Je, kuna madhara gani yatokanayo na uvutaji sigara kwa vijana hasa kijana Albino?

Kuna madhara mengi ambayo hutokana na uvutaji sigara.
Madhara mengi yanampata mvutaji kwani moshi unaingia
kwenye mapafu na kuendelea kuleta madhara mengine sehemu
nyingine za mwili.

Unaweza pia kupata madhara kwa kukaa karibu na mtu
anayevuta (hii inaitwa mvutaji baki). Uvutaji unafanya mwili
wako kunyonya sumu ijulikanayo kama nikotini. Nikotini ndio
chanzo kikubwa cha matatizo yatokanayo na uvutaji.
Uvutaji sigara unahusishwa na magonjwa mengi. Kiungo cha
mwili kinachoathirika kwanza ni mapafu. Uvutaji husababisha
kukohoakohoa, vichomi na kulipuka kwa kifua kikuu (TB) na
hatimaye saratani ya mapafu. Uvutaji pia unaathiri ngozi.
Ngozi ya mvutaji inakuwa nyepesi kwani inaathiri mishipa ya
damu iliyopo karibu chini ya ngozi. Hali hii inaifanya ngozi
kushindwa kujitengeneza upya (regenerate). Kwa vile Albino
tayari wana matatizo ya ngozi ni vizuri kama hawatavuta na
kwa wale wanaovuta basi waache kuvuta.

Je, kuna madhara gani ya kunywa pombe kwa vijana hasa kijana Albino?

Athari za pombe kwa mtu anayeishi na ualbino ni sawa na zile
zinazowapata watu wengine.
Mtu akiwa katika hali ya ulevi anaweza kuzembea katika
kufanya uamuzi sahihi kwa mfano kuhatarisha maisha yake
kwa kuendesha baiskeli yake kimchoromchoro, kujamiiana
bila kuvaa kondomu na kadhalika. Mbali na hayo, watu wenye
matatizo ya kunywa pombe husahau kujiweka katika hali nzuri
kwa maana hawajali kula chakula. Tabia hii inamuweka katika
hatari ya kuandamwa na maradhi.
Pombe zinaweza pia kuingiliana na maisha/uhusiano wa kimwili.
Mwanzo kabisa pombe inaweza kukusisimua na kukufanya
mchangamfu (kutoona aibu), lakini kadiri unavyoendelea
kunywa unaanza kusinzia na kwa upande wa wanaume wengine,
uume kukosa nguvu. Unaweza kushawishika kutoa aibu uliyo
nayo kwa kunywa pombe lakini mara nyingi hii haileti mvuto
kutoka kwa wenzi wako.

Kunywa pombe pia kunaleta uharibifu wa kudumu kwenye ubongo
ambao unamfanya mtu kupata matatizo ya kumbukumbu.
Pombe imewekwa kwenye kundi la vilevi tegemezi. Mwili
ukishazoea pombe, ni rahisi sana watu kutumia pesa zote
kwa ajili ya pombe na kusahau kufanya mambo mengine
yatakayomletea maendeleo katika maisha yake.

Watu wanaoishi na ulemavu wanapewa huduma za upasuaji hasa wakati wa kujifungua?

Upasuaji unafanyika kwa wanawake wote ambao wamegundulika
kuwa na tatizo la kujifungua kwa njia ya kawaida. Hii inafanyika
bila kujali hali yao kwa maana kwa watu wenye ulemavu na
wasio na ulemavu. Kila mwanamke atapata huduma hiyo kama
itakuwepo sehemu anapoishi.
Tatizo lililopo hapa Tanzania kwa sasa hivi hasa sehemu
zilizojitenga ni umbali wa kufikia huduma hii. Umbali huu
unamfanya mama aliyeanza uchungu wa kujifungua kushindwa
kuweza kufika kwa muda unaotakiwa.

Haki za ujinsia na afya ya uzazi zinamhusu pia mtu anayeishi na ualbino?

