Dondoo za Urembo na Mitindo

Madhara ya kuchora tattoo mwilini

Tattoo ni nini?
Hii ni uwekaji wa wino kwenye ngozi ya ndani kitaalamu kama dermis kubadilisha rangi kabisa maisha yako yote au kwa muda tu, inateemea na uwekaji..
Kwa dunia ya sasa kujichora tatoo ni kama fasheni fulani kwenye jamii, ukienda kuchora tattoo kuna uwezekano mkubwa sana isitoke maisha yako yote hivyo kwa usalama wako ni vizuri ukamuona mtaalamu wa tattoo ambaye ni maarufu na ana sifa kubwa katika shughuli hizo, anaweza kua ana gharama kubwa lakini binafsi itakusaidia.kwa sasa nchi ya marekani inaongoza kwa kua na watu wengi wenye tattoo duniani.

Hivyo kabla hujaamua kujichora tattoo basi madhara yake haya hapa..

Kansa ya ngozi; hapo mwanzoni wataalamu walikua wanasema hakuna mahusiano kati ya kansa ya ngozi na na tabia ya kujichora tattoo lakini hivi karibuni tafiti kutoka uingereza zinaonyesha kuna aina fulani za wino ambazo zinaweza kusababisha kansa zikitumika kuchora tattoo.

Allergy ya ngozi; haijalishi unaweka tattoo kwa muda au ya moja kwa moja kumetokea kesi nyingi za watu wanaopata allergy baada ya kupakwa tattoo, utafiti unaonyesha rangi nyekundu ndio inaongoza kwa kusababisha allergy hizo huku rangi zingine kama nyeusi, purple na zingine hazisababishi. mara nyingi allergy hizi huonekana mtu akikaa juani.

makovu; mwili unataambua tattoo kama adui wake hivyo hujaribu kuiondoa kwa njia mbalimbali na kwa kufanya hivyo husababisha makovu ya muda mrefu ambayo yanaweza kuleta magonjwa mengine ya ngozi.

Maambukizi ya ukimwi na ugonjwa wa hepatitis; tabia ya kurudia sindano zilezile wakati wa kuchora tattoo kunaweza kusababisha maambukizi ya virusi vya ukimwi na maambukizi ya virusi vinavyoshambulia ini kitaalamu kama hepatitis b. ugonjwa huu wa hepatitis b husababisha kansa ya ini ambayo haitibiki. ni vizuri kua makini ili uone kama sindano inayotumika kwako ni mpya.

Matatizo kipindi cha kufanya kipimo cha MRI; hichi kipimo ni cha mionzi na kirefu chake ni magnetic resonance imaging, hutumika kupima viungo vya mwili ambavyo havionekani kwa macho ndani ya mwili wa binadamu kama x ray inavyofanya. tatizo ni kwamba kipimo hiki kina sumaku kali kiasi kwamba mtu hatakiwi kuingia kwenye mtambo huo akiwa amevaa chuma chochote na hata kama kiko ndani ya mwili kitavutwa nje, sasa mara nyingi tattoo nyeusi hua imetengenezwa na compound kitaalamu kama iron oxide ambayo ina chembechembe za chuma. hii inaweza ikaleta changamoto kubwa kwenye vipimo.

Kubadilika kwa ngozi ya rangi; sehemu inayochorwa tattoo hubadilika moja kwa moja na kua na rangi tofauti, hakuna jinsi unaweza ukaitoa hiyo rangi tena, hata baada ya muda mrefu tattoo ikipungua nguvu lakini ngozi haiwezi kua kama zamani.

Hutaruhusiwa kuchangia damu; mara nyingi watu wenye tattoo hawaruhusiwi kuchangia damu kwani wana hatari ya kusambaza ugonjwa kwenda kwa mtu mwingine, kimsingi mtu aliyechora ndani ya muda mfupi ndio haruhusiwi lakini kwasababu wakati mwingine sio rahisi kutofautisha tattoo mpya na ya zamani basi hawa watu huwa hawaruhusiwi kabisa.mchezaji wa kimataifa christian ronaldo hachori tattoo kwa sababu ya hili.

Unaweza kukosa fursa mbalimbali; kuna kampuni mbalimbali duniani haziwapi watu kazi kwasababu wamechora tattoo kulingana na imani za kampuni husika lakini pia kazi yeyote ya jeshi duniani hairuhusu tattoo hivyo kama wewe unayesoma hapa umeshachora tattoo ujue kazi ya jeshi huna tena.

Tattoo huingiliana na matumizi ya dawa fulani; kama wewe unatumia dawa za kuzuia damu isingane mwilini ukichora tattoo inaweza kufanya utoke damu nyingi sana kwani dawa hizo huzuia uwezo wa mwili kukausha damu na kuponyesha vidonda.

Magonjwa ya ngozi; wakati mwingine bacteria huweza kuvamia sehemu zenye vidonda vya tattoo na kusababisha kutopona haraka, dalili huweza kua homa kali, maunivu makali na sehemu ya tattoo kuvimba.

Damu kuganda juu ya ngozi[haematoma]; hii husababishwa na kuvuja kwa damu nyingi chini ya ngozi, huonekana sana pembeni pembeni ya sehemu ambapo rangi ya tatoo imepita na huchelewesha kupona kwa kidonda.

Nini kifanyike kwa wanaopenda tattoo?

Siku hizi kuna tattoo zinachorwa juu ya ngozi kama hina na kuondoka baada ya muda fulani, hizi hazina madhara kabisa, huchorwa kwa bei ndogo na hukupa nafasi ya wewe kubadilisha tatoo za aina mbalimbali kwenye sehemu moja ya mwili.

Je tattoo inafutika?

Ni ngumu sana kuifuta tattoo na hii ni changamoto kwa watu ambao wamechora tattoo za majina au sura za wapenzi wao wa zamani. kuna kikaa kinaitwa laser ambacho kinaweza kutumika kufuta tattoo yote au sehemu ndogo tu ya tattoo. mara nyingi rangi nyeusi zinaweza kutoka ukilinganisha na rangi zingine. maumivu yanayotumiaka kuiondoa tattoo ni makali kuliko maumivu ya kuiweka na hapa kwetu tanzania siana uhakika kama huduma hii ya kuondoa tattoo ipo.

