Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Tambi za sukari

Mahitaji

Tambi (spaghetti 1/2 ya packet)
Mafuta (vegetable oil)
Sukari (sugar 1/2 kikombe cha chai)
Hiliki (cardamon 1/2 kijiko cha chai)
Chumvi (salt 1/2 kijiko cha chai)
Tui la nazi (coconut oil 1 kikombe cha chai)
Maji kiasi

Matayarisho

Tia mafuta kiasi kwenye sufuria kisha ibandike jikoni (katika moto wa wastani) yakisha pata moto kiasi tia tambi na uanze kuzikaanga kwa kuzigeuzageuza kila mara mpaka zitakapokuwa za yangi ya light brown. baada ya hapo ipua na umwage mafuta ya kwenye tambi (bakiza kidogo sana kwani usipofanya hivyo tambi zitakuwa na mafuta sana) Baada ya hapo zirudishe jikoni na kisha utie hiliki, chumvi, sukari, tui la nazi na maji kiasi. Zifunike kisha ziache zichemke mpaka maji yakauke. Baada ya hapo zigeuze na uzipike mpaka ziive. Nahapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Kabichi

Mahitaji

Kabichi 1/2 kilo
Nyanya ya kopo 1/2
Kitunguu 1
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Kwanza kabisa bandua magada ya juu ya kabichi, kisha ioshe na uikaushe maji baaba ya hapo katakata kabichi (inapendeza zaidi kama ikikatwa nyembamba) kisha saga pamoja nyanya na kitunguu. Baada yahapo tia katika sufuria ya kupikia, ipike mpaka maji yote yatakapokauka kisha tia chumvi, curry powder na mafuta pika kwa muda kiasi kisha tia kabichi na upunguze moto. Pika mpaka kabishi itakapoiva kisha ipua na itakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuila kwa wali au ugali.

Jinsi ya kupika Cookies Za Jam Ya Peach Na Raspberry

MAHITAJI

Unga kikombe 1 Β½

Siagi Β½ kikombe

Sukari Β½ kikombe

Yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jam ya peach na raspberry

MAANDALIZI

Wash oven moto wa takriban 180 – 190 Deg F
Piga siagi na sukari katika mashine mpaka iwe laini na nyororo (creamy) kisha weka yai na vanilla.
Tia unga kidogo kidogo uchanganye kwa mwiko wa mbao (wooden spoon).
Pakaza mkononi unga uchukue vidonge ubonyeze kufanya vishimo vya kuwekea jam.
Panga katika treya uliyopakaza siagi.
Tia nusu yake jam ya peach na nusu jam ya raspberry
Bake katika oven kiasi robo saa mpaka ziwive na kugeuka rangi ya brown light.
Epua vikiwa tayari

Jinsi ya kupika Visheti Vya Kastadi Vya Shepu Ya Kombe

Viamba upishi

Unga wa ngano 1 Kilo

Siagi ΒΌ kilo

Mayai 2

Kastadi (custard) 3 vijiko vya supu

Baking powder 1 kijiko cha chai

Maziwa 1 Β½ gilasi

Mafuta Ya kukaangia kiasi katika karai

Maandalizi na upikaji

Weka unga katika bakuli kubwa kisha changanya na unga wa kastadi na baking powder.
Tia siagi uchanganye vizuri.
Tia mayai, kisha maziwa ya baridi uchanganye vizuri usiukande sana.
Fanya madonge kisha kata vipande vidogovidogo kisha ubonyeze kwa kidole uvikwaruze kwenye chujio lenye tundu itokee shepu (design) yake.

5- Tia mafuta katika karai yakipata moto, kaanga visheti hadi viive. Usiache hadi vikageuka rangi sana.

6- Eupua, weka katika sufuria au chombo kikubwa kusubiri shira.

Vipimo Vya Shira

Sukari Β½ kilo

Hiliki ilosagwa 1 kijiko cha chai

β€˜arki (rose flavor) 5 matone

Maji 1 gilasi

Namna Ya Kutyarisha

Changanya sukari na maji uipike hadi iwe nzito.
Ukiona mapovu yanatoka tia hilik na β€˜arki .
Mwagia katika visheti uchanganye vizuri hadi vishike na sukari.

Mapishi ya Ndizi na Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi mbichi – 10-12

Nyama ng’ombe – 1 kilo moja

Kitunguu maji – 2

Nyanya/tungule – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 7

Tangawizi mbichi – 1 kipande

Ndimu – 2 kamua

Chumvi – kiasi

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi – 3 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Saga kitunguu thomu na tangawiz mbichi.
Weka nyama katika sufuria tia kijiko kimoja cha kitunguu thomu na tangawizi, chumvi na ndimu kisha chemsha hadi iive.
Menya ndizi ukatekate
Weka mafuta katika sufuria tia kitunguu maji kilokatwakatwa ukaange kidogo tu kisha tia nyanya/tungule uendelea kukaanga.
Tia tangawizi na thomu ilobakia.
Tia ndizi, kaanga kidogo kisha tia supu ya nyama na nyama yake.
Ziache ndizi ziive zikiwa tayari tia tui la nazi zikiwa tayari.

