Kwa nini siku hizi kuna tofauti ya wanaume katika jamii kuwa wazi/tayari kuwa na uhusiano na wanawake Albino?

Mapenzi ya kweli hayabagui dini, kabila wala rangi. Kwa
kawaida, mapenzi ni matokeo ya hisia za mvuto. Kwa maana
hiyo, inawezekana kweli wanaume hawa wamevutiwa na hawa
wanawake enye ualbino. Ni muhimu pia kuwa na uhakika kuwa
anayesema anakupenda, anasema ukweli na zaidi anathamini
penzi lako unalomwonyesha. Pia katika jamii kuna imani kuwa
karibu na Albino kunaongeza bahati ya kutajirika.

Kwa nini Albino wengi hawataki kuoa/kuolewa au kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi?

Watu ambao wanaonekana tofauti na wengine (ama kwa misingi
ya kabila, rangi, dini, kimo au hata ualbino) wanapata shida
ya kujichanganya katika jamii. Jambo hili linazidi kufanya hali
kuwa ngumu katika kupata nafasi ya kuanza uhusiano. Kwa hiyo,
siyo sahihi kulinganisha hali hii kwa watu wanaoishi na ualbino
kwani hali hii huwatokea watu tofauti.
Albino labda hawajiamini katika kuanzisha uhusiano wa
kimapenzi kutokana na uzoefu wa kunyanyapaliwa na kubaguliwa.
Wao mara nyingi wanakuwa na woga wa kukataliwa na labda
aliye na nia ya kutaka kuwa mwenzi. Awali ya yote ni kwamba
ili upendwe ni lazima wewe ujiamini na kujipenda mwenyewe.
Changamoto walizonazo familia zenye watoto wanaoishi
na ualbino ni hasa katika kuwajengea hali ya kujiamini na
kuwaelimisha kuwa ulemavu walionao ni katika muonekano
(wa ngozi, nywele na macho). Pamoja na kuwa na muonekano
huo, watoto Albino wana uwezo sawa kama watu wengine.

Kadri utakavyojiendeleza kielimu na katika mafunzo ndivyo
itavyokuwa rahisi kwako katika kujitegemea na kumpata
mwenzi wa kuishi naye.

Mimi ni msichana Albino ninaogopa kuwa na rafiki mwanaume kwa kuhofia kuwa anataka tu kujamiiana na mimi na halafu aniache

Wakati mwingine kuwa na muonekano tofauti na watu wengine
huvuta udadisi. Na hasa tukikumbuka kwamba uvumi uliopo
unasema kuwa Albino wako tofauti katika kujamiiana jambo
ambalo linaimarisha udadisi huu. Kwa maana hiyo basi, chukua
muda wa kutafakari. Kama vile tunavyofanya katika urafiki
mwingine ni lazima uchukue muda, ujaribu kujenga mazingira
ya kusikilizana na kuelewana. Mnaweza kufanya shughuli nyingi
pamoja na baada ya muda utaweza kugundua kama urafiki wenu
ni wa kweli kwa maana anakupenda wewe kama ulivyo na siyo
kwa kitu kingine. Baada ya hapo ndipo unaweza kuingia katika
uhusiano wa karibu bila kuogopa kuachwa.

Nina rafiki wa kike ambae ni Albino wa ngozi na tunapendana sana, lakini kwa nini anakataa kujamiiana na mimi?

Rafiki yako wa kike ana haki ya kukataa kujamiiana na wewe.
Labda hayuko tayari kujamiiana au anapenda kusubiri mpaka
afunge ndoa. Maamuzi yake yatakuwa yametokana na kuogopa
matokeo ya kujamiiana katika umri mdogo au labda anafuata
maadili yaliyo kwenye dini yake. Na hata kuwa na wasiwasi kuwa
uhusiano wenu siyo wa kuaminika. Kama kweli unampenda na
unajali uhusiano weu mpe muda wa kufikiria, taratibu. Endelea
kusikilizana kwa makini na kuchunguza kwa uwazi na muweze
kufanya maamuzi sahihi. Kwa lolote lile mtakaloamua hakikisha
kuzuia matokeo yanayotokana na mimba.

Kwa nini vijana wengine Albino wanaanza kujamiiana katika umri mdogo?

Kuna sababu nyingi ambazo zinamfanya kijana kuanza kujamiiana
katika umri mdogo. Baadhi ya sababu hizi ni kama vile:
β€’ Ushindani kati ya vijana wa kuwa na vitu vya anasa kama
vile simu ya mkononi, saa na vitu vya kuchezea. Ama kutaka
mahitaji ya pesa kwa ajili ya kulipa ada ya shule.
β€’ Shinikizo kutoka kwa rika wa kumfanya mtu ajiingize kwenye
kujamiiana. Shinikizo rika unakuwa na nguvu zaidi kwa
kijana Albino kwani yeye tayari anajiona ametengwa na
hivyo kushawishika zaidi katika mambo wanayofanya wengine
ili akubalike na wanarika hao.
β€’ Kwa kuamini kwamba njia halisi ya kuonyesha mapenzi ni kujamiiana
na pia kulazimika kujamiiana hata kama ni kinyume
na matakwa yake kwa mtazamo kuwa haya ndio mapenzi ya
kweli.