Madhara ya Kuvaa viatu virefu

NI wazi kuwa viatu virefu huvutia sana vinapo kuwa vimevaliwa.Tulio wengi hasa mabinti au wanawake tunaokwenda na wakati hupenda kuvaa viatu virefu ilikuongeza muonekano wa umbile lako nikiwa na maana kuwa miguu huonekana yenye kuvutia zaidi unapo kuwa umevaa viatu virefu.

Kutokana na utafiti wa kitaalamu, mwanamke ana uwezo wa kutembea wastani wa hatua 10,000 kwa siku.Visigino virefu hufanya nguvu inayotumika kutembea hatua moja kuwa kubwa kuliko kawaida, huku vikikunyima raha ya kutembea kwa uhuru kiasi kwamba wengine hufikia hatua ya kuvua na kutembea peku.

Leo hii napenda kukujuza madhara ya uvaaji wa wa viatu virefu.Kwa kawaida, miguu ya binadamu hasa visigino, vimeumbwa ili kuuzuia uzito wa mwili juu ya ardhi.Uvaaji wa viatu virefu hufanya uzito wa mwili kubebwa na kisigino, hivyo uzito wa mwili kushindwa kuhimili uzito wote.

Matokeo yake husababisha misuli na mishipa ya miguu, kiuno, mgongo na shingo kufanya kazi kubwa ya kujaribu kusawazisha uzito.Kazi ambayo kwa kawaida hufanywa na visigino.Tatizo hilo hupelekea kiuno,Miguu na mgongo kuwa katika hatari ya matatizo ya kiafya pamoja na kuteguka na kuvunjika miguu.

Visigino virefu hubadili muundo wa mifupa ya miguu, hivyo hupelekea magoti na misuli ya mapaja kufanya kazi ya ziada ili kuupa mwili usawa.Kwa kuwa misuli inafanya kazi kubwa, uwezekano wa kupatwa na maumivu makali ya miguu na kushindwa kutembea katika siku za baadae huwa mkubwa zaidi. Visigino virefu husababisha maumivu ya visigino, damu kuvilia ndani ya miguu, mpangilio wa mifupa ya vidole kuvurugika, mishipa na misuli ya mapaja kuuma, neva za fahamu kufungana na kushindwa kufanya kazi yake.

Tatizo huendelea kwa vifundo vya miguu, magoti, na mifupa ya kwenye mapaja kushindwa kujivuta na kulegea na hivyo kusuguana wakati wa kutembea.

Jambo la kuzingatia kwa wale wanaopenda kuvaa viatu virefu,ni vema kama unapenda kuvaa viatu virefu hakikisha hutembei umbali mrefu kama una usafiri sio mbaya ukivaa viatu virefu,na kwa wale wanao kwenda ofisini jitahidi kuwa na viatu flati ndani ya mkoba wako ili unapokuwa umechoka unavua na kuvaa viatu vyako pia ukiwa ofisini waweza kuvua viatu virefu.

Mpenzi msomaji kama huwezi kutembelea viatu virefu nivema ukipitwa na wakati kuliko kujiabisha barabarani na kuonekana rimbukeni ikiwa wewe ni mjamzito epuka uvaaji wa viatu virefu.Usikose kujumuika nami katika safu hii ya urembo na mitindo.

Umuhimu wa kuvaa soksi

Miguu ni sehemu mojawapo inayotoa jasho sana hivvo ni vema kuiweka mikavu kuzuia ukuaji wa bacteria au fungus.Wakaka tunajua umuhimu wa soksi au tunavaa bila kujua na wengine hatuvai? Hii ni kwa wadada pia wanaovaa viatu kama raba au hata nyumbani. Ni vema sana kufahamu kwanini tunavaa soksi na mda mwingine soksi gani tuvae.

1. KUZUIA MAGONJWA YA NGOZI MIGUUNI.

Tumia sekunde tatu tu kuvaa soksi na ujikinge na maradhi haya ya fungus na bacteria, kama sio mpenzi was soksi nashauri ufikirie tena maamuzi yako ya kutovaa soksi.

2. EPUKA HARUFU MBAYA YA MIGUU

Image result for atletes foot
Kwa kweli hii ni kero kwako na wanaokuzunguka.Usipovaa soksi jasho lote la miguu litaenda kwenye viatu na ivo viatu kutoa harufu.Soksi hunyonya lile jasho na huzuia harufu iyo. Aya basi tushtuke aibu hii ya nini katika karne ya watanashati sisi.Tuvae soksi na kubadili kila siku.

3. LAINISHA NGOZI YA MIGUU YA YAKO

Nani hapendi miguu soft?? wadada kutwa kusugua miguu saloon.Simple ukirud nyumban kama sakafu ni ngumu vaa soksi zako nyepesi safi miguu iwe laini.Baadhi ya viatu pia vina surface ngumu kwa chini (wakaka) ukiweka soksi zako safi hamna maneno.

4. KUPUNGUZA MAUMIVU MIGUUNI

Hii hasa kwa watoto wadogo ..tuwazoeze mapema kuvaa soksi.Mtoto anatembea ndani Mara akanyage maji mara vitu vya ncha Kali….Pia kuna viatu ukivaa bila soksi lazima upate maumivu na kupata zile sugu nyeusi.

5. KUPATA JOTO NYAKATI ZA BARIDI

Wale was mikoa iliyo na baridi kwa sasa naamini tuna soksi za kutosha za miguuni na mikono.Kama kuna sehemu inayongoza kutoa joto ni miguuni na mikononi.Basi vaa soksi ili kuzuia joto lisipotee.

6. MVUTO

Ili sio geni, mi mtu akivaa viatu bila soksi kwa kweli napunguza maksi za utanashati…wengine wanasema kuna viatu vya kutovaa soksi. .hakuna kitu kama icho kuna soksi ndogo ambazo hazionekani kwa juu zimejaa tele madukani tutafte.Ebu mtu kavaa kiatu chake safi akiweka na soksi safi inaonekana mvuto lazima uwepo….Nani hapendi kuvutia??basi sote tunapenda tuvae soksi

Siandiki mengi sana, soksi sio jambo geni, tubadilike tujijali,.Ok unavaa soksi Je?unavaa soksi pea moja mara ngapi, unafua na kukausha vizuri maana soksi mbichi ni janga jingine la uchafu na maradhi.Kitu kingine ujue aina ya soksi nyakati za joto usivae soksi ambazo ni nzito sana vaa nyepesi, ambazo ni nzito vaa nyakati za baridi. Na soksi za watoto tununue ambazo hazibani sana.