Jinsi ya kupika Mboga Za Majani Makavu (Aina Yoyote)

Viamba upishi

Mboga za majani makavu ΒΌ kg
Mafuta vijiko vikubwa 3-4
Karanga zilizosagwa kikombe Β½
Maziwa au tui la nazi kikombe 1
Kitunguu 1
Nyanya 2
Chumvi (kama kuna ulazima)
Maji baridi

Hatua

β€’ Loweka mboga za majani makavu na maji kwa dakika 10-15.
β€’ Osha , mboga na katakata nyanya na vitunguu.
β€’ Kangaa, pukusua na saga karanga zilainike.
β€’ Kanga kitunguu, weka nyanya, koroga zilainike.
β€’ Ongeza mboga zilizolowekwa na maji yake kwenye rojo, koroga na funikia mpaka maji yakaukie na ive. Punguza moto.
β€’ Koroga karanga zilizosagwa na maji, ongeza kwenye mboga ukikoroga kwa dakika 5.
β€’ Onja chumvi, pakua kama kitoweo.
Uwezekano
Weka nyanya kidogo.
Tumia tui la nazi au krimu badala ya maziwa.
Weka nyama au dagaa au Mayai badala ya Karanga.

Virutubishi, kazi zake katika mwili na vyanzo vyake

Virutubishi

ni viini vilivyoko kwenye chakula ambavyo vinauwezesha mwili kufanya kazi zake, karibu vyakula vyote huwa na kirutubishi zaidi ya kimoja ila hutofautiana kwa kasi na ubora. Kila kirutubishi kina kazi yake mwilini na mara nyingi hutegemeana ili viweze kufanya kazi yake kwa ufanisi. Hakuna chakula kimoja chenye virutubishi vya aina zote isipokuwa maziwa ya mama kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto, ni mhimu kula vyakula vya aina mbalimbali ili kuwezesha mwili kupata virutubishi mchanganyiko vinavyohitajika.

Aina za virutubishi vinavyohitajika mwilini

  1. Kabohaidreti / vyakula vya wanga
  2. Mafuta ya Wanyama na Mimea
  3. Protini
  4. Vitamini na Madini
  5. Maji

Kabohaidreti / vyakula vya wanga

Kabohaidreti / vyakula vya wanga huvipa mwili nguvu inayoihitajika kujiendesha. Vyakula
hivi vyaweza kuwa sahili au changamani. Hii inahusu jinsi ambavyo chakula chaweza
kubadilisha sukari katika mwili. Vyakula vya wanga na sukari huvipa mwili nguvu
inayohitajika kuufanya upumue na kuendelea kuishi, kuwa na mwendo na utoaji joto, na kwa
ukuaji na utengenezaji wa mkusanyiko wa seli (tishu). Baadhi ya wanga na sukari
hubadilishwa kuwa mafuta mwilini.
Ufumwele utokanao na kabohaidreti hufanya kinyesi kiwe laini na kingi na huondoa kemikali
za sumu, na hivyo hufanya matumbo yawe na afya njema. Hupunguza uyeyushaji na
ufyonzaji wa virutubishi katika vyakula, na husaidia kupunguza unene.

Vyanzo vya kabohaidreti

Vyanzo vikuu vya kabohaidreti ni:

β€’ Nafaka

– Mahindi/ugali
– Serena
– Mtama
– Mchele
– Unga wa ngano

β€’ Mizizi ya vyakula vya wanga

– Viazi vitamu
– jimbi
– Viazi mviringo
– Muhogo mbichi
– Unga wa muhogo
– Ndizi

Mahitaji ya kabohaidreti mwilini

– Mahitaji hutofautiana kutegemea na umri, jinsi, jinsia, shughuli, hali ya kiafya
– Kula mara tatu au zaidi kwa siku.

Mafuta ya Wanyama na Mimea

Mafuta ya wanyama na mimea kwenye chakula na tishu ya shahamu kwenye miili yetu huwa
na shughuli nyingi

Kazi za mafuta ya wanyama kwenye mwili

β€’Β Virutubishi:Β mafuta ya wanyama hutoa tindikali za mafuta muhimu, ambazo
huhitajika katika ukuaji wa kawaida kwa watoto wachanga na watoto wengine na
kwa uzalishaj wa michanganyiko ya aina ya kihomoni inayorekebisha upeo mpana
wa shughuli za kimwili na kukufanya uwe mwenye afya njema.
β€’Β Usafirishaji:Β mafuta ya wanyama hubeba mafuta ya miyeyusho ya vitamini (A, D,
E, na K) na kurahisisha ufyonzaji wake.
β€’Β Ufahamu:Β mafuta ya wanyama huchangia kwenye harufu nzuri na ladha ya
chakula.
β€’Β Umbile la asili:Β mafuta ya wanyama hufanya chakula (hususan nyama na vyakula
vya kukaushwa) kuwa nyororo.
β€’Β Ukinaishaji:Β mafuta ya wanyama hukipa chakula ukinaishaji, hivyo hujikuta
umeshiba na kutosheka kwa muda mrefu baada ya chakula.
β€’Β Mafuta ya wanyama ni chanzo cha utoaji wa mkusanyiko wa kalori.Β Hili ni jambo
jema unapokuwa kwenye safari ndefu, itumiayo nguvu nyingi, ukiwa umebeba
chakula chako.