Haki za msingi; hasa zile zinazohusiana na kuthaminiwa na
kuheshimiwa kama binadamu zinawahusu binadamu wote
kuanzia siku unayozaliwa. Mataifa yote Ulimwenguni yameridhia
mikataba ya Kimataifa inayokubaliana na matamko haya ya
haki. Haki hizi ziko dhahiri katika sheria za nchi husika. Haki
muhimu za ujinsia na afya ya uzazi ni hizi:
• Kupata habari juu ya ujinsia na mada zinazohusu afya ya
uzazi.
• Mwanamke au mwanaume kuamua kwa uhuru na kuwajibika,
kama anataka kujamiiana lini na mtu gani.

• Kuamua idadi ya watoto anaotaka kuzaa na hao watoto
wapishane miaka mingapi.
• Kupata huduma za afya ya uzazi.
• Kuamua bila kulazimishwa nani wa kufunga naye ndoa.
• Kulindwa dhidi ya mila zenye madhara kama vile ukeketaji
wa wanawake.
Watu wote wakiwemo wale wanaoishi na ualbino au ulemavu
wa aina yoyote wanalindwa na haki za binadamu. Changamoto
iliyopo ni kwa wale watu wanaoishi na ualbino kutoa sauti katika
kutetea na kuhamasisha jamii juu ya haki zao.

Je, mimi ni msichana Albino ninaweza kupata mimba kama nikijamiiana mara moja tu?

Ndiyo msichana anaweza kupata mimba kwa kujamiiana mara
moja tu bila kujali ana rangi gani ya ngozi. Wasichana weupe,
weusi na wanaoishi na ualbino au wasio na ulemavu wa ngozi
wanafanana wote inapokuja kwenye suala la uwezekano wa
kupata mimba. Kinachobainisha/ kinachosababisha upatikanaji
wa mimba ni wakati tendo la kujamiiana linapofanywa na hatua
ya mzunguko wa hedhi. Kama yai lililopevuka kwa ajili ya
kurutubishwa litakuwa tayari basi ujauzito utatokea mara tu
baada ya mbegu ya mwanaume kuingia, (wakati wa kujamiiana).
Ujauzito unaweza kutokea hata kama msichana alikuwa bado
bikira na ni mara yake ya kwanza kujamiiana.

Je, wazazi ambao wote ni Albino wanaweza kupata mtoto ambaye siyo Albino?

Kwa kawaida, wazazi wote wakiwa Albino watazaa mtoto
Albino. Kwa maana hiyo basi, iwapo watu wawili wanaoishi na
ualbino wataamua kuunda familia itakuwa vizuri wafikirie kwa
makini kama wangependa kuzaa pamoja wakizingatia matatizo
ambayo wamewahi kupitia wao wenyewe kama Albino ndani ya
jamii. Ualbino ni hali ya kurithi na inabidi mtoto Albino abebe
vinasaba kutoka kwa wazazi pande zote ili aweze kuonyesha
ualbino. Hata hivyo, kuna aina zaidi ya moja ya ualbino na
pia aina tofauti za vinasaba, kama wazazi watakuwa na aina
tofauti ya ualbino na aina tofauti katika vinasaba, uwezekano
wa kupata mtoto asiyekuwa na ulemavu wa ngozi unakuwepo.
Lakini matukio kama haya yamejitokeza mara chache sana
ulimwenguni.

Je, ni kweli kuwa ulemavu unaweza kugundulika mara tu mtoto anapozaliwa?

Ni kweli kuwa daktari anaweza kufanya vipimo vya kugundua
kama mtoto aliye tumboni ni mwenye ulemavu au la. Baadhi ya
vipimo hivi ni “ultra sound” ambacho kinawezesha kuona picha ya
umbo la mtoto akiwa bado tumboni. Vipimo vingine vinaangalia
damu. Lakini ualbino hauwezi kugundulika kwa vipimo hivi.
Pia baada ya kuzaliwa daktari ana uwezo wa kutambua kama
mtoto ana ulemavu / hitilafu kama vile moyo, kwenye damu
kama vile “sickle cell”. Ualbino unaweza kugundulika mara tu
mtoto anapozaliwa au baada ya wiki chache.

Je, mtu anaweza kuzuia kupata mimba baada yakujamiiana bila kinga (kufanya ngono zembe) kwa mfano amebakwa?