Dawa za nywele zinazosababisha uvimbe kwenye Kizazi kwa wanawake

Dawa za kulainisha nywele (relaxer) zimekuwa zinapendwa na wanawake wengi wa Afrika kwa kuwa zina uwezo wa kulainisha nywele na kumfanya apendeze na awe wa kuvutia.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa hizo zinasababisha uvimbe kwenye kizazi kutokana na kemikali za dawa hizo ambazo huingia mwilini kupitia majeraha au ngozi wakati wa kupaka.

Daktari wa Manispaa ya Ilala, Laurent Chipata alifanya utafiti na kubaini kuwa dawa za nywele na vipodozi zina kemikali ambazo husababisha uzalishwaji wa vichocheo kwa kiasi kikubwa na kusababisha uvimbe kwenye kizazi uitwao fibroids au leimyoma.

“Kemikali hizi hupenya kwenye ngozi na wakati mwingine hata kwa harufu tu, husababisha kuzalishwa kwa wingi wa vichocheo aina ya estrogen ambavyo huchangia kuota kwa uvimbe wa fibroids,” anasema.

Dk Chipata anasema kukua kwa uvimbe kwenye kizazi hutokea katika kipindi ambacho mama yupo kwenye uzazi yaani kabla hajakoma hedhi.

Utafiti wa Dk Chipata ulifanywa nchini na kujumuisha wanawake wa kada tofauti tofauti wanaotumia dawa za nywele na wale wasiotumia na ukubwa wa tatizo hili ulibainika.

“Zipo kemikali tofauti tofauti zinazosababisha uvinbe kwenye kizazi, zipo za kwenye dawa za kilimo kama DDT na za kwenye mafuta ya ngozi kama vile mercury na hydroquionone,” anasema.

Dk Chipata anasema madhara yanayopatikana katika kemikali za vipodozi ni makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine husababisha saratani au kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya zebaki (mercury).

“Dawa za nywele zina madhara si lazima zipenye kwenye ngozi baada ya mtu kupata jeraha la kuungua bali zinaweza kupenya zenyewe kwenye ngozi kutokana na mfumo wa ngozi,” anasema.

Anashauri kuwa ni vyema watu wakasoma kipodozi kimetengenezwa kwa nini kabla ya kukitumia na kuongeza kuwa ni salama zaidi kubaki na ngozi au nywele halisi badala ya kujibadilisha.

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekataza vipodozi vyenye kemikali kama biothionol, hexachlorophene, mercury, vinyl chloride, zirconium na bidhaa zenye aerosol, chloroquionone, steroids, methylene na chloroform.

Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2012 na Dk Lauren Wise na wenzake nchini Marekani na kuchapishwa kwenye jarida la afya la nchini Marekani ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye vichocheo vya estrogen ambavyo kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke na wakati mwingine kwenye mji wa mimba. Kitaalamu uvimbe au vivimbe hivi hujulikana kama fibroids au myoma.

Dk Wise anasema aliwafanyia uchunguzi wanawake wanaotumia dawa za kulainisha nywele na kuangali umri walioanza kutumia dawa hizo, mara ngapi, waliungua kiasi gani na walikaa na dawa hizo kichwani kwa kipindi gani.

Aliwafuatilia wanawake 23,580 wanaotumia dawa za kulainisha nywele na baada ya kipindi fulani walipimwa. Kati yao, 7146 waligundulika kuwa na uvimbe kwenye kizazi baada ya kupimwa kwa mionzi na wengine kufanyiwa upasuaji.

Kwa nini relaxer ni hatari kwa wanawake?
Dk Wise anasema mchanganyiko ulio kenye dawa za nywele hasa zilizoandikwa “Lye Relaxer” ni sodium hydroxide wakati makopo ya dawa yaliyoandikwa “No Lye Relaxer” yana calcium hydroxide na guanidine carbonate.

Bidhaa za kulainishwa nywele zilizoandikwa ‘no lye relaxer’ zinadaiwa kusababisha majeraha kwa kiasi kidogo ukilinganisha na zile zilizoandikwa “Lye Relaxer”.

Madhara ya Kujichubua

Katika baadhi ya sehemu duniani watu wanaamini kuwa ngozi angavu huashiria uzuri, utajiri na uwezo(kifedha) alionao mtu.Katika baadhi ya sehemu watu wenye ngozi nyeusi huchukuliwa kuwa wapo chini ya kiwango, hii hupelekea watu hawa kutumia ving´arisha ngozi kama krimu, vidonge au nyenzo zingine kubadilisha ngozi zao.

Tafiti zinaonyesha kwamba wavulana na wasichana hupendelea kutumia bidhaa zinazong´arisha ngozi ili waweze kupata hadhi nzuri katika kundi la familia zao, na jamii. Kwa kweli,hata matangazo yanayoonyeshwa kwenye televisheni mbalimbali huonyesha kitu hiki. Mambo hayo yote huwa na athari kubwa juu ya mawazo ya vijana wa kiume na wakike ambayo hupelekea kuwafanya wachague chochote wanachomudu kati ya krimu au vidonge.

Madhara ya kujichubua ni yapi?
Mtu anaeyejichubua anaweza kupata kansa ya ngozi, chunusi, uvimbe katika ngozi, ngozi kuwa nyembamba,Kuongezeka kwa hamu ya kula na uzito,kutokwa na mabaka, pumu, kupata watoto wenye kasoro, kupata matatizo ya akili, kuharibika kwa ini, kuharibika kwa mishipa ya fahamu pamoja na figo kutokana na kiwango kikubwa cha zebaki(mercury) kilichomo katika krimu,Osteoporosis(kupungua kwa uzito wa mifupa ambapo huongeza hatari ya kuvunjika kwa mifupa)

Baadhi ya madhara haya huonekaa mara moja na mengine hujitokeza kadri mtu anavyotumia ving´arisha ngozi.

Madhara ya Uvaaji wa Wigi au nywele Bandia

Katika miongo kadhaa iliyopita, uvaaji wa wigi umekuwa fasheni katika sekta ya urembo na hutumika hususani na wanawake. Ingawa uvaaji wa wigi huwafanya wanawake hao kuonekana mithili ya mtu aliyevaa kofia ngumu (helmet), lakini yaonekana ni mapendeleo ya wengi.

Wanaume wengi hujiuliza , “Ni kwanini kina mama hupendelea kuvaa wigi na kusuka nywele za bandia?, wakati hupendeza na kuwa warembo zaidi wakiwa na nywele zao za asili”?