Mafuta ya wanyama mwilini hufanya yafuatayo:

β€’ Mafuta ni muundo mkuu wa mwili wa kuhifadhi nishati (ambazo ni muhimu wakati wa
ugonjwa au kupungua kwa ulaji chakula)
β€’ Mafuta hutoa sehemu kubwa ya nishati inayotumika kwenye kufanyiza kazi misuli.
β€’ Mafuta hukinga viungo vya ndani na kuhami miili yetu dhidi ya hali za joto
zinazopitiliza mipaka.
β€’ Mafuta huunda malighafi kuu ya utando wa seli (hususan seli za ubongo na za
mishipa ya fahamu)
β€’ Mafuta hugeuzwa kuwa aina nyingi za homoni (ikiwemo homoni za mambo yahusuyo
mapenzi)
Mafuta ki kitu kizuri! Isipokuwa tu pale uzuri unapozidi kiwango ndipo kunapokua na tatizo.

Aina za mafuta:

mafuta yaliyokolea dhidi ya yale yasiyokolea
Kama ambavyo kuna aina kuu mbili za kabohaidreti, kuna aina kuu mbili za mafuta
kutegemea na mfumo wake wa kikemia; mafuta yaliyokolea na yale ambayo hayajakolea.
Aina hizi za mafuta zina athali tofauti kabisa kwa afya yako.

1. Mafuta yaliyokolea

β€’ Huwa na kawaida ya kuongeza lehemu β€œmbaya” kwenye damu na kuongeza
uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo.
β€’ Mafuta yaliyokolea huwa na kawaida ya kuganda kwenye hali ya joto la kawaida.
β€’ Hupatikana kwa wingi kutokana na vyanzo vya mafuta ya wanyama.
Vyanzo vya mafuta yaliyokolea
β€’ Siagi, malai, mafuta ya nyama ya ngΓ³mbe, ngozi ya kuku, mafuta ya maziwa yenye
malai, jibini, aisikirimu, siagi, samli, mafuta ya nguruwe/ya kupikia, mafuta
yatokanayo na nyama, mawese mekundu, na nazi.
β€’ Yaliyopo nje ya utaratibu: mafuta ya nchi za joto (ikiwemo ya nazi na mawese) yana
kiwango kikubwa cha mafuta yaliyokolea.

2. Mafuta yasiyokolea

β€’ Mafuta yasiyokolea ni aina ya mafuta ambayo kwa ujumla yanahusishwa na afya bora.
β€’ Yana kwaida ya kushusha viwango vya lehemu na kupunguza hatari za magojwa ya
moyo.
β€’ Mafuta yasiyokolea huwa na kawaida ya kuwa ya mmiminiko katika joto la kawaida.
β€’ Hupatikana kwa wingi kutokana na mimea.
Vyanzo vya mafuta yasiyokolea
β€’ Mafuta yatokanayo na mboga za majani, mizeituni, miparachichi, njugu, mafuta ya
karanga, maharagwe meupe, mbegu za alizeti, mbegu za ufuta na aina nyingine za
mbegu, mafuta ya samaki na soya.
β€’ siagi, samli, mafuta ya nguruwe/ya kupikia, maziwa yenye malai, jibini, mafuta
yatokanayo na nyama, mawese mekundu, na nazi.

Kuna mafuta yatokanayo na kuchujwa kwa mafuta ya mbogamboga na kugandishwa. Mafuta
haya huishia kuwa na tabia za mafuta yaliyokolea. Mafuta haya pia hayapashwi kutumiwa
kwa wingi.

Vyanzo ni:

β€’ majarini, mafuta ya nguruwe, vyakula vya kukaangwa, donati, keki, biskuti, aiskrimu.

Mahitaji ya mafuta mwilini

Mahitaji ya mafuta huelezewa kama β€˜ni asilimia ya mahitaji yote ya nishati’. Kiwango chote
cha asilimia ya nishati kinachopashwa kitokane na mafuta katika mlo bora uliokamilika ni
kama ifuatvyo:
β€’ Asilimia 30-40 kwa watoto hadi kufikia miaka miwili kwenye milo ya nyongeza
β€’ Asilimia 15-30 kwa watoto wakubwa na wengi wa watu wazima; kwa watu wazimu
wenye afya – hadi asilimia 35 inakubalika.
β€’ Angalau asilimia 20 hadi 30 kwa akina mama wenye umri wa kuweza kuzaa (15-45).

Protini

Protini ni zana za ujenzi wa misuli yetu, viungo na baadhi ya vitu vingi vinavyotengeneza
miili yetu. Hutoa tindikali muhimu za amino zitumiwazo na mwili kutengeneza misuli ya tishu.
Mwili unahitaji protini na kalori kila siku.
Unapokosa kupata kalori na protini za kutosha kila siku, mwili wako hutumia akiba yake
kufidia pengo la ukosefu wa nishati. Hali hii huinyima mwili wako kalori unazohitaji kuufanya
uwe na afya bora na hivyo kusababisha kupungua kwa uzito.

