Kwa nini Albino tunaonekana kama mzigo katika familia zetu?

Watu wanaohitaji kupewa uangalizi maalumu wanaweza
kuonekana ni mzigo kwa kuwa wanaweza wakawa wanaomba
kupewa mahitaji au msaada maalumu tofauti na watu wengine
wa kawaida. Wazazi na wanafamilia wengine wanaweza
kuchukizwa na matamshi wanaotoa watu wengine pamoja na
kulazimika kuvumilia utani na matusi. Ndugu wanapaswa kujua
kwa nini ndugu yao Albino ni tofauti na kwa nini anahitaji
uangalizi maalumu.
Familia ndiyo msingi wa kumwezesha mtoto Albino kujitambua
na kukubali hali aliyo nayo. Familia inayoweza kumkubali mtoto
wao Albino inaneemeka na kuwa yenye furaha kwa sababu
mtoto Albino anakuwa kiungo maalumu katika familia, yaani
inaipa familia hali ya kuwa na nguvu yao iliyoungana.

Kwa nini jamii inatuchukia sisi Albino?

Siyo watu wote katika jamii wanawachukia au kuwatenga Albino.
Wazazi, ndugu zenu, rafiki zenu wanawapenda na kuwajali. Ni
jambo la kawaida kwa watu wa aina fulani kuwakataa au kuwakwepa
wale ambao wanaonekana tofauti na wao. Kwa mfano, katika jamii
ya watu weupe ni kawaida kuwakwepa au kuwakataa wale wenye
rangi nyeusi na hivyo ndivyo ilivyo pia kwa jamii ya watu weusi
kuwakataa au kuwakwepa watu weupe.
Jamii ya watu weusi huwaogopa, na hivyo huwakwepa Albino
kwa kuwa hawajui kilichotokea mpaka wakawa hivyo. Hali hiyo
inaimarishwa na uvumi potofu unaosambazwa kuwa ukimgusa
Albino unaweza ukageuka rangi ukawa mweupe au ukiwa na mimba
na ukamcheka au ukakutana na Albino, utazaa Albino. Ukweli ni
kwamba uvumi huu ni potofu na ni upuuzi mtupu. Ualbino ni hali
inayorithiwa na si ya kuambukizwa. Hakuna sababu ya kumuogopa
Albino. Mtazamo hasi wa jamii unaweza kubadilishwa endapo watu
watakuwa na ufahamu zaidi kuhusu ualbino na wanapowafahamu
watu wa aina hii vizuri zaidi kwamba ni watu wakarimu na wenye
urafiki. Na wewe unaweza ukachangia katika kuendeleza uelewa
huu kama utashiriki na watu kwa urafiki na kwa uwazi.

Albino anaathirikaje na unyanyapaa na ubaguzi katika jamii?

Watu wengi huwaona Albino kama watu tofauti na watu wengine
na kuwakwepa, wanaweza hata kubadili upande wa barabara
ili wasikutane nao au kukaa karibu nao katika daladala. Wengi
wanaamini katika uongo na uvumi unaosambazwa. Jamii inawatenga
katika matukio mengi na kwa hiyo kuimarisha uvumi usiyo na
usahihi uliopo kuhusu Albino. Hii inapelekea kunyanyapaliwa,
kubagulliwa na kuwekwa pembeni. Mbaya zaidi, ni kuwa ubaguzi
huu huchangia katika kushuka kujithamini kwa kijana Albino.
Akisha kuwa hajithamini ni vigumu kukubalika au kupata kazi. Kwa
hiyo, ubaguzi unaleta mzunguko wa madhara kwa Albino. Hitaji
muhimu kwa binadamu ni kupendwa, kukubalika na kutunzwa.
Kwani ualbino unatokea katika familia bila kutarajiwa. Kuwepo kwa
ualbino katika familia kunaweza kuwa kichocheo cha kukubalika
na kupendwa miongoni mwa ndugu, wazazi, mababu na mabibi.
Changamoto kubwa iliyopo Tanzania ni kupambana na unyanyapaa
na ubaguzi na kugombea haki sawa kwa ajili ya Albino.

Kuna fikra kuwa Albino ni watu wa kawaida je, kisayansi hii ni kweli?

Hii ni kweli kabisa. Watu wanaoishi na ualbino ni watu wa
kawaida kama binadamu wengine wote na wanaweza kuwa
wa aina tofauti kama binadamu wengine. Wanaweza kuwa
wadogo au warefu, wanene au wembamba, warembo au wasio
warembo, wenye vipaji au wa wastani. Wanaweza kuwa na
uthubutu au wenye aibu, wachangamfu au jeuri, wenye tabia ya
ushirikiano au wenye tabia ya uhasama.
Kumbuka kuwa utofauti wao upo tu kwenye muonekano wa ukosefu
wa rangi kwenye ngozi, nywele na macho. Wakati umefika kwa
jamii kujifunza kuwakubali Albino kama binadamu wengine, wenye
hisia, mahitaji, uwezo na wanastahili haki zote za binadamu kama
alivyo mtu mwingine yoyote.

Kwanini Albino wanakuwa na mabaka meusi kwenye ngozi zao?