Wigi huvaliwa zaidi na kinamama wenye asili ya Afrika au Wamarekani wa asili ya Afrika. Lakini tukiangalia moja ya chimbuko hasa la uvaaji wigi ni ubaguzi uliokuwepo wakati wa utumwa ambapo wale wenye ngozi nyeupe na nywele shombeshombe walipewa kazi za ndani na wale wasio na ngozi nyeupe na nywele zisizo shombeshombe walifanyishwa kazi ngumu za mashambani.

Watumwa waliopelekwa barani Amerika hawakuweza kuzihudumia nywele zao kutokana na hali ngumu, na mabwenyenye waliwashusha hadhi na kuwavunja moyo kwa kuwaambia hawakuwa na nywele bali ni “manyoya”.

Lakini sababu nyingine inayodhaniwa kuwaathiri wanawake wa asili ya Afrika ni fikra kuwa mwanamke mwenye nywele ndefu pengine hadi mgongoni ni mrembo zaidi. Pia siku hizi warembo na wanaoshiriki katika mashindano ya urembo hujaribu kurefusha nywele zao ili kuwa na viwango na aina za mitindo ya ughaibuni.

Pamoja na kuwa wanawake wanajaribu kuwa warembo kwa uvaaji wa wigi, zifuatazo ni baadhi ya hasara au madhara kiafya ya uvaaji wigi na usukaji wa nywele za bandia.

Uvaaji wa wigi au nywele za bandia waweza kukusababishia mzio (allergy), endapo malighafi au kemikali zilizotumika kutengeneza wigi hiyo zitasisimua mfumo wa kinga ya mwili wa mvaaji.

Kupata m-ba ni tatizo jingine kutokana na uvaaji wigi, hii hutokana na kukosekana kwa hewa ya kutosha ya Oksijeni katika ngozi ya kichwa (scalp hypoxia) na katika tishu za shina la nywele. Kwa hiyo kama utaamua kuvaa wigi uhakikishe imetengenezwa kwa viwango vya ubora unaotakiwa na inapitisha hewa ya kutosha ya Oksijeni.

Pia waweza kunyonyoka nywele hata kama una nywele nzuri zenye afya, na kama utachagua kuvaa wigi na unataka kuepuka madhara hakikisha kuwa nywele zako ni safi, usilazimishe kuvaa wigi iliyo ndogo na yenye kubana sana, hakikisha unapata muda wa kupata hewa na nywele zako zinapakwa mafuta kuepuka ukavu wa ngozi ya kichwa na nywele kukatika .

Maumivu ya kichwa ni tatizo ambalo laweza kusababishwa na uvaaji wigi au usukaji wa nywele bandia. Wigi iliyo ndogo husababisha mkandamizo kichwani na kusababisha maumivu ya kichwa ya mara kwa mara.

Upotevu wa muda na fedha ni dhahiri kwa kuwa ufumaji wa nywele za bandia waweza kuchukua muda mrefu, itamlazimu mvaaji wigi kubadili kwa kununua mpya kila baada ya muda fulani au kuwa na wigi nyingi kwa ajili kubadili kulingana na fasheni.

Harufu mbaya huweza kujitokeza endapo mba na jasho vitachanganyikana na hupelekea uwepo wa bakteria au fangasi na kusababisha muwasho mkali, hii yaweza kumkosesha raha mvaaji wigi na mwenye kufuma nywele za bandia hasa pale anapokuwa katika majumuiko ya kijamii.Kama utachagua kuvaa wigi hakikisha nywele zako zinasafishwa na shampoo au sabuni, zinakaushwa vizuri na kupakwa mafuta.

Endapo mwanamama atachagua kuvaa wigi,asisahau kuwa nywele zake za asili zinahitaji matunzo,na azingatie wakati wa kununua wigi au nywele za bandia, ahakikishe ananunua yenye ubora unaotakiwa ili kuepuka madhara ya kiafya anayoweza pata kutokana na uvaaji wigi au anapofuma nywele za bandia.

Benson Chonya

Namna ya uvaaji wa mavazi mbalimbali kwa wanaume

Wanaume wanajali mavazi yao pia, sio wanawake tu. Ila, mwanaume anabidi aelewe kwamba badala ya kufuata mitindo, kupendeza kwenye tukio lolote kuna nguo ambayo utaihitaji. Nguo hizi ni kama:

1. T-Shirt ya Pamba

Ukitaka t-shirt itakayo dumu kwa muda mrefu, nunua t-shirt zilizotengenezwa kwa pamba tu. Pia, kuwa na t-shirt kadhaa zenye rangi tofauti, zikiwemo:

Za rangi ya kawaida kama Nyeupe, nyeusi, rangi ya kijivu
Za rangi kali kama Njano, bluu nyepesi na kijani
Uzuri wa t-shirt ni kwamba zinaweza kuvaliwa na chochote kile. Kwa hiyo, kuwa na aina nyingi kabatini.

2. Polo Shirts

Mwanaume yoyote anatakiwa kuwa na Polo Shirt (t-shirt zenya kola) kadhaa. Zinafaa sana kuvaliwa kazini kwenye siku za Ijumaa au weekend.

3. Mashati ya kawaida

Mashati ya kawaida, ya mikono mirefu au mifupi, ni mazuri kuvaa na jinzi na viatu au raba. Pia, zipo za aina na rangi tofauti kwa hiyo tafuta itakayokufaa.

4. Mashati ya shughuli/sherehe rasmi

Kutegeamea na ajira yako, shati ya aina hii inaweza ikawa nguo utakayoishia kuvaa kuliko zote. Kwa hiyo, lazima uwe nazo za kutosha za aina mbalimbali.

Pia hata kama huzihitaji kwa kila siku, utazihitaji kwa sherehekama harusi au mkutano mkubwa wa kikazi.

Muhimu kuliko vyote ni kuhakikisha unajua saizi yako na kwamba unavaa shati linalo kutosha vizuri kabisa. Zaidi ya hapo, fikiria tai utakayoivalia.

5. Bukta

Kwa kuzingatia joto lote la Tanzania, bukta ni muhimu.

Kuna aina nyingi za bukta na zenye rangi tofauti. Zinaendena na polo shirt pamoja na viatu vya kawaida. Ni mazuri kuvaa kwenye wikiendi ukiwa umetulia na washkaji.

6. Suruali za kawaida

Suruali za aina hii zina faraja na zinavaliwa kwenye mazingira mbalimbali. Pia, kama polo shirt zinapatikana kwa rangi nyingi kwa hiyo zinaweza kuvaliwa na mashati, viatu, kodia n.k za ain nyingi.

