Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Pilau Ya Sosi Ya Soya Na Mboga

Viambaupishi

Kuku (mkate mkate vipande) 1

Mchele wa Basmati (rowanisha) 3 magi

Mdalasini 1 mchi mmoja

Vitunguu maji (vilivyokatwa vyembamba) 6

Mchanganyiko wa mboga za barafu 1 magi

(karoti, mahindi, njegere)

Kabichi (iliyokatwa katwa nyembamba) 1 magi

Pilipili mbichi (iliyosagwa) 3

Pilipili boga iliyokatwa vipande vidogo vidogo 1

Pilipili manga 1 kijiko cha chakula

Chumvi 1 kijiko cha chakula

Sosi ya soya (soy sauce) 5 vijiko vya chakula

Kotmiri iliyokatwa katwa 1 magi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa 2 vijiko vya chakula

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Tia mafuta ndani ya karai. Yakipata moto kiasi, mimina vitunguu maji na mdalasini 1 mzima kaanga. Itachukua muda kidogo. Kaanga mpaka viwe rangi ya hudhurungi (brown). Viepue na uweke kando.

2. Ndani ya sufuria kubwa, mimina kuku, chumvi, thomu na tangawizi, sosi ya soya, pilipili manga, pilipili mbichi, chemsha mpaka kuku awive na maji yakauke.

3. Changanya vitunguu ulivyokaanga, kabichi, pilipili, mboga, kotmiri, mchanganyiko wa mboga za barafu na weka kwa muda wa dakika tano au kumi. Tia na mafuta kidogo uliyokaangia vitunguu .

4. Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja. Ukishauchuja umwagie katika masala ya kuku.

5. Nyunyizia mafuta kidogo uliokaangia vitunguu.

6. Weka moto mdogo mpaka wali ukishawiva. Uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa.

KIDOKEZO:

Unaweza kuupika wali huo ndani ya jiko, yaani badala ya kutia masala kwenye sufuria ukayatia katika bakuli au treya ya jiko (oven), kisha ukamwagia wali uliouchuja humo na kuupika kaitka moto wa 400-450 Deg kwa muda wa dakika 15-20.

Jinsi ya kuandaa biskuti za Siagi Na Jam

MAHITAJI

Unga – 2 Vikombe
Sukari ya icing – 1 Kikombe
Siagi – 250 gm
Yai – 1
Vanilla – 2 Vijiko vya chai
Baking powder -1 Kijiko cha chai
Jam – ΒΌ kikombe
Lozi – ΒΌ kikombe

JINSI YA KUPIKA

Koroga siagi na sukari katika mashine ya keki (cake mixer) mpaka iwe laini (creamy).
Tia yai na vanilla koroga mpaka mchanganyiko uwe laini kama sufi.
Tia unga na baking powder changanya na mwiko.
Chota mchanganyiko kwa mkono (kiasi cha kijiko kimoja cha supufanya duara kisha weka kwenye treya ya kupikia.
Bonyeza kila kiduara katikati kwa kidole, kisha weka jam na tupia lozi zilizomenywa na kukatwa katwa.
Pika (bake) katika oven moto wa 375Β° F kama muda wa dakika 15 hivi huku unazitazama tazama

Mapishi ya Mihogo ya nazi na kuku

Mahitaji

Mihogo kilo 1
Kidali cha kuku 1 kikubwa
Nyanya 1 kubwa
Kitunguu maji 1 cha wastani
Swaum/tangawizi i kijiko cha chai
Nazi kopo 1
curry powder 1 kijiko cha chai
Binzari manjano 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/2
Pilipili 1
Chumvi kiasi

Matayarisho

Saga pamoja nyanya, kitunguu na swaum/ginger pamoja na vimaji kidogo. Kisha vitie kwenye sufuria isiyoshika chini na uvishemshe mpaka maji yote yakauke kisha tia mafuta na upike ktk moto mdogo mpaka viive.Baada ya hapo tia spice na uzipike kidogo kisha tia mihogo na kuku (kuku na mihogo vikatwe vipande vya wastani) vichanganye vizuri kisha tia nazi na vimaji kiasi,limao chumvi na pilipili na ufunike kisha punguza moto. Pika mpaka mihogo na kuku viive na ibaki rojo kidogo kisha ipua na mihogo yako itakuwa tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Kabichi

Mahitaji

Kabichi 1/2 kilo
Nyanya ya kopo 1/2
Kitunguu 1
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Kwanza kabisa bandua magada ya juu ya kabichi, kisha ioshe na uikaushe maji baaba ya hapo katakata kabichi (inapendeza zaidi kama ikikatwa nyembamba) kisha saga pamoja nyanya na kitunguu. Baada yahapo tia katika sufuria ya kupikia, ipike mpaka maji yote yatakapokauka kisha tia chumvi, curry powder na mafuta pika kwa muda kiasi kisha tia kabichi na upunguze moto. Pika mpaka kabishi itakapoiva kisha ipua na itakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuila kwa wali au ugali.