Vyanzo vya protini

Protini yaweza kupatikana kwenye vyakula vya wanyama na mimea.

1. Vyanzo vitokanavyo na wanyama

β€’ Nyama, kuku/mabata n.k., samaki, mayai, jibini, maziwa na mtindi.
β€’ Vyakula hivi vinachukuliwa kuwa kama β€˜kamili’ au β€˜vyenye kiwango cha juu’cha
protini kwa kuwa vina aina zote za β€˜tindikali muhimu za amino’. β€˜Muhimu”inamaanisha
lazima vitumiwe kwenye milo yetu; miili yetu haiwezi kuzitengeneza.

2. Vanyzo vitokanavyo na mimea

β€’ Bidhaa zitokanazo na soya, (tofu, tempeh), maziwa ya soya na mazao mengine
yatengenezwayo na soya), maharagwe, mbegu na njugu.
β€’ Viwango vidogo vya protini vinapatikana vilevile kwenye mikate, mahindi /ngano, na
aina nyinge ya nafaka, na mbogamboga pia.
β€’ Vyanzo hivi vya protini vinachukuliwa kama β€˜si kamili’kwa kuwa vinakosa moja au
zaidi ya tindikali muhimu za amino.
β€’ Protini ya maharagwe meupe ndiyo ya kipekee. Haya yanachukuliwa kuwa ni kamili.

Mahitaji ya protini mwilini

Mahitaji hutofautiana kulingana na umri, jinsi, jinsia, na shughuli.

Vitamini na Madini

β€’ Vitamini husaidia mwili kugeuza chakula kuwa nishati na tishu.
β€’ Kuna aina 13 za vitamini kwa ujumla: Vitamini A; vitamini B; vitamini B mchanganyiko
unayojumuisha vitamini B1, Vitamini B2, Viamnini B3 vitamin, B6, Vitamini C, Vitamin
B12 tindikali ya pantotheniki (pantothenic acid), na biotini (biotin); na vitamini C, D, E,
na K.
β€’ Madini yanahitajika katika ukuaji na utunzaji wa miundo ya mwili. Yanahitajika pia
katika kutunza juisi za uyeyushaji chakula na mimiminiko iliyopo ndani na
kandokando mwa seli.
β€’ Madini hayatokani na mimea wala wanyama. Mimea hupata madini kutokana na maji
au udongo, na wanyama hupata madini kwa kula mimea au wanyama wanaokula
mimea.
β€’ Vitamini na madini hujulikana pia kama vyakula vya ujenzi na ulinzi wa mwili.
β€’ Vijirutubishi ambavyo havipatikani kwa wingi na ambavyo husababisha matatizo
mengi yatokanayo na utapiamlo wa ukosefu wa vijirutubish duniani ni kama
vifuatavyo; madini ya joto, zinki, vitamini A, chuma na folate.

Vyanzo vya Vitamini na Madini

β€’ Mboga jamii ya machungwa, kama vile viazi vitamu vya njano na karoti, matunda jamii
ya machungwa kama vile, embe, papai, na mawese mekundu ni vyanzo vizuri sana
vya vitamini A.
β€’ Matunda mengi yatokanayo na jamii ya michungwa na mboga zisizoivishwa sana
huwa na vitamini C.
β€’ Mboga za kijani kibichi hutupatia folate na kiasi cha vitamini A.
β€’ Mbogamboga nyingi (mf. nyanya, vitunguu) hutoa vijirutubishi muhimu vya nyongeza
viwezavyo kukinga mwili dhidi ya magonjwa sugu kama ya mioyo.
β€’ Njia bora ya kuhakikisha tunapata vijirutubishi na ufumwele wa kutosha ni kula aina
mbalimbali za mbogamboga, matunda na nafaka zisizokobolewa kila siku.
β€’ Nyama, viungo vya ndani vya wanyama na maini ya aina zote ni chanzo kizuri sana
cha vitamini A.

Mahitaji ya vitamin na madini mwilini

β€’ Vitamini na madini vinahitajika kwa viwango vidogo vidogo.
β€’ Mahitaji hutegemea umri, jinsi na kiwango cha shughuli, na ulaji wa aina mbalimbali
za matunda, mbogamboga na nafaka zisizokobolewa.

Maji

Maji ni kirutubishi muhimu sana. Hakika, zaidi ya nusu ya mwili ni maji. Unaweza kuishi bila
ya chakula kwa wiki kadhaa, bali hauwezi kuishi zaidi ya wiki moja bila ya maji.
Mwili unahitaji maji ili kufanya kazi.

Umuhimu wa maji mwilini

β€’ Kuhifadhi joto la mwili;
β€’ Kusafirisha virutubishi mwilini;
β€’ Kuvifanya viungo viwe na unyevunyevu;
β€’ Kuyeyusha chakula;
β€’ Kuondoa uchafu mwilini;
β€’ Kupoza mwili.
(Fikiria matumizi ya maji unapojenga nyumba; bila ya maji: saruji, mchanga na zege
havitakuwa na matumizi yeyote).

