Mungu anajibu sala kutokana na nia
Mungu anamjibu mtu sala zake kutokana na anachonuia.
Mungu anamjibu mtu sala zake kutokana na anachonuia.
Ukitaka kupata amani, tumaini katika Ahadi za Mungu. Ahadi ya Mungu ni hii “Hatoacha kutusaidia wala kututupa”.
Usifadhaike moyoni pale unapokuwa katika matatizo au unapopitia changamoto katika maisha. Kumbuka kuwa Mungu yupo, anayaona hayo na anataka kukusaidia, ni wewe tuu kumpa nafasi ya kukusaidia. Hatumpi Mungu nafasi pale tunapozani tunaweza wenyewe.
Upendo wa Mungu hauna kikomo. Mama anaweza kumchoka na kumtelekeza mwanae lakini Mungu kamwe hamchoki mtu.
Kufanya Mambo mema ndipo kunaleta furaha ya kweli kwa Binadamu yeyote yule. Hakuna Binadamu anayefurahia kufanya maovu. Mema hayaambatani na majuto lakini uovu wowote unamajuto. Hata waovu wanafanyiana mema ili wapate furaha.
Kukosa hata mara moja inahesabika ni kukosea mbele ya Mungu. Kwa kuwa kwa Mungu hakuna kusema, ‘Kukosea mara moja sio kosa bali kurudia kosa ndio kosa’. Mbele ya Mungu kila kosa lina uzito wake haijalishi ni kosa la mara ya kwanza.
Sala yoyote ili iwe SALA lazima itolewe kwa Imani, Upendo, Unyenyekevu na kwa Matumaini. Sala kama hii ndiyo ipendezayo mbele ya Mungu.
Mungu anaporuhusu ukaingia katika majaribu na mateso hana nia ya kukutesa bali anataka kukuimarisha. Mungu ni mwema kila wakati.
Hakuna kitu cha Muhimu zaidi Duniani kama kumjua Mungu na kumuishi Mungu. Kila binadamu ameumbwa kwa ajili hii. Na Mungu anachotaka ndicho hichi, kumjua na kumuishi. Mengine yote ni maziada. Ukimuishi Mungu atakufanikisha katika yote.
Sala ni kama chakula cha Roho, Bila sala roho inakufa. Tusali daima ili roho zetu ziwe hai siku zote.
Usiogope wala usisite kutubu na kuomba msamaha kwa Mungu. Uwe na Amani na Matumaini katika Huruma ya Mungu itokayo katika Upendo wake wa Mfano wa baba awapendavyo wanawe. Mungu anasubiri kukupokea kwenye mikono yake Ili akutunze kama mtoto wake kama utatubu na kumrudia yeye. Amua kumwendea leo! Anakungoja ni wewe tuu…
Basi, nasema hivi: Mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Maana tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya Roho; na matakwa ya Roho hupingana na Tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamuwezi kufanya yale mnayotaka nyinyi wenyewe.
(Wagalatia 5:16-22)
Basi, nasema hivi: Mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Maana tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya Roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamuwezi kufanya yale mnayotaka nyinyi wenyewe.
“Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtatimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa maana mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.” (Wagalatia 5:16-17)
Kuongozwa na Roho Mtakatifu maana yake ni kuacha maisha yetu yaongozwe na maadili na kanuni za kiroho zinazotoka kwa Mungu. Roho Mtakatifu hutupa nguvu, hekima, na mwongozo wa kila siku katika safari yetu ya kiroho. Tunapoongozwa na Roho, tunakuwa na uwezo wa kupambana na tamaa za kidunia ambazo zinatufanya tuwe mbali na Mungu.
“Lakini Roho wa kweli atakapokuja, atawaongoza awatie kwenye kweli yote. Kwa maana hatasema kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayasema, naye atawapasha habari za mambo yajayo.” (Yohana 16:13)
“Basi, kama mlivyopokea Kristo Yesu Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye mizizi na kujengwa ndani yake, na kuthibitishwa katika imani, kama mlivyofundishwa, mkizidi kutoa shukrani.” (Wakolosai 2:6-7)
“Basi, enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli.” (Waefeso 5:8-9)
Tamaa za kidunia ni yale mambo yanayotupotosha na kutufanya tuishi kinyume na mapenzi ya Mungu. Ni lazima tujifunze kuzishinda kwa kuimarisha uhusiano wetu na Mungu kupitia maombi, kusoma Neno la Mungu, na kushirikiana na wengine waaminio. Roho Mtakatifu hutusaidia kuona na kutambua uovu na udanganyifu wa tamaa za kidunia na kutupa nguvu ya kuzishinda.
