Nukuu za Dini

Mungu ni zaidi ya Mzazi na upendo wake ni zaidi ya wa Wazazi

Wakati wazazi waliweza kuaamua kuzaa mtoto tuu, Mungu yeye alikuchagua wewe utungwe mimba na kukulinda ungali tumboni mwa mama yako….Wakati wazazi wanasubiri kwa shauku kuona muonekano wako wewe, Mungu anawaweka wajukuu wa wazazi wako/ watoto wako ndani mwako…. Wakati wazazi wakitafuta chakula kwa ajili yako, Mungu yeye aliwawezesha kukipata…. Wakati wazazi wakingoja kuona unavyoendelea kukua huku wakiwaza hatima ya maisha yako Mungu anakuendeleza na alishapanga maisha yako tangu alipokuchagua uwe mtu ukiwa tumboni mwa mama yako…. Wazazi wanaweza kukuombea kwa Mungu lakini Mungu ndiye anayeamua akufanyie nini maana Wewe ni wa kwake….Wewe na wazazi wako ni watoto wa Baba mmoja ambaye ndiye Mungu.

Mungu ni Mwaminifu

Mungu ni Mwaminifu Sana na mwenye mipango na subira katika kila kitu hasa Sala na maombi yetu kwake. Tunaposali leo Mungu anatusikia na kujibu leo, kesho au hata miaka kumi ijayo. Inawezekana hata baraka zako za leo ni majibu ya Sala zako miaka kumi iliyopita. Sali bila kuchoka kwani hujui Sala zako zitakusaidia lini. Usitegemee majibu ya Sala zako wakati huo huo, amini katika uaminifu wa Mungu kwani anajua lini ni siku sahii ya kukujibu.

Maana ya kubarikiwa

Kubarikiwa ni Kutokutindikiwa na kuwa na matumaini ya siku zijazo. Kubarikiwa ni kuwa na amani, furaha, na matumaini katika maisha ya sasa na yajayo. Kubarikiwa sio kuwa na mali nyingi. Yesu hajawahi kumwambia mtu kuwa utakua tajiri sana kwa kuwa umebarikiwa wala hajawahi kumuahidi kumpa mtu utajiri. Unaweza ukawa na mali nyingi lakini zikakufanya ukakosa Amani, furaha na matumaini ya siku zijazo. Ndiyo maana Mungu anatupa kulingana na vile tunavyohitaji ili visiwe mtego kwetu.

Mnyororo wa Baraka za Mungu

Usiache kusali na kutenda mema kwa kuwa huwezi jua ni watu wangapi wanategemea sala na matendo yako mema. Kumbuka Mungu alimwambia Abraham kama akikuta Wacha Mungu wengi hataiharibu Sodoma na Gomora. Vivyo hivyo Inawezekana wapo watu wengi wanaonufaika na Sala na matendo yako, hasa watu wako wa karibu uwapendao. Unapokuwa mtu wa Sala na mcha Mungu unabarikiwa wewe na wale wa karibu yako. KAMWE USIACHE KUMCHA MUNGU NA KUSALI. Ukiwa mregevu ni sawa na unakata Mnyororo wa Baraka za Mungu kwako na wenzako.

Toba, msamaha na Baraka

Inashangaza kwa sasa watu wengi hawapendi kuambiwa kuhusu kutubu dhambi zao bali wanataka waambiwe watabarikiwa. Kama vile wewe huwezi kumvika mwanao nguo nzuri kabla ya kumuogesha vivyo hivyo na Mungu hawezi kukubariki kabla ya kukutakasa. Unapotubu unasamehewa na kutakaswa dhambi zako kisha unakua umefungua milango ya baraka. Huwezi kubarikiwa bila kutubu kweli.

Mawazo ya Mungu tunapokua na shida na mateso

Mawazo ya Mungu ni makuu. Mungu anatuwazia mema daima. Hata unapopitia shida na matatizo katika maisha nia ya Mungu inabaki kuwa njema ya Kukuonyesha ukuu wake na kukuwezesha kumjua yeye. Pengine usingejua matendo ya Mungu bila kupitia shida na changamoto katika maisha. Mungu hapendi upate shida bali anaruhusu hayo ili upate faida ya kumjua na kujua uwezo wake. Hata Yesu ilibidi apitie mateso na kifo ili uwezo wa Mungu udhihirike baada ya kufufuliwa. Amini kuwa kuna mema mbele yako baada ya mateso haya ya sasa.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About