Vyanzo vya maji mwilini

β€’ Maji yenyewe
β€’ Juisi za matunda
β€’ Supu
β€’ Maziwa
β€’ Uji
β€’ Vinywaji visivyo na kafeini (vinywaji vyenye kafeini na kileo vina madawa ya
kuongeza mkojo (diuretics) inayosababisha upotevu wa maji mwilini)

Mahitaji ya maji mwilini

Lita 1.5 au glasi 8 kwa siku.

Mapishi ya Half cake (Keki)

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) kikombe 1na 1/2
Sukari (sugar) 1/4 kikombe
Barking powder 1/2 kijiko cha chai
Magadi soda (bicarbonate soda) 1 kijiko cha chai
Mafuta 2 vijiko vya chai
Mafuta ya kukaangia
Maji ya uvuguvugu kiasi

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote (kasoro mafuta ya kuchomea) kisha ukande (hakikisha unakuwa mgumu) Baada ya hapo sukuma na ukate shape uipendayo (hakikisha unakata vipande vinene kiasi na sio kama mandazi) Baada ya hapo ziweke sehemu yenye joto na uache ziumuke. Zikisha umuka zikaange katika moto mdogo ili ziive mpaka ndani. Zikisha iva zitoe na uziweke katika kitchen towel ili zichuje mafuta. Ziache zipoe na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya samaki aina ya salmon

Wakati mwingine mtu unakuwa umechoka na usingependa kupoteza muda jikoni, so mlo wa chapchap unakuwa ni wazo zuri, Mlo huu ni rahisi kuuanda na hata haikuchukui zaidi ya dakika ishirini chakula kinakuwa tayari mezani.

Mahitaji

Salmon fillet 2
Potatao wedge kiasi
Lettice kiasi
Cherry tomato
Limao 1
Swaum
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Mmarinate samaki na chumvi, swaum na nusu ya limao kisha muweke pembeni, baada ya hapo washa oven kisha tia potato wedge zikisha karibia kuiva anza kumpika samaki, tia mafuta kidogo sana kama kijiko kimoja cha chai hivi katika frypan isiyoshika chini yakisha pata moto kiasi muweke samaki wako (upande wenye ngozi chini kwanza) Mpike mpaka uone rangi ya kahawia kwa chini kisha mgeuze upande wa pili, uku samaki wako akiwa anaendelea kuiva, tayarisha salad yako kwa kusafisha lettice na nyanya kisha zichanganye pamoja kisha tengeneza salad dressing pembeni , kamua limao kisha tia olive oil na chumvi kidogo, Baada ya hapo samaki na potato wedge vitakuwa vimeiva, andaa mlo wako na utakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Viazi vya nyama

Mahitaji

Viazi (potato) 1 kilo
Nyama ya ng’ombe 1/2 kilo
Nyanya ya kopo iliyosagwa 1/2 tin
Vitunguu maji 2
Tangawizi/ swaum 1 kijiko cha chai
Hoho 1
Curry powder 1 kijiko cha chai
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/2
Chumvi
Coriander
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Safisha na katakata nyama ktk vipande vidogovidogo kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu mpaka viwe vya brown kisha tia nyama, swaum/ tangawizi, chumvi na limao. Ichanganye vizuri kisha funika na uipike mpaka iive na maji yote yakauke yani yabaki mafuta tu. Baada ya hapo tia viazi vilivyokatwa vipande vya wastani vikaange kwa muda wa dakika 10 kisha tia pilipili na curry powder na nyanya. Funika na punguza moto.Pika mpaka nyanya iive vigeuze kisha tia vimaji kidogo vya kuivishia viazi. Viazi vikikaribia kuiva(hakikisha vinabaki na rojo kidogo) tia hoho na upike kwa muda wa dk 5 kisha malizia kwa kutia coriander. Changanya vizuri kisha ipua na viazi vyako vitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Chapati za Kusukuma kitaalamu