Kama umebakwa au kulazimishwa kujamiiana unaweza kupata
huduma katika hospitali, kituo cha afya , zahanati au kutoka
kwa mhudumu wa afya ambaye atakupatia vidonge vya dharura
vya kuzuia mimba. Hivi ni vidonge ambavyo vinatumika ili
kupunguza uwezekano wa kupata mimba kama ulijamiiana bila
kinga, au umesahau kutumia njia yako ya uzazi wa mpango au
ulilazimishwa kujamiiana.

Ili ufanye kazi, njia hii ya dharura ya kuzuia mimba inatakiwa
itumiwe ndani ya saa 120 (ndani ya siku tano) baada ya tukio.
Inakuwa vizuri zaidi kama njia hii ya dharura itatumika punde
bila kusubiri kwani kwa kufanya hivyo, ufanisi wake unakuwa
wa kuaminika zaidi.

Hii njia ya dharura inazuia tu mimba kutungwa, haiwezi kusababisha
kutoka kwa mimba pindi mimba ikishatunga. Utakapotafuta
msaada wa kupata huduma ya vidonge vya dharura
vya kuzuia mimba hasa kwa wale waliobakwa au kulazimishwa ,
mwombe mhudumu akusaidie kupata huduma ya kuzuia maambukizo
ya UKIMWI. (Post exposure prophylasis). Unaweza
kupata taarifa zaidi kwa mtoa huduma wa uzazi wa mpango
kwenye kliniki za serikali, kliniki za UMATI, kliniki za Marie
Stopes au sehemu yoyote wanapotoa njia za kisasa za uzazi
wa mpango.

Kuna athari gani za mimba za utotoni hasa kwa kijana Albino?

Katika masuala ya athari za mimba katika umri mdogo ni
kwamba vijana Albino hawana tofauti na vijana wengine . Bado
inashauriwa na kutiliwa mkazo umuhimu wa msichana kutopata
mimba akiwa na umri chini ya miaka 18.

Sababu kubwa ikiwa ni
kuwa mwili wa msichana
ambaye umri wake ni chini
ya miaka 18 haujakomaa
vya kutosha kuweza
kuhimili ujauzito bila
matatizo. Katika umri huu
mdogo, uwezekano mkubwa
wa kupata matatizo
yanayotokana na ujauzito,
hasa wakati wa kujifungua.
Uzoefu umeonyesha
kuwa mara nyingi wakati
wa kujifungua mtoto
anashindwa kutoka na
inabidi mama afanyiwe
upasuaji. Pia katika
umri huu uwezekano ni
mkubwa mtoto kuzaliwa
njiti (hajafikia muda wa
kuzaliwa).
Tatizo jingine linaweza kutokea pale ambapo kichwa cha mtoto
ni kikubwa au mama anakuwa na uchungu wa muda mrefu na
kusababishwa kuchanika kwenye mfumo wa uzazi kwenye njia
ya haja ndogo au hata na njia ya haja kubwa na mama kupata
fistula. Hali hii ikitokea itamfanya mama hatimaye awe anavuja
ama haja ndogo au haja kubwa au vyote viwili kupitia njia ya
ukeni.

Mbali na madhara haya ya kiafya, msichana anaweza kupata
matatizo mengine ya kijamii kama vile kufukuzwa shule,
kusababisha ugomvi ndani ya familia na jamii. Kwa mantiki hii,
ni muhimu kwa vijana kusubiri hadi kufikia miaka 18 wakiwa
tayari kuchukua / kubeba majukumu kama wazazi.

Je, kuna vipimo ambavyo vinaweza kugundua hali ya kuwepo kwa ualbino wakati kichanga kikiwa bado tumboni?

Hakuna kipimo rahisi cha kuwezesha kuonyesha kama mama
mjamzito amebeba kinasaba cha ualbino. Lakini uwezekano upo,
kama wazazi watakuwa wamepata mtoto Albino. Uwezekano wa
kujua kama mimba inayofuatia kichanga kitakuwa na ualbino kwa
kutumia kipimo maalamu kinachovuta maji yaliyo kwenye mji wa
mimba na kupima hayo majimaji kuona kama kuna kinasaba cha
Albino. Hata hivyo, vipimo hivi ni vya gharama kubwa na kwa
kiasi kikubwa kwa sasa vinapatikana, katika hospitali kubwa
maalumu za nchi zilizoendelea (Ulaya, Marekani na kadhalika).