7. Jinzi

Jinzi zinaweza kuvaliwa kokote, siku yoyote.

Iwe ijumaa kazini au jumamosi usiku, hata kazini kwenye siku ya kazi (kutegemea na masharti ya kazini kwako), jinzi zitavaliwa tu. Zipo za aina nyingi, rangi tofauti na zinavaliwa na chochote kile.

Ila, ni muhimu kujua saizi yako ile upendeza unavyostahili. Pia, jinzi zenye ubora zitakuwa na bei zaidi ila bora ununue jinzi yenye ubora itakayodumu kwa miaka kuliko jinzi isiyo na ubora itakyodumu kwa miezi.

8. Koti la suti

Mwanaume yoyote anatakiwa kuwa na koti za suti za rangi ya bluu na kijivu kabatini. Rangi hizi zinaendana na sherehe rasmi na zisizo rasmi, na zinavaliwa na aina mbalimbali ya mashati na viatu.

Ila, muhimu zaidi ya rangi ni saizi. Hakikisha unajua saizi yako na kwamba koti zinakutosha vizuri.

9. Chupi na Soksi

Hakikisha chupi zako ni nzuri, zinakutosha na ni safi (usije ukajiaibisha). Kama zimechakaa, zitupe.

Soksi nazo ni vilevile. Ila, unahitaji kuwa na aina tofauti za soksi kwa ajili ya mavazi tofauti. Hakikisha rangi ya soksi zako zina ukali au ni nzito kidogo ya suruali yako.

10. Viatu

Kwa kawaida, viatu ni vitu vya kwanza vya mtu kuangalia akikuona, hasa na wanawake. Kwa, sio swala la kupuuzia.

Cha muhimu ni kwamba ni visafi na ziko katika hali nzuri.

Ndio, inabidi ujaribu nguo mbalimbali ila ujue kinachokupendeza. Ila, kuwa na mavazi yasiyo na mbwembwe nyingi si mbaya. Bahati nzuri, nguo tulizoorodhesha hapo juu zitakusaidia kupendeza bila kuweka juhudi saaaaana.

Njia za kutunza nywele zako

Suala la kutunza nywele za asili wengi hutamani japokuwa ukweli kwamba kuna changamoto kadhaa, lakini kwa mtu aliye makini anao uwezo wa kupata kilicho bora katika nyewle zake. Leo tunaangazia vitu vya kufanya ili kukuza na kutunza nywele za asili.

Kwanza kabisa unapaswa kuzikubali nywele zako na kuzipenda , jambo hilo litapelekea mahusiano mazuri, kuelewa tatizo la nywele zako na kuanza kuchukua hatua taratibu ya kuzipatia uvumbuzi tatizo hilo.

Pili, unapaswa kufanya usafi wa kina wa ngozi na nywele zenyewe kwasababu endapo nywele zitaachwa chafu, basi ule uchafu unaziba matundu ya nywele na kuzuia njia kama vile ambavyo matundu ya uso yakiziba unapata chunusi.

Tatu, ni kulinda unyevu wa nywele . pale zinapooshwa, yale mafuta asilia ya kuzilinda huondoka na uchafu. Nywele inabaki ikiwa na udhaifu fulani maana haiwezi hata kushikilia hayo maji yaliyoo vizuri na zikikauka zinakuwa kavu sana. Ni vizuri kabla hazijakauka vizuri, zikafanyiwa ‘condition’ , kwa zile nywele ambazo ni nyepesi na chache pia kuna bidhaa zinasaidia kutunza vizuri unyevu na hivyo kuwa na afya nzuri.

Hatua nyingine ni ya kupaka mafuta kichwani, kwani mafuta yana umuhimu mno katika ukuaji wa nywele na mafuta mazuri ni ya nazi ambayo yamewafaa baadhi ya watumiaji wengi .

Njia nyingine ni ya kuzichambua vizuri nyele kabla ya kuzichana, hapa mtu anatakiwa kuwa na subira na nywele zake , asifanye pupa kuzichana na ikiwezekana aziloweshe maji kidogo halafu ndipo azichane kwa chanuo kubwa lenye upana wa kutosha (wide toothed comb) ili kuzipa afya na kuepuka kujiumiza wakati wa kuzichana.

Pia mtu anayetunza nywele za asili anatakiwa kupunguza matumizi ya vitu vyenye moto katika nywele zake kama vile pasi ya nywele na vingine kama hivyo. Nywele zinatakiwa zichanwe kawaida na ziachwe zikauke zenyewe kwa hewa bila kuzilazimisha.

Mambo ya Kuzingatia ili uwe mrembo siku zote

Katika Jamii nyingi duniani, dhana ya urembo imekuwa na mitazamo tofauti kwa watu wengi. Kila mmoja anautafakari urembo kwa namna yake kulingana na malezi na tamaduni za mahali husika. Wako wanaoamini kuwa mrembo ni lazima awe na ngozi nyeupe, wengine hudhani kuwa ili kuonekana mrembo, lazima uwe na nywele ndefu, lakini pia wapo wanaodhani kwamba ili uwe mrembo ni lazima uwe na umbo namba nane na wapo wanaojua urembo ni kuwa mwembamba (kimbaumbau au Miss) au kuwa mrefu na wapo wanaoamini urembo ni kuwa mnene.

Hiyo yote ni mitazamo tu, lakini tafsiri halisi kutoka kwa wataalamu wa urembo ni kwamba; urembo ni hali ya kuwa na afya bora.

Je, Mpenzi msomaji ulikuwa unajua hili? Nakuomba Kabla hujafanya chochote kuhusu afya yako, unatakiwa kuamini kwamba wewe ni mrembo. Ikiwa utasimama katika hilo ni kweli utakuwa mrembo siku zote. Basi ili kubaki kuwa mrembo tujifunze haya machache leo ya kufanya:

1. SAFISHA NGOZI YAKO:

Hakikisha ngozi yako inakuwa safi muda wote. Unaweza kutumia njia mbalimbali kama vile kuondoa ngozi zilizokufa mara kwa mara. Kuondoa mafuta yaliyogandamana katika ngozi kwa kufanyia masaji ngozi yako ili kurahisisha mzunguko wa damu yako.
Ikiwa hili litafanyika kwa umakini ni wazi kuwa matatizo ya kuwa na chunusi au weusi katika ngozi yako havitakuwepo kwako.

