Je, Tanzania kuna wataalamu wanaosaidia watu wenye matatizo ya ulevi wa kupindukia?

Ndiyo. Hapa Tanzania kuna kitengo maalumu kinachojishughulisha
na masuala ya akili. Wataalamu mbalimbali hufanya kazi pamoja
kama vile matibabu ya magonjwa ya akili na wanasaikolojia.
Wanaustawi wa jamii ambao wana mbinu za kuelewa kiwango
cha unywaji pombe katika jamii kulingana na tamaduni
mbalimbali ambao pia wana utaalamu wa masuala ya utoaji
ushauri, wanaweza kushirikiana na wataalamu wa afya ambao
hufanya kazi hospitalini na kwenye jamii.

Je, pombe ni moja ya sababu za kuenea kwa Virusi vya UKIMWI na VVU au magonjwa mengine yatokanayo na kujamiiana?

Matumizi mabaya ya pombe ndiyo yanayosababisha kuenea kwa
VVU au magonjwa mengine yatokanayo na kujamiiana. Tabia
ya ulevi ya kupindukia huwaweka watu katika hatari kubwa ya
kupata na kueneza magonjwa haya.
Pombe husababisha watu kusahau hatari ya kuwa na wapenzi
wengi na pia kufanya mapenzi na watu ambao hawafahamu hali
za afya zao. Husahau kujilinda wao wenyewe na wapenzi wao, kwa
kutumia kondomu na kusahau majukumu yao ya familia.

Watu wanaokunywa pombe kupita kiasi hudhoofisha mfumo wa
kinga mwilini, hivyo basi, virusi huingia miilini mwao kirahisi.
Kumbuka, bado hakuna tiba ya UKIMWI. Njia pekee ya kinga
ni kubadili tabia.

Je, kwa nini akina mama wajawazito hawatakiwi kunywa pombe?

Wanawake wajawazito ambao hunywa pombe au kuvuta sigara
wanahatarisha afya na maisha ya mtoto aliye tumboni. Mtoto aliye
tumboni hurutubishwa kupitia damu ya mama. Kama mama atavuta
sigara au kunywa pombe, sumu illiyopo katika sigara au pombe
inapoingia kwenye damu yake itamfikia mtoto pia. Pombe hushambulia
moyo uendeleao kukua na ubongo wa mtoto aliye tumboni.
Akina mama wanaokunywa kupita kiasi wakiwa wajawazito
wanaweza kupata watoto wenye magonjwa ya moyo au mtindio
wa akili, kwa sababu chembechembe za ubongo hazikui vizuri.
Mara nyingi watoto huzaliwa na upungufu katika mwonekano
wa sura. Kwa mtoto pombe ni sumu kali, hata kama ni kwa kiasi
kidogo, itamdhuru.

Mama anaekunywa pombe anaweza kuwa hajali au kusahau
kujilinda mwili wake na mtoto anayekua.
Kama akipata maambukizo ya VVU na mtoto pia anaweza
akapata virusi vya UKIMWI.
Wanawake wanaovuta sigara wakiwa wajawazito wana
uwezekano mkubwa wa kuzaa watoto ambao hufariki ghafla bila
sababu ya kueleweka katika mwaka wao wa kwanza wa maisha.
Watoto wa akina mama wanaovuta sigara mara nyingi huzaliwa
na umbo dogo kuliko wengine kwa sababu watoto walipata
chakula kidogo walipokuwa bado tumboni mwa mama zao.
Ujumbe upo wazi: Wanawake wanaotaka watoto wenye afya
wasivute kabisa sigara wala kunywa pombe wakiwa wajawazito.

Kwa nini watu wanakuwa wagomvi na wakali wanapokuwa wamelewa?

Madhara ya pombe husababisha watu walioolewa kugombana.
Kutokana na ushawishi wa pombe watu hupoteza tabia zao
za kawaida na kuona vigumu kuhimili mihemko na kushindwa
kufanya maamumzi katika hali hiyo. Matokeo yake, mlevi
huyachukulia tofauti mazingira na maneno. Watu waliolewa hukasirishwa haraka na vitu ambavyo wangevipuuza kama
wasingekuwa wamelewa. Mara nyingi huwapiga watu wakati
wangetatua hali hiyo kwa njia tofauti kama wasingelewa.
Kama jambo hili litatokea miongoni mwa rafiki zako au familia,
jaribu kuwa mbali na uepuke ulevi. Usijaribu kujadiliana na mtu
aliyelewa kwa sababu kwa vyovyote hatakuelewa.

Ni kwa nini ni vigumu kuacha kuvuta sigara?

Ndiyo hatari kuu ya matumizi ya dawa za kulevya ambayo
unayazoea na kufikiri huwezi kufanya lolote bila ya kutumia.