Ngozi ya Albino haina jinsi ya kujilinda na mionzi ya jua. Inaungua
sana baada ya kupatwa na jua na ngozi huwasha na kuuma. Ngozi
ya Albino inajitahidi kujilinda na mionzi ya jua lakini ina pigimenti
nyeusi kidogo sana kwa hiyo inatengeneza mabaka meusi1. Kwa
hiyo, mabaka meusi huonyesha kuwa ngozi haijalindwa ipasavyo
dhidi ya jua. Kama Albino atajilinda na jua ngozi yake inakuwa na
mabaka kidogo sana au bila mabaka.

Vijana Albino wafanye nini ili kulinda ngozi yao?

Pamoja na matatizo ya kuona, ngozi ya Albino ni rahisi sana
kudhurika kwa mionzi ya jua. Hatima yake ikiwa ni uwezekano
mkubwa wa kupata saratani ya ngozi. Hivyo basi, kila Albino
anashauriwa daima kujikinga dhidi ya mionzi ya jua kwa kuvaa
nguo za mikono mirefu, kuvaa kofia pana, kuvaa miwani ya jua na
kwa wale wenye uwezo kujipaka mafuta maalumu yanayosaidia
kukinga ngozi dhidi ya mionzi ya jua.

Kwa nini ngozi ya Albino inafanana ya watu weupe?

Ngozi ya Albino ina ukosefu wa rangi. Inaonekana kama ya watu
weupe ambao wana kiasi cha pigimenti ndogo. Tofauti na watu
weupe ngozi ya Albino haigeuki rangi katika jua kuwa kahawia.
Sawa na watu weupe Albino lazima ajikinge na mionzi ya jua kwa
kuvaa nguo ndefu za kufunika ngozi au kutumia losheni maalumu
ya kupaka ngozi. Mfano mzuri ni wa mama wa Malkia wa Uingereza
ambaye anayo ngozi nyororo kama ya mtoto mchanga huku akiwa
na miaka 100 sasa kwa sababu hakuwahi kujiweka juani.

Kwa nini Albino wanawekwa katika kundi la watu wenye ulemavu?

Ulemavu maana yake ni hitilafu katika mwili au akili inayomwekea
mipaka mtu asiweze kufanikisha shughuli fulani katika maisha
yake. Albino wanatambuliwa kama watu wenye ulemavu Tanzania
hasa kwa ajili ya uwezo wao wa kutokuweza kuona vizuri. Dalili
za kutokuwa na uwezo wa kuona hutofautiana kuanzia wale
ambao hawaoni karibu, wasioweza kuona mbali na wale ambao
wanashindwa kuona vizuri au kuona mawingumawingu.

Nini matatizo ya watoto Albino shuleni?

Ingawaje, akili zao hazina hitilafu watoto Albino mara nyingi
hawafanyi vizuri shuleni, na huchukuliwa kuwa ni wajinga kwa
sababu hawawezi kusoma vizuri ubaoni. Mara nyingi watoto
Albino hujikuta wameaachwa katika shughuli za nje, ya
madarasa zinazojumuisha wenzao shuleni.
Walimu lazima watambue watoto Albino darasani mwao na
wawe na mikakati maalumu wa kuwawezesha kufuatilia masomo.
Wanafamilia pamoja na walimu shuleni wahakikishe kuwa
Albino hawatengwi katika shughuli za vikundi. Kuwakutanisha
na Albino wenzao au na watu wenye Albino kwenye familia zao
na jamii kwa ujumla itawasaidia zaidi.
Watoto Albino wanajifunza kufidia upungufu walionao wa
kujithamini kwa kuweka jitihada katika masomo na shughuli
nyingine. Wana mwelekeo wa kushinda zaidi katika mambo
wanayojaribu. Watu weusi wengi wanaoishi na ualbino
wamefanikiwa kuwa mafundi wazuri, wanasheria, wakunge
wajasiriamali wataalamu wa kompyuta na hata maprofessa wa
vyuo vikuu.

Nini kifanyike ili kurekebisha matatizo ya macho ya Albino?

Kuishi kwa kushindwa kuona sawasawa ni changamoto ya
msingi waliyonayo Albino, inaathiri elimu yao (hususan katika
usomaji), katika kujumuika (ikiwemo kushiriki katika michezo
na kukubalika na rika lao) na katika uwezo wa kutembea katika
mazingira magumu. Matatizo huanzia pale ambapo udhaifu huu
usipotambuliwa na marekebisho yoyote yasifanywe na familia
au jamii. Kama marekebisho yatafanyika ama kwa kutumia
miwani ya macho, au kuwa na vitabu vyenye maandishi makubwa
au kutumia lensi ya kukuza maandishi au kwa kuwapa nafasi ya
mbele darasani watoto Albino wanaweza kufanya vizuri kama
watoto wengine.

Nini matatizo ya macho ya Albino?