Kwa nini siku hizi kuna tofauti ya wanaume katika jamii kuwa wazi/tayari kuwa na uhusiano na wanawake Albino?

Mapenzi ya kweli hayabagui dini, kabila wala rangi. Kwa
kawaida, mapenzi ni matokeo ya hisia za mvuto. Kwa maana
hiyo, inawezekana kweli wanaume hawa wamevutiwa na hawa
wanawake enye ualbino. Ni muhimu pia kuwa na uhakika kuwa
anayesema anakupenda, anasema ukweli na zaidi anathamini
penzi lako unalomwonyesha. Pia katika jamii kuna imani kuwa
karibu na Albino kunaongeza bahati ya kutajirika.

Kwa nini Albino wengi hawataki kuoa/kuolewa au kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi?

Watu ambao wanaonekana tofauti na wengine (ama kwa misingi
ya kabila, rangi, dini, kimo au hata ualbino) wanapata shida
ya kujichanganya katika jamii. Jambo hili linazidi kufanya hali
kuwa ngumu katika kupata nafasi ya kuanza uhusiano. Kwa hiyo,
siyo sahihi kulinganisha hali hii kwa watu wanaoishi na ualbino
kwani hali hii huwatokea watu tofauti.
Albino labda hawajiamini katika kuanzisha uhusiano wa
kimapenzi kutokana na uzoefu wa kunyanyapaliwa na kubaguliwa.
Wao mara nyingi wanakuwa na woga wa kukataliwa na labda
aliye na nia ya kutaka kuwa mwenzi. Awali ya yote ni kwamba
ili upendwe ni lazima wewe ujiamini na kujipenda mwenyewe.
Changamoto walizonazo familia zenye watoto wanaoishi
na ualbino ni hasa katika kuwajengea hali ya kujiamini na
kuwaelimisha kuwa ulemavu walionao ni katika muonekano
(wa ngozi, nywele na macho). Pamoja na kuwa na muonekano
huo, watoto Albino wana uwezo sawa kama watu wengine.

Kadri utakavyojiendeleza kielimu na katika mafunzo ndivyo
itavyokuwa rahisi kwako katika kujitegemea na kumpata
mwenzi wa kuishi naye.

Mimi ni msichana Albino ninaogopa kuwa na rafiki mwanaume kwa kuhofia kuwa anataka tu kujamiiana na mimi na halafu aniache

Wakati mwingine kuwa na muonekano tofauti na watu wengine
huvuta udadisi. Na hasa tukikumbuka kwamba uvumi uliopo
unasema kuwa Albino wako tofauti katika kujamiiana jambo
ambalo linaimarisha udadisi huu. Kwa maana hiyo basi, chukua
muda wa kutafakari. Kama vile tunavyofanya katika urafiki
mwingine ni lazima uchukue muda, ujaribu kujenga mazingira
ya kusikilizana na kuelewana. Mnaweza kufanya shughuli nyingi
pamoja na baada ya muda utaweza kugundua kama urafiki wenu
ni wa kweli kwa maana anakupenda wewe kama ulivyo na siyo
kwa kitu kingine. Baada ya hapo ndipo unaweza kuingia katika
uhusiano wa karibu bila kuogopa kuachwa.

Nina rafiki wa kike ambae ni Albino wa ngozi na tunapendana sana, lakini kwa nini anakataa kujamiiana na mimi?

Rafiki yako wa kike ana haki ya kukataa kujamiiana na wewe.
Labda hayuko tayari kujamiiana au anapenda kusubiri mpaka
afunge ndoa. Maamuzi yake yatakuwa yametokana na kuogopa
matokeo ya kujamiiana katika umri mdogo au labda anafuata
maadili yaliyo kwenye dini yake. Na hata kuwa na wasiwasi kuwa
uhusiano wenu siyo wa kuaminika. Kama kweli unampenda na
unajali uhusiano weu mpe muda wa kufikiria, taratibu. Endelea
kusikilizana kwa makini na kuchunguza kwa uwazi na muweze
kufanya maamuzi sahihi. Kwa lolote lile mtakaloamua hakikisha
kuzuia matokeo yanayotokana na mimba.