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour 1/2 of kilo)
Siagi (butter vijiko 2 vya chakula)
Yai (egg 1)
Chumvi (1/2 ya kijiko cha chai)
Hiliki (ground cardamon 1/4 ya kijiko cha chai)
Maji ya uvuguvugu (warm water)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Weka unga wa ngano katika bakuli la kukandia, kisha tia chumvi na hiliki na uchanganye kwanza, baada ya hapo tia siagi na uichanganye vizuri na unga mpaka ipotee. Baada ya hapo tia tena yai na uchanganye vizuri. Mchanganyiko ukishachanganyika vizuri sasa unaweza kutia maji ya uvuguvugu kidogo, kidogo huku ukiwa unauchanganya ili kupata donge. Baada ya hapo anza kukanda hilo donge mpaka mabuje yote yapotee na unga uwe mlaini, ambapo itakuchukua kama dakika 15. Baada ya hapo tawanyisha unga katika madonge ya wastani (yasiwe makubwa sana au madogo sana) Ukimaliza hapo, andaa kibao cha kusukumia chapati kwa kukitia unga kidogo ili chapati isinatie kwenye kibao. Sukuma donge moja la chapati mpaka liwe flat na kisha weka kijiko kimoja cha mafuta na usambaze. ukisha maliza ikunje (roll). Fanya hivyo kwa madonge yote yaliyobakia.
Baada ya hapo andaa chuma cha kuchomea (fry-pan) katika moto wa wastani. Kisha anza kusukuma chapati (ni vizuri ukaanza na zile ulizozikunja mwanzo ili kuzipa nafasi zile za mwisho ziweze kulainika) ukiwa unasukuma hakikisha zinakuwa flat (na zisiwe nene sana au nyembamba sana) Ukishamaliza hapo tia kwenye chuma cha kuchomea. Acha iive upande mmoja then igeuze upande wa pili. Tia mafuta ama kijiko kimoja kikubwa upande wa chini wa chapati na uanze kuukandamiza kwa juu uku ukiwa unaizungusha. fanya hivyo uku ukiwa unaigeuza kuiangalia kwa chini ili isiungue. ikishakuwa ya brown, geuza upande wa pili na urudie hivyohiyvo mpaka chapati iive. Rudia hii process kwa chapati zote zilizobakia.

Siri ya chapati kuwa laini ni kutia siagi au mafuta ya kutosha kipindi unazikanda na pia kuzikanda mpaka unga uwe laini.

Jinsi ya kupika Biryani ya mbogamboga

Biriani ni miongoni mwa vyakula ambavyo ni nadra sana kupikwa katika familia nyingi tofauti na vyakula vingine. Inawezekana ni kutokana na watu wengi kutoelewa namna ya kuoika chakula hiki kutokana na kuhitaji viungo vingi ambavyo huwapa usumbufu wapishi.
Kuna aina mbalimbali za upishi wa biriani ambapo mara nyingi hutofautiana kutokana na viungo vinavyotumika katika upishi.
Biriani la mbogamboga ni miongoni mwa aina hizo za upishi. Chakula hiki kinaweza kuliwa na kila mtu hususan wale wasiotumia nyama wala samaki.

Mahitaji:

Β½ kg mchele wa basmati
Kitunguu maji kikubwa 1
Nyanya 1 kubwa
Karoti 1 kubwa
Njegere robo kikombe
Kiazi ulaya 1 kikubwa
Tangawizi za kusaga kijiko 1
Kitunguu swaumu cha kusaga kijiko 1
Karafuu kijiko 1
Majani ya kotimili fungu 1
Maziwa ya mtingi ΒΌ kikombe
Chumvi na pilipili kiasi
Unga wa dhani kijiko 1 cha mezani
Juisi ya limao kijiko 1 cha mezani
Mafua ΒΌ lita

Maandalizi:

Chemsha mchele na kisha weka pembeni
Osha mbogamboga zote isipokuwa vitunguu na nyanya
Changanya mtindi na tangawizi pamoja na kitunguu swaumu viache vikae kwa muda wa saa moja
Chukua sufuria weka mafuta na kisha kaanga vitunguu maji, weka nyanya, chumvi, kotimili na limao halafu weka karafuu na kanga hadi vichanganyike vizuri
Miminia mchanganyiko wa mtindi na baadaye weka pilipili na baadaye weka unga wa dhania
Chukua mchele uliochemshwa changanya na mchanganyiko huo
Palia moto juu ya chakula chako na acha kwa muda wa dakika 30
Baada ya hapo chakula chako cha biriani kitakuwa tayari kwa kuliwa

Jinsi ya kupika Baklawa Za Pistachio Na Lozi

VIAMBAUPISHI

Philo (thin pastry) manda nyembamba – 1 paketi

Siagi – ΒΌ Kikombe cha chai

Baking powder – 2 Vijiko vya chai

Pistachio/ lozi – 2 vikombe vya chai

Mafuta – Β½ Kikombe

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 Vikombe vya chai

Maji – 2 Β½ Vikombe vya chai

ndimu – Β½ kijiko cha chai

JINSI YA KUANDAA

Tafuta treya iliyokuwa sawa na ukubwa wa hizo manda nyembamba (philo) au zikate hizo manda kwa ukubwa wa treya (mraba au mstatili)
Kisha yeyusha siagi changanya na mafuta.
Kisha panga manda moja pakaza mafuta juu yake kisha weka manda nyingine juu yake kisha pakaza mafuta tena weka manda nyingine juu yake, endelea kufanya hivyo mpaka ziwe kama sita au saba kisha nyunyizia pistachio na lozi halafu panga tena manda na mafuta manda na mafuta tena sita au saba kisha nyunyizia tena pistachio na lozi.
Panga namna hivyo mpaka treya ijae inapofika manda ya mwisho kata vipande vya mraba vidogodogo humo humo kwenye treya kisha nyunyizia mafuta yaliyobaki.
Washa moto wa oven 350Β°F kwa muda wa dakika 20 au hadi rangi ibadilike kidogo (isikauke sana)
Chemsha syrup yako kama shira ya majimaji lakini isiwe nzito sana ikishakuwa tayari mwisho tia ndimu acha ipoe kidogo kisha miminia juu ya treya yote halafu malizia kunyunyizia pistachio na lozi zilizobaki.
Zikishakuwa tayari zipange kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

ANGALIZO

Ukishatoa treya kwenye oven wacha ipoe kidogo na syrup yako pia wacha ipoe kidogo kabla hujamimina, ukitia ya motomoto zitalainika.
Manda nyembamba za baklawa zinauzwa tiyari madukani kwenye pakiti.