Je, kuna madhara yoyote yanayompata kijana Albino wa kike au wa kiume anayeamua kutoanza kujamiiana hadi afikie umri uliokubalika?

Ukweli ni kwamba hakuna athari zinazojulikana kwakusubiri au
kuacha kujamiiana hadi mtu afikie umri unaokubalika / utu uzima
au hata muda mrefu zaidi. Pia via vya uzazi havitaathirika kwa
njia moja au nyingine (havisinyai wala kutoweka.) Kuna uvumi
potofu unaodai kuwa watu wanaoacha kujamiiana kwa muda
mrefu wanaota chunusi na upele usoni au pia kwenye sehemu
zao za siri na wengine kuchanganyikiwa. Hakuna ukweli wowote
kuhusu uvumi huu. Kuwa na chunusi usoni ni mojawapo ya hali
inayowakabili vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 19. Hali ya
kuota chunusi inasababishwa na kuwepo mafuta mengi kwenye
ngozi. Hali hii hubadilika kadri umri unavyosogea mbele. Mara
nyingi inashauriwa kufanya mazoezi ya mwili ili kuwezesha
vitundu vilivyopo kwenye ngozi kufunguka na kuwezesha ngozi
kupumua.
Hakuna madhara ya kiafya ambayo yanatokana na kuacha
kujamiiana, bali kinyume ni kuwa, kuna madhara mengi ya
kiafya, hisia na ya kimwili yanayotokana na kujamiiana katika
umri mdogo kama vile mimba zisizotarajiwa, uambukizo wa
magonjwa yatokanayo na kujamiiana pamoja na Virusi vya
UKIMWI.

Hatua gani zichukuliwe dhidi ya wanaowakeketa au kuwachezea unyago Albino juani?

Swali hili linaonyesha mambo mawili ambayo ni mabaya. Jambo
la kwanza ni ukeketaji ambao ni kinyume dhidi ya haki ya afya
ya uzazi kwa mwanamke na ni uvunjaji sheria ya kukeketa mtoto
wa kike. Jambo la pili ni kuwacheza Albino unyago juani. Kitendo
hiki ni kuwaumiza Albino kwa sababu ya ulemavu walionao wa
ngozi watapata madhara wakikaa sana juani. Pia hii ni aina ya
unyanyapaa kwa nini weusi wachezeshwe ndani na Albino juani?

Hii ni imani potofu. Ushauri unaotolewa hapa ni kutoa taarifa
kwenye serikali na jamii husika ili wachukue hatua. Kwa sababu
ni vitendo labda vilivyokubalika na jamii kama mila, ni muhimu
kuhusishwa watu wenye umaarufu katika hiyo jamii ili waweze
kushawishi jamii kubadilika. Watu hawa ni kama viongozi wa
dini na wazee mashuhuri katika jamii.

Ni hatua gani zinazochukuliwa na serikali ili kukomesha vitendo vya kuwinda Albino?

Kufuatia vitendo vibaya vya mauaji ya Albino, vilivyozuka
Tanzania tangu mwaka 2007 hadi sasa, Serikali imechukua
hatua kadhaa kurekebisha hali hiyo. Hatua hizo ni pamoja
na:
β€’ Kuliagiza jeshi la polisi kuwatafyta na kuwakamata wauaji
wa aalbino.
β€’ Kumteua Albino kuwa Mbunge wa Viti Maalumu Wanawake.
β€’ Kutangaza hadharani kuwa mauaji haya siyo utamaduni
β€’ bali ni uhalifu mbaya ambao lazima uchukuliwe hatua za
kisheria.
β€’ Kutaka mikoa yote watangaze majina ya watu wote wanahusika
na mauaji haya.
β€’ Kuliagiza jeshi la polisi kuwatafuta na kuwakamata
wauaji wa Albino.
β€’ Kuanzishwa kamati maalumu ya mahakimu ili kuharakisha
hukumu za wauaji.
β€’ Viongozi wa juu wote wanalaani vitendo hivi katika mikutano
ya hadhara na matukio maalumu kama wakati wa mbio
za Mwenge wa Uhuru mwaka 2009.

Kwani Albino hawatakiwi kuishi duniani?