Mboni katika macho ya Albino haina pigimenti ya rangi. Kwa
hiyo, ni rahisi macho yao kuathiriwa na mwanga. Kwani mboni
ndiyo inayolinda jicho la ndani lisipatwe na mwanga mkali.
Vilevile kama mboni inavyolinda jicho dhidi ya mionzi ya jua,
inakuwa vigumu kuona kwa usahihi utofauti katika picha. Kwa
hiyo uwezo wa kuona unatiwa mawingu mawingu. Hivyo basi, ni
muhimu sana kukwepa inavyowezekana mionzi ya jua na kulinda
macho kwa kuvaa miwani ya jua.

Albino mara
nyingi hawaoni
vizuri, na hii
i n a t o f a u t i a n a
k w a m m o j a
hadi mwingine.
Inawezekana ni
kutoona mbali,
kutoona karibu au kuona mawingumawingu (ukungu).
Matatizo haya hutofautiana katika Albino. Ukweli ni kuwa
Albino anaweza kushiriki katika michezo mbalimbali, baadhi
wanaweza kuendesha magari na wengi wanaweza kusoma
maandishi ya kawaida.

Je, Albino abadili/ageuze nywele rangi (die) au avae nywele bandia (wigi)?

Suala hili litatagemea na kila mtu anavyopendelea. Baadhi ya
watu hupendelea kuacha nywele zao katika hali asilia kama
walivyozaliwa, wengine wanapendelea kuzigeuza rangi kuwa
nyeupe au nyeusi na wengine wanapendelea kuvaa nywele bandia
zenye rangi nyeusi, kahawia au nyeupe. Jambo la msingi ni
wewe kujisikia vizuri. Kwa kadri unavyojisikia vizuri ni ndivyo
utakavyojiamini na ukijipenda na wengine watakupenda.

Ualbino unarithiwa vipi?

Watoto wengi wanaozaliwa na ualbino, wazazi wao wana rangi
ya ngozi, nywele na macho inayafanana na watu wa kabila /asili
yao. Mwili wa kila mwanadamu una seti mbili za vinasaba (moja
hutoka kwa mama na moja hutoka kwa baba). Mtu anaweza
kuwa na rangi ya asili ya kawaida, lakini akawa na kinasaba cha
ualbino. Kama mtu ana kinasaba kimoja cha rangi ya asili na
kimoja cha ualbino atakuwa na taarifa za vinasaba vya kutosha
kutengeneza rangi ya asili. Kinasaba cha ualbino ni seli dhoofu
haiwezi peke yake kuonyesha ualbino mpaka mtu awe nazo
mbili kwa pamoja.
Kama wazazi wote wawili wana vinasaba vya ualbino na wote
hawaonyeshi ualbino, kuna uwezekano wa kupata mtoto Albino
kati ya mmoja katika wanne kwa kila mimba.

Ualbino husababishwa na nini?

Watu wenye ualbino hawana uwezo kabisa au wana uwezo mdogo
wa kuwa na rangi kwenye ngozi zao, nywele na macho. Rangi hii
huitwa β€œmelanini”. Rangi ya ngozi itategemeana na kiasi cha
melanini kilichopo. Hali ya kuzalisha melanini imekaa katika
vinasaba vyetu. Kama vinasaba vya kutoa melanini havipo au
vimebadilishwa madhara yake ni ukosefu au upungufu wa rangi.
Kwa hiyo hali ya ualbino ni ya kurithi. Inaweza kurithishwa
kutoka kwa wazazi kwenda kwa mtoto.

Nini maana ya Ualbino?

Albino wana ngozi nyeupe, nywele nyeupe au nyekundu na macho
ya kijivu au ya bluu. Ngozi yao ni nyeupe zaidi kuliko ndugu zao
wa familia moja au watu wa jamii yake
ambao hawana hali ya ualbino. Ngozi hii inaonekana zaidi kuwa
nyeupe katika familia za watu weusi, ingawaje, ualbino
hutokea kwa watu wa kila taifa, rangi, kabila na dini. Albino
wako katika mabara yote ulimwenguni.

Nini maana ya neno Albino?

Neno Albino linamaanisha
mtu mweupe, linatokana na
neno la lugha ya Kilatini –
albus-linamaanisha β€œeupe”.
Kuanzia karne ya 17 neno
Albino limekuwa likitumika
katika kueleza hali ya kundi
la viumbe hai (watu, wanyama
na hata mimea) ambao wana
upungufu au ukosefu wa rangi
katika ngozi, macho na nywele.
Kwa binadamu ni bora kutumia
maneno β€œWatu wanaoishi na
ualbino
kwani itamaanisha kuwa ni watu kama wengine ila wanaishi na
hali tofauti ya β€œualbino”. Katika kitabu hiki maneno haya mawili
yatatumika.
Lugha inajenga dhana na kuunda hali ya ukweli / uhalisi. Kwa
sababu hiyo ni lazima tuache kutumia maneno kama β€œzeruzeru”.
Neno hili linamaanisha sifuri mara mbili au mtu asiye na
thamani. Utumiaji wa neno hili ni dharau ya utu na kulaumu
watu wanaoishi na ualbino kama kosa lao.

Shopping Cart
3
    3
    Your Cart
    🏠 Home πŸ“– Reading πŸ–ΌοΈ Gallery πŸ’¬ AI Chat πŸ“˜ About