Mapishi ya Pilau Ya Nafaka Na Nyama Ya Kusaga

VIAMBAUPISHI

Mchele – 3 vikombe

Nyama ya kusaga – 1 LB

Mchanganyiko wa Nafaka upendazo; maharagwe, njegere, mbaazi n.k 1 mug

Vitunguu maji kata vipande vipande – 3 vya kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi – 2 vijiko vya supu

Mafuta – Β½ Kikombe

Mchanganyiko wa bizari (Garam Masala) – 2 vijiko vya chai

Vipande vya supu (Maggi cubes) – 3

Maji (inategemea mchele) – 5

Chumvi – Kiasi

MAPISHI

Osha mchele na roweka.
Weka mafuta katika sufuria na kaanga vitunguu mpaka viwe brown.
Tia Thomu na tangawizi, kaanga kidogo.
Weka nyama ya kusaga, chumvi na garam masala, endelea kukaanga mpaka nyama iwive.
Mwaga maji yaliomo katika kopo la nafaka na utie nafaka pekee humo.
Tia maji na vipande vya supu (Maggi cubes) huku unavivuruga, koroga kidogo.
Tia mchele, koroga kidogo.
Funika na pika kwa moto mdogo mpaka karibu na kukauka ukikorogoka kidogo. (kama unavyopika pilau ya kawaida)
*Epua uipike katika moto wa oven 350-400 Deg kwa muda wa dakika 15.
*Kama sufuria uliyotumia sio ya kupikia katika oven, mimina katika chombo chochote kinachotumika kwa oven kama bakuli la pyrex au treya za foil.
Pakua katika sahani na iko tayari kuliwa.

Mapishi ya Boga La Nazi

Vipimo

Boga la kiasi – nusu yake

Tui zito la nazi 1 Β½ gilasi

Sukari Β½ kikombe

Hiliki Β½ kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Menya boga kisha katakata vipande vya kiasi.
Weka katika sufuri tia maji kiasi ya kuchemshia na kuwiva bila ya kubakia maji mengi.
Changanya tui na sukari na hiliki kisha mimina juu ya boga wacha katika moto dakika chache tu bila ya kufunika.
Epua mimina katika chombo likiwa tayari.

Jinsi ya kutengeneza Muhogo Wa Nazi Na Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Muhogo – 3

Tui La Nazi – 2 vikombe

Chumvi – kiasi

Pilipili mbichi – 2

Mafuta – 1 kijiko moja

Kitunguu maji – 1 kidogo

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chambua muhogo ukatekate au tumia iliyo tayari.
Chemsha muhogo katika sufuria kwa maji kidogo na chumvi, funika uive muhogo.
Karibu na kukauka maji tia tui, kitunguu maji ulichokatakata na pilipili mbichi.
Unaupika moto mdogo mdogo hadi ukauke tayari kuliwa na samaki au kitoweo chochote kingine

Mapishi ya Ndizi Mbichi Za Nyama Ng’ombe

Vipimo

Ndizi mbichi – 10

Nyama – kilo 1

Nazi ya kopo – 1

Chumvi – 1 Kijiko cha chakula

Ndimu – 1

Bizari ya manjano – 1 Kijiko cha chai

Pili pili mbichi – 3

Nyanya (tomatoes) – 2

Kitunguu maji – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi iliyosagwa – 1 Kijiko cha chakula

Namna ya Kutayarisha Na Kupika

Kata nyama vipande vipande na uisafishe.
Chemsha nyama weka chumvi, thomu, tangawizi na ndimu. Iache iwive.
Kata kata nyanya na kitunguu, kisha mimina kwenye nyama inayochemka, weka na bizari nusu kijiko. Wacha supu iwive kisha weka pembeni. Ukumbusho: Hakikisha supu inakuwa kiasi na si nyingi.
Menya maganda ndizi na uzikate vipande vipande vya kiasi.
Zikoshe ndizi na uziweke ndani ya sufuria.
Weka maji ndani ya sufuria kisha zichemshe ndizi mpaka ziwe laini kidogo.
Zimwage maji ndizi kisha mimina supu na nyama ndani ya ndizi.
Mimina nazi pili pili na bizari nusu kijiko ndani ya ndizi na uziweke kwenye jiko zichemke mpaka zibakie na urojo kiasi. Onja chumvi na uongeze kadri utakavyopenda.
Weka pembeni zipoe.
Pakua ndizi kwenye sahani au bakuli tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Ndizi za nazi na utumbo