Kwa upande wa sigara unaweza kuzoea hali yake ya kukutuliza na
hali ya kutamani kila unapojisikia. Kwa wengi hamu hiyo hutokea
baada ya kazi nzito, pamoja na pombe, au baada kula. Kwa hiyo,
kama unataka kuacha uvutaji wa sigara inabidi ubadili tabia na
kuepuka vishawishi na pia kupambana na nafsi na matamanio
yako. Hii ni hatua kubwa inayohitaji msimamo mkali.
Utakapoanza kupunguza matumizi ya sigara au kuacha kabisa
utajisikia mpweke au mkiwa. Hali hii inaweza ikawa mbaya na
kuumiza. Mara nyingi utajihisi kujawa na wasiwasi, utakosa
usikivu, utajisikia kusinzia ingawa utakosa usingizi usiku,
mapigo ya moyo hushuka na pia shinikizo. Hamu ya kula na
uzito kuongezeka iwapo utendaji wako wa kazi hupungua.
Ukishatawaliwa na sigara basi kuvuta kwako si tabia bali ni
ugonjwa. Watu wengi wanaotegemea nikotini hawavuti kwa
starehe inayoletwa na starehe ya uvutaji, bali kuepuka maumivu
yanayosababishwa na kuacha sigara.

Je, unaweza kufa kutokana na kuvuta sigara na kunywa pombe?

Ndiyo. Unaweza kufa kutokana na kuvuta sigara au kunywa
pombe. Lakini pale tu utakapozidisha. Kama utavuta idadi kubwa
ya sigara unaweza kupata kwa wingi sumu, iitwayo nikotini iliyo
katika tumbaku. Hii inaweza kusababisha kifo cha ghafla. Hii
huwatokea hasa watu ambao wana magonjwa ya moyo. Uvutaji
sigara kwa wingi na kwa kipindi kirefu unaweza kusababisha
kifo kutokana na saratani.
Pombe inaweza kukuua ghafla. Kama utakunywa kiasi kikubwa
cha pombe. Matokeo yake yanaweza yakawa ni kusimama kabisa
kwa shughuli za ubongo. Hii inamaanisha kuwa sehemu maalumu
katika ubongo ambazo zinaratibu uvutaji hewa na mapigo ya moyo
hazitaweza tena kufanya kazi na matokeo yake ni kifo.
Lakini pombe pia ni chanzo cha ajali nyingi za barabarani na
kazini. Kumbuka kwamba pombe ni chanzo cha vifo vingi kuliko
dawa zingine za kulevya.

Magonjwa yatokanayo na sigara

Kuna matatizo na magonjwa mengi na ya aina mbalimbali
unayoweza kuyapata kutokana na utuvaji wa sigara. Kiungo
rahisi kuathirika ni mapafu. Baada ya kuvuta huo moshi, kaboni
na tindikali iliyomo kwenye tumbaku huishia kwenye mapafu.
Malimbikizo haya ya kaboni na tindikali husababisha ugumu
katika kupumua na kusabisha usaha kwenye mapafu. Matatizo
haya ya mapafu humfanya mvutaji awe mwepesi kupata
maambukizo mengine.
Hii inaweza ikawa kikohozi sugu na pia inaweza kusababisha
nimonia (kichomi) pamoja na kifua kikuu na sarakani. Nikotini
vilevile ni mbaya kwa tumbo. Husababisha kupoteza hamu ya
kula na maumivu katika sehemu za chini ya tumbo.

Unaweza ukaona kwamba wavutaji wakubwa wa sigara wakawa na
meno meusi au machafu. Hii ni kwa sababu kaboni imejilimbikiza juu
ya meno, na hivyo kubadilika kwa rangi. Watu wanaovuta mara kwa
mara hutoa harufu mbaya mdomoni na hupata matatizo ya ngozi.

Je, sigara ni sumu kwa binadamu?

Ndiyo. Nikotini iliyo kwenye tumbaku ni sumu. Ukiwa na kiwango
kikubwa cha nikotini katika damu utajisikia kichefuchefu,
kutapika, kujaa kwa mate mdomoni, maumivu ya sehemu za
chini ya tumbo, kuharisha, na kujihisi dhaifu. Dalili nyingine
ni kuumwa na kichwa, kizunguzungu, kuongezeka kwa mapigo
ya moyo, kupata shinikizo la damu, kutetemeka na kutokwa na
jasho baridi. Nikotini nyingi inaweza kusababisha ukosefu wa
umakini na pia ukosefu wa usingizi.

Je, ni kweli kuwa madhara ya uvutaji moshi wa sigara yako ni kidogo kuliko yale yatokananyo na kuvuta moshi kutoka kwa mvutaji?