Kwa nini vijana wengine Albino wanaanza kujamiiana katika umri mdogo?

Kuna sababu nyingi ambazo zinamfanya kijana kuanza kujamiiana
katika umri mdogo. Baadhi ya sababu hizi ni kama vile:
• Ushindani kati ya vijana wa kuwa na vitu vya anasa kama
vile simu ya mkononi, saa na vitu vya kuchezea. Ama kutaka
mahitaji ya pesa kwa ajili ya kulipa ada ya shule.
• Shinikizo kutoka kwa rika wa kumfanya mtu ajiingize kwenye
kujamiiana. Shinikizo rika unakuwa na nguvu zaidi kwa
kijana Albino kwani yeye tayari anajiona ametengwa na
hivyo kushawishika zaidi katika mambo wanayofanya wengine
ili akubalike na wanarika hao.
• Kwa kuamini kwamba njia halisi ya kuonyesha mapenzi ni kujamiiana
na pia kulazimika kujamiiana hata kama ni kinyume
na matakwa yake kwa mtazamo kuwa haya ndio mapenzi ya
kweli.

Je, kuna madhara yoyote yanayompata kijana Albino wa kike au wa kiume anayeamua kutoanza kujamiiana hadi afikie umri uliokubalika?

Ukweli ni kwamba hakuna athari zinazojulikana kwakusubiri au
kuacha kujamiiana hadi mtu afikie umri unaokubalika / utu uzima
au hata muda mrefu zaidi. Pia via vya uzazi havitaathirika kwa
njia moja au nyingine (havisinyai wala kutoweka.) Kuna uvumi
potofu unaodai kuwa watu wanaoacha kujamiiana kwa muda
mrefu wanaota chunusi na upele usoni au pia kwenye sehemu
zao za siri na wengine kuchanganyikiwa. Hakuna ukweli wowote
kuhusu uvumi huu. Kuwa na chunusi usoni ni mojawapo ya hali
inayowakabili vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 19. Hali ya
kuota chunusi inasababishwa na kuwepo mafuta mengi kwenye
ngozi. Hali hii hubadilika kadri umri unavyosogea mbele. Mara
nyingi inashauriwa kufanya mazoezi ya mwili ili kuwezesha
vitundu vilivyopo kwenye ngozi kufunguka na kuwezesha ngozi
kupumua.
Hakuna madhara ya kiafya ambayo yanatokana na kuacha
kujamiiana, bali kinyume ni kuwa, kuna madhara mengi ya
kiafya, hisia na ya kimwili yanayotokana na kujamiiana katika
umri mdogo kama vile mimba zisizotarajiwa, uambukizo wa
magonjwa yatokanayo na kujamiiana pamoja na Virusi vya
UKIMWI.

Hatua gani zichukuliwe dhidi ya wanaowakeketa au kuwachezea unyago Albino juani?

Swali hili linaonyesha mambo mawili ambayo ni mabaya. Jambo
la kwanza ni ukeketaji ambao ni kinyume dhidi ya haki ya afya
ya uzazi kwa mwanamke na ni uvunjaji sheria ya kukeketa mtoto
wa kike. Jambo la pili ni kuwacheza Albino unyago juani. Kitendo
hiki ni kuwaumiza Albino kwa sababu ya ulemavu walionao wa
ngozi watapata madhara wakikaa sana juani. Pia hii ni aina ya
unyanyapaa kwa nini weusi wachezeshwe ndani na Albino juani?

Hii ni imani potofu. Ushauri unaotolewa hapa ni kutoa taarifa
kwenye serikali na jamii husika ili wachukue hatua. Kwa sababu
ni vitendo labda vilivyokubalika na jamii kama mila, ni muhimu
kuhusishwa watu wenye umaarufu katika hiyo jamii ili waweze
kushawishi jamii kubadilika. Watu hawa ni kama viongozi wa
dini na wazee mashuhuri katika jamii.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About