2. SAFISHA NYWELE ZAKO:

Tumia bidhaa za nywele, ambazo zinaendana na nywele zako na hakikisha unazingatia mambo muhimu katika uboreshaji wa nywele zako.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kutokutumia vifaa vinavyounguza vywele.

Epuka kuosha nywele kwa maji ya moto, pia kuchana nywele zikiwa na maji, kwani unaweza kusababisha kukatika kwa nywele zako.

3. USIPAKE VIPODOZI MARA KWA MARA:

Tumia vipodozi pale inapobidi, usipendelee kutumia vipodozi mara kwa mara kwani wakati mwingine matumizi ya mara kwa mara ya vipodozi, husababisha madhara katika ngozi yako, hasa unapotumia bila kufuata maelekezo ya wataalamu.

4. PATA USINGIZI WA KUTOSHA:

Hakikisha unapata usingizi wa kutosha kila siku. Kwa mujibu wa wataalamu, unatakiwa kulala si chini ya saa nane kila siku. Ikiwa utapata usingizi wa kutosha ni wazi kuwa macho yako yataonekana yenye nuru siku zote. Pia utazidi kuonekana kuwa mrembo zaidi.

5. FANYA MAZOEZI YA VIUNGO:

Hakikisha mazoezi yanakuwa sehemu ya maisha yako, hii itasaidia kukufanya uonekane siyo tu mrembo, bali pia mwenye kujiamini.

6. SAFISHA MENO YAKO:

Usafi wa meno pia ni miongoni mwa mambo ya kuzingatia unapoamua kuboresha urembo wako. Hakikisha unapiga mswaki walau mara mbili kwa siku kila siku au kila baada ya kula.

Haya yameorodheshwa na wataalamu mbalimbali kuwa ni mambo yanayochangia urembo wa asili na mvuto wa ngozi na mwili.

Mavazi ya Ofisini kwa Wadada

Wengi wetu tunashindwa kutofautisha mavazi ya sehemu husika mfano Ofisini, michezoni, na yale ya usiku na sehemu nyinginezo leo nitagusia vazi la ofisini kwa akina dada.

Unapotaka kuvaa vazi ,lazima uangalie vazi unalolivaa mda gani na mahala unapokwenda,siyo vazi la kutokea usiku au la kimichezo unalivaa ofisini,utakuwa kichekesho mbele za watu hata kwa wafanyakazi wenzio.

Mavazi ya kiofisi yanaeleweka lakini hasa kwa mwanamke basi vaa sketi fupi au ndefu na blauzi ya heshima iliyofunika kitovu chako, au suti ya heshima na koti na hata suruali ambayo haijakubana sana inafaa sana kwa ofisi.

Kama utapendelea kuvaa gauni basi angalia mkao wa hilo gauni ukoje maana mara nyingi gauni huwa halipendezi kuwa vazi la ofisini bali vazi la jioni.

Namna nzuri ya kuhudumia nywele zako za asili kirahisi

Kwa wale ambao tuna nywele asilia (natural hair), tayari tunafahamu changamoto kadhaa tunazokumbana nazo. Kwa wale mnaofikiria kuanza kuwa na nywele asilia, karibuni sana tuendelee kujuzana namna ya kutunza nywele zetu kama tulivyopewa na Mungu.

Katika mada ya leo, nitakwenda kuzungumzia vitu vya kuzingatia ili kuikuza nywele yako asilia kwa haraka zaidi. Je,unazifahamu nywele zako vizuri?Una nywele za aina gani? Zina tabia gani? Zinataka nini?

Zifuatazo ndizo njia ya kuzihudumia nywele zako;

1. Kuzikubali kama zilivyo na kuzipenda.

Utasikia ..hiki kipilipili changu ni steelwire ya kimataifa, ..hakitikisiki hata upepo wa dunia yote ungevumia pande hizi. Mwingine oh..nywele zangu kama miti ya mibuyu kichwani…hazishikiki.T atizo ni kwamba hamjafahamiana vizuri yani wewe na nywele zako. Hata mimi niligombana nazo sana huko nyuma kabla ya kuzielewa vizuri. Jenga mahusiano mazuri tu na nywele zako,zielewe,ukifikia hapo utaanza kuzipatia hata hazitakusumbua.

2. Usafi wa ngozi ya nywele na nywele zenyewe.

Nywele zenye afya huanzia kwenye ngozi safi ya nywele.Nafahamu unataka nywele zako zisidumae kwa hiyo zioshe vizuri.Wakati uliopita nilizungumzia kuziosha kwa product zilizo rafiki( ‘friendly’) .Ngozi safi ya nywele itasababisha nywele kupata njia ya kujitokeza nje kwa urahisi.Unapoziacha chafu,ule uchafu unaziba matundu ya nywele zako na kuzuia njia,kama ambavyo matundu ya uso yakiziba unapata machunusi maana uchafu unajaa basi kwa nywele hazitakua vizuri.

3. Linda unyevu wa nywele zako

Kila mtu akisikia kiu hunywa maji.Nywele zako zinahitaji kulindwa zisisikie kiu.Unapoziosha,yale mafuta asilia ya kuzilinda huondoka na uchafu.Nywele inabaki ikiwa na udhaifu fulani maana haiwezi hata kushikilia hayo maji yaliyopo vizuri,na zikikauka zinakua kavu sana.Ni vizuri kabla hazijakauka vizuri,ukazi-’condition’.Kwa nywele ambazo ni nyepesi na chache,pia kuna product za kuzisaidia ziweze kutunza vizuri unyevu na hivyo kuwa na afya nzuri.

4. Zifahamu nywele zako

Yani hapa ndo shule ilipolalia kabisaa maana ukizijua tu basi utazihudumia kwa usahihi. Unatakiwa kuangalia namna gani nywele zako zinanyonya unyevu .Unajuaje?

Chukua kikombe,kijaze maji safi.Ukipata glass itakuwa vizuri zaidi.

Chomoa unywele mmoja kichwani,hakikisha unatoka na kale kamzizi kake keupe keupe hivi.

Tumbukiza unywele wako kwenye glass yako ya maji hakikisha imeingia yote.Kama ikizama hapo hapo na hainyanyuki tena,basi nywele zako zinanyonya unyevu kwa haraka kabisa.Kama inachukua muda kuzama,au haizami kabisa,nywele zako zinanyonya unyevu taratibu au zinanyonya kwa shida.