Mapishi ya Ugali Mchuzi Wa Samaki Nguru Wa Nazi Na Bamia Za Kukaanga

Vipimo Vya Ugali:

Unga wa mahindi/sembe – 4

Maji – 6 takriban

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chota unga kidogo katika kibakuli uchanganye na maji kidogo .
Weka maji mengineyo katika sufuria kwenye moto.
Changanya na mchanganyiko mdogo ufanya kama uji.
Kisha kidogo kidogo unaongeza sembe huku unakoroga na kuusonga ugali hadi uive.

Vipimo Vya Mchuzi Wa Samaki Wa Nazi

Samaki nguru – 5 vipande

Pilipili mbichi ilosagwa

Kitunguu maji kilosagwa – 1 kimoja

Nyanya ilosagwa – 2

Haldi/tumeric/bizari ya manjano – ΒΌ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 kamua

Tui la nazi zito – 2 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Baada ya kumuosha samaki, weka katika sufuria.
Tia chumvi, ndimu, pilipili mbichi ilosagwa.
Tia vitunguu na nyanya zilosagwa
Mkaushe kwa hivyo viungo, akianza kukauka tia tui la nazi.
Acha kidogo tu katika moto tui liwive mchuzi ukiwa tayari.

Vipimo Vya Bamia

Bamia – Β½ kilo takriban

Nyanya kopo – 1 kijiko cha chai

Methi/uwatu/fenugreek seeds ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Dania/corriander ilosagwa – Β½ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta – 1 kikombe cha kahawa

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata bamia kwa urefu.
Weka mafuta katika karai, kisha tia bizari zote na nyanya kopo, kaanga kidogo.
Tia bamia endelea kukaanga, kisha acha katika moto mdogomdogo ufunike.
Kila baada ya muda funua karai ukaange bamia hadi ziwive zikiwa tayari.

Jinsi ya kupika Biskuti Ya Keki Kavu kwa kizungu Shortcake

Viamba upishi

Unga 2 Magi (vikombe vya chai)

Sukari iliyosagwa 2/3 Magi (kikombe cha chai)

Siagi β€… 220Β g

Unga wa mchele Β½ Magi

Yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya vitu vyote hivyo kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.

2. Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30Β cm au (8 in kwa 12 in)

3. Choma kwenye moto 325˚C kwa muda wa saa nzima au mpaka ibadilike kuwa rangi ya dhahabu.

4. Epua acha ipoe kisha kata vipande kama mstatili, weak kwenye sahani tayari kunywewa na chai.

Mapishi ya wali wa hoho nyekundu

Mahitaji

Pilipili hoho (Red pepper 3)
Cougette 1
Kitunguu (onion 1)
Uyoga (mashroom 1 kikombe cha chai)
Carrot 1
Nyanya (fresh tomato 1)
Nyanya ya kopo iliyosagwa (tomato paste 3 vijiko vya chai)
Giligilani (fresh coriander)
Binzari manjano (Turmaric 1/2 ya kijiko cha chai)
Curry powder 1/2 ya kijiko cha chai
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Kata hoho kati na utoe moyo wake kisha ziweke pembeni, Kisha katakata cougette, kitunguu, uyoga, carrot, nyanya katika vipande vidogo vidogo, Weka sufuria jikoni na uanze kupika uyoga kwa muda wa dakika 5, kisha weka curry powder, turmaric na chumvi na kaanga kidogo kisha weka vegetable zilizobakia pamoja na nyanya ya kusaga pamoja na giligilani. Zikaange kwa muda wa dakika 5 kisha zitie kwenye hoho na kisha uzibake kwa muda wa dakika 20 na hapo zitakuwa tayari kuseviwa na wali.
Wali: angalia katika recipe zilizopita

Jinsi ya kupika Mseto Kwa Mchuzi Wa Samaki Wa Nazi

Vipimo vya mseto

Tanbihi: Kiasi ya vipimo inategemea wingi wa watu, unaweza kupunguza au kuongeza. Hiki ni kiasi cha watu 6 takriban.