Albino ni binadamu kama alivyo binadamu mwingine na ana haki
sawa za kuishi na kufaidi kuwepo kwake hapa duniani kama
ilivyo kwa binadamu wengine. Kuua Albino kwa sababu yoyote
ile ni jambo baya sana ambalo linakemewa na serikali, dini zote,
na kila mwanadamu mwenye akili timamu na maadili ya utu na
watetea haki za binadamu.
Kitendo hiki vilevile kinapingana na haki za binadamu kwa hiyo
wavunjaji wa haki hizi wanashtakiwa kisheria.

Watu wanaoua Albino wanapata faida gani?

Hakuna uchunguzi wa kisayansi ambao umeonyesha faida
yoyote inayopatikana kwa kuua Albino.
Madai ya kuwepo kwa faida katika mauaji ya Albino ni uvumi
mtupu unaoimarishwa na imani ya kishirikina na hazina msingi.
Kwa bahati mbaya uvumi huu umeimarika katika baadhi ya
jamii na hivyo kupelekea Albino kupata madhara makubwa
ya kujeruhiwa na wakati mwingine kuuawa katika jitihada za
kupata damu au viungo vya miili yao.
Kuua na kujeruhi ni kosa la jinai linaloadhibiwa kisheria. Serikali
kwa sasa ina msimamo mkali wa kukomesha makosa haya ya jinai
kwa kutumia sheria kuhukumu watuhumiwa wanapokamatwa hii
ni pamoja na kuelimisha jamii.

Inatokeaje, katika baadhi ya mazingira baba anakataa kuwa mtoto si wake?

Katika mazingira fulani, baba anapomuona mtoto ana ngozi
nyeupe anakataa ya kwamba mtoto si wake akimlaumu mama wa
mtoto kuwa amekuwa na mahusiano ya ngono na mzungu. Huu
ni upuuzi kwa sababu kila mtu anajua kuwa watoto waliozaliwa
kutoka familia za watu weusi na wazungu siyo Albino kwa mfano
Rais wa Marekani Obama ni mtoto wa mama mzungu na baba
mweusi.

Dhana hii potofu ni matokeo ya uelewa mdogo na kutoaminiana.
Watu watakapokuwa na ufahamu na uelewa kuhusu ualbino
watapunguza kuwa na hisia kama alivyofanya huyu mzazi
aliyetajwa hapa juu.

Kwa nini watu wasio na ualbino wanaogopa kuoa Albino kwa imani kuwa watawazalia watoto Albino?

Ualbino ni hali ya
kurithi, hii inamaanisha
kuwa unapata ualbino
kutoka kwa wazazi
wako. Watu wawili
weusi wanaweza kupata
Albino endapo kila
mmoja wao atakuwa
na kinasaba cha ualbino.
Hali hii huwezi kuiona
au kuijua. Unaweza tu
kuitambua baada ya
kujifungua. Takribani
mtu mmoja katika watu
70 ana kinasaba cha
ualbino lakini si rahisi
kujua ni nani anacho.
Endapo Albino ataoa
mwanamke mweusi,
uwezekano wa kuzaa
Albino ni mdogo sana.
Albino wengi waliooa au
kuolewa na watu weusi
wamepata watoto
ambao ni weusi.

Kwa upande mwingine, wanandoa ambao wamekwisha
pata mtoto Albino kuna uwezekano wa kupata mtoto mwingine
Albino katika uzazi wa pili.
Kuzaliwa Albino ni lazima mtoto huyo arithi vinasaba vya
ualbino kutoka kwa wazazi wote wawili, yaani mama na baba.

Watu wanaamini kuwa Albino wana joto katika mapenzi kuliko watu weusi, Je, hiyo ni kweli?

Hii siyo kweli,
tofauti
baina ya Albino
na mtu a s i
ekuwa na ualbino
i m e e l e z w a
hapo mwanzoni
ambapo tofauti
ipo tu kwenye
muonekano wa
rangi ya ngozi,
nywele n a macho. Mifumo yao yote mingine ya mwili iko sawa na watu
wasio na ualbino.
Watu wanaweza tu kuanzisha uvumi kama huo popote pale.
Ipo pia mifano kama: Wajerumani wanaamini kuwa Wafaransa
wana joto katika mapenzi, Wazungu pia huamini kuwa Waafrika
wana joto n.k. Hizo ni hisia tu na siyo ukweli. Katika jamii wapo
watu ambao wanapenda kufanya ngono sana, wapo wa wastani
na wapo wale ambao hawajisikii msukumo wa kujamiiana. Uvumi
huu unatokana na mawazo ya kifikra na siyo ukweli halisi.

Kwa nini Albino wanatengwa katika masuala ya mapenzi na wale watu ambao siyo Albino?