(Wala usihofu,zipo namna ya kuzifanya zinyonye unyevu kwa haraka,tutajuzana.)Ni kwamba ‘cuticle’ zake zimefunga haswa,ndio maana unyevu au maji haviingii kwa haraka.

Kwa hiyo ukifanya ‘deep conditioner’ kwa kutumia joto kama la drier lakini uwe moto mdogo sana au ufanye ‘hot oil treatment’ itakusaidia ‘cuticle’kufunguka na unyevu kupita.

Mbadala,unaweza baada ya kuosha suuza na maji ya vuguvugu halafu weka mafuta ya kimiminika.Inasaidia sana.

Mimi nina aina gani?..Nina nywele zinazonyonya unyevu haraka.

5. Mafuta ya Kupaka kichwani.

Ni ya muhimu mnoo!.Nimefanya utafiti wa kina nimeona mafuta ya nazi yanaweka afya nzuri kwa nywele aina nyingi hivyo na mimi nikaanza kuyatumia. Kwangu mimi,mafuta ya nazi ya kutengeneza mwenyewe yamenikubali sana. Japo huwa nanunua pia mafuta kama ya olive(extra virgin) na ya tea tree.

6. Kuzichambua vizuri kabla ya kuchana.

Uwe mkarimu na mwenye subira kwa nywele zako. Mimi zikijifunga huwa nazichambua kwa mikono taratibu wakati mwingine nazilowesha na maji kwa mbali halafu nachana kwa chanuo lenye mapana sio ambalo reli zake zimebanana. sio kitana. Chanuo kubwa(wide toothed comb).

7. Usizisumbue mara kwa mara na usuke mitindo ya kuzitunza zikue.

Kama unataka zikue haraka, usizisumbue sana. Unaweza ukasuka mitindo mizuri tu ukakaa nazo wiki nzima au kadri zitakavyodumu. Au upunguze kuzichana mara kwa mara lakini utafute siku kama wikiendi ukae uzichambue taratibu na vidole kuondoa mafundo. Kuchana mara kwa mara zinapukutika,zinaanguka. Zitakua lakini sio kwa kasi ya kama ukizisuka ukaziacha kwa muda.

8. Punguza matumizi ya vitu vya moto kwenye nywele zako kama pasi ya nywele na vingine vya hivyo.

Mimi dryer la nywele situmii zaidi ya mara mbili kwa mwezi. Mara nyingi naziacha zikauke na hewa hata kama nimezifunga rollers natoa kesho baada ya masaa 24

Jinsi ya Kuondoa Makovu Mwilini

Makovu sio kidonda naomba hili uelewe, ila makovu ni alama ya majeraha ambayo yamebaki kwenye ngozi baada ya kupona majeraha.
Kuna baadhi ya watu husumbuliwa na shida ya kuwa na makovu sehemu mbalimbali ya mwili.
Hivyo kama wewe ni miongoni mwao maandishi haya yanakuhusu sana.

Zifuatazo ndizo mbinu za kuondoa makovu mwilini.

1. Tango

Unachotakiwa kufanya ni; Pondaponda tango na kisha kutumia mchanganyiko wake kwa kupaka juu ya kovu. Hii husaidia sana kulainisha makovu na ikiwa utatumia kwa muda mrefu huondoa makovu pia.

2. Aloe vera.

Unachotakiwa kufanya ni; kata majani hayo na utumie utomvu wake kupaka katika makovu kisha mara baada ya muda Fulani utaona mabadiliko na itapunguza na kuondoa makovu.

3. Asali

Unachotakiwa kufanya; Paka asali juu ya kovu na kuiacha usiku kucha. Rudia mara kwa mara kupaka asali hadi pale kovu litakapotoweka.

Faida za kuogea maji ya Moto

Watu wengi hupendelea kutumia maji ya moto kuoga pale hali ya hewa inapobadilika na kuwa ya baridi au wakati mwingine mtu anaumwa hivyo anatumia maji ya moto.
Sehemu kama Dar es Salaam ni mara cheche utakuta wakazi wake wanaogea maji ya moto kutokana na hali ya joto katika jiji hilo.

Lakini kwa ajili ya urembo na afya ya ngozi, maji ya moto yanatajwa kuwa ni kitu muhimu sana kama vilivyo vipodozi vingine vinavyoisaida ngozi yako kuwa nyororo.

Hizi hapa ni baadhi ya faida zitokanazo na matumizi ya maji ya moto angalau mara tatu kwa wiki

Kulainisha na kutunza ngozi

Maji ya moto husaidia kulainisha ngozi yako tofauti na ukitumia maji ya baridi. Maji ya moto hasa yaliyo katika jakuzi ambapo utatumia muda mrefu kidogo ngozi yako ikiwa kwenye maji, husaidia kuilainisha ngozi yako na kuiweka katika hali nzuri.

Usingizi

Kama huwa unapata matatizo kupata usingizi usiku, amka oga kwa kutumia maji ya moto kwani husaidia kulainisha misuli ya mwili wako na itakaa sawa na utaweza kupata usinngizi.

Kukuweka katika hali nzuri

Kuna wakati mwingine mtu hujisikia uchovu wa mwili na kutotaka kufanya chochote (Off mood). Ukioga kwa maji ya moto yatakusaida kukuondolea uchovu na utajisikia mwenye nguvu na upo tayari kukabiliana na changamoto za siku.

Kuchangamsha ubongo

Unapooga kwa kutumia maji ya moto husaidia kuchangamsha ubongo na kuufanya uweze kufanyakazi kwa ufanisi na kwa haraka zaidi.

Kushusha shinikizo la damu

Ukiachanna na masuala ya urembo, kuoga maji ya moto kunatajwa kuwa ni njia ya haraka ya kusaidia kushusha shinikizo la damu. Tafiti zinaonyesha kuwa mtu mwenye shinikizo la damu la kupanda, akioga kwa maji ya moto husaidia kushusha.

Kusaidia mzunguko wa damu

Ukioga kwa kutumia maji ya moto husaidia kusisimu na kuitanua mishipa ya damu hivyo kuwezesha damu kuwa na mzunguko mzuri mwilini.

Licha ya kuwa maji ya moto ni mazuri kiafya, unashauriwa kuto oga kwa maji ya moto sana kwani huathiri ngozi.

Jinsi ya kuondoa weusi kwenye magoti na viwiko vya mikono

Ngozi nyeusi katika magoti na nyuma ya mikono hutokana na mkusanyiko wa cells zilizokufa, na hata unavyoweka pressure kwenye magoti na vipepsi vya mikono yako. Kama ukiwa unaweka mikono kwenye meza ukiwa kazini, ule msuguano unafanya ngozi iwe nyeusi.