Chooko – 3 Vikombe

Mchele – 2 Vikombe

Samli – 2 vijiko Vya supu

Chumvi – kiasi

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Safisha na kosha chooko utoe taka taka zote.
Osha mchele kisha roweka pamoja na chooko kwa muda wa saa au zaidi.
Pika chooko na mchele ukiongeza maji inapohitajika, tia chumvi, funika pika moto mdogo mdogo huku unakoroga kwa mwiko kila baada ya muda huku unaponda ponda.
Karibu na kuwiva na kupondeka tia samli endelea kupika hadi karibu na kukauka. Epua.

Samaki

Vipande vya samaki (nguru) – 6 – 7 (4LB)

Kitunguu saumu na tangawizi iliyosagwa – 2 vijiko vya supu

Pilipili ya unga nyekundu – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa ukipenda – 1 kijiko cha chai

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Ndimu – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutaysha Na Kupika

Changanya thomu/tangawizi, pilipili, bizari, chumvi pamoja na ndimu iwe masala nzito.
Paka vipande vya nguru kwa masala hayo weka akolee dakika kumi hivi.
Kaanga vipande vya nguru katika mafuta madogo kwenye kikaango (fyring pan) uweke upande.

Mchuzi Wa Nazi

Vitunguu maji – katakata vidogodogo – 4

Nyanya zilizosagwa (crushed) – 3- 4

Nyanya kopo – 1 kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Bizari ya mchuzi – 1 kijiko cha chai

Bamia zilizokatwa ndogo ndogo – 2 vikombe

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 vijiko vya supu

Tui la nazi – 3 Vikombe au 800 ml

Namna Ya Kupika

Katika karai au sufuria, tia mafuta ukaange vitunguu hadi vianze kugeuka rangi.
Tia nyanya zilizosagwa, nyanya kopo, uendelee kukaanga, kisha tia bizari, chumvi.
Tia nazi na mwisho tia bamia uache ziwive kidogo tu.
Tia vipande vya samaki vilivyokwisha kaangwa.
Tayari kuliwa na mseto upendavyo.

Vidokezo:

Bizari nzuri kutumia ni ya ‘Simba Mbili’ inaleta ladha nzuri katika mchuzi.
Ni bora kupika mchuzi kwanza kabla ya mseto kwani mseto ukikaa kwa muda unazidi kukauka.

Mapishi ya Tende Ya Kusonga Ya Lozi Na Cornflakes

VIAMBAUPISHI

Tende zilizotolewa kokwa – 1 Kilo

Cornflakes – 1 Β½ kikombe

Lozi Zilokatwa katwa – 1 kikombe

Siagi – ΒΌ kilo

MANDALIZI

Mimina tende na siagi kwenye sufuria bandika motoni moto mdogo mdogo mpaka zilainike. Kwa muda wa dakika 10.
Isonge kidogo kwa mwiko au kuikoroga ichanganyike vizuri.
Changanya Cornflakes na lozi kwenye tende mpaka zichanganyika vizuri.
Pakaza treya au sinia mafuta au siagi kidogo.
Mimina mchanganyiko wa tende, zitandaze vizuri na ukate vipande saizi unayopenda. Zikiwa tayari kuliwa kwa kahawa.

Mambo ya msingi kufahamu kuhusu Lishe

Nini maana ya lishe?

β€’ Lishe yahusu mafunzo ya chakula na jinsi miili yetu inavyotumia chakula kamakichocheo cha ukuaji, kuzaana na utunzaji wa afya.
β€’ Lishe inajumuisha mchakato wa utoaji virutubishi vinavyohitajika kwa afya, ukuaji, kuendelea na kuishi.

Umuhimu wa lishe bora

Lishe bora ni muhimu katika mambo yafuatayo

β€’ Utoaji nishati ili kuishi, uwepo wa mwendo, utendaji kazi, na joto.
β€’ Ukuaji, uendeleaji, ujengaji mwli, urejeshaji na utengenezaji wa seli na mikusanyika ya seli hizo (tishu)
β€’ Ufanyaji michakato ya kikemia kama vile uyeyushaji chakula, umetaboli na utunzaji mwili.
β€’ Kinga dhidi ya magonjwa, upigaji vita maambukizi na uponaji magonjwa.
β€’ Ili afya njema iweze kudumishwa, mlo wa kila siku lazima ukamilishe shughuli nne zilizotajwa hapo awali. Vyakula vinavyokamilisha moja au zaidi ya shughuli tatu huitwa virutubishi.