Mahitaji

Ndizi mshale 10
Utumbo wa ng’ombe 1/2 kilo
Nazi ya kopo 1
Nyanya 1
Kitunguu kikubwa 1
Tangawizi/ swaum 1 kijiko cha chakula
Olive oil kiasi
Limao 1
Chumvi
Curry powder 1 kijiko cha chai
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Coriander ya powder 1/2 kijiko cha chai
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Pilipili kali nzima (usiipasue)

Matayarisho

Safisha utumbo kisha uweke ktk pressure cooker pamoja na chumvi kiasi, limao, tangawizi, swaum na maji kiasi kisha uchemshe kwa muda wa nusu saa. Baada ya hapo menya ndizi kisha zikate vipande vidogo kiasi ili ziwahi kuiva, kisha ktk sufuria ya kupikia tia vitunguu na nyanya kisha ndizi kwa juu yake na supu ya utumbo kiasi chumvi kidogo na mafuta kiasi kisha bandika jikoni na uchemshe mpaka ndizi zikaribie kuiva. Zikisha karibia kuiva tia utumbo na spice zote, pilipili nzima na tui la nazi kisha changanya vizuri na uache vichemke mpaka ndizi na tui la nazi vitakapoiva na rojo ibaki kiasi. Baada ya hapo Ndizi zako zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali Wa Kichina Wa Kuku Na Mboga Mchanganyiko

Vipimo

Mchele wa basmati/pishori – 4 vikombe vikubwa (mugs)

Kuku – 2

Vitnguu vya kijani (sprin onions) katakata – 5 miche

Maharage machanga (spring beans) katakata – kiasi kujaza mug moja

Pilipili boga la (capsicum) katakata – 1

Karoti katakata vipande virefu – 1

Kitunguu thomu (garlic) kuna (grate) – 1 kubwa

Tangawizi mbichi kuna (grate) – 1 kubwa

Sosi ya soya (soy sauce) – 2 vijiko vya supu

Kidonge cha supu – 1

Mafuta ya kupikia – ΒΌ kikombe cha chai

Chumvi – kiasi

Pilipili manga – 1 kijiko cha supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha kuku vizuri, katakata vipande, weka katika sufuria, tia chumvi, pilipili manga, mfunike, umkaushe motoni huku ukimgeuza geuza.

Roweka mchele kisha uchemshe uive nusu. Chuja maji, tia siagi kidogo ili usigandane.

Weka karai ya kupika mboga (wok) au sufuria kisha tia mafuta yashite moto.

Tia kitunguu thomu, tangawizi, kaanga kidogo.

Tia mboga zote, ulizokatakata.

kaanga kidogo, kisha tia sosi ya soya na kidonge cha supu. Usizipike sana mboga mpaka zikalainika mno. Sababu zitaiva katika mchele

Changanya kuku na mboga kisha changanya vyote katika mchele, urudishe katika moto.

Funika upike hadi uive kamilifu.

Pakua kwenye sahani.

Mapishi ya wali kuku wa Kisomali

Mahitaji ya wali

Mchele – 3 vikombe

Vitunguu (viliokatwa vidogo vidogo) – 2

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 kijiko cha chai

Bizari ya pilau – 1 kijiko cha supu

Mdalasini – 1 kijiti

Hiliki – 3 chembe

Pilipili manga nzima – chembe chache

Siagi – Vijiko 2 vya supu

Chumvi – kiasi

Mahitaji kwa kuku

Kuku kidari (Breast) kata vipande vipande – 2 LB

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Kotmiri iliyokatwa ndogo ndogo – kiasi

Bizari ya pilau (cummin au jiyrah) – 1 kijiko cha chai

Pilipili kubwa tamu la kijani – 1

Pilipili kubwa tamu nyekundu – 1

(zikate vipande vipande)

Karoti iliyokunwa – 1 – 2

Chumvi – Kiasi

Mapishi ya Wali:

Roweka mchele kwa muda fulani kutegemea mchele
Katika sufuria tia mafuta na kaanga vitunguu hadi vibadilike rangi kidogo.
Tia thomu iliyosagwa, mdalasini, bizari ya pilau, hiliki, pilipili manga na chumvi, kaanga kidogo.
Tia mchele kaanga kidogo, kisha tia maji ya moto kiasi kutegemea na aina ya mchele kama kawaida ya kupika wali kama pilau.
Tia sigai, funika upikike wali hadi uwive.

Mapishi ya Kuku:

Mchanganye kuku pamoja na thomu/tangawizi iliyosagwa, chumvi, pilipili mbichi.
Katika karai tia mafuta yapate moto vizuri.
Mtie kuku, bizari ya pilau (jiyrah) na ukaange, karibu na kuiva tia vitunguu.
Tia mapilipili makubwa, kotmiri, na kaanga kwa dakika moja tu uzime moto na epua weka kando.

Shopping Cart
39
    39
    Your Cart
    Kitabu cha SMS Maalumu kwa Umpendaye
    Kitabu cha SMS Maalumu kwa Umpendaye
    1 X Sh2,500 = Sh2,500
    🏠 Home πŸ“– Reading πŸ–ΌοΈ Gallery πŸ’¬ AI Chat πŸ“˜ About