Kama una magoti myeusi na nyuma ya mikono pia ni peiusi, tumia hizi njia asili kuweza kuondoa weusi huo:

Tumia Aloe Vera Juice.

Juice ya Aloe Vera inasaidia kuondoa weusi, all you have to do ni kupaka juice hiyo kwenye sehemu yenye weusi na uache kwa nusu saa kisha nawa na upake moisturizer. Rudia kufanya hivi mara mbili kila siku.

Tumia Binzari Manjano, Asali na Maziwa.

Changanya vyote hivi utapata mchanganiko mzito, paka kwenye magoti na kwenye mikono yako palipo na weusi. Kaa nayo kwa dakika 30, nawa na paka moisturizer. Rudia hii kila siku kwa wiki 3-4, utapata matokeo mazuri.

Tumia Ndimu.

Chukua pamba na uitumie kupaka juice ya ndimu katika sehemu zenye weusi. Au unaweza kuikata tu ndimu na kuipaka directly kwenye sehemu zenye weusi. Kaa nayo kwa lisaa 1 kisha nawa. Rudia hivi kila siku hadi weusi utakapopotea.

Tumia Olive Oil na Sukari.

Changanya vizuri, hii itakuwa kama exfoliation/scrub kwa ajili ya magoti na mikono. Paka katika hizo sehemu zenye weusi kisha kuwa kama una-massage polepole. nawa kwa maji ya uvuguvugu kisha paka moisturizer.

Faida na namna ya kutumia mafuta ya Zaituni Olive Oil kwenye nywele

Faida ya Mafuta Ya Zaituni Olive Oil kwenye nywele.

1. Yanasaidia kufanya mzunguko wa damu kufanya kazi vizuri kwenye ngozi ya kichwa na kupenyeza hadi kwenye shina ya nywele kisha kuifanya nywele inayoota kuwa imara

2. Yanasaidia kupambana na mba kwenye ngozi ya kichwa

3. Yanasaidia uzalishwaji wa mzizi au shina ya nywele

4. Yanasaidia uzalishwaji wa melanin ambayo inafanya kazi ya kutoa rangi ya nywele inayotakiwa.

5. Yanasaidia kuifanya nywele isiwe kavu sana.

NAMNA YA KUZIHUDUMIA NYWELE:

Unaweza kuchanganya na Mdalasini pamoja na Asali.

1. Olive oil vijiko 2 vya chakula

2. Asali kijiko 1 cha chakula

3. Mdalasini kijiko 1 cha chai

Pasha moto olive oil kisha changanya vyote kwa pamoja pakaa kwenye nywele acha kwa muda wa dakika 20 kisha osha nywele zako na upakae mafuta zikishakauka.

Ninashauri utumie mafuta haya kwenye nywele na ngozi ni mazuri sana. Ukiwa na mba pakaa kwenye ngozi mba itaisha na muwasho utaondoka.

Madhara ya Kuvaa/ Kuweka Kope Za Bandia

Mapokeo ya urembo wa kisasa katika nchi zinazoendelea ni sehemu ya mchango wa urembo na mvuto tunaouona kwa baadhi ya wasichana na wanawake ambao kwa hakika unaleta hamasa ya kuangalia.
Hata hivyo, urembo huu huja na hatari zake ambazo wengi wanaweza kuzichukulia poa kwa kuwa hazitokei kwa haraka ama katika muda unaoweza kutolewa ushahidi kwa sasa.

Moja kati ya urembo unaofanywa na wanawake wengi wa kisasa ni kuweka kope za bandia juu ya kope halisi, kweli wengi wanakuwa na mvuto wa aina yake wakikuangalia hasa mtoto wa kiume. Lakini hatari inayotokana na urembo huo ni kubwa zaidi ya matokeo ya muda mfupi.

Wataalam wanaeleza kuwa kope za bandia ambazo hugundishwa kwa kutumia gundi ya nywele inayotumika kugundisha nywele bandia kwa wenye vipara inaweza kuwa chanzo cha upofu wa mtumiaji.

Gundi hiyo hupukutika taratibu sana kiasi cha kutoshtukiwa na kuelekea kwenye mboni ya jicho ambayo ndio moyo wa ‘kuona’. Endapo mtumiaji ataendelea kwa muda mrefu kutumia kope hizi bandia anaweza kujikuta anakuwa na tatizo la kuona ama hata upofu wa haraka katika maisha yake ya baadae.

Hata hivyo, hatari kubwa imeelekezwa kwa maduka ama vibanda vinatumia vifaa vya bei nafuu ikiwemo gundi inayotumika. Ukwepaji wa gharama ama kutokuwa na uwezo wa kutumia gharama kubwa kunamuingiza mrembo kwenye hatari zaidi.

Kuwa mwangalifu, urembo usiwe chanzo cha kuhatarisha afya yako. Kumbuka Afya ni uhai wa mwili wako.

Madhara ya kuvaa miwani ya Urembo maarufu kama miwani ya Jua

Miwani za urembo maarufu kama miwani za jua zimetajwa kuwa na madhara kwa watumiaji wake kutokana na watu kutofahamu saizi za namba ambazo wanapaswa kuzivaa kabla ya kununua.

Akifafanua kwenye kipindi cha Supamix kinachorushwa East Africa Redio, Daktari Ningwa wa Upasuaji wa macho kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dk.Neema Daniel Kanyaro amesema watu wengi amekuwa wakivaa miwani pasipokjua kwamba zinaweza kuwasababishia matatizo ya kuona.

Dk. Kanyaro amesema kwamba watu wamekuwa wakivaa miwani za jua kama urembo pasipo kwenda kupima kujua ni aina gani ya miwani wanazotakiwa kuzitumia lakini pia bila kujua kama miwani hizo zina namba ambazo kila mtu ana namba kutokana na uono wake.

“Miwani ni dawa lakini usivae bila kupima kwani inaweza kukusababishia matatizo ikiwemo uoni hafifu. Unaweza kukuta unavaa miweani nyeusi lakini kumbe siyo namba yako. Kama hujijui unaweza kuta ukitazama unaona giza kumbe umeshaua macho kwa urembo” amesema.

Akizungumzia kuhsu presha ya macho Dk. Kanyaro amesema kwamba ugonjwa huo hauna dalili za moja kwa moja bali ni lazima kupima na huathiri watu wa rika zote.

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About