Virutubishi

Aina za irutubishi vikuu tunavyohitaji kwa wingi. Hivi ni:

β€’ kabohaidreti (vyakula vya wanga, sukari na vyakula vya ufumwele):
β€’ mafuta yatokanayo na wanyama – haya yapo ya aina kadhaa
β€’ Protini- kuna mamia ya aina mbalimbali za protini.
β€’ Maji.

Virutubishi vidogovidogo tunavyohitaji kwa kiwango kidogo. Kuna aina nyingi ya hivi bali vile vinavyoelekea kukosekana kwenye mlo ni:

β€’ madini – madini ya chuma (angalia Kisanduku cha 6, ukurasa 16), madini ya joto na zinki.
β€’ vitamnini – vitamini A, vitamini za kundi B (ikiwemo folate) na vitamini C. Kama chakula chaweza kuwa chanzo bora cha kirutubishi au la hutegemea:
β€’ Kiwango cha kirutubishi katika chakula. Vyakula vyenye viwango vingi vya virutubishi vidogovidogo kulinganisha na viwango vyake vya nguvu huitwa vyakula β€˜vilivyosheheni virutubishi’ (nutrient-rich) au wakati mwingine huitwa vyakula vyenye β€˜ujanzo mwingi’ wa virutubishi (nutrient dense). Vyakula hivi hupendwa kwa kuwa hutoa virutubishi vyote vinavyohitajika. Kiambatisho hiki kinaorodhesha vyakula vinavyotoa viwango muhimu vya virutubishi mbalimbali.
β€’ Kiwango cha chakula kinachotumika mara kwa mara.

Jinsi ya kutengeneza Nangatai

MAHITAJI

Unga wa ngano – 2 – 2 ΒΌ Vikombe

Siagi – 1 Β½ Kikombe

Sukari – 1 Kikombe

Yai – 1

Vanilla -Tone moja

Baking Powder -kijiko 1 cha chai

Chumvi – Kiasi kidogo (pinch)

Unga wa Kastadi – 2 Vijiko vya supu

MATAYARISHO

Changanya vitu vyote isipokuwa unga.
Tia unga kidogo kidogo mpaka mchanganyiko uwe sawa.
Kisha fanya duara ndogo ndogo uzipange kwenye treya na utie rangi katikati.
Halafu zichome katika moto wa 300Β°F kwa muda wa dakika 20 – 25 na zisiwe browni .
Kisha panga kwenye sahani tayari kuliwa na chai.

Mapishi mazuri ya Chapati za maji

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour) ( 1/4 kilo)
Yai (egg 1)
Sukari (sugar 1/4 kikombe cha chai)
Chumvi (salt 1/4 kijiko cha chai)
Hiliki (ground cardamon 1/4 kijiko cha chai)
Maji kiasi
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Tia unga kwenye bakuli, kisha weka sukari, chumvi, hiliki na maji kiasi. Kisha koroga mpaka mchanganyiko wako uwe mzito. Baada ya hapo tia yai na ukoroge tena. hakikisha mchanganyiko hauwi mzito sana au mwepesi sana.Baada ya hapo onja kama kila kitu kimekolea. Injika chuma cha kupikia chapati (fry-pan) jikoni katika moto wa wastani. Baada ya hapo tia nusu kijiko cha chakula cha mafuta katika fry-pan na kisha yatandaze. Hakikisha chuma kinapata moto na weka upawa mmoja wa unga wa chapati na uutandaze mpaka uwe flat. Baada ya hapo subiri mpaka chapati ikauke juu na kisha igeuze upande wa pili tia mafuta kijiko 1 kikubwa cha chakula kwa upande wa chini na wa juu kisha uanze kuikandamiza kwa juu na kijiko ili iweze kuiva vizuri kwa chini. Ikisha kuwa ya rangi ya brown igeuze na upike upande wa pili kiasi kisha iipue na uiweke kwenye sahani yenye kitchen towel ili kukausha mafuta. Rudia hii process kwa unga wote uliobakia. Na chapati zitakuwa tayari

Mapishi ya viazi mbatata Vya Nazi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Mbatata / viazi – 2 kilo

Nyama ng’ombe – Β½ kilo

Kitunguu maji – 2

Tungule/nyanya – 2

Nazi /tui zito – 2 vikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic) ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

pilipili shamba/mbichi ilosagwa – kiasi

Mdalasini – 1 kipande

Bizari ya manjano – Β½ kijiko cha chai

Bizari ya pilau/jiyrah/cummin – Β½ kijiko cha chai

Ndimu/limau – 1

Namna Ya Kupika:

Chemsha nyama kwa kutia; chumvi, tangawizi, kitunguu thomu, mdalasini, na bizar zote.

