kwa jinsi gani naweza kutengeneza nywele zangu ili ziwe za kuvutia?

Basi nasi bila ya haiana yeyote ile tunakuletea somo hili maalum kwa ajili ya watu wote ambao wanatamani kujua namna ya kuzifanya nywele zako zivutie. Kwanza kabisa kuna vitu vingi vinavyoweza kufanya nywele zako zikakosa afya na mvuto, vitu kama vumbi, upepo, mvua, jua, maji na madawa tunayoweka kwenye nywele zetu pamoja na vyakula tunavyokula ni chanzo kikuu cha nywele zetu kuharibika na kukosa afya na mvuto

Hivyo zifuatazo ndizo njia ya kufanya nywele zako zivutie:

Tumia shampoo inayoendana na nywele zako

Tumia shampoo inayoendana na nywele zako, kuna nywele za aina tofauti. kuna nywele kavu, zenye mafuta, mchanganyiko, na pia kuna nywele nyepesi, laini, ngumu na nzito. zipo aina tofauti za shampoo zinazoendana na aina ya nywele zilizopo . hivyo basi ni vyema unapotaka kuosha nywele ukajua ni aina gani ya shampoo utumie, pia kwenye condition napo unatakiwa kufanya hivyo hivyo.

Usichane nywele kwa nguvu zikiwa mbichi.

Jaribu kuzichana nywele kwa kichanuo kikubwa, au jaribu kuziacha mpaka zikauke ndo uzichane. unapochana nywele mbichi tumia kitana kikubwa na chana taratibub ukianzia nyuma kuja mbele. kuchan nywele zikiwa mbichi bila kufuata utaratibu kutafanya nywele zako zikatike na ziharibike.

Kula vyakula venye protin na matunda

kula vyakula venye protin na matunda kutasaidia kuimalisha afya ya nywele zako na kuzifanya ziwe nzuri na za kuvutia.

Kata ncha za nywele zako

kukata ncha za nywele zako kunasaidia kufanya nywele zako kujizaa upya, mara nyingi seli katika ncha za nywele hufa. seli zinapokufa huzui nywele zinazozaliwa kushindwa kustawi vyema na hivyo kuzifanya nywele zako kukosa afya. japo wanawake wengi huwa hawapendi kukata ncha za nywele zao wakihofia nywele zao kuonekana fupi. lakini ukweli ni kwamba unapokata ncha za nywele zako unasaidia nywele zako kupata nafasi ya kukua vizuri na kuwa zenye afya nzuri na kuvutia.

Osha nywele zako angalau mara moja kwa wiki

kuosha nywele zako angalau mara moja kwa wiki kutasaidia kuzifanya nywele zako ziwe na afya. Hata kama uko busy sana basi jitahidi isipite wiki mbili bila kuonsha nywele zako.

Zifunge nywele zako kabla ya kulala

Unapotaka kulala hakikisha unazifunga nywele zako, unaweza kuzisuka mabutu au kuzifuna vizuri na kuzibana. kulala huki ukiwa umeziachia nywele zako hufanya nywele zikatike na kuharibika

Tumia mafuta asili

Badala ya kutumia mafuta yenye kemikali nyingi kutoka viwandani, jaribu kutumia mafuta ya asili katika kutunza nywele zako. tumia mafuta kama ya nazi au parachichi kupaka nywele zako.

Zilinde nywele zako na jua

W akati utakapokuwa unaelekea kwenye sehemu yenye jua kali, vumbi au upepo. zilinde nywele zako kwa kuzifunika na kofia, scarf au mtandio. Pia unaweza kuzipaka sunscreen.

Madhara ya Kuvaa/ Kuweka Kope Za Bandia

Mapokeo ya urembo wa kisasa katika nchi zinazoendelea ni sehemu ya mchango wa urembo na mvuto tunaouona kwa baadhi ya wasichana na wanawake ambao kwa hakika unaleta hamasa ya kuangalia.
Hata hivyo, urembo huu huja na hatari zake ambazo wengi wanaweza kuzichukulia poa kwa kuwa hazitokei kwa haraka ama katika muda unaoweza kutolewa ushahidi kwa sasa.

Moja kati ya urembo unaofanywa na wanawake wengi wa kisasa ni kuweka kope za bandia juu ya kope halisi, kweli wengi wanakuwa na mvuto wa aina yake wakikuangalia hasa mtoto wa kiume. Lakini hatari inayotokana na urembo huo ni kubwa zaidi ya matokeo ya muda mfupi.

Wataalam wanaeleza kuwa kope za bandia ambazo hugundishwa kwa kutumia gundi ya nywele inayotumika kugundisha nywele bandia kwa wenye vipara inaweza kuwa chanzo cha upofu wa mtumiaji.

Gundi hiyo hupukutika taratibu sana kiasi cha kutoshtukiwa na kuelekea kwenye mboni ya jicho ambayo ndio moyo wa ‘kuona’. Endapo mtumiaji ataendelea kwa muda mrefu kutumia kope hizi bandia anaweza kujikuta anakuwa na tatizo la kuona ama hata upofu wa haraka katika maisha yake ya baadae.

Hata hivyo, hatari kubwa imeelekezwa kwa maduka ama vibanda vinatumia vifaa vya bei nafuu ikiwemo gundi inayotumika. Ukwepaji wa gharama ama kutokuwa na uwezo wa kutumia gharama kubwa kunamuingiza mrembo kwenye hatari zaidi.

Kuwa mwangalifu, urembo usiwe chanzo cha kuhatarisha afya yako. Kumbuka Afya ni uhai wa mwili wako.

Shopping Cart
2
    2
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About