Watu huogopa kujaribu vitu au mambo ambayo hawajayazoea
au yale ambayo yapo tofauti. Jinsi unavyozidi kujua ukweli
kuhusu sababu za ualbino ndipo unavyoweza kujenga mtazamo
chanya ikiwemo kuwapenda.
Wapo pia watu wengi katika jamii yetu ambao wana mahusiano
ya kimapenzi na Albino na ambao wapo katika ndoa. Watu
wengine katika jamii wanapoona mifano hiyo inasaidia katika
kuondoa wasiwasi na kuondoa imani potofu.

Kama Albino akiathirika na VVU anaweza kutumia ARVs kama watu wengine?

Katika suala hili la UKIMWI hakuna tofauti yoyote kati ya
Albino na watu wengine katika jamii. Albino wanaweza kupata
maambukizo kama watu
wengine, na mahitaji yao ni yaleyale, kijamii, kisakolojia na kiafya.
Albino watapewa ARVs kama watu wengine kwa kufuata
utaratibu uleule wa matibabu ya UKIMWI kama wanavyofanyiwa
watu wasio Albino. Kwa hiyo kama Albino anakataliwa kupewa
huduma za dawa za kufubaza VVU (ARVs) basi atoe taarifa
kwa vyombo husika ukiwemo uongozi katika jamii au kwenye
Chama cha Albino ili waweze kuwasaidia kufuatilia haki zao.

Watu wanasema kuwa unaweza kupona UKIMWI kwa kujamiiana na Albino. Hii ni kweli?

Watu wanaweza kuvumisha uongo wowote ili kupotosha
ukweli na kufanya mambo yao maovu wanayoyapenda. Wapo
wanaosema kuwa unaweza kupona UKIMWI kwa kujamiiana na
bikira, mtu mlemavu au Albino, hizi ni imani potofu na hazina
msingi wowote.

Imani hii kuwa kwa kujamiiana na Albino mtu anaweza kupona
VVU / UKIMWI siyo kweli kabisa. Mpaka sasa hakuna tiba
ya UKIMWI ingawa kuna maendeleo makubwa yanayotokana
na dawa za kufubaza VVU (Anti-retrovirals kwa kifupi ARVs).
ARVs zimesaidia watu wengi wanaoishi na VVU kuishi maisha
bora kiafya lakini ARVs haziponyi UKIMWI. Mtu akisha athirika
na VVU ataendelea kuwa na maambukizo kwa maisha yake yote
na hakuna uponyaji wowote unapatikana kwa kujamiiana na
Albino.
Imani hizi potofu pia zinaathiri makundi mengine katika jamii
yetu, kwa mfano; kujamiiana na bikira kunaweza kuponya
UKIMWI, hii imepelekea kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji
wa watoto. Ni muhimu kwa vijana Albino kufahamu ukweli
kuhusu VVU/UKIMWI na pia mila hizi potofu ili waweze
kujikinga.

Njia ya kutambua kama umeambukizwa Virusi vya UKIMWI (VVU)?

Njia pekee ya kujitambua kama umepata maambukizo ya
VVU ni kufanya kipimo cha damu (HIV-test). Vipimo hivi
vinapatikana katika vituo vya afya na pia kupitia vituo maalumu
vya ushauri nasaha vya kupima kama vile vya Angaza, huduma
hizi zimesambaa nchi nzima. Kipimo hiki huchukua kiasi kidogo
cha damu na kawaida majibu hupatikana baada ya muda mfupi.
Mshauri nasaha ataongea na wewe na kukuelimisha zaidi kuhusu
kipimo na maana ya majibu.

Kwa nini watu wanaamini kuwa Albino hawana maambukizo ya Virusi vya UKIMWI (VVU)?

Imani hiyo si kweli kabisa. Inawezekana ni kupotoshwa kwa
makusudi wa ukweli kuhusu jambo hilo kunakofanywa na watu
wachache katika jamii ili kuendeleza matendo yao maovu. Watu
wanaweza kufuata imani potofu na zisizo na msingi wowote ili
kukwepa ukweli kuhusu VVU na UKIMWI. Kwa mfano; imani
kuwa mtu anaweza kupona UKIMWI kwa kufanya mapenzi na
bikira, mlemavu au Albino ni za uongo na hazina msingi wowote.
VVU huambukizwa kupitia majimaji ya mwili, na njia kuu ya
maambukizo ni kujamiiana bila kinga. Njia pekee za kuzuia
maambukizo ni kuacha kabisa kufanya ngono, kuwa na mpenzi
mmoja muaminifu au kutumia kondomu.Watu wanaoeneza imani hizi
potofu wanatafuta njia mbadala ya kuhalalisha tabia zao mbaya.

Wewe pia kama Albino unatakiwa kupambana na imani hizo
potofu kwani zinalenga kueneza madhara kwa watu wanaoishi
na ualbino.

Shopping Cart
2
    2
    Your Cart
    🏠 Home πŸ“– Reading πŸ–ΌοΈ Gallery πŸ’¬ AI Chat πŸ“˜ About