Ipike nyama mpaka iwive na ibakishe supu yake kidogo.

Changanya tui la nazi pamoja na supu ilobakia.

Panga mbatata katika sufuria.

Tia nyama

Mwagia vitunguu na nyanya ulizotayarisha, tia pilipili.

Mwagia supu ulochanganya na tui

Funika upike mpaka viwive .

Tia ndimu

Mapishi – Fish Finger

Leo tunaangalia mapishi ya fish finger ( sijui kama unaweza kusema kidole cha samaki)!, Ni mlo mzuri hasa kuliwa kama kitafunio au mboga ya pembeni.

Mahitaji

500g Fileti ya samaki
120g Chenga za mkate
100g Unga wa ngano
Mayai 2
Ndimu 1
Kitunguu saumu 1
Kotmiri
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Menya vitunguu saumu kisha visage

Katakata fileti kwa muundo wa mraba (kama vidole) kisha paka mchanganyiko wa vitunguu saumu

Kata ndimu na kamulia kwenye fillet yako

Weka chenga za mkate kwenye bakuli kisha uchanganye chumvi kiasi na kata kata kotmiri majani 3 na uchanganye pamoja.

Kwenye bakuli lingine weka mayai na uyapigepige yawe kama uji mzito

Weka unga kwenye bakuli jingine.

Chukua kipande cha fillet kiweke unga kidogo kisha kizamishe kwenye yai na baada ya hapo kizamishe kwenye mchanganyiko wa chenga za mkate. Fanya hivyo kwa vipande vyote.

Weka mafuta kwenye kikaago na subiri yachemke kisha weka fillet zako vizuri na zikaange pande zote hadi zimekuwa rangi ya brown ( hakikisha moto sio mkali sana).

Epua na weka pembeni mafuta yote yakauke

Weka kwenye sahani tayari kwa kula.

Jinsi ya kupika Donati

Viamba upishi

Unga
2 Magi (kikombe kibuwa cha chai)

Sukari
1/3 Kikombe cha chai
Mayai 5

Siagi 4 Vijiko vya chakula

Hamira 1 Kijiko cha chakula

Baking Powder 1 Kijiko cha chai

Vanilla 1 Kijiko cha chai

Hiliki zilizosagwa 1 Kijiko cha chai

Sukari ya laini ya unga

(icing sugar) 1 Magi

Jinsi ya kuandaa na kupika

Unavunja mayai, unatia sukari, hamira, baking powder, vanilla na hiliki ikisha unapiga kwa kutumia mchapo wa kupigia keki. Unapiga mchanganyiko kwa muda wa dakika tano.

Unatia siagi kwenye sufuria na unaiyayusha na kuipasha moto mpaka iwe moto ikisha unaimimina kwenye mchanganyiko na unapiga tena kwa dakika mbili tu.

Unatia unga kwenye sinia au bakuli kubwa ikisha unamimina ule mchanganyiko kwenye unga na unaukanda kutumia mkono, mpaka ulainike.

Ukiona unga mwingi basi ongeza maziwa kidogo mpaka uwe sawa, na ukiona unga mwepesi sana basi unaweza kuongeza unga kidogo pia mpaka ukae sawa mfano wa unga wa maandazi.

Sukuma na ukate madonge kama unavyoyaona hapo juu. Tumia kifuniko cha chupa kwa kukatia kiduara kidogo katikakti ya madonge.
Ukimaliza kukata madonge yote, yaweke kidogo yavimbe halafu teleka mafuta na uyachome.
Ukitoa kwenye mafuta yachuje moto na kabla ya kupoa yawe moto moto yarovye kwenye icing sugar na uhakikishe yote yameenea sukari juu.
Ukimaliza tia kwenye sahani acha zipowe na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Mlenda wa bamia na nyanya chungu

Mahitaji

Bamia (okra) 20
Nyanya chungu (garden eggs) 5
Magadi soda (Bicabonate soda) 1/4 ya kijiko cha chai
Nyanya (fresh tomato) 1
Chumvi (salt) kidogo
Pilipili 1/4

Matayarisho

Osha bamia, nyanya chungu na nyanya kisha vikatekate katika vipande vidogovidogo. Baada ya hapo vitie kwenye sufuria na vitu vyote vilivyobakia na kisha tia maji kidogo.Chemsha mpaka bamia na nyanya chungu ziive na vimaji vibakie kidogo sana. Baada ya hapo ziponde na mwiko kidogo kisha zikoroge na uipue na mlenda utakuwa tayari kwa kuliwa na ugali.