“Basi, ndugu zangu, sisi tuna deni, si kwa mwili, kufuatana na mwili; kwa maana kama mkiishi kufuatana na mwili, mnakufa; bali kama mkiyaangamiza matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.” (Warumi 8:12-13)
“Wala msiifanye miili yenu kuwa silaha za dhambi kwa kutenda uovu, bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama watu waliotolewa katika wafu na kupewa uhai, na miili yenu iwe silaha za haki kwa Mungu.” (Warumi 6:13)
“Kwa maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome; tukibomoa mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinue juu ya elimu ya Mungu; tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo.” (2 Wakorintho 10:4-5)
Kutembea katika nuru ya Roho Mtakatifu ni kuishi maisha yaliyojaa matunda ya Roho, kama vile upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole, na kiasi. Tunapojitahidi kuishi kwa njia hii, tunakuwa mashahidi wa kweli wa Kristo na tunavutia wengine kwake. Ni muhimu kufahamu kwamba hatuwezi kutembea katika nuru ya Roho kwa nguvu zetu wenyewe, bali kwa neema na uwezo wa Roho Mtakatifu ndani yetu.
“Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.” (Wagalatia 5:22-23)
“Nanyi mkivumiliana na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo nanyi. (Wakolosai 3:13)
“Tazama ni jinsi gani upendo wa Baba alivyotupa, kwamba tuitwe watoto wa Mungu; na ndivyo tulivyo.” (1 Yohana 3:1)
Kuongozwa na Roho Mtakatifu ni wito wa kila Mkristo. Ni mwaliko wa kuacha maisha yetu yaongozwe na Mungu, na kuishi kulingana na mapenzi yake. Tamaa za kidunia ni kikwazo kikubwa kwa uhusiano wetu na Mungu, lakini kwa nguvu na mwongozo wa Roho Mtakatifu, tunaweza kuzishinda na kuishi maisha yaliyojaa matunda ya Roho. Tuishi maisha ya kuongozwa na Roho, tukijua kwamba Mungu yupo nasi na anatupatia nguvu ya kushinda kila jaribu na changamoto.
Hakuna Maisha ya Kikristo bila Kusali. Kama kuna Mkristo anaishi bila kusali huyo siyo Mkristo bali Mkristo mfu. Sala ndiyo uhai wa Mkristo. Hakuna Njia nyingine yoyote ya kumfikia Mungu isipokua sala.
Wakati wazazi waliweza kuaamua kuzaa mtoto tuu, Mungu yeye alikuchagua wewe utungwe mimba na kukulinda ungali tumboni mwa mama yako….Wakati wazazi wanasubiri kwa shauku kuona muonekano wako wewe, Mungu anawaweka wajukuu wa wazazi wako/ watoto wako ndani mwako…. Wakati wazazi wakitafuta chakula kwa ajili yako, Mungu yeye aliwawezesha kukipata…. Wakati wazazi wakingoja kuona unavyoendelea kukua huku wakiwaza hatima ya maisha yako Mungu anakuendeleza na alishapanga maisha yako tangu alipokuchagua uwe mtu ukiwa tumboni mwa mama yako…. Wazazi wanaweza kukuombea kwa Mungu lakini Mungu ndiye anayeamua akufanyie nini maana Wewe ni wa kwake….Wewe na wazazi wako ni watoto wa Baba mmoja ambaye ndiye Mungu.
Fikiria umenunua zawadi nzuri ya gharama sana na unataka kumpa mtu umpendaye sana. Akipokea zawadi yako unafurahi sana, akikataa kuipokea zawadi inaumiza sana, lakini inaumiza zaidi akiipokea kisha akaitupa mbele yako na kuona haina maana. Hiki ndicho kinachotokea kwa Yesu. Yesu yupo kwa ajili ya kutupa zawadi ya Wokovu alyogharamia kwa uhai wake. Tunapoipokea tunamfurahisha sana, tukiikataa tunamhuzunisha na tunapoipokea na kuiacha baadae tunamhuzunisha kwelikweli.
Mungu ni mwema sana tunapokua wadhambi anapotuadhibu haimaanishi kuwa anatuchukia. Inamaanisha kuwa anatuonya na hapendi turudie makosa.
Kwa njia ya sala Binadamu anampa Mungu Utukufu, Mungu anampa Binadamu Wokovu na Neema.
Kubarikiwa ni Kutokutindikiwa na kuwa na matumaini ya siku zijazo. Kubarikiwa ni kuwa na amani, furaha, na matumaini katika maisha ya sasa na yajayo. Kubarikiwa sio kuwa na mali nyingi. Yesu hajawahi kumwambia mtu kuwa utakua tajiri sana kwa kuwa umebarikiwa wala hajawahi kumuahidi kumpa mtu utajiri. Unaweza ukawa na mali nyingi lakini zikakufanya ukakosa Amani, furaha na matumaini ya siku zijazo. Ndiyo maana Mungu anatupa kulingana na vile tunavyohitaji ili visiwe mtego kwetu.
Jifunze na jijengea tabia ya kumsikiliza Mungu rohoni mwako unaposali. Sala ni mazungumzo ya Mungu na mwanadamu. Mazungumzo yanahusisha kuongea na kusikiliza.
Mungu haangalii matemdo ya mtu ya nje tuu, bali anaangalia ndani kabisa mawazo ya mtu na nia yake. Nia ya mtu ndiyo inayoonyesha mtu alivyo.
Recent Comments