Uvutaji wa aina zote una madhara. Kama utavuta sigara na
kuvuta moshi kwa kutumia mdomo hadi kwenye mapafu yako
utapata madhara moja kwa moja kwenye viungo vyako.
Kama nitasimama karibu na mvutaji na kuvuta moshi, kuna
madhara ambayo siyo ya moja kwa moja. Kwa upande mwingine
kama jirani wa mvutaji unaweza kuvuta sumu nyingi itokanayo
na tumbaku kwa sababu hakuna kitu cha kuichuja. Sigara za
viwandani zina kishungi ambacho huchuja tindikali mbalimbali
zenye sumu, kama vile kaboni na asidi ya magamba ya miti,
ambazo zina madhara kwa mapafu.

Je, gongo na sigara husaidia uyeyushaji wa chakula?

Ni imani na fikra potofu kwamba, ukinywa gongo au kuvuta
sigara kwa kiasi kidogo baada ya chakula itasaidia kuyeyusha
baadhi ya vyakula vya mafuta. Pombe inaweza hata kupunguza
mtiririko wa kawaida wa kimiminika muhimu kwa uyeyushaji wa
chakula (tindikali) na hivyo kuchelewesha kuliko kurahisisha
uyeyushaji wa chakula.
Nikotini ya sigara kwa upande mwingine inaongeza kazi katika
utumbo mpana na hivyo kurahisisha uyeyushaji wa chakula.
Lakini kwa upande mwingine nikotini huchochea utengenezaji
wa tindikali tumboni ambayo husababisha maumivu ya tumbo.

Je, ni kweli kwamba mtu anayekunywa pombe anaishi kwa muda mrefu kuliko yule ambaye hanywi kabisa?

Si kweli. Mpaka sasa wanasayansi hawajathibitisha kwamba
mtu anayekunywa pombe kidogo ndiye anayeishi kwa muda
mrefu. Kwa ujumla, watu wanaoishi katika hali ya usafi, afya
njema na maisha yenye furaha ndio wanaoishi kwa muda
mrefu kuliko wale ambao hawajijali kimwili na kiakili. Kimsingi,
kunywa pombe ni kutojijali. Unywaji wa pombe kwa kiasi hauna
madhara, lakini inakupasa kuwa macho katika unywaji huo ili
usizidishe kupita kiasi.

Je, ukinywa pombe unaongeza damu?

Si kweli.
Pombe haiongezi damu, vitamini wala nguvu. Ukweli ni kwamba unywaji pombe kupita kiasi huvuruga ufyonzaji wa vitamini na madini kutoka kwenye chakula kuingia mwilini.

Vitamini ni muhimu kwa kuimarisha kinga ya mwili ambayo inasaidia kujikinga na magonjwa, pamoja na maradhi kama UKIMWI. Kwa hivyo, unatakiwa uhakikishe unakula matunda na mboga za majani kwa sababu vinakuongezea vitamini.

ATHARI ZA ULEVI KATIKA JAMII

Watu wanokunywa kupitia kiasi huathiri jamii kwa njia
mbalimbali. Madhara mengine hutokea kwa kuwa wanafanya
vitu ambavyo wasingevifanya iwapo wasingekuwa wamelewa.

Watu wakilewa, huweza kuwa na hasira, wagomvi hivyo basi
huwadhuru wengi kiakili na kimwili. Isitoshe, ajali nyingi za
kazini na barabarani hutokea watu wakiwa wamelewa. Mara
nyingi watu wasiokuwa na hatia na vilema hupoteza maisha yao
kutokana na ajali zinazohusiana na ulevi.

Watu wanaokunywa
pombe kupita kiasi hupunguza uangalifu na hivyo basi kuchangia
katika kuenea kwa VVU kwenye jamii. Watu wanaokunywa pombe
wanaweza pia kufanya ujambazi katika jamii. Pia wanaokunywa
kupita kiasi si wafanyakazi wa kutegemewa kwani hutumia
muda mwingi nje ya sehemu zao za kazi.

Watu waliozoea kunywa pombe nyingi hupoteza pesa zao nyingi
kununua pombe na muda wao mwingi kufikiria jinsi ya kupata
pesa za kunywea pombe.

Kutokana na gharama za kununua
pombe familia zao hukosa pesa za vitu muhimu kama kodi ya
nyumba, ada na sare za shule na chakula.

Vijana wanaokunywa pombe huanza kuiba pesa nyumbani kwao
ili kununulia pombe. Matumizi mabaya ya pombe mara nyingi
husababisha matatizo au kuvunjika kwa familia, au urafiki.

Vilevile husababisha matokeo mabaya shuleni au kuacha kabisa
shule, hali ambayo inaweza kusababisha kukosa nafasi za kazi,
kujitegemea wewe mwenyewe na kusaidia famila yako na jamii.