Jinsi ya kuandaa Ndizi Mbichi Za Supu Ya Nyama Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi mbichi – Kisia

Nyama ng’ombe – Β½ kilo

Pilipili ya kusaga – 1 kijiko cha chai

Tangawizi ya kusaga – 2 vijiko vya supu

Thomu (garlic/saumu) – 1 kijiko cha supu

Bizari mchuzi – 1 kijiko cha chai

Nazi ya unga (ukipenda kuongezea) – 2 vijiko cha supu

Chumvi – Kiasi

Ndimu – 1 kamua

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama ng’ombe katika sufuria, tia tangawizi, thomu, pilipili mbichi, bizari, chumvi. Roweka kidogo ukipenda kisha ikaushe yenyewe kwa maji yake
Ongezea maji ya kiasi yasizidi mno, kisha funika na chemsha.
Menya ndizi, ukatekate.
Nyama ikikaribia kuiva, weka ndizi uendelee kupika mpaka viive vyote.
Tia nazi ya unga kidogo tu ukipenda. Koleza kwa bizari mchuzi, pilipili, na ndimu
Epua mimina katika chombo cha kupakulia zikiwa tayari.

Jinsi ya kutengeneza juisi ya nyanya

Viamba upishi

Nyanya 1Β kg
Maji Iita Β½
Chumvi kijiko kidogo 1
Sukari

Hatua

β€’ Osha nyanya, katakata na chemsha na maji mpaka zilainike.
β€’ Chuja juisi.
β€’ Pima juisi – vikombe 2 vya juisi kwa kikombe 1 cha sukari, weka
kwenya sufuria safi .
β€’ Ongeza chumvi, chemsha ukikoroga mpaka ichemke.
β€’ Mara ikichemka epua, pozesha na weak kwenya chombo safi kwa
kunywa.

Madhara ya kula yai bichi

Yai bichi linaweza kuwa na vijidudu viitwavyo kwa kitaalamu β€œSALMONELLA” vinavyoweza kusababisha tumbo kuuma, kichefuchefu na pia kuharisha.
Vijidudu ya β€œSalmonella” vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa watoto, wazee na wale wenye hali dhaifu ya kimwili kama wagonjwa wa UKIMWI.

Pia yai bichi lililowazi linaweza kuwa zalio zuri la vimelea vya maradhi mbalimbali. Inashauriwa kupika yai mpaka liive kabisa, na kuhakikisha kwamba hakuna ute unaoteleza.

Kama ni yai la kuchemsha, lichemshwe kwa dakika kumi zaidi baada ya maji kuchemka. Pia ni muhimu kuhakikisha kwamba vyombo vilivyotumika k u k o rogea yai bichi vinaoshwa kwa maji na sabuni kabla ya kuvitumia tena kwa matumizi mengine ili kuepuka maradhi.

Mapishi ya Maharage na spinach

Mahitaji

Maharage yaliyochemshwa kiasi
Spinach zilizokatwa kiasi
Vitunguu maji 2
Nyanya 1/2 kopo
Swaum/Tangawizi 1 kijiko cha chakula
Curry powder 1 kijiko cha chai
Olive oil
Chumvi

Matayarisho

Kaanga vitunguu vikianza kuwa vya brown tia tangawizi/swaum kisha nyanya. Pika mpaka nyanya ziive kisha tia curry powder na chumvi. Vipike kiasi kisha tia maharage na maji kidogo kisha funika na uache vichemke. Baada ya muda tia spinach vipike pamoja na maharage mpaka ziive kisha ziipue. Baada ya hapo mboga yako itakuwa tayari kwa kuseviwa.

Shopping Cart
🏠 Home πŸ“– Reading πŸ–ΌοΈ Gallery πŸ’¬ AI Chat πŸ“˜ About