Madhara ya sigara na pombe kwa mtoto

Watoto hawatakiwi kunywa pombe wala kuvuta sigara!

Watoto hasa ndio wapo katika hatari zaidi ya kupata madhara
yatokanayo na uvutaji sigara na unywaji pombe, kwa sababu
bado wanaendelea kukua. Wanaweza wakaathiri miili yao na ubongo
kwa maisha yao yote. Wana hatari zaidi ya kuathirika katika
maendeleo yao ya kijamii na kisaikolojia. Matumizi mabaya ya pombe
na sigara yanaweza yakaleta madhara katika makuzi ya mtoto.

Wanawake wanaweza kulewa haraka kuliko wanaume?

Wasichana na wanawake wanaweza kulewa kwa ujumla.
Mara nyingi, hulewa pombe haraka kuliko wanaume. Hii
inatokana na uzito mdogo wa miili yao, na kiasi cha mafuta na
maji katika miili yao. Kilevi husambaa kiasi kikubwa katika miili
ya wanawake. Maini yao huharibika kirahisi zaidi kuliko maini
ya wanaume.

Kutokana na kilevi, wanawake au wasichana huwa wepesi
kufanya vitu ambavyo wasingefanya kama wasingelewa.
Wanaume hutumia nafasi hii kuwashawishi kufanya mapenzi
bila kuchukua tahadhari yoyote kama vile kutumia kondomu ili
kupunguza maambukizo ya VVU.

Madhara ya pombe kwa mwili na akili

Pombe huingia kwenye damu na kuzunguka mwili mzima pamoja
na kwenye ubongo wako. Ina madhara kwa viungo vya mwili
wako na ubongo wako na hivyo huathiri tabia na hisia zako.

Unywaji wa pombe kupita kiasi unaweza kuathiri viungo vingi
kwa mfano, ini ambalo ndilo huathirika zaidi. Ini hilo linafanya
kazi ya kufyonza kilevi katika mwili wako. Kama ukinywa zaidi
utaathiri ini kiasi kwamba halitaweza kufanya kazi kikamilifu au
litashindwa kabisa hatimaye utakufa. Kilevi kingi husababisha
kansa ya ini na tumbo.

Hatari kubwa siku hizi ni kupata na kusambaza virusi vya
UKIMWI. Mlevi mara nyingi huwa mzembe na husahau kinga
muhimu kama vile kutumia kondomu wakati wa kufanya mapenzi.
Anaweza pia kufanya mapenzi na watu ambao hafahamu afya
zao, kama ni wagonjwa au la. Zaidi ya hayo mlevi mara nyingi
huwa dhaifu, hivyo ni rahisi kushambuliwa na magonjwa
mbalimbali pamoja na VVU.

Pombe inaathiri pia uwezo wa kufanya tendo la ndoa. Huwa ni
vigumu kwa uume kusimama. Pia huathiri ubongo hasa sehemu
zile zinazomiliki ufahamu na mihemko.

Kwanza unaweza kujisikia mchangamfu na huru, lakini mara
tu unaanza kujisikia taabu na kushindwa kutembea vizuri.
Utakuwa na matatizo ya kutoona vizuri na matatizo ya kutoa
uamuzi sahihi. Watu huanza kuwa na vijitabia vya ajabu na
vipya baada ya kulewa. Kugombana na watu wengine na kufanya
mambo yasiyokubalika kama vile kujikojolea mbele za watu.
Kama utaendelea kunywa kuna uwezekano mkubwa wa kupata
madhara. Kila dhara huharibu mamilioni ya seli za ubongo wa
binadamu.

Kwanza hutakuwa na kumbukumbu ya nini kimetokea, lakini
unaweza pia kupoteza kabisa kumbukumbu zako. Kama ukinywa
pombe kupita kiasi kwa muda mrefu unaweza kupungukiwa
akili na mwisho kuharibu kabisa akili. Pombe pia ni dawa ya
kulevya kwani huweza kukutawala. Watu waliotawaliwa na
pombe, hutumia pesa nyingi na muda mwingi kwenye pombe,
hali ambayo inaweza kuwa ni mzigo mzito kwa familia na jamii,
na pindi mtu anapotawaliwa, ni vigumu kunywa kidogo au kuacha
kabisa. Kama mtu atajaribu kuacha, hupata matatizo kama
kutetemeka, mapigo ya moyo kuongezeka, kutokwa na jasho
jingi, na kukosa usingizi wakati wa usiku. Hali hiyo husababisha
maumivu na ni hatari kwa watu ambao wametawaliwa na pombe.

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home πŸ“– Reading πŸ–ΌοΈ Gallery πŸ’¬ AI Chat